Search

Mahubiri

Somo la 11: Maskani

[11-6] Ahadi ya Mungu Iliyothibitishwa Katika Agano Lake la Tohara Bado Inafaa na Ni Muhimu Kwetu (Mwanzo 17:1-14)

Ahadi ya Mungu Iliyothibitishwa Katika Agano Lake la Tohara Bado Inafaa na Ni Muhimu Kwetu
(Mwanzo 17:1-14)
“Abramu alipokuwa na miaka tisini na tisa, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, ‘Mimi ni Mungu Mwenyezi; uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana.’ Kisha Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema: ‘Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na wazawa wengi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na wazawa wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa wazawa wako baada yako. Nami nitakupa wewe na wazawa wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.’ Mungu akamwambia Ibrahimu: ‘Nawe ulishike agano langu, wewe na wazawa wako kwa vizazi vyao baada yako. Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na wazawa wako baada yako: Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa; mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi. Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako. Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele. Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu huyo atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.’”
 

Katika sura ya 17 ya kitabu cha Mwanzo, agano la tohara ambalo Mungu amelianzisha na kulithibitisha na Ibrahimu linatuonyesha sisi juu ya tohara ya kiroho ambayo kwa hilo dhambi zote zinaondolewa toka kwa waisraeli kwa kuiweka mikono yao juu ya mwanasadaka wa kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania na kwa jinsi hiyo walizipitisha dhambi zao kwa mnyama huyo wa sadaka ya kuteketezwa. Kwa maneno mengine, agano ambalo Mungu alilolianzisha na kulithibitisha na Ibrahimu lilikuwa ni wonyesho unaoonyesha juu ya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa zitakazokuja baadaye. Ahadi ambayo Mungu aliifanya kwa Ibrahimu kwa tohara, kwamba atakuwa Mungu wake na Mungu wa wazawa wake, ilitabiri hali ikiliheshimu Hema Takatifu la Kukutania, kwamba wazawa wa Ibrahimu watazipitisha dhambi zao katika sadaka ya kuteketezwa kwa kuiweka mikono yao juu ya kichwa cha mwanasadaka. Ni lazima tutambue na tuamini kuwa hii inatuonyesha sisi kwa nyongeza kwamba katika kipindi cha Agano Jipya Yesu atazichukua dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana.
Mungu alimwahidi Ibrahimu, “Tazama mbinguni, zihesabu nyota, kama kweli utaweza kuzihesabu. Hivi ndivyo watakakavyokuwa wengi wazawa wako” (Mwanzo 15:5). Akimtokea tena Ibrahimu, Mungu aliahidi tena, “Nitakufanya uwe na wazawa wengi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na wazawa wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa wazawa wako baada yako.” (Mwanzo 17:6-7).
Ahadi ambayo Mungu aliifanya kwa Ibrahimu na wazawa wake ilikuja kwa kupitia tohara. Tohara hii inafanana na tendo la kuweka mikono juu ya mnyama wa sadaka wakati waisraeli walipotoa sadaka zao za kuteketezwa kwa Mungu. Pia ilitueleza kabla, kwamba katika kipindi cha Agano Jipya, ondoleo la dhambi limetimizwa kwa Yesu kuzichukua dhambi za ulimwengu kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana. Ni lazima tutambue na kuamini kuwa tohara ya Agano la Kale iliyoahidiwa na Mungu kwa Ibrahimu inadhihirishwa katika Agano Jipya kwa tohara ya kiroho ya kuziosha dhambi iliyotimizwa kwa ubatizo wa Yesu. Na kwa nyongeza, inatueleza kuwa imani ya Ibrahimu ilihitajika sana kwa waisraeli pale walipotoa sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania.
Mungu alimwambia Ibrahimu, “mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi. Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako.” (Mwanzo 17:11-12). Kwa maneno mengine, Mungu aliiweka ahadi yake kwa Ibrahimu na wazawa wake kupitia tohara. Aliahidi kuwa atakuwa Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa wazawa wake, lakini iliwapasa Ibrahimu na wazawa wake kutahiriwa: “Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele.” (Mwanzo 17:13).
Hii ndiyo sababu katika watu wote wa ulimwengu, ni waisraeli tu ndio waliokuwa wakikata magovi yao tangu zama za Ibrahimu. Siku hizi, tohara imeenea sana kwa sababu ya faida zake za kiafya, lakini kwa wakati huo, ni wanaume wa kiisraeli tu ndio waliotahiriwa. Hii ilikuwa ni alama ya ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu, na Mungu alimfanya yeye pamoja na watu wa Israeli, wazawa wake, kubeba katika miilia yao alama hii ya agano alilolianzisha na kulithibitisha nao.
Mwanzo 17:11 inasema, “mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi.” Hivyo, tohara ilikuwa ni alama ya agano. Kwa kurudia tena, hivi ndivyo Mungu alivyoifanya ahadi yake: “Je, unafahamuje kuwa ninyi ni watu wangu? Utatambua kwa kuangalia kovu la tohara yako. Kuanzia sasa na kuendelea, kila mwanamume atakayezaliwa miongoni mwenu atatahiriwa govi yake. Kwa njia hii, agano langu litakuwa katika mwili wenu kwa kuwa ni agano la milele. Ninakuahidi wewe kuwa Mungu wako na Mungu wa wazawa wako. Na ninaahidi kukubariki wewe, kukuongeza kwa uzao, na kukufanya kuingia katika nchi ya Kanaani na kuishi ndani yake milele, na kuwafanya mataifa toka kwako, na kuwainua wafalme toka kwako” (Genesis 17:4-14).
Mungu alisema kuwa agano alilolianzisha na kulithibitisha na Ibrahimu na wazawa wake litakuwa katika miili yao. Kwa maneno mengine, ahadi ya Mungu ilichapishwa katika makovu ya waisraeli waliowekewa alama. Mungu alitoa ahadi yake kwa watu wa Israeli kupitia tohara yao, na kwa jinsi hiyo kutahiriwa kwa wanaume au kutotahiriwa kulionyesha ikiwa watu hao walikuwa ni wazawa wa Ibrahimu au hapana. Kwa hiyo, wale waliotahiriwa walitambuliwa na kubarikiwa na Mungu kuwa ni wazawa wa Ibrahimu ilhali wale ambao hawakutahiriwa hawakutambuliwa wala kubarikiwa hivyo.
 

Kwa Kweli Ibrahimu Ni Mtu Muhimu Sana Kwa Watu wa Israeli
 
Kwa watu wa Israeli, Ibrahimu ambaye ni baba wa imani, ni wa muhimu sana hata kuliko Musa ambaye ni baba wa Sheria. Japokuwa kuna waisraeli wengi ambao hawamkumbuki Nuhu, ni waisraeli wachache tu ndio ambao hawamkumbuki Ibrahimu. Baadhi yao wanaweza kumkumbuka Shem, Sethi, na Methusela, lakini Ibrahimu anabakia kuwa ni baba wa imani asiyesahaulika kwa watu wote wa Israeli. Wote wanamtambua, wanamwamini, na wanamfuata kama baba wa taifa lao. Kwa hiyo, ahadi ambayo Mungu aliifanya kwa waisraeli kupitia Ibrahimu bado inabaki kuwa ya maana na yenye kufaa.
Watu wa Israeli wanahakika na kuamini kuwa, “Sisi ni wazawa wa Ibrahimu. Watu wetu wanabeba alama ya tohara katika miili yao. Hivyo Mungu, ni Mungu wetu, na sisi tu watu wake mwenyewe.” Sababu inayowafanya waisraeli wajihesabu kuwa wao ni watu wateule ni kwa sababu bado wanaliamini agano ambalo Mungu alilolianzisha na kulithibitisha na Ibrahimu kwa kupitia tohara.
Ibrahimu alikuwa na wanawake wawili: mke wake wa kisheria Sarai ambaye baadaye Mungu alimpa jina la Sara, na mke wake wa pili aliyeitwa Hajiri, ambaye alikuwa ni mjakazi wa Sarai. Kwa kuwa ilionekana kana kwamba Sarai hangeweza kumzalia mtoto, Ibrahimu, katika mawazo yake binafsi alifikiria juu ya kuwa na mtoto kupitia Hajiri (Mwanzo 16:1-4). Lakini Mungu alisema wazi kuwa kwa sababu Sarai alikuwa ndiye mke halali wa Ibrahimu, basi kwa kupitia mtoto wa Sarai ndio Mungu atampatia Ibrahimu wazawa wengi kama nyota za angani. Kwa kuwa Mungu aliahidi kuwa atawatambua wale tu waliozaliwa katika mwili wa Sarai kuwa watu wake, Ishmaeli, ambaye alizaliwa toka kwa mke wa pili Hajiri hakutambuliwa kwa jinsi hiyo mbele za Mungu.
Ikiwa watu wa Israeli wasingelitahiriwa, basi ahadi ya Mungu aliyoifanya kwao ingekuwa haina maana na isingelifaa. Mungu aliwaeleza watahiriwe kama alama ya agano lake ili kwamba agano hili liwe katika miili yao. Kwa hiyo, waisraeli walihakikisha kuwa wanatahiriwa kwani kutotahiriwa kungeizuia ahadi ya Mungu kutendeka na kufaa. Bila shaka hakukuwa na mtu yeyote miongoni mwa watu wa Israeli ambaye hakutahiriwa, kwa sababu wanafahamu vizuri kuwa, wasiotahiriwa ni kama wamataifa ambao kwao ahadi ya Mungu haina maana.
 


Tohara ya Kiroho

 
Agano ambalo Mungu alilianzisha na kulithibitisha na Ibrahimu na wazawa wake lilitimizwa lote kupitia ondoleo la dhambi zote kulikotimizwa na Yesu Kristo alipokuja hapa duniani na akazichukua dhambi za wanadamu kwa kubatizwa na Yohana Mbatizaji.
Mungu aliwaeleza waisraeli kulifanya lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania na pazia lake la kufunika kwa kulifuma kwa nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa (Kutoka 26:31, 27:16). Kupitia muundo huu wa kina na wa wazi wa Hema Takatifu la Kukutania, Mungu ametufundisha kuwa wokovu unakuja kupitia Yesu Kristo. Wale wanaouamini ukweli kuwa Bwana alikuja hapa duniani, akazichukua dhambi za wanadamu kwa ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana katika umri wa miaka 30, na kuwa alikufa Msalabani, akafufuka tena toka kwa wafu, na kwamba ametusamehe dhambi zetu zote—basi wote wanaoamini hivyo ni wazawa wa Ibrahimu. Mungu amekuwa ni Mungu wa wale wanaoamini katika nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu na kitani safi ya kusokotwa za Hema Takatifu la Kukutania.
Kwa kuuamini ubatizo wa Yesu, ni lazima sisi sote tutahiriwe kiroho. Tohara hii ya kiroho si kitu kingine bali ni kuzikata dhambi za mioyo yetu kwa kuamini kuwa dhambi zetu zote zilipelekwa kwa Yesu Kristo kwa kupitia ubatizo wake (Warumi 2:29).
Kwa hiyo, wale waliopokea ondoleo la dhambi sasa kwa kuiamini injili ya maji na Roho iliyodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, nyekundu na kitani safi ya kusokotwa wote hao ni wafalme katika Ufalme wa Mungu na ni wana wa Mungu mwenyewe. Kama ambavyo Mungu aliahidi, “wafalme watatoka kwako (Mwanzo 17:6),” Ni kweli kuwa watu wake wanainuka kila mahali ulimwenguni.
Ikiwa tunataka kufanyika wazawa wa Ibrahimu, ni lazima tuuamini ubatizo ambao Yesu aliupokea hapa duniani na damu yake Msalabani. Kwa kweli, siwezi kusisitiza vya kutosha zaidi kuhusu ilivyo muhimu kufahamu na kuamini katika ubatizo wa Yesu. Yesu Kristo ni Mfalme wa wafalme. Yeye ni Mfalme wa wafalme aliyekuja akivaa kanzu ya zambarau (Yohana 19:5). Yesu Kristo ni Mfalme wa ulimwengu na ndiye muumbaji. Kwa kuwa yeye ni Mwana pekee wa Mungu, alikuja hapa duniani kwa unyenyekevu na kwa mapenzi ya Mungu ili kutuokoa toka katika dhambi zetu zote, alizichukua dhambi zetu zote kwa ubatizo wake mara moja. Ili kuziondoa dhambi zetu, alizikata dhambi zote toka katika mioyo yetu na akaziweka katika mwili wake binafsi kwa ubatizo wake, na alihukumiwa kwa ajili ya dhambi zetu zote kwa kuimwaga damu yake Msalabani. Kwa hiyo, wote wanaouamini ukweli huu wanaweza kuwa wazawa wa Ibrahimu.
Ibrahimu, familia yake, na wazawa wake wote walitahiriwa kimwili. Hata watumwa waliokuwa wamenunuliwa kwa fedha toka kwa wa mataifa wote pia walitahiriwa. Walipoliamini agano na wakatahiriwa, hata hawa watumwa walibarikiwa, na Mungu pia alikuwa ni Mungu wao. Kwa hiyo, ni kwa imani ndipo tunapokuwa wana wa Mungu, na ni kwa imani ndipo tunabarikiwa na Mungu, ni kwa imani ndipo tunaingia mbinguni, na ni kwa imani ndipo tunaishi kama wafalme katika dunia hii. Katika kipindi cha Agano Jipya, imani hii ni imani ya wale wanaoamini kwamba Yesu alizichukua dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake.
Hata hivyo, watu wengine wanadai kuwa ubatizo huu wa Yesu si wa muhimu kiasi hicho, kwani wanaamini kwamba wamesamehewa dhambi zao kwa kuiamini damu ya Yesu tu pale Msalabani. Japokuwa wanaamini juu ya suala la kuweka mikono juu ya kichwa cha mwanasadaka wa sadaka ya kuteketezwa lililofanyika katika kipindi cha Hema Takatifu la Kukutania, lakini wanaweka mkazo kidogo sana juu ya ubatizo wa Yesu mwenyewe. Kwa hiyo wanakazia kuwa kwa sababu imani ya Ibrahimu ilikubaliwa kabla ya kuja kwa Yesu hapa duniani na hata kabla ya Hema Takatifu la Kukutania la Musa, hivyo bado wanaokolewa kwa kuliamini Neno la damu la Msalaba tu hata bila ya kuliamini Neno la wazi la ubatizo wa Yesu.
Lakini ni lazima tukumbuke kuwa wakati Mungu alipomwambia Ibrahimu kumletea ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo dume wa miaka mitatu, na hua, na kind la njiwa—ili kumfanya Ibrahimu kutambua kuwa Mungu atampatia nchi ya Kanaani na wazawa wake kuwa urithi wao—Mungu alikuwa na wazo la sadaka ya kuteketezwa kwa moto katika fikra zake. Mwanzo 15:17 inasema, “Jua lilipokwisha kutua na giza kuingia, tanuru ifukayo moshi na mwenge uwakao moto vikapita katikati ya vile vipande vya nyama.” Mungu alizikubali pia sadaka za kuteketezwa za Habeli na imani yake, lakini hakuitakabali imani ya Kaini, ambaye hakuiamini imani hii ya sadaka ya kuteketezwa.
Miongoni mwa Wakristo wa leo, kuna watu wengi ambao wanafahamu kimakosa kuwa wanaokolewa kwa kumwamini Yesu kiupofu hata bila ya kutahiriwa kiroho kwa imani. Wanaamini tu juu ya kusulubiwa kwa Yesu tu na hawauamini ukweli kuwa dhambi zao zote zilipelekwa kwa Yesu kwa kupitia ubatizo wake. Watu wa jinsi hii hawawezi kamwe kuwa watu wa Mungu mwenyewe, kwa sababu kuamini kwa jinsi hiyo hakuwezi kuziondoa dhambi zao toka katika mioyo yao. Kama alivyosema kuwa alama ya agano lake ipo katika mwili wa waliotahiriwa, hivyo basi wasiotahiriwa hawana la kufanya kuhusiana na ahadi hii ya Mungu.
Je, watu wanaweza kuokolewa toka katika dhambi bila ya kuuamini ubatizo ambao Yesu aliupokea toka kwa Yohana Mbatizaji? Je, watu wa jinsi hiyo wanaweza kuwa wana wa Mungu? Je, wanaweza kuingia Mbinguni? Je, wanaweza kuwa wafalme wa Ufalme wa Mungu? Jibu kwa maswali haya ni hapana! Kifungu kikuu cha maandiko tulichokisoma leo kinatoa ushahidi wa wazi kwa jibu hili. Kwa sasa, ahadi ambayo Mungu aliifanya kwa Ibrahimu ni ahadi sawa na ile aliyoifanya kwako na kwangu, sisi ambao tumepokea ondoleo la dhambi kwa kumwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wetu katika ubatizo wake na damu yake Msalabani. Hivyo, kwa wale wanaoamini, Neno lilelile la baraka ambalo Mungu aliliongea kwa Ibrahimu linatumika hata kwao.
 


Waamini wa Kweli wa Yesu Hawafuati Mafundisho Binafsi Waliyojiundia

 
Neno la Mungu katika Biblia ni la wazi na ukweli kamili wa wokovu; kadri tunavyolisoma na kulitafakari, ndipo linapozidi kuwa la wazi zaidi. Miongoni mwa Wakristo wa leo, wapo wengi ambao imani yao ina makosa ambao wanamwamini na kumfuata Mungu kwa mawazo yao binafsi, na ambao hawatambui kuwa wanachokiamini ni uongo. Msingi wa imani wa watu wa jinsi hiyo ni msingi potofu. Kuamini kiupofu kwamba Yesu amewaokoa kwa vyovyote vile kunaweza kuzitosheleza dhamiri zao binafsi, lakini ni lazima watambue kuwa Mungu haikubali imani yao ya kiupofu.
Bwana wetu alisema yeyote anayetaka kumfuata ni lazima ajikane mwenyewe na kisha auchukue Msalaba wake mwenyewe. Yeyote anayeamini katika Neno la Mungu ni lazima aweke chini mawazo yake na aamini kwa kadri ambavyo Neno la Mungu linasema. Leo hii, mimi na wewe ni lazima tuamini katika ondoleo la dhambi ambalo Yesu Kristo ametupatia kwa kuja hapa duniani, kwa kuzichukua dhambi za ulimwengu kwa ubatizo wake, kwa kuimwaga damu yake Msalabani, na kwa kufufuka kwake tena toka kwa wafu.
Katika siku hizi, kuna watu wengi ambao hawaamini hivyo, lakini ambao kwa upofu wanaendelea kulishikilia jina la Yesu, wakisema kuwa wana njia yao ya kuamini. Imani ya watu wa jinsi hiyo haijishughulishi na injili ya maji na Roho ambayo ilitolewa na Yesu. Kwa mfano, kuna watu wanaodai kuwa Yesu alionekana walipokuwa wakiomba katika milima fulani, wakisisitiza kuwa hivyo ndivyo walivyookolewa. Kwa mfano, kuna wale wanaodai kuwa dhambi zao zilipotea pale walipoenda Kanisani, walipofunga, walipokesha usiku wakiomba, eti kwa sababu walikuwa wamehuzunishwa sana na dhambi zao ambazo wasingeweza kuzitoa kwa sala zao za kawaida za toba.
Aina hizi za imani hazijihusishi na wokovu wa kweli unaopatikana kupitia injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana wetu. Ni wapi panaposema katika Neno la Mungu kwamba Mungu atazisamehe dhambi zetu tukiwa na imani ya jinsi hiyo? Hakuna popote! Watu hawa hawafahamu dhahiri kuwa Mungu ndiye mkamilifu na kwamba Yesu ni Mwenyezi, wanaliazima jina la Kristo, wanaongeza ufahamu wao wa Mungu usio wa uhakika katika imani yao isiyo ya uhakika—kwa hiyo wanaliitia jina la Mungu bure, na wanajikusanyia hasira ya Mungu zaidi. Watu wa jinsi hiyo wamejitengenezea Yesu wa kufikirika tu na aina fulani ya wokovu wao binafsi, na wanaamini uongo unaotokana na fikra zao binafsi.
Mwanzo 17:14 inasema, “Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu huyo atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.” Mungu ametuahidi kwa wazi kwamba atatuokoa toka katika dhambi zetu kupitia tohara ya kiroho. Na Mungu ametuahidi sisi bila kubadilika kuwa ni wale tu wanaozaliwa upya kwa maji na kwa Roho ndio watakuwa wana wake. Kwa hiyo, wale wanaoiamini damu ya Yesu tu Msalabani bila ya kuuamini ubatizo wake hawawezi kamwe kufanyika wana wa Mungu. Watu wa jinsi hiyo wamemkana Mungu, kwa kuwa hawajaiamini injili iliyotabiriwa na Mungu, na kwa hiyo wataondolewa toka katika watu wa Mungu na watalaumiwa na Mungu.
Msingi wa imani unaoweza kutuokoa toka katika dhambi zetu si mwingine bali ni injili ya maji na Roho. Ni pale tu injili ya maji na Roho inapokuwa imewekwa kama msingi wetu ndipo tunapoweza kuliamini Neno la Mungu kwa ukamilifu. Je, inawezekanaje kwa wamataifa wa kiroho ambao mioyo yao inabaki haijatahiriwa, je, wanaweza kulibeba Neno la Mungu katika mioyo yao? Kamwe hawawezi kufanya hivi! Kwa sababu injili ya maji na Roho inaturuhusu kutahiriwa kiroho, hali ikituwezesha kufanyika wana wa Mungu, bila ya kuwa na msingi huu kamili, Neno la Mungu litakuja kwetu kama elimu fulani ya ufahamu tu.
Hii ndio sababu mafundisho ya kiroho kwa watumishi waliozaliwa upya yanaweza kueleweka na yapo kwa wale ambao kimsingi wanaamini katika injili ya maji na Roho. Kwa maneno mengine, ni wale tu ambao wamezaliwa upya kwa maji na kwa Roho ndio wanaoweza kulikisia na kulielewa Neno la Mungu. Tunapokutana na watu ambao, kwa kukosa ufahamu wa injili ya maji na Roho wanadai kuwa wamezaliwa upya kupitia damu ya Msalaba, japokuwa wanasema kuwa sisi sote tunamwamini Mungu mmoja, kwa kweli tunahisi kuwa tunazungumzia juu ya Mungu tofauti na wa kwao. Ni nani ambaye ni Mungu halisi hapa? Mungu halisi ni Mungu aliyelitoa Neno lake la ahadi kwa Ibrahimu.
Mungu alimwahidi Ibrahimu na wazawa wake, “Na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele.” (Mwanzo 17:13). Je, iko wapi alama inayotuonyesha kuwa tumepokea ondoleo la dhambi zetu? Inapatikana katika mioyo yetu. Kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu Kristo katika mioyo yetu, tumefanyika kuwa wana wa Mungu, ambao mioyo yao imepokea tohara ya kiroho kwa kuiamini injili ya kweli. Tumefanyika wana wa Mungu kwa kuamini kwa mioyo yetu yote kwamba Bwana alibatizwa kwa ajili ya dhambi zetu ili kuzichukua dhambi hizi zote na kwa jinsi hiyo tumetahiriwa kiroho, yaani tumepokea tohara ya kiroho.
Ni kwa imani yetu katika ukweli huu kwamba tulizipeleka dhambi zetu zote kwa Yesu Kristo, na kisha Yesu akazichukua dhambi hizi kuzipeleka Msalabani, alisulibiwa kwa ajili yetu, akafufuka tena toka kwa wafu, na kwa hiyo ametuokoa wote toka katika dhambi zetu. Kwa maneno mengine, ni kwa imani hata tumefanyika kuwa wana wa Mungu. Ni kwa imani hata tumefanyika watu wasio na dhambi. Je, tuna dhambi yoyote iliyobakia ndani yetu? Kwa kweli sio hivyo! Kwa kweli hata hivyo hatuna dhambi! Yote haya yalitimizwa na ukweli mzuri wa injili.
 


Je, Tunawezaje Mimi na Wewe Kuwa Wazawa wa Ibrahimu?

 
Tumefanyika wazawa wa Ibrahimu kwa sababu tulitahiriwa kiroho kwa kuziamini kazi za Yesu zilizodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu za Hema Takatifu la Kukutania. Ni kwa sababu tunaamini katika ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani kuwa tumetahiriwa kiroho na kufanyika wana wa Mungu. Ni kwa sababu tunaamini kuwa Yesu alizichukua dhambi zetu zote kwa ubatizo wake na alihukumiwa kwa ajili ya dhambi zetu zote pale Msalabani na kwa jinsi hiyo tumepokea ondoleo la dhambi. Na hivi ndivyo mimi na wewe tulivyofanyika wazawa wa Ibrahimu kiroho.
Wale waliozaliwa upya kwa maji na kwa Roho ni lazima watambue sasa jinsi walivyo. Wewe na mimi, tunaoamini katika injili ya maji na Roho, sote tu wana wa Mungu na watu wake mwenyewe, ambao tumetahiriwa kiroho kwa imani, yaani tumepokea tohara ya kiroho kwa imani.
Sisi ni wafalme wa Ufalme ujao wa Miaka 1000 ujulikanao kama Ufalme wa Milenia ambao utatawala uumbaji wote wa Mungu na kufurahia utukufu wake wote. Hivi ndivyo hali yetu ilivyobadilika kwa sasa. Je, watu wa ulimwengu huu wanafahamu vizuri kuwa sisi ni akina nani? Kwa kweli hawafahamu. Lakini sisi ndio ambao hali zetu za kiroho zimebadilika kwa kuliamini Neno la Mungu. Kwa hiyo, tunaweza kujifahamu wenyewe kwa hakika bila kuyumba wala kubadilika.
Wale waliozaliwa upya kwa Neno la Mungu wanafahamu kuwa wao ni akina nani. Kimsingi tupo tofauti kabisa na wale ambao wanajitangaza katika wao wenyewe katika jamii za dini za kidunia, ambao wanahubiri mafundisho potofu hata pale ambapo hawafahamu kitu, na ambao wanawatazama vibaya wale waliozaliwa upya, ambao ni watu wa kweli wa Mungu. Kama ambavyo watu wa Israeli wanajiamini wenyewe kuwa ni watu wateule wa Mungu na kama vile wanavyouhesabu uzao wa Ishmaeli kuwa ni tofauti na wa kwao, sisi ambao ni wazawa wa kiroho wa Ibrahimu pia tunayo haki ya kujihesabu sisi wenyewe kuwa ni watu wateule wa Mungu.
Sisi tunaoiamini injili ya maji na Roho kwa bahati tumefanyika wazawa wa Ibrahimu kwa kupitia imani yetu. Tunaweza kuuingia Ufalme wa Mbinguni kwa imani yetu katika injili ya nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu zilizodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania.
Na kama ambavyo Mungu alimwahidi Ibrahimu kwamba atawafanya wazawa wake kuwa wengi kama zilivyo nyota za angani, basi tunaweza kushuhudia kwa macho yetu jinsi ambavyo agano hili limetimizwa kwetu. Hii ni baraka ambayo Mungu ametupatia sisi.
Kwa kupitia tohara ya mioyo yetu, Mungu ametuokoa toka katika dhambi za ulimwengu. Na tohara hii ya kiimani imefanyika kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa vilivyotumika katika kulitengeneza lango la Hema Takatifu la Kukutania.