Search

Mahubiri

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 11] Je, Waisraeli Wataokolewa? 

Warumi 11:1 inasema, “Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila la Benyamini.” Kwa maneno mengine, Mungu hakuwaacha Wasraeli kwa kuwa hata Paulo mwenyewe alikuwa ni Mwisraeli. 
Katika Warumi 11:2-5, Mungu anasema kuwa, “Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali. Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa yako mabaki waliochaguliwa kwa neema.” 
Kama ambavyo Mungu ametueleza kuwa kutakuwa na Waisraeli wengi watakaokuwa wakimrudia yeye kwa kumwamini Yesu, na kwa sababu hiyo Wayahudi wengi wataokolewa toka katika dhambi zao. Ni lazima tuamini kuwa wakati wa mwisho utakapowadia, basi idadi kubwa ya Wamataifa wasio Wayahudi itakombolewa toka katika dhambi zao kwa kuamini katika haki ya Mungu na hivyo kuja kwa Yesu Kristo. 
Paulo aliuliza, “Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya?” Hapa, Paulo anauelezea ukweli kuwa kutakuwa na Waisraeli wengi ambao wataiamini haki ya Mungu ambayo itaiondolea mbali dhambi zao. Maandiko, kwa kupitia Neno la Mungu lililozungumzwa na Eliya yanatueleza kuwa wengi miongoni mwa Waisraeli watampokea Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao. Sisi tunaliamini Neno hili. 
Katika Maandiko, namba “7” inamaanisha ukamilifu. Mungu aliuumba ulimwengu huu katika siku sita na kisha akapumzika katika siku ya saba. Mungu aliahidi kuwa alikuwa amejibakizia watu elfu saba ambao hawatampigia magoti Baali. Hii inamaanisha kuwa kutakuwa na Waisareli wengi ambao wataupokea wokovu toka katika dhambi zao kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao. 
Hali akiuelezea uhusiano uliopo kati ya Waisareli na Wamataifa Paulo aliamini kuwa watu wengi miongoni mwa Waisareli wataokolewa. 
 

Je, Wamejikwaa Ili Kuanguka?
 
Paulo alisema katika Warumi 11:6-12 kuwa ikiwa Waisraeli wangelimpokea Yesu kikamilifu kuwa ni Mwokozi wao, basi kusingekuwa na kipindi cha wokovu kwa Wamataifa. Kwa kuwa Waisraeli hawakumpokea Yesu kuwa ni Mwokozi wao Mungu aliwaruhusu Wamataifa kuwa na nafasi ya kuokolewa kutokana na injili ya maji na Roho. Kwa kupitia jambo hili Mungu aliazimia kwamba Waisraeli wawaonee wivu Wamataifa ambao walimwamini Yesu na kufanyika kuwa watoto wake. Kisha Waisraeli wataanza kumpokea Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao na hatimaye kuupokea ukweli kuwa kwa hakika Yesu Kristo ndiye Masihi wao. 
 

Shina ni Takatifu na Kwa Hiyo Matawi Pia ni Matakatifu 
 
Warumi 11:13 inasema, “Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa, Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu.” Paulo alisema kuwa anaitukuza huduma yake kama mtume kwa Wamataifa. Alipenda kuwaokoa jamaa zake wenye mwili na damu moja kama yake kwa kuwafanya wapate wivu kuhusiana na Wamataifa waliozaliwa upya. 
“Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa? Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika” (Warumi 11:15-16). Kifungu hiki kina maanisha kuwa ikiwa Ibrahimu, ambaye ni shina la Waisraeli aliokolewa na kuipata haki ya Mungu kwa kuamini Neno la Mungu, basi ni wazi kuwa inawezekana kabisa kwa Waisraeli ambao ni matawi ya Ibrahimu kuokolewa pia. 
Kwa wakati huo huo, Paulo aliwaonya Wamataifa waliozaliwa upya kwamba wasijidai kwa kuwa wamefanyika kuwa watu watakatifu wa Mungu kama tawi la mzeituni mwitu lililokatwa na kisha kupandikizwa katika mzeituni uliokuwa umepandwa. Kama Warumi 11:18 inavyosema, “Usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.” 
Sisi tumefanyika kuwa watu wa Mungu kwa kuwa tuliokolewa toka katika dhambi zetu kwa kuamini katika haki ya Mungu, lakini ikiwa tutaiacha haki ya Mungu, basi na sisi pia tutaachwa. Sisi hatuwezi kufanya hivi kwa sababu Yesu Kristo ameitimiza haki yote ya Mungu kwa kutuokoa toka katika dhambi zetu zote na kwa kweli tumeokolewa toka katika dhambi zetu zote. Sisi tumeokolewa kwa imani yetu katika haki ya Mungu kamilifu na wala si kwa matendo yetu. Sisi, Wamataifa tulifanyika kuwa watu wake kwa kupitia imani yetu katika haki ya Mungu hali tukiwekwa mbadala mahali pa matawi yaliyovunjika ya Waisraeli. 
 

Tunaweza Kusimama Imara Kwa Kuwa Na Tunaamini Katika Haki ya Mungu. 
 
Kwa hiyo, kwa kuamini katika haki ya Mungu, Wakristo na Wayahudi wanaweza kuungamanishwa kwa Yesu kuwa watu wake. Ikiwa hatuiamini haki ya Mungu, basi kwa hakika tutakufa kutokana na dhambi zetu na hukumu ya Mungu. Paulo aliwaonya jambo hili Waisraeli kwanza lakini hata sisi hatulikwepi onyo hilo pia. 
Mungu aliamua kutuonea huruma sisi wa Wamataifa na kwa hiyo alituokoa sisi kiukamilifu kwa haki yake. Wale wanaofahamu na kuamini katika haki ya Mungu wameokolewa toka katika dhambi zao zote. Ikiwa Wakristo wote wa leo hawaiamini haki ya Mungu ambayo imewaokoa kikamilifu basi watatupwa katika maangamizi hata kama wanakiri ya kuwa Yesu ni Mwokozi wao. 
Warumi 11:23-24 inasema, “Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena. Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao mwenyewe?” Kwa maneno mengine, Mungu ana uwezo na nguvu kumwongoza kila mmoja kuwa na imani katika haki yake. Uwezo huo na nguvu vimeahidiwa katika haki ya Mungu kwa kupitia injili ya maji na Roho. 
Kwa Waisraeli na Wamataifa wote, matendo yao hayawezi kuwaongoza wao kuwa wana wa Mungu. Bali wanaweza kufanyika watoto wa Mungu kwa kuamini katika haki ya Mungu na ahadi yake ya kuwafanya kuwa watoto wake. Haki ya Mungu inaiondolea mbali haki ya Sheria. Kwa kupitia haki ya Mungu, Waisraeli na Wamataifa wote katika ulimwengu mzima wataokolewa kwa imani yao. Hii ni baraka ya wokovu mkuu wa Mungu ambayo itatimizwa kwa kupitia injili inayoenezwa nasi. Nguvu ya Mungu ni ahadi yake ya imani iliyofanywa katika haki yake. 
Hebu tuangalie Warumi 11:26-27, “Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, 
‘Mwokozi atakuja kutoka Sayuni, 
Atamtenga Yakobo na maasia yake. 
Na hili ndilo agano langu nao, 
Nitakapowaondolea dhambi zao.’” 
Mungu ameahidi kuwa hatimaye atawaokoa Waisraeli hapo mwisho wa wakati. Kwa hiyo, Mungu mwenyewe aliahidi kuyaondoa maovu na uchafu toka katika akili za Waisraeli na kuwafanya wamwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wao. Ingawa walikuwa na mababa waaminifu, Waisraeli wenyewe bado hawajaupokea wokovu. Lakini Mungu amependa ili wao waokolewa katika wakati mfupi ujao kwa kuigusa mioyo yao na kuwafanya waamini katika haki yake. 
 

Mungu Ametufunga Sote Katika Uasi Ili Kwamba Aweze Kuturehemu!
 
Hebu tusome aya ya 32 ambayo ni aya mashuhuri sana. “Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.” Kila mtu ana asi na kusimama kinyume na Mungu. Hakuna hata mmoja anayeweza kumheshimu Mungu kikamilifu, lakini sababu iliyomfanya Mungu kutufunga sote katika uasi ni ili kwamba aweze kutupatia huruma na upendo. Huu ni ukweli wa kushangaza. 
Kwa kupitia kifungu hiki tunaweza kufahamu ya kuwa ni kwa nini Mungu aliwafunga wanadamu katika kuasi. Jambo hili ni la kushangaza sana. Mungu alituweka sisi kuwa ni waasi ili aweze kutuvika kwa haki yake kamilifu na upendo wenye rehema. Tunaweza kuamini na kumshukuru Mungu kwa dhumuni lake hili la kushangaza. Mungu aliwafunga hata Waisraeli katika uasi ili aweze kuwapatia upendo wa haki yake. Lakini bado Waisraeli wanamwangalia Yesu kwa dharau hali wakimchukulia kuwa ni mtu wa hali ya chini kutoka Nazarethi ilhali Wamataifa wengi wanamtumia Yesu kama njia ya kupata fedha. 
Wale wasioutii upendo wa Mungu wenye rehema hawana lolote la kuchagua zaidi ya kupelekwa kuzimu. Mungu amekwisha iandaa kuzimu inayowaka kwa moto kwa ajili yao, lakini Mungu hapendi kuona watu wakienda kuzimu kwa kuwa anawaonea huruma sana. “Ninawezaje kukupeleka kuzimu?” Baada ya idadi kubwa ya Wamataifa kuja katika wokovu wake basi Waisraeli wengi watamwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wao katika kipindi ambacho Mpinga-Kristo atawatesa katika nusu ya kipindi cha mwisho cha miaka saba ya mapigo. Katika kipindi kijacho idadi kubwa ya waamini wanaomkiri Yesu kuwa ni haki ya Mungu watainuka miongoni mwa Waisraeli. 
“Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.” Kifungu hiki cha kutisha kinaeleza kuwa Mungu amewaruhusu wenye dhambi wote kuokolewa kwa kuamini katika haki yake. 
Mungu alimweleza Paulo kuwa atawafanya Waisraeli kutubu na kumwamini Kristo wakati idadi ya kutosha ya Wamataifa watakapokuwa wameuawa kwa ajili ya imani yao katika kipindi cha mapigo. Kama ambavyo Paulo anasema katika Warumi 11:33, “Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!”
Hekima ya kweli na utajiri wa kimungu vinatoka kwa Mungu. Mungu aliwafanya wanadamu wote kuwa ni viumbe wenye mapungufu tangu awali. Hii inaonyesha hekima ya Mungu inayoturuhusu sisi kuupokea wokovu. Kwa sababu hii, kule kumwamini Yesu hata katika siku za mwisho kutawaokoa hata Waisraeli. Sisi sote hatukuwa na chaguo zaidi ya kutupwa katika shimo la takataka na moto, lakini Mungu alituokoa sisi toka katika dhambi zetu zote kwa haki yake ambayo aliipanga na kisha kuitimiza. Mungu amependa kuwa wenye dhambi waweze kuokolewa kwa ubatizo wa Yesu na damu yake kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Hema Takatifu la Kukutania katika Agano la Kale wakati ambao wanadamu wote walijaribiwa na Shetani na kuzivunja Sheria za Mungu. 
Inawezekanaje basi mtu akajaribu kusimama kinyume na hekima ya Mungu? “Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.” Ni nani anayeweza kuupinga ukweli huu, kwamba Mungu ametufunga sisi katika uasi ili aweze kutupatia rehema zake? Ni nani anayeweza kudiriki kusema kuwa Mungu amekosea kwa kufanya hivyo? Hakuna hata mmoja! Utukufu wote na utajiri na heshima ni vyake milele na milele. 
Mtume Paulo hali akiwa amejawa na Roho Mtakatifu aliandika, “Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mshauri wake? Au ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena? Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.” (Warumi 11:34-36).
Ingawa tuna mapungufu mengi, tunaishi hali tukiieneza injili ya haki ya Mungu. Wale wanaosimama kinyume na injili hii ya haki ya Mungu ni maadui wake. Na hiyo ni sawa kabisa! Watu wa jinsi hiyo wanaweza kuinuka hata miongoni mwetu, kwa hiyo ni lazima tuombe na tufahamu ili kwamba asiwepo mtu miongoni mwetu ambaye ataangukia katika jaribu hilo. Katika mazingira yoyote yale sisi hatupaswi kuwa kinyume na injili hii. Hatupaswi kamwe kugeuka na kusimama kinyume na injili ya maji na Roho kwa kuwa na mioyo isiyoamini. Wale wanaosimama kinyume na injili hii wataangamizwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ule ujao. 
Wakati wa Waisraeli kuamini umekaribia. Itakuwa ni jambo la kufurahisha sana ikiwa watu bilioni sita waliopo katika ulimwengu huu watamgeukia Mungu na kuupokea wokovu. Wenye haki, yaani wale wanaoiamini haki ya Mungu hawapaswi kuuangalia tu wakati uliopo, bali wanapaswa kuiangalia kazi ya Mungu iliyopangwa kwa ajili ya Waisraeli na kisha kuziandaa imani zao kuingia na kuishi katika nchi na mbingu mpya. Wenye haki wanapaswa wakati wote kuishi kwa imani na matumaini. 
Ninamshukuru Mungu, kwa kuwa ninafahamu kuwa siku ambayo Waisraeli watamwamini Kristo kuwa ni Mwokozi wao imekaribia. 
Na uje mara, Bwana Yesu!