Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[2-1] Barua Kwa Kanisa la Efeso (Ufunuo 2:1-7)

(Ufunuo 2:1-7)
“Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu. Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.”
 

Mafafanuzi 
 
Aya ya 1: “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu.”
Kanisa la Efeso lilikuwa ni kanisa la Mungu lililopandwa kwa imani inayoamini katika injili ya maji na Roho ambayo Paulo aliihubiri. Katika kifungu hiki, “vinara saba vya dhahabu” vina maanisha ni makanisa ya Mungu, yaani makusanyiko ya wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho, na “nyota saba” zina maanisha kuwa ni watumishi wa Mungu katika yale makanisa. Kwa upande mwingine, sentensi inayosema, “Yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume,” ina maanisha kuwa Mungu mwenyewe anawashikilia na anawatumia watumishi wake. 
Ni lazima tutambue kuwa yale ambayo Mungu ameyaeleza kwa makanisa saba ya Asia kwa kupitia mtumishi wake Yohana, ndiyo yanayoelezwa kwa makanisa yake yote katika wakati wa sasa ambao unakabiliana na ujio wa nyakati za mwisho. Mungu anaongea nasi na anatueleza jinsi ya kuyashinda majaribu na mateso yanayotungojea kwa kupitia makanisa yake na watumishi wake. Ni lazima tumshinde Shetani kwa kusikia na kuamini katika Neno la Ufunuo. Mungu anaongea na kila mmoja kuhusu makanisa yake.
 
Aya ya 2: “Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;”
Mungu alilisifia na kulikubali Kanisa la Efeso kwa ajili ya matendo yake, taabu yake, kwa subira yake, kwa kutokuvumilia mabaya, na kwa kuwajaribu na kuwapambanua mitume wa uongo. Katika kifungu hiki tunaweza kuona jinsi imani ya Kanisa la Efeso ilivyokuwa kubwa na jinsi walivyokuwa wamejitoa kwa Bwana. Lakini ni lazima tutambue kuwa haijalishi jinsi mwanzo wa imani unavyoweza kuwa mzuri, ikiwa imani hiyo itakuja kupotoka baadaye, basi imani hiyo itakuwa ni bure. Imani yetu ni lazima iwe imani ya kweli ambayo mwanzo wake na mwisho wake vibakie kuwa sawa.
Lakini imani ya mtumishi wa Kanisa la Efeso haikuwa hivyo, na kwa sababu hiyo mtumishi huyu alionywa na kukemewa na Mungu kwamba atakiondoa kinara chake toka mahali pake. Kama historia ya kanisa inavyoonyesha, makanisa saba ya Asia Ndogo yalishutumiwa kwamba vinara vyake vilikuwa vimeondolewa. Ni lazima tujifunze toka kwa Kanisa la Waefeso na tukumbuke kuwa makanisa yetu ni lazima yathibitishwe na Mungu kuwa ni mali yake kwa kuyaweka katika imani ya injili ya maji na Roho, na kwamba ni lazima tuwe watumishi wa Mungu ambao tunayatunza makanisa yetu kwa imani hii.
 
Aya ya 3: “tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka.”
Bwana wetu anayaangalia makanisa yake yote na anafahamu vizuri jinsi watakatifu wake wanavyotaabika kwa ajili ya jina lake. Lakini watakatifu wa Kanisa la Efeso walikuwa wakiiacha imani yao ya kwanza na kuanza kuangukia katika njia yenye makosa kwa kuipunguza nguvu injili ya maji na Roho kwa kutumia imani nyingine.
 
Aya ya 4: “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.”
Matendo ya imani ya mtumishi na watakatifu wa kanisa la Efeso yalikuwa ni makubwa sana kiasi kuwa Bwana mwenyewe aliyakubali na kuwasifia kwa ajili ya matendo yao, taabu yao, na uvumilivu wao. Walikuwa wamewajaribu na kuwang’amua mitume wa uongo, walikuwa wamevumilia na kutaabika kwa ajili ya jina la Bwana, na wala hawakuchoka. Lakini katikati ya haya matendo makuu ambayo walisifiwa, walikuwa wamepoteza kitu kimoja ambacho ni cha muhimu sana kuliko matendo hayo: walikuwa wameuacha upendo wao wa kwanza uliotolewa na Yesu Kristo.
Je, hii ina maanisha nini? Ina maanisha kuwa walishindwa kuifuata na kuitunza injili ya maji na Roho ambayo iliwaruhusu kukombolewa mara moja toka katika dhambi zao zote kwa kuwa na imani katika Bwana. Kwa upande mwingine, kuiacha injili ya maji na Roho kuna maanisha kuwa walikuwa wameyaruhusu mafundisho ya uongo na injili nyingine kuingia katika kanisa lao.
Je, hizi injili nyingine na hayo mafundisho mengine yalikuwa ni yapi? Injili na mafundisho hayo mengine yalikuwa ni falsafa za kidunia na mawazo ya kibinadamu. Mambo haya bado yanasimama kinyume dhidi ya ukweli wa wokovu ambao Mungu amewapatia wanadamu. Mambo hayo yanaweza kuwa na faida kwa mwili wa mwanadamu, au pengine yanaweza kuwa mazuri kwa kuleta umoja na amani miongoni mwa watu, lakini mambo hayo hayawezi kuifanya mioyo ya watu kuungana na moyo wa Mungu. Hivi ndivyo mtumishi na watakatifu wa Kanisa la Efeso walivyoishia kuibadili imani yao kwenda katika imani ya kihaini ambayo ililaumiwa na Mungu. Na hii ndiyo sababu walikemewa na Bwana.
Tunapoangalia katika historia ya kanisa, tunaweza kuona kuwa injili ya maji na Roho ilianza kupungua mapema katika kipindi cha Kanisa la Mwanzo. Hivyo, kwa kujifunza toka katika somo hili, ni lazima tuishikilie kwa nguvu injili ya maji na Roho, ni lazima tumfurahishe Bwana kwa imani yetu isiyoyumba, na kisha tumshinde Shetani na ulimwengu katika mapambano yetu dhidi yao.
Je, ule “upendo wa kwanza” kwa mtumishi na watakatifu wa Kanisa la Efeso ulikuwa ni nini? Upendo wao wa kwanza si kitu kingine bali ni injili ya maji na Roho ambayo Mungu aliwapatia. Injili ya maji na Roho ni Neno la wokovu ambalo lina nguvu ya kumkomboa kila mtu toka katika dhambi zote za ulimwengu.
Mungu aliwafunulia Paulo, Yohana na watumishi wa makanisa saba ya Asia juu ya jinsi injili ya maji na Roho ilivyo na aliwaruhusu kuifahamu. Hivi ndivyo walivyoweza kuiamini injili hii, na hivyo ndivyo injili hiyo ilivyowawezesha wale walioisikia kuokolewa toka katika dhambi zote za ulimwengu.
Injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana wetu inapatikana katika Neno la ubatizo wa Kristo na damu yake Msalabani. Pamoja na hayo, mtumishi wa Kanisa la Efeso, pamoja na kuwa alikuwa amekutana na Bwana kwa kupitia injili ya maji na Roho na kwamba alikuwa ameihubiri injili hiyo kwa uaminifu hapo mwanzo, maandiko yanaonyesha kuwa mtumishi huyo alikuja baadaye kuiacha injili hiyo. Hivyo, Bwana alimkemea kwa ufahamu na imani yake potofu.
 
Aya ya 5: “Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”
Kule kusema kuwa mtumishi wa Kanisa la Efeso alikuwa ameanguka toka katika upendo wa Mungu kuna maanisha kuwa kusanyiko lile la waumini walikuwa wameiacha injili ya maji na Roho. Hii ndiyo sababu Bwana aliwaambia kukumbuka mahali walipoipotezea imani yao, watubu, na kisha kuyafanya matendo ya kwanza.
Je, ni jambo gani ambalo linaweza kuwa lililifanya Kanisa la Efeso kuipoteza injili ya maji na Roho? Udhaifu wa imani wa Kanisa la Waefeso ulianza kutokana na mawazo ya kimwili ya mtumishi wake, na mawazo hayo ndiyo yaliyosababisha kulipeleka kanisa pembeni. Injili ya maji na Roho ni ya kutoka kwa Mungu, ni ukweli mkamilifu ambao umeufunua uongo wote wa mafundisho mengine ya kiimani ya dini zote hapa ulimwenguni. Hii ina maanisha kuwa wakati Kanisa la Efeso lilipohubiri na kuieneza injili ya maji na Roho, basi ugomvi kati ya kanisa na watu wa kidunia ulikuwa hauwezi kukwepeka.
Matokeo ya ugovi huo yalisababisha waamini wa kanisa la Efeso kushindwa kuhusiana vizuri na watu wa kidunia kiasi kuwa waliingizwa katika kuteswa kwa ajili ya imani yao. Ili kukwepa mateso hayo na kuwafanya watu waweze kuingia katika kanisa la Mungu kwa urahisi, basi mtumishi wa Kanisa la Efeso aliiacha injili ya maji na Roho na akaruhusu injili ya kifalsafa zaidi kufundishwa.
Injili ya kifalsafa inayotamkwa hapo juu ni injili ya uongo inayotokana na mawazo ya kibinadamu inayolenga katika kurudisha mahusiano si tu kati ya Mungu na wanadamu bali pia kuleta amani katika mahusiano ya wanadamu. Aina hii ya imani ya mshazari na mlazo si aina ya imani ambayo Mungu anaitaka tuwe nayo. Imani ambayo Mungu anataka tuwe nayo ni imani ambayo inarudisha mahusiano na amani kati yetu na Mungu kwa unyenyekevu.
Sababu iliyomfanya mtumishi wa Kanisa la Efeso kuipoteza injili ya maji na Roho ni kwa sababu alijaribu kuyakubali yale ambayo hayawezi kukubaliwa katika kanisa la Mungu—yaani kuwakubali watu wa kidunia wasioamini katika injili ya maji na Roho na kisha kuyarekebisha mafundisho yake ili yaendane na matakwa ya watu hao wa kidunia. Kanisa la Mungu linaweza kupandwa katika msingi wa Neno la injili ya maji na Roho tu.
Lakini kuna watu wengi sana katika wakati wa sasa kama ilivyokuwa katika kipindi cha Kanisa la Mwanzo ambao wanafikiri kuwa inatosha kumwamini Yesu kwa kiasi fulani ili waweze kuokolewa; pia watu hao hawaoni sababu ya kuamini katika injili ya maji na Roho. Lakini kumwamini Yesu hali ukiiacha injili ya maji na Roho iliyotolewa na Mungu ni imani yenye makosa makubwa. Wale wote wanaomwamini Bwana kama kutekeleza matendo ya kidini hali wakiwa hawajitoi kwa moyo wote watakuwa ni maadui wa Mungu. Hii ndiyo sababu Bwana alimkemea na kumtia moyo mtumishi wa Kanisa la Efeso kuitubia imani yake potofu na kisha kurudi katika imani yake ya kwanza, ambayo ni imani ya kweli ambayo aliipata alipoisikia injili ya maji na Roho kwa mara ya kwanza.
Hapa kuna somo la muhimu sana kwetu sote: ikiwa kanisa la Mungu litaanguka na kuiacha imani yake katika injili ya maji na Roho, basi ni dhahiri kuwa Mungu hataendelea tena kuliita kanisa hilo kuwa ni kanisa lake. Hii ndiyo sababu Bwana alisema kuwa atakiondoa kinara toka mahali pale na kisha kuwapatia waamini wa injili ya maji na Roho.
Kanisa ambalo limeiacha na haliihubiri tena injili ya maji na Roho si kanisa la Mungu. Ni muhimu kwetu kutambua kuwa kuiamini, kuilinda, na kuihubiri injili ya maji na Roho ni vitu muhimu sana kuliko matendo mengine yoyote yale.
Sehemu hii ya Asia Ndogo mahali yalipokuwepo haya makanisa saba kama kifungu cha maandiko hapo juu kinavyoonyesha, kwa sasa ni eneo la Waislamu. Hivyo, Bwana amekiondoa kinara, ambacho ni kanisa la Mungu toka huko Asia Ndogo hadi hapa tulipo na ametufanya kuihubiri injili ya maji na Roho katika ulimwengu wote. Lakini katika kanisa la kweli la Mungu kuna ukweli wa injili ya maji na Roho. Kanisa la Mungu haliwezi kuishi pasipo kuwepo kwa ukweli huo. Katika kipindi cha utume, wanafunzi kumi na mbili wa Yesu walikuwa na imani katika injili ya maji na Roho (1 Petro 3:21, Warumi sura ya 6, 1 Yohana sura ya 5).
Ni bahati mbaya kwamba makanisa ya Mungu katika Asia Ndogo walikuwa wameipoteza injili ya maji na Roho tangu katika wakati au kipindi cha Kanisa la Mwanzo, na kwa sababu hiyo eneo hili likaja kuwa la Waislamu. Zaidi ya yote, hata Kanisa la Rumi lilikumbwa na tatizo la kuipoteza injili ya maji na Roho baada ya kupitisha tamko la Milan lililotolewa na Kaisari wa Warumi aliyeitwa Konstatino.
 
Aya ya 6: “Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.”
Wanikolai walikuwa ni wale waliolitumia jina la Yesu kutafuta na kupata vitu vya kidunia. Lakini Kanisa la Efeso lilichukia mafundisho ya Wanikolai na matendo yao. Tendo hili la kuwachukia Wanikolai lilikuwa ni moja ya mambo ambayo Mungu aliyasifia katika Kanisa la Efeso.
 
Aya ya 7: “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.”
Watumishi na watakatifu wa Mungu ni lazima wasikie yale ambayo Roho Mtakatifu anawaambia. Kile ambacho Roho Mtakatifu anawaambia ni kuilinda na kuieneza injili ya maji na Roho hadi mwisho. Ili kufanya hivyo, ni lazima wapambane na kuwashinda wale wanaoueneza uongo. Kushindwa vita dhidi ya wanaoeneza uongo ni sawa na maangamizi. Waamini na watumishi wa Mungu ni lazima wawashinde adui zao kwa silaha zao—ambazo ni Neno la Mungu na injili ya maji na Roho.
Mungu alisema, “Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.” Mungu atatoa matunda ya mti wa uzima “kwa yeye atakayeshinda.” Lakini kushinda huko ni kumshinda nani au kukishinda kitu gani? Tunapaswa kuwashinda kwa imani wale ambao hawaamini katika injili ya maji na Roho. Waamini ni lazima wajihusishe katika vita ya kiroho inayoendelea kati yao na wale wasioieneza kweli, na ni lazima waamini wawe ndio washindi katika vita hizi kwa imani yao. Pia ni lazima wampatie Mungu utukufu wote na kisha waishi maisha ya ushindi kwa imani yao katika injili ya maji na Roho. Ni wale tu watakaowashinda adui zao kwa imani katika kweli ndio watakaoweza kuishi katika Mbingu na Nchi Mpya zinazotolewa na Mungu.
Katika kipindi cha Kanisa la Mwanzo, wale walioamini na kuilinda injili ya maji na Roho walikabiliana na kifo cha kuifia-dini. Vivyo hivyo, wakati muda utakapowadia, kutakuwa na wafia-dini wengi sana watakaojitokeza.