Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[3-6] Imani ya Kweli kwa Maisha ya Ufuasi (Ufunuo 3:14-22)

(Ufunuo 3:14-22)
 
Imani ya Kanisa la Laodikia ilikuwa ni ile iliyopaswa kutapikwa na Bwana. Hivyo, Bwana aliwashauri wanunue kwake dhahabu iliyosafishwa katika moto ili kwamba waweze kuwa matajiri katika imani yao. Imani hii ya uvuguvugu inaweza pia kuonekana miongoni mwa wenye haki wa kipindi hiki. Hii ni kwa sababu kwa kuwa waliipokea imani hii bure, basi wanashindwa kufahamu jinsi imani hii ilivyo ya thamani. Hivyo Mungu aliongea maneno haya ya kuwaonya na akatoa ushauri kwa wenye haki ili awapatie imani ambayo ni kama dhahabu iliyosafishwa kwenye moto. Pia tunaweza kuona katika kifungu hiki cha maandiko kuwa Mungu aliyataka makanisa yote saba huko Asia kuwa na imani inayoshabihiana, yaani imani moja. Bwana aliwaamuru wote walio na masikio kusikia kile ambacho Roho Mtakatifu anayaambia makanisa.
Toka Ufunuo 3:17, tunaona kuwa Kanisa la Walaodikia lilikuwa limetegwa katika hali ya kujidanganya lenyewe, huku wakidhania kuwa ule utajiri wao wa mali ulikuwa ni sawa na na baraka za Mungu za kiroho na kwamba ulikuwa ukitokana na imani yao. Mungu alionyesha dhahiri umaskini wa kiroho na udhaifu uliokuwepo katika kusanyiko hili la Walaodikia lililokuwa limepotoshwa.
Kanisa la Laodikia pengine lilionekana kama ni tajiri kiimani, lakini ukweli ni kuwa kanisa hilo lilikuwa halina imani na lilikuwa masikini. Imani ya kanisa hili ilikuwa ni ile ya uvuguvugu, ilikuwa imejawa na uzembe wa kiroho, na iliupenda ulimwengu kuliko kumpenda Yesu.
Ufunuo 3:14-22 inaongelea juu ya maisha mfuasi. Wafuasi wa kweli wa Yesu ni wale wanaotii na kulifuata Neno la Kristo. Wale wote waliozaliwa tena upya kwa kuamini katika Yesu Kristo wanastahili kuwa wafuasi wake. Bwana anatutaka sisi sote kuishi maisha ya mfuasi. Ni lazima tutambue kwa hakika kuwa tumepewa haya maisha ya ufuasi. 
Katika kifungu cha maandiko, Bwana alisema kuwa atawatapika watakatifu wasioishi maisha ya ufuasi. Kama ilivyoandikwa katika aya ya 15-16, “Nayajua matendo yako, yakuwa hu baridi wala hu moto; ingelikuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.” Ikiwa waliookolewa si baridi wala moto mbele za Bwana, basi hali hiyo inaonyesha juu ya umaskini wao wa kiroho. Pia watu wa jinsi hiyo bado hawayafahamu maisha ya ufuasi. Lakini yeyote aliyezaliwa tena upya anapaswa kuishi maisha ya mfuasi. Sisi tumekombolewa toka katika dhambi zetu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Huu ndio wokovu wetu.
Je, ni nini basi ambacho tulipewa mara baada ya wokovu wetu na kuzaliwa tena upya? Tulipewa maisha yanayojaribu kuwa kama Bwana, yanayojaribu kufuata na kuyatii maagizo yake, na kulitafuta Neno lake. Haya ndiyo maisha ya mfuasi. Mungu alilikemea Kanisa la Laodikia kwa kuwaambia kuwa wao “si moto wala si baridi” akiwa na lengo la kuutaka ufuasi huu toka kwa watakatifu wake.
Imani isiyo baridi wala moto ni imani ya uvuguvugu. Je, ni aina gani hii ya imani ambayo ni ya uvuguvugu na ambayo inampatia mwanadamu starehe kwa kuwa si ya baridi wala si ya moto? Ni imani inayojaribu kuwa na njia zote mbili, mfano ni kuwa na keki na kisha kuila. Ni imani isiyofuata wala kuyaishi maisha ya ufuasi. Wale walio na imani ya uvuguvugu ni wale ambao pamoja na kuwa wamekwisha okolewa, bado hawayafuati mapenzi ya Yesu. Watu wa jinsi hiyo wanaweza kuonekana kana kwamba wanamfuata Yesu, lakini ukweli ni kuwa hawamfuati—kwa lugha nyingine, imani ya wale ambao wanakanyaga pande mbili za uzio ndio inayoitwa imani ya uvuguvugu.
Ulimwengu unaielezea imani ya jinsi hiyo, yaani imani ya uvuguvugu kuwa ni yenye busara. Imani hii inaweza kuwa ya busara kwa vigezo vya kidunia, lakini hii ndiyo aina ya imani inayomfanya Bwana kuwatapika walio na imani hiyo. Ni kitu gani kinachomfanya Bwana kutapika imani ya uvuguvugu? Unapaswa kuwa na uelewa mzuri juu ya aina hii ya imani ya uvuguvugu ilivyo. Wale ambao imani yao ni ya uvuguvugu hawajiungi wala hawajitengi toka katika kazi za makanisa ya Mungu; wanafanya na wakati huo huo hawafanyi. Watu wa jinsi hiyo maisha yao ya kiimani yakiwa kwenye alama 60, basi wao hubakia hapo bila jitihada ya kuongeza wala kupunguza.
Wale ambao maisha yao ya kiimani ni kama haya basi watu hao ni masikini wa kiroho. Kama aya ya 17-18 zinavyosema, “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”
Wale ambao imani yao ni ya uvuguvugu wanachukulia mafanikio na utajiri wao wa kidunia kuwa ndio mafaniko ya kiroho. Pamoja na kwamba wanahisi kuwa wao ni wanyonge, wachovu, na masikini, ukweli ni kuwa hawaitambui hali hiyo kikamilifu. Hawa ni watu ambao hawajitambui wao wenyewe. Wao hujifikiria hivi, “Nipo salama. Mimi ni mkweli, mhalisia, na ninakubaliwa na wengine, kwa hiyo pamoja na kuwa nimeokolewa nafikiri ni sahihi kwangu kuishi kwa jinsi hii,” na kwa sababu hiyo wao huishi maisha yao kwa kufuata viwango vyao binafsi. Watu wa jinsi hii ni waaminifu sana kwa ulimwengu lakini si waaminifu kwa kanisa la Mungu. Imani yao ni imani ya uvuguvugu. Hivyo Mungu anasema kuwa atawatapika watoke katika kinywa chake.
Wao huja kanisani wakiwa na msukumo wa kuogopwa kuondolewa kanisani. Wao hukaa hadi mwisho wa ibada na huondoka mara ibada inapokuwa imekwisha. Watu wa jinsi hiyo hawashiriki katika kazi za kanisa kwa kujitolewa, na kama wakijitolea, basi watahakikisha kuwa wamejitolea kidogo sana. Wao hufanya lakini kiuhalisia hawafanyi, na hawafanyi huku wakitaka waonekana kuwa wanafanya. Kwa kweli hawa ni watu ambao ni masikini kiroho.
Bwana anatoa ushauri huu kwa watu wa jinsi hiyo: “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.” Mungu aliwaambia kununua kwake dhahabu iliyosafishwa katika moto ili waweze kuwa matajiri.
Ikiwa unapenda kumfuata kweli Bwana, na ukiwa unataka Bwana aithibitishe imani yako, basi ni lazima ujifunze juu ya imani yako. Inawezekanaje kujifunza imani? Ni lazima ujifunze kwa imani kwa gharama ya sadaka na kwa kuamini katika Neno. Kifungu hiki cha maandiko kinatueleza kununua dhahabu iliyosafishwa katika moto. Hii ina maanisha kuwa kuna majaribu na mateso mengi kwa ajili yetu hasa tunapofikia hatua ya kulifuata Neno la Mungu. Lakini tunaweza kuyashinda majaribu hayo yote na mateso kwa kuliamini na kulifuata Neno la Mungu. Kwa kufanya hivyo, mioyo yetu inasafishwa, na inatupatia imani inayolitambua Neno la Mungu kuwa ni kweli na hatimaye tunaliamini hilo Neno kwa mioyo yetu yote. Hii ndiyo imani ambayo ni sawa na dhahabu safi.
Hivyo, ili kuipata imani ya kweli ni lazima tulipe gharama ya sadaka, kwa kuwa pasipo kulipa gharama ya sadaka hatuwezi kamwe kujifunza juu ya imani. Kwa maneno mengine, hatuwezi kujifunza juu ya imani bila kuyapitia magumu. Ikiwa tunapenda kweli kuwa watu wa imani, na ikiwa tunapenda kuishi maisha ya ufuasi ya Bwana, na ikiwa tunapenda kubarikiwa kwa sababu ya imani yetu, basi ni lazima tulipe gharama ya sadaka. Pasipo kujitoa kama sadaka, basi hatuwezi kuyafikia maisha ya kiimani tunayoyatamani.
Ni nani aliye na imani yenye nguvu tangu mwanzo? Hakuna. Hii ni kwa sababu watu hawaifahamu imani ambayo kanisa linawafundisha kuhusu Neno. Ni lazima tutii kile ambacho kanisa linatuongoza na kisha tukifuate kwa imani. Lakini ili kufanya hivyo kunajumuisha pia magumu; na kwa sababu hiyo uvumilivu unahitajika katika nyakati mbalimbali. Hii ndio sababu kule kufanyika watu wa imani kwa kupokea maelekezo ya Neno, faragha, na mafundisho mara nyingi kunafuatana na sadaka ya kujitoa. Pamoja na kuwa watu wanapenda kujifunza imani, lakini kwa kuwa hawapendi kujitoa kama sadaka, basi ukweli ni kuwa hawawezi kuwa na imani ya kweli ya kusafishwa. Hii ndio sababu Bwana anatueleza kununua kwake dhahabu iliyosafishwa kwa moto ili kwamba tuweze kuwa matajiri katika imani.
Unaweza kueleza maana ya Neno hili hasa unapojifunza toka katika imani ya watakatifu waliotutangulia na kwa kuyafuata maisha yao. Ikiwa unalisikia Neno la nadharia tu halafu huyafuati yale ambayo Neno hilo linakuamuru uyafanye, na ikiwa unashiriki katika kushuhudia, maombi, au katika mikutano na halafu ukawa huyaweki unayofundishwa katika vitendo, basi ni hakika kuwa huwezi kujifunza imani. Kwa kuwa una imani kidogo, ndio maana unaipima imani yako kwa vigezo vyako binafsi ya kidunia na kuiona kuwa si mbaya sana. Unajifikiria, “Nimeokolewa, nina pesa, na katika mambo ya kidunia ninafanya vizuri, na kwa sababu hiyo mimi ni bora kuliko wengine. Ndiyo, nina hakika kwamba mimi ni bora kuliko watu hawa.”
Ikiwa unapenda kweli kujifunza juu ya imani ya kweli ambayo ni kama dhahabu, basi ni lazima ulipe gharama ya kujitoa kama sadaka. Je, ni rahisi kutii na kufuata? Kwa kweli kutii kunagharimu sadaka ya kujitoa. Je, ni rahisi kujitoa sadaka? Kwa kweli si rahisi. Lakini ikiwa unataka kukwepa usije ukatapikwa, basi ni lazima utii kwa kujitoa sadaka.
Lakini wale ambao hawajajifunza imani ya kweli, ni masikini wa kiroho na hawapendi kujitoa sadaka. Ili kutii, ni lazima mtu ayavunje mawazo na nia yake kwanza. Pasipokuwa tayari kufanya hivyo, basi mioyo yao itaendelea kuwa katika unyonge wa kiroho kadri muda unavyozidi kwenda. Kwa sababu ya kutotambua ukosefu wao wa kiimani, basi watu hao hujikuta wakiishia kuwalaumu watakatifu waliowatangulia kiimani. Ni lazima ujifunze imani ya kweli. Unapoingia katika vita za kiroho na ukawa unapigana ukiwa upande wa Mungu, basi imani yako itasafishwa hasa pale unapopata makovu ya kiroho ambayo yatakufanya utambue maana ya kuishi maisha ya ushindi wa kiroho. Unaweza kuifahamu imani hii hasa unapokuwa umepata uzoefu kwa kuitenda.
Mungu alimkemea mtumishi wa Kanisa la Laodikia kwa kuandika hivi, “Huufahamu uchi wako wala umaskini wako. Umeokolewa, lakini imani yako ni ya uvuguvugu—haijulikani kuwa ni hii au ile. Kitu pekee ambacho unacho ni wakovu wako ambao umeuweka mbali. Kwa kweli hauna kitu kingine chochote zaidi ya wokovu.”
Je, watumishi wa Mungu au watangulizi wetu wa kiroho wanafanyika kuwa watangulizi wetu wa imani pasipo kuishi maisha ya ufuasi? Kwa kweli si hivyo! Watumishi na watangulizi hao waliyapitia matatizo ya aina nyingi kwa ajili ya Bwana, katika hali ya furaha na huzuni. Mungu anakuongoza kwa kukuwekea mbele yako wale ambao wameyapitia mambo yote ambayo na wewe pia utayapitia. Hivyo ni lazima uamini katika ukweli kuwa Mungu anakufundisha na kukuongoza kwa kupitia wale ambao waliifuata njia ya imani kabla yako.