Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[2-4] Uwe Mwaminifu Hadi Kifo (Ufunuo 2:8-11)

(Ufunuo 2:8-11)
 
Wakati wa kipindi cha Kanisa la Mwanzo, Wakristo wengi walikuwa wakizunguka katika nchi wakitafuta mahali salama ambapo wangeliweza kuukwepa mkono wa mateso wa dola ya Rumi. Dola ya Rumi iliendeleza sera yake ya mateso hata baada ya kufa kwa Mfalme Nero, kwa kuwa Wakristo waliendelea kuyakiuka mamlaka ya mfalme. Watakatifu wa kwanza walipokea na kutambua mamlaka ya kidunia ya wafalme wa Kirumi, lakini walikataa kuyatambua mamlaka hayo walipotakiwa kuikana imani yao. Kwa kuwa walisimama kinyume na madai ya mamlaka ya kirumi, basi historia ya Kanisa la Mwanzo ilijazwa na mateso na mauaji ya kuifia-dini.
Ni lazima tujiulize ikiwa Neno la Ufunuo lina umuhimu wowote kwa waamini wa leo. Zaidi ya yote, Neno la Ufunuo liliandikwa takribani miaka elfu mbili iliyopita, si wakati wa sasa, na pia liliandikwa kwa makanisa saba ya Asia, na wala si kwetu. Je, neno kama hilo linawezaje kuwa na umuhimu kwetu?
Neno la Ufunuo ni muhimu kwa sababu ni Neno la Mungu linalotufunulia siri za mambo yatakayokuja baadaye. Ni lazima tutambue kuwa sasa tunaishi katika kipindi au wakati wa farasi mweusi ambao ni wakati wa tatu kati ya “nyakati nne za farasi” zinazoelezewa katika Ufunuo sura ya 6. Baada ya kupita nyakati za farasi mweupe na farasi mwekundu, kwa sasa tunaishi katika wakati wa mwishoni wa farasi mweusi. Hivi karibuni ulimwengu mzima utakabiliana na njaa kubwa, njaa ya kimwili na ya kiroho. Bila shaka ni muhimu kusema kuwa wakati huu wa njaa umeshafika. Mara wakati huu wa njaa utakapopita, yaani wakati wa farasi mweusi, basi utawasili wakati wa farasi wa kijivujivu.
Mihuri saba inayozungumziwa katika Ufunuo sura ya 6 ina maanisha kuwa wakati Mungu alipokuwa anaumba ulimwengu alipanga katika Kristo jumla ya nyakati saba. Wakati wa kwanza, yaani wakati wa farasi mweupe, ni wakati wa injili; wakati wa pili, yaani wakati wa farasi mwekundu, ni wakati Shetani ambapo Ibilisi analeta mkanganyiko mkuu duniani, anahamasisha vita, na kuendelea kulitesa kanisa la Mungu. Nyakati hizi zinafuatiwa na wakati wa farasi mweusi, wakati ambapo njaa ya kimwili na ya kiroho inauharibu ulimwengu. Wakati huu wa farasi mweusi ulishaanza kitambo
Wakati huu wa farasi mweusi utakapokwisha, wakati wa farasi wa kijivujivu utawadia ambapo Mpinga Kristo atainuka, na kisha mapigo ya matarumbeta saba yanayoelezewa katika Ufunuo sura ya 8 yataanza. Wakati tarumbeta la mwisho litakapopigwa, watakatifu watanyakuliwa na baada ya hapo yatafuata mapigo ya mabakuli saba. Kisha kutakuwa na karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo mawinguni kwa watakatifu wataokuwa wamenyakuliwa, na mara baada ya kuisha kwa mapigo ya mabakuli saba, Bwana atarudi duniani akiwa pamoja nasi na kuuanzisha Ufalme wa Milenia. Kisha Ufalme wa Mileni utafuatiwa na Mbingu na Nchi Mpya ambazo zitawatelemkia watakatifu ambao walikuwa wanaishi katika Ufalme wa Milenia baada ya ule ufufuo wao wa kwanza.
Kwa hiyo, vifungu vya maandiko katika Kitabu cha Ufunuo, kama vile “Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima,” na “Yeye ashindaye hatapatikana na mauti ya pili,” ni vifungu ambavyo ni muhimu sana kwetu. Kwa maneno mengine, Neno la Ufunuo ni la muhimu sana kwa Wakristo wanaoishi katika ulimwengu wa sasa. Kama kitabu cha Ufunuo kisingelikuwa na maana kwetu, basi Neno lote la Mungu lisingelikuwa na maana.
Mpango wa nyakati saba zinazofunuliwa katika Kitabu cha Ufunuo zinatekelezwa na kukamilishwa katika Kristo Bwana wetu. Wakati wa farasi wa kijivujivu utakapowadia, Mpinga Kristo atajitokeza. Tunahitaji kufahamu toka katika Neno la Mungu juu ya mpango ambao Mungu anao kwa ajili yetu katika wakati huo. Kwa kweli ni muhimu sana kwetu sote kufahamu toka katika Neno la Ufunuo jinsi Mungu alivyoupanga mpango wake mzima kwa ajili yetu na jinsi atakavyoutimiza mpango huo—yaani kufahamu kuwa ni mapigo gani yataushukia ulimwengu, mambo yatakayotokea kwa waamini, shida zitakazowapata wasio amini, n.k. Ni lazima ukubali na kuamini katika umuhimu wa Neno hili la ufunuo.
Pia ni lazima uwe na uelewa sahihi juu ya kile ambacho Kitabu cha Ufunuo kinazungumzia, kama vile miaka saba ya Dhiki Kuu na kuja kwa Kristo mara ya pili. Wakristo wengi wa siku hizi wanaamini katika fundisho la kiimani la kunyakuliwa kabla ya dhiki, fundisho ambalo lilionekana kwa mara ya kwanza huko Uingereza katika miaka ya 1830 na kisha likasambazwa na kufanywa kuwa mashuhuri na mwanazuoni aliyeitwa C. I Scofield, ambaye alikuwa ni Profesa katika Taasisi ya Biblia ya Moody.
Nadharia hii inadai kuwa kunyakuliwa kwa watakatifu kutatokea kabla ya miaka saba ya Dhiki Kuu kuanza. Kwa mtazamo huu, Wamataifa watanyakuliwa kwanza, na kisha Mungu ataanza kazi yake ya wokovu kwa watu wa Israeli. Pia kunyakuliwa kwa watakatifu kutakutangulia kuja kwa Mpinga Kristo na yale mapigo ya mabakuli saba.
Kwa ujumla, Wakristo wengi wanaamini ama katika nadharia ya amilenia [yaani kuwa hakuna utawala wa Milenia] au katika nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Lakini ukweli ni kuwa hizi ni nadharia tu ambazo zimejengwa kutokana na ufahamu duni wa Biblia. Badala ya kujibu maswali mengi ambayo watu wanayo kuhusu Kitabu cha Ufunuo, nadharia hizi zimeleta shida zaidi kuliko kuleta mema kwa kusababisha kutokea kwa maswali zaidi na mashaka kuhusiana na Neno la Ufunuo.
Ikiwa nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki ingelikuwa sahihi, basi Kitabu cha Ufunuo kingelikuwa na umuhimu gani kwa waamini wa Wamataifa? Dhiki Kuu na mfululizo wa matukio yaliyotabiriwa katika Ufunuo yangelikuwa hayana maana kwetu, kwa kuwa sisi sote tungelinyakuliwa kabla ya hayo yote. Hii ndiyo sababu watu wengi wanalichukulia Neno la Ufunuo kama sehemu ya udadisi kuliko imani.
Lakini ni lazima tutambue kuwa Neno la Ufunuo ni la muhimu sana kwetu tunaoishi katika ulimwengu wa sasa. Hebu nikuulize hili: Je, unaliamini Neno la Mungu? Au unayaamini maneno ya wanazuoni? Kuna nadharia nyingi sana kuhusiana na nyakati za mwisho kuanzia amilenia, kunyakuliwa baada ya Ufalme wa Milenia, kunyakuliwa kabla ya dhiki, kunyakuliwa katikati ya dhiki, na kadhalika. Nadharia hizi zinazopendekezwa na wanazuoni ni nadharia tete au nadharia zisizo na uhakika zinazotoa madai ya kudhania
Je, wewe unaiamini nadharia ipi kati ya hizi? Watu wengi wanasema kuwa wanaiamini nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki kwa sababu wamekuwa wakifundishwa na wachungaji wao hivyo. Lakini hebu nikueleza wazi na kwa uhakika: wewe na mimi tutayapitia mapigo ya matarumbeta saba na tutaishi katikati ya Dhiki Kuu. Kwa kuwa tumepangiwa kuipitia Dhiki Kuu, basi imani yetu ni lazima iwe ya kweli na imara itakayotuwezesha kuyashinda majaribu na mateso yanayotungojea.
Je, ni kitu gani kitatokea ikiwa ungelikuwa unaamini katika nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, hali ukijifikiria, “nitanyakuliwa kabla ya Dhiki Kuu; hivyo siwezi kujali kuhusiana na kipindi hicho,” halafu ukawa haujaiandaa imani yako kwa nyakati za mwisho? Wakati kipindi cha miaka saba ya Dhiki Kuu kitakapokuja kama Neno la Mungu linavyosema, wale wote ambao hawajaiandaa imani yao kwa ajili ya Mateso watajikuta katika mkanganyiko mkuu, wakiteseka, na pengine hata kufa—maana yake ni kuwa imani yao katika Yesu itaweza kutikiswa. Wengi wao hawataweza kuyashinda Mateso na kwa sababu hiyo wataishia kushindwa katika vita yao ya kiimani. 
Kabla ya kutokea kwa nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, Wakristo wengi walikuwa wakiamini kwamba wataipitia miaka yote saba ya Dhiki Kuu, na kwamba watanyakuliwa baada ya mateso hayo wakati Kristo atakaporudi kwa mara ya pili. Hali wakijua kuwa watapaswa kuipitia miaka saba ya mateso, Wakristo hao waliiandaa imani yao kwa nia hali wakiwa na uoga mkuu. Bila shaka kitendo cha kuyapitia mapigo yote bila shaka kilikuwa ni kitendo cha kuogopesha, kama ambavyo kinavyoweza kuwa kwa kila mtu yeyote. Lakini imani ya jinsi hiyo ilikuwa pia ni nadharia ya kitaaluma iliyotokana na kutolifahamu Neno la Mungu.
Kisha wapo wahafidhina wanaoamini juu ya amilenia. Watu hawa wanautazama Ufalme wa Milenia kama ni lugha ya picha. Wanautazama Ufalme huo kama ni lugha ya picha inayoonyesha jinsi Wakristo watakavyopata amani kwa kupitia wokovu wao. Ikiwa madai ya kitaaluma kama hayo yangelikuwa ni ya kweli, basi tusingelijali yanayotokea hapa ulimwenguni kwa maana sisi sote tungelipaishwa na Mungu mawinguni kabla ya Mateso kuanza.
Lakini ikiwa nadharia hizo zingelikuwa si za kweli, ni jambo gani basi ambalo lingelitokea? Kungelitoka suala la kukabiliana na Dhiki Kuu pasipo kuziandaa imani zetu, na katika hali kama hiyo tungelinyamazishwa na hofu ya kutojiandaa. Tusingeliweza kuilinda imani yetu, tungelisalimu mbele ya mawimbi ya majaribu na mateso, na hatimaye tungeliishia kuzolewa na mkondo ule ule ambao utauzoa ulimwengu. Lakini Mungu ametueleza kuwa wale ambao majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima—yaani wale ambao wamezaliwa tena upya kwa maji na Roho—hawatasalimu amri
Mungu anatueleza katika Neno lake la Ufunuo kuwa wale wanaozaliwa tena upya watayashinda majaribu na Dhiki Kuu kwa imani, na kwamba Bwana atawainua katikati ya haya Mateso na kuwapeleka mawinguni. Hivyo, nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki inapingana na ukweli huu, na kwa sababu hiyo madai hayo yanaonyesha kuwa ni yale yaliyoundwa na wanadamu. Kwa maneno mengine, madai hayo ni uongo na si ukweli. 
Pamoja na hayo kuna watu wengi sana ulimwenguni kote ambao wameipokea nadharia hii ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Wale wanaoyaamini mafundisho ya Scofiled ya kunyakuliwa kabla ya dhiki wanaamini kama ifuatavyo:
1. Miaka saba ya Dhiki Kuu itaanza baada ya kutokea kwa Mpinga Kristo katika nyakati za mwisho
2. Mpinga Kristo atautawala ulimwengu katika kipindi cha miaka saba ya Dhiki Kuu; katika miaka mitatu na nusu ya kwanza atatawala kama mtawala mkarimu, na nusu ya miaka hiyo atatawala kama dikteta mwovu.
3. Hekalu la Yerusalemu litajengwa upya na sadaka za kuteketezwa zitaanzishwa tena.
4. Mpinga Kristo atafanya agano la miaka saba na Israeli.
5. Baada ya miaka mitatu na nusu ya kwanza ya Dhiki, Mpinga Kristo atalivunja agano lile na Israeli. 
6. Miaka mitatu na nusu inayofuata itakuwa ni wakati wa Dhiki Kuu kwa Waisraeli. Katika kipindi hiki injili ya Ufalme wa Milenia itahubiriwa badala ya injili ya neema.
7. Watu 144,000 miongoni mwa Waisraeli watanusurika katika kipindi hicho cha dhiki.
8. Dhiki hiyo itaishia kwa kuwepo na vita ya Armagedonia
Baada ya kuwa ameielezea Dhiki Kuu kwa maneno hayo hapo juu, Scofield hakutaja lolote kuhusiana na yale ambayo yatatokea kwa Wamataifa katika kipindi cha Dhiki. Kwa maneno mengine, Scofield anadai kuwa Wamataifa wote ambao wanamwamini Kristo watanyakuliwa kabla ya kuanza kwa Mapigo, na kwamba ni baada ya kunyakuliwa kwao ndipo Mungu atakapoanza kufanya kazi miongoni mwa watu wa Israeli. Kazi ya Mungu itatimizwa kwa ukombozi wa Waisraeli 144,000 na kwamba kwa sababu hiyo ataikamilisha kazi yake ya wokovu. Kisha Ufalme wa Milenia utaanza.
Chanzo cha ushawishi kwa Scofield na madai yake juu ya kunyakuliwa kabla ya dhiki unatoka kwa John Nelsom Darby, mwanzilishi wa kundi linalojulikana kama Wandugu wa Plymouth, ambao walianza kuifafanua nadharia hii baada ya kukutana na kiongozi wa Kipentekosti. Kwa kweli kiongozi huyu alikuwa ni msichana mwenye umri wa miaka 15 aliyeitwa Margaret MacDonald wa Skotlandi, ambaye mwaka 1830 alidai kuwa alipata maono toka kwa Mungu ambapo aliona Wakristo wakinyakuliwa kabla ya Dhiki Kuu. Ni baada ya Darby kumtembelea msichana huyo ndipo alipoanza kufundisha nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki.
Mafundisho ya Darby yalikwenda baadaye kwa Scofield, ambaye ni mwanatheolojia wa Kimarekani. Scofield, ambaye alikuwa ameutumia muda wake mwingi wa maisha katika kuandika kamusi yake ya Biblia, kwa nyakati fulani alikuwa akitafakari ikiwa kunyakuliwa kutatokea kabla au baada ya Dhiki. Wakati Scofield alipoisikia nadharia ya Darby ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, basi aliipenda na akazama katika nadharia hiyo, na baada ya kuridhishwa na madai yake, basi aliichukua nadharia hii na kuiweka katika kamusi yake. Hivi ndivyo Scofield alivyofikia hatua ya kuamini na kuitetea nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, na hivi ndivyo Wakristo wengi wa leo walivyofikia hatua ya kuifuata nadharia hiyo.
Kabla nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki haijapanuliwa, Wakristo wengi walikuwa wakiamini juu ya kunyakuliwa baada ya dhiki. Lakini Scofield, ambaye alikuwa ni Profesa katika Taasisi ya Biblia ya Moody huko Marekani, alikuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya mafundisho ya kiimani, hasa kutokana na kamusi yake ya Biblia. Nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki ilienea na kuaminiwa na jamii nyingi za Kikristo kwa sababu ya ushawishi aliokuwa nao Scofield kwa jamii hizo.
Kwa bahati mbaya, na kwa matokeo hayo, Wakristo wengi siku hizi wamelala katika imani yao. Wamelala katika imani kwa sababu wanafikiri kuwa kuinuka kwa Mpinga Kristo hakutawaletea chochote. Hawaoni umuhimu wa kuiandaa imani yao kwa ajili ya wakati wa Dhiki Kuu, kwa sababu wanaamini kuwa watanyakuliwa kabla ya mateso kuanza. Lakini Bwana wetu ametueleza kuwa macho wakati wote, kwa kuwa hakuna anayefahamu saa ambapo bwana harusi atakuja. Hata hivyo, wale wasioliheshimu Neno la Mungu na badala yake wanaheshimu mafundisho ya kunyakuliwa kabla ya dhiki bado wapo katika usingizi mzito.
Lakini sasa ni wakati wa kuamka. Sasa ni wakati wako kuachilia mbali imani yako potofu ya kunyakuliwa kabla ya dhiki na kisha uliamini Neno la kweli. Nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki na nadharia ya kunyakuliwa baada ya dhiki hazina msingi wowote wa kibiblia; hivyo inakupasa urudi katika Neno la kweli la Mungu. Neno la Ufunuo (6:8) linatueleza kuwa, “Nikaona, na tazama farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.” 
Hapa inaelezwa kuwa jina la yeye aliyeketi juu ya farasi wa kijivujivu, ambaye ni Mpinga Kristo, alikuwa ni Mauti na kwamba Kuzimu alimfuata. Hii ina manisha kuwa Mpinga Kristo ni muuaji ambaye anawapeleka waathiriwa wake kuzimu. Pia andiko linasema kuwa atapewa mamlaka juu ya robo ya nchi ili kuua kwa upanga, kwa njaa, kwa kifo, na kwa hayawani wa nchi. Kwa meneno mengine, Mpinga Kristo atafanya manyanyaso na mauaji kama yale yaliyofanywa na watawala wa Kirumi—na kwamba wakati huu hali itakuwa mbaya zaidi kwa kuua, kudharirisha, na kuwatesa Wakristo na kuiharibu imani ya
Unapaswa kutambua kuwa wakati wa farasi wa kijivujivu ni wakati wa Mpinga Kristo. Bwana anatueleza kuwa, “Mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua? (Mathayo 16:3).” Tunaposhindwa kupambanua ishara za nyakati, basi hatuwezi kufahamu aina ya imani tunayopaswa kuwa nayo, na kwa sababu hiyo hatuwezi kupanda mbegu wala kuvuna matunda—kwa maneno mengine, hatuwezi kufanya kazi kwa ajili ya Bwana. Hivi sasa, wakati wa farasi mwekundu umepita na sasa tunaishi katika wakati wa farasi mweusi. Kwa sasa ulimwengu utakumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na utakabiliana na njaa kali. Njaa itaenea sana ulimwenguni kote. Baada ya mambo haya yote kupita, basi watu wengi watajuta kwa kuugua. Hivyo usiwe miongoni mwa hao watakaojuta na badala yake uwe mmoja wa wale ambao imani yao inaweza kuzitambua ishara za nyakati.
Wakati wa sasa ni wakati wa farasi mweusi. Wakati huu wa farasi mweusi utakapopita, wakati wa farasi wa kijivujivu utawadia. Mpinga Kristo ambaye atatokea katika wakati huu atawaua na kuwatesa watakatifu hali akiufanya wakati huu kuwa kama wakati wa kufia-dini.
Ufunuo 13:6-8 inasema, “Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa. Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.” Maelezo haya yanamzungumzia Mpinga Kristo. Kifungu hiki cha maandiko kinatueleza mmoja kati ya watawala wa dunia atapewa nguvu ya Shetani ili kumkufuru Mungu na kuwatesa watakatifu. Huyu ni mtoto wa Ibilisi akiwa na nguvu ya yule joka. Kwa mamlaka hii atapigana vita na kuwashinda watakatifu. Hii ina maanisha kuwa atawashinda kwa kuwaua huku wakiifia-dini. Hii pia ina maanisha kuwa ni kifo cha watakatifu cha kimwili kwa kuwa Mpinga Kristo hawezi kuichukua na kuiondoa imani ya watakatifu.
Kile ambacho Scofiled alikieleza ni kuwa watakatifu hawatakabiliana na Dhiki Kuu kabisa. Lakini ukweli ni kuwa pasipo uwepo wa miaka saba ya Dhiki Kuu, basi hakutakuwa na Ufalme wa Milenia kwa ajili ya watakatifu. Watakatifu watatoka katika Dhiki Kuu wakiwa kama wafia-dini. Unabii huu wa Biblia umepangwa ndani ya Kristo Yesu tangu mwanzo wa ulimwengu. Historia nzima ya ulimwengu itaishia katika kazi ambazo Kristo atazikamilisha.
Ni lazima uweze kuzitambua nyakati saba ambazo Mungu amezipanga kwa ajili yetu. Wakati wa kwanza ni wakati wa farasi mweupe, ambao ni wakati ambapo Neno la Mungu linaanza kufanya kazi yake. Wakati wa pili ni wakati wa farasi mwekundu, ambao ni wakati wa ibilisi. Wakati wa tatu wa farasi mweusi ni wakati wa njaa ya kimwili na ya kiroho. Wakati wa nne wa farasi wa kijivujivu ni wakati wa kuinuka kwa Mpinga Kristo. Huu ni wakati wa matarumbeta saba, na wakati wa mauaji ya kuifia-dini. Kushindwa kuutambua wakati wa farasi wa kijivujivu unawafanya watu wengi kuchanganyikiwa
Pasipo kuufahamu wakati huu, ni hakika kuwa hatuwezi kuyaishi maisha yetu kama Wakristo tuliozaliwa tena upya. Ikiwa tutakuwa hatuyafahamu yale yanayotungojea, tutawezaje basi kuwa tayari kwa ajili ya mambo ya baadaye? Hata watu wanaoendesha biashara, ili waweze kufanikiwa ni lazima wayafahamu mabadiliko na mwenendo wa wakati. Inawezekanaje kwa sisi waamini wa Kristo, kuwa tayari kwa ajili ya ujio wake ikiwa sisi wenyewe hatujui lolote kuhusiana na yale yanayotungojea?
Ni lazima tuwe na ufahamu mzuri juu ya Dhiki Kuu na kisha kuwa tayari kwa ajili ya mateso hayo. Watakatifu wataishi ndani ya miaka mitatu na nusu ya Dhiki, na ni katika kipindi hiki ndipo watakapouawa kwa kuifia-dini. Hawatakipitia kipindi chote cha miaka saba ya Dhiki, bali wataipitia nusu ya kwanza ya kipindi hicho, na kisha baada ya kuifia-dini watafufuliwa na kunyakuliwa. Watakatifu watakapokuwa wamenyakuliwa, hiyo haimanishi kuwa Bwana atashuka duniani, bali Bwana atawainua kwenda mawinguni katika karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo.
Wakati huo dunia hii itakuwa imeelemewa na mapigo ya mabakuli saba. Wale watakaorudi duniani pamoja na Kristo baada ya mateso ni wale tu ambao dhambi zao zimesamehewa na kuwa safi kama theluji kwa kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Hii ndio sababu ni lazima tuiandae imani yetu kwa kuufahamu wakati huu na umuhimu wake kwetu.
Bwana wetu alimwambia malaika wa Kanisa la Simirna kuwa, “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahaudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani. Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.” Kutokana na kifungu hiki tunaweza kuona kuwa Kanisa la Smirna liliteswa sana na Wayahudi. Lakini Bwana alisema kuwa hawa Wayahudi hawakuwa Wayahudi halisi bali ni sinagogi la Shetani. Bwana aliyasema haya si kwa Kanisa la Smirna tu, bali kwa makanisa yote ya Asia.
Kulikuwa na jamii kubwa ya Wayahudi huko Smirna ambao pamoja na ukweli kuwa walikuwa wakimwamini Mungu mmoja ambaye aliaubudiwa na Wakristo, hata hivyo Wayahudi hao waliwatesa watakatifu wa Kanisa la Smirna kama Warumi walivyofanya. Mungu aliwaambia watakatifu waliokuwa wakikabiliana na mateso haya kuwa, “Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima,” na “Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.” Mungu aliwaeleza watakatifu kuwa ni lazima washinde. Vivyo hivyo, sisi nasi, ni lazima tupambane na Mpinga Kristo hadi mwisho na kumshinda katika vita yetu ya kiimani. Ndipo Bwana wetu atakapotupatia taji ya uzima—kwa maneno mengine, atatubariki kwa kuturuhusu kuishi katika Ufalme wa Milenia na katika Mbingu na Nchi Mpya.
Je, una ujasiri wa kuuawa na kuifia-dini kwa ajili ya imani? Sasa ni wakati wako kuiandaa imani yako ya kuuawa kwa kuifia-dini. Na ili kufanya hivyo, ni lazima uwe na imani ya ukombozi inayokuwezesha kikamilifu kusimama mbele za Bwana—yaani imani inayoweza kupokea kuuawa kwa kuifia-dini pasipo kusita.
Ni lazima tuiandae imani hii sasa. Bwana wetu amemweleza kila mtu kuwa hakuna atakayeingia au kuuona Ufalme wa Mungu pasipo kuamini katika injili ya maji na Roho. Bwana ametueleza kuwa imani katika injili hii ni imani ya kuuawa na kuifia-dini katika nyakati za mwisho.
Kama kuna dhambi katika mioyo ya watu, itawezekanaje kwa watu kama hao kuuawa na kuifia-dini? Mbali na kuuawa kwa kuifia-dini, hao ni aina ya watu ambao watawaongoza wengine katika kuipokea alama ya Mnyama! Hakuna zaidi ya injili ya maji na Roho inayoweza kuzisafishilia mbali dhambi zetu. Hata yale maombi yako ya toba na taratibu nyingine za kiibada unazozifanya kila siku haziwezi kuzisafisha dhambi zako. Kitendo cha kujaribu kuzisafisha dhambi zako kwa maombi ya toba ni upotezaji wa muda na nguvu.
Wale wanaojaribu kufanya hivyo wanaamini zaidi katika yale ambayo watheolojia wamewaambia kuliko yale ambayo Neno la Mungu linawaambia. Je, kitendo cha wanazuoni, ambao wanaonekana kuwa ni wataalamu wa Biblia na wanaoaminiwa na Wakristo wengi, kudai na kuamini juu ya amilenia hakuonyeshi kuwa hawaifahamu Biblia? Kwa mujibu wa wafuasi wa amilenia, wao wanaamini kuwa hakutakuwa na Ufalme wa Milenia wala kuuawa kwa watakatifu kwa kuifia-dini katika kipindi cha Dhiki Kuu. Kwa wale wanaoamini katika nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki au amilenia, basi kwao Kitabu cha Ufunuo kitakuwa hakina maana yoyote ile!
Neno la Ufunuo ni Neno la Mungu. Ni Neno la Mungu lililoandikwa na Mtume Yohana, ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa Kristo aliyependwa kuliko wote. Hakuna anayeweza kulikana hili.
Sitoi changamoto kwa nadharia zilizopo na mafundisho ya kiimani ya watheolojia bila sababu, bali ninafanya hivyo kuiandaa imani yako ili uweze kuwa mwaminifu kwa Bwana hadi mwisho. Pia ninafanya hivyo ili kuwafundisha katika Neno la Maandiko ili uweze kuwa tayari kuyavumilia mateso ya wakati wa Dhiki Kuu hali ukiwa na utayari wa kuuawa kwa kuifia-dini.
Ili kufanya hivyo, ni lazima uiandae imani yako kwa injili ya maji na Roho sasa. Kwa upande mwingine, wale wasioamini katika injili ya maji na Roho watamtii Shetani na wataishia kuwa maadui wa Mungu, kwa kuwa wale ambao majina yao hayajaandikwa katika Kitabu cha Uzima watamwabudu Shetani. Hivi ndivyo Neno la Mungu linavyotueleza. 
Mungu atawafanya watakatifu kuuawa na kuifia-dini katikati ya kipindi cha Dhiki Kuu. Wakati miaka mitatu na nusu ya ile miaka saba ya Dhiki Kuu itakapopita, basi wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho watauawa kwa kuifia-dini. Mara baada ya kuuawa kwao kwa kuifia-dini utafuatia ufufuo na kunyakuliwa kwao. Huu ndio muhtasari mzima wa Kitabu cha Ufunuo na hii ndio sababu ninarudia rudia dondoo zake muhimu.
Unapaswa kukumbuka kuwa wakati wa Mpinga Kristo utakapowadia, kutakuwa na watu wengi ambao mara baada ya kuuawa na kuifia-dini kwa sababu ya injili ya maji na Roho watafufuliwa na kunyakuliwa kwa wakati huo huo. Wakati wa farasi wa kijivujivu utakapowadia, basi mauaji ya imani yatachanua kwa kuuawa na kuifia-dini. Mara wakati utakapowadia, imani ya kweli itazaa matunda ya kweli na itachanua maua mazuri
Kuna mimea fulani jangwani ambayo inachipua, inachanua, na kuzaa matunda kwa muda wa wiki moja. Hii ni kwa sababu imeizoea hali ya jangwani ambapo mvua ni hapa na maji ni adimu. Mimea hiyo ni lazima ichipue, ichanue, na kuzaa matunda haraka kwa kuwa ukosefu wa maji unaweza kudumu kwa muda mrefu
Imani ya wale watakaokuja kuamini katika injili ya maji na Roho katika kipindi cha miaka saba ya Dhiki Kuu ni kama mimea hii ya jangwani. Kwa watu kama hao watahitaji muda mfupi tu wa kuamini, kufuata, na kisha kuuawa kwa kuifia-dini pamoja nasi. Kucharuka kwa Mpinga Kristo kutafikia kilele chake katikati ya kipindi cha Dhiki Kuu, yaani miaka mitatu na nusu tangu kuanza kwa mateso hayo.
Hapo ndipo mauaji ya kuifia-dini ya watakatifu yatakapotokea. Hata wale ambao wamekwisha isikia injili ya maji na Roho lakini bado hawajaipokea katika mioyo yao wataweza kuipata imani ya kweli na kuungana nasi katika kuuawa kwetu kwa kuifia-dini ikiwa tu wataiamini injili hii wakati wa kipindi cha Mateso hata kama kitakuwa ni kifupi. Hii ndiyo sababu tunaieneza injili ili kuwaamsha Wakristo katika ulimwengu mzima toka katika usingizi wao wa kiroho. Tutaihubiri injili ya maji na Roho hadi mwisho wa ulimwengu hadi siku ile tutakapouawa kwa kuifia-dini. Kama kusingelikuwa na kuuawa kwa kuifia-dini basi injili hii tunayoieneza ingelikuwa na uzuri gani wa kuitumikia? Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wanaweza kuuawa kwa kuifia-dini katika nyakati za mwisho. Ni lazima tuiandae imani yetu sasa.
Ikiwa hatuiandai imani yetu sasa katika kuyapokea mauaji ya kuifia-dini, basi ni hakika kuwa tutakuja kujuta hapo baadaye. Wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, tutakuwa tumetingwa na mambo yetu binafsi na kusema, “Bwana, nimetingwa sana hivi sasa. Naomba uningojee kidogo; sasa ninatubu.” Ikiwa hii ndiyo aina ya imani ambayo tutaishikilia hadi siku ya mwisho basi Bwana atatuambia, “Kwa nini usirukie katika ziwa la moto wewe mwenyewe? Kwa kuwa unastahili kabisa kuingia humo!” Wale walio na dhambi hivi sasa ni lazima watambue kuwa watakuja kuishia kama hivyo. Hii ndiyo sababu Mungu alisema, “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”
Wakati ambapo watakatifu watakuwa wakiuawa kwa kuifia-dini, mazingira ya kiasili ya ulimwengu yatakuwa yameharibiwa kikamilifu. Misitu itakuwa imeungua; bahari, mito, na chemchemi zitakuwa zimegeuka na kuwa damu iliyooza; na jua, mwezi, na nyota zitakuwa zimepoteza mwanga wake na kusababisha ulimwengu mzima kuwa katika giza. Wakazi wake ambao watakuwa wakiongozwa na roho chafu watakuwa wamepoteza akili zao, tabia zao zitakuwa mbaya, na lengo lao litakuwa ni kuzunguka na kuwaua watoto wote wa Mungu watakaoweza kuwapata. Hii ndiyo sababu ni lazima ufahamu na kuamini katika Neno la Ufunuo.
Makanisa ya leo yametawaliwa na wazo la kujenga makanisa makubwa na marefu. Yanatumia mamilioni ya dola katika kuyajenga makanisa yao huku mioyo yao ikiwa imejawa na dhambi, na si imani inayoweza kuyakubali mauaji ya kuifia-dini kwa ajili ya Yesu. Watu hawa wanapaswa kwanza kuifanya mioyo yao kusafishwa toka katika dhambi zao.
Muda si mrefu ulimwengu utaingia katika kipindi cha Dhiki, yaani kipindi cha farasi wa kijivujivu. Ninatumaini kuwa utakuwa na aina ya imani inayoweza kuyapokea mauaji ya kuifia-dini na kubaki mwaminifu kwa Kristo hadi kifo. Tunapaswa kuamini katika Neno la Ufunuo baada ya kuwa tumelichunguza tukiwa na roho ya watu wa Beroya.