Search

Utafiti Wa Maskani

Kinara cha taa cha Dhahabu

Mahubiri Yanayohusiana

· Kinara cha Taa cha Dhahabu (Kutoka 25:31-40)

Kinara cha Taa cha Dhahabu
(Kutoka 25:31-40)
“Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, kitako chake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho; nacho kitakuwa na matawi sita yenye kutoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara upande wake mmoja, na matawi matatu ya kinara upande wake wa pili. Vikombe vitatu vilivyofanywa kwa mfano wa maua ya mlozi katika tawi moja; tovu na ua; na vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi la pili, tovu na ua; vivyo hivyo hayo matawi yote sita yatokayo katika kile kinara; na katika hicho kinara vikombe vinne vilivyofanywa kwa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake, na maua yake; na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, kwa hayo matawi sita yatokayo katika kile kinara. Matovu yake na matawi yake yatakuwa ya kitu kimoja nacho; kiwe chote pia kazi moja ya kufua, ya dhahabu safi. Nawe zifanye taa zake saba; nao wataziwasha hizo taa zake, zitoe nuru mbele yake. Na makoleo yake, na visahani vyake, vyote vitakuwa vya dhahabu safi. Kitafanywa cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo hivi vyote. Nawe angalia uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani.”
 
 
Kinara cha taa cha Dhahabu
Kinara cha taa cha dhahabu kilifanywa kwa talanta moja ya dhahabu safi. Kitako chake kilipondwa toka katika talanta moja ya dhahabu safi pamoja na matawi yake matatu yakitokeza toka katika pande zake mbili, na taa saba ziliwekwa juu ya kile kitako na katika matawi yake sita. Kwa kuwa kinara cha taa kiliundwa kutokana na talanta moja ya dhahabu safi, kwa kweli kilikuwa ni kitu kizuri sana cha kukitazama na kukishika. 
Juu ya kinara cha taa cha dhahabu kulikuwa na taa saba za kuwekea mafuta ambazo ziliwashwa ili kutoa mwanga katika Mahali Patakatifu wakati wote. Mtu anaweza kuingia katika Mahali Patakatifu kwa kuuinua na kuufungua mlango wa Hema Takatifu la Kukutania uliofumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Wale wanaoweza kupaingia mahali hapa ni wale tu wanaoamini katika kazi za wokovu zilizodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu. Kwa hiyo, hakuna anayeweza kupangia Mahali Patakatifu pasipo kuwa na imani hii, kwa kuwa mahali hapo ni sehemu ambayo imeruhusiwa kwa ajili ya wale wanaolifahamu fumbo la nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa lililodhihirishwa katika mlango wa kisitiri (pazia) wa Hema Takatifu la Kukutania. 
Kwa hiyo, ni wale tu wanaoamini katika wokovu wa ajabu ulifanyizwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa ndio wanaoweza kuwa wanachama wa Kanisa la Mungu. Rangi nne za mlango wa kisitiri wa Hema Takatifu la Kukutania ni kivuli cha injili ya maji na Roho, inayoonyesha juu ya ujio wa Yesu, ambaye alizichua dhambi zetu za ulimwengu katika mwili wake kwa kubatizwa na kisha kubeba adhabu ya dhambi zetu kwa kusulubiwa na kwa kuimwaga damu yake. 
Hakuna zaidi ya hii injili ya maji na Roho inayoweza kuwa ni injili ya kweli ya ondoleo la dhambi ambayo Bwana ametupatia. Injili ya maji na Roho imeundwa kwa ubatizo ambao Yesu Kristo aliupokea na hukumu ya Msalaba ambayo aliibeba ili kutupatia baraka ya ondoleo la dhambi. Kwa hiyo, ni wale tu wanaoamini kwa mioyo yao katika ukweli huu ndio wanaoweza kupewa ondoleo la dhambi zao zote. Kwa maneno mengine, Mungu anawaruhusu wale tu wanaoamini katika ukweli wa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa kupaingia Mahali Patakatifu. 
Kama ambavyo kinara cha taa cha dhahabu kilivyong’aa wakati wote ndani ya Mahali Patakatifu, basi vivyo hivyo wale ambao wamefanyika kuwa wana wa Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho watauangazia ulimwengu huu kwa mwanga wa wokovu unaowaokoa watu toka katika dhambi zao. Kwa maneno mengine, ni wale tu waliopokea ondoleo la dhambi kwa kupitia injili ya maji na Roho ndio wanaoweza kulitimiza jukumu la kinara cha taa ambacho kinatoa mwanga wa wokovu ili kwamba watu wengine waweze kuufahamu ukweli huu na kisha kupokea ondoleo la dhambi zao. 
Kinara cha taa cha dhahabu kilikuwa na maua, na matovu ya mapambo. Kama ambavyo Mungu aliamuru kuwa taa saba ziwekwe juu ya kinara cha taa, basi kinara cha taa kilipowashwa giza liliondoka katika Mahali Patakatifu wakati wote. Hii inamaanisha kuwa wenye haki waliosafishwa dhambi zao kwa kuamini katika injili ya maji na Roho watakusanyika pamoja, watalijenga Kanisa la Mungu na kisha watauangazia ulimwengu huu. Mwanga wa kinara cha taa uliong’aa katika Mahali Patakatifu ni injili ya maji na Roho unaoliondoa giza la ulimwengu huu. 
Ili kutuokoa sisi toka katika dhambi, Yesu Kristo alikuja hapa duniani, akafanyika katika mwili wa mwanadamu. Akazichukua dhambi zetu katika mwili wake, alibatizwa na Yohana, na kisha akabeba adhabu ya dhambi zetu na akasulubiwa. Hivyo, Yesu amefanyika kuwa mwanga wa wokovu. Katika ua wa Hema Takatifu la Kukutania, wenye dhambi walizipitisha dhambi zao juu ya mnyama wa sadaka ya kuteketezwa kwa kuiweka mikono yao juu ya kichwa cha mwanasadaka na kisha kumfanya mwanasadaka huyo kubeba adhabu ya dhambi zao kwa kumchinja mwanasadaka huyu. 
Vivyo hivyo, Yesu Kristo ameukamilisha wokovu wetu kwa kubatizwa na kufa Msalabani kwa mujibu wa sheria ya Mungu, na kwa hiyo amefanyika kuwa mwanga wa wokovu kwa wanadamu wote. Kwa kupitia huduma zilizodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, Yesu Kristo ameutimiliza wokovu wa mwanadamu. Kwa hiyo, sisi tumeokolewa toka katika dhambi zetu kwa kuamini katika injili ya ubatizo na damu ambayo Yesu Kristo ametupatia. Wote wanaomwamini Yesu ni lazima pia waugundue mwanga huu wa ukweli. 
Yesu Kristo ameangaza mwanga wa wokovu katika ulimwengu huu ili kwamba wale tu ambao wamezaliwa tena upya kwa maji na Roho waweze kuingia katika Ufalme wa Mungu. Kwa hiyo, ni wale tu waliozaliwa kwa maji na Roho ndio wanaoweza kufanyika sehemu ya Kanisa la Mungu na wanaweza kustahilishwa kung’aa na kuueneza mwanga wa maji na Roho katika ulimwengu wote. Mungu amewakabidhi injili hii ya maji na Roho na amewaruhusu kung’aa na kutoa mwanga wa injili ya kweli kwa kuwa wanaamini katika injili ya maji na Roho na kuieneza. 
Kwa hiyo, ni lazima tutambue kuwa kazi hii ya kuuneza mwanga wa injili ulimwenguni mwote inaweza kufanywa na wale tu ambao wanaoamini katika injili ya maji na Roho kuwa ni ukweli halisi. Wenye dhambi hawawezi kuingia Mahali Patakatifu. Ni wale tu wanaoamini katika injili iliyodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu za mlango wa Hema Takatifu la Kukutania ndio wanaoweza kuingia. Kwa hiyo, ni wale tu wanaoufahamu ukweli wa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kuamini katika mioyo yao ndio wanaoweza kuja katika Hema Takatifu la Kukutania na kubeba jukumu la kuuangaza mwanga angavu wa wokovu. 
Katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania, kisitiri kilichoundwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu pia kiliiangazia njia. Kwa wale ambao wanaolitafuta Hema Takatifu la Kukutania ili kutoa matoleo yao, Mungu alifanya lango la ua wake kwa rangi zilezile nne. Lakini watu wa wakati wa Agano la Kale hawakuweza kufanyika wakamilifu daima kwa kupitia sadaka zao za kila siku. Hivyo iliwapasa kuendelea kumsubiri Masihi. Hata hivyo, wakati Yesu Kristo ambaye ni Masihi alipokuja walishindwa kutambua kuwa amefanyika kuwa Masihi wa kweli kwa kutoa sadaka moja ya kudumu kwa mujibu wa ufunuo uliofanyizwa katika rangi nne za mlango wa kisitiri wa Hema Takatifu la Kukutania. 
Hii ni sawasawa na Wakristo wa leo ambao pamoja na kuliitia jina la Yesu bado hawatambui kuwa Yesu alikuja katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa na kwamba ametuokoa sisi kikamilifu. Wakati watu wa Agano la Kale walipotoa sadaka zao za kuteketezwa kila siku kwa kuiweka mikono yao juu ya kichwa cha mwanasadaka na kwa damu ya mwanasadaka, bado walipaswa kuamini kuwa Mwokozi atakuja katika njia hii kama ambavyo ilivyokuwa kwa mwanasadaka wao wa kuteketezwa. 
Vivyo hivyo, watu wa ulimwengu huu ni lazima waamini kwamba Yesu Kristo ambaye ni Mwokozi alikuja hapa duniani, akazichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa kubatizwa kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa ya Agano la Kale wa kuwekea mikono na damu, alisulubiwa na kuimwaga damu yake, na kwa hiyo amewaokoa watu wake toka katika dhambi. Lakini kwa sababu hawa hawaufahamu utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Agano la Kale hawafahamu ikiwa Yesu alikuja kwa ubatizo wake na damu, au kwa damu ya Msalaba tu, au kama Mwokozi wa kawaida tu. 
Katika macho ya Mungu, ile imani ambayo Wakristo wa leo wanaiweka mahali pa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa wa Agano la Kale ni mbaya kama ule wa watu wa Israeli. Kwa sababu hawana imani ya kweli katika Masihi ambaye amedhihirishwa katika utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa, wanashindwa kuamini kuwa Masihi alikuja, akabatizwa, na kisha akaimwaga damu yake. Lakini watu wote wa ulimwengu huu wakiwamo watu wa Israeli ni lazima waamini katika injili ya maji na Roho kwamba Yesu amewaokoa wao toka katika dhambi zao kwa kupitia huduma za ubatizo wake na kusulubiwa kwake. 
Ili kukuokoa wewe na mimi toka katika dhambi zetu zote na adhabu ya dhambi hizo, Yesu Kristo alibatizwa na kumwaga damu yake. Kwa kupitia ukweli ulioshikiliwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu za mlango wa Hema Takatifu la Kukutania, ambayo ni kivuli cha injili ya maji na Roho, basi sisi tunaweza kumfahamu Yesu Kristo. Ukweli huu wa wokovu ni kuwa watu wanaweza kupokea ondoleo la dhambi zao kwa kuamini katika injili ya kweli katika mioyo yao. Kwa kuamini katika injili ya maji na Roho ambayo Yesu Kristo ametupatia kwa kuja hapa ulimwenguni, kwa kubatizwa, na kwa kufa Msalabani, basi ni lazima uwe na imani inayoweza kukuokoa katika moyo wako. Ukweli huu umekuokoa wewe toka katika dhambi zako zote. 
Katika Nyumba takatifu ya Mungu, kulikuwa na milango mitatu ya kisitiri. Milango hii yote ilifumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Kama nilivyokwisha kukuambia tena na tena, rangi hizi nne zinaufunua kwa wazi wokovu wa Mungu: Mungu ameweka sheria ya ondoleo la dhambi iliyokamilishwa katika nyuzi za bluu, zambarau na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa ili kutuokoa sisi toka katika dhambi zetu. Kwa hiyo, ikiwa tunaamini kwa mujibu wa sheria hii ya ondoleo la dhambi, basi Mungu ataipokea na kuikubali imani yetu na atatuokoa milele toka katika dhambi zetu. 
Ni kwa kuamini katika injili ya maji na Roho iliyodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu ndipo yoyote miongoni mwetu anaweza kuokolewa toka katika dhambi zote milele. Kwa kufahamu na kuamini katika ukweli huu wa maana wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa uliotolewa na Mungu, mtu yeyote anaweza kumwendea Mungu. Katika sehemu ya kuingilia ya Mahali Patakatifu, Nyumba ya Mungu, kulikuwa na nguzo tano na kisitiri kilichokuwa kimefumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa kilichokuwa kimening’inizwa katika nguzo hizi. Ili sisi tuweze kumwendea Mungu, ni lazima tuwe na imani nne zilizodhihirishwa katika rangi nne zilizopo katika mlango wa kisitiri. 
Imani inayoonyeshwa katika nyuzi za bluu ina maanisha kuwa Yesu Kristo alizipokea dhambi zetu kwa kubatizwa, na imani inayodhihirishwa katika nyuzi nyekundu ni kwamba Yesu alibeba adhabu ya dhambi kwa kusulubiwa na kuimwaga damu yake. Imani inayofunuliwa katika rangi ya zambarau inaamini kuwa Yesu ni Mungu mwenyewe, na imani inayodhihirishwa katika kitani safi ya kusokotwa inaamini katika Neno lake pana kwamba Mungu ametufanya sisi kuwa tusio na dhambi kwa kuzitoweshea mbali dhambi zetu kwa kutumia nyuzi hizo zilizokwisha tajwa hapo juu—ambazo ni nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu. Ukweli huu unaitwa injili ya maji na Roho. Kwa hiyo, kwa kuamini kuwa Yesu ametuokoa sisi kwa kupitia maji na Roho tunaweza kuingia katika Ufalme wa Mungu. Hii ni imani ya wale wanaoweza kuufungua mlango wa Hema Takatifu la Kukutania na kisha kuingia katika Mahali Patakatifu. 
Lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania lililofumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu linatuwezesha sisi kutambua mpango wa Mungu juu ya jinsi atakavyotuokoa, lango linatuonyesha sisi kuwa wokovu wetu unatoka katika ondoleo la dhambi lililowekwa na Mungu na kwamba haupatikani kwa jitihada zetu wenyewe za kujifanyia. Hata ikiwa tutaomba kwa ajili ya msamaha wa dhambi zetu kila siku, pasipo sadaka ya kuteketezwa ili kuzipatanisha dhambi zetu, yaani kule kuzipitisha dhambi zetu kwa kuiweka mikono yetu juu ya kichwa cha mwanasadaka na kwa kuimwaga damu hatuwezi kuokolewa toka katika dhambi zetu za milele. Ni mpaka pale mwanasadaka wa kuteketezwa aliyekuja kutuokoa sisi toka katika dhambi zetu anapozichukua dhambi za ulimwengu za milele katika mwili wake ndipo tunapoweza kuokolewa kikamilifu kwa kuamini katika ukweli huu na hivyo kupokea ondoleo la dhambi. 
Ikiwa tunayo imani katika mioyo yetu inayoamini katika ukweli huu wa injili, basi tutakuwa tayari kuieneza injili ya wokovu ambayo inaleta uzima wa milele katika nafsi zilizopotea. Kwa kuamini katika huduma za Yesu zilizodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu tunaweza kuuangazia ulimwengu huu kwa ukweli wa ondoleo la dhambi. Kinara cha taa katika Mahali Patakatifu kilikuwa na taa saba, na kwa hiyo taa hizi zilipowashwa mwanga wake uliakisiwa na kuta za Hema Takatifu la Kukutania zilizokuwa zimeundwa kwa mbao na kisha kufunikwa kwa dhahabu na hivyo kupafanya pale Mahali Patakatifu kung’aa kwa mwanga angavu. Ikiwa kungekuwa hakuna kinara cha taa katika Mahali Patakatifu, basi kungekuwa na giza tu. Hii ndio sababu Mungu amewaweka watakatifu, watumishi wake wanaoamini katika injili ya maji na Roho katika ulimwengu huu wa giza ili waangaze.
 


Jukumu la Kinara cha Taa cha Dhahabu ni Nini?

 
Kinara cha taa cha dhahabu kinatuonyesha sisi kuwa Mungu ametupatia imani inayoamini katika ukweli ambao unafanyika kuwa mwanga au nuru ya ulimwengu. Imani yetu ni kuamini kuwa Yesu Kristo alizaliwa katika dunia hii, alibatizwa, na akamwaga damu yake Msalabani. Kwa meneno mengine, Mungu anatuambia sisi kuung’arisha mwanga wa wokovu kwa imani hii. Tunapoishikilia injili ya wokovu katika mioyo yetu na kuieneza imani hii, basi ndipo wakati huu ule mwanga wa ukweli unapong’aa. Kisha watu wataona na kuja katika mwanga huu angavu na kutambua kuwa Bwana amewaokoa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, na kisha kufanyika watu wa Mungu mwenyewe. Mwanga huu wa ukweli ni injili ya maji na Roho iliyokuwa imepangwa na kutimizwa na Mungu Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. 
Sisi tunaieneza kwa wale ambao wanahitaji kuokolewa hali tukiwa na imani katika ukweli kuwa Yesu alikuja hapa duniani, alibatizwa na akasulubiwa, akamwaga damu yake na kufa, na akafufuka tena toka kwa wafu ili kutupatia sisi ondoleo la dhambi zote. Ikiwa Yesu Kristo asingelibatizwa na kusulubiwa kwa ajili yetu, wewe na mimi tusingeliweza kamwe kuokolewa toka katika dhambi zetu. 
Kwa sababu Yesu alibatizwa, akamwaga damu yake, na akasulubiwa kwa ajili yetu, basi aliweza kuwapatia wenye dhambi wote imani inayoweza kuwaokoa. Sisi hatujaribu kueneza mafundisho yaliyopotoshwa hapa. Sisi tunaueneza mwanga wa wokovu uliodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa katika ulimwengu wote. Kwa sababu tuna imani inayofahamu na kuamini katika ubatizo wa Yesu na sadaka yake Msalabani, sisi tunaueneza mwanga wa maisha kwa wale ambao mioyo yao imo katika giza. Kwa hiyo wale wote wenye ukweli huo ambao wameangaziwa na mwanga huu nao pia wataubeba ushuhuda hali wakishangazwa jinsi ambavyo dhambi zote zimetoweka toka katika mioyo yao. Watu wote wa ulimwengu watakuja pia kuufahamu ubatizo ambao Yesu aliupokea pamoja na sadaka yake Msalabani ambayo aliitoa ili kuzitoweshea mbali dhambi zote za ulimwengu, na kwa kuamini kuwa hili ni ondole lao la dhambi, basi watakuja kuutambua mwanga wa ukweli. 
Ni kwa nini Yesu Kristo alipaswa kuja hapa duniani? Ni kwa nini ilimpasa kubatizwa? Ni kwa nini ilimpasa kufa Msalabani? Ni kwa nini ilimpasa kufufuka tena toka kwa wafu baada ya siku tatu? Sababu ya haya yote ni kwamba Yesu Kristo ni Masihi. Ili kuzitimiza kazi zote za wokovu kama Masihi, Yesu alibatizwa na kuimwaga damu yake, na kwa hiyo ameuangaza mwanga wa wokovu kwa wenye dhambi. Kwa hiyo, tunaweza kuwafanya watu wengi kuufahamu ukweli huu na kisha kuuamini na hivyo kupokea uzima wa milele pale tutakapoueneza mwanga huu katika ulimwengu mzima. 
Wewe na mimi ni kinara cha taa kinachotoa mwanga katika ulimwengu huu kwa mwanga wa injili ya maji na Roho. Kwa kupitia injili ambayo tunaieneza, watu watakuja kuufahamu mwanga unaowaokoa. Wale ambao wanautafuta mwanga katika ulimwengu huu wa giza watauona mwanga huu unaong’aa tunaoueneza, watakuja katika mwanga wa ukweli, na kisha wataokolewa toka katika dhambi zao zote. Wanadamu wote wanaweza kuokolewa kwa kuja katika imani inayoamini katika ukweli huu. 
Injili hii si suala la kinadharia. Kwa hiyo, ni lazima tuamini kwa mioyo yetu ya kweli. Tunaweza kufanya kazi ya kuieneza injili pale tunapoamini kiukweli katika huduma za Yesu zilizodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Lakini hata kama tumepokea ondoleo la dhambi, pasipo kuwa na taa ambapo mafuta yanaweza kuwekwa ndani yake, basi hatuwezi kutoa mwanga milele, na kwa hiyo Mungu ametupatia sisi Kanisa la Mungu, ambalo ni kinara cha taa. Katika kila tawi la kinara cha taa kulikuwa na vibakuli vidogo na chini ya hivi vibakuli kuwa na matovu yaliyokuwa yamerembeshwa. Hii ina maanisha kuwa hakuna kitu chochote zaidi ya Kanisa kinachojengwa kwa imani. 
Mahali pekee ambapo wale waliopokea ondoleo la dhambi kwa kuamini katika mioyo yao wanakusanyika ni katika Kanisa la Mungu la kweli. Kiongozi wa Kanisa ni Yesu Kristo na Kanisa ni mwili wake. Kama vile mwili unavyotembea kwa kadri kichwa kinavyouelekeza mwili, basi Kanisa pia linaitembeza mikono yake na miguu kama linavyoamriwa na Yesu Kristo. Hivi ndivyo injili inavyohudumiwa. Ni kitu gani basi ambacho Kanisa la Mungu linakitafuta? Hali ukiwa umefungwa katika dhambi nyeusi ulimwengu wote unakufa, na Kanisa linazitazama na kuzitafuta nafsi katikati yake ambazo haziwezi kukwepa zaidi ya kuelekea kufungwa kuzimu. Kanisa la Mungu linawaangazia hao kwa mwanga wa wokovu. Hivi ndivyo mimi na wewe tunavyofanya katika Kanisa lake kwa imani yetu katika injili.
Katika nchi ambako kuna historia ndefu ya Ukristo, kuna watu wengi ambao wamesoma na kuwa na ufahamu mkubwa wa Biblia. Ninaamini kwamba miongoni mwa watu wa jinsi hiyo ambao wamekuwa wakiutafuta ukweli halisi wanapokuja kukutana na ukweli huu, basi mara moja watapokea ondoleo la dhambi zao. Hivyo, ili kuieneza injili ya maji na Roho kwa watu wa jinsi hiyo, mimi ninafanya kazi kwa kuwaunganisha na watakatifu wote waliozaliwa tena upya katika imani. 
Tofauti na dini nyingine, Ukristo umeweka msingi wake wa imani katika Neno, kwa sababu hiyo watu watapokea ondoleo la dhambi ikiwa tu tutalieneza Neno kiusahihi. Lakini kuna wale ambao kwa makusudi na kwa hila wanasimama kinyume na ukweli huu, wakijaribu kulisukumia mbali na kutoliamini hata kama likihubiriwa kwao kiasi gani. Hasahasa, kuna wale wanadini wenye ugumu wa moyo ambao hawaliamini Neno la Mungu, na watu wa jinsi hiyo hawawezi kuamini kamwe katika ukweli huu wa maji na Roho. Lakini je, inakuwaje basi kwa wale wanaoikubali Biblia kuwa ni Neno la Mungu? Watu wengi wasiohesabika miongoni mwao watapokea ondoleo la dhambi pale watakapoisikia na kuiamini injili hii. 
Ni kwa sababu nina imani hii ndio maana nimekuwa nikimtumikia Mungu pamoja nawe hadi siku hii ya leo. Katika siku zijazo, injili hii itaenezwa kwa watu wengi sana kazi kubwa za injili zitainuliwa. Inaweza kuwa Mungu anafanya kazi mahali ambapo hatuwezi kuona na watu maelfu wanapokea ondoleo la dhambi kila siku. Na kama vile kwako wewe na mimi, kundi kubwa la watu watafanyika kuwa taa na wataeneza kwa watu wengine wa ulimwenguni kote ile imani iliyo katika mioyo yao inayoamini katika wokovu unaodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Ninaamini kuwa kadri wanavyouangazia ulimwengu mzima, waamini wapya wataendelea kuinuka na wao pia watalelewa na kisha wataineneza injili hii tena. 
Sisi ambao sasa tumefanyika kuwa taa za Mungu tunauangaza mwanga wa wokovu kwa imani yetu inayoamini katika ukweli uliodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Nyuzi za bluu zinatoa mwanga wa ukweli kuhusu ubatizo wa Yesu—ambao maana yake ni kuwa Yesu alizibeba dhambi za ulimwengu wote kwa kubatizwa na Yohana; nyuzi za zambarau zinatoa mwanga wa ukweli kuwa Yesu Kristo ni Mfalme wa wafalme; nyuzi nyekundu zinatoa mwanga wa ukweli kuwa Yesu alizibeba dhambi za ulimwengu hadi Msalabani na kisha akaimwaga damu yake juu ya dhambi hizo; na nyuzi za kitani safi ya kusokotwa zinatoa mwanga wa ukweli kuwa Neno la Mungu limewafanya wenye dhambi kuwa ni wenye haki. Neno la injili ya maji na Roho iliyotolewa na Mungu ni mwanga wa ukweli unaodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. 
Injili hii pia inatueleza sisi kuwa Yesu atarudi tena hapa duniani kama Bwana wa ujio wa pili, atatufanya sisi kuwa hai tena, na atatufanya sisi kutawala pamoja naye katika miaka ile elfu moja katika utawala wa Milenia na kisha atatuwezesha sisi kuingia katika Ufalme wa milele wa Mungu na kuishi milele. Je, unawezaje kutafakari jinsi ambavyo uzima wa milele ulivyo?
Ulimwengu huu ni mpana sana kiasi kuwa wanasayansi wanasema kuwa kuna mfumo wa nyota ndani ya mfumo wa nyota katika makundi mengi ya nyota na sayari yasiyohesabika nje kabisa ya mfumo wetu wa jua. Eneo la ulimwengu mzima ambao Mungu aliiumba ni kubwa sana na la kushangaza. Nje ya ulimwengu wetu, kuna idadi kubwa ya mizingo ya kimaumbile ambayo hata hatuifahamu na ambayo inapatikana katika makundi ya nyota na sayari mbalimbali. Vimwondo ambavyo vinaanguka sasa kwa kweli ni vipande toka katika sayari ambazo zilianguka mbali sana katika makundi mengine ya nyota na sayari katika mabilioni ya miaka iliyopita na kwamba ni hadi sasa ndio yanaifikia hali ya hewa ya duniani na kuungua. 
Kwa maneno mengine, tunathibitisha sasa yale yaliyotokea katika mabilioni ya miaka yaliyopita. Vivyo hivyo, himaya kubwa ya ulimwengu iliyoumbwa na Mungu inabakia kuwa haifahamiki vya kutosha. Lakini pamoja na kuwa ulimwengu bado haufahamiki vizuri kwetu sisi, kwake Mungu ulimwengu ni kitu kidogo sana kama vile kiganja cha mkono. Mungu ni yeye anayejua yote na aliye mahali popote. Yeye aliyeviumba vitu vyote na akaanzisha utaratibu wa ulimwengu. 
Sisi tunauangazia ulimwengu kwa mwanga wa ukweli kwamba kwa kuamini katika injili ya maji na Roho watu wote wanaweza kupokea ondoleo la dhambi la milele na kisha kuufurahia uzima wa milele. Wana wa Mungu wanao mwanga angavu wa maisha ambao unawaruhusu kuishi milele pamoja na Yesu Kristo. Mungu anaishi pamoja nasi milele hali akituruhusu kuifurahia raha yake na kujivika utukufu wake. Kwa nini? Kwa sababu tunaamini katika mwanga wa injili wa nguvu yake. Mara tulipougundua mwanga huu uliotuwezesha kuufahamu ukweli, basi hatukuweza kufanya lolote zaidi ya kuueneza mwanga huu kwa wengine. 
Na pale tulipoona ukuu wa Mungu unavyofanya kazi katika ulimwengu mzima, imani yetu katika kazi zake ilizidi kuchipuka. Baadhi ya nyota zilipotea katika mabilioni ya miaka iliyopita, lakini bado macho yetu yanaziona leo kwa sababu zilikuwa ni mabilioni ya mwanga miaka mingi iliyopita mbali na sayari hii! Tunaweza kutafakari juu ya dhana ya “umilele” pale tunapochunguza juu ya mwanzo na mwisho wa ulimwengu. 
Sisi ambao tumefanyika kuwa sehemu ya Kanisa la Mungu sasa tunayaishi maisha yetu kwa kuueneza mwanga wa injili ya kweli kwa kuwa tunaamini katika ukweli uliodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu. Tunaamini kwamba wokovu huu unatupa hakika ya uzima wa milele na maisha yenye baraka katika Ufalme wa Baba yetu. Na tunatambua kuwa Mungu anataka watu wote waokolewe na kisha waufikie ufahamu wa kweli (1 Timotheo 2:4). Kwa hiyo, wale wanaoufahamu mwanga wa wokovu ni lazima waendelee kuieneza injili ya maji na Roho, jukumu ambalo Mungu amewakabidhi. 
Mungu ametubariki sisi ili kwamba tuweze kuifanya kazi hii. Hali tukitambua jinsi ambavyo ukweli huu ni mkuu na wenye baraka, jambo la muhimu kwetu kulifanya linakuwa ni kuliendeleza jukumu hili tulilopewa kwa imani. Ninaamini kuwa ninyi nyote mtaijaza mioyo yenu kwa mwanga ambao unaufahamu ukweli wa Mungu. Kwa neema ya Mungu wewe na mimi tumekuja kuamini katika huduma za wokovu zilizodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, na tumefanyika kuwa mwanga wa wokovu kwa ulimwengu mzima, yaani wale ambao wanauangazia ulimwengu mzima. Halleluya! Ninatoa shukrani zangu zote kwa Mungu.