Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[2-8] Barua Kwa Kanisa la Thiatira (Ufunuo 2:18-29)

(Ufunuo 2:18-29) 
“Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana. Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake; nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine. Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja. Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa, naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyazi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu. Nami nitampa ile nyota ya asubuhi. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 18: “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana.”
Makosa ya Kanisa la Thiatira yalikuwa ni kuruhusu mafundisho ya Yezebeli kanisani. Yezebeli, aliyekuwa mke wa Mfalme Ahabu alileta ibada ya miungu katika Israeli na akawashawishi watu wake kufanya zinaa na kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu. Kwa kupitia yale maelezo yanayoonyesha kuwa Yesu ana “macho yake kama mwali wa moto,” Mungu anaonyesha kuwa atawakemea na kuwahukumu wale wote walio na imani potofu katika makanisa yake.
 
Aya ya 19: “Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza.”
Lakini kwa wakati huo huo, Mungu alimwambia mtumishi wake wa Kanisa la Thiatira na watakatifu wake kwamba matendo yao ya sasa yalikua ni mema kuliko yale ya kwanza.
 
Aya ya 20: “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.”
Tatizo la Kanisa la Thiatira ni kwamba liliyapokea mafundisho ya nabii wa kike wa uongo. Mioyo ya watakatifu wa Thiatira iliishia katika kuzifuata tamaa za miili yao kutokana na kitendo cha kuyaruhusu mafundisho ya kahaba Yezebeli aliyekuwa nabii wa uongo wa kike ndani ya kanisa na kwa kuyafuata mafundisho yake. Kwa sababu ya hilo, hasira ya Mungu inayotisha ilikuwa ikiwajia.
Kanisa la kweli la Mungu haliwaiti wale wasioamini katika injili ya maji na Roho kuwa ni watakatifu. Wala haliwaweki watu wasio na Roho Mtakatifu katika nafasi za uongozi wa kanisa. Kwa kuwa wale wasio na Roho Mtakatifu wanaufuata mwili na ulimwengu badala ya kumfuata Mungu, watu wa jinsi hiyo hawawezi kuruhusiwa ndani ya kanisa la Mungu.
 
Aya ya 21: “Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.”
Hii inatueleza kuwa wale walio wa mwili ambao hawajampokea Roho Mtakatifu hawawezi kumtambua na kuisikia sauti ya Roho Mtakatifu. Hii ndio sababu nabii wa kike wa uongo hakuweza kutubu toka katika zinaa yake. Kwa hiyo, nabii huyo alipigwa na upanga wa Roho Mtakatifu na akafa kimwili na kiroho.
Katika kanisa la kweli la Mungu, wanaoweza kutambuliwa kama watumishi wa kweli wa Mungu ni wale tu wanaoamini katika Neno la injili ya maji na Roho. Wale wasioamini katika injili ya maji na Roho, hata kama ni wachungaji kwa kiwango cha juu hapa duniani, ukweli ni kuwa hawawezi kuwa viongozi waaminifu wanaoweza kuwaongoza wana wa Mungu kwenda kwa Mungu. Hivyo ni lazima tuwatambue manabii wa uongo na kuwafukuza watoke katika makanisa yetu. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo kanisa la Mungu linapoweza kuihimili na kuing’amua mitego ya Shetani na kisha kumfuata Mungu kiroho.
 
Aya ya 22: “Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake”
Kifungu hiki cha maandiko kinatueleza kuwa ikiwa mtumishi wa Mungu hawezi kutambua na kuwang’amua waongo, basi Mungu mwenyewe atawatafuta wale wanaoabudu miungu kiroho na kuwatupa katika dhiki kuu. Watakatifu na watumishi wa Mungu ni lazima watambue kuwa Mungu mwenyewe ndiye anayeyaweka makanisa yake kuwa safi na kuyaongoza katika njia sahihi.
Katika kanisa la kweli la Mungu hakuna nafasi kwa manabii wa uongo. Kama kungelikuwa na manabii wa uongo, basi Mungu mwenyewe angeliwatafuta na kuwahukumu. Wakati manabii hawa wa uongo wanapoleta mkanganyiko kwa kanisa la Mungu, basi ni hakika kuwa Mungu atawaadhibu kwa dhiki kuu.
 
Aya ya 23: “nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.”
Mungu anawafukuzilia mbali manabii wa uongo toka katika kanisa lake ili kwamba kila mtu aweze kutambua kuwa Mungu analilinda kanisa lake. Watakatifu wanaweza kuona kuwa Mungu analitunza kanisa lake, na kwamba atawapa thawabu kwa matendo yao ya imani njema.
 
Aya ya 24: “Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.”
Kifungu hiki kina maanisha kuwa wale waliokwishafanyika kuwa watakatifu wa Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho ni lazima waishikilie imani yao hadi mwisho wa dunia. Wale wanaoamini katika injili hii hawana njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuyaishi maisha yao kwa kuiunganisha mioyo yao na kanisa na watakatifu wa Mungu na kisha kuilinda imani yao hadi mwisho. Kanisa la kweli la Mungu sio tu kwamba linapaswa kuihubiri injili ya maji na Roho tu, bali kanisa la kweli linapaswa pia kuwaumbua waongo kwa imani katika injili hii ya maji na Roho.
 
Aya ya 25: “Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja.”
Waamini hawapaswi kuipoteza imani yao katika injili ya maji na Roho na pia wanapaswa kuishikilia hadi siku ile Bwana atakaporudi. Katika injili yao ya maji na Roho kuna nguvu kubwa na mamlaka ambayo ni zaidi ya ile inayohitajika katika kumshinda Shetani. Watakatifu wanaweza kumpendeza Mungu kwa imani hii. Ikiwa watakatifu wanaishi kwa imani yao katika injili ya maji na Roho na kisha wakabakia katika kanisa la kweli la Mungu, basi wanaweza kuvumilia na kushinda katika nyakati za mwisho.
 
Aya ya 26: “Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,”
Watakatifu wanaweza kuwashinda adui zao wote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho ambayo Mungu amewapatia. Vita hii ya imani ni vita ambayo inatupatia ushindi wakati wote. Hivyo, wakatifu wote watapigana dhidi ya Mpinga Kristo na kisha kuuawa na kuifia-dini katika nyakati za mwisho, na kwa sababu hiyo watapewa nguvu ya kutawala pamoja na Bwana.
 
Aya ya 27: “Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyazi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.” 
Kama kifungu cha maandiko kinavyoeleza, Bwana atawapatia watakatifu waliouawa kwa kuifia-dini mamlaka yake ya kifalme. Hivyo, wale watakaoshinda watatawala wakiwa na uweza ambao una nguvu kama fimbo ya chuma ambayo inaweza kupondaponda vyombo vya mfinyanzi.
 
Aya ya 28: “Nami nitampa ile nyota ya subuhi.”
Wale wanaopigana dhidi ya maadui kwa kuaamini katika injili ya maji na Roho watapewa baraka ya kuutambua ukweli wa Neno la Mungu.
 
Aya ya 29: “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”
Watakatifu wote wanaweza kuisikia sauti ya Roho Mtakatifu akija kupitia kanisa la Mungu, hii ni kwa sababu Roho Mtakatifu anaongea na watakatifu wote kwa kupitia mtumishi wa Mungu. Watakatifu ni lazima watambue kuwa kile wanachokisikia kwa kupitia kanisa la Mungu ni sauti ya Mungu. 