Search

Mahubiri

Somo la 11: Maskani

[11-5] Jinsi Ambavyo Waisraeli Walianza Kutoa Sadaka Katika Hema Takatifu la Kukutania: Msingi wa Kihistoria (Mwanzo 15:1-21)

Jinsi Ambavyo Waisraeli Walianza Kutoa Sadaka Katika Hema Takatifu la Kukutania: Msingi wa Kihistoria
(Mwanzo 15:1-21)
“Baada ya mambo hayo, neno la BWANA lilimjia Abramu katika maono, likisema, ‘Abramu, Usiogope. Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana’. Lakini Abramu akasema, ‘Bwana Mungu, utanipa nini hali ninaendelea kuishi bila mtoto, na mrithi wa nyumba yangu ni Eliezeri wa Dameski?’ Tazama hujanipa mtoto; mmoja aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye atakayekuwa mrithi wangu!’ Ndipo neno la BWANA lilipomjia likisema, ‘Huyu hatakuwa mrithi wako, bali atakayetoka katika mwili wako ndiye atakayekuwa mrithi wako’. Kisha Mungu akamleta Abramu nje na kumwambia, ‘Tazama mbinguni, zihesabu nyota, kama kweli utaweza kuzihesabu. Hivi ndivyo watakakavyokuwa wengi wazawa wako’. Abramu akamwamini BWANA, naye Mungu akamhesabu kuwa mkamilifu. Kisha Mungu akamwambia Abramu, ‘Mimi ndimi BWANA niliyekuleta toka Uru katika mji wa Wakaldayo, ili nikupe nchi hii uimiliki’. Ndipo Abramu akasema, ‘Bwana Mungu, nitajuaje kuwa nitaimiliki nchi hii?’ Ndipo BWANA akamwambia, ‘Niletee ndama wa miaka mitatu, mwanambuzi jike wa miaka mitatu, kondoo dume wa miaka mitatu, na hua na kinda la njiwa’. Abramu akaleta wanyama hao wote na akampasua kila mnyama vipande viwili, akavipanga katika mistari miwili vikielekeana; lakini wale ndege hakuwakata vipande viwili. Na tai walipoiendea hiyo mizoga, Abramu akawa anawafukuza. Jua lilipokuwa likitua, Abramu alishikwa na usingizi mzito; giza nene na hofu vikamfunika. Ndipo Mungu akamwambia Abramu: ‘Ufahamu hakika ya kuwa wazawa wako watakaa kama wageni katika nchi isiyo yao, watatumikishwa na kuteswa kwa miaka mia nne. Hata hivyo nitaliadhibu taifa watakalolitumikia; kisha baada ya kitambo watatoka wakiwa na mali nyingi. Lakini wewe utaishi miaka mingi na utazikwa kwa amani katika uzee mwema. Wazawa wako watarudi hapa katika kizazi cha nne, kwa sababu uovu wa Waamori bado haujakamilika’. Jua lilipokwisha kutua na giza kuingia, tanuru ifukayo moshi na mwenge uwakao moto vikapita katikati ya vile vipande vya nyama. Siku hiyo, BWANA akafanya agano na Abramu, akisema, ‘Nimewapa wazawa wako nchi hii, toka mto Naili wa Misri hadi ule mto mkubwa wa Eufrati, yaani nchi za Wakeni, Wakenizi, Wakedmoni, Wahiti, Waperizi, Warefaimu, Waamori, Wakanaani, Wagirgashi, na Wayebusi.’”
 


Imani ya Ibrahimu Katika Neno la Mungu

 
Ninaiheshimu na kuitamani sana imani ya Ibrahimu kama inavyoonyeshwa katika Biblia. Tunapoiangalia imani ya Ibrahimu, tunaweza kuona mateso na juhudi ya imani yake ambayo kwa hiyo alimfuata Yehova, na kwa jinsi hiyo hatuwezi kufanya lolote bali ni kuitamani imani ya Ibrahimu. Mungu alimbariki sana Ibrahimu, kama inavyoonyeshwa katika Mwanzo 12:3, ambapo Mungu alisema, “Nitawabariki wote watakaokubariki, Na nitamlaani yeyote atakayekulaani; na katika wewe jamaa wote wa dunia watabarikiwa.” Baraka hizi nyingi zinaonekana pia katika Mwanzo 15:1, ambapo Mungu alitamka kwa Ibrahimu kuwa “Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana”. Mungu alikuwa na upendo maalum kwa Ibrahimu kiasi kwamba Mungu alijiona kuwa ni Mungu wa Ibrahimu.
Baada ya kumuongoza Ibrahimu kutoka katika Uru, mji wa Wakaldayo, Mungu alijifunua kwake, na akamwambia, “Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana”. Baada ya Mungu kusema haya, Ibrahimu alimuuliza Mungu, “Utanipa nini?” Maneno haya ya Ibrahimu hayakuwa maneno ya kutokuamini yanayotoka katika moyo mgumu kuuliza kuwa Mungu atampa nini; bali yalikuwa ni maneno yaliyojaa haja ya kina ya Ibrahimu ya kubarikiwa na Mungu. Je, ni aina ipi ya baraka ambayo Ibrahimu aliitarajia toka kwa Mungu? Hii inaonekana katika maneno ambayo Ibrahimu alimwambia Mungu: “Bwana Mungu, utanipa nini? Kwa maana sina mtoto, mtumishi wangu Eliezeri wa Dameski ndiye mrithi wangu, kwa kuwa atakuwa ni mwana wangu wa kupanga ambaye atarithi vitu vyangu vyote! Utanipa nini?” Hapa inatupasa kufahamu jinsi ambavyo Ibrahimu alihitaji sana kuwa na mtoto wake binafsi. Pengine wale ambao wamechagua kwa hiari yao kutokuwa na watoto wanaweza wasimuonee huruma Ibrahimu katika hitaji lake, lakini ukweli ni kuwa alitamani sana kuwa na mtoto wake binafsi kama mrithi wake.
Kama ambavyo Mungu anawapatia baraka wana wake wote walioumbwa kwa mfano wake; wanadamu pia wanatamani sana kuwapatia watoto wao mambo mazuri. Kama tulivyoona wakati Ibrahimu alipomwambia Mungu, “mtumishi wangu atakuwa mrithi wangu”, tunaweza kutambua jinsi ambavyo alihitaji kubarikiwa na Mungu ili kwamba aweze kuwa na mtoto ambaye atakuwa mrithi wake. Kisha Mungu akamwambia Ibrahimu, “Hiyo si kweli, mmoja atakayetoka katika mwili wako ndiye atakayekuwa mrithi wako. Mmoja anayezaliwa katika mwili wa mke wako atakuwa mrithi wako, na sio mtumishi wako Eliazeri wa Dameski”.
Kisha Mungu akamleta Ibrahimu nje na kumwambia, Tazama mbinguni, zihesabu nyota. Hivyo Ibrahimu akaziangalia nyota. Nyota zisizohesabika mandhari nzuri ya kupendeza ilionekana angani. Wakati Mungu alipomwambia Ibrahimu kuzihesabu nyota na kuona kama anaweza kuzihesabu, Ibrahimu alimjibu Mungu kuwa ni nyingi mno na ni vigumu kuzihesabu zote. Kisha Mungu akamuahidi Ibrahimu kuwa atampa wazawa wengi kama zilivyo nyota za angani.
Ibrahimu akaliamini lile Neno la ahadi ambalo Mungu alimpatia. Hivi ndivyo alivyoweza kuwa baba wa imani ambaye aliliamini kwa hakika Neno la Mungu. Hivyo Mungu alimwambia, “Imani yako ni sahihi. Ni kweli kuwa unaliamini Neno langu. Hivyo nitakubariki kwa kukupatia wazawa wengi kama zilivyo nyota za angani.”
 


Sadaka ya Ibrahimu ya Kuteketezwa na Ahadi ya Mungu juu ya Nchi ya Kanaani

 
Mungu alimuongoza Ibrahimu kutoka katika nchi ya Ukaldayo na alimuahidi kuwa atampatia yeye na uzao wake nchi ya Kanaani. Je, kuna uthibitisho gani kuwa Mungu ataitimiza ahadi hii? Hii inaonekana kwa jinsi ambavyo Mungu alimwambia Ibrahimu, “Niletee ndama wa miaka mitatu, mwanambuzi jike wa miaka mitatu, kondoo dume wa miaka mitatu, na hua na kinda la njiwa. Huu ni uthibitisho wa agano ambalo nimelifanya nawe la kuwapatia wazawa wako nchi ya Kanaani”. Hii inaonyesha kuwa wazawa wa Ibrahimu watakuja kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa Mungu ili kusafishwa dhambi zao; na ahadi ya Mungu kwao ilikuwa kwa imani hii uzao wa Ibrahimu utaingia katika nchi ya Kanaani.
Ibrahimu alipokuwa amelala katika usingizi mzito wakati akitoa sadaka ya kuteketezwa, Mungu alimtokea na kumuahidi, “Ufahamu hakika ya kuwa wazawa wako watakaa kama wageni katika nchi isiyo yao, watatumikishwa na kuteswa kwa miaka mia nne. Hata hivyo nitaliadhibu taifa watakalolitumikia; kisha baada ya kitambo watatoka wakiwa na mali nyingi. Lakini wewe utaishi miaka mingi na utazikwa kwa amani katika uzee mwema. Wazawa wako watarudi hapa katika kizazi cha nne.” (Mwanzo 15:13-16).
Kwa maneno mengine, Mungu aliahidi kuwa atawafanya wana wa Israeli kufanikiwa katika nchi ya Misri, na kisha atawaongoza kurudi nchi ya Kanaani. Ili Mungu aweze kufanya hivyo, aliamua kuwaamuru kutoa sadaka ambazo zinaondoa dhambi zao katika Hema Takatifu la kukutania. Ili kumuonyesha Ibrahimu kuwa ataitimiza ahadi hii Mungu aliamua kuupitisha mwenge uliowaka juu ya vipande vile vya wanyama vilivyokuwa vimekatwa toka katika wanyama ambao Ibrahimu alimtolea Mungu sadaka ya kuteketezwa.
Kwa jinsi hii Mungu alimuahidi Ibrahimu kuwa atamfanya yeye pamoja na wazawa wake kuwa watu wake, wanaotokana na sadaka ya ondoleo la dhambi kama inavyodhihirishwa katika sadaka ya kuteketezwa. Mungu pia alimuahidi Ibrahimu, “Nimewapa wazawa wako nchi hii, toka mto Naili wa Misri hadi ule mto mkubwa wa Eufrati, yaani nchi za Wakeni, Wakenizi, Wakedmoni, Wahiti, Waperizi, Warefaimu, Waamori, Wakanaani, Wagirgashi, na Wayebusi.” Sababu iliyomfanya Mungu atoe ahadi hii ni kwamba alifahamu kuwa ataziosha dhambi za Ibrahimu na wazawa wake kupitia sadaka ya kuteketezwa. Mchakato ambao Mungu aliutumia kulitimiza Neno alilomuahidi Ibrahimu unaonekana katika historia nzima ya Agano la Kale.
Mungu alimfanya Yusufu kuwa waziri mkuu wa Misri na aliiongoza familia yote ya Yakobo kwenda katika nchi ya Misri ili wakaongezeke (Mwanzo 41:37-45; Mwanzo 47). Lakini baada ya muda mrefu, alitokea Farao ambaye hakuifahamu vizuri huduma nzuri ya Yusufu aliyoifanya kwa jamii ya Misri na akaanza kuwatesa wana wa Israeli ambao walikuwa wakifanikiwa katika nchi. Mara waisraeli walifanywa kuwa watumwa, wakatumikishwa kazi za shuruti katika Misri (Kutoka 1:8-14). Hata hivyo wana wa Israeli waliendelea kufanikiwa jambo ambalo lilimfanya Farao aendelee kuwatesa zaidi kwa mizigo mizito ya utumwa. Ilikuwa wakati ule wana wa Israeli walipokuwa wakiteseka chini ya kongwa la utumwa kwa miaka 400 ndipo walipoanza kumtafuta Mwokozi.
Kwa kupitia Musa, Mungu aliwaongoza kutoka katika nchi ya Misri ili kukwepa kongwa la utumwa (Kutoka 14:21-25). Kwa wana wa Israeli ambao sasa walikuwa wametoroka katika nchi ya Misri, Mungu aliwapatia utoaji wa sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania kwa kupitia Musa. Mungu aliwafanya wasafishe dhambi zao kwa kumtolea sadaka zao za kuteketezwa. Hivyo wana wa Israeli waliipokea Sheria toka kwa Mungu (Kutoka 20) na utaratibu wa kutoa sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania (Mambo ya Walawi 1-4). Kwa kupitia sheria and utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania, waisraeli walikuja kufahamu juu ya sadaka ya kuteketezwa ambayo ingaliwafanya kusamehewa dhambi zao, na Mungu aliwafanya wote walioamini katika ukweli huu kuwa watu wake, na Mungu akalibariki taifa la Israeli ili kuwa ufalme wa kikuhani na taifa takatifu la Mungu (Kutoka 19:6).
Mwishoni, tunaweza kuona kwamba kupitia sadaka ya kuteketezwa, Mungu aliitimiza ahadi yake kwa Ibrahimu ya kwamba atampatia wazawa wengi kama zilivyo nyota za angani na kwamba atawapatia nchi ya Kanaani. Wakati Waisraeli walipoondoka Misri, idadi ya wanaume waliokuwa na zaidi ya miaka 20 na walioweza kupigana katika vita walikuwa zaidi ya 600,000. Kimsingi, Mungu aliitimiza ahadi yake kwa Ibrahimu kwa uhakika.
Tunapoitazama imani ya Ibrahimu, ya kwamba aliliamini Neno la Mungu la ahadi, tunaona kuwa Mungu aliikubali imani hii ya Ibrahimu. Kwa maneno mengine, sababu iliyomfanya Mungu kumpenda na kumbariki Ibrahimu ni ile imani yake katika Neno la Mungu. Kwa sababu Ibrahimu aliamini katika Neno la Mungu, Mungu alipendezwa na imani yake. Hivyo basi, Mungu alihitaji kujenga taifa la Israeli kutoka katika Ibrahimu, na kwa kupitia sadaka ya kuteketezwa iliyotolewa na wazawa wake, kuitimiza ahadi ya kutahiriwa.
Tunaweza kuona kuwa imani ya Ibrahimu ilikubaliwa na Mungu pale alipokuwa akiitoa sadaka ya kuteketezwa kwa Mungu. Imani hii inaturuhusu pia kusamehewa dhambi zetu zote si kwa matendo yetu, bali kwa imani katika Neno la Mungu. Kwa wale ambao wameipokea tohara ya kiroho ambayo inaziondoa dhambi zao kwa kupitia sadaka ya kuteketezwa kwa kuamini katika Neno lake Mungu kama Ibrahimu alivyofanya, basi Mungu ameruhusu nchi ya Kanaani kuwa baraka yake. Kwa hiyo, Mungu anapenda tuwe na imani kama aliyokuwanayo Ibrahimu. Mungu anataka mimi na wewe leo hii tupokee ondoleo la dhambi katika mioyo yetu kwa kuliamini Neno lake kama vile Ibrahimu alivyofanya na ili tuurithi ufalme wa Mungu. Mungu Baba alizipeleka dhambi zote kwa Yesu Kristo kupitia ubatizo wake na akamfanya kuwa “Mwanakondoo wa Mungu” kwa binadamu wote. Mungu anatuhitaji tuamini katika kweli yake kama Ibrahimu alivyofanya. Mungu anataka kuwafanya waamini wa jinsi hiyo kuwa watu wake milele na milele.
Mungu anatuonyesha sisi kuwa kama vile ambavyo Ibrahimu alibarikiwa sana kwa sababu ya imani yake katika Neno la Mungu, hata sasa wewe na mimi tunaweza pia kupokea baraka zote za Mungu kwa imani ile ile ambayo Ibrahimu alikuwa nayo. Mungu alimuita Musa katika Mlima Sinai, akampatia amri na utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa, na akawabariki wote wanaoamini katika Neno lake kuwa watu wake mwenyewe.
Mungu ametufanya sisi pia kuwa watu wake kwa kupitia ondoleo la dhambi kama inavyoonyeshwa katika utaratibu wa Hema Takatifu la Kukutania hata kama tumeshindwa kuifuata sheria yake. Kupitia imani yetu katika ukweli unaodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania, Mungu ametuwezesha kupokea baraka zake za milele. Hivyo, inatupasa sote tuwe watu wa Mungu kwa kuuamini ukweli huu uliodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania. Ni pale tu tutakapoamini katika mioyo yetu kuwa Mungu ametuletea Yesu Kristo na ametupatia wokovu wetu kwa kupitia Hema Takatifu la Kukutania ndipo tunapoweza kupokea baraka nyingi.
 


Kama Ambavyo Ibrahimu Aliliamini Neno la Mungu, Sisi Nasi ni Lazima Tumwamini Mungu kwa Msingi wa Neno lake

 
Ibrahimu alibarikiwa si kwa sababu ya matendo yake mema, bali kwa sababu ya imani yake katika Neno la Mungu. Kupitia sheria, Mungu ametuwezesha kuzifahamu dhambi zetu na kwa kupitia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania, ametuwezesha kupokea ondoleo la dhambi zetu zote kwa kuzipeleka dhambi zetu kwenye sadaka ya kuteketezwa isiyo na mawaa na kuitoa damu yake kwa Mungu. Kwa namna iyo hiyo, Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alizichukua dhambi zetu zote kwa kupitia ubatizo wake, alihukumiwa kwa sababu ya dhambi zetu kwa kifo pale msalabani na ametusamehe dhambi zetu zote kwa kufufuka kwake toka kwa wafu. Dhambi zetu zote zinaweza kusamehewa na tunaweza kuwa wana wa Mungu kwa kuamini katika ukweli huu. Biblia inatuambia kuwa wale tu wanaoamini katika kweli yake kwa mioyo yao wanaweza kupokea baraka zote za Mungu. Kwa kuliamini neno la Mungu, ni lazima tulifanye Neno lake la wokovu kuwa jambo muhimu na la baraka ambalo halipatikani popote.
Ni kwa nini Ibrahimu alipokea baraka nyingi toka kwa Mungu? Alibarikiwa kwa sababu aliamini kile ambacho Mungu alimwambia. Hata leo, ikiwa mimi na wewe tutaliamini Neno la Mungu lililoandikwa katika Biblia tunaweza kuwa na imani kama aliyokuwanayo Ibrahimu na hivyo kupokea baraka nyingi za Mbinguni. Hili si jambo gumu la kufanya. Kama tunataka kuwa na ushahidi unaoonyesha kuwa sisi tu watu wa Mungu, tunachotakiwa kufanya si kujaribu kumridhisha Mungu kwa matendo yetu bali ni kwa kuliamini Neno la Mungu kwa mioyo yetu.
Mungu alimuahidi Ibrahimu kwa Neno lake kwamba atampatia nchi ya Kanaani kwa wazawa wake. Sisi sote tunaoishi katika nyakati za sasa ni lazima tuamini kuwa huduma nne za Yesu, ambazo zilidhihirishwa na kutabiriwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, rangi zilizokuwemo katika Hema Takatifu la Kukutania, zimetuokoa kutoka katika dhambi zetu zote. Na kwa kuamini hivyo, ni lazima tupokee ondoleo la dhambi zetu, tufanyike wana wa Mungu, na kisha tuurithi Ufalme wa Mbinguni.
Ni lazima tuamini kwa hakika katika Neno la Mungu, kwa sababu hakuna Neno la Mungu hata moja ambalo linaishia utupu. Pia ni vema tuliamini Neno la Mungu kwa sababu Neno lake ni kweli kamili na muhimu sana kwa imani yetu. Ni lazima kwa hakika tufahamu Neno lake la Maji na Roho Mtakatifu, na ni sharti tuliamini pasipo kuwa na shaka. Je, ni kwa nini tuliamini Neno la Mungu la Maji na Roho Mtakatifu? Ni kwa sababu ndiyo kweli halisi. Je, unaamini sasa? kama unaamini ukweli huu kwa moyo wako wote na kuukiri kwa kinywa chako, ni kweli kuwa utakubaliwa na Mungu. “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu” (Warumi 10:10). Hii ndiyo sababu inayoifanya imani kuwa ya muhimu sana. Pia ni jambo la muhimu sana kuamini katika Neno la Mungu kwa mioyo yetu yote. Jambo la muhimu sana kwetu si kuamini yale ambayo wanadamu wanayasema, ila ni katika Neno la Mungu lililoandikwa; na jambo la muhimu sana kwetu si kuamini Neno kwa kufuata mawazo yetu binafsi na hisia, bali ni kuliamini Neno kwa mioyo yetu mizuri. Hii ndiyo sababu watumishi wa Mungu na wale ambao waliokolewa zamani wanaliamini Neno la Mungu kama lilivyo.
Kwa kupitia alama ya tohara, Mungu alifanya agano lake na Ibrahimu na wazawa wake na akawapatia utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania ili waweze kumwamini Yesu Kristo ambaye ni Masihi aliyetabiriwa kuwa atakuja; ambaye atawasamehe dhambi zao zote kwa ubatizo wake na kwa damu yake Msalabani na hivyo kwa imani hii wangeingia katika Ufalme wa Mungu.
Ninaamini katika Neno la Mungu la agano. Sio kwamba Ibrahimu pekee ndiye alibarikiwa kwa kuliamini Neno la Mungu, bali sisi sote pia tunaweza kubarikiwa kama yeye alivyobarikiwa kwa kuliamini Neno lake. Ninaamini kuwa Mungu alilijenga Hema Takatifu la Kukutania ili atuokoe kutoka katika dhambi zetu. Hii ndiyo sababu Mungu aliwaongoza wazawa wa Ibrahimu kutoka mbali katika nchi ya Misri hadi katika Mlima Sinai na akawapa Sheria na utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania. Ni lazima tutambue kuwa ukweli huu ni tukio la kimungu toka kwa Mungu.