Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[3-5] Barua Kwa Kanisa la Laodikia (Ufunuo 3:14-22)

(Ufunuo 3:14-22)
“Na kwa malaika wa kanisa lililo Laodikia andika; haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, yakuwa hu baridi wala hu moto; ingelikuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. Yeye aliye na sikio na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”
 
 
Mafafanuzi
 
Aya ya 14: “Na kwa malaika wa kanisa lililo Laodikia andika; haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.” 
Bwana wetu alikuja hapa duniani na akamtii Mungu Baba hadi kifo chake ili kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Kwa maneno mengine, Yesu aliitii kila amri kwa kusema “Amin” ilimradi kama ilikuwa ni kwa ajili ya mapenzi ya Mungu. Bwana wetu ni mtumishi mwaminifu wa Ufalme wa Mungu Baba na shahidi wa kweli anayejishuhudia mwenyewe kuwa ni Mwana wa Mungu na Mwokozi. Bwana wetu ni Mungu wa uumbaji na mwanzo wa uumbaji.
 
Aya ya 15: “Nayajua matendo yako, yakuwa hu baridi wala hu moto” 
Mungu alimkemea mtumishi wa Kanisa la Laodikia kwa ajili ya imani yake ya uvuguvugu. Mtumishi huyu alistahili kuipata hasira ya Mungu. Ikiwa imani ya mtu yeyote ni ya uvuguvugu mbele za Mungu, basi mtu wa jinsi hiyo anatakiwa kuifanya imani yake kuwa wazi kwa kuifanya kuwa baridi au moto. Imani ambayo Mungu anaitaka kwetu ni imani iliyo wazi kwamba ni ya baridi au ya moto. Imani hii ya wazi ni hitaji muhimu sana katika kuiamini injili ya maji na Roho.
Inapofikia hatua ya kumwamini Mungu, basi kunakuwepo na aina mbili za waamini. Kwa upande mmoja, kuna wale wanaoamini kuwa injili ya maji na Roho ndiyo injili ya kweli, na kwamba hakuna injili nyingine zaidi ya hii. Kwa upande mwingine, kuna wale wanaoamini kuwa mbali na injili ya maji na Roho pia kuna injili nyingine. Ukweli ni kuwa imani ya hawa wanaoamini kuwepo kwa injili nyingine ni imani ya uvuguvugu.
Wao wanafikiri kuwa inatosha kumwamini Yesu, na kwamba hakuna haja ya kutenganisha kati ya injili ya kweli na injili za uongo. Baadhi yao wanadiriki kufikiri kuwa Yesu si Mwokozi pekee na kwamba wokovu unaweza kupatikana katika dini nyingine za ulimwengu huu. Kama ilivyo imani ya watu kama hawa ndivyo imani ya mtumishi wa Kanisa la Laodikia ilivyokuwa ya vuguvugu, na ilikuwa haiwezi kutenganisha kati ya injili ya kweli na injili za uongo—yaani kusema bayana kuwa hakuna injili nyingine zaidi ya injili ya maji na Roho. Hii ndiyo sababu mtumishi huyu aliyaleta mashaka yake kwa Mungu na akaipata hasira ya Mungu.
 
Aya ya 16: “Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.” 
Bwana Mungu wetu alihitaji imani ya wazi toka kwa mtumishi wake. Tunapaswa kutambua kuwa Mungu haikubali imani ambayo si baridi wala si moto. Hivyo, tunapomwamini Bwana ni lazima tuiweke mioyo yetu wazi na bila kigugumizi hali tukiipima mioyo yetu kwa Neno la Mungu na huku tukisimama imara katika mapenzi yake kwa kuliamini Neno la Mungu. Hivyo, wale waliozaliwa tena upya wanapaswa kwa wazi kabisa kusimama katika upande wa injili ya kibiblia ya maji na Roho, na kisha kukabiliana na wale wanaoeneza injili nyingine zaidi ya injili hii ya kweli. Mungu anatueleza kuwa ikiwa wenye haki hawatasimama katika upande wa wazi wa kiimani, basi Mungu atawatapika. Je, imani yako imesimama wapi?
 
Aya ya 17: “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”
Wale ambao imani yao mbele za Bwana ni ya vuguvugu wanaiamini imani yao kuwa ipo sawa, na kwa sababu hiyo wanajisahau katika umaskini wa imani yao. Kwa kuwa mtumishi wa Kanisa la Laodikia alikuwa ameridhishwa na imani yake ya uvuguvugu, basi kwa sababu hiyo hata yeye alishindwa kujiona jinsi alivyokuwa mnyonge. Hivyo, ili aweze kuwa na imani ya wazi na sahihi alihitaji kukabiliana na majaribu na mateso kwa ajili ya kweli, na kisha kuipitia vita ya kiimani dhidi ya waongo. Ni hapo tu ndipo angeliweza kufahamu jinsi alivyokosa imani, alivyo maskini, na jinsi alivyo uchi. Sisi sote tunapaswa kuwa na imani ya wazi mbele za Bwana.
 
Aya ya 18: “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”
Mungu alimweleza malaika wa Kanisa la Laodikia kuifanya upya imani yake. Mtumishi wa Kanisa la Walaodikia alipaswa kuijenga upya misingi ya imani yake katika injili ya maji na Roho na kuvikwa katika vazi lote la haki. Pia alipaswa kujitazama yeye mwenyewe, kuielewa upya imani yake, na kurudi katika imani hiyo. Alipaswa kuitunza imani hiyo kwa uvumilivu na kulitimiliza tumaini lake kwa kuifanya upya imani yake.
Wewe pia unapaswa kuyapitia maonezi makubwa na mateso kwa ajili ya injili ya maji na Roho, ambayo ni injili ya kweli iliyotolewa na Mungu. Ni hapo tu ndipo unapoweza kutambua jinsi injili hii ya maji na na Roho ilivyo ya kweli na ya thamani. Je, umewahi kuivunja haki yako binafsi ya kibinadamu ili kuweza kuifuata na kuitunza haki ya Mungu inayopatikana kupitia injili ya maji na Roho? Wale walioivunja haki ya mwanadamu wanafahamu jinsi haki ya Mungu ilivyo ya baraka na thamani. Unapaswa kutambua kuwa pasipo imani yako inayoamini katika Bwana, basi maisha yako ya imani yatabadilika na kuwa mabaya. Hivyo, ni lazima ujifunze toka katika imani ya Bwana aliyoitoa kwa watumishi wake waliotutangulia kabla yetu, na kisha kuifunika aibu ya kutokuwa na imani.
Hatupaswi kusahau ule ukweli kuwa ili kujifunza imani ya kweli inatakiwa kujitoa. Kwa kuwa imani ya kweli inapatikana kwa kuyafuata mapito ya kiimani ya watangulizi wa kiroho hatua kwa hatua; ni lazima tulipe gharama ya kujitoa sadaka. Pia ni lazima tuwe tayari kupoteza vitu vya kidunia kwa ajili ya kuujenga Ufalme wa Mungu na kwa ajili ya kuiendeleza imani yetu, na kisha kuachilia mbali kila kitu kwa ajili ya Bwana.
 
Aya ya 19: “Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.”
Bwana anawakemea na kuwarudi wale wanaofahamu na kuamini katika upendo wake ikiwa tu imani yao itakuwa haina matendo. Hivyo, wale wanaopendwa na Bwana ni lazima wafanye kazi kwa juhudi kwa ajili yake na kisha wamfuate kwa imani.
 
Aya ya 20: “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.”
Wale waliofanyika kuwa watumishi wa Mungu wanayashirikisha maisha yao pamoja na Mungu katika hali ya furaha na katika huzuni. Wale wanaofanya kazi kwa ajili ya Bwana wanaishi wakati wote kwa kuamini katika Neno la Bwana, na Bwana anazitimiza kazi zake zote kwa kupitia imani ya watumishi wake.
 
Aya ya 21: “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.” 
Imani ya kweli inapatikana au inapotezwa kutegemeana na mtu kuwa tayari kukubali kuifia-dini au la. Wale wanaopigana na Shetani kwa kuamini katika Neno la Bwana watapata ushindi na kutukuzwa na Bwana. Watakatifu na watumishi wa Mungu wapo katika vita ya kiroho dhidi ya Shetani wakati wote. Katika vita hii ya kiroho, wanaweza kushinda kwa kuamini katika Neno la Mungu. Hivyo wale watakaoshinda katika vita dhidi ya Shetani watatukuzwa na Mungu.
 
Aya ya 22: “Yeye aliye na sikio na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”
Watakatifu ni lazima waisikilize sauti ya Mungu wakati wote na kufuata uongozi wa Roho Mtakatifu. Wanapofanya hivyo, imani yao inafanyika kuwa ile inayotembea na Roho Mtakatifu, na kwa sababu hiyo ushindi wa kiroho utakuwa ni wao.