Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[4-1] Mtazame Yesu Anayeketi Katika Kiti cha Enzi cha Mungu (Ufunuo 4:1-11)

(Ufunuo 4:1-11)
“Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. Mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti; na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi. Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu. Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu. Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma. Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye. Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mbawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele; ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema,
Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, Kupokea utukufu na heshima na uweza;
Kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, 
Na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: “Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo.”
Hapo kabla lango la Mbinguni lilikuwa limefungwa. Lakini lango hili lilifunguliwa wazi wakati Yesu alipowakomboa wenye dhambi toka katika maovu yao kwa kuja hapa duniani, kwa kubatizwa na Yohana, kwa kufa Msalabani, na kwa kufufuka tena toka kwa wafu. Mungu alimfunulia Mtume Yohana yale ambayo yanaungojea ulimwengu huu katika nyakati za mwisho kwa kupitia malaika zake.

Aya ya 2: “Mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti”
Kwa kupitia lango la Mbinguni lililofunguliwa, Yohana aliweza kuona kuwa kuna kiti kingine cha enzi kimeandaliwa Mbinguni, na kwamba aliyekuwa ameketi katika kile kiti cha enzi alikuwa ni Yesu Kristo. Kiti kile cha enzi kilikuwa kimezungukwa na wenye uhai wanne, wazee 24, na Roho saba za Mungu.
Bwana alikipokea kiti cha enzi cha Mungu toka kwa Baba kwa ajili ya kuikamilisha kazi ya Mungu ya kuwaokoa wenye dhambi toka katika dhambi za ulimwengu. Alipokuwa angali hapa duniani, Yesu alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa kuupokea ubatizo toka kwa Yohana Mbatizaji, na akawakomboa wenye dhambi wote toka katika maovu yao kwa kufa Msalabani na kufufuka tena toka kwa wafu. Hii ndiyo sababu Mungu Baba alikiruhusu kiti hiki cha enzi huko Mbinguni kuwa cha Mwanawe. 
Wakati mwingine kuna tabia ya kumwona Yesu kama aliyewekewa mipaka, na hasa kwa kumtambua kama Mwana wa Mungu na Mwokozi na si zaidi ya hapo. Lakini, kwa sasa Yesu Kristo ameketi katika kiti cha enzi cha Mungu kama Mfalme mkuu ambaye anatawala Mbinguni.
Kwa kweli, hii haimaanishi kuwa Yesu alishindana dhidi ya Mungu kwa ajili ya kukipata kiti hiki cha enzi. Kiti cha enzi cha Mungu Baba bado kipo pale. Mungu aliruhusu kuwepo kwa kiti kingine cha enzi Mbinguni kwa ajili ya Mwana wake, akimtawaza kuwa Mfalme wa Mbinguni na kumfanya kuwa hakimu wa wale wote wanaosimama kinyume dhidi ya Mungu. Baba alimwinua Yesu Kristo juu zaidi kuliko yeyote yule Mbinguni na duniani kama Mungu. Kwa sasa Yesu Kristo ni Mungu, aliye sawa na Baba. Hivyo ni lazima tumsifu na kumwabudu Yesu, ambaye ni Mungu na Mwokozi wetu.
 
Aya ya 3: “na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.” 
Aya hii inaelezea juu ya utukufu wa Mungu akiwa ameketi katika kiti kipya cha enzi.
 
Aya ya 4: “Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu.”
Watumishi wa Yesu Kristo Mungu wetu walikuwa wameketi kukizunguka kile kiti cha enzi. Maandiko yanasema hapa kuwa kiti cha enzi cha Mungu kilizungukwa na viti vya enzi vingine 24, na kwamba katika viti hivi vya enzi waliketi wazee 24 wakiwa na taji za dhahabu vichwani mwao. Kwa kweli ilikuwa ni baraka kubwa ya Mungu kuwaruhusu hawa wazee 24 kuketi katika viti hivi 24 vya enzi. Hawa wazee ndio wale ambao walipokuwa hapa duniani walifanya kazi kwa nguvu na kuuawa kwa kuifia-dini kwa ajili ya Ufalme wa Bwana. Neno hili linatueleza kuwa Ufalme wa Mbinguni sasa umefanyika kuwa Ufalme wa Bwana Mungu wetu ukidumu milele chini ya utawala wake.
 
Verse 5: “Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.”
Mungu ndiye anayeziumba na kuzitawala roho zote.
 
Aya ya 6: “Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma.”
Wale wenye uhai wanne pamoja na wale wazee 24 ni watumishi wa Ufalme wa Mungu. Wao huyatafuta mapenzi ya Mungu wakati wote na wanautukuza utakatifu na utukufu wa Mungu. Na hao ndio wale wanaoyatimiza mapenzi ya Mungu kwa unyenyekevu.
 
Aya ya 7: “Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye.”
Hawa wenye uhai wanne ni watumishi wa Mungu ambao wamejitoa kwa ajili ya majukumu tofauti ambayo kila mmoja amepatiwa, na watumishi hao wanayatumikia malengo ya Mungu kwa uaminifu.
 
Aya ya 8: “Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mbawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.”
Kama Mungu asivyolala, basi wale wenye uhai wanne wapo macho wakati wote wakiwa karibu naye, huku wakimsifu Mungu kwa utukufu na utakatifu wake. Wanamtukuza mtakatifu wa Mungu ambaye alifanyika Mwanakondoo na pia wanazitukuza nguvu zake kuu. Wanamsifu Mungu kama aliyekuwako, aliyeko, na atakayekuwako. Hivyo yule anayetukuzwa na wenye uhai hawa ni Mungu Baba na Yesu Kristo, ambaye ni Mungu.
 
Aya ya 9: “Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele”
Hivyo, watumishi wa Mungu wanampatia Mungu utukufu, heshima, na shukrani yeye aketiye katika kiti cha enzi milele na milele.
 
Aya ya 10: “ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema,”
Wakati wale wenye uhai wanne walipokuwa wakimsifu Mungu, wale wazee 24 waliokuwa wameketi katika viti vya enzi pia walizitupa taji zao mbele za Mungu na wakamsifu Mungu wakisema, “Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, Kupokea utukufu na heshima na uweza.”
 
Aya ya 11: “Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, Kupokea utukufu na heshima na uweza; Kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, Na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.”
Sifa ambazo wale wazee 24 walimpatia Mungu zilitoka katika imani ambayo inaamini kuwa Mungu alistahili kupokea utukufu, heshima, na uweza, kwa kuwa alikuwa ameviumba vitu vyote na kwamba vitu vyote vinaishi au vipo kwa sababu ya uwepo wa wake.