Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[1-2] Ni Lazima Tuzifahamu Nyakati Saba (Ufunuo 1:1-20)

(Ufunuo 1:1-20)
 
Ninamshukuru Mungu anayetupatia tumaini katika nyakati hizi za giza. Ni matumaini yetu kuwa kila kitu kitajidhihirisha kama kilivyoandikwa katika Kitabu cha Ufunuo, na kwamba tutaendelea kusubiri kwa imani ili kwamba Neno lote la unabii litimizwe.
Mambo mengi yameandikwa kuhusiana na Kitabu cha Ufunuo. Wakati ambapo wanazuoni wanaendelea kutoa nadharia na ufafanuzi mwingi, ukweli unabaki kuwa ni vigumu kuipata walau kazi yao moja ambayo imeelezewa vizuri kwa ukaribu na Biblia. Ni kwa neema ya Mungu tu, kwamba baada ya kuwa nimetumia masaa mengi yasiyo na hesabu kusoma Neno la Ufunuo, sasa nimeweza kuandika kitabu hiki. Hata sasa ninapoongea moyo wangu umejawa na ukweli wa Ufunuo. Pia Roho Mtakatifu amenijaza nilipokuwa nikiandaa komentare na mahubiri kwa ajili ya kitabu hiki.
Kwa kweli ni jambo la kushangaza kiasi kuwa moyo wangu umejazwa sana na tumaini la Mbinguni na utukufu wa Ufalme wa Milenia. Pia nimefikia hatua ya kutambua jinsi ambavyo Bwana wetu anavyokutukuza kufia-dini kwa watakatifu. Sasa, nipo tayari kukushirikisha Neno la hekima ambalo Mungu amenionyesha na kisha kukusaidia wewe ili uweze kulifahamu.
Ninapoandika kitabu hiki juu ya Ufunuo, utukufu wa Mungu unaujaza moyo wangu zaidi. Kusema kweli, nilikuwa sijatambua jinsi Neno la Ufunuo lilivyo kuu.
Mungu alimwonyesha Yohana ulimwengu wa Yesu Kristo. Maneno ya ufunguzi “Ufunuo wa Yesu Kristo” yana maanisha nini? Kamusi inalifafanua neno ufunuo kama tendo la kudhihirisha au kuwasilisha ukweli wa kimungu. Hivyo, ufunuo wa Yesu Kristo maana yake ni kudhihirisha yale ambayo yatakuja kutokea baadaye katika Yesu Kristo. Kwa lugha nyingine, Mungu alimwonyesha Yohana, ambaye alikuwa mtumishi wa Yesu Kristo mambo yote ambayo yatakuja kutokea katika wakati wa mwisho.
Kabla hatujalichunguza Neno la Ufunuo, kuna jambo moja ambalo tunapaswa kuwa na hakika nalo kabla—jambo hilo ni kwamba tuchunguze ikiwa ni kweli kuwa Neno la Ufunuo lililoandikwa ni lugha ya picha au ni ukweli. Kwa kweli yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Ufunuo ni ukweli wenye uhakika, maana kwa kupitia maono ambayo Yohana aliyaona Mungu ametudhihirishia sisi kwa kina juu ya yale ambayo yatakuja kutokea hapa ulimwenguni.
Ni kweli kuwa wanazuoni wengi wamekwishaandika nadharia nyingi za kitheolojia na mafafanuzi kuhusiana na unabii wa Ufunuo. Pia ni kweli kuwa juhudi za wanazuoni hawa zimekuwa na lengo la kuufunua ukweli wa Ufunuo kwa kadri ya uwezo wao wote. Lakini nadharia hizo zimeleta madhara zaidi kwa jumuia ya Ukristo kwa kuwa nadharia hizo hazikubaliani na ukweli wa Biblia na kwa sababu hiyo zimeleta mkanganyiko zaidi. Kwa mfano, wanazuoni wahafidhina wamekuwa wakiunga mkono kitu kinachoitwa ‘amilenia’—maana yake wanadai kuwa hakuna Ufalme wa Milenia. Lakini mawazo kama hayo ni kinyume kabisa na ukweli wa Biblia.
Ufalme wa miaka elfu moja umeandikwa kwa kweli katika sura ya 2 ya Ufunuo, ambapo imeandikwa kuwa watakatifu si tu kwamba watautawala Ufalme huu, bali pia wataishi pamoja na Kristo kwa miaka elfu moja. Kwa upande mwingine, sura ya 21 inatueleza kuwa baada ya Ufalme wa Milenia, watakatifu watairithi Mbingu Mpya na Nchi Mpya na kisha wataishi na kutawala pamoja na Kristo milele. Mambo haya yote ni ukweli. Biblia inatueleza kuwa kweli hizi zote zitatokea sio kama utimilifu katika lugha ya picha bali zitatokea kama utimilifu halisi katika historia.
Lakini tukiwaangalia Wakristo leo hii, tutaona kuwa wengi wao wanaonekana kuwa na matumini kidogo juu ya Ufalme wa Milenia. Je, mtazamo huo si sawa na kuukana ukweli? Je, hii haiwezi kumaanisha kuwa ahadi za Mungu kwa waamini wake zitakuwa ni maneno matupu? Kama kusingekuwa na Ufalme wa Milenia unaowangojea waamini, na kama kusingekuwa na Mbingu na Nchi Mpya, basi ni dhahiri kuwa imani ya wale ambao wameokolewa kwa kumwamini Yesu kama Mwokozi wao ingeligeuka na kuwa isio na maana.
Kuhusiana na jambo hili, watheolojia wengi na watumishi wengi siku hizi wanadai kuwa alama 666 inayotabiriwa katika Ufunuo ni lugha ya picha. Lakini bila kufanya kosa: siku ya unabii huu itakapotimilizwa, basi imani ya nafsi zenye bahati mbaya hii, yaani zile nafsi zilizoamini katika uongo huu zitajikuta ni kama nyumba iliyojengwa juu ya mchanga.
Ikiwa wale wanaomwamini Yesu hawataliamini Neno la kweli lililodhihirishwa kwao katika Biblia, basi Mungu atawachukulia wao sawa na wale wasioamini. Hii inaweza kumaanisha kuwa si tu kwamba hawaifahamu injili ya maji na Roho iliyotolewa na Mungu, bali pia itamaanisha kuwa Roho Mtakatifu hakai ndani ya mioyo yao. Hii ndiyo sababu mioyo yao haina matumaini juu ya Ufalme wa Milenia au juu ya Mbingu na Nchi Mpya ambayo Mungu ametuahidia. Hata kama watakuwa walimwamini Yesu, ukweli utabaki kuwa hawakumwamini Yesu kwa mujibu wa ukweli wa Neno la Mungu ulioandikwa. Kile kilichoandikwa katika Ufunuo ni Neno la Mungu ambalo linatuonyesha kile ambacho kwa hakika kitakuja kutokea katika ulimwengu huu.
Sura ya 2 na ya 3 ya Ufunuo inarekodi Neno la kutia moyo kwa makanisa saba ya Asia. Ndani ya maneno hayo kuna maoni na maonyo ya Mungu kwa makanisa hayo saba. Kwa hakika, Mungu aliahidi kuwa taji ya uzima itatolewa kwa wale ambao watavumilia kwa uaminifu na kuyashinda mateso watakayoyapata. Hii ina maanisha kwa hakika kuwa kufia-dini kunawangojea waamini wote wa nyakati hizo za mwisho.
Neno la Ufunuo linazungumzia kuhusu kufia-dini kwa watakatifu, kufufuka kwao na kunyakuliwa, na ahadi ya Ufalme wa Milenia na Mbingu Mpya na Nchi Mpya ambazo Mungu amezifanya kwa ajili yao. Neno la Ufunuo linaweza kuwa ni ufariji mkuu na baraka kwa wale wanaoamini juu ya uhakika na uhalisia wao wa kufia-dini, lakini Neno hilo halina mengi ya kuwapatia wale wasioamini juu ya kufia-dini. Hivyo tunaweza kuishi katika uvumilivu hali tukitii kwa imani yetu isiyotingishika katika Neno la ahadi lililoandikwa katika Ufunuo na hasa juu ya nyakati za mwisho.
Kwa kweli somo kubwa na lililoelezewa sana katika Neno la Ufunuo ni kufia-dini, ufufuo na kunyakuliwa kwa watakatifu, na Ufalme wa miaka elfu moja na Mbingu na Nchi Mpya. Na hii ndiyo sababu kuwa madhumuni ya Mungu kwa Kanisa la Mwanzo yalikuwa na lengo la kuwafanya watakatifu kuilinda imani yao hadi mwisho kwa wao kuifia-dini. Kwa kuwa Mungu alikuwa amepanga mambo haya yote ndio maana alizungumza juu ya kufia-dini kwa watakatifu wote. Kwa maneno mengine, Mungu ametueleza kuwa watakatifu wote watamshinda Mpinga Kristo kwa kupitia tendo la kufia-dini katika nyakati za mwisho.
Uelewa mkamilifu juu ya sura ya 1-6 ni wa muhimu sana katika kukielewa Kitabu cha Ufunuo kwa ukamilifu wake. Sura ya 1 inaweza kuelezewa kama utangulizi, wakati sura ya 2 na ya 3 zinazungumzia juu ya kufia-dini kwa watakatifu wa Kanisa la Mwanzo. Sura ya 4 inatueleza juu ya kuketi kwa Kristo katika kiti cha enzi cha Mungu. Sura ya 5 inatueleza juu ya Yesu Kristo kulifungua gombo la mpango wa Baba na utimilifu wake, na sura ya 6 inazungumzia juu ya nyakati saba ambazo Mungu ameziweka kwa wanadamu. Ni muhimu sana kuielewa sura ya 6 kwa kuwa itakufungulia mlango wa kukielewa kitabu chote cha ufunuo.
Sura ya 6 inaweza kuelezewa kama ni alama kuu kwa nyakati saba ambazo Mungu Baba amezipanga kwa wanadamu katika Yesu Kristo. Katika alama hii kuu ya Mungu kunapatikana utoaji wa Mungu wa vipindi saba ambavyo Mungu atavileta kwa wanadamu. Ikiwa tunazifahamu na kuzielewa nyakati hizi saba, basi tutaweza kutambua kuwa sasa tunaishi katika wakati upi kati ya hizo nyakati saba. Pia tutatambua juu ya aina ya imani inayohitajika ili tuweze kuvumilia na kuushinda wakati wa farasi wa kijivujivu, ambao ni wakati wa Mpinga Kristo anayekuja.
Kama inavyoelezewa katika Ufunuo 6, wakati muhuri wa kwanza ulipofunguliwa alitokea farasi mweupe. Aliyempanda huyo farasi mweupe alikuwa ameshika upinde, na alipewa taji na kisha akaenda akishinda na kushinda. Mpanda farasi anayezungumziwa hapa ni Yesu Kristo, lakini ule ukweli kuwa mpanga farasi huyo alikuwa na upinde una maanisha kuwa Yesu ataendelea kupambana na kumshinda Shetani. Kwa lugha nyingine, wakati wa farasi mweupe unazungumzia wakati wa ushindi wa injili ya maji na Roho ambao Mungu ameuruhusu duniani, na wakati huu utaendelea hadi pale madhumuni ya Mungu yatakapotimilizwa.
Wakati wa pili ni wakati wa farasi mwekundu. Wakati huu unahusu kuja kwa wakati wa Shetani, ambapo Shetani ataidanganya mioyo ya watu ili iweze kufanya vita huku akiindolea mbali amani duniani na kuwatesa watakatifu.
Baada ya wakati wa farasi mwekundu unakuja wakati wa farasi mweusi, yaani wakati ambapo njaa itazipiga nafsi na miili ya wanadamu. Wewe na mimi sasa tunaishi katika kipindi hiki chenye njaa ya kiroho na kimwili. Wakati huu unafuatiwa na wakati wa farasi wa kijivujivu ambapo Mpinga Kristo atainuka, na kwa kule kuonekana kwake ulimwengu utaangukia katika mateso ya kifo.
Wakati wa farasi wa kijivujivu ni wakati wa nne. Katika wakati huu, ulimwengu utapigwa kwa mapigo ya tarumbeta saba, ambapo theluthi ya misitu itaungua, theluthi ya bahari itageuka kuwa damu, na theluthi ya jua na mwezi vitageuka na kuwa giza.
Wakati wa tano ni wakati wa ufufuo wa watakatifu na kunyakuliwa. Kama ilivyoandikwa katika Ufunuo 6:9-10, “Na alipoufungua muhuri wa tano nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?”
Wakati wa sita ni maangamizi ya ulimwengu wa kwanza. Kwa mujibu wa Ufunuo 6:12-17, “Nami nikaona, alipoufungua muhuri wa sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu, na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi. Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka hali pake. Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima, wakiiambia milima na miamba, tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo. Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?”
Ni kitu gani basi kitatokea katika wakati wa saba ambao Mungu ameuweka kwa ajili yetu? Katika wakati huu wa mwisho, Mungu atawapatia watakatifu Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya.
Katika nyakati hizi saba ni wakati upi ambapo sisi tunaishi hivi sasa? Baada ya kuwa tumeshapita wakati wa farasi mwekundu ambapo ulimwengu ulikumbwa na vita nyingi, sasa tunaishi katika wakati wa farasi mweusi.
Neno lote la Ufunuo halijaandikwa kwa mtazamo hasi tu, bali limeandikwa kwa mtazamo chanya kwa waamini. Mungu alisema kuwa hapendi kuwaptia waamini wa siku za mwisho tumaini la Ufalme wa Miaka elfu moja tu, bali pia alisema hatawaacha kama yatima hapa ulimwenguni.
Hata hivyo, ili tuweze kuufahamu ukweli uliodhihirishwa katika Ufunuo ni lazima kwanza tuachilie mbali mafundisho ya uongo kama vile nadharia za kunyakuliwa kabla ya dhiki, amilenia, na kunyakuliwa baada ya dhiki, na kisha tuyarudie Maandiko.
Mungu amezipanga nyakati saba kwa ajili yetu katika Yesu Kristo. Nyakati hizi zote saba zilipangwa na Mungu kwa ajili ya watakatifu katika Yesu Kristo tangu mwanzo wa uumbaji wake. Hata hivyo, kwa kuwa wanazuoni wengi hawazifahamu nyakati hizi zilizopangwa na Mungu, basi wamefikia hatua ya kutoa mafafanuzi yao binafsi na nadharia ambazo hazina msingi juu ya Neno la Ufunuo, na kwa sababu hiyo watu wamechanganywa zaidi. Lakini sisi sote tunapaswa kuzitambua nyakati saba zilizopangwa na Mungu, na kisha kwa ufahamu na imani katika ukweli huu, tumshukuru na kumtukuza Mungu kwa yote ambayo ameyafanya kwa ajili yetu. Mipango yote ya Mungu kwa watakatifu imepangwa na inatimilizwa ndani ya nyakati hizi saba.
Ninaamini kuwa majadiliano yangu hadi sasa yamekupatia uelewa wa msingi juu ya vifungu vya utangulizi katika kitabu cha Ufunuo. Kwa kupitia Kitabu cha Ufunuo, tunaweza kuona kuwa uumbaji wa Mungu ulianzisha mwanzo wa nyakati saba ambazo amezipanga katika Yesu Kristo kwa injili ya maji na Roho. Kwa kuzifahamu hizi nyakati saba, imani yetu itafanyika kuwa imara zaidi. Na kwa kuzifahamu nyakati hizo, basi sisi tutaweza kuyatambua majaribu ambayo yanatungojea hali tunapoishi katika kipindi hiki cha farasi mweusi, na kwa ufahamu huu tutaweza kuishi kwa imani.
Waamini—ambao ni pamoja na mimi na wewe—tunapaswa kuuawa na kuifia-dini mara wakati wa farasi wa kijivujivu utakapowadia ukiwa sehemu ya zile nyakati saba zilizopangwa na Mungu. Waamini watakapolitambua hili mioyo yao itajazwa matumaini na macho yao yataweza kuona yale ambayo walikuwa hawayaoni hapo kabla. Wakati watumishi na watakatifu wa Mungu watakapotambua kuwadia kipindi cha kufia-dini, basi maisha yao yatasafishwa kutokana na uchafu wote, maana mara watakapotambua kuwa wamepangiwa kuwa wafia-dini katika kipindi cha farasi wa kijivujivu, basi mioyo yao itaandaliwa kwa kitambo kidogo na kuwa safi na tayari.
Sisi sote tutauawa na kuwa wafia-dini kwa namna ile ile kama watakatifu wa Kanisa la Mwanzo walivyouawa na kuifia-dini. Ni lazima utambue kuwa wakati kipindi cha farasi wa kijivujivu kitakapowadia, basi ni dhahiri kuwa kuuawa na kuifia-dini ni kitu ambacho hakiwezi kukwepeka kwa waamini wa kweli, maana mara baada ya kuifia-dini kitakachofuata ni ufufuo.
Baada ya kuifia-dini kitakachofuata ni ufufuo, na ufufuo huo utaandamana na kunyakuliwa, na katika kunyakuliwa tutaonana na Bwana mbinguni. Baada ya kuuawa kwa watakatifu kwa kuifia-dini, Bwana wetu atawafufua watakatifu toka katika kifo na kisha atawaleta katika unyakuo katika karamu ya harusi mbinguni.
Wakati wa kunyakuliwa kwa watakatifu utakapowadia, ulimwengu utakuwa umeharibiwa sana kiasi kuwa itakuwa ni mahali pasipowezekana watu kuishi vizuri. Theluthi ya misitu itakuwa imeungua; bahari, mito, na hata vijito vitakuwa vimegeuka na kuwa damu. Je, utapenda kuishi katika ulimwengu kama huo zaidi ya vile ulivyokwisha ishi? Katika hali kama hiyo watakatifu watakuwa na sababu zaidi ya kujiunga na kuifia-dini, maana hakutakuwa na tumaini lolote litakalokuwa limesalia kwa ajili ya ulimwengu.
Je, unapenda kuishi katika ulimwengu ulioharibika hali ukitetemeka kwa hofu? Kwa kweli hapana! Mwisho wa nyakati kutakuwa na kuuawa kwa watakatifu kwa kuifia-dini, na baada ya mauaji hayo ya kuifia-dini kutakuwa na ufufuo na kunyakuliwa, na baada ya ufufuo na kunyakuliwa kutakuwa na utukufu wa kuishi milele na Mungu katika Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya.
Biblia inatueleza wazi kuwa baada kufikia nusu ya Dhiki Kuu—ambayo ni miaka mitatu na nusu katika kipindi cha miaka saba—watakatifu watauawa na kuifia-dini kwa sababu ya kusimama kinyume na Mpinga Kristo kwa imani yao, na baada ya hayo kutafuatiwa na ufufuo na kunyakuliwa na kisha kufuatiwa na ujio wa pili wa Kristo. Kwa maneno mengine, kurudi kwa Kristo na ufufuo wa watakatifu kutatokea baada ya kuuawa na kuifia-dini kwa watakatifu katika kipindi cha Dhiki Kuu. Sasa ni wakati wako kuwa na mawazo sahihi juu ya mada hizo.
Je, tunaweza kuuawa na kuifia-dini hata kabla ya kipindi cha farasi wa kijivujivu hakijafika? Kwa kweli jibu ni hapana. Lakini nadharia ya “kunyakuliwa kabla ya dhiki” inafundisha kuwa watakatifu wote watanyakuliwa na Mungu kabla ya kuanza kwa Dhiki Kuu, na kwamba hawataipitia ile miaka saba ya Dhiki. Mtazamo huu unadai kuwa hakuna kuuawa kwa kuifia-dini, na pia mtazamo huu hauamini kuwa kipindi au wakati wa farasi wa kijivujivu utawajia watakatifu.
Ikiwa nadharia hii ya “kunyakuliwa kabla ya dhiki” ni ya kweli, basi ufiaji-dini kwa watakatifu unaotajwa katika sura ya 13 ya Ufunuo una maanisha nini? Hapa inaelezwa wazi wazi kuwa watakatifu watauawa kwa ajili ya kuifia-dini kwa sababu watakatifu hao, ambao majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima cha Mungu hawatamsujudia wala kumtii Shetani.
Wale wanaofundisha nadharia ya “kunyakuliwa baada ya dhiki” pia wanakosa uelewa sahihi wa kipindi cha farasi wa kijivujivu, na kuuawa kwa kuifia-dini, ufufuo, na kunyakuliwa kwa watakatifu. Kwa mujibu wa nadharia hii, watakatifu watabakia katika ulimwengu huu hadi mwisho wa tarumbeta ya saba ya mapigo itakapolia. Lakini kitabu cha Ufunuo kinatueleza bayana kuwa ufufuo na kunyakuliwa kwa watakatifu kutatokea mara baada ya malaika wa mwisho atakapolipiga tarumbeta lake—yaani kwa maneno mengine, kabla ya mabakuli saba ya ghadhabu hayajamwagwa. Hii ndiyo sababu kitabu cha Ufunuo ni Neno kuu la faraja na baraka kwa wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho.
Dhana ya “Amilenia” imeleta mkanganyiko na kuwafanya watu kukata tama, na si dhana ya kweli. Kile ambacho Bwana amekiahidi kwa wanafunzi wake—kuwa watakatifu watapewa mamlaka ya kutawala juu ya miji mitano au kumi—ndicho kitakachotokea hasa katika Ufalme wa Milenia.
Ni lazima ukumbuke kuwa nadharia kama vile za kunyakuliwa kabla ya dhiki, kunyakuliwa baada ya dhiki, na amilenia, yaani dhana inayoamini kuwa hakutakuwa na mateso, ni nadharia ambazo hazina msingi na zinazoleta mkanganyiko kwa waamini.
Sasa, ni kwa nini Mungu alitupatia Kitabu cha Ufunuo? Mungu alitupatia Neno la Ufunuo ili kutuonyesha yale ambayo atatupatia katika vile vipindi au nyakati saba na kuwapatia tumaini la kweli la Mbinguni wale waliofanyika kuwa wanafunzi wa Yesu.
Hata sasa, mambo yanatokea kama yalivyopangwa na Mungu. Wakati huu tunaoishi sasa ni wakati wa farasi mweusi. Muda si mrefu, kipindi hiki cha farasi mweusi kitapita na kipindi cha farasi wa kijivujivu kitawadia. Na katika kipindi hiki cha farasi wa kijivujivu mauaji ya kufia-dini yataanza kwa watakatifu yakifuatiwa na kuinuka kwa Mpinga Kristo. Wakati huu ni wakati ambapo ulimwengu mzima utajumuishwa na kuunganishwa chini ya mamlaka ya Mpinga Kristo. Wanafunzi wa Yesu ni lazima wajiandae sasa na kuwa tayari kukabiliana na ujio wa kipindi cha farasi wa kijivujivu kwa imani.