Search

Mahubiri

Somo la 11: Maskani

[11-2] Bwana Wetu Aliyeteseka Kwa Ajili Yetu (Isaya 52:13-53:9)

Bwana Wetu Aliyeteseka Kwa Ajili Yetu
(Isaya 52:13-53:9)
“Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara; 
Atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. 
Kama vile wengi walivyokustaajabia, 
Uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote, na umbo lake zaidi ya wanadamu; 
Ndivyo atakavyowastusha mataifa mengi. Wafalme watamfumbia vinywa vyao; 
Maana mambo wasiyoambiwa watayaona, na mambo wasiyoyasikia watayafahamu.
Ni nani aliyeisadiki habari tuliyoileta? 
Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani? 
Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, 
Na kama mzizi katika nchi kavu. 
Yeye hana umbo wala uzuri; 
Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. 
Alidharauliwa na kukataliwa na watu; 
Mtu wa huzuni nyingi ajuaye sikitiko. 
Na kama mtu ambaye watu huficha nyuso zao; 
Alidharauliwa na wala hatukumhesabu kuwa kitu.
Hakika ameyachukua masikitiko yetu 
Amejitwika huzuni zetu; 
Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, 
Amepigwa na Mungu na kuteswa. 
Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, 
Alichubuliwa kwa maovu yetu; 
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, 
Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
Sisi sote kama kondoo tumepotea; 
Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; 
Na BWANA ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.
Alionewa lakini alinyenyekea, 
Wala hakufunua kinywa chake; 
Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, 
Na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake, 
Naam, hakufunua kinywa chake. 
Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa, 
Na maisha yake ni nani atakayeyasimulia? 
Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; 
Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. 
Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya—
Na pamoja na matajiri katika kufa kwake, 
Ingawa hakutenda jeuri, 
Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.”
 

Injili Sasa Inaenea Ulimwenguni Pote
 
Wakati huu kwa kweli unaelekea mwisho. Toka katika siasa hadi kwenye uchumi, kila kitu kinaelekea mwisho. Kimsingi, upepo wa vita unavuma sana pale ambapo mataifa yenye nguvu yanapojaribu kupanua ushawishi wao katika maeneo mengine ya dunia yaliyosalia. Karibu kabisa na nyumbani kwangu, Korea ya Kaskazini ilitangaza hivi karibuni kuwa ilikuwa ikiendeleza kutengeneza silaha za nyuklia, jambo ambalo lilisababisha mshituko mkubwa katika jumuiya ya kimataifa. Katika kipindi hiki cha shida katika ulimwengu, ninatumaini kuwa kila mmoja anayehusishwa katika mabishano haya atakuwa tayari kusuluhisha masuala yao kwa busara, na si katika ujinga, na kisha kufikia makubaliano ili wote waweze kufanikiwa kwa pamoja.
Ni lazima tuombe kila siku, ili Mungu aweze kutupatia muda wa kutosha unaoturuhusu kuineneza injili zaidi. Si kwa sababu ninaogopa kufa. Bali ni kwa sababu kuna nchi nyingi ambako injili ya kweli haijahubiriwa bado, na kuna nchi pia ambazo injili ya kweli inakaribia kuchanua. Hamu yangu ni kuendelea kuieneza injili ya asili zaidi na zaidi, pale injili inapochipuka na kuchanua, kwa kuwa injili inahitajika kuhubiriwa zaidi.
Kwa kweli, Mungu anavifanya vitu vyote ili vifanye kazi kwa pamoja kwa mazuri, lakini kinachoniogopesha ni kuwa wanadamu wanaweza kuwa wajinga sana. Kuna watu wengine ambao wanatishia maisha ya watu wengine hata pale ambapo hawatambui kuwa ni lini na wapi na wao watakabiliana na kifo chao; baadhi yao wanajaribu hata kuendesha mauaji ya kimbari ili kumuua kila mtu.
Ninaamini kuwa kwa hakika Mungu anatawala mioyo ya viongozi wote wa ulimwengu. Pia ninaamini kuwa atatupatia amani.
Katika zama hizi, watu wa Israeli bado wanamsubiria Masihi waliyeahidiwa. Ni lazima watambue kuwa Masihi wao si mwingine bali ni Yesu. Ni lazima wamtambue Yesu kuwa ni Masihi ambaye wamekuwa wakimsubiri na kumwamini hivyo. Katika kitambo kifupi, injili ambayo inampendeza Bwana wetu itaingia Israeli ikiwa ni pamoja na nchi nyingine ambako mlango wa injili bado haujafunguliwa bado. Kwa kweli, injili inaenezwa ulimwenguni pote vizuri kiasi kuwa inachanua kikamilifu katika zama hizi za nyakati za mwisho.
Nimeambiwa kuwa Seminari ya Kitheolojia huko Bangladeshi imeyafanya machapisho yetu ya kiingereza kama vitabu vya lazima kusomwa na wanafunzi wake ili waweze kupata shahada zao. Baada ya kukutana na injili ya maji na Roho kwa mara ya kwanza, wanafunzi wote katika seminari hii, hata kabla hawajashangaa watapokea ondoleo la dhambi zao.
Kama hivi, nitumaini kuwa wanatheolojia wote wa ulimwengu watapokea ondoleo la dhambi kwa kuifahamu na kuiamini injili ya maji na Roho. Na sisi ambao tumepokea ondoleo la dhambi kabla yao ni lazima tuombe bila kukoma ili jambo hili liweze kutokea. Sio tuombe tu, bali ni lazima tuishi maisha yetu kwa imani.
 

Masihi Alikuja Hapa Duniani Takribani Miaka 700 Baada ya Unabii wa Isaya
 
Isaya alikuwa ni nabii aliyeishi karibu miaka 700 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo hapa duniani. Pamoja na kuwa alitangulia kabla ya kuja kwa Yesu Kristo kwa miaka 700, na kwa sababu alifahamu mambo mengi kuhusu Masihi, Isaya alitabiri yote kuhusu jinsi Masihi atakavyokuja na jinsi atakavyofanya kazi yake ya wokovu kana kwamba alimuona Masihi kwa macho yake mwenyewe. Ukianzia Isaya 52:13 na kuendelea sura za 53 na 54, Isaya aliendelea kutabiri, kwa wazi na kwa kina, juu ya jinsi ambavyo Masihi atawaokoa wanadamu kutoka katika dhambi. Ni jambo la kushangaza sana kwamba Isaya alitabiri kwa usahihi kabisa kuwa Yesu Kristo atakuja hapa duniani na kuzichukua dhambi zote katika ubatizo wake, na kuimwaga damu yake Msalabani na hivyo kuuleta wokovu kwa wote. Na baada ya miaka 700 kupita tangu Isaya alipoutoa unabii wake, Yesu Kristo alikuja hapa duniani na akazitimiza kazi zake zote kwa usahihi kama ilivyotabiriwa na Isaya.
Isaya alitabiri kwamba Masihi atakuja ulimwenguni na atatenda kwa busara. Kama ilivyotabiriwa katika Isaya 52:13, “Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara;Atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana.” Kwa sababu Yesu Kristo alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu na kwa kweli alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa ubatizo wake, na angeweza kutoa maisha yake juu ya Msalaba na hivyo kuhukumiwa kwa dhambi zote za mwanadamu. Kama Isaya alivyotabiri, kila kitu kilifanywa kwa busara. Kwa sababu ya Yesu Kristo, dhambi zote za mwanadamu zimetoweka, zimeshughulikiwa kwa busara, na kwa kweli jina lake limekuwa juu sana, limetukuzwa na kuinuliwa kama vile ilivyotabiriwa mwanzo. Kile ambacho Isaya alikitabiri kimetokea.
Hata hivyo, Bwana wetu alipokuja hapa duniani, watu wa Israeli hawakumtambua kikamilifu. Pamoja na kuwa Bwana wetu alikuja hapa duniani na akazichukua dhambi za ulimwengu zikiwamo na zile za waisraeli, akafa Msalabani, na akafufuka tena toka kwa wafu, hata hivyo watu wa Israeli hawakuweza kuuamini hata ule ubatizo wa Masihi wala damu yake. Kwa kweli, waisraeli hawakuwa wametambua kuwa Masihi alikuwa amezaliwa katika taifa lao, pia hawakutambua kuwa kwa ubatizo wake na Msalaba hajazishughulikia tu dhambi za waisraeli pekee bali na dhambi za wanadamu wengine wote. Hawakutambua kuwa huyu Yesu Kristo alikuwa ni Mwana wa Mungu, Masihi wa kweli wa watu wa Israeli. Waisraeli ni lazima watambue sasa kuwa Yesu kwa kweli ndiye Masihi ambaye wamekuwa wakimngojea kwa miaka hii yote.
 


Kuteseka kwa Yesu Kulilenga Kuzifanya Dhambi za Ulimwengu Kutoweka

 
Wakati alipokuja hapa duniani kwa kweli aliteseka sana isivyoweza hata kuelezewa vizuri. Kama inavyoonyeshwa katika Isaya 53, Masihi alionekana kuwa mtu wa huzuni. Kwa kuzichukua dhambi nyingi za ulimwengu, aliteseka sana—sana kiasi kuwa tulimficha nyuso zetu.
Lakini ni wachache wanaomtambua Yesu kuwa ni Masihi. Kwa sababu aliteswa sana na watu wa nyakati zake, wengi wameshindwa kumtambua na kumwamini Yesu Kristo Masihi na Mwokozi. Bwana wetu alikuja hapa duniani akiyanyenyekea mapenzi ya Baba kwa kazi ya kuwaokoa wanadamu toka katika dhambi za ulimwengu; ili kuitekeleza kazi hiyo, Yesu aliteseka sana. Haikutosha tu kwa yeye kuja hapa duniani ambayo aliiumba katika mwili wa mwanadamu, ambaye alimuumba kwa mfano wake, bali alidharauliwa, alidhihakiwa, aliadhibiwa, na aliteswa sana kiasi kuwa maandiko yanatueleza kuwa tulizificha nyuso zetu mbele ya uso wake, kwa sababu ilikuwa ni vigumu kumwangalia. Mbali na kusifiwa kama Masihi katika dunia hii, alitendewa na kunyanyaswa vibaya kana kwamba ni mtu mwenye wazimu, ambaye mateso yake hayakuweza kuelezewa vizuri kwa maneno. Kama vile tunavyogeuza nyuso zetu tunapomuona mtu fulani akinyanyaswa na kuonewa vibaya, Masihi alinyanyaswa mbele ya uumbaji wake mwenyewe kwa kiwango cha juu kiasi kwamba waisraeli katika nyakati hizo walizificha nyuso zao mbele yake.
Wakati Yesu alipokuja hapa duniani, alionekanaje? Wakati Masihi alipokuja hapa duniani, kwa kweli alikuwa ni kama mche mwororo, kama mzizi katika nchi kavu. Hakukuwa na mengi ya kuzungumzia, kwa maneno mengine, katika mwonekano wake wa nje. Kwa kweli, hata pale tunapomlinganisha Bwana wetu na sisi wenyewe, hakukuwa na vitu vingi vilivyo vya kuvutia kwa Masihi. Mwonekano wa nje wa Masihi wetu ulikuwa wa kawaida na hakukuwa na kitu cha kujivunia.
Wakati Masihi alipokuja hapa duniani, bila shaka hakukuwa na uzuri wowote katika mwonekano wake ambao ungetufanya kumtamani au kumsifu. Lakini bila kujali mwonekana huu, kama Masihi wetu, alitenda kwa busara, alipokea kule kuwekewa mikono na Yohana ili kuzichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa, alisulibiwa na kuimwaga damu yake, alifufuka toka kwa wafu, na kwa jinsi hiyo alituokoa toka katika dhambi zetu zote. Kwa sababu Masihi alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana basi aliweza kusulubiwa na kuimwaga damu yake kwa ajili yetu.
Kama Isaya 53:3 inavyosema, “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi ajuaye sikitiko. Na kama mtu ambaye watu huficha nyuso zao; Alidharauliwa na wala hatukumhesabu kuwa kitu.” Kwa sababu Masihi wetu alikuja hapa duniani na kuzifanya dhambi zote za ulimwengu kutoweka kwa kuwekewa mikono na kwa kumwaga damu yake, basi alitakiwa kunyanyaswa kwa jinsi hiyo na watu wa Israeli na askari wa kirumi.
 

Mateso ya Masihi Yalitabiriwa Takribani Miaka 700 Iliyopita
 
Ukweli kuwa Masihi atakuja duniani, na kuwa atabatizwa na Yohana, atamwaga damu yake Msalabani, na kwamba atafufuka toka kwa wafu ulikuwa umekwisha tabiriwa na nabii Isaya kama miaka 700 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo. Kama alivyotabiri nabii Isaya kuhusu kuja kwa Masihi, Yesu Kristo alikuja hapa duniani kama ilivyotabiriwa. Masihi Yesu alizaliwa kwa bikira katika hori la kulishia kwa unyenyekevu, alichukua dhambi za ulimwengu kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana Mbatizaji, alielekea Msalabani, ambako aliimwaga damu yake na akafa kwa ajili ya wokovu wetu, na baada ya siku tatu akafufuka toka kwa wafu. 
Kama vile ambavyo mikono iliwekwa juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka ya kuteketezwa na kama ambavyo damu yake ilimwagwa katika Siku ya Upatanisho (Mambo ya Walawi 16), siku ambayo dhambi za mwaka mzima zilisafishwa, vivyo hivyo Yesu alizichukua dhambi zetu zote kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana na akamwaga damu yake na kisha akafa Msalabani sawasawa na Neno la unabii. Baada ya kuzibeba dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake, Yesu alipitia miaka mitatu ya mateso katika maisha yake ya kijamii. Sababu iliyomfanya Yesu, Masihi kusulubiwa ni kutokana na ubatizo wake toka kwa Yohana Mbatizaji, ambapo dhambi zote za ulimwengu zilipitishwa kwake, na hii ndiyo sababu iliyomfanya adharauliwe, ateswe, na anyanyaswe na kila mtu.
Kwa kweli, watu hawakukana kuwa Yesu ni Masihi tu, bali baadhi ya Wayahudi na Warumi walimchukia na kumtesa Yesu kupita inavyoweza kuelezewa. Walimchukia na kumkataa kupita kiasi.
Kwa kweli Yesu alichukua dhambi zote za mwanadamu mara moja kwa kuupokea ubatizo toka kwa Yohana Mbatizaji katika Mto Yordani, kisha akamwaga damu yake Msalabani. Masihi alibatizwa na Yohana na akamwaga damu yake Msalabani ili kuyatimiza mapenzi ya Baba yake. Aliachwa uchi pale Msalabani na walimtukana. Watu wote waliomzunguka Yesu wakati ule walimdhihaki na kumsuta, “Ikiwa kweli ndiwe Mwana wa Mungu, shuka na ujiokoe wewe mwenyewe!”
Wakati Yesu alipoanza maisha yake ya wazi kwa ubatizo wake, kwa kweli ilimlazimu kupitia mateso mengi yaliyoletwa na mwanadamu. Pamoja na kuwa Yesu alikuwa ameshazibeba dhambi za ulimwengu kwa ubatizo wake kwa ajili ya usalama wa mwanadamu, watu wa siku hizo, hawakuweza kulifahamu jambo hili, na badala yake walimchukia Yesu ambaye alikuja kama Masihi wao, waliendelea kumsulubisha, wakamletea mateso mengi, walimkana na kumtukana. Kwa kweli, Yesu Masihi alichukiwa sana, maandiko yanatumbia kuwa alifanyiwa kama mnyoo alipokuwa hapa duniani.
Kwa kweli, hufahamu sawasawa jinsi ambavyo Mafarisayo walimchukia Yesu. Mafarisayo hawa hawakuweza kumwacha Masihi peke yake, ambaye alionekana kutishia uongozi na umashuhuri wao. Kwa hiyo walimchukia Masihi, kila wakati walijaribu kutafuta kosa juu yake, na hawakusita kuanzisha mashambulizi ya kila aina kwa Yesu kila mara mipango yao mibovu iliposhindwa. Masihi alibeba matusi ya aina zote na walimkana hali wakiwa wamejazwa na chuki na uovu. Hivyo, Isaya alitabiri jinsi ambavyo Masihi ataonewa. Hivyo tunaweza kuthibitisha toka katika unabii wa wazi na wa kina wa Nabii Isaya uliotolewa miaka 700 kabla ya kuja kwa Masihi jinsi ambavyo Yesu atafanyiwa hapa duniani.
 


Je, Watu Walimwamini Yesu Kristo Masihi Aliyekuja kwa Maji na Damu?

 
Hata hivyo, ukiachilia mbali mateso, Yesu Masihi kwa ukimya alizifanya na kuzikamilisha kazi zake. Sasa watu wa Israeli na wengine wote ulimwenguni pote lazima watambue na kuamini kuwa huyu Masihi ni Yesu Kristo. Ili kuzifanya dhambi za waisraeli na za kila mtu katika ulimwengu mzima kutoweka, ilimbidi Masihi kupokea ubatizo wake katika muundo wa kuwekewa mikono, na kwa kweli alisulubiwa na akateseka sana—na kwa kufanya hivyo, amewaokoa waamini kikamilifu katika huduma zake toka katika dhambi zao zote, na ameikubali imani ya hawa waamini kwa jumla. Pamoja na ukweli kuwa Masihi alikuja hapa ulimwenguni katika hali ya unyenyekevu, na pamoja na ukweli kuwa alibatizwa, alikufa Msalabani, na akafufuka toka kwa wafu ili kuzifanya dhambi za kila mmoja kutoweka, wale waliomwamini walikuwa ni wachache sana. Ili sisi tuweze kuishi, ni lazima tuamini kuwa Yesu ndiye Mwokozi wetu wa kweli na Masihi, na kwamba si Masihi kwa ajili ya waisraeli tu bali kwa ajili ya wanadamu wote.
Pamoja na kuwa Yesu alizichukua dhambi zetu sisi kwa ubatizo wake na akazibeba huzuni zetu, magonjwa yetu, na laana zetu, watu wengine wanaweza kufikiri, “Je, ni dhambi gani ambayo aliyoifanya hata akapata mateso kama hayo?” Lakini, Yesu ni Mwana wa Mungu asiye na dhambi. Kwa kuzibeba dhambi zetu zote, Masihi aliteseka sana kwa ajili yetu akapata laana zote, huzuni, na mateso ya dhambi zetu. Kwa kuptia mateso yote ambayo Yesu ameyapata katika miaka 33 ya maisha yake tangu alipokuja hapa duniani, ametuokoa sisi sote toka katika dhambi zetu zote.
Katika zama hizo, hali wakilisikia Neno la Mungu likizungumzwa kupitia Nabii Isaya, je, watu wa zama hizo walimwamini Yesu Kristo kuwa ni Masihi, aliyekuja kwa maji na kwa Roho? Ni nani aliyeamini katika injili ya maji na Roho ambayo tunaihubiri sasa? Hata sasa, kuna watu wengi ambao hawana mvuto katika injili ya maji na Roho pamoja na kuwa wanadai kuwa wanamwamini Yesu.
Hapa katika kifungu kikuu cha maandiko, Nabii Isaya anatabiri kuwa Mwana wa Mungu atakuja duniani, atatenda kwa busara, atazichukua dhambi zetu zote, atahukumiwa kwa sababu ya dhambi zetu, na kisha atatuokoa. Lakini sio wengi walioupokea ukweli huu alioutimiza. Hata hivyo, nina hakika kuwa kuanzia sasa na kuendelea, watu wa mataifa yote watamtambua Yesu Kristo kama Masihi wao na watamtukuza sana. Je, sasa unafahamu kuwa Yesu Masihi aliteswa kwa sababu ya dhambi za watu wa Israeli, kwa sababu ya dhambi zako na zangu, na kwa sababu ya dhambi za wanadamu wote? Nabii Isaya, ambaye angalipenda wewe ufahamu na kuamini ukweli huu, alitabiri juu ya huduma ya Masihi kwa namna hii.
 

Masihi Alikuwa ni Kama Mzizi Katika Nchi Kavu
 
Hivi ndivyo ambavyo Nabii Isaya alieleza kabla juu ya kuja kwa Yesu Kristo Masihi, kwamba atakapokuja hapa duniani, atakuja katika hali ya huzuni. Isaya alisema kuwa Masihi atakuwa “Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu” (Isaya 53:2). Wakati Yesu Kristo alipokuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, hakuwa mtu ambaye mtu mwingine angeweza kuona kitu chochote cha kuvutia toka kwake. Hakuwa na umbile lenye misuli, hakuwa mrefu na mwenye umbo zuri, kama vile Arnold Schwarzenegger au Sylvester Stallone. Kwa kweli, alikuwa ni mwenye umbile dogo kiasi kwamba kama tungelimwangalia tungemuonea huruma na kumhuzunikia. Hata hivyo, Neno lake lilikuwa ni kama upanga wa sime wenye makali huku na huku.
Yesu Masihi hakuwa tu mwenye umbile lenye mtazamo wa kimaskini, bali pia alikuwa ni maskini katika raslimali. Yusufu, baba yake wa kambo, alikuwa ni seremala wa kawaida. Kama ingekuwa leo hii, familia ambavyo ilikuwa ikitunzwa na seremala ilikuwa ni familia isiyo na maisha mazuri na bila shaka ilikuwa mbali na maisha ya kutosheka kwa wingi wa vitu. Ni kwa kufanya kazi kwa nguvu ndipo maseremala wanapoweza kupata kitu cha kuwasaidia.
Baada ya kuwa masihi amekuja hapa duniani hakuhudhuria shule yoyote. Na kwa hiyo Mafarisayo walitaka kumdhihaki kwa ajili ya hilo, lakini hawakuweza kufanya hivyo, kwani ilidhihirisha wazi kuwa Yesu Kristo Masihi ndiye hasa Mwana wa Mungu. Yesu hakuwahi kufika katika shule ya Gamalieli, ambayo ilikuwa ni shule maarufu sana ya Kiyahudi kwa wakati huo, mahali ambapo mwanazuoni mkuu wa Sheria aitwaye Gamalieli alifundisha Sheria. Katika shule hii, wanafunzi waliweza kujifunza toka kwa mwalimu mkuu wa Sheria, hawakufundishwa tu elimu ya dunia hii tu bali walifundishwa pia juu ya Sheria yenyewe. Lakini Yesu hakufundishwa katika shule kama hiyo. Hata hivyo, hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kuwa alihudhuria masomo shuleni. Hata hivyo, hakukuwa na Sheria hata moja ya Agano la Kale ambayo Masihi huyu hakuifahamu, wala mahali ambapo Agano la Kale lilifundisha kuhusu Masihi, alikuwa na elimu ya hali ya juu na alikuwa na imani kuu kuliko yeyote. Hakukuwa na chochote alichokisema ambacho kilikuwa ni cha kipuuzi au ambacho kilikuwa kinyume na Sheria ya Mungu.
 

Kwa Nini Ilibidi Masihi Ateswe, Aonewe, na Adharauliwe?
 
Ili kuwa Masihi halisi wa watu wa Israeli na kuwaokoa toka katika dhambi zao zote na kuwafanya watu wa Mungu, Masihi wetu alikuja hapa duniani na kwa hiari akayapokea mateso yote, matusi, dharau, dhihaka. Mateso na kukataliwa ambako Masihi alikupitia kwa ajili ya watu wa Isareli kwa kweli yalikuwa ni ya kujitoa na yenye unyanyasaji mkubwa. Mateso ambayo Masihi aliyapata kwa ajili yetu yalikuwa ni mateso makubwa ambayo yangetufanya tuzifiche nyuso zetu toka kwake. Kwa sababu Yesu alikuwa ni Masihi ambaye angetuokoa toka katika dhambi zetu na hukumu, kwa hakika ametuokoa toka katika dhambi zetu kwa kunyanyaswa na kudharauliwa mbele ya watu wote kupita jinsi inavyoweza kuelezwa. Kwa hiyo Yesu alinyanyaswa katika ulimwengu huu.
Kwa sababu Yesu alikuwa ni Masihi aliteswa sana na kunyanyaswa, watu wa nyakati hizo hawakuweza kumwangalia uso wake. Tusisahau kamwe kuwa japokuwa Masihi alikuja kama Masihi wangu na wako, na ni kweli kuwa ndiye Masihi wa watu wote, ili kulitimiza jukumu na kazi za Masihi, Masihi huyu aliteswa sana na kwa kuteswa huko ametuokoa toka katika dhambi zetu na adhabu iliyotustahili kutokana na dhambi.
Hata pale Masihi aliposulubiwa, watu hawakuacha kumdhihaki: “Kwa nini usishuke kutoka hapo juu ya Msalaba? Kama kwlei wewe ndiwe Mwana wa Mungu, basi ushuke chini toka katika Msalaba. Inawezekanaje ukawa ndiwe Mwana wa Mungu? Kama kweli wewe ndiwe Mwana wa Mungu, basi shuka chini na umwokoe mwizi aliyetundikwa karibu nawe; na zaidi shuka chini ujiokoe wewe mwenyewe!” Waliendelea na dhihaka yao: “Ooh, sawa, kwa nini usibadilishe jiwe hili kuwa mkate? Kama ndiwe Mwana wa Mungu tupatie uthibitisho! Tuonyeshe uthibitisho ili tukuamini. Ikiwa huwezi hata kufanya hivyo, wewe ni Masihi wa aina gani? Ni huzuni sana!”
Basi watu walimtukana Masihi, walimkana, walimdhihaki bila kukoma. Walimvua nguo akawa uchi, walimpiga makofi, na wakampiga. Kristo aliteseka kwa dhihaka kuu, unyanyasaji, matusi kwa kiwango ambacho hakijaonekana kabla na ambacho hakitaonekana tena. Pia aliadhibiwa kwa adhabu ya kusulubishwa, adhabu ambayo ilikuwa ni maalum kwa waliotenda makosa makubwa ya jinai kwa wakati huo. Masihi wetu alichapwa mijeledi na askari, mikono na miguu yake ilipigiliwa misumari Msalabani, na akamwaga damu yake yote aliyokuwanayo katika mwili wake.
Kwa kweli Yesu alibeba dharau na dhihaka, maumivu na mateso, ili aweze kuitimiza huduma yake kama Masihi kwa ajili yetu. Kwa kusulubiwa kwake alizichukua dhambi zetu zote, laana zetu zote, magonjwa yetu yote, na adhabu yetu yote ya dhambi. Aliyabeba mateso yote ambayo mimi na wewe tulitakiwa kuyapata, na aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Masihi huyu sasa amekuwa ndiye Mwokozi kwa sisi tunaoamini kuwa Yesu ndiye Mwokozi. Kwa hiari yake alikubali kuwa Masihi wetu. Alikuja hapa duniani kulingana na mapenzi ya Baba yake, na akazichukua dhambi zetu na adhabu ya dhambi katika Msalaba kwa ajili yetu, na kisha akafufuka tena toka kwa wafu—ili kutuokoa!
Kaka zangu na dada zangu, Je, unafikiri kuwa ilikuwa rahisi kwa Yesu kuyapitia mateso hayo yote mbele za watu wote? Kama tungekuwa mahali pake, ingekuwa ni sisi ndio tuliopata dharau na mateso haya ya kuachwa uchi, kutukanwa, kuteswa, na kusulubiwa sio tu mbele ya ndugu na jamaa wanaotupenda bali mbele ya adui zetu, bila shaka tungepata wazimu kabla ya kufa! Yesu alisulibiwa ili kila mtu aweze kuona mateso yake, sio mahali palipojificha bali mahali pa juu ili wote waweze kumnyooshea vidole vyao na kumdhihaki.
Mateso makubwa, huzuni, na magumu yalimpata Kristo hata kabla ya kusulubiwa kwake. Kabla ya kumpigilia kwa Yesu kwa misumari Msalabani, watu walihakikisha kuwa anapitia mateso ya aina mbalimbali. Aliletwa mbele ya umati na akahukumiwa mbele yao, alidhihakiwa, na alipigwa kofi na mtumishi wa Kuhani Mkuu. Alidhihakiwa! Watu walimpiga uso wake, walimchapa mijeledi, na walimpiga kwa mawe! Yesu Masihi aliyapitia mateso haya yote kwa ajili yetu sisi na wala si kwa ajili ya kitu kingine!
Maandiko yanatueleza kuwa aliteswa kwa ajili yetu, maandiko yanasema, “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu” (Isaya 53:5). Masihi aliyapitia mateso ya jinsi hiyo ili aweze kuwakomboa watu wote wakiwemo Waisraeli toka katika dhambi zao na adhabu ya dhambi zao. Masihi huyu alishughulikia dhambi za ulimwengu na adhabu ya dhambi kwa kuupokea ubatizo toka kwa Yohana, na akaikamilisha huduma yake kama Masihi kwa kunyanyaswa na watu wake mwenyewe, askari wa kirumi, na watu wa mataifa mengine.
Mungu alitabiri kuwa Masihi atawaokoa watu hawa waliosimama kinyume naye toka katika dhambi zao zote—toka katika dhambi zao zote zilizowahi kufanywa na wanadamu wote. Na kama ilivyokwisha kutabiriwa, Yesu Kristo alikuja hapa duniani kama Masihi, kwa kweli aliyapitia mateso haya yote na alituokoa mimi na wewe toka katika dhambi zetu na adhabu ya dhambi kwa kuimwaga damu yake ya thamani.
Kwamba tumeokolewa toka katika dhambi na adhabu ya ya dhambi kwa kumwamini Masihi hakukuja tu bila malipo ya dhabihu. Ni kwa sababu Yesu Kristo alikuja hapa duniani na akayapata mateso haya yote ili tuwe wasio na dhambi. Na ni kwa sababu Masihi alihukumiwa kwa ajili ya dhambi zetu zote ili sisi tuweze kuipokea karama ya wokovu na ondoleo la dhambi na kuwa wana wa Mungu kwa kuamini kwa mioyo yetu. Ni kwa sababu ya Masihi wetu ndio tungaliweza kuwa watu wenye furaha jishi hiyo.
Ni lazima tumshukuru Masihi kwa kutupatia furaha hii na kwa kutukirimia baraka zake. Wokovu ambao Masihi ametupatia ulikuja kwetu kupitia imani tu, pamoja na kuwa hatujampatia sadaka yoyote, yeye mwenyewe alitoa sadaka isiyo na gharama mbele za Mungu Baba. Ni lazima tuamini kuwa Mungu mwenyewe ndiye aliyetuokoa kwa kuteseka mateso haya yote na ni lazima tumshukuru kwa tendo hilo.
 

Sikia, Ee Israeli, Geuka Nyuma na Umwamini Yesu Kristo
 
Watu wa Israeli ni lazima watubu sasa na kumwamini Yesu ambaye ni Masihi kuwa Mwokozi wao. Hadi kipindi hiki cha sasa, Waisraeli bado hawatambui kuwa Masihi wao alikwisha kuja. Kama ilivyokwisha kutabiriwa na Nabii Isaya kwamba Masihi, Mtumishi wa Mungu, atakuja hapa duniani. Na kwa Neno hili la unabii lilieleza kuwa kwa kuja kwake hapa duniani Masihi atatuokoa wote kwa kuzichukua dhambi zote za wanadamu kwa ubatizo wake na kwa kusulubiwa Msalabani. Yesu Kristo ametimiza kwa kweli kazi zake za wokovu. Watu wa Israeli ni lazima sasa wageuke, waufahamu na kuuamini ukweli huu. Ni lazima wazikiri dhambi ambazo watu wao wenyewe walizitenda kwa kumsulubisha Yesu. Na ni lazima wazitambue nafsi zao kuwa ni zenye dhambi tangu kuzaliwa kwao, na kwa kumwamini Masihi ndipo waweze kuokolewa toka katika dhambi zao zote na adhabu ya dhambi.
Kwa sasa hakuna Masihi mwingine. Kwa sababu Yesu Kristo amekwisha kuja kama Masihi, kwa hiyo hakuna Masihi mwingine yeyote. Inawezekanaje hasa kukawepo na Masihi mwingine? Je, inawezekanaje kukawepo na Mwokozi mwingine? Wakati watu wa Israeli wanapoyapitia magumu au watakapoyapitia magumu siku za usoni, je, wanatumaini kuwa atakuwepo mtu mashuhuri mwenye sifa kama wale waigizaji wa filamu za Hollywood ambaye ndiye atakayekuwa Masihi wao?
Tangu sasa, waisraeli ni lazima wamtambue Yesu Kristo kuwa ni Masihi wao. Ni lazima waamini kuwa Yesu Kristo ndiye Masihi wao wa kweli. Masihi wao amekwisha kuja hapa duniani miaka 2,000 iliyopita. Ili kuzichukua dhambi zao na kuwafanya kuwa wana wa kweli wa Ibrahimu, alibatizwa, kama ambavyo wao walipaswa kubatizwa, na alisulubiwa, ili kwamba waweze kupokea tohara ya kiroho. Masihi alifanyika Mwokozi wa kweli wa watu wa Israeli kwa kuzichukua dhambi zao kwa ubatizo wake toka kwa Yohana, kwa kuubeba Msalaba na kuimwaga damu yake na kunyanyaswa, na kisha kwa kufufuka tena toka kwa wafu. 
Waisraeli ni lazima watubu na kumwamini Masihi. Ni lazima wamwamini Yesu Kristo sasa kuwa ni Masihi wao. Kilichobakia kutimizwa sasa ni kwa watu wa Israeli kumwamini Yesu Kristo kuwa Masihi wao. Ni lazima watambue kuwa Masihi aliyetabiriwa na Isaya ndiye huyu Yesu Kristo. Ni lazima watambue na kuamini kuwa huyu aliyetabiriwa si mwingine bali ni Yesu Kristo mwenyewe. Unabii wa Agano la Kale umetimizwa wote kupitia Yesu Kristo bila kuacha waraka wowote mdogo au mkubwa. Katika kifungu kikuu cha maandiko, kinaeleza kuwa mataifa mengi watastushwa.
Isaya 52:14-15 inasema, “Kama vile wengi walivyokustaajabia, uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote, na umbo lake zaidi ya wanadamu; Ndivyo atakavyowastusha mataifa mengi. Wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona, Na mambo wasiyoyasikia watayafahamu.”
Kwa kuja hapa duniani, Yesu Kristo aliyakabili mateso ambayo yalikuwa makubwa zaidi kuliko ya yule aliyefanya makosa ya jinai na akaadhibiwa kifo hapa duniani. Alijitoa mwenyewe kwa kuyachukua maumivu zaidi na mateso kuliko watuhumiwa wowote wa jinai katika ulimwengu huu, aliyafanya haya yote ili kuwafanya wanadamu kuwa watu wake mwenyewe. Amewaokoa watu wake ambao watapokea ondoleo la dhambi kwa kumwamini yeye. Hivi ndivyo alivyowaokoa wanadamu.
Watu watasikia habari nzuri za wokovu ambazo hawajawahi kuzisikia wala kuziona hapo kabla. Wale ambao hawajasikia kuwa Masihi ni Yesu Kristo kwa hakika watasikia na kisha wataamini.
 


Yesu ni Masihi, Ambaye Aliwahi Kuja na Atakayekuja Tena

 
Siku hizi tunazikaribia nyakati za mwisho. Utakuwa ni muda wa kifo na mapigo. Wale wanaomwamini Masihi kwa hakika hawana hofu ya kifo. Kinyume chake wanaomwamini Masihi wanasubiri kwa hamu furaha ya Mbinguni na ufufuo wao ambao utafuata baada ya kifo chao. Kwamba giza linaishukia dunia hakumaanishi kuwa sisi wenye haki tutatiwa giza kwa giza hilo. Wakati injili hii itakapokuwa imetawanywa kikamilifu, ndipo Masihi atakapokuja.
Yesu Kristo, Masihi wetu alikuja hapa duniani kama Mwanakondoo wa Mungu, kama sadaka ya kuteketezwa, na akabatizwa na Yohana, na akautoa mwili wake Msalabani. Kama vile kondoo mbele ya wakatao manyoya yake, Yesu Masihi alizichukua dhambi zetu kwa ukimya, akapata mateso makubwa kwa kuichukua hukumu ya adhabu katika Msalaba, akafufuka baada ya siku tatu, na hivyo akafanyika Mwokozi mkamilifu kwa wale wote wanaomwamini.
Ni wachache tu waliofahamu kwa wakati ule kuwa Masihi alikuwa ni Yesu Kristo. Walikuwepo wachache waliofahamu kuwa Yesu Kristo alifanyika kuwa Masihi wetu kwa kuzaliwa kimyakimya katika ulimwengu huu takribani miaka 2000 iliyopita, akiishuhudia injili ya Ufalme kwa miaka mitatu baada ya ubatizo wake, kufa Msalabani, na kisha kufufuka tena toka kwa wafu. Wale wachache ambao walimtazama na kumwamini Mungu walishuhudia kuwa Bwana wetu ni Masihi wa kweli ambaye katika hali ya ukimya alizitimiza kazi zake.
Wale watumishi wa Mungu wakizieneza habari duniani pote kuwa Masihi ametuokoa toka katika dhambi zetu kwa kuja hapa duniani na kwa kuteswa kwake. Kwa kweli, Mungu mwenyewe anaieneza injili ya maji na Roho akiruhusu mbinu za kiuchapaji kukua, kwa kuitawala historia ya ulimwengu, na kwa kuyafanya mataifa yanayohubiri injili hii kuwa yenye nguvu na matajiri.
“Yesu ni Masihi. Yesu ni Masihi. Yesu ndiye Masihi! Kama unamwamini Yesu kuwa Masihi wako utaokoka. Yesu ni Mwana wa Mungu. Yesu ni Muumbaji aliyeumba ulimwengu wote. Yeye ni Mungu. Yeye ni Masihi Mwokozi wetu.” Watumishi wa Mungu waliendelea kuwahubiri watu kuwa Yesu ni Masihi, na pia kuhusu ubatizo wake, kifo chake Msalabani, na ufufuko wake.
Vijana wachache wa kiisraeli wametambua kuwa miaka 2,000 iliyopita, kijana mmoja aliyeitwa Yesu alikuja hapa duniani na kwamba alipofikisha umri wa miaka 30 alizichukua dhambi za wanadamu kwa kubatizwa na Yohana. Kwa wakati ule, ni wanafunzi wa Yesu tu ndio waliofahamu kuwa Yesu alikuwa ni Masihi, na ufahamu huu ulishirikishwa kwa watu wachache tu ambao walikuwa na hofu ya Mungu—wengine wote walibakia na umbumbumbu kuhusu ukweli huu. Yote katika yote, kulikuwa na watakatifu kama 500 (1 Wakorintho 15:6) katika taifa la Israeli ambao walifahamu kuwa Masihi alizichukua dhambi za ulimwengu na kuzipeleka Msalabani, na kwamba alikufa kwa ajili ya hizo, na kwamba akafufuka tena toka kwa wafu. Wengine wote hawakujua chochote.
Katika siku ya hamsini tangu kifo cha Yesu Kristo na ufufuko wake, Roho Mtakatifu aliwashukia wanafunzi wake. Wakati wanafunzi wa Yesu walipokuwa wakiomba katika chumba cha juu, Roho Mtakatifu aliwashukia na akawafanya wanene kwa lugha mpya na kushuhudia kuwa Masihi ni Yesu Kristo. Kisha wanafunzi wa Yesu, pasipo kuogopa kifo, walishuhudia kwa ujasiri, “Yesu ni Masihi. Masihi ni Mwokozi wetu. Yesu aliyefufuka ni Masihi wetu.” Hivyo watu wengi wakaamini siku hiyo.
Kupitia Yesu Masihi, kwa hakika Mungu ametuokoa wewe na mimi toka katika dhambi zetu na adhabu ya dhambi. Kwa sababu aliteseka sana ili aweze kutuokoa toka katika dhambi zetu na hukumu, basi tunapaswa kumwamini; wale wote wasioamini ni lazima watubu, wageuke na kuamini; na ni lazima sisi sote tuueneze ukweli huu kwa imani.
Kwa kweli watu wa Israeli kwa sasa wanahofu sana kutokana na hali tete waliyomo. Hivyo ni lazima walisikie Neno hili la Hema Takatifu la Kukutania kuwa Mungu amesema nao. Sisi nasi tunaingia katika nyakati za mwisho. Nina hakika kuwa injili ya maji na Roho iliyodhihirishwa katika utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania itapata mwanya wa kuingia kwa watu wa Israeli. Ninahakika kuwa na wao pia watakuja kuamini kwamba Yesu Kristo ndiye Masihi ambaye walielezwa na Mungu.
Mungu alikwisha waeleza watu wa Israeli kuhusu utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa, na waliuamini. Kwa kweli, bado wanatamani kutoa sadaka kwa Mungu kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania. Wapo wahafidhina miongoni mwa waisraeli ambao bado wanaishi katika nyika. Watu hawa bado wanaishi nyikani hadi sasa wakiendelea kutoa sadaka kwa njia hii. Kwa maneno mengine wanatoa aina ya sadaka ambayo ilikwishawahi kutolewa katika Hema Takatifu la Kukutania hapo mwanzo. Pengine ni wazawa wa Haruni. Ili kuzitunza desturi za familia zao wanaishi katika nyika badala ya kuishi mijini. Japokuwa ni waisraeli, wanaishi kama kabila linalojitegemea wakiwa wamejitenga toka katika watu wa kawaida. Tunatakiwa kuwahubiria watu hawa Neno la Hema Takatifu la Kukutania kuwa Masihi amekwisha kuja tayari na kwamba ametuokoa kulingana na imani yetu.
Ni lazima tumshukuru Yesu kwa kuja hapa duniani, kwa kuteseka, kwa kuhukumiwa badala yetu, kwa ajili ya kutuokoa mimi na wewe kama Mwokozi wetu toka katika dhambi zetu na adhabu ya dhambi.
 

“Upendo Una Nguvu Kama Kifo, na Wivu ni Katili kama Kaburi”
 
Ukweli kuwa tumeokolewa toka katika dhambi zetu zote na hukumu ya dhambi hakukufikiwa kwa kubahatisha kama vile inavyokuja barua ambayo hukuitarajia. Wokovu wetu si kama barua za mfuatano zinazotueleza kuzituma kwa upya kwa watu 20 na kwamba kama tusipotii tutapata mikosi. Pia wokovu wetu wa ondoleo la dhambi si kama wa vipeperushi vingi ambavyo vinatangaza ofa ya sahani mbili za piza kwa bei ya sahani moja ambapo tunaweza kuagiza na kuyajaza matumbo yetu kwa yale yaliyomo katika mioyo yetu.
Kwa kweli wokovu wetu umekuja kwa Mungu kumtuma Mwanae kuja kwetu, kwa kuzipitisha dhambi zetu zote kwake, na kwa kumfanya ateseke na kuteswa kwa ajili ya dhambi zetu zote. Hii ndiyo sababu ambayo mimi na wewe tunatakiwa kumwamini na kumshukuru Yesu kwa mioyo yetu yote. Ukisha fahamu jinsi ambavyo wokovu wetu ulikuja, ni nani basi miongoni mwetu anayeweza kuutupa wokovu huo kama jozi ya viatu vilivyokaa, au akauacha kama vile chombo kilichovunjika na kuwekwa darini, au kuudharau kama vile hautuhusu?
Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye pamoja na kuwa anahudhuria Kanisa la Mungu bado hajapokea ondoleo la dhambi? Je, kuna yeyote ambaye bado hajaiamini injili ya maji na Roho? Kama kuna watu wa jinsi hiyo, ni lazima watubu wote na kumwamini Masihi kabla hawajachelewa. Ikiwa umepotea, na hauna hakika ni njia ipi ya kuifuata, naomba uliamini Neno la ukweli kwa moyo wako wote. Wale wasioamini wanaukataa upendo huu wa Mwana wa Mungu, upendo ambao kwa huo amewaokoa kwa kuyapitia mateso haya yote kwa ajili yao.
Wale wote wanaodharau thamani ya upendo wake na kuukataa watafuatiwa na laana. Maandiko yanatueleza, “Upendo una nguvu kama kifo, na wivu ni katili kama kaburi” (Wimbo wa Sulemani 8:6). Upendo wa Mungu una nguvu sana na mkuu kiasi kuwa unaweza kuiletea adhabu ya Mungu iliyo katili sana kwa watu wanaoukataa upendo wa Mungu hadi mwisho. Kwa maneno mengine, ni kuwa ikiwa mtu atakufa angali mwenye dhambi, mtu wa jinsi hiyo atateseka sana kwa maumivu yasiyo na huruma ya kuzimu na kaburi. Mateso ambayo ni yenye chuki na ukatili kama kaburi. Wakati Masihi anapokuwa amekupenda kiasi hiki, pale alipobatizwa, alipomwaga damu yake, na alipoteseka kwa mateso mbalimbali, ili tu aweze kukuokoa, usipouamini upendo huu na kisha ukaukataa, kwa hakika utateseka kutokana na maumivu haya yenye ukatili. Na maumivu haya si mengine bali ni kuzimu.
Hivyo Mungu akasema, “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu” (Waebrania 9:27). Tunapokufa, mwili wetu unaweza kufikia mwisho, lakini mbele za Mungu huo sio mwisho wetu. Ili Mungu aweze kuwakanyaga daima wale ambao wanaukataa upendo wa Mungu, Mungu amewafanya waishi milele na wasife, na kwa hakika atawaletea mateso yasiyo na huruma. Kwa maneno mengine ni kwamba atawatupa katika tanuru ya moto iwakayo daima, na atawafanya wayapate mateso ya moto pasipo kuangamia, pasipo mwisho, na milele na milele. Mateso haya ya kikatili si mengine bali ni chuki ya ukatili ya Mungu. Je, unafikiria kuwa Mungu hatafanya vitu kama hivyo? Usisahau kuwa hakuna lisilowezekana kwa Mungu!
Upendo mkuu wa Mungu kwetu sisi ni ule ukweli kuwa aliteseka kwa ajili yetu, ametuokoa toka katika laana zetu zote, dhambi zetu zote, na adhabu zetu zote. Upendo huu wa Masihi ndio unaoweza kuondoa matatizo yako yote. Kwa kweli, hakuna kilicho kikuu zaidi ya upendo huu wa Masihi. Pasipo imani katika Masihi, upendo wa Mungu hauwezi kuwa wetu. Upendo huu tumepewa na Mungu tu, yeye aliyefanyika Masihi wetu, na ni Baba yake ndiye aliyemtuma kuja kwetu. Mwenyezi Mungu katika utatu ametupenda kwa jinsi hii, na kwa hiyo ametuokoa toka katika dhambi zetu na adhabu. Na ndiyo sababu kwanini ni lazima tumwamini Masihi, tumshukuru, tumtukuze, na ni lazima turidhishwe na imani katika Masihi huyu.
Ni shukrani iliyoje kwa Masihi kutupatia sisi injili ya maji na Roho? Ikiwa mtu hafahamu jinsi upendo huu usivyo wa kulipia, jinsi ambavyo hauwezi kubadilishwa na kitu chochote duniani, basi mtu wa jinsi hiyo bila shaka ni miongoni mwa watu wajinga sana. Ni kiasi gani cha mateso na shida ambazo Bwana wetu aliyapitia kwa ajili yetu? Kwa sababu tunamshukuru sana kwa upendo wake, japokuwa hatujitoshelezi bado tunazitoa nguvu zetu zilizobakia katika kuueneza upendo wake kwa wale wasioufahamu.
Ili kuzifanya kazi hizo za Mungu, ni lazima pia tupate mateso na magumu. Hatuwezi kujitafutia mafanikio yetu binafsi kwa ajili yetu. Ikiwa kweli tumeokolewa kwa kuupokea upendo wake wa kujitoa na ikiwa tumevikwa kwa huo, basi ni lazima tuwashirikishe watu wengine upendo huu. Kama vile Yesu alivyokumbana na mateso yote ili kuzifanya dhambi zetu kutoweka, si kwa upendo wa kimwili, bali kwa upendo wake wa kweli, basi ni lazima tuzitende kazi zake kwa imani, tukiwa na hiari ya kuyapokea magumu, mateso, chuki, na dharau. Ikiwa mambo haya yanamaanisha kuwa wengine pia watalipokea ondoleo la dhambi zao basi inatubidi tuwe radhi kuzitenda kazi hizo hata katika magumu. Ni lazima tuteseke kwa chuki kwa jina la upendo. Ikiwa kweli mimi na wewe tumepokea ondoleo la dhambi, basi ninaamini kuwa upendo huo umejengwa katika mioyo yetu.
Na kwa wale waliozaliwa upya, ambao wanafahamu hasa jinsi ambavyo walikuwa kabla na jinsi ambavyo upendo wa Kristo wa wokovu ulivyo na nguvu, basi watazaa matunda. Waliokoka ni miti inayozaa matunda ya wokovu, “kwa matunda yake mti hutambulikana” (Mathayo 12:33). Kabla ya kuokoka, ulikuwa umelowekwa kabisa katika dhambi zako, kiasi kuwa usingelalamika kama ingetokea kuwa unatupwa kuzimu. Sasa kwa kuwa umeamini kuwa Mungu amefanyika Mwokozi wako kwa kuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu na akateseka kwa ajili yako, na kwamba kwa kuteseka kwa niaba yako amekuokoa toka katika dhambi zako na hukumu. Hivyo, kwa kuamini hivyo basi umekwisha okolewa. Ikiwa kweli umepokea upendo huu, basi mimi na wewe ni lazima tuwe na mioyo inayotamani kuishi kwa ajili ya watu wengine.
Ikiwa mtu hana moyo wa jinsi hiyo, basi mtu wa jinsi hiyo hajapokea ondoleo la dhambi. Kwa kusema kweli, mtu wa jinsi hii anajifanya tu na wala hajapokea ondoleo la dhambi.
Kama vile Kristo alivyokutana na mateso yote na akatuokoa toka katika dhambi zetu zote na hukumu kwa sababu alitupenda; basi ikiwa tumeokolewa kwa kuamini katika upendo huu, basi upendo huu unapatikana katika mioyo yetu. Kwa nini? Kwa sababu Kristo anaishi sasa katika mioyo yetu. Kama vile alivyoteseka kwa ajili yetu na kwa kuwa alitupenda, basi ni lazima tuwe na shauku ya kuishi kwa ajili ya watu wengine na kukabiliana na magumu kwa ajili yao. Kwa sasa kwetu sisi tuliopokea ondoleo la dhambi hatuna dhambi yoyote iliyobakizwa katika mioyo yetu, mioyo yetu yote imebadilishwa ili kufanana na moyo wa Yesu Kristo.
Ninamshukuru Yesu Kristo kwa kuja hapa duniani, kwa kubatizwa na kumwaga damu yake Msalabani, kwa kuyapokea mateso yake yote kwa ajili yetu, na hivyo kwa kufanyika Masihi wetu ambaye ametuokoa toka katika dhambi zetu zote.