Search

Mahubiri

Somo la 11: Maskani

[11-1] Wokovu wa Wenye Dhambi Uliofunuliwa katika Hema Takatifu la Kukutania (Kutoka 27:9-21)

Wokovu wa Wenye Dhambi Uliofunuliwa katika Hema Takatifu la Kukutania
(Kutoka 27:9-21)
“Nawe utaufanya ua wa Hema Takatifu la Kukutania. Kwa upande wa Kusini kuelekea Kusini kutakuwa na chandarua ya nguo ya kitani safi yenye kusokotwa, kwa huo ua, urefu wake upande mmoja utakuwa ni dhiraa mia. Na nguzo zake zitakuwa nguzo ishirini na vitako vyake vitakuwa ishirini na vitakuwa vya shaba. Kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. Na vivyo hivyo, upande wa Kaskazini, urefu wake hiyo chandarua utakuwa ni dhiraa mia, na nguzo zake ishirini, na vitako vyake ishirini vitakuwa vya shaba, na kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. Na kwa upande wa magharibi, upana wa ua kutakuwa na chandarua ya dhiraa hamsini; nguzo zake kumi na vitako vyake kumi. Upana wa ule ua upande wa mashariki kuelekea mashariki utakuwa ni dhiraa hamsini. Chandarua upande mmoja wa lango itakuwa na upana wa dhiraa kumi na tano; nguzo zake zitakuwa tatu na vitako vyake vitatu. Na kwa upande wa pili ni vivyo hivyo, chandarua ya dhiraa kumi na tano; nguzo zake tatu na vitako vyake vitatu. Na kwa lile lango la ua kutakuwa na kisitiri cha dhiraa ishirini, kitakuwa na nguo ya rangi ya bluu, zambarau, na na nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa, kazi ya mshona taraza; Itakuwa na nguzo nne na vitako vyake vinne. Nguzo zote za ule ua ziuzungukazo pande zote zitakuwa na vitanzi vya fedha; kulabu zake za fedha na vitako vyake vya shaba. Urefu wa huo ua utakuwa dhiraa mia, na upana wake utakuwa dhiraa hamsini kotekote, na kwenda juu kwake dhiraa tano, uwe wa nguo ya kitani safi na vitako vyake vitakuwa vya shaba. Vyombo vyote na vigingi vyake vyote vitumikavyo katika Hema Takatifu la Kukutania, na vigingi vyote vya ule ua vitakuwa vya shaba. Nawe waamuru wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya nuru, ili kuifanya ile taa kuwaka daima. Ndani ya hilo Hema Takatifu la Kukutania, nje ya hilo pazia, lililo mbele ya huo ushuhuda, Haruni na wanawe wataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele ya BWANA; itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyao vyote kwa ajili ya wana wa Israeli.”
 
 
Uzio wa ua wa mstatiri wa Hema Takatifu la Kukutania ulikuwa na kipimo cha dhiraa 100 kwa urefu. Katika Biblia, dhiraa ilihesabiwa kutokana na urefu unaoanzia katika kiwiko cha mkono hadi kwenye ncha ya kidole kama kiasi cha sentimita 45 au inchi 18 katika vipimo vya kisasa. Kwa hiyo, kule kusema kuwa Hema Takatifu la Kukutania lilikuwa na dhiraa 100 kwa urefu kunamaanisha kuwa lilikuwa na mita 45 au futi 150; na kwamba upana wake ulikuwa dhiraa 50 maana yake ni kuwa lilikuwa na wastani wa takribani mita 22.5 au futi 75 kwa upana. Hivyo, hivi ndivyo vipimo ya Nyumba ambavyo Mungu aliishi miongoni mwa watu wa Israeli katika kipindi cha Agano la Kale.
 
 
Ua wa Nje wa Hema Takatifu la Kukutania Ulizungukwa na Uzio
 
Nguzo za ua wa Hema
Je, umewahi kubahatika kuuona muundo wa Hema Takatifu la Kukutani katika picha au mchoro? Kwa ujumla, Hema Takatifu la Kukutania liligawanyika ua wake na Hema Takatifu lenyewe ambalo ni Nyumba ya Mungu. Katika Hema hili Takatifu la Kukutania, ambayo ni Nyumba ya Mungu kulikuwa na muundo wa kitu kilichoitwa Madhabahu Takatifu. Madhabahu hii takatifu ilifunikwa na vifuniko vinne tofauti: kifuniko cha nguo ya kitani safi ya kusokotwa, na nguo ya nyuzi za bluu, zambarau, na ya na nyekundu; na nyingine ya manyoya ya mbuzi; na ile iliyotengenezwa kutokana na ngozi ya kondoo; na kifuniko cha ngozi ya melesi.
Katika upande wa mashariki wa ua wa Hema Takatifu la Kukutania kulikuwa na lango lake lenye nguo za nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Kama tungaliingia kupitia lango hili tungaliweza kuona madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na birika la kunawia, pia tungaliweza kuliona Hema Takatifu la Kukutania lenyewe. Hema Takatifu la Kukutania liligawanyika katika Mahali Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu ambapo sanduku la Ushuhuda la Mungu liliwekwa. Uzio wa ua wa Hema Takatifu la Kukutania ulijengwa kwa nguzo 60 na mapazia yake ya kitani safi nyeupe. Kwa upande mwingine, Hema Takatifu la Kukutania lenyewe lilijengwa kwa mbao 48 na nguzo 9. Tunahitaji kuwa na angalau wazo la jumla la vifaa vya nje vya Hema Takatifu la Kukutania ili tuweze kufahamu kuwa Mungu anazungumza nini kwetu kupitia muundo wa Hema hili.
Mungu aliishi ndani ya Hema Takatifu la Kukutania lililokuwa limejengwa kwa mbao 48. Mungu alidhihirisha uwepo wake kwa watu wa Isreali kwa nguzo ya wingu nyakati za mchana na kwa nguzo ya moto nyakati za usiku juu ya Hema Takatifu la Kukutania. Na utukufu wa Mungu ulipajaza mahali patakatifu ambapo Mungu mwenyewe aliishi. Ndani ya Mahali Patakatifu kulikuwa na meza ya mikate ya wonyesho, kinara cha taa, na madhabahu ya uvumba; na ndani ya Patakatifu pa Patakatifu kulikuwa na Sanduku la Ushuhuda na kiti cha Rehema. Maeneo haya katika Hema Takatifu la Kukutania yalikuwa na mipaka kwa waisraeli wa kawaida kuingia; ni makuhani tu na Kuhani Mkuu ndio walioruhusiwa kuingia kwa utaratibu wa Hema Takatifu la Kukutania. Imeandikwa, “Basi, vitu hivi vikiisha kutengenezwa hivyo, makuhani huingia katika hema hiyo ya kwanza daima, wakiyatimiza mambo ya ibada. Lakini katika hema hiyo ya pili kuhani mkuu huingia peke yake, mara moja kila mwaka; wala si pasipo damu, atoayo kwa ajili ya nafsi yake na kwa dhambi za kutokujua za hao watu” (Waebrania 9:6-7). Hii inatujulisha kuwa katika zama za sasa, wale wenye imani ya dhahabu tu inayoamini katika injili ya maji na Roho wanaweza kuishi maisha yao pamoja na Mungu hali wakimtumikia.
Je, nini maana ya mkate uliowekwa juu ya meza ya mikate ya wonyesho? Inamaanisha ni Neno la Mungu. Je, madhabahu ya uvumba inamaanisha nini? Inatujulisha juu ya maombi. Ndani ya Patakatifu pa Patakatifu kulikuwa na Sanduku la Ushuhuda na kiti cha Rehema kilichotengenezwa kwa dhahabu safi na ambacho kiliwekwa juu ya hilo sanduku. Kulikuwa na Makerubi waliozinyoosha mbawa zao kwenda juu wakikifunika kiti cha Rehenma kwa mbawa zao na walikuwa wameelekeana kukitazama kiti cha Rehema. Hiki kilikuwa ni kiti cha Rehema mahali ambapo neema ya Mungu ilikaa. Ndani ya Sanduku la Ushuhuda kulikuwa na mbao mbili za mawe ambazo zilikuwa zimeandikwa amri kumi za Mungu, kulikuwa na fimbo ya Haruni iliyochipuka, na kulikuwa na bilauri iliyokuwa imejaa mana. Sanduku lilifunikwa kwa mfuniko wa dhahabu (kiti cha Rehema), na juu yake makerubi walikiangalia kiti cha Rehema.
 

Je, Wale Waliopokea Ondoleo la Dhambi Wanaishi Wapi?
 
Mahali ambapo wale waliopokea ondoleo la dhambi wanaishi ni ndani ya Mahali Patakatifu. Mahali Patakatifu palijengwa kwa mbao 48 ambazo zilifunikwa dhahabu. Hebu jaribu kufikiria juu ya hilo. Wakati unauangalia ukuta wa dhahabu wa mbao 48, je ni kwa kiasi gani ukuta huo utang’aa? Ndani ya Mahali Patakatifu na vyombo vyake vyote vilitengenezwa kwa dhahabu safi kwa jinsi hiyo viling’aa sana.
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na birika la kunawia katika ua wa nje wa Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa vyote kwa shaba; na uzio wa ua ulitengenezwa kwa nguzo zilizofunikwa kwa fedha na kitani safi nyeupe. Kinyume chake, vyombo vyote ndani ya Mahali Patakatifu vilitengenezwa kwa dhahabu; kinara cha taa kilikuwa cha dhahabu, na vivyo hivyo meza ya mkate wa wonyesho ilikuwa ya dhahabu. Kwa kuwa vifaa vyote katika Mahali Patakatifu na kuta zake tatu vilitengenezwa kwa dhahabu vilipafanya ndani ya Mahali Pakatifu kung’aa sana kwa miali ya dhahabu.
Kule kung’aa kwa miali ya dhahabu ndani ya Mahali Patakatifu kunatujulisha kuwa watakatifu waliookoka wanaishi maisha ya thamani ya imani ndani ya Kanisa la Mungu. Watakatifu wanaoishi katika imani yao katika injili ya maji na Roho ni kama dhahabu safi inayopatikana katika Mahali Patakatifu. Maisha ambayo wakatifu wanaishi ndani ya Mahali Patakatifu ni maisha ya baraka yanayopatikana katika Kanisa ambamo wanajilisha katika Neno la Mungu, wanaomba na kumsifu Mungu, na wanakwenda mbele ya kiti cha enzi cha Mungu ambaye amejivika neema yake kila siku. Haya ndiyo maisha ya kiimani ndani ya Mahali Patakatifu. Ni lazima uzingatie katika moyo wako kuwa ni wenye haki tu wale ambao wameokolewa kupitia injili ya maji na Roho ndio wanaoweza kuishi maisha haya ya thamani ya kiimani ndani ya Mahali Patakatifu.
 

Mungu Alizigawa Sehemu ya Ndani na Sehemu ya Nje ya Mahali Patakatifu Vizuri
 
Kwa kuwa nyumba nyingi zina uzio, ua wa Hema Takatifu la Kukutania pia ulikuwa na uzio uliotengenezwa kwa nguzo 60 na zilizungukwa na mapazia ya kitani safi. Upande wa mashariki wa ua kulikuwa na lango lililotengenezwa kwa nguo za nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa zilizowekwa kwa kila mmoja kuona na ambazo zilikuwa na upana wa mita 9 (sawa na futi 30). 
Katika kujifunza juu ya Hema Takatifu la Kukutania, ni lazima tutambue vizuri juu ya imani nzuri ambayo Mungu anaihitaji kutoka kwetu. Pia ni vizuri tutambue kuwa ipi ni imani ya waliookoka, na kwa kupitia vifaa vilivyotumika katika Hema Takatifu la Kukutania tuweze kufahamu jinsi ambavyo Mungu ametuokoa. Ili tuweze kujifunza juu ya imani ya dhahabu na ing’aayo kama ilivyo ndani ya Mahali Patakatifu ni lazima kwanza tutazame kwa uangalifu juu ya birika la kunawia, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na uzio uliwekwa katika ua wa nje wa Hema Takatifu la Kukutania na vifaa vyote vilivyotumika. Kwa kufanya hivyo tunaweza kufahamu kuwa kwa imani ipi tunaweza kuingia katika Mahali Patakatifu penye mng’ao wa dhahabu. 
Je, kulikuwa na kitu gani katika ua wa nje wa Hema la Kukutania? Kulikuwa na birika la kunawia na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na ilizungukwa na nguzo 60 za miti. Na katika nguzo hizi yalitundikwa mapazia ya kitani safi kama uzio wa ua. Nguzo za uzio huu zilitengenezwa kutokana na mti wa Mshita ambao licha ya ugumu wake ulikuwa uking’aa sana. Nguzo zilizotengenezwa kutokana na mti huu zilikuwa na urefu wa takribani mita 2.25 (sawa na futi 7.5) jambo ambalo liliwafanya watu wengi wenye urefu wa kawaida kutochungulia ndani ya Hema Takatifu la Kukutania kwa kutokea nje ya uzio wa ua wa nje. Ikiwa kitu kiliwekwa makusudi ili mtu aweze kusimama juu yake hapo ndipo aliyefanya hivyo angaliweza kuona ndani ya ua; bila kufanya hivyo hakuna ambaye angaliweza kuchungulia ndani. Hii inatujulisha kuwa kwa kutumia juhudi zetu binafsi hatuwezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu. 
Chini ya hizo nguzo za mti wa mshita za ua wa nje kuliwekwa vitako vya shaba na zilifunikwa na vifuniko vya fedha kwa juu. Kwa kuwa nguzo zisingeweza kusimama zenyewe, utepe wa fedha ulizisaidia nguzo kushikamana moja kwa nyingine. Na pia utepe huo ulizisaidia nguzo kusimama kwa uthabiti katika mzunguko, vitanzi vya fedha vilivyowekwa katika vifuniko vya fedha vya nguzo vilifungwa katika vigingi vya shaba kwa kamba (Kutoka 35:18). 
 


Je, Vifaa Gani Vilitumika Katika Lango la Ua wa Hema Takatifu la Kukutania?

Lango la mahakama
Vifaa vilivyotumika katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania vilikuwa ni nguo za nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa. Urefu wa kwenda juu ya lango ulikuwa ni mita 2.25 (sawa na futi 7.5), na upana wake ulikuwa takribani mita 9 (sawa na futi 30). Kulikuwa na kisitiri cha nguo ya nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa ambazo zilining’inizwa katika nguzo nne. Kwa jinsi hiyo, yeyote aliyetaka kuingia katika ua wa Hema Takatifu la Kukutania aliweza kulipata lango lake kirahisi.
Nguo za nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa zilizotumika katika lango la Hema Takatifu la Kukutania zinadhihirisha kuwa Mungu atatuokoa kutoka katika dhambi zetu zote kwa kazi nne za Mwanae Yesu. Pia nguzo zote 60 za mti na uzio wa kitani safi wa ua wa Hema Takatifu la Kukutania zinadhihirisha wazi mbinu ambayo kwa hiyo Mungu atatuokoa mimi na wewe kupitia Mwanae Yesu.
Kwa maneno mengine, kupitia lango la ua wa nje wa Hema Takatifu la Kukutania Mungu analifunua fumbo la wokovu kwetu kwa wazi. Hebu tena tuvipitie vifaa vilivyotumika katika lango la Hema Takatifu la Kukutania: nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Nyuzi hizi nne ni muhimu sana kwetu ili tuweze kuokolewa kwa kumwamini Yesu. Ikiwa vifaa hivi visingekuwa muhimu, Biblia isingeandika habari zake kwa kina kiasi hiki.
Vifaa vyote vilivyotumika katika lango la Hema Takatifu la Kukutania vilikuwa ni muhimu sana kwa Mungu ili aweze kutuokoa mimi na wewe. Ukweli kuwa lango lilikuwa na nguo za nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa ni muhimu sana kwa Mungu ili kuwaokoa wenye dhambi. Hii ni kwa sababu nyuzi hizi nne zilikuwa ni ufunuo halisi wa wokovu kamili wa Mungu. Hivi ndivyo ambavyo Mungu aliamua. Hii ndio sababu Mungu alimuonyesha Musa muundo wa Hema Takatifu la Kukutania katika Mlima Sinai na akamweleza Musa kulifanya lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania sawasawa na maagizo yake.
 


Nini Maana ya Nyuzi za Bluu, Zambarau, na Nyekundu na Kitani Safi ya Kusokotwa?

 
Lango la Hema Takatifu lilitengenezwa na pazia la nguo za nyuzi za bluu, zambarau, na na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa; pia ile shela kati ya Mahali Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu ilifumwa kwa nyuzi hizi nne. Si tu kwa mavazi haya bali hata naivera na kifuko cha kifuani vya Kuhani Mkuu vilifumwa pia kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Hizi nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa zinatueleza nini? Je, nyuzi hizi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa zilikuwa na umuhimu maalum ili Bwana wetu aweze kutuokoa? Ni lazima tuhakikishe kuwa tunayachunguza mambo haya kwa ukaribu.
Kwanza, nyuzi za bluu zinatujulisha juu ya ubatizo wa Yesu Kristo. Wale ambao hawafahamu juu ya umuhimu wa ubatizo hawafahamu kuwa nyuzi za bluu zinamaanisha ubatizo wa Yesu Kristo. Kwa kweli, wale ambao hawajazaliwa upya wanadai kuwa nyuzi za bluu zinaonyesha kuwa “Yesu Kristo ni Mungu, na kwamba alikuja duniani katika mwili wa mwanadamu.” Kwa upande mwingine wengine wanadai kuwa “nyuzi za bluu zinabeba maana ya Neno.” Hata hivyo, Biblia inatueleza kuwa nyuzi za bluu zinamaanisha, “Ubatizo wa Yesu, ambao kwa huo alizipokea dhambi za ulimwengu baada ya kuja hapa duniani.” Maandiko yanatuonyesha wazi kuwa nyuzi za bluu zinatuonyesha juu ya ubatizo wa maji ambao Yesu aliupokea toka kwa Yohana Mbatizaji. Nilipokuwa nikilisoma Neno juu ya Hema Takatifu la Kukutania nilikuja kutambua kuwa, “Mungu anataka kutuonyesha umuhimu wa imani yetu katika ubatizo wa Yesu.”
Joho lililovaliwa na Kuhani Mkuu alipokuwa akitoa sadaka lilikuwa limefumwa kwa nyuzi za bluu. Kisahani cha dhahabu kilikuwa kikining’inia katika kilemba ambacho Kuhani Mkuu alikivaa kichwani pake, na utepe uliokifunga kisahani katika kilemba ulikuwa na rangi ya bluu. Maneno “Utakatifu kwa BWANA” yaliandikwa katika kisahani hiki cha dhahabu. Tunaweza kuona kuwa utepe wa bluu uliokifunga kisahani cha dhahabu katika kilemba cha Kuhani Mkuu unadhihirisha kwa wazi ubatizo wa Yesu ambao unatoa utakatifu kwa Bwana.
Kwa njia hii, kupitia utepe wa bluu uliokifunga kisahani cha dhahabu katika kilemba, Mungu anazungumza nasi kuhusu wokovu wetu wa kweli. Kwa maneno mengine, kipini cha chuma kinachotupatia utakatifu ni bluu, na huu ndio ubatizo wa Yesu. Japokuwa rangi ya bluu kwa jumla inatukumbusha juu ya anga la bluu, kwa kweli rangi ya bluu haimaanishi Mungu peke yake. Nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa; nyuzi za bluu kwa hakika zinamaanisha ubatizo wa Yesu Kristo. Kwa lugha nyingine, nyuzi za bluu zinatujulisha kuwa Yesu Kristo alizichukua dhambi za wenye dhambi wote wa ulimwengu huu kwa kubatizwa (Mathayo 3:15). Kama Yesu hangelizichukua dhambi za kila mtu kwa kubatizwa, sisi waamini tusingeweza kumpatia “Bwana utakatifu”. Kama isingekuwa kwa ubatizo ambao Yesu aliupokea, tusingeliweza kamwe kuvishwa utakatifu mbele za Mungu.
Je, unaifahamu maana ya kiroho ya amri ya Mungu ya kulifuma lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania kwa nyuzi za bluu kwa mujibu wa muundo aliouonyesha kwa Musa? Lango la ua kuelekea katika Hema Takatifu la Kukutania ambapo Mungu aliishi linatujulisha juu ya Yesu Kristo. Lango la ua, ambalo linasimama badala ya Yesu Kristo, lilifumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa kwa sababu kwa uwazi kabisa Mungu alipenda kuufunua ukweli unaotuongoza katika wokovu. Nyuzi za zambarau zinamwakilisha Roho Mtakatifu, na zinatueleza kuwa “Yesu ni Mfalme wa wafalme.” Na nyuzi nyekundu zinaiwakilisha damu ya Yesu aliyoimwanga Msalabani. Kama ilivyokwisha elezwa, nyuzi za bluu zinauwakilisha ubatizo wa Yesu aliuopokea toka kwa Yohana Mbatizaji.
Hivyo basi, nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu zinatujulisha juu ya ubatizo wa Yesu, Mungu kufanyika mwili, na kifo chake Msalabani. Kazi za Yesu zilizodhihirishwa katika nyuzi hizi tatu zinatupatia imani inayotuwezesha kwenda mbele za Yehova kwa utakatifu. Hili ndilo fumbo halisi la kiroho la nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu kwamba Yesu, ambaye ni Mungu mwenyewe, alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, alizichukua dhambi za wenye dhambi katika mwili wake kwa kubatizwa, na akabeba adhabu na laana kwa dhambi zote kwa kuimwaga damu yake.
Pengine ulikuwa na mawazo hayo ya mbali ya kuhusu nyuzi za bluu kwamba zinamdhihirisha Mungu na Neno lake. Lakini unapaswa sasa ufahamu vizuri kuwa nyuzi za bluu kwa kweli zinamaanisha ubatizo wa Yesu Kristo. Ubatizo ambao kwa huo Yesu alizibeba dhambi zetu zote ni wa muhimu sana na hauwezi kuachwa katika matendo yake; na kwa hiyo, Mungu anatueleza juu ya umuhimu wake katika Hema Takatifu la Kukutania katika Agano la Kale.
 


Ubatizo Ulikuwa ni Njia Ambayo Yesu Alizibeba Dhambi Zetu

Ubatizo Ulikuwa ni Njia Ambayo Yesu Alizibeba Dhambi ZetuNguzo za ua wa Hema Takatifu la Kukutania zilitengenezwa kwa mbao za Mshita. Vitako vya shaba viliwekwa chini ya nguzo hizi, na vifuniko vya fedha vilivalishwa kwa juu. Hii inatueleza kuwa wenye dhambi ni sharti kwanza wahukumiwe kwa dhambi zao. Ni kwa wale tu waliokwisha hukumiwa kwanza kwa dhambi zao ndio wanaoweza kuokolewa. Kwa hiyo, wale ambao hawajahukumiwa bado ni kweli kwamba hawajaokoka na hawawezi kukwepa bali wanashutumiwa kubeba adhabu ya milele kwa dhambi zao wanapokwenda mbele za Mungu.
Kama ilivyoandikwa, “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti,” (Warumi 6:23) Kwa hakika wenye dhambi watatakiwa kuhukumiwa kwa adhabu ya Mungu inayotisha kwa sababu ya dhambi zao. Kwa hiyo wenye dhambi ni lazima wahukumiwe na Mungu mara moja kwa ajili ya dhambi zao na kisha waishi tena kwa kufunikwa na neema yake. Hii ndiyo maana ya kuzaliwa upya. Imani ya nyuzi za bluu, kwamba Yesu Kristo alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kupitia ubatizo, na imani ya na nyuzi nyekundu kwamba Yesu amewakomboa wenye dhambi wote kwa kuhukumiwa katika Msalaba – Hakuna imani nyingine zaidi ya hii inayotufanya tufe mara moja kwa ajili ya dhambi zetu na kisha kuzaliwa upya. Ni lazima utambue kuwa hukumu ya milele inawasubiri wale tu ambao kwa kutokuamini kwao hawawezi kupita katika hukumu kwa imani.
Ubatizo wa Yesu ulikuwa ni njia ambayo Yesu alizichukua dhambi zetu zote ili aweze kutuokoa toka katika dhambi zetu zote. Yesu alibatizwa na Yohana Mbatizaji ili aweze kuzichukua dhambi katika mwili wake. Yesu ni Mungu mwenyewe lakini ili aweze kutuokoa alikuja hapa Duniani katika mwili wa mwanadamu, akazichukua hatia zote za wenye dhambi katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana Mbatizaji, mwakilishi wa wanadamu, na akahukumiwa kwa haki kwa ajili ya wenye dhambi kwa kuimwaga damu yake na maji pale Msalabani. Lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania linatueleza kwa uwazi na kwa kina juu ya kazi za Yesu ambazo amezitimiza kama Mwokozi wetu. Kupitia lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania, Mungu anatueleza kwa uwazi kuwa Yesu amefanyika Mwokozi wa wenye dhambi.
Kitani safi ya kusokotwa inatuonyesha juu ya Neno la Agano Jipya na Agano la Kale ambalo limeelezwa kwa kina na linakubaliana. Je, ni kwa mchanganyo wa kiasi gani kila msokoto wa uzi ulifumwa na kuungamanishwa ili kuitengeneza kitani hii safi ya kusokotwa? Kupitia kitani safi ya kusokotwa Mungu anatuonyesha kwa kina jinsi alivyotuokoa.
Tunapoliangalia like zulia, tunaliona kuwa limeungamanishwa kwa kufumwa kwa nyuzi mbalimbali. Kama kwa jinsi hii Mungu aliwaambia waisraeli kulitengeneza lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania kwa kufuma nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu kwa kitani safi ya kusokotwa. Hii inatueleza kuwa Yesu aliyekuja kwetu kupitia maji (ubatizo), damu (Msalaba), na Roho Mtakatifu (Yesu ni Mungu), ambavyo vimefichwa katika Neno la Mungu la kutatanisha, ni mlango halisi wa wokovu. Kwa kuwa na imani sahihi katika Yesu Kristo iliyodhihirishwa katika Neno la Mungu lenye utatanishi na kwa kuvishwa katika upendo wake tumeokolewa kikamilifu kwa imani.
Yesu Kristo hakutuokoa sisi bila utaratibu. Tunaweza kuona jambo hili tunapolitazama Hema Takatifu la Kukutania. Yesu amewaokoa wenye dhambi kwa uangalifu. Tunaweza kutambua jambo hili jinsi Yesu alivyowaokoa watu kwa uangalifu wakati tunapozitazama nguzo za uzio. Kwa nini kulikuwa na idadi ya nguzo 60 katika uzio? Ni kwa sababu namba 6 inasimama badala ya mwanadamu na namba tatu inasimama badala ya Mungu. Katika Ufunuo 13, alama ya 666 inaonekana; na Mungu anatuambia kuwa namba hii ni namba ya mnyama na kwamba wenye hekima wanalifahamu fumbo la namba hii. Kwa hiyo, namba 666 inamaanisha kuwa mwanadamu anatenda kama Mungu. Je, mapenzi ya mwanadamu ni yapi? Je, si kujifanya kama kiumbe safi cha kimungu? Kama kweli tunataka kuwa kama viumbe wa kimungu basi tunapaswa kuzaliwa upya kwa kumwamini Yesu na kufanyika wana wa Mungu. Nguzo 60 zinabeba maana hii kwa uangalifu.
Hata hivyo, badala ya kuwa na imani, watu wanatenda tendo baya la kujivuna wanapojaribu kuwa washiriki wa asili ya kimungu kwa juhudi zao wenyewe. Hakuna sababu nyingine zaidi ya hii inayowafanya watu walifafanue Neno kulingana na tamaa za mwanadamu na za kutokuamini katika mawazo yao ya kibinadamu waliyojiundia; watu wa jinsi hii hawana imani bali wana tamaa ambayo inasimama kinyume na Mungu. Kwa sababu ya hii tamaa ya mwili inayojaribu kujifanya timilifu na kufikia ukamilifu wa miili yao, watu wa jinsi hiyo wanaishia wakiwa wameondolewa mbali kutoka katika Neno la Mungu.
 

Neno la Wokovu Limefunuliwa katika Vifaa Vyote vya Hema Takatifu la Kukutania
 
Vyombo na vifaa vyote vya Hema Takatifu la Kukutania vilikuwa ni muhimu sana ili Yesu Kristo aweze kuwaokoa wenye dhambi na kuwavuta waingie katika Mahali Patakatifu. Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ilikuwa ni ya muhimu, birika la kunawia lilikuwa ni la muhimu, na nguzo, vitako vya shaba, vifuniko vya fedha, vitanzi na tepe za fedha vilikuwa ni muhimu. Vitu hivi vyote ni vyombo vinavyopatikana nje ya Mahali Patakatifu, na vifaa vyake vyote vilikuwa ni muhimu katika kumbadili mwenye dhambi kuwa mwenye haki.
Vitu hivi vyote vilikuwa ni vya muhimu katika kuwawezesha wenye dhambi kuingia na kuishi katika Ufalme wa Mungu; lakini kitu cha muhimu sana miongoni mwa hivyo vifaa ilikuwa ni nyuzi za bluu (ubatizo wa Yesu). Nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu zilitumika kulitengeneza lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania. Nyuzi hizi zinatujulisha juu ya kazi tatu za Yesu ambazo tunazihitaji tunapomwamini Mungu. Kwanza, Yesu alikuja ulimwenguni na alizichukua dhambi zetu katika mwili wake katika ubatizo wake; pili, Yesu ni Mungu (Roho); na tatu, Yesu alikufa Msalabani ili kubeba adhabu ya dhambi zote ambazo alizichukua katika mwili wake kupitia ubatizo wa Yohana katika Mto Yordani. Huu ndio mpangilio sahihi wa imani ya kweli inayohitajika kwa wenye dhambi ili waweze kuokolewa na kuwa wenye haki.
Tunapoisoma Biblia, tunaweza kutambua jinsi Bwana wetu alivyo wa kutatanisha. Tunaweza kuona kwa wazi kuwa yeye aliyetuokoa sisi kwa uangalifu mkubwa, msokoto kwa msokoto kama vile ilivyo kwa kitani safi ya kusokotwa, ni Mungu mwenyewe na wala hakuna mwingine. Zaidi ya hayo, Mungu aliwafanya waisraeli kulijenga lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania kwa kufuma nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu juu ya kitani safi iliyokuwa na urefu wa mita 9. Kwa jinsi hiyo, Mungu alihakikisha kuwa kila aliyelitazama Hema Takatifu la Kukutania, hata kama akiwa mbali, angaliweza kulitambua lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania.
Mapazia ya kitani safi nyeupe yaliyokuwa yamening’inizwa katika nguzo za ua wa Hema Takatifu la Kukutania yanadhihirisha utakatifu wa Mungu. Kwa jinsi hiyo, tunaweza kutambua kuwa wenye dhambi hawawezi kamwe kudiriki kulisogelea Hema Takatifu la Kukutania na kwamba wanaweza kuingia katika ua wake pale tu wanapokuwa wameokolewa kwa kuamini katika huduma za Yesu zilizodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu zilizokuwa zimefumwa katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania. Kwa njia hii, Mungu amewawezesha wenye dhambi kufahamu kuwa Yesu Kristo ameziondoa dhambi zao zote na amewaokoa kupitia maji, damu, na Roho Mtakatifu.
Sio tu hayo lakini vifaa vya vyombo vyote ambavyo vinaliunda Hema Takatifu la Kukutania, pamoja na lango la ua wake pia vinatuonyesha Neno la Mungu lenye utatanishi ambalo Mungu alilihitaji ili kuwageuza wenye dhambi kuwa wenye haki. Kwa sababu Mungu aliwaambia waisraeli kulifanya lango la ua wa Hema Takatifu kuwa kubwa ili kila mmoja aweze kuliona, na kwa sababu lango hili lilitengenezwa kwa nyuzi zilizofumwa kiutatanishi za bluu, zambarau na nyekundu juu ya kitani safi ya kusokotwa; Mungu aliwafanya wote kufahamu kwa wazi Neno muhimu linaloweza kuwabadili wenye dhambi kuwa wenye haki.
Lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania linatueleza kuwa Mungu ametuokoa sisi kwa ukamilifu, ambao tulikuwa kama mti wa mshita, kutoka katika dhambi kupitia nyuzi za bluu (ubatizo wa Yesu), na nyuzi nyekundu (damu ya Msalaba), na nyuzi za zambarau (Yesu ni Mungu). Mungu ameazimia kuwa wale wanaoamini vizuri katika ukweli huu wanaweza kuingia Mahali Patakatifu ambapo ni Nyumba ya Mungu.
 
 
Yesu Kristo Anatueleza Sisi
 
Mungu anatueleza sisi kuishi maisha ya kiimani yanayong’aa na kuangaza kama dhahabu; ni sharti tuoshwe dhambi zetu zote kwa kupitia ubatizo wa Yesu na kisha kwenda mbele za Mungu. Hii ndio sababu Mungu mwenyewe alionyesha muundo wa Hema Takatifu la Kukutania kwa Musa, akalijenga kupitia Musa, na akawafanya watu wa Israeli kupokea ondoleo la dhambi kupitia taasisi hii ya Hema Takatifu la Kukutania. Hebu tufanye majumuisho ya imani iliyotuchukua kupitia ua wa Hema Takatifu la Kukutania na katika Mahali Patakatifu. Kupitia ua wa Hema Takatifu la Kukutania, Mungu anaendelea kuzungumza nasi juu ya imani yetu katika ukweli kwamba Yesu ametuokoa kupitia maji, damu, na Roho Mtakatifu. Imani katika lango la ua ambalo lilifumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, katika kitendo cha Kuhani Mkuu kuiweka mikono yake juu ya mwanakondoo wa kuteketezwa na kumwagwa kwa damu ya mwanakondoo huyu wa kuteketezwa, na kwa imani ambayo Kuhani Mkuu aliiosha mikono yake na miguu katika birika—mambo haya yote yanatufahamisha kuwa imani yetu katika injili ya maji na Roho ni imani ya dhahabu halisi inayotuwezesha kuingia na kuishi katika Mahali Patakatifu kwa utukufu.
Kupitia Hema Takatifu la Kukutania, Mungu ameturuhusu sisi sote kuipokea neema ya wokovu na baraka zake. Kupitia Hema Takatifu la Kukutania, tunaweza kuzifahamu baraka ambazo Mungu ametupatia. Tunaweza kutambua na kuamini katika neema ya wokovu ambao umetuwezesha kwenda mbele ya kiti cha enzi cha neema ya Mungu na kisha sisi sote kuokolewa mara moja. Je, unaweza kulitambua hili? Kupitia Hema Takatifu la Kukutania, tunaweza kuona jinsi ambavyo Mungu ametuokoa mimi na wewe kwa ukamilifu, pia tunaweza kuona jinsi Mungu alivyoupanga wokovu wetu kwa utatanishi, na tunaweza kuona jinsi ambavyo hatimaye aliutimiza mpango wa wokovu kulingana na mpango huu na jinsi alivyowabadili wenye dhambi kuwa wenye haki.
Je, kwa namna yoyote ile umekuwa ukimuamini Yesu kimakosa kwa muda wote huu? Je, ulikuwa unaamini kuwa rangi ya bluu inamaanisha anga tu? Je, ulikuwa unafahamu kuwa imani ya zambarau na ya rangi nyekundu, kwamba Yesu Kristo, Mfalme wa wafalme, alikuja hapa duniani na akatuokoa katika Msalaba, na je umekuwa ukiamini hivyo? Kama ndivyo, huu ni wakati wa kuipata imani ya kweli. Ninaamini kuwa wote mtafahamu vizuri juu ya ubatizo wa Yesu, imani ya rangi ya bluu, na kwa hiyo mtaitambua na kuiamini neema ya wokovu isiyopimika ambayo Mungu amewapatia.
Mungu hajatuokoa sisi kupitia damu na Roho Mtakatifu tu. Kwa nini? Kwa sababu Mungu anasema nasi wazi kwa rangi za bluu, zambarau, na nyekundu, na kwa kupitia nyuzi hizi tatu Mungu anatueleza sisi kwa hakika jinsi ambavyo Yesu ametuokoa. Kwa kupitia Hema Takatifu la Kukutania, Mungu wetu ametuonyesha sisi kazi za Yesu za wokovu kwa kina. Baada ya kueleza kupitia Musa kulijenga Hema Takatifu la Kukutania, Mungu aliahidi kuwa atatuokoa katika njia hii. Kama ilivyoahidiwa, Yesu Kristo alikuja katika mwili wa mwanadamu na alizibeba dhambi zetu katika mwili wake kwa kubatizwa katika maji (bluu) ya Mto Yordani. Kwa kupitia ubatizo wake, Yesu amewaokoa wenye dhambi toka katika dhambi zote. Inatatanishaje, jinsi gani ni sahihi, na jinsi gani wokovu wetu ni hakika!
Tunapoingia katika Mahali Patakatifu, tunaweza kuona kinara cha taa, meza ya mkate wa wonyesho, na madhabahu ya uvumba. Kabla ya kuingia Patakatifu pa Patakatifu tunaishi kwa kitambo katika Mahali hapa Patakatifu ambapo panang’aa sana kwa dhahabu, hali tukilishwa kwa mkate wa Neno katika mioyo yetu. Je, hii si baraka nzuri?, Kabla ya kuingia Ufalme wa Mungu, tunaishi katika Kanisa lake kama watu ambao tumeokolewa kikamilifu kwa kuzaliwa upya kupitia injili ya maji na Roho. Kanisa la Mungu linalotupatia mkate wa uzima ni Mahali Patakatifu.
Katika Mahali Patakatifu—ambapo ni, Kanisa la Mungu—kulikuwa na kinara cha taa, meza ya mkate wa wonyesho, na madhabahu ya uvumba. Kinara cha taa pamoja na mpini wake, matawi, bakuli, vifundo cha mapambo, na maua, vilitengenezwa kwa kipande kimoja kwa kuiponda talanta moja ya dhahabu. Kinara cha taa ambacho kilitengenezwa kwa kuiponda talanta moja ya dhahabu safi kinatueleza kuwa sisi wenye haki ni lazima tuungane na Kanisa la Mungu.
Katika meza ya mkate wa wonyesho, uliwekwa mkate usiotiwa chachu, ukimaanisha mkate wa Neno la Mungu halisi ambalo ni safi na huru mbali na ubaya na mafundisho mabaya ya ulimwengu. Mahali Patakatifu pa Mungu—ambapo ni, Kanisa la Mungu—panalihubiri hili Neno safi la Mungu lisilo na chachu, na katika Kanisa hilo watu wanaishi kwa imani safi bila kutenda mabaya mbele za Mungu.
Mbele ya pazia kuelekea Patakatifu pa Patakatifu paliwekwa madhabahu ya uvumba. Katika madhabahu ya uvumba ndipo mahali ambapo maombi yalitolewa kwa Mungu. Kwa kupitia vyombo katika Mahali Patakatifu, Mungu anatueleza kuwa tunapokwenda mbele zake ni sharti tuwe na umoja, imani katika Neno lake safi, na maombi. Ni wenye haki tu wanaoweza kuomba, kwa kuwa Mungu husikiliza maombi ya wenye haki tu (Isaya 59:1-2, Yakobo 5:16). Na ni wale tu wanaomba mbele za Mungu ndio wanaoweza kumuona.
Kwa hiyo, Mahali Patakatifu panatueleza kuwa ni fahari sana kwa sisi kuokolewa katika Kanisa la Mungu. Vifaa vikuu vilivyotumika katika Hema Takatifu la Kukutania—nyuzi za bluu (Yesu alibatizwa), na nyuzi nyekundu (Alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kupitia ubatizo wake, alikufa msalabani na akabeba adhabu ya dhambi zetu), na nyuzi za zambarau (Yesu ni Mungu)—vinatuonyesha juu ya imani ambayo hatuwezi kamwe kushindwa kuwa nayo. Vifaa hivi vitatu ndivyo vinavyoijenga imani yetu yote. Tunapoamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu na Mungu mwenyewe katika uwepo wake, na kwamba ametuokomboa, ndipo tunapoweza kuingia katika Mahali Patakatifu ambapo Mungu anaishi tuking’aa katika dhahabu. Ikiwa hatuamini katika kazi za Yesu ambazo zimedhihirishwa katika nyuzi hizi tatu, basi hatuwezi kamwe kupaingia Mahali Patakatifu hata kama tunamwamini Yesu kwa nguvu. Si Wakristo wote wanaweza kuingia katika Patakatifu pa Patakatifu.
 

Wale Wanaokaa katika Ua wa Hema Takatifu la Kukutania Pamoja na Imani yenye Makosa
 
Siku hizi kuna Wakristo wengi ambao hawawezi kuingia katika Mahali Patakatifu hata pale wanapoikiri imani yao. Kwa maneno mengine kuna watu wengi ambao wanajaribu kuokolewa kwa imani yao yenye upofu. Na hao si wengine bali ni wale wanaofikiri kuwa wanaweza kuokolewa kwa kuamini katika damu ya Yesu Kristo, na kwamba ni Mungu na Mfalme wa wafalme. Wanamwamini Yesu kiurahisirahisi tu. Hali wakiamini katika damu ya Yesu wanasimama mbele ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na wanaomba kwa upofu, “Bwana, mimi bado ni mwenye dhambi leo. Nisamehe Bwana. Ninakushukuru sana Bwana kwa kusulubiwa na kufa kwa ajili yangu. Ee Bwana, ninakupenda!”
Baada ya kufanya hivi nyakati za asubuhi, wanakwenda katika maisha yao ya kila siku na kisha wanarudi tena jioni katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kutoa sala ile ile waliyoitoa asubuhi. Watu wanaoisumbua madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kila asubuhi, jioni, na kila mwezi hawawezi kuzaliwa upya bali wanaangukia katika dhana potofu ya kuamini kulingana na mawazo yao binafsi.
Wanaweka sadaka ya kutekekezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ikiiva kwa miali ya moto na wanatoa sadaka zao kwa moto. Kwa sababu nyama inaungua katika miali ya moto mahali pale, harufu ya nyama inayoungua inasambaa na moshi mweusi na mweupe unaendelea kuongezeka. Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa sio mahali ambapo tunalia tukimuomba Mungu ili azifanye dhambi zetu kuondoka, bali ni mahali ambapo panatukumbusha juu ya moto wa kutisha wa kuzimu.
Hata hivyo, watu hupaendea mahali hapa kila asubuhi na jioni na kusema, “Bwana, nimetenda dhambi. Tafadhali nisamehe dhambi zangu.” Kisha wanarudi nyumbani wakiwa wameridhika kana kwamba wamesamehewa dhambi zao kiukweli. Pia wanaweza hata kuwa na furaha ya kuimba, “♫Nimesamehewa, ♪umesamehewa, ♫sisi sote tumesamehewa.” Lakini hisia za jinsi hiyo ni za kitambo cha muda mfupi tu. Mara baada ya muda mfupi, wanarudia kutenda dhambi tena na wanajikuta wapo mbele ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa mara nyingine tena wakitubu, “Bwana, mimi ni mwenye dhambi.” Wale ambao wanakwenda mara kwa mara katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kila siku pamoja na ukiri wao wa kiimani katika Yesu, bado ni wenye dhambi. Watu wa jinsi hiyo hawawezi kamwe kuingia katika Ufalme Mtakatifu wa Mungu.
Je, ni nani basi anayeweza kupokea ondoleo la dhambi kikamilifu na kuingia katika Mahali Patakatifu pa Mungu? Ni wale ambao wanafahamu na kuamini katika fumbo la nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu zilizowekwa na Mungu. Wale wanaoamini katika hili wanaweza kupita katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa imani yao katika kifo cha Yesu ambaye alizipokea dhambi zao, wanaiosha mikono na miguu yao katika birika la kunawia na hii inawakumbusha kuwa dhambi zao zote zilipelekwa kwa Yesu kupitia ubatizo wake, na kisha wanapaingia Mahali Patakatifu pa Mungu. Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho na wamepokea ondoleo la dhambi wanaingia katika Ufalme wa Mbinguni kwa imani, kwa kuwa imani yao imethibitishwa na Mungu.
Ninatumaini kuwa utatambua na kuamini kuwa maana ya kibiblia ya nyuzi za bluu ni ubatizo wa Yesu. Siku hizi wapo watu wengi wanaodai kumwamini Yesu, lakini ni watu wachache wanaopiga hatua ya kuamini katika maji (nyuzi za bluu), ambao ni ubatizo wa Yesu. Huu ni ukweli wa kina na wa kusikitisha unaoonekana dhahiri. Hii ni sababisho la huzuni kuu kwamba watu wengi wanaiacha imani ya maana sana ya ubatizo toka katika imani yao ya Kikristo, ilhali hata Yesu hakuja tu duniani kama Mungu na sio kuwa alikuja na kufa Msalabani tu bali pia alibatizwa. Ninatumaini na ninaomba kuwa hata sasa, ninyi nyote mtafahamu na kuamini katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na hivyo mtakuwa ndio wale wanaoingia katika Ufalme wa Mungu.
 
 
Ni Lazima Tumwamini Bwana Aliyefunuliwa bkatika Nyuzi za Bluu, Zambarau, na Nyekundu za Hema Takatifu la Kukutania, Ambavyo ni Vitu Halisi Vilivyotuokoa
 
Bwana wetu ametuokoa mimi na wewe. Tunapoliangalia Hema Takatifu la Kukutania, tunaweza kuona jinsi mbinu aliyoitumia Mungu kutuokoa ilivyochanganuliwa kwa uangalifu. Hatuwezi kumshukuru vya kutosha kwa tendo hili la kutuokoa. Tunashukuru sana kwamba Bwana ametuokoa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, na kwamba ametupatia imani inayoamini katika nyuzi hizi za bluu, zambarau, na nyekundu!
Wenye dhambi hawawezi kamwe kuingia katika Mahali Patakatifu kabla ya kuvishwa neema ya Mungu na kupitia adhabu yake ya kutisha kwa dhambi zao. Je, inawezekana kwa wale ambao dhambi zao hazijahukumiwa kuufungua mlango wa Hema Takatifu la Kukutania na kuingia katika Mahali Patakatifu? Haiwezekani! Watu wa jinsi hiyo wanapoingia katika Mahali Patakatifu, watalaaniwa kwa kufanywa vipofu mara baada ya kuiona nuru ya kung’aa. “Aah, mahali hapa panang’aa sana! Uh-oh, inawezekanaje mbona sioni kitu chochote? Nilipokuwa inje nilifikiria kuwa ninaweza kuona kila kitu ndani ya Mahali Patakatifu kwa kule kupaingia tu mahali hapa. Kwa nini sioni kabisa kitu chochote, na kwa nini mahali hapa kuna giza kiasi hiki? Naliweza kuona vizuri nilipokuwa inje ya Mahali Patakatifu… niliambiwa kuwa Mahali Patakatifu ni paangavu; inawezekanaje kuwa mahali hapa pana giza zaidi kiasi hiki?” Hawawezi kuona kwa sababu ni vipofu wa kiroho, kwa sababu hawana imani ya nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu. Kwa hiyo, wenye dhambi hawawezi kamwe kuingia Mahali Patakatifu.
Bwana wetu ametuwezesha kutofanyika vipofu katika Mahali Patakatifu, bali tuweze kuzipokea baraka za kuishi Mahali Patakatifu milele. Kwa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa vinavyopatikana katika kila upande wa Hema Takatifu la Kukutania, Mungu ametueleza sisi kwa ukamilifu njia ya wokovu wetu, na kutokana na Neno hili la unabii, kwa kweli ametukomboa kutoka katika dhambi zetu zote.
Bwana wetu ametuokoa kupitia maji, damu, na Roho Mtakatifu (1 Yohana 5:4-8), ili kwamba tusiwe vipofu bali tuishi milele katika neema yake ya utukufu. Ametuokoa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Bwana wetu ametuahidi sisi kwa Neno la Mungu la kutatanisha, na ametueleza kuwa ametuokoa kwa kuitimiza ahadi hii.
Je, unaamini kuwa wewe na mimi tumeokolewa kupitia kazi za kutatanisha za Yesu zinazodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa? Ndiyo! Je, tumeokolewa bila utaratibu? Hapana! Hatuwezi kuokolewa bila kuamini katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu.
Nyuzi za bluu hazimaanishi Mungu. Zinamaanisha ubatizo wa Yesu ambao kwa huo alizichukua dhambi zote za kila mwenye dhambi ulimwenguni katika Mto Yordani.
Inawezekana kwa watu kusimama mbele ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa bila ya kuamini katika nyuzi za bluu, yaani ubatizo wa Yesu. Watu hao wanaweza kufika hadi kwenye birika la kunawia mara baada ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, lakini hawawezi kuingia katika Mahali Patakatifu ambapo Mungu anaishi. Ni wana wa Mungu tu, yaani wale ambao wamepokea ondoleo la dhambi kwa kuamini kikamilifu katika injili ya maji na Roho ndio ambao wanaweza kuufungua mlango wa Hema Takatifu la Kukutania na kisha kuingia Mahali Patakatifu. Lakini, kwa wale wenye dhambi, bila kujali ni nani, hawawezi kamwe kuingia Mahali Patakatifu. Je, ni umbali gani tunaotakiwa kuufikia ili tuweze kuufikia wokovu? Ukweli ni kuwa, hatuokolewi ati kwa sababu ya kuingia katika ua wa Hema Takatifu la Kukutania, bali pale tunapoingia Mahali Patakatifu ambapo Mungu yupo.
 

Tofauti kati ya Imani Ndani ya Hema Takatifu la Kukutania na Imani Nje ya Hema Takatifu la Kukutania
 
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na birika la kunawia katika ua wa inje wa Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa vyote kwa shaba, na uzio ulitengenezwa kwa mbao, fedha, na shaba. Lakini tunapoingia ndani ya Hema Takatifu la Kukutania, vifaa vilivyotumika ni tofauti kabisa. Tabia kuu ya Hema Takatifu la Kukutania ni kwamba ni “nyumba ya dhahabu.” Kuta zile tatu zilijengwa kwa mbao 48 za mti wa mshita ambazo zote zilifunikwa kwa dhahabu. Meza ya mkate wa wonyesho na madhabahu ya uvumba zilitengenezwa pia kwa mti wa mshita na kufunikwa kwa dhahabu, na kinara cha taa kilitengenezwa kwa kuponda talanta ya dhahabu. Kwa hali hiyo, vyombo vyote ndani ya Mahali Patakatifu vilitengenezwa kwa au kwa kufunikwa kwa dhahabu safi.
Kwa upande mwingine, vitako chini ya mbao vilitengenezwa kwa kitu gani? Vilitengenezwa kwa fedha. Wakati vitako vya nguzo za uzio wa ua wa Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa kwa shaba, vitako vya mbao za Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa kwa fedha. Na wakati nguzo za uzio wa ua zilitengenezwa kwa miti, mbao za Hema Takatifu la Kukutania zilitengenezwa kwa mbao za mshita zilizofunikwa kwa dhahabu. Lakini vitasa vya nguzo tano za mlango wa Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa kwa shaba.
Japokuwa vitako vya mbao za Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa kwa fedha, vitako vya nguzo za mlango wa Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa kwa shaba. Je, hii inamaanisha nini? Inamaanisha kuwa yeyote anayekuja mbele ya uwepo wa Mungu ni lazima ahukumiwe kwa dhambi zake. Je, inawezekanaje sasa kwenda mbele za Mungu wakati tunahukumiwa kifo? Ikiwa sisi wenyewe tutakufa basi hatuwezi kwenda mbele za Mungu.
Kwa kupitia shaba iliyotumika kutengenezea vitako vya nguzo tano za mlango wa Hema Takatifu la Kukutania, Mungu anatueleza kuwa ni lazima tuhukumiwe kwa sababu ya dhambi zetu, Yesu alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake na alihukumiwa kwa ajili ya dhambi hizi badala yetu. Sisi ndio tuliopaswa kuhukumiwa kutokana na dhambi zetu. Lakini mtu fulani alibeba hukumu hii ya dhambi zetu zote kwa jili yetu. Mtu huyu aliyehukumiwa kwa haki na akafa kwa niaba yetu si mwingine bali ni Yesu Kristo.
Imani inayodhihirishwa na nyuzi za bluu ni imani inayoamini kuwa Yesu Kristo alizipokea dhambi zetu zote zilizofikishwa kwake kupitia ubatizo wake na kwamba ametusamehe dhambi zetu zote. Kama vile Mungu alivyoutoa uhai wa Yesu Kristo kwa ajili ya adhabu ya dhambi zetu zote ambazo zilifikishwa kwa Yesu kupitia ubatizo, na kuwa ametatua tatizo la dhambi zetu zote, basi hatuikabili kamwe hukumu ya dhambi zetu. Imani inayodhihirishwa na nyuzi nyekundu ni imani katika damu ya Yesu aliyoimwaga pale Msalabani. Imani hii inaamini kuwa Yesu Kristo alibeba hukumu na adhabu ya dhambi zetu ambayo tulistahili kuikabili.
Wale tu ambao wamezipeleka dhambi zao zote kwa Yesu kwa kuamini katika ubatizo wake, na kwamba wamekwisha hukumiwa kutokana na dhambi zao zote kwa kuiamini damu ya Yesu Kristo ambayo aliimwaga pale Msalabani kwa kifo cha mwili wake kwa ajili ya dhambi hizi zote, wanaweza kuingia Mahali patakatifu. Hii ndiyo sababu vitako vya mlango wa Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa kwa shaba. Kwa jinsi hiyo, ni lazima tuiamini damu ya Kristo ambaye alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake na kisha akahukumiwa adhabu kwa ajili yetu.
Mungu ameazimia kuwa wale tu ambao wanahakika ya ukweli kuwa Yesu Kristo ambaye amewaokoa ni Mungu mwenyewe (nyuzi za zambarau), wale wanaoamini katika ubatizo wa Yesu (nyuzi za bluu), na wale wanaona ukweli kuwa Yesu alihukumiwa na kuadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao (nyuzi nyekundu) wanaweza kuingia Mahali Pakatifu. Mungu amewaruhusu wale tu ambao wamehukumiwa mara moja kwa ajili ya dhambi zao kwa kumwamini Yesu, na ambao wanaamini kuwa Yesu amewaokoa kutoka katika dhambi zao zote kupaingia Mahali Patakatifu.
Vitako vya nguzo za mlango wa Hema Takatifu la Kukutania vilitengenezwa kutokana na shaba. Vitako vya shaba vina maana ya kiroho kwamba Mungu amewaruhusu wenye dhambi ambao wanazaliwa kama wana wa Adamu kupaingia Mahali Patakatifu, ambapo ni makazi yake, pale tu bila kujali ni akina nani, wanapokuwa na imani ya nyuzi za bluu (ubatizo wa Yesu), na nyuzi nyekundu (hukumu ya haki ya Yesu kwa niaba ya wenye dhambi), na nyuzi za zambarau (Yesu ni Mungu mwenyewe). Ukweli kuwa vitako vitano vya nguzo za mlango viliundwa kwa shaba unatueleza juu ya injili ya Mungu, kwamba kama ilivyoandikwa katika Warumi 6:23, “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu,” Yesu amezisamehe dhambi zetu zote kwa maji, damu, na kwa Roho.
 

Tusidharau Bali Tuliamini Neno na Tumwamini Mungu
 
Kumwamini Yesu hakumaanishi kuwa unaokolewa bila kanuni. Na wala kuhudhuria ibada Kanisani kwako hakumaanishi kuwa umezaliwa upya bila kanuni. Katika Yohana 3 Bwana wetu anasema kwamba ni wale tu wanaozaliwa upya kwa maji na kwa Roho wanaweza kuona na kuingia katika Ufalme wa Mungu. Kwa uhakika Yesu alimwambia Nikodemo, aliyekuwa kiongozi wa Wayahudi na mwamini wa Mungu, “Wewe ni mwalimu wa Wayahudi, na bado hufahamu jinsi ya kuzaliwa upya? Ni pale tu mtu anapozaliwa upya kwa maji na kwa Roho ndipo mtu huyo anaweza kuuona na kuuingia Ufalme wa Mungu.” Watu wanaomwamini Yesu Kristo wanaweza kuzaliwa upya pale tu wanapokuwa na imani ya nyuzi za bluu (Yesu alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake mara moja pale alipobatizwa), na nyuzi nyekundu (Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu), na nyuzi za zambarau (Yesu ni Mwokozi, ni Mungu na ni Mwana wa Mungu). Kwa hiyo, kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu zinazopatikana katika kila upande wa Hema Takatifu la Kukutania, wenye dhambi zote ni sharti waamini kuwa Yesu ni Mwokozi wa wenye dhambi.
Ni kwa sababu watu wengi wanamwamini Yesu bila kuuamini ukweli huu kwamba hawawezi kuzaliwa upya wala kulifahamu Neno la Mungu la kuzaliwa upya. Bwana wetu ametueleza wazi kuwa kama tukikiri kumwamini Yesu, na kama hatujazaliwa upya, basi hatuwezi kamwe kuingia Mahali Patakatifu, ambapo ni Ufalme wa Baba, na wala hatuwezi kuishi maisha sahihi ya kiimani.
Katika mawazo yetu ya kibinadamu, tunaweza kufurahishwa iwapo wakristo wote wangethibitishwa kuwa wamezaliwa upya bila ya kujali wanachokiamini. Je, si ndivyo? Kama tungekuwa tunaokolewa kwa kuliitia jina la Yesu na kuikiri imani yetu katika yeye kwa maneno tu bila hata ya kufahamu mambo muhimu aliyoyafanya kumuokoa mwanadamu, bila shaka watu wangeona ni rahisi sana kumwamini Yesu. Tunaweza kumshukuru Yesu kila tunapokutana na mkristo mpya, akiimba, “♫Nimesamehewa; ♪Umesamehewa; ♫sisi sote tumesamehewa.” “Kwa kuwa kuna waamini wengi, je ni alama gani ya ushuhuda? Maana mambo yanaonekana mazuri kama yalivyo. Je, hili si jambo la kushangaza na kufurahisha?” kama ingelikuwa hivi, watu wangefikiri juu ya wokovu kiurahisi, ukizingatia kuwa yeyote atakayeliitia jina la Bwana ataokoka, na kwamba wokovu wao utakuja hata kama wanaishi vyovyote vile wapendavyo. Lakini Mungu alitueleza kuwa hatuwezi kuzaliwa upya kwa imani potofu ya jinsi hiyo. Kinyume chake, Mungu alituambia kuwa wale wanaodai kuwa wameokolewa hata bila ya kuifahamu injili ya maji na Roho wote wanaihalifu sheria.
 

Kinachozaliwa Upya ni Roho Yako sio Mwili Wako.
 
Yesu alifanyika mwanadamu, akaja hapa duniani, na ametuokoa kupitia injili ya maji na Roho. Yusufu, baba yake wa Yesu wa kufikia alikuwa ni seremala (Mathayo 13:55), na Yesu aliitumikia familia yake chini ya baba huyu seremala, Yesu mwenyewe alifanya kazi kama seremala kwa miaka 29 ya kwanza ya maisha yake. Lakini alipofikisha miaka 30, aliianza kazi yake ya kimungu ambayo ni kutekeleza huduma katika jamii.
Kwa vile Yesu alikuwa na asili zote mbili, yaani asili ya kimungu na asili ya kibinadamu, sisi wenye haki tuliozaliwa upya pia tuna asili mbili tofauti. Tuna asili ya mwili na asili ya Roho. Hata hivyo, mtu anapokiri kuwa anamwamini Yesu wakati Roho yake haijazaliwa upya, basi mtu huyu hajazaliwa upya―hii ni kusema kuwa, mtu huyu hana Roho iliyozaliwa upya. Ikiwa mtu anajaribu kumwamini Yesu bila kuzaliwa upya katika Roho yake, basi mtu huyu ni yule anayejaribu kuzaliwa upya katika mwili kama ilivyokuwa kwa Nikodemo, na kwa jinsi hiyo ni mtu ambaye kamwe hajazaliwa upya. Japokuwa Yesu alikuwa ni Mungu bila shaka alikuwa pia katika mwili wa mwanadamu wenye madhaifu mengi. Kwa hiyo, tunaposema kuwa tumezaliwa upya, inamaanisha kuwa Roho zetu zimezaliwa upya na sio miili yetu.
Ikiwa wale wote wanaokiri kumwamini Yesu wangekuwa wamezaliwa upya, Ningejitahidi kujulikana kama mchungaji mwema. Kwa sababu gani? Kwa sababu nisingekuwa nachukizwa na wale ambao hawauamini ukweli, na kwa hivyo nisingekuwa butu sana katika mahubiri yangu nikitumaini kuwa watakuja kuufahamu ukweli. Ningejulikana kama mchungaji mwenye adabu, mwema, na mzuri, hali nikiwaeleza watu jinsi wanavyoweza kuwa watakatifu katika miili yao. Kwa kweli, ninaweza kuupamba mwonekano wangu kama hivyo, lakini mimi sifanyi hivyo kamwe. Sio kwa sababu sina uwezo wa kukupandikizia katika mawazo yako mtazamo wa, “Mchungaji huyu anaifuatisha sura takatifu na yenye huruma ya Yesu.” Ni kwa sababu mwili wa mwanadamu hauwezi kubadilika, na kwa sababu kuwa mpole kiasi, mwema, mwenye huruma katika mwili hakumaanishi kuwa mtu huyu ni mwenye haki aliyezaliwa upya. Hakuna anayeweza kuzaliwa upya katika mwili. Ni Roho, ambayo ni sehemu nyingine ya mwanadamu ambayo ni lazima izaliwe upya kwa kuliamini Neno la Mungu.
Unapomwamini Yesu, ni lazima uufahamu ukweli. “Mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:32). Ni ukweli wa Mungu tu unaotufanya tuzaliwe upya, unaoziweka huru nafsi zetu toka katika kifungo cha dhambi, na unatufanya tuzaliwe upya kama wenye haki. Ni pale tu tunapofahamu, amini, na kuihubiri Biblia kiusahihi ndipo tunapoweza kuingia Mahali Patakatifu na kuishi maisha yetu katika imani ya kweli na kisha kukiendea kiti cha Rehema cha Mtakatifu wa Watakatifu. Injili ya maji na Roho inayozifanya nafsi zetu kuzaliwa upya ndio ukweli, na imani yetu katika imani hii inatufanya tusamehewe dhambi zetu zote na inaturuhusu kuishi katika himaya ya kiimani pamoja na Mungu. Injili ya maji na Roho iliyo katika mioyo yetu inatuwezesha kuishi kama watoto wa Mungu tuliozaliwa upya katika himaya ya kiroho inayong’aa pamoja na Bwana katika furaha.
Kumwamini Yesu katika upofu ni imani isiyo sahihi. Ukiangalia katika mtazamo wa kibinadamu, nina mapungufu mengi. Sizungumzi hivi kwa midomo tu, bali ninapofanya jambo fulani, ndipo ninapotambua kwamba nina mapungufu mengi. Kwa mfano, ninapojiandaa kwa ajili ya kambi la kibiblia ili kwamba washiriki watakatifu na wageni waweze kulisikia Neno kwa raha, waweze kuvutiwa katika mioyo yao kwa neema ya Mungu, waweze kupokea baraka ya kuzaliwa upya, na kisha warudi wakiwa wamepumzika kimwili na kiroho, ndipo ninapojikuta kuwa kuna mambo mengi ambayo nilishindwa kufikiria na kuyatayarisha kabla ya siku ya tukio. Vitu ambavyo vingeweza kutekelezwa kwa kuongeza kiwango cha kufikiria na umakini huonekana baada ya kuwa matayarisho yote yamekwisha fanyika muda mfupi kabla ya kuanza kambi ya kibiblia. Huwa ninashangaa, kwa nini sikufikiria juu ya hivyo vitu vidogo na kuviandaa mapema? Ikiwa ningelifikiria kwa kina kidogo na kwa uangalifu katika kuipanga kambi ya kibiblia, watakatifu na nafsi mpya wangeliweza kulisikia Neno vizuri, wangeokoka, na wangekuwa wametumia muda wao vizuri. Pia ninapofanya kazi siku nzima, kwa sababu ya ukosefu wa utendaji bora kwa upande wangu, kuna nyakati nyingi ambapo matokeo ya kazi husika hayalingani na juhudi zangu. Mimi binafsi ninatambua wazi kuwa nina mapungufu mengi.
“Kwa nini sifanyi jambo hili? Kwa nini sikufikiria juu ya jambo hili? Nilichotakiwa kukifanya ilikuwa ni kuwa makini zaidi, lakini kwa nini sikuweza kuwa makini zaidi, na kwa nini siwezi kuwa makini zaidi” Ninapohuduma katika injili ndipo ninapotambua kuwa nina mapungufu ya mara kwa mara. Ndipo mimi mwenyewe ninapotambua na kukiri, “Hivi ndivyo nilivyo, hivi ndivyo nilivyo mwenye mapungufu.” Sizungumzi hivi kwa midomo yangu tu, na sijifanyi kuwa muungwana, bali ni mtu ambaye wakati mwingine ninashindwa kuungamanisha mambo madogo na hivyo kuyafanya mambo kwenda bila utaratibu. Ninapojitazama mimi mwenyewe, kwa hakika ndipo ninapoyaona mapungufu yangu mengi.
 


Tunaupokea Utakatifu Kupitia Imani ya Uzi wa Bluu

 
Watu wanapojifikiria wenyewe, wanahisi kuwa wanaweza kufanya kila kitu vizuri bila kufanya makosa yoyote. Lakini wanapolitatua jukumu, ndipo umashuhuri wao na mapungufu yao yanapodhihirika kwa wazi. Ndipo wanapogundua kuwa kwa kweli hawajitoshelezi na kwamba hawana msaada bali ni kutenda dhambi na kufanya makosa. Pia, watu wanapofikiria kuwa wanaendelea vizuri, wanajidanganya wenyewe kuwa wanaenda katika Ufalme wa Mungu kwa sababu ya jinsi imani yao ilivyo nzuri.
Lakini mwili haubadiliki kamwe. Hakuna mwili usio na mapungufu, na mara nyingi mwili hufanya mabaya na unadhihirisha mapungufu yake. Ikiwa, kwa uwezekano wowote, unafikiria kuwa utaingia katika Ufalme wa Bwana wetu kwa sababu ya mambo mazuri ambayo mwili wako umeyatenda, ni lazima utambue kuwa haijalishi jinsi ambavyo mwili wako umefanya vizuri, ni jambo lisilo na maana mbele za Mungu. Kitu pekee kinachotuwezesha kuingia Ufalme wa Bwana ni imani yetu katika Neno la kweli―nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, na kwamba Bwana ametuokoa. Kwa sababu Bwana wetu ametuokoa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, tunaweza kupangia Mahali Pakatifu kwa kule kuamini tu katika ukweli huu.
Ikiwa Mungu asingelituokoa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, sisi sote tusingeliweza kuingia Mahali Patakatifu. Hata kama imani yetu ina nguvu kiasi gani bado hatuwezi kupaingia Mahali Pakatifu. Kwa nini? Kwa sababu ikiwa ingekuwa ni kesi, ingemaanisha kuwa imani yetu ya mwili inatakiwa kuwa nzuri kila siku ili tuweze kupaingia. Ikiwa tunaweza kuungia Ufalme wa Mungu pale tu imani yetu inapokuwa nzuri kila siku, je itakuwaje kwetu sisi ambao miili yetu ni midhaifu kila siku? Je, tunawezaje kuifanya imani yetu kuwa nzuri ili kuuingia Ufalme wa Mungu pale inapokuwa hakuna njia kwa sisi wenyewe kupokea ondoleo la dhambi, na tunapokuwa hatuna imani ya kuweza kugeuka pale tunapofanya dhambi kila siku? Itaibidi miili yetu iwe miili mitakatifu ambayo haitendi dhambi kabisa au itatulazimu kutoa maombi yetu ya toba na kufunga kila siku, lakini ni nani ambaye mwili wake ni mtakatifu na anayeweza kufanya hivyo?
Ikiwa Mungu asingalituokoa sisi kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, asingelikuwepo hata mmoja ambaye angaliweza kuingia Ufalme wa Mungu. Jinsi tulivyo ni kuwa imani yetu inaweza kuwa nzuri kwa kitambo tu na inaweza kupotea kitambo kinachofuata. Wakati imani yetu inapokuwa nzuri na inapopotea kwa kitambo tunachanganyikiwa tukijiuliza ikiwa tuna imani au la, na mara nyingi tunaishia kwa kuipoteza hata ile imani nzuri tuliyokuwa nayo. Hatimaye, tunakuwa wenye dhambi zaidi baada ya kuwa tumekwisha mwamini Yesu. Lakini Yesu ametuokoa sisi kikamilifu, wenye dhambi, kwa mujibu wa mpango wake wa wokovu unaodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Ametupatia ondoleo la dhambi zetu.
Ni pale tu tunapokuwa na ushahidi huu ndipo tunapoweza kukivaa kisahani cha dhahabu, “utakatifu kwa Bwana,” katika kilemba chetu kama Kuhani Mkuu (Kutoka 28:36-38). Ndipo tunapoweza kuuendeleza ukuhani wetu. Wale wanaoweza kuushuhudia “utakatifu kwa Bwana” kwa watu wanapomtumikia kama makuhani ni wale ambao wanao ushahidi katika mioyo yao kwamba wamepokea ondoleo la dhambi kupitia injili ya maji na Roho.
Kisahani cha dhahabu kilifungwa katika kilemba cha Kuhani Mkuu, na utepe uliokifunga kisahani hiki katika kilemba ulikuwa na rangi ya bluu. Kwa nini Mungu aliamuru kilemba kifungwe kwa utepe wa bluu? Kilichohitajika kwa Bwana wetu ili aweze kutuokoa ilikuwa ni uzi wa bluu, na uzi huu wa bluu unamaanisha ubatizo wa Yesu ambao kwa huo alizipokea dhambi zetu zote katika mwili wake. Ikiwa Bwana asingeliziondoa dhambi zetu kwa kuzichukua katika mwili wake katika Agano Jipya kupitia ubatizo wake, kwa muundo ule ule wa Agano la Kale wa kuiweka mikono juu ya mwanasadaka wa kuteketezwa, hatuwezi kuupokea utakatifu toka kwa Yehova hata kama tunamwamini Yesu kwa kiasi gani. Na hii ndiyo sababu kisahani cha dhahabu kilifungwa katika kilemba kwa utepe bluu. Wote wanaomuona Kuhani Mkuu akiwa na kisahani cha dhahabu kilichoandikiwa “utakatifu kwa Bwana” wakumbuke kuwa wanatakiwa kuwa watakatifu mbele za Mungu kwa kupokea ondoleo la dhambi zao. Hii inawafanya watu wafikiri jinsi wanavyoweza kuwa watakatifu mbele za Mungu.
Sisi nasi tunapaswa kujikumbusha jinsi ambavyo tumefanyika wenye haki. Je, tumewezaje kuwa wenye haki? Hebu tusome Mathayo 3:15. “Yesu akajibu akamwambia [Yohana], ‘Kubali hivi sasa, kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote.’ Basi akamkubali.” Yesu ametuokoa sisi sote toka katika dhambi zetu kwa kubatizwa. Kwa kuwa Yesu alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa ubatizo wake, wale wanaoamini katika ubatizo huo hawana dhambi. Ikiwa Yesu asingelibatizwa, tungethubutuje kusema kuwa hatuna dhambi? Je, umepokea ondoleo la dhambi kwa ukiri wako wa imani katika kifo cha Yesu Msalabani kwa machozi katika macho yako? Wapo watu wengi ambao wanaona vigumu kusikitishwa na kifo cha Yesu, mtu ambaye hawana uhusiano naye kwa njia yoyote, ndipo wanapojaribu kukamua machozi kwa kuwakumbuka mababu zao waliokufa zamani, au magumu waliyokuwa nayo walipougua, au magumu na mateso ya miaka iliyopita. Ikiwa unalia kwa kukumbuka mambo kama hayo au unalia kwa kusikitishwa kwa kusulubiwa kwa Yesu ukweli ni kuwa dhambi zako haziwezi kuondolea kwa jinsi hii.
Kama vile kisahani cha dhahabu kilichoandikwa “utakatifu kwa Bwana” kilifungwa kwa utepe wa bluu katika kilemba cha Kuhani Mkuu, basi kinachoziondoa dhambi zetu na kutufanya watakatifu ni ubatizo wa Yesu. Mioyo yetu ilipokea ondoleo la dhambi kwa sababu Yesu alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo, kwa sababu Yehova alizibebesha dhambi zetu zote juu yake, na kwa sababu hiyo dhambi zote za ulimwengu zilipitishwa kwa Yesu kupitia ubatizo wake. Haijalishi ni kwa kiasi gani mioyo yetu inaweza kuwa na hisia mbaya, na haijalishi ni kwa kiwango gani matendo yetu yanaweza kuwa mabaya, tumefanyika wenye haki na tumeokolewa kikamilifu kwa Neno la nyuzi za bluu lililoandikwa katika Biblia. Tunapouangalia mwili wetu, hatuwezi kuheshimiwa, lakini kwa sababu imani ya nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu imo katika mioyo yetu—kwamba, kwa sababu tunayo injili sahihi ya maji na Roho inayotuambia kuwa Yesu alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kupitia ubatizo na akabeba adhabu yetu Msalabani—tunaweza kwa ujasiri na uthabiti kuongea kuhusu injili hii. Ni kwa sababu tunayo injili ya maji na Roho kwamba tunaweza kuishi kwa imani yetu kama wenye haki, na pia tunaweza kuhubiri imani hii ya haki kwa watu wengine.
Hatuwezi kutoa shukrani za kutosha kwa neema ya Bwana wetu. Kwa kuwa wokovu wetu haukuja bila utaratibu, basi tunamshukuru Bwana wetu kwa huo. Wokovu tulioupokea si wa mchezo kwamba kila mtu anaweza kuupokea hata kama haamini ipasavyo. Kumuita Bwana kwa mawazo binafsi, “Bwana Bwana,” hakumaanishi kuwa kila mtu anayefanya hivyo anaweza kuokoka. Kwa kuwa tunaushahidi katika mioyo yetu kuwa dhambi zetu zimepotea kupitia injili ya maji ya Roho, tunamshukuru sana Bwana kwa wokovu wake mkuu kwamba ametuokoa kikamilifu kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa.
Biblia inatueleza kuwa yeyote anayemwamini Yesu Kristo Mwana wa Mungu anao ushahidi katika moyo wake (1 Yohana 5:10). Ikiwa hakuna ushahidi katika mioyo yetu tutakuwa tukimfanya Mungu kuwa mwongo, na hivyo ni lazima wote tuwe na ushuhuda wa mwisho katika mioyo yetu. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kuwa na shida ikiwa baadhi ya watu watakupa changamoto kwa kusema, “Nionyeshe ushahidi kuwa umeokolewa. Unasema kuwa watu wanapopokea ondoleo la dhambi, wanampokea Roho Mtakatifu kama karama, na kwamba kuna ushahidi wa wazi wa wokovu. Nionyeshe ushahidi huu.” Unaweza kunionyesha ushahidi kwa kujiamini kama ifuatavyo: “Mimi ninayo ndani yangu injili ya maji na Roho ambayo kwa hiyo Yesu ameniokoa kikamilifu. Kwa sababu nimeokolewa kikamilifu na Yesu, sina dhambi.”
Ikiwa hauna uthibitisho wa wokovu wako katika moyo wako, basi haujaokolewa. Haijalishi ni kwa kiwango gani watu wanamwamini Yesu, imani tu haiukamilishi wokovu wao. Huo ni kama vile upendo usio na majibu. Ni upendo ambao haujishughulishi na jinsi ambavyo mtu mwingine anajihisi. Wakati mtu fulani ambaye hatuwezi kumpenda ana moyo wa kuhangaika, akitegemea kitu fulani toka kwetu, mtu wa jinsi hiyo anajisikia upendo, na anatuangalia kana kwamba anayetaka kupendwa, hii haimaanishi kuwa tutapaswa kumpenda pia. Vivyo hivyo, Mungu hawakumbatii katika mikono yake wale ambao hawajapokea ondoleo la dhambi zao eti kwa sababu tu mioyo yao inahangaika kumtafuta Mungu.
Tunapompenda Mungu, ni lazima tumpende kwa kuliamini Neno lake katika kweli. Upendo wetu kwake usiwe wa upande mmoja. Ni lazima tumueleza Mungu juu ya upendo wetu kwake, na ni lazima tutafute kwanza uhakika ili kufahamu ikiwa Mungu anatupenda kabla ya kumpenda yeye. Ikiwa tutatoa upendo wetu kwa mtu mwingine ambaye hatupendi tutaishia kuvunjika moyo.
Bwana wetu ametufunika katika utukufu wa wokovu toka katika dhambi zetu ili tusiweze kuhukumiwa kwa sababu ya dhambi zetu. Ameturuhusu kuingia katika Ufalme wa Mungu na kuishi pamoja na Mungu, na ametupatia karama inayotuwezesha kupokea ondoleo la dhambi kupitia neema ya Mungu. Wokovu wa Mungu umetuletea baraka nyingi za kiroho zisizohesabika za Mbinguni. Kwa maneno mengine, wokovu huu pekee ambao Mungu ametupatia umetuwezesha kupokea baraka hizi zote toka kwake.
 

Wokovu Ambao Yesu Mwenyewe Ametuletea
 
Bwana wetu ametuokoa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu. Ametupatia wokovu uliofanywa kwa nyuzi tatu tofauti. Wokovu huu wa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu si kitu kingine bali ni karama ya wokovu iliyotolewa na Mungu. Ni karama hii ya wokovu inayotuwezesha sisi kuingia na kuishi katika Mahali Patakatifu.
Injili ya maji na Roho imetubadilisha wewe na mimi kuwa wenye haki. Imeturuhusu kuingia katika Kanisa la Mungu na kuishi maisha ya usafi. Na injili ya kweli imetuwezesha kujilisha katika Neno la Mungu la kiroho na kuipokea neema yake. Imeturuhusu pia kwenda mbele ya kiti cha neema cha Mungu na kuomba, na kwa jinsi hiyo imetupatia imani ambayo kwa hiyo twaweza kuichukua neema ya Mungu aliyotupatia kama mali yetu. Kwa wokovu wetu pekee, Mungu amezifanya baraka kuu kuwa mali yetu. Hii ndiyo sababu inayoufanya wokovu kuwa wa thamani sana.
Yesu alituambia kuzijenga nyumba zetu za imani katika mwamba (Mathayo 7:24). Mwamba huu si mwingine bali ni wokovu wetu unaokuja kupitia injili ya maji na Roho. Kwa hiyo, inatupasa sisi sote kuishi maisha yetu ya kiimani kwa kuokolewa―kufanyika wenye haki kwa kuokolewa na kuyafurahia maisha ya mile le kwa kuokolewa, na kuingia Mbinguni kwa kuokolewa.
Nyakati za mwisho za ulimwengu huu zinatukaribia. Kwa hiyo, katika nyakati hizi, watu wanasababu za msingi za kuokolewa kwa Neno sahihi. Kuna baadhi ya watu wanaosema kuwa mtu anaweza kuokolewa kwa kumwamini Yesu tu bila ya kuifahamu imani ya nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, na kwamba hakuna sababu ya kuzungumzia juu ya maisha ya kiimani, kwa sababu inatosha kwa mtu kuokolewa katika njia ya kawaida.
Hata hivyo, sababu inayonifanya nirudie sana kuongelea jambo hili ni kuwa ni wale tu waliopokea ondoleo la dhambi katika mioyo yao ndio wanaoweza kuishi maisha yao ya imani ambayo Mungu anayakubali. Kwa sababu moyo wa kila mtakatifu aliyepokea ondoleo la dhambi ni hekalu takatifu ambalo Roho Mtakatifu anakaa, hivyo mtakatifu huyo anatakiwa kuishi maisha ya imani ili asiweze kuuchafua utakatifu huu.
Wenye haki wanaishije maisha yao kwa viwango tofauti na vile ambavyo wenye dhambi wanaishi. Kutokana na msimamo wa Mungu, jinsi ambavyo wenye dhambi wanaishi ni chini kabisa ya kiwango chake. Maisha yao yamejazwa na unafiki tu. Wanajitahidi sana kuishi kwa mujibu wa Sheria. Wanajiwekea utaratibu na viwango vyao vinavyowaongoza jinsi ya kutembea, jinsi ya kuishi, jinsi ya kuongea, na jinsi ya kucheka.
Lakini mambo kama haya yameondolewa mbali toka katika maisha ya kiimani ambayo wenye haki wanaishi. Mungu anawaeleza wenye haki kwa wazi na kwa kina, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na nguvu zako zote na mpende jirani yako kama nafsi yako.” Huu ni mfano wa maisha ambao Mungu amewapatia wenye haki. Ni sahihi kwetu wenye haki kuishi maisha yetu kwa kumpenda Mungu kwa mioyo yetu yote, na kufuata matakwa yake kwa nguvu zetu zote. Ili kuwatumikia majirani ni lazima tuwekeze bila kuhesabu katika huduma ya Mungu. Na haya ndiyo maisha ya Wakristo.
Ikiwa tutabakia katika hatua ambayo tunafikiri kuwa kwa namna yoyote hatutendi dhambi, basi hatuwezi kuyafuata maisha ya uaminifu ya Wakristo waliozaliwa upya. Kabla sijazaliwa upya, niliishi maisha ya kujitakia haki katika dhehebu la kihafidhina la Presibeterian, na kwa hiyo kwa mujibu wa maisha ya kisheria, nilijitahidi kufuata sheria kwa mapana yake. Siku hizi watu hawafanyi hivyo kamwe, lakini kwa sababu nimekuwa nikiyaongoza maisha yangu ya kidini kwa muda mrefu, ninaweza kabisa kuifuata Sheria katika maisha yangu ya kila siku. Niliiheshimu sana sheria kiasi kwamba sikufanya kazi katika siku ya Bwana, kwa maana Sheria inaamuru kuwa tuikumbuke Sabato na kuitakasa, kwa hali hiyo sikuweza kabisa hata kupanda gari siku za Jumapili. Ikiwa ningekuambia kuishi kama nilivyoishi kwa hakika kusingepatikana hata mmoja ambaye angeweza kuishi maisha ya kisheria kama yale. Hivi ndivyo ambayo maisha yangu ya kisheria yalivyokuwa kabla sijazaliwa upya. Hata hivyo, haijalishi ni kwa kiwango gani nilitumia ili kuishi kiutakatifu katika siku zangu za kidini kwani jitihada hizo zote hazina lolote la maana mbele za Mungu na haziendani na mapenzi ya Mungu.
Ndugu wasomaji, je mnayo imani ya nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu? Kwa sababu wokovu wa Yesu umo katika nyuzi hizi tatu, basi tunaweza kuingia Mahali Patakatifu kwa imani yetu. Wokovu wetu ulitimizwa miaka 2,000 iliyopita. Hata kabla hatujatokea kumfahamu, Yesu Kristo alikwisha zichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa kubatizwa na akabeba adhabu ya dhambi zetu kwa kufa Msalabani.
 

Wokovu Toka Katika Dhambi Umo Katika Yesu Kristo
 
Wakati wale ambao hawajazaliwa mara ya pili wanaingia katika Hema Takatifu la Kukutania, hawaingii kupitia lango la ua wake bali wanauparamia uzio isivyo haki. Wanasema, “Kwa nini kitani safi ya uzio ni nyeupe kiasi hicho? Inatupatia mzigo sana kuitazama. Walipaswa kuipaka rangi nyingine ama nyekundu au ya bluu. Na hizo ndizo za kisasa katika zama hizi. Lakini uzio huu ni mweupe mno! Unashikamana kwa haraka sana. Na kwa nini ni mrefu sana kiasi hiki? Ni zaidi ya mita 2.25 (ambazo ni sawa na futi 7.5). Urefu wangu binafsi haufikii mita 2; je, nitatakiwaje kuingia ndani ya uzio huu wakati uzio huu ni mrefu mno? Safi, nitaupanda uzio huu kwa kutumia ngazi!”
Watu wa jinsi hiyo wanajitahidi kuingia Mahali Patakatifu kwa kutumainia matendo yao mema. Wanaupandia uzio wa ua wa Hema Takatifu la Kukutania kwa matoleo yao, kazi za misaada, na uvumilivu, na wanauruka uzio wakisema, “Kwa hakika ninaweza kuuruka urefu wa mita 2.25 (futi 7.5) kwa njia yoyote.” Hivyo baada ya kuwa wamerukia ndani ya ua wa Hema Takatifu la Kukutania, wanaangalia nyuma yao na wanaona madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Kisha wanaacha kuiangalia madhabahu na wanaelekeza macho yao kupaangalia Mahali Patakatifu, na kitu cha kwanza wanachokiona ni birika la kunawia likiwa mbele ya Mahali Patakatifu.
Urefu wa nguzo za uzio wa ua wa Hema Takatifu la Kukutania ni mita 2.25 (futi 7.5), lakini urefu wa nguzo na kitanzi cha mlango wa Mahali Patakatifu ambapo Mungu anaishi ni mita 4.5 (futi 15). Watu wanaweza kuingia katika ua wa Hema Takatifu la Kukutania kwa hiari yao wenyewe kama wana dhamira ya kutosha. Lakini hata kama wakiuruka uzio wa mita 2.25 (futi 7.5) na kuingia katika ua wa Hema Takatifu la Kukutania, wanapajaribu kuingia mahali ambapo Mungu anaishi watakutana na nguzo zenye urefu wa mita 4.5 (futi 15) na kitanzi cha mlango wa Mahali Patakatifu. Watu wanaweza kuuruka urefu wa mita 2.5 (futi 8.3) kwa jitihada zao binafsi. Lakini hawawezi kuruka zaidi ya mita 4.5 (futi 15) uliowekwa na Mungu. Huu ndio ukomo wao.
Hii inamaanisha kuwa tunapomwamini Yesu kwa mara ya kwanza, tunaweza kuamini kama ni sehemu ya dini tu. Pia baadhi ya watu wanaweza kumwamini Yesu kama Mwokozi kwa hiari yao wenyewe, na wanaweza kuamini kuwa Mwokozi ni miongoni mwa wenye hekima wakuu wanne. Bila ya kujalisha jinsi watu wanavyoamini, wanaweza kuwa na imani yao wanayoichagua, lakini hawawezi kuzaliwa kweli kwa upya kupitia imani za jinsi hiyo.
Ili kuzaliwa kweli upya, ni lazima wapitie lango la nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu kwa imani yao. Tunazaliwa upya mbele za Mungu kwa kuamini kuwa Yesu ni Mwokozi wetu na mlango wa ukweli, na kwamba ametuokoa kupitia maji, damu, na Roho. Imani inayoamini katika kazi za Yesu zilizodhihirishwa katika nyuzi tatu si imani nyingine bali ni imani ya maji, damu, na Roho. Watu wako huru kuamini katika kitu fulani, lakini hakuna ushahidi mzuri unaonyesha kuwa wataokolewa na kubarikiwa kwa kuamini hivyo. Isipokuwa ni kwa imani yetu tu katika injili ya maji na Roho ndipo tunapoweza kupokea kibari toka kwa Mungu na neema kuu na baraka za wakovu wa Mungu. Lengo la imani hii ya injili ya maji na Roho ni kutufunika sisi kwa neema ya Mungu.
Je, unalichukulia Hema Takatifu la Kukutania kuwa ni kama ni ua wa mstatili tu, ukiwa na nyumba iliyojengwa ndani yake? Dhana hii haiwezi kuleta faida yoyte kwa imani yako. Hema Takatifu la Kukutania linatueleza juu ya imani yote kikamilifu, na ni lazima tufahamu kwa hakika juu ya imani hii ilivyo.
Usipolifahamu vizuri Hema Takatifu la Kukutania, unaweza kufikiria kuwa urefu wa Hema Takatifu la Kukutania ni kama urefu wa uzio wake wa mita 2.25 (futi 7.5). Lakini sio hivyo. Hata kama tusingeliingia katika ua bali tulitazame Hema Takatifu la Kukutania toka nje ya uzio tungeliweza kuona kuwa Hema Takatifu la Kukutania ni refu mara mbili ya urefu wa uzio. Japokuwa tusingeweza kuona chini ya Hema Takatifu la Kukutania bado tungeliweza kuona mlango wake vizuri, kitu ambacho kinatuambia kuwa Hema Takatifu la Kukutania ni refu zaidi kuliko uzio wa ua wake.
Wale ambao wamepokea ondoleo la dhambi kwa kumuamini Yesu na kwa sababu hiyo wameingia katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania ni lazima waithibitishe imani yao sahihi katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na birika la kunawia, na kisha ndipo waingie Mahali Patakatifu. Ili kupaingia Mahali Patakatifu, lazima kuwe na kujikana binafsi bila kushindwa. Vyombo vyote ndani ya Mahali Patakatifu ni lazima vitofautishwe na vyombo vinavyopatikana nje ya Mahali Patakatifu.
Je, unafahamu ni kitu gani ambacho shetani anakichukia sana? Anauchukia mstari uliochorwa unaogawa kati ya ndani na nje ya Mahali Patakatifu. Kwa sababu Mungu anatenda miongoni mwao wanaogawa ndani na nje ya Mahali Patakatifu, Shetani anachukia kuwa mstari huo unachorwa na anajaribu kuwazuia watu kuuchora mstari huu. Lakini kumbuka hivi: Mungu anafanya kazi kwa wazi ndani ya wale wanaouchora mstari huu wa kiimani. Mungu anafurahishwa na watu wa jinsi hiyo wanauchora mstari huu wa kugawa, na anawashushia baraka zake juu yao ili waweze kuishi Mahali Patakatifu wakiwa na imani yao safi.
Amini kuwa vyombo vyote katika ua wa nje wa Hema Takatifu la Kukutania na vifaa vyote vilivyotumika vilitayarishwa na kupangiliwa na Mungu ili watu waweze kupokea ondoleo la dhambi zao. Na unapopaingia Mahali Patakatifu kwa kuamini hivi, Mungu atakushushia neema na baraka kuu.
 

Kiti cha Rehema Ni Mahali Ambapo Neema ya Wokovu Inapokelewa
Kiti cha Rehema Ni Mahali Ambapo Neema ya Wokovu Inapokelewa
Katika Patakatifu pa Patakatifu, makerubi wawili wakiwa wameyakunjua mabawa yao wanaangalia chini toka katika kifuniko kilicholifunika Sanduku la Ushuhuda. Nafasi kati ya makerubi wawili inaitwa kiti cha rehema. Kiti cha Rehema ni mahali ambapo Mungu anatupatia neema yake kwetu. Mfuniko wa Sanduku la Ushuhuda ulinyunyuziwa kwa damu pale Kuhani Mkuu aliponyunyizia damu ya mwanasadaka iliyotolewa kwa ajili ya watu wa Israeli, alinyunyuzia damu mara saba katika kiti hiki cha rehema. Hivyo Mungu alishuka katika katika kiti cha rehema na akawapatia rehema zake watu wa Israeli. Kwa wale wanaoamini katika hili, baraka za Mungu, ulinzi, na uongozi unaanzia hapa. Kuanzia pale na kuendelea, wanakuwa watu halisi wa Mungu ambao wanaruhusiwa kupaingia Mahali Patakatifu.
Miongoni mwa Wakristo wengi wa ulimwengu huu, wako baadhi ambao imani yao imewaruhusu kupaingia Mahali Patakatifu ilhali wengine hawana imani ya jinsi hiyo inayoweza kuwaruhusu kupaingia Mahali Patakatifu. Je, ni aina ipi ya imani uliyonayo? Tunahitaji imani inayoweza kuchora kwa wazi mstari wa wazi wa wokovu na kisha kuingia Mahali Patakatifu pa Mungu, kwa kuwa kwa kufanya hivyo tu ndipo tunapoweza kubarikiwa sana na Mungu.
Lakini si rahisi kiasi hicho kuwa na imani ya jinsi hii. Kwa sababu Shetani anawachukia watu wanapouchora mstari wa wazi wa wokovu, mara nyingi anajitahidi kuufuta mstari huu. “Huhitaji kuamini kwa namna ile. Sio kila mtu anaamini kama hivyo, kwa nini unaweka mkazo sana katika imani ya jinsi hiyo hali ukiirudiarudia? Usijali; endelea na mkumbo wa awali.” Kwa kusema hivyo, Shetani anajaribu kuuchafua na kuuchanganya mstari huu wa wazi wa wokovu. Pia, Shetani anafunua madhaifu yetu ya mwili na anajaribu kuyabadilisha kuwa matatizo. Je, utakuwa ni mmoja wa wale wanaosikiliza maneno ya uongo ya Shetani akijaribu kututenganisha na Mungu? Au utayaishi maisha yako hali ukijikumbusha juu ya wokovu wako kila siku, ukijiunga pamoja na Kanisa, ukilifuata Neno la Mungu, ukiyaishi maisha ya maombi, na kupokea neema ambayo Mungu ameishusha juu yako?
Kusema kweli, wale waliopokea ondoleo la dhambi wanapenda kujikumbusha juu ya wokovu wao. Wanapenda kudumu katika injili ya maji na Roho mara kwa mara. Kutafakari juu ya injili ni jambo jema na muhimu kwako. Je, wewe hautendi hivi? “Ooh, ni habari ile ile tena, kwani tumeokolewa lini? Vifaa vya habari na mpango unaweza kuwa tofauti, lakini ni habari ile ile ya kale. Nimeichoka sana habari hiyo!”
Je, inawezekana kukawa na mtu anayesema hivi? Nitajisikia huzuni ikiwa nitalazimika kuizungumzia habari hiyohiyo inayonihusu mimi kila siku, lakini Biblia inapotuambia kuwa tujikumbushe juu ya wokovu wetu kila siku, je mimi nitafanya nini? Wakati Agano Jipya na Agano la Kale linapotuambia juu ya injili ya maji na Roho, basi kuhubiri kitu kingine zaidi ya injili hii ndio uovu mbele za Mungu. Neno lote katika Biblia linazungumzia juu ya injili ya maji na Roho. “Wokovu, maisha ya imani, imani, kuishi kiroho, vita dhidi ya Shetani, Mbingu, utukufu, neema, baraka, ufufuko, uzima wa milele, tumaini, na Roho Mtakatifu”—dhana hizi zote muhimu kwa watakatifu zinahusishwa na injili hii ya kweli. Kuzungumzia jambo jingine lolote zaidi ya haya ni uzushi na mafundisho ya uongo. Kitu kinachoonekana kuwa kinafanana lakini ni tofauti kwa yaliyomo si kitu kingine bali ni mafundisho ya uongo. Injili zinazoonekana kuwa zinafanana kwa nje lakini ambazo kwa ndani ni tofauti na injili ya maji na Roho ni injili za uongo za dini za uongo.
Ni jinsi gani ni vya kupendeza kuwa Kanisa la Mungu linalitangaza Neno la Mungu kila siku, na si maneno ya uongo ya dini za uongo? Ni baraka kuwa tumeunganishwa na Kanisa la Mungu, tukisikia na kuamini katika Neno halisi la Mungu. Kwa kuihubiri kila wakati injili ya maji na Roho, Kanisa la Mungu linawawezesha watakatifu kufikiri juu ya neema ya Mungu kila siku, kumwomba Mungu, na kumsifu Mungu, na kuishi maisha ambayo hayauelekei uovu. Je, hauna furaha kuwa umelisikia na kuliamini Neno la ukweli mara moja ambalo linakuruhusu kupokea ondoleo la dhambi? Mimi pia nina furaha sana.
Ikiwa ningeshurutishwa kuhubiri kitu kingine zaidi ya injili hii ya maji na Roho kwa kweli ningeteseka sana. Ikiwa ningeshurutishwa kutolihubiri Neno la wokovu bali kwamba nihubiri mafundisho mengine ya wanadamu, kwa kweli ningehitaji kutoroka. Sio kwa sababu sina kitu cha kuzungumzia. Yapo mambo mengi yanayohusiana na masuala ya kibinadamu ambayo ninaweza kuyazungumzia, lakini masuala haya sio ya msingi na ni mafundisho ya ufisadi yaliyo chacha hasa kwetu sisi tuliozaliwa upya.
Ni injili hii ya maji na ya Roho tu ambayo kwa hivyo Yesu, Mungu mwenyewe ametuokoa, ni Neno la Mungu la thamani ambalo linatoa utamu wake hata pale tunapolitafuna mara kwa mara. Kuna hadithi nyingi sana ambazo ninaweza kukuambia, lakini ninapenda zaidi ninapozungumzia juu ya injili ya maji na Roho inayotuokoa. Ndipo ninapokuwa na furaha sana. Ninakuwa na furaha zaidi pale ninapozungumzia juu ya wokovu huu, kwa kuwa hapa ndipo ninapoweza kufikiria kwa upya juu ya kumbukumbu za zamani, nikijikumbusha jinsi ambavyo Bwana ameniokoa, nikimshukuru tena kwa mara nyingine, na nikijilisha tena katika mkate wa wokovu.
Ninaamini kuwa wewe pia, unafurahia zaidi pale unapolisikia Neno hili la wokovu. Pengine unaweza kulalamika kuwa ni habari ile ile kila siku, lakini ya kina, ukafikiria, “Sasa kwa kuwa nimeisikia tena, ni nzuri zaidi. Mara ya kwanza haikuwa nzuri kiasi hicho, lakini ninapoendelea kuisikia, ninaweza kuona kuwa hakuna habari nyingine ambayo ni ya maana kuisikiliza kama ilivyo kwa hii. Nilifikiria kuwa habari ya leo inaweza kuwa na umaalum fulani, lakini hitimisho linaniambia kuwa ilikuwa ni habari ile ile kwa mara nyingine. Lakini bado nina furaha.” Ninahakika kuwa hivi ndivyo moyo wako unavyohisi.
Kaka zangu na akina dada, ninachokihubiri hapa ni Neno la Yesu. Wahubiri ni lazima wahubiri Neno la Yesu. Kuhubiri mambo ambayo Yesu ameyafanya kwa ajili yetu na kuueneza ukweli wa maji na wa Roho kupitia Neno lililoandikwa ndio kitu ambacho Kanisa la Mungu linapaswa kufanya. Kwa sasa tunayaongoza maisha yetu ya kiimani katika Kanisa. Hakuna maisha mengine zaidi ya haya ambayo ni maisha yetu ya kiimani kwamba, tukipaingia Mahali Patakatifu, tukiangaziwa chini ya kinara cha taa chenye matawi saba yaliyotengenezwa kwa kuponda talanta moja ya dhahabu, tukila mkate katika nyumba ya dhahabu safi, tukiomba katika madhabahu ya uvumba, tukielekea katika Hekalu la Mungu, tukimwabudu, na tukiishi katika nyumba hii ya dhahabu.
Wewe na mimi kwa sasa tunaishi maisha ya imani tuliyopewa na Mungu. Tukipokea ondoleo la dhambi na tukiishi maisha ya imani basi hivi ndivyo maisha ndani ya Nyumba ya dhahabu ya Mungu yalivyo. “Ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku hadi siku” (2 Wakorintho 4:16). Kwa imani yetu ya nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa ilivyodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania, nafsi zetu zinaishi katika Nyumba ya Mungu inayong’aa kwa dhahabu.
Ninatoa shukrani zangu kwa Mungu daima kwa kutuokoa sisi kutoka katika dhambi zetu zote na adhabu. Halleluya!