Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[17-1] Hukumu ya Kahaba Akaaye Katika Maji Mengi (Ufunuo 17:1-18)

(Ufunuo 17:1-18)
“Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi; ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake. Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi. Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake. Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI. 
Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu. Na yule malaika akaniambia, Kwani kustaajabu? Nitakuambia siri ya mwanamke huyu, na ya mnyama huyu amchukuaye, mwenye vile vichwa saba na zile pembe kumi. Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako. Hapo ndipo penye akili zenye hekima. Vile vichwa saba ni milima saba anayokalia mwanamke huyo. Navyo ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka, na mmoja yupo, na mwingine hajaja bado. Naye atakapokuja imempasa kukaa muda mchache. Na yule mnyama aliyekuwako naye hayuko, yeye ndiye wa nane, naye ni mmoja wa wale saba, naye aenenda kwenye uharibifu. Na zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi, ambao hawajapokea ufalme bado, lakini wapokea mamlaka kama wafalme muda wa saa moja pamoja na yule mnyama. Hawa wana shauri moja, nao wampa yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao. Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana-kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio walioitwa, na wateule, na waaminifu. Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha. Na zile pembe kumi ulizoziona, na huyo mnyama, hao watamchukia yule kahaba, nao watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa moto. Maana Mungu ametia mioyoni mwao kufanya shauri lake, na kufanya shauri moja, na kumpa yule mnyama ufalme wao hata maneno ya Mungu yatimizwe. Na yule mwanamke uliyemwona, ni mji ule mkubwa, wenye ufalme juu ya wafalme wa nchi.’”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, “Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi,”
Ili kuweze kuitafsiri vizuri sura ya 17 ni muhimu sana kumfahamu huyu kahaba, mwanamke, na Mnyama anayetajwa katika kifungu kikuu. Huyu “kahaba” anayetajwa katika aya ya 1 anasimama kumaanisha dini za ulimwengu, ilhali “mwanamke” ana maanisha ni ulimwengu. Na kwa upande mwingine, “Mnyama,” anasimama kumwakilisha Mpinga Kristo. Na sentensi isemayo “maji mengi” ina maanisha ni mafundisho ya Ibilisi. Sentensi hii, “Nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi,” inatueleza kwamba Mungu atazihukumu dini za ulimwengu ambazo zinakaa katika mafundisho ya Shetani.
 
Aya ya 2: “ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake.”
Na hili neno “uasherati” lina maanisha juu ya kuupenda ulimwengu huu na vitu vyake kuliko kumpenda Mungu Mwenyewe. Matendo ya uasherati yana ambatana na kutengeneza sanamu za vitu vya hapa ulimwenguni, na kisha kuviabudu na kuvipenda kana kwamba ni Mungu. 
Msemo huo hapo juu, “ambaye wafalme wa nchi wamezini naye,” una maanisha kwamba viongozi wa ulimwengu huu wameishi maisha yao wakiwa wamelewa dini za ulimwengu, na kwamba watu wote wa kidunia pia wamelewa kwa dhambi ambazo dini za ulimwengu zinazitoa.
 
Aya ya 3: Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi. 
Sentensi inayosema, “mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana,” inatueleza kwamba watu wa ulimwengu huu wataiunganisha mioyo yao pamoja na moyo wa Mpinga Kristo ili kuwatesa na kuwaua watakatifu. Inaonyesha kwamba watu wa kiulimwengu wataishia kuwa watumishi wa adui wa Mungu, huku wakizifanya kazi za Mpinga Kristo kwa kuongozwa naye. Mnyama ni Mpinga Kristo anaye simama kinyume na Mungu. Mpinga Kristo anawatala wafalme wengi, pia anatawala mataifa mengi ya ulimwengu. 
Hali akiwa na kiburi cha majivuno, Mpinga Kristo hatasita kumkufuru Mungu na kusema maneno ya majivuno. Atamkufuru Mungu kwa kunena maneno ya kiburi na majivuno, huku akidai kwamba yeye ni Mungu au ni Yesu Kristo, na atajiinua juu kana kwamba yeye ni Mungu. Hivyo, nguvu zake zitainuka na kuwatawala wafalme wote wa ulimwenguni na mataifa yote yaliyomo ndani yake.
Sentensi inayosema, “mwenye vichwa saba na pembe kumi,” hivi “vichwa saba” vina maanisha ni wafalme saba wa ulimwenguni, na “pembe kumi” zina maanisha ni mataifa ya ulimwengu.
 
Aya ya 4: Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.
Sentensi inayosema, “mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu,” inatueleza kwamba dini za kidunia, hali zikiwa zimepangiliwa na Mpinga Kristo, zitamfikiria Mpinga Kristo kuwa ndiye mfalme wao. Kwa hiyo, wataona kwamba inafaa kwa wale wote wanaosimama kinyume nao kuuawa, na kwa sababu hiyo watayatekeleza mawazo yao kwa kufanya matendo dhidi ya watakatifu. 
Na ili kuupamba ulimwengu huu kama ufalme wao wa milele wa furaha, watajipamba kwa dhahabu za ulimwenguni, watajipamba kwa vito vya thamani sana na kwa lulu. Lakini imani yao inapendelea zaidi juu ya raha kiasi gani wanaweza kupata katika miili yao wanapokuwa hapa ulimwenguni. Kwa kuwa Mungu anapowaangalia watu wa hapa ulimwenguni, atauona ulimwengu uliojaa dhambi zao chafu, na kwa sababu hiyo wote wataonekana kuwa ni machukizo mbele zake.
 
Aya ya 5: Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI. 
Pamoja na kuwa watu wa kidini wa hapa ulimwenguni watajaribu kujitambulisha kuwa wao ni malkia, ukweli ni kuwa watadhihirishwa kuwa ni makahaba. Kwa upande mmoja, jina lake “Babeli Mkuu,” linatuonyesha juu ya tabia yake ya majivuno, ya kuabudu sanamu, na ya kikahaba na ya kunyanyasa, ilhali kwa upande mwingine neno “mama” linatuonyesha kwamba majeshi yote ya Mpinga Kristo katika historia yanabeba asili yake toka katika ulimwengu wenyewe, na kwamba ulimwengu ndio mzizi mkuu wa kila aina ya ukahaba na rushwa. 
Pamoja na kuwa ulimwengu huu umepambwa kwa vito vizuri na vinavyo metameta, Mpinga Kristo anayesimama kinyume na Mungu na anayefanya kazi katika mioyo ya watu hawa wa ulimwengu atafanya kazi akiwa kama mama yao. Kwa hiyo, Bwana wetu ameamua kuwaangamiza wote kwa mapigo yake makuu ya mabakuli saba. 
 
Aya ya 6: Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu. 
Hili neno “watakatifu” lina maanisha ni watu wa imani katika historia yote ya Kanisa ambao wamekuwa wakiamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu Kristo. Sentensi inayosema “mashahidi wa Yesu” ina maanisha ni wale miongoni mwa watakatifu ambao wameushuhudia ukweli kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu na Mwokozi wao, na ambao waliuawa kama wafia-dini na mashahidi katika kuilinda imani yao. 
Aya hii inasisitiza kwamba yeye ambaye atawatesa na kuwaua watakatifu si mwingine zaidi ya watu wa dini za hapa ulimwenguni. Watayafanya maovu hayo wakiwa kama kikosi tangulizi cha Mpinga Kristo. 
Hapa Yohana anatueleza kwamba alipomuona yule mwanamke, “alistaajabu, ajabu kuu.” Kwa kweli ulimwengu huu ni ulimwengu wenye udadisi. Watakatifu hawajafanya lolote la kuudhuru ulimwengu huu, lakini ulimwengu huu unajipanga pamoja na Mpinga Kristo na kuwaua watakatifu wengi. Je, ulimwengu huu si kitu cha kustaajabisha? Watu wa ulimwengu huu watawafanya watakatifu kubeba mambo haya yote. Kwa kuwa ulimwengu huu upo chini ya Mpinga Kristo, basi watu wake, ambao ni kama watumishi wake, watawakamata watakatifu na kuwaua. 
Hivyo, watu hao wataonekana kuwa ni wageni na kuwashangaza sana kwetu. Tunapowaangalia watu wa ulimwenguni, je, kwa kiasi fulani hawaonekani kuwa ni wa kushangaza? Wakati watu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, inawezekanaje basi wakawa watumishi wa Mpinga Kristo na kisha kuwaua watu—na si kila mtu, bali ni watu wengi sana wanaomwamini Mungu? Hii ni kwa sababu ulimwnegu huu unamtumikia Shetani. 
 
Aya ya 7: Na yule malaika akaniambia, Kwani kustaajabu? Nitakuambia siri ya mwanamke huyu, na ya mnyama huyu amchukuaye, mwenye vile vichwa saba na zile pembe kumi.”
Hili neno “mwanamke” lina maanisha ni watu wa ulimwengu huu. Aya hii inatueleza kwamba Mnyama, anayeitwa Mpinga Kristo, atawatawala wafalme wote wa ulimwenguni na mataifa yao, na atazifanya kazi zake kupitia wafalme hao yaani kazi ya kusimama kinyume na Mungu, ya kuwatesa watakatifu, na ya kuwaua watakatifu. Na hili neno “siri ya mnyama huyu” ina maanisha ni utambulisho wa Mpinga Kristo, ambaye anatembea kwa kufuata amri ya Shetani. Naye atayageuza mataifa ya ulimwengu huu kuwa mali yake. 
Watu wa ulimwengu huu, wakiwa wameungana na Mpinga Kristo, wataishia kuwa vyombo vya Shetani katika kuwaua kimbari idadi kubwa ya watu wa Bwana. Ulimwengu huu pamoja na Mpinga Kristo ni vyombo vya Shetani, ambavyo kwa sasa vimefichwa katika macho yetu. Lakini baada ya kupita miaka mitatu na nusu katika ile miaka ya Dhiki Kuu, ulimwengu pamoja na Mpinga Kristo watainuka na kuwaua watakatifu. 
Sasa, mtu anaweza kushangaa, kwamba itawezekanaje kwa jambo hili kutokea, ukizingatia kwamba ulimwengu huu una watu wa matabaka mbalimbali, wasomi, na watu makini, yaani kuanzia wanasiasa hadi wakufunzi hadi wanafalsafa na wenye shahada za uzamivu. Lakini kwa kuwa ulimwengu utafanya uhaini pamoja na Mpinga Kristo, basi ndio maana mambo haya yote ikiwemo mauaji ya kimbari ya watakatifu, yatatokea. Kwa hiyo, hii taarifa ya kwamba ulimwengu utasalimu amri kwa Mpinga Kristo na kisha kuwa watakatifu ni kitu cha msingi sana katika kulifumbua fumbo la Mpinga Kristo. 
 
Aya ya 8: “Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako.”
Aya hii inatueleza kwamba Mpinga Kristo alionekana kati ya wafalme wa zama za kale, na kwamba pamoja na kuwa kwa sasa hayupo katika ulimwengu wa sasa, huyo Mpinga Kristo atakuja kutokea hapa ulimwenguni hapo baadaye. Pia inatueleza kwamba watu wa ulimwengu huu watashangaa sana mara watakapomwona Mpinga Kristo akitokea na kuwaua watakatifu. 
Mpinga Kristo atayatekeleza madhumuni yake kwa kushiriki katika siasa mpya za ulimwengu huu. Ataendelea kuwa ni fumbo kubwa kwa watu wa ulimwengu huuu na atatangazwa kama ni wa kushangaza. Kwa kuwa atayabeba matatizo mengi ya kisiasa, kiuchumi, kifikra, na ya kidini na kisha kuyatatua kwa uwezo wake, basi watu wengi watafikiri na kumfuata wakifikiri kuwa yeye ni Kristo Yesu atakayekuja tena katika nyakati za mwisho. Hivyo, Mpinga Kristo atabaki kuonekana kama ni wa kushangaza mbele za macho ya watu wa ulimwengu. 
 
Aya ya 9: “Hapo ndipo penye akili zenye hekima. Vile vichwa saba ni milima saba anayokalia mwanamke huyo.”
Aya hii inatueleza kwamba Mpinga Kristo ataanzisha sheria zake binafsi ili kuwatawala watu wa ulimwengu na kisha atazigeuza sheria hizi kuwa chombo chake cha utawala ili kuyatekeleza madhumuni yake. Sababu itakayowafanya watu wa ulimwengu kuungana pamoja ni ili waweze kuwa chini ya utawala wa Shetani kwa kuipokea chapa ya Mpinga Kristo, na kisha kusimama kinyume na Mungu na watakatifu wake, na kisha kuyaweka matumaini yao katika sheria zilizoundwa na Mpinga Kristo. 
 
Aya ya 10: “Navyo ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka, na mmoja yupo, na mwingine hajaja bado. Naye atakapokuja imempasa kukaa muda mchache.”
Aya hii inatueleza kwamba wafalme wanaosimama dhidi ya Mungu wataendelea kujitokeza toka katika ulimwengu huu, sawasawa na walivyotokea wafalme kama hao zamani. Wakati muda wa mwisho wa Dhiki Kuu utakapowadia, kiongozi wa ulimwengu huu atainuka kama Mpinga Kristo na kisha kuwaua watakatifu. Lakini mateso ya kiongozi huyu wa ulimwengu, ambaye atakuwa ni Mpinga Kristo, yatadumu kwa muda mfupi tu yakiwa yameruhusiwa na Mungu. 
 
Aya ya 11: “Na yule mnyama aliyekuwako naye hayuko, yeye ndiye wa nane, naye ni mmoja wa wale saba, naye aenenda kwenye uharibifu.” 
Kifungu hiki kinatueleza kwamba Mpinga Kristo anayekuja hapa ulimwenguni atainuka akiwa kama mmoja wa wafalme wa mwisho wa ulimwengu huu. Wakati Mpinga Kristo atakapoonekana kati ya wafalme wa ulimwengu, watu wengi wa ulimwenguni watamfuata kama atakavyo, kwa kuwa baada ya kupokea roho ya Mnyama, ataonyesha nguvu kama Mungu na kutenda ishara na miujiza mingi. Watumishi wa Mungu na watakatifu pia watauawa na Mpinga Kristo, lakini mambo haya yote yatadumu kwa muda mfupi tu huku yakiwa yamepewa kibali na Mungu. Baada ya mambo hayo kupita, Mpinga Kristo atafungwa katika shimo la kuzimu lisilo na mwisho, kisha atatupwa katika jehanamu ya kutisha, ambako hataachiliwa kamwe. 
 
Aya ya 12: “Na zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi, ambao hawajapokea ufalme bado, lakini wapokea mamlaka kama wafalme muda wa saa moja pamoja na yule mnyama.”
Aya hii inatueleza kwamba mataifa kumi yataziunganisha nguvu zao ili kuutawala ulimwengu. Baada ya mataifa haya kumi kuungana, yatazitumia nguvu zao juu ya ulimwengu pamoja na Mpinga Kristo kwa muda mfupi. Lakini aya hii pia inatueleza kwamba wafalme wa ulimwengu bado hawajapokea ufalme unaotawaliwa na Mpinga Kristo. Hata hivyo, hapo baadaye kidogo, wafalme hawa wa ulimwengu watatawala huku Mnyama wakiwa wafalme wa giza kwa muda. Lakini utawala wao utadumu kwa muda mfupi tu, na kwa hiyo, watatawala juu ya mamlaka ya giza kwa huo muda mfupi. 
 
Aya ya 13: “Hawa wana shauri moja, nao wampa yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.”
Wakati utakapowadia, wafalme wa ulimwengu huu watazihamishia nguvu zao na mamlaka yao kwa Mpinga Kristo. Wakati huo, Kanisa la Mungu, watakatifu wake, na watumishi wake watateswa sana na Mpinga Kristo na kisha kuuawa kama wafia-dini. Lakini Mpinga Kristo mwenyewe ataangamizwa kwa nguvu na mamlaka ya Yesu Kristo na kwa upanga wa Neno utokao katika kinywa cha Yesu. 
 
Aya ya 14: “Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana-kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio walioitwa, na wateule, na waaminifu.”
Pamoja na kuwa Shetani atatafuta kufanya vita dhhidi ya Yesu Kristo, ukweli ni kuwa hataweza kulingana naye kabisa. Pia watakatifu, watamshinda Mpinga Kristo katika mapambano dhidi yake. Bwana atawapatia watakatifu nguvu ya kupigana na kumshinda Mpinga Kristo kwa imani yao. Kwa hiyo, watakatifu hawatayaogopa mapambano yao dhidi ya Mpinga Kristo, bali wataishi katika nyakati za mwisho kwa amani na utulivu kwa kumwamini Bwana Mungu wao. Kisha watawashinda maadui zao kwa imani yao katika Bwana. 
Ushindi huu wa watakatifu una maanisha kwamba watailinda imani yao na kisha kuuawa kama wafia-dini. Wakati huu utakapowadia, watakatifu watamshinda Shetani na Mpinga Kristo kwa kuvipokea vifo vya kuifia-dini kwa imani katika Yesu Kristo na kwa tumaini lao kwa Ufalme wa Mbinguni, watashiriki katika ufufuo na katika unyakuo, kisha watapokea Ufalme mpya wa Kristo, na kisha wataishi milele katika utukufu. 
 
Aya ya 15: Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha.”
Dini za ulimwengu zimewadanganya na kuwatawala watu wa mataifa yote kwa mafundisho ya Shetani. Aya hii inatueleza kwamba mafundisho ya kishetani yanayofanya kazi katikati ya dini za ulimwengu yamepenyeza katika mataifa yote na lugha za ulimwengu, na kwamba ushawishi wao umefikia kiwango kikubwa cha kuweza kuleta maangamizi katika roho za watu. 
 
Aya ya 16: “Na zile pembe kumi ulizoziona, na huyo mnyama, hao watamchukia yule kahaba, nao watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa moto.”
Kifungu hiki kinatueleza kwamba mataifa ya ulimwengu huu yataungana na Mpinga Kristo katika kuwaua na kuwaangamiza watu wa kidini. Kwa maneno mengine, kifungu hiki kinatuleza kwamba watu wa ulimwengu huu na Mpinga Kristo watawachukia na kuwatukana watu wa kidunia, kisha watazifuta dini zote za ulimwengu machoni mwao. Pamoja na kuwa watu wa kidunia waliwaua watakatifu hapo zamani huku wakiungwa mkono na Mpinga Kristo, sasa wao nao wataangamizwa na Shetani na watu wa kidunia. Hatimaye itaonekana wazi kwamba Shetani alizitumia dini za ulimwenguni ili kujifanya kuwa ni Mungu. 
 
Aya ya 17: “Maana Mungu ametia mioyoni mwao kufanya shauri lake, na kufanya shauri moja, na kumpa yule mnyama ufalme wao hata maneno ya Mungu yatimizwe.”
Aya hii inatueleza kwamba watu wa ulimwengu huu watazitoa nguvu na mamlaka yao kwa Shetani. Kwa hiyo, watakuwa ni watu wa Mpinga Kristo kwa kuwa wataipokea chapa yake kwa hiari, wataona fahari kuwa watumishi wa huyu Mpinga Kristo, pia watawaua wale watakaokataa kuipokea chapa yake. Hata hivyo, mateso yao kwa watakatifu yataruhusiwa kwa muda mfupi tu ambao Neno la Mungu limeruhusu. Katika kipindi hicho kilichoruhusiwa, Mpinga Kristo atayashusha maovu yote ya moyo wake na kwa uhuru wake atasimama dhidi ya Mungu na watakatifu wake. 
 
Aya ya 18: “Na yule mwanamke uliyemwona, ni mji ule mkubwa, wenye ufalme juu ya wafalme wa nchi.”
Hapa Mungu anatueleza kwamba ulimwengu huu utazitengeneza sheria mpya ili kutawala na kuongoza kupitia wafalme wake, na kwamba wafalme wa ulimwengu watatawaliwa kwa kujifunga katika sheria hizi mpya. Hiyo nguvu kuu ya ulimwengu huu itatawala juu ya wafalme wote wa ulimwenguni, kama vile mtu awezavyo kutawala. Kwa maneno mengine, ulimwengu utazitengeneza sheria ambazo zitawafunga wafalme wote kikamilifu, na itakuwa ni kana kwamba mungu anawatawala. 
Hili neno “mji mkubwa” lina maanisha ni taasisi za kisiasa ambazo kwa hizo Mpinga Kristo atatawala. Kila mtu katika ulimwengu huu ataishia kuitumikia taasisi inayotawala ulimwengu, ambayo Mungu amewapatia, kana kwamba taasisi hiyo ni Mungu Mwenyewe, na kisha watatawaliwa na taasisi hiyo. Watu wataangamizwa kwa kuwa watu wamefanyika kuwua watumishi wa Shetani. 
Zaburi 49:20 inatueleza kwamba, “Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, amefanana na wanyama wapoteao.” Kwa hiyo, watu wa ulimwengu huu wanapaswa kufahamu mapema jinsi mpango wa Shetani ulivyo, kisha waamini sasa katika injili ya maji na Roho inayohubiriwa na watakatifu wa nyakati hizi, na kisha kukwepa laana ya kugeuzwa kuwa watmishi wa Shetani na badala yake kuishi hali wakiwa wamevikwa baraka ya Ufalme wa Mungu wa milele.