Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[10-1] Je, Unafahamu Wakati wa Kunyakuliwa ni Lini? (Ufunuo 10:1-11)

(Ufunuo 10:1-11)
“Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto. Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi. Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao. Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike. Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni, akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya; isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii. Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi. Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali. Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kitabu kikawa kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu. Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.”
 

Mafafanuzi
 
Msingi wa sura hii unapatikana katika aya ya 7: “isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Kwa maneno mengine, unyakuo utatokea wakati huu.
 
Aya ya 1: “Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.”
Malaika mwenye nguvu anayeonekana katika sura ya 10 ni mtendaji wa Mungu anayeshuhudia kazi za Mungu zitakazokuja. Mwonekano wa malaika huyu unalenga kuonyesha jinsi nguvu za Mungu na ukuu wake ulivyo. Pia ni kuonyesha kuwa Mungu ataziharibu bahari za ulimwengu huu, na kwamba atawafufua na kuwanyakua watakatifu kwenda mbinguni.
 
Aya ya 2-3: “Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi. Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.” 
Mungu anafanya mambo yote kwa mujibu wa mipango yake. Siku ya mwisho itakapowadia, Mungu ataiharibu nchi na bahari. Kwa maneno mengine, Bwana wetu ataiharibu bahari ya kwanza na ardhi ya kwanza.
Kifungu hiki kinaonyesha mapenzi ya Mungu yasiyoshindwa katika kutimiza mambo yote ambayo ameyapanga, na pia kuonyesha ukamilifu wa kazi zake. Katika Biblia, namba saba inabeba maana ya ukamilifu. Mungu aliitumia namba hii wakati alipokamilisha kazi zake zote na akapumzika. Vivyo hivyo, kifungu hiki kinatueleza kuwa nyakati za mwisho, Mungu atawakomboa watu wengi toka katika maangamizi, bali kwa upande mwingine ni hakika Mungu atauharibu ulimwengu huu.
 
Aya ya 4: “Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike.”
Mungu alimwamuru Yohana kutoandika yale ambayo ngurumo saba zilitamka, ili kuficha unyakuo wa watakatifu miongoni mwa wale wasiookoka. Mungu anazificha baadhi ya kazi zake kwa muda kwa kuwa maadui wa Mungu wanawachukia na kuwatesa watakatifu.
Pia wakati wa Nuhu, wakati Mungu alipouangamiza ulimwengu kwa maji, Mungu alificha ujio wa gharika kwa watu wengine na badala yake alimwambia Nuhu tu. Hata sasa, Mungu anaihubiri injili ya maji na Roho katika ulimwengu mzima, na anawapatia Ufalme wa Mbinguni wale wanaoamini. Lakini nje ya wale walio na imani hii ya kweli, Mungu hajamfunulia yoyote yule juu ya unyakuo. Mungu ameumba ulimwengu mpya katika Ufalme wake kwa ajili ya wenye haki na anatamani kuishi pamoja nao.
 
Aya ya 5-6: “Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni, akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya;”
Mambo haya yote yanaweza kuapizwa kwa jina la Mungu, kwa kuwa hata kiapo cha mwisho kimefanyika si kwa jina la anayeapiza, bali kwa jina la yeye aliye mkuu. Hivyo, Mungu ni msimamizi wa mwisho kwa watakatifu wote wa nyakati za mwisho na kwa wale wote waliokwisha kufanyika watakatifu.
Hapa, malaika mwenye nguvu anaapa kwa jina la Mwenyezi kuwa unyakuo utakuja kwa hakika. Kiapo hiki kinatueleza kuwa Mungu ataumba Mbingu Mpya na Nchi Mpya na kisha ataishi na watakatifu wake katika ulimwengu huo mpya. Pia kifungu hiki kinaonyesha kuwa Mungu hacheleweshi uumbaji wa ulimwengu mpya, na kwamba ataukamilisha uumbaji huo haraka kwa ajili ya watakatifu wake.
 
Aya ya 7: “isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.”
Aya hii inatueleza kuwa wakati tarumbeta la mwisho litakapolia katika dhiki ya mwisho, basi watakatifu wote watanyakuliwa. Kitu ambacho kitawashangaza watu wengi katika ulimwengu huu ni wakati ambapo unyakuo wa watakatifu utakapotokea.
Ufunuo 10:7 inatueleza kuwa, “isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Maneno haya, “siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii” yana maanisha nini? Yana maanisha kuwa kama ambavyo injili ya maji na Roho ni injili ya kweli, na kwamba yeyote anayeamini katika injili hii anapokea upatanisho na Roho Mtakatifu katika moyo wake, basi ni hakika kuwa unyakuo wa watakatifu utatokea wakati tarumbeta la saba litakapolia.
Baada ya pigo la sita kati ya yale matarumbeta saba litakapokuwa limekwisha, watakatifu watauawa ili kuifia dini maana Mpinga Kristo, baada ya kuwa ameonekana duniani na kuanzisha utawala wake, atamtaka kila mtu kupokea alama ya yule mnyama, yaani Mpinga Kristo. Baadaye kidogo, yaani baada ya malaika wa saba kupiga tarumbeta lake, basi watakatifu wote waliouawa na walio hai na walioilinda imani yao watafufuliwa na kunyakuliwa. Baada ya hapo mapigo ya mabakuli saba, ambayo ni mapigo ya mwisho kwa mwanadamu yataanza. Wakati huu, watakatifu hawatakuwepo katika ulimwengu huu, bali watakuwa mbinguni pamoja na Bwana baada ya unyakuo. Wakatifu ni lazima wafahamu kuwa unyakuo wao utatokea baada ya mlio wa tarumbeta la malaika wa saba, ambalo ni tarumbeta la mwisho.
Pia, Mtume Paulo anatueleza katika 1 Wathesalonike 4 kwamba Bwana atashuka toka mbinguni pamoja na mlio wa sauti ya malaika mkuu. Wakristo wengi wanafikiri kuwa Bwana atakuja hapa duniani baada ya kutokea kwa unyakuo, hiyo si kweli. Unyakuo utakapotokea, Bwana wetu hatakuja hapa duniani, bali ataonekana mawinguni.
Kwa hiyo, Wakristo wanaofikiria hivyo kimakosa kuwa Bwana atakuja hapa duniani mara baada ya kutokea kwa unyakuo wa watakatifu wa kweli wanapaswa kuachana na ufahamu wao usio sahihi, na wanapaswa kuufahamu ukweli na kuuamini kiusahihi kwa kukumbuka kwamba unyakuo wa watakatifu utatokea mara baada ya mlio wa tarumbeta la malaika wa saba.
“Hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Unapaswa kutambua kwamba siri ya Mungu inayotajwa hapa inahusu kunyakuliwa kwa watakatifu ambako kutakuja kukiambatana na mlio wa pigo la tarumbeta la saba. Sasa, kwa kifupi, Mungu atauharibu ulimwengu wa kwanza na kisha atatengeneza ulimwengu wa pili. Ulimwengu huu wa pili ni maalumu kwa ajili ya Mungu kuishi pamoja na wale ambao wamezaliwa tena upya katika ulimwengu huu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, na pia katika kutimiza kwa uaminifu ahadi zote ambazo Mungu mwenyezi alizifanya kwa watu wake. Haya ni mapenzi ya Mungu, ambayo Muumbaji wa ulimwengu mzima alikuwa ameyaweka kwa ajili yake na kwa ajili ya watakatifu.
Wakati malaika atakapolipiga tarumbeta la saba, mapigo ya tarumbeta la saba yatakuwa yamekwisha, na hapo ndio mapigo ya mwisho ya mabakuli saba yatamiminwa. Neno linatueleza kuwa, “katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.” Siri ya Mungu inayotajwa hapa ni kwamba watakatifu watanyakuliwa sambamba na mlio wa tarumbeta la malaika wa saba.
Kwa sasa watakatifu wanaishi katika ulimwengu huu, lakini ili waweze kuishi katika ulimwengu mpya na bora zaidi watapaswa kuuawa na kuifia-dini, kisha kufufuliwa na kunyakuliwa. Ni hapo tu ndipo watakapoalikwa katika karamu ya Mwana-kondoo pamoja na Bwana na kisha kutawala pamoja naye kwa miaka elfu moja. Baada ya milenia hii, Mpinga Kristo, Shetani, na wafuasi wake wote watapokea hukumu ya Mungu ya milele. Kuanzia hapo na kuendelea, watakatifu watakatifu watabarikiwa kwa kuishi pamoja na bwana katika Mbingu mpya kwa baraka ya milele. Hii ni siri ya Mungu. Tunachoweza kwa sasa ni kumshukuru Mungu kwa kutufunulia siri hii sisi ambao tuna ile imani ya kweli. Mungu anatueleza kuwa atazitimiza ahadi zote mara malaika wa saba atakapolipiga tarumbeta lake.
 
Aya ya 8: “Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.”
Mungu anatueleza kuwa watakatifu na watumishi wa Mungu ni lazima waendelee kuihubiri injili ya maji na Roho hadi siku ya mwisho itakapokuja. Injili hii inahusu ukweli wa ondoleo la dhambi, kufia-dini, ufufuo, kunyakuliwa, na chakula cha harusi ya Mwana-kondoo. Ili watakatifu na watumishi wa Mungu waweze kuihubiri injili hadi mwisho, wanapaswa kwanza kujilisha Neno la Mungu kwa imani yao kabla ya ujio wa Dhiki Kuu. Mungu anataka aina mbili ya imani toka kwetu. Kwanza ni imani inayohusu kuzaliwa tena upya, na pili ni imani ya kupokea kuifia-dini katika kuilinda imani yetu ya kweli.
 
Aya ya 9: “Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.”
Watakatifu na watumishi wa Mungu ni lazima kwanza wajilishe Neno la Mungu na kisha kulieneza kwa watu wengine wengi. Aya hii inatueleza kuwa pamoja na kuwa mioyo ya wale wanaoliamini Neno la Mungu inapata utamu, ukweli ni kuwa kuihubiri injili hii kwa nafsi zilizopotea si jambo rahisi hivyo, kwa kuwa kunaambatana na kujitoa sadaka. Hiki ndio anachotueleza Mungu katika kifungu hiki.
 
Aya ya 10: “Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kitabu kikawa kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.”
Wakati Yohana alipolila Neno la Mungu kwa imani, moyo wake ulijawa na furaha. Lakini Yohana alikutana na magumu mengi alipokuwa akiuhubiri ukweli unaoshuhudiwa na Neno la Mungu kwa watu wasiouamini ukweli huo.
 
Aya ya 11: “Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.”
Watakatifu ni lazima watoe unabii kwa kila mtu kwamba baraka za Mungu zilikuja kwa kupitia injili ya maji na Roho. Pia wanapaswa kutoa unabii tena kwamba dhumuni la Bwana wetu kwa ulimwengu huu katika nyakati za mwisho ni kuhakikisha kuwa kila mtu anaingia katika baraka ya Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Kile ambacho Mungu alimwamuru Yohana kukitolea unabii ni kulihubiri Neno la kweli—kwamba ulimwengu mpya unakuja hivi punde, unaletwa na Mungu, na kwamba yeyote anayetaka kuingia katika ulimwengu huo ni lazima ahesabiwe haki kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Watakatifu na watumishi wa Mungu ni lazima walihubiri Neno la Mungu tangu mwanzo hadi mwisho tena na tena, ili kwamba kila mtu katika ulimwengu huu aweze kuwa na imani ambayo itamruhusu kuingia na kuishi katika Ufalme wa Bwana wetu.