Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[2-7] Wafuasi wa Fundisho la Imani ya Wanikolai (Ufunuo 2:12-17)

(Ufunuo 2:12-17)
 
 
Njia ya Balaamu
 
Hapa inaeleza kuwa miongoni mwa makanisa saba ya Asia, Kanisa la Pergamo lilikuwa na baadhi ya waamini walioyafuata mafundisho ya kiimani ya Wanikolai. Watu hawa walikuwa wametekwa na tamaa za kuujenga umashuhuri na utajiri wao, na hawakupenda kujishughulisha katika kuziokoa roho. Hivyo, watumishi wanapaswa kuwa makini ili kwamba wasije wakaishia katika kuyafuata mafundisho haya ya Balaamu. Balaamu aliwafanya watakatifu kuuabudu ulimwengu na kwa sababu hiyo aliwapelekea kupata maangamizi.
Mungu alitupatia Neno lake kwamba, wale watakaoshinda atawapatia mana iliyofichwa na jiwe jeupe. Kwa lugha nyingine, hii ina maanisha kuwa wachungaji wanaoufuata ulimwengu wataishia kuipoteza mana yao. Mana ina maanisha ni “Neno la Mungu,” na kuipoteza mana iliyofichwa maana yake ni kuyapoteza mapenzi ya Mungu ambayo yamefichika katika Neno la Mungu.
Wakati wa watumishi waliozaliwa tena upya wanapoufuata ulimwengu, basi ni hakika kuwa wanafikia hatua ya kupoteza mwelekeo wa Neno la Mungu. Hili ni tarajio la kutisha. Kwa kweli ninauogopa uwezekano huu na wewe pia unapaswa kuuogopa uwezekano huo. Mungu anatueleza kuwa wale watakaoshinda atawapatia mana iliyofichwa na jiwe jeupe, lakini wale watakaoshindwa na ulimwengu kwa kufanya mapatano nao na kwa kusalimu amri kwa umashuhuri na raha na starehe zake hawatapewa hii mana.
Biblia inatueleza kuwa, “nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.” Neno la Mungu ni la kweli! Wale wanaoupenda ulimwengu ni wale ambao hawajaokolewa toka katika dhambi zao kwa kutokuamini katika ubatizo wa Yesu Kristo na damu yake Msalabani. Watu hawa hawaufahamu ukweli kuwa Kristo amezisamehe dhambi zao zote kwa ubatizo wake.
Baadhi ya imani ya watu juu ya Yesu ipo katika uwanja wa kinadharia tu. Wao wanafikiri kuwa Yesu alizichukulia mbali dhambi zao, na kwa sababu hiyo wamefanywa kuwa wenye haki, lakini imani yao haina kitu kwa sababu hakuna Roho Mtakatifu katika mioyo yao. Imani ya jinsi hii ni imani ya kinadharia. Ikiwa mtu ameupokea ukombozi kwa kweli, basi mtu huyo ni lazima apambane na kuyashinda mambo ya ulimwengu—yaani mambo kama umashuhuri wa kidunia, heshima, utajiri, au mamlaka. Kuushinda ulimwengu maana yake ni kulishikilia Neno la Mungu ambalo limeturuhusu kuzaliwa tena upya, kupambana dhidi ya wale wanaofuata utajiri na heshima ya ulimwengu huu, na kisha kumhifadhi Roho Mtakatifu katika mioyo yetu.
Mungu anatueleza kuwa ataayaandika majina ya wale waliokombolewa na ambao Roho Mtakatifu anakaa ndani ya mioyo yao katika Kitabu cha Uzima. Kama Biblia inavyotueleza, “mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya,” wale waliozaliwa tena upya na walio na Roho Mtakatifu ndani ya mioyo yao wanafahamu kuwa hawako kama walivyokuwa hapo zamani. Wanatambua kuwa nafsi zao za kale sasa zimefanyika kuwa uumbaji mpya kwa kuamini katika maji na damu ya Yesu Kristo. Kwa imani yao hiyo wanafahamu kuwa majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima. Hivi ndivyo wanavyoweza kuiona mana ya Mungu iliyofichwa, na hivi ndivyo watumishi na watakatifu wa Mungu wanavyoweza kulisikia Neno la Mungu la kweli, ambayo ni sauti bora sana ya Mungu.
Mana ilitolewa kwa Waisraeli wakati walipokuwa wakizungukazunguka nyikani kwa miaka arobaini kabla ya kufika katika nchi ya ahadi ya Kanaani. Kwa mujibu wa maelezo ya Biblia, mana ilikuwa ni kama mbegu ndogo ya giligilani yenye umbo la duara. Wakati Waisraeli walipoamka asubuhi, ardhi iliyokuwa imewazunguka ilikuwa imefunikwa na mana, kana kwamba usiku uliopita kulikuwa na theluji. Kisha Waisraeli waliikusanya mana na kuila asubuhi. Huu ulikuwa ni mkate wao wa kila siku. Pengine waliikaanga, pengine waliichemsha; bila kujali, hiki kilikuwa ndicho chakula kikuu cha Waisraeli katika ile miaka 40 ya kutangatanga nyikani.
Kwa kuwa mana ilikuwa ndogo kama mbegu ya giligilani, basi mtu asingeliweza kushibishwa kwa kuila mana moja tu. Bali Mungu aliwapatia mana nyingi kila usiku ili kwamba mahitaji ya kila Mwisraeli yaweze kufikiwa kwa siku—yaani haikuwa mana isiyotosha kwa siku moja wala inayozidi kwa siku moja kwa maana mana haikuweza kuhifadhiwa. Lakini katika siku ya sita, Mungu aliwapatia mana ya kutosha itakayoweza kukaa kwa siku mbili, ili kwamba Waisraeli wasiweze kukusanya mana siku ya Sabato.
 

Mkate wa Uzima
 
Neno la Mungu ndiyo mana yetu, yaani mkate wa uzima. Katika Neno la Mungu kunapatikana mkate kwa ajili ya roho, ambao ni mkate wa uzima. Si kwamba utaweza kuuona mkate wa kawaida katika kifungu fulani cha maandiko, bali mapenzi makuu ya Mungu yanapatikana katika Maandiko yote, hata yale yanayoonekana kuwa ni madogo.
Kwenu watumishi na watakatifu wa Mungu, ni vema kufahamu kuwa Mungu hakufanya mapatano na ulimwengu huu, Mungu ametoa mkate wa uzima. Mungu anaendelea kutoa na kumpatia kila moja mkate wake wa kila siku ambao unayatosheleza mahitaji yetu ya kimwili na ya kiroho.
Kwa sababu ya uwepo wa mana hii, Waisraeli hawakupata njaa kamwe katika miaka 40 ya kutangatanga nyikani pamoja na kuwa jangwa halikuwapatia chochote kinachoweza kulika. Vivyo hivyo, kwa wale wanaoyakataa matendo ya Wanikolai, basi Mungu anawaahidia kuwa atawapatia mkate wake uliofichwa ili wale. Mungu anawapatia watumishi wake ambao hawayafuati mambo kama hayo ya utajiri na cheo Neno lake lililo bora sana, ambalo ni Neno la Uzima linalowaruhusu kuzaliwa tena upya kwa kupitia injili ya maji na Roho.
Ni lazima tuyachukie na kuyakataa matendo ya Wanikolai yaliyopo katika jamii za Kikristo leo hii. Hatupaswi kuifuta imani ya wale ambao hawajazaliwa tena upya, na ni lazima tukatae kuufuatisha ulimwengu huu. Ingawa ni sheria ya Mungu kuwa miili yetu inayafuata mambo ya mwili na roho zetu zinayafuata mambo ya Roho, ukweli ni kuwa tunapaswa kulikataa fundisho la kiimani la Wanikolai, tuyachukie matendo yote yanayoufuatisha ulimwengu, na badala yake tujilishe mana ya Mungu kwa kuamini katika Neno la kweli ambalo Mungu ametupatia. Sisi sote ni lazima tuishi kwa imani hali tukitambua kuwa sasa tumefanyika kuwa wenye haki na kwamba tuna Roho Mtakatifu anayekaa ndani ya mioyo yetu.
Waliozaliwa tena upya ni lazima wapambane na ulimwengu. Ni lazima wapambane na Wanikolai. Kama unavyofahamu vizuri, wachungaji wengi sana siku hizi wanaufuata utajiri na umashuhuri wao binafsi, wanajisifia wao wenyewe, wanaufuatisha ulimwengu, na wanajaribu kufanikiwa kwa njia za kidunia. Ni lazima tupambane na hawa manabii wa uongo.
Sisi pia tuna miili yetu, na kwa sababu hiyo tunatamani kuyafuata mapato ya kidunia. Lakini wale walio na Roho Mtakatifu ndani yao ni lazima wafahamu kuwa hawawezi kuufuta ulimwengu katika mioyo yao, na kwamba ni lazima wayakane mambo ya ulimwengu, na kwamba ni lazima waishi kwa imani. Ikiwa moyo wako unaungana na wale wanaoufuata ulimwengu, ukaithibitisha imani yao, na ukaufuata ulimwengu kama wanavyoufuata wao, basi utaishia kutembea katika njia ya Balaamu kuelekea katika maangamizi yako makuu. Hii ni njia itakayokupeleka katika maangamizi yako binafsi ya kimwili na kiroho. Unapoufuata ulimwengu, basi ni hakika kuwa utaipoteza imani yako. Mungu alisema kuwa atawatapika watu wa jinsi hiyo toka katika kinywa chake; watu hawa hawataila tena mana na wataishia kuipoteza imani yao kikamilifu.
Sababu iliyomfanya Mungu alikemee Kanisa la Pergamo ni kwa sababu waumini wake waliyafuata mafundisho ya Balaamu. Mungu alimkemea mtumishi wa Kanisa la Pergamo kwa sababu, pamoja na kuwa alikuwa ni mtumishi aliyezaliwa tena upya na ambaye moyo wake ulikaliwa na Roho Mtakatifu, ukweli ni kuwa alikuwa akitafuta kutambuliwa na ulimwengu na kwa sababu hiyo aliliongoza kanisa lake kana kwamba alikuwa ni mtu wa kidunia. Si hivyo tu, pia alilipanda fundisho hilo hilo potofu miongoni mwa waumini wake na akawapotosha. Mtumishi wa jinsi hiyo ni sawa tu na mchungaji wa kidunia ambaye hajazaliwa tena upya. Kwa kifungu hiki cha maandiko, Mungu ametoa onyo kali na la wazi kwa aina ya watumishi wa Mungu ambao matamanio yao yapo katika misingi ya mapato ya kidunia na kuongeza idadi ya viti vya kukalia kanisani: “Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.”
 

Imani Inayokuongoza Kwenda Katika Maangamizi 
 
Ni kitu gani kitakachotokea ikiwa mtu atapigana na Mungu? Kwa kweli hupaswi kufikiria hata kwa sekunde—maana kwa hakika hii itakuwa ndiyo njia rahisi ya mtu huyo kuelekea katika maangamizi yake. Kule kusema “yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili,” ina maanisha kuwa Neno la Mungu ni upanga wenye makali kuwili. Haijalishi kuwa wewe ni nani; ikiwa utakuwa umepigwa na Neno la Mungu, basi ni hakika kuwa utakufa. Neno la Mungu ni upanga wenye nguvu unaoweza “hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta” (Waebrania 4:12). Pia ni chanzo cha mtiririko wa fikra na nia ya moyo ili kwamba watu waweze kuvishwa katika ukombozi unaotolewa na maji na damu ya Kristo Yesu.
Kuna watu wengi ambao pamoja na kuwa wanamwamini Yesu wanaangukia katika mtego wa uanasheria, na kwa sababu hiyo Sheria inaishia kuwapiga hadi kifo. Ili kuepukana na matokeo haya ya kuhuzunisha, basi ni lazima tupambane na kuzishinda imani za jinsi hiyo za kidunia. Wafanyakazi wa Mungu ni lazima wayashinde mafundisho ya uongo, na pia ni lazima wahakikishe kuwa makundi yao hayadanganywi na uongo wa jinsi hiyo. Yeyote anayeupenda ulimwengu na kuangukia katika mitego yake ataiona imani yake ikitoweka.
Makanisa mengi ya leo yanaelezewa kama si makanisa bali ni kama biashara. Hali hii ni ya huzuni sana lakini ndio ukweli halisi. Ni kwa nini makanisa haya yamejikuta yakichukuliwa au kuelezewa kama biashara? Ni kwa sababu makanisa ya leo yametingwa sana katika kuufuata ulimwengu, yakiwa ndio ya kwanza yanayofuata na kuabudu vigezo vya kidunia. Sisemi kuwa wale waliozaliwa tena upya hawana kabisa tamaa za mwili. Ukweli ni kuwa hawa waamini waliozaliwa tena upya wana tamaa za mwili, lakini tamaa hii imefunikwa na imani yao. Wao hawayafuati mambo ya mwili kama wasioamini wanavyofuata tamaa zao za kimwili kwa mioyo yao yote.
Wale ambao hawajazaliwa tena upya wanajiwekea viwango vyao binafsi, na wanaishi maisha yao hali wakifurahia kila kitu wanachoweza kukifanya ndani ya viwango hivyo walivyojiwekea. Kuabudu sanamu na uzinzi ni mambo ya kawaida kwao. Mbaya zaidi, baadhi yao wanadiriki hata kumwabudu Ibilisi. Je, waliozaliwa tena upya wanaweza kufanya mambo kama haya? Kwa kweli hapana! Hawawezi kufanya mambo kama hayo kwa sababu waliozaliwa tena upya wanaelewa jinsi matendo haya yalivyo machafu. Kwa kuwa sisi tuliozaliwa tena upya tupo tofauti sana kimsingi na wale wanaoufuata utukufu wa dunia hii na kila tamaa ya mwili, basi hatupaswi kuishi maisha yetu yakiwa yamegubikwa na mapito ya kidunia, na wala hatuwezi kuishi hivyo.
Wale wanaoyafuata matendo ya Wanikolai ni wale wanaoufuata utajiri wa dunia tu. Kwa kweli hakuna ubaya mtu anapojaribu kujipatia mahitaji ya maisha au anapojaribu kuwa tajiri. Lakini inapotokea kuwa lengo kuu la maisha yako ni kujilimbikizia mali na kuangukia katika kuabudu sanamu, basi ni hakika kuwa imani yako itaharibiwa. Wale wanaohudumu kwa ajili ya fedha na wale wanaokwenda kanisani kwa ajili ya utajiri wa kidunia basi ni vema wajue kuwa wanayafuata matendo ya Wanikolai. Watu hawa mwishoni watashindwa na ulimwengu kwa sababu pamoja na kudai kuwa wanamwamini Mungu, ukweli ni kuwa mioyo yao bado haijakombolewa kikamilifu toka katika dhambi zao zote.
 

Aina Nne za Uwanja wa Moyo
 
Injili ya Mathayo inatueleza mfano ambao Yesu aliuzungumza kuhusiana na mpanzi ambaye mbegu zake zilianguka katika udongo au viwanja vya aina nne tofauti. Kiwanja cha kwanza ambapo mbegu ziliangukia ilikuwa ni njiani; na cha pili ilikuwa ni kwenye mwamba; na cha tatu ilikuwa ni ardhi yenye miiba na vichaka; na cha nne kilikuwa ni udongo mzuri. Hebu tuangalie kila aina ya kiwanja au udongo.
Njiani au njia ina maanisha kuwa ni mioyo migumu. Mtu huyu analisikia Neno la Mungu, lakini kwa kuwa halipokei Neno hilo kwa haraka katika moyo wake, basi mbegu hizo zinanyakuliwa kwa haraka sana na ndege. Kwa maneno mengine, kwa kuwa mtu huyo analiangalia Neno la wokovu linaloweza kumruhusu kuzaliwa tena upya kwa maji na Roho kiakili, basi ndege (Shetani) analinyakua hilo Neno na kwa sababu hiyo imani ya mtu huyo haianzi hata kule kuota.
Je, mahali penye mwamba ni mahali gani? Hii ina maanisha ni wale ambao pamoja na kuwa wamelipokea Neno kwa furaha, hawawezi kudumu sana kwa kuwa hawana mizizi katika udongo mzuri. Kwa upande mwingine, wale ambao wanazipokea mbegu hali wakiwa katikati ya miiba na vichaka ina maanisha ni wale wanaoujali ulimwengu huu na udanganyifu wa mali na utajiri vinalisonga Neno ambalo wamelipokea kwa furaha pale mwanzoni.
Mwisho, wale wanaozipokea mbegu katika udongo mzuri ni wale ambao wanazaa matunda katika mioyo yao kwa kulipokea Neno la Mungu kikamilifu na kulifuata.
Je, katika viwanja hivi ni kiwanja kipi kinachouwakilisha moyo wako? Ikiwa moyo wako upo kama njia ambayo haijaandaliwa kabisa ili kuifanya mbegu ya Neno kukua, basi ni hakika kuwa mbegu hiyo itanyakuliwa na ndege, na kwa sababu hiyo baraka za Neno hili zitakuwa hazina maana kabisa kwako. Ni lazima tutambue kwamba, kwa kuwa sisi ni mbegu ya dhambi, basi kama isingelikuwa Neno la Mungu, basi tungelibakia kuwa tusio na maana kabisa mbele za Mungu. Kwa upande mwingine, ikiwa mioyo yetu ni kama uwanja au udongo wenye mwamba, basi ni hakika kuwa mbegu ya Neno haiwezi kupata mizizi na kwa sababu hiyo haliwezi kuhimili dhoruba ya mvua, upepo, au ukame. Watu wa jinsi hii wanatakiwa kuvibadilisha viwanja vyao. Haijalishi jinsi wanavyoweza kuwa wamelipokea Neno la Mungu kwa furaha mwanzani, ukweli ni kuwa kama Neno hilo lisipoweza kukua na kisha likanyauka wakati wa shida ndogo, basi ni wazi kuwa kule kulipokea kwao Neno la Mungu mwanzoni hakukuwa na hakuna maana yoyote.
Pia ni lazima tuishinde mioyo ya udongo au uwanja wenye miiba na vichaka. Ni lazima tupambane na kuikata miiba na vichaka vinavyotishia maisha yetu. Ikiwa tutaviachiliza vichaka na miiba, basi ni hakika kuwa miiba itakua na kutuzuia tusiweze kupata mwanga wa jua. Ikiwa tutazuiliwa mwanga wa jua na kisha kupoteza virutubisho vya ardhini kwa kunyonywa na miiba, basi ni dhahiri kuwa mti huu wa Neno utakufa baadaye.
Tunapokabiliana na majaribu na dhiki katika maisha yetu, basi ni lazima tuyashinde majaribu hayo kwa ujasiri. Ni lazima tupambane na miiba inayoizuia njia yetu inayoziziba nyuso zetu kwa nguvu zetu zote, tufanye hivyo kana kwamba maisha yetu yanategemea sana mwanga huo. Wakati fedha za dunia hii zinapoturudisha nyuma au wakati umashuhuri wa fedha hizo unapotutishia, basi ni lazima tupambane na kuyashinda hayo yote. Kwa kuwa mashaka ya dunia na tamaa zake ni mambo yanayoleta mauti kwa nafsi na roho, basi ni lazima tuyashinde. Tunapoishi maisha kama hayo ya kiroho ya ushindi, basi miili na nafsi zetu zitafanikiwa, kwa kuwa zitapokea mwanga wa jua na virutubisho toka kwa Mungu.
Kwa watakatifu na watumishi wa Mungu waliozaliwa tena upya ni lazima tuwe na vita ya kiroho dhidi ya ulimwengu wakati wote. Hivyo hatupaswi kuwafuatisha Wanikolai. Wanikolai walisemekana kujihusisha na utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii. Lakini kazi ya msingi ya kanisa si kuitumikia jamii. Itakuwa ni makosa makubwa kufikiri kuwa kazi ya msingi ya kanisa ni kutoa huduma za jamii.
 

Kataa Kwa Ujasiri!
 
Mungu anatueleza kuwa sisi ni chumvi ya dunia hii. Je, Mungu ana maanisha nini anaposema hivyo? Wakati Mungu anapotuambia kuwa sisi ni chumvi ya dunia, ina maanisha kuwa sisi tunahitajika na ulimwengu. Jukumu la chumvi ni kulihubiri Neno la maji na damu ya Kristo kwa kwenye dhambi ili kwamba waweze kukombolewa toka katika dhambi zao, na kufanywa wana wa Mungu, na kisha kuruhusiwa kuingia Mbinguni. Kama ambavyo chumvi inahitajika katika kutupatia radha, ulimwengu huu unawahitaji wenye haki waliozaliwa tena upya kama radha yao. Wenye haki waliozaliwa tena upya ni lazima walihubiri Neno la maji na Roho na kuwaongoza watu kuelekea katika ukombozi wao. Ni lazima tulitimize jukumu hili la chumvi na kuzisaidia nafsi ili ziweze kuzaliwa tena upya. Ni lazima tuwageuze wenye dhambi kuwa wenye haki.
Je, kanisa la kweli la Mungu ni lipi? Kanisa la kweli la Mungu ni mahali ambapo watu wanakusanyika ili kumwabudu Mungu; ni mahali ambapo wanamsifu Mungu; na ni mahali ambapo wanamwomba Mungu. Wakati majaribu yanapokuja, watumishi wa Mungu ni lazima wawe tayari kuyazuia. Pia watakatifu ni lazima waweze kuyazuia majaribu ya ulimwengu yanayokuja toka kwa Shetani. Ibilisi anaweza kukujaribu akisema, “Sahau imani yako; nitakufanya uwe tajiri! Hupaswi kuhudhuria kanisa la waliozaliwa tena upya; njoo kwenye moja ya makanisa yangu, na nitakufanya hata uwe mzee wa kanisa!” Lakini kwa kuwa Shetani anajaribu kuwafanya watu wakati wote kujikwaa na kisha kuwapeleka katika mitego yake, basi ni lazima tuwe tayari kupambana naye na kumshinda ili tuweze kuilinda imani yetu hadi mwisho.
Mara nyingi wale walio na imani potofu wanajaribu kuwatega na kuwajaribu waliokombolewa kwa vitu mbalimbali. Wanawajaribu kwa fedha na umashuhuri. Shetani anatuonyesha viwango vya kidunia na anatueleza kuiacha imani yetu katika Mungu. Tunachopaswa kuwa nacho katika nyakati kama hizo ni imani katika Bwana kwamba atatupatia mahitaji yetu yote, na kwa imani hii tunaweza kukataa kwa ujasiri na kuyashinda majaribu ya Shetani.
Mzizi wa baraka unapatikana katika Mungu. Mungu ndiye anayetubariki kiroho na kimwili. Kwa kuwa tunafahamu kuwa Ibilisi hambariki mwanadamu, basi ni hakika kuwa tunaweza kupambana dhidi yake. Pia kuna nyakati ambapo tunapambana na matamanio yetu binafsi. Wakati tamaa na choyo inapoanza kuonekana hasa pale tunapoiruhusu mioyo yetu kuchukuliwa na mkondo wa dunia hii, basi huo ni wakati ambapo tunapaswa kupambana na nafsi zetu. Pia ni lazima tupambane na watu wa kidunia ambao wanajaribu kuiteka imani yetu. Tumepangiwa kupigana vita vya kiroho dhidi ya nguvu zote za kidunia.
Kwa nini tupigane vita vya kiroho? Kwa sababu ikiwa Mkristo hatashiriki katika vita vya kiroho, hii itamaanisha kuwa imani ya Mkristo huyo imekufa. Ni vema kufahamu kuwa kutaendelea kuwa na hila ya kuiharibu imani yetu hadi siku ile hukumu ya wenye haki na wenye dhambi itakapoisha, yaani siku ulimwengu utakapofikia mwisho. Hii ndiyo sababu tunapaswa kushiriki katika vita vya kiroho bila kukoma. Ikiwa tutawavumilia wale wanaosimama kinyume na Mungu na kujaribu kuiharibu imani yetu, basi ni hakika kuwa tutaishia tukipoteza kila kitu hadi uhai wetu. Pasipo kuwa na nia thabiti ya kutoruhusu kitu kingine chochote zaidi ya imani yetu kututawala, basi ni hakika kuwa hatutapoteza tulivyonavyo tu, bali tutakataliwa pia na Mungu. Ni lazima tuweze kumtambua yule anayesimama pamoja nasi na yule asiyesimama nasi ili tuweze kupambana na kuwashinda adui zetu. Hali tukiwa na mioyo ya kusaidiana sisi kwa sisi, basi ni lazima tusimame kidete dhidi ya maadui zetu—hadi ifikie mahali ambapo hawawezi kujaribu chochote juu yetu.
Wanikolai ni maadui zetu. Ni maadui zetu kwa sababu wao ni “sinagogi la Shetani” ambao hatuwezi kuwavumilia wala kufanya nao kazi pamoja. Sisi ambao tumesamehewa dhambi zetu hatupaswi kuwavumilia Wanikolai ambao wanashiriki katika kuabudu sanamu na ambao wanatafuta kupata mali tu, badala yake tunapaswa kujitoa katika kumtumikia Bwana na kazi yake ya haki ya kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani.
 

Utafuteni Kwanza Ufalme wa Mungu
 
Yesu alituambia “kuutafuta kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake,” hali akitutia moyo kuzifanya kazi za Mungu kwanza badala ya kazi za mwili. Sisi tuliozaliwa tena upya tuna matamanio ya kiroho. Matamanio haya si matamanio ya kimwili, bali ni matamanio ya Roho. Hivi ndivyo tunavyoweza kwanza kuzitumikia kazi za Mungu na Ufalme wake. Sisi tunamtumikia Mungu kwanza, lakini pia tunazifanya kazi za mwili. Kama Biblia inavyotueleza, “Mwanadamu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Kwa maneno mengine, sisi hatuishi kwa miili yetu tu, bali kwa miili na roho. Ni lazima tuweze kuweka mlinganyo kati ya mambo haya mawili. Ikiwa tutayafuata matendo ya Wanikolai hali tukifikiri kuwa suala la msingi ni furaha yetu hapa duniani, basi ni hakika kuwa tutaishia kupambana na maangamizi yetu binafsi. Hii ndiyo sababu kuwa tunapaswa kuyatafuta kwanza matamanio ya kiroho.
Baadhi ya watu wanachukia sana wakati mada ya Mbinguni na kuzimu inapozungumziwa. Wao huuliza, “Umewahi kufika kuzimu? Je, umeiona kuzimu kwa macho yako binafsi?” Lakini maswali haya yanatoka katika mawazo ya kishetani. Hiyo haipatikani kwa watu wa kawaida kama hawa, bali hata kwa wachungaji wengi ambao wametumia muda mwingi wakisomea theolojia na huku wakihudumia makundi yao huku wakiwa hawana uhakika juu ya Mbinguni na ufahamu wa kuzaliwa tena upya. Kwa kweli hii ni bahati mbaya sana na hali mbaya kwa jumla, kwa kuwa watumishi wasioamini hivyo na ambao hawajazaliwa tena upya hawawezi kuwaongoza wale wasiojua chochote kuweza kuzaliwa tena upya. Wakati nafsi nyingi zinapokuwa zimefungwa katika mawazo ya Shetani na kusimama kinyume dhidi ya Mungu, inawezekanaje kwa nafsi hizo kujifunza toka kwa wachungaji wao ambao hawafahamu wala hawaamini juu ya Mbingu na wasio na uhakika juu ya wokovu wao?
Kule kusema “penye kiti cha enzi cha Shetani,” ina maanisha kuwa Shetani sasa anatawala juu ya ulimwengu wote. Kipindi hiki tunachoishi ni kipindi ambacho ulimwengu umejazwa na Wanikolai ambao wanauangazia ulimwengu usiku kwa misalaba inayowaka na wanayaendesha makanisa yao kana kwamba wanaendesha biashara. Mungu ametueleza kuwa haya si makanisa yake bali ni “masinagogi ya Shetani.” Ulimwengu wa leo umejawa na watu wengi sana waliokamatwa na mawazo ya Shetani na ambao wanafuatilia tamaa za ulimwengu huu hali wakijifanya kuhudumu, kuhudhuria kanisani, na kuliitia jina la Bwana. Hata hivyo, kule kuzaliwa tena kwa nafsi zao na tumaini lao la Mbinguni yametoweka muda mrefu uliopita. Sasa tunaishi na kumtumikia Bwana katika ulimwengu wa aina hii.
 

Vita ya Kiroho Dhidi ya Wale Ambao Hawajazaliwa Tena Upya
 
Tunaishi hapa duniani mahali ambapo “ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani.” Ni lazima tuilinde imani yetu na kuwa tayari kukabiliana na adui anapoleta changamoto. Ni lazima tulilinde na kulitunza “jiwe jeupe” kwa uangalifu hadi siku ile Bwana wetu atakaporudi—yaani kulilinda jiwe jeupe kwa kuamini katika injili ambayo imeturuhusu kuzaliwa tena upya kwa maji na damu.
Ni lazima tuishi kwa kula mana, ambayo ni Neno la Mungu. Ili kufanya hivyo, ni lazima tupambane na kuyashinda matendo ya Wanikolai. Ni lazima tuwakatae. Hatupaswi kuwa karibu na wale wanaotafuta fedha na umashuhuri wa duniani tu. Ingawa tunaweza kuvumilia na kuusamehe udhaifu wao, ukweli ni kuwa hatuwezi kuuvunja mkate na wale wanaosimama kinyume dhidi ya ukweli na wenye tamaa kwa fedha tu na kisha kufanya kazi ya Mungu pamoja nao.
Je, majina ya wale waliozaliwa tena upya kwa kuamini katika injili ya maji na Roho yameandikwa wapi? Majina hayo yameandikwa katika Kitabu cha Uzima. Je, kule kuandikwa kwa jina katika jiwe jeupe kuna maanisha nini? Kuna maanisha kuwa tumefanyika kuwa watoto wa Mungu. Pia imeandikwa kuwa hakuna anayelifahamu hili jina jipya isipokuwa “yeye anayelipokea.” Hii ina maanisha kuwa hakuna mwingine anayeufamu wokovu wa Yesu zaidi ya wale waliozaliwa tena upya katika injili ya maji na Roho. Wenye dhambi hawafahamu jinsi wanavyoweza kufanywa kuwa wenye haki—maana yake ni kuwa ni wale tu walioyapata majina yao mapya toka kwa Yesu ndio wanaofahamu jinsi dhambi zao zilivyotoweshwa.
Ni lazima tupambane dhidi ya Wanikolai; na si dhidi ya mtu fulani, bali ni dhidi ya Wanikolai. Kiini cha kifungu hiki cha maandiko ni kwamba ni lazima tupambane na kuwashinda Wanikolai ambao pamoja na kuwa wanamwamini Mungu na kulifahamu Neno la kweli bado wanaendelea kutolitii na kulikataa Neno la Mungu na kufuata masuala ya fedha, mali, utajiri, umashuhuri, na miili yao tu.
Pia ni lazima tupambane dhidi ya nafsi zetu wenyewe. Ikiwa hatuwezi kumfuata Mungu kwa sababu ya majivuno yetu, basi ni lazima tupambane na mioyo yetu. Pia ni lazima tushiriki katika vita vya kiroho dhidi ya wale wanaodai kumwamini Yesu bila kuzaliwa tena upya.
Pamoja na ukweli kuwa tunapungukiwa na utukufu wa Mungu, Bwana ametuokoa kwa maji na damu yake. Ni lazima tuilinde imani yetu kwa kuamini katika Neno hili na kisha kuishi maisha yetu kama watumishi wa Mungu, hali tukimtolea shukrani Mungu kwa wokovu wake mkamilifu ambao ametupatia. Ni lazima tuutafute kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake. Hebu sisi sote tuwe wale wanaoshinda kwa kupambana hadi mwisho katika imani.
 

Wale Watakoshinda Watapewa Mana
 
Kesi kubwa ya kutoweka katika historia ya mwanadamu itakuwa ni kunyakuliwa kunakokuja. Kwa wakati huo huo, kuja kwa Yesu mara pili ni jambo ambalo linavuta shauku ya watu wengi kwa wale wote wanaomwamini Kristo. Baadhi ya watu wanafikiri, “Bila shaka watu wengi sana watatoweka wakati watakatifu watakaponyakuliwa; kwa kuwa watu toka katika kada zote za kimaisha watatoweka, kuanzia marubani hadi makondakta wa treni, hadi waendesha teksii, bila shaka ulimwengu utakumbwa na aina mbalimbali za ajali, huku ndege zikianguka toka juu, treni zikiacha reli, huku barabara ikiwa imejazwa na ajali za magari.” Kitabu ambacho kilikuwa kimepewa jina la Kunyakuliwa kiliwahi kuwa ndicho kinachoongoza kwa mauzo hapo zamani. Watu hawa waliamini kuwa watakatifu watakaponyakuliwa watatowekea mawinguni. Hivyo, sio tu kwamba watu walitubu na kuyaandaa maisha yao kwa ajili ya siku ya kunyakuliwa kwao, bali baadhi yao walidiriki hata kuacha shule na kuacha ajira zao, kwa kweli hali hii ilikuwa ni ya kuchekesha.
Ni muda mfupi tu uliopita, dhehebu moja ambalo linakumbatia fundisho la kiimani la kunyakuliwa kabla ya dhiki liliwafanya waumini wake kutoa mali zao zote kwa kanisa na kisha kungojea siku ya kunyakuliwa kwao ambayo viongozi wa dhehebu hilo walikuwa wameitabiri. Kwa kweli siku ambayo ilitabiriwa na viongozi hao na ambayo ilingojewa sana iliwadia na ikaisha na kupita kama siku nyingine zinavyopita—yaani walingojea bure tu! Kila kitu ambacho walikiamini kwa uaminifu wote na ambacho walikingojea sana kilithibitishwa kuwa ni uongo.
Lakini baadhi yao waliitangaza kwa nguvu sana siku nyingine katika mwaka 1999 kuwa ndiyo siku ya kunyakuliwa kwao, na wakaisubiri sana. Hata hivyo, kama ilivyokuwa mwanzo, wao nao walithibitisha kuwa walikuwa wamedanganywa na waongo. Hali wakiwa wametiwa katika aibu kwa unabii wao ambao haukutimia, basi waliamua kutoweka au kutaja muda tena wa kurudi kwa Kristo. Tunaweza kuona katika matukio haya jinsi fundisho la kunyakuliwa kabla ya dhiki lisivyopatana na Neno la Mungu kabisa.
Moja ya jambo muhimu sana katika Kitabu cha Ufunuo ni kurudi kwa Yesu mara ya pili na kunyakuliwa kwa watakatifu. Kwa wale Wakristo wote waaminifu, tumaini la kweli na kulingonjea ni wakati Kristo atakapokuja hapa ulimwenguni na kuwachukua waamini wake kwenda mawinguni. Kwa kweli, ni muhimu sana kwa Wakristo kusubiri kwa nguvu ujio wa Kristo katika imani yao. Yeyote anayeamini katika Yesu ni lazima aisubiri siku ya kurudi kwa Bwana kwa matarajio makubwa.
Ni vema kuwa na aina ya imani inayosubiri kuja kwa Bwana mara ya pili na kunyakuliwa kuliko kuwa na imani isiyo amini katika hayo. Kile ambacho watabiri wa mambo ya baadaye walikikosea na kutoka katika njia sahihi ni kule kutenga siku maalum na wakati wa kunyakuliwa. Wengi kati ya hawa watabiri walitumia kuhesabu yale majuma sabini yanayotajwa katika Daniel sura ya 9, pia katika Zakaria kama msingi wa kufanyia mahesabu yao ambayo ndiyo yaliyowapatia tarehe ambazo walizitabiri.
Katika 1 Wathesalonike sura ya 4 kuwa wakati Kristo atakaporudi hapa duniani, watakatifu watanyakuliwa mawinguni ili kukutana na Bwana. Hivyo ni sahihi kwamba wale wote wanaomwamini Yesu ni vema waendelee kuisubiri siku ya kunyakuliwa kwao. Lakini kitendo cha kupiga mahesabu na kupanga au kutaja siku au tarehe maalum ya kunyakuliwa ni kitu ambacho si sahihi kabisa, kwa kuwa huo ulikuwa ni udhihirisho wa jinsi wanavyoidharau hekima ya Mungu. Ilikuwa ni makosa kabisa kujaribu kufanya hesabu na kuufahamu unabii wa Biblia kwa kutumia kanuni za mahesabu zilizoundwa na wanadamu.
Sasa, ni wakati gani ambapo kunyakuliwa kutatokea? Ufunuo sura ya 6 inaeleza juu ya kunyakuliwa kwa watakatifu; kwa mujibu wa sura hiyo, kunyakuliwa kutatokea katika wakati wa nne wa farasi wa kijivujivu ambapo kutakuwa na mauaji ya kuifia-dini, na mara baada ya mauaji hayo ndipo kunyakuliwa kutakapofuata katika wakati wa tano kati ya zile nyakati saba. Kunyakuliwa kwa watakatifu kunaelezewa kwa kina na kutatokea kiuhalisia wakati utakapowadia.
Mungu amezipanga nyakati saba kwa mwanadamu, wakati wa kwanza ni wa farasi mweupe. Huu ni wakati ambapo injili ya maji na Roho inaanza na kuendelea kushinda. Wakati wa pili ni wa farasi mwekundu. Wakati huu ni ishara ya kuanza kwa kipindi cha Shetani. Wakati wa tatu ni wa farasi mweusi ambapo ulimwengu utakumbwa na njaa ya kimwili na njaa ya kiroho. Wakati wa nne ni wakati wa farasi wa kijivujivu. Huu ni wakati ambapo Mpinga Kristo atainuka na watakatifu watauawa kwa kuifia-dini. Wakati wa tano ni kipindi ambacho watakatifu watafufuliwa na kunyakuliwa baada ya mauaji yao ya kuifia-dini. Wakati wa sita unahusisha maangamizi kamili ya uumbaji wa kwanza—yaani ulimwengu huu ulioumbwa na Mungu, na baada ya hapo utafuata wakati wa saba ambapo Mungu atauanzisha Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya ili aweze kuishi na watakatifu wake milele. Hivyo, Mungu amevipanga hivi vipindi saba tofauti kwa wanadamu wote. Hivyo ni vema kwa wale wote wanaomwamini Yesu kufahamu na kuziamini hizi nyakati saba ambazo Mungu amezipanga kwa ajili yao.
Inakadiriwa kuwa mwishoni mwa karne iliyopita hapa Korea peke yake kulikuwa na watu zaidi ya 100,000 ambao walijitenga kuingojea siku yao ya kuja kwa Kristo mara ya pili na kunyakuliwa kwao. Takribani Wakorea milioni 12 wanasemekana kuwa ni Wakristo. Kati ya hao, Wakristo 100,000 waliusubiri ujio wa Yesu na kunyakuliwa kwao. Kwa lugha nyingine, hawa ni waamini wa kina ambao wanaliamini Neno la Mungu kama lilivyoandikwa na ndio waliosubiri kurudi kwa Bwana—ni Wakristo 100,000 tu kati ya milioni 12 ambayo ni chini ya asilimia 1.
Hata hivyo, tatizo lao ni kuwa hawakuwa na uelewa sahihi wa nyakati ambazo Mungu amezipanga kwa ajili yao. Kwa sababu ya kutokuwa na uelewa mzuri wa injili ya maji na Roho, Wakristo wengi wa Kanisa la Mwanzo walifanya makosa kujaribu kupiga mahesabu kwa msingi wa ufahamu wao duni kuhusiana na wakati wa kurudi kwa Kristo na kunyakuliwa kwa watakatifu. Hivyo Mtume Paulo aliwaonya, “kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo” (2 Wathesalonike 2:2).
Tukiongea kwa mujibu wa kihistoria, watu wengi waliendelea katika kutokuufahamu mpango wa Mungu na waliendelea kupata tarehe zisizo sahihi kuhusiana na kurudi kwa Bwana bila mafanikio. Ninaamini kuwa kuna hitaji la kusahihisha imani yao potofu. Lakini sina shauku ya kuwakemea kwa ukali—ninachotaka ni kuwasahihisha tu. Kwa nini? Kwa sababu kushindwa kwao kulitokana na kutozifahamu nyakati saba zilizopangwa na Mungu kwa ajili ya mwanadamu. Walipiga mahesabu vibaya kuhusu tarehe za kuja kwa Yesu mara ya pili kwa kuwa walizitumia vibaya namba zinazotajwa katika Biblia huku wakiziangalia kwa mtazamo wa kibinadamu.
Makosa haya hayajatendeka kwa Wakristo Wakikorea tu, bali ni makosa ambayo ni ya kawaida katika sehemu nyingine za dunia. Viongozi wa Kanisa kutoka katika maeneo mbalimbali ya dunia, na baadhi yao wakiwa ni watu mashuhuri sana wamewahi kufanya makosa kama hayo hayo. Moyo wangu una shauku ya kuushuhudia mpango wa Mungu kwa wale wote ambao wamemwamini Yesu na kusubiri juu ya tarehe yao ya kunyakuliwa kwao, ili waweze kuwa na uelewa mzuri na usio na makosa juu ya mpango wa Mungu kwao. Ninatumaini kuwa hata wao wataipata ile baraka ya kunyakuliwa na Mungu.
Kunyakuliwa na Mungu kutatokea mara baada ya wakati wa farasi wa kijivujivu na baada ya kuuawa kwa watakatifu kwa kuifia-dini. Wakati wa miaka saba ya Dhiki Kuu itakapoanza katika wakati huu wa farasi wa kijivujivu, Mpinga Kristo atainuka kama kiongozi mwenye nguvu sana kuliko wengine hapa ulimwenguni na atautawala ulimwengu wote.
Mpinga Kristo ataanza kuwatesa watakatifu wakati Dhiki Kuu itakapoanza, huku mateso hayo yakizidi katika nusu ya kipindi hicho cha Dhiki Kuu—yaani miaka mitatu na nusu—na yatafikia ukomo wake katika mwaka wa mwisho wa saba. Hapa ndipo wakati ambapo watakatifu watauawa ili kuilinda imani yao. Kisha wakati huu utafuatiwa mara moja na wakati wa sita, ambapo watakatifu waliouawa kwa kuifia-dini watafufuliwa na kunyakuliwa.
Wale wanaomwamini Yesu ni lazima wazifahamu nyakati vizuri. Ikiwa wanaamini juu ya kunyakuliwa kabla ya dhiki au kunyakuliwa katikati ya dhiki, basi ni vema wafahamu kuwa maisha ya kiimani yatabadilika kwa namna tofauti kabisa. Ikiwa waamini watakusubiri kunyakuliwa kwao kwa busara hali wakiwa na imani sahihi, au ikiwa watapanga na kuchagua tarehe yao maalum ya kunyakuliwa—ukweli ni kuwa mambo hayo yote yatategemea ikiwa wameiweka imani yao katika Neno la Mungu au la.
Ikiwa utayafuata mafundisho haya juuu ya Neno la Ufunuo kwa utulivu wote, basi ni hakika utaweza kuona jinsi yalivyo na maana, na kwa sababu hiyo utaweza kuyatatua maswali yako yote kwa usahihi. Lakini ikiwa hauna uelewa sahihi wa kunyakuliwa na kisha ukashindwa kuufuata, basi ni hakika kuwa imani yako itaharibika.
Nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki ilifundishwa na Scofield aliyekuwa mtheolojia wa Kimarekani, ambaye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuiingiza nadharia hii katika kamusi yake ya Biblia. Kamusi yake ya Biblia ilitafsiriwa sehemu mbalimbali na ikatumiwa maeneo mengi duniani. Nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki iliweza kuenea na kutumiwa na wengi kutokana na matumizi makubwa ya Kamusi ya Biblia ya Scofield. Kwa kuwa Kamusi ya Biblia ya Scofield ilikuwa imeandikwa na mtheolojia mashuhuri toka katika nchi yenye nguvu sana, basi kitabu au kamusi hiyo ilitafsiriwa katika lugha nyingi mbalimbali na ikasomwa na idadi kubwa ya Wakristo.
Scofield mwenyewe hakuwa na wazo kuwa nadharia yake ya kunyakuliwa kabla ya dhiki itaenea kiasi hicho duniani. Matokeo yake yalikuwa ni kukubaliwa na kupokelewa kwa nadharia hiyo ya kunyakuliwa kabla ya dhiki na Wakristo wote ulimwenguni. Lakini kabla ya nadharia ya Scofield ya kunyakuliwa kabla ya dhiki haijatokea, Wakristo wengi walikuwa wakiamini juu ya nadharia ya kunyakuliwa baada ya dhiki.
Nadharia ya kunyakuliwa baada ya dhiki inadai kuwa Kristo atarudi mwishoni mwa ile miaka saba ya Dhiki Kuu, na kwamba atawanyakua watakatifu wakati huo. Hivyo, watu wengi walikuwa na hofu kubwa ya Dhiki kabla ya kunyakuliwa na kuja kwa Bwana mara ya pili. Wakati wanauamsho walipohubiri toka katika mimbari zao juu ya kuja kwa Kristo mara ya pili, watu walikimbilia kufanya toba huku wakilia na kuzihuzunikia dhambi zao, na waliendelea kutoa maombi yao ya toba mara kwa mara. Hivyo, aliyeweza kulia sana kuliko wengine alichukuliwa kuwa ndio kipimo cha kumtambua yule aliyebarikiwa zaidi. Watu wa jinsi hiyo, pamoja na kuwa walikuwa wamemwamini Yesu waliyamwaga machozi mengi sana.
Lakini imani hii ya zamani kuhusu kunyakuliwa baada ya dhiki ilianza kupotea na badala yake kutokea imani ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Kwa nini ilikuwa hivi? Watu waliona raha zaidi kutoka katika nadharia ya kunyakuliwa baada ya dhiki na kwenda katika nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki kwa sababu kwa kufanya hivyo walijihakikishia kuwa hawatakabiliana na majaribu na dhiki ambazo wangelipaswa kuzipitia. Kwa kweli si jambo la kushangaza kuwa watu hao wangelipenda zaidi kunyakuliwa mawinguni kabla ya magumu ya kutisha ya Dhiki Kuu hayajawashukia. Kwa sababu hiyo, nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki ilienea haraka kama moto wa porini, kwa kuwa ilikuwa inatoa imani yenye raha kuliko ile ya kutisha inayowahakikishia kukutana na mateso ya Dhiki Kuu.
Kama watu wanavyopenda vitu vitamu kuliko vichungu, vivyo hivyo watu wanapenda mambo rahisi kuhusiana na imani yao. Watu wanapenda kuchagua na kuamini chochote kinachowapendeza kwa radha kati ya nadharia mbalimbali ambazo wanazuoni wamezitoa. Hivi ndivyo watu wengi sana walivyoishia kuiamini nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki kwa urahisi sana. Wale waliounga mkono mtazamo huu wa kunyakuliwa kabla ya dhiki walifikiri kuwa walipaswa kuitunza miili yao ibaki safi ndipo waweze kunyakuliwa. Na kwa sababu hiyo walijitoa sana katika maisha yao ya kiimani. Lakini nadharia nyingine iliitingisha imani yao juu ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Hali wakiwa na imani yao katika Yesu na hali wakisubiri kurudi kwa Bwana mara ya pili, ukweli ni kuwa walifanya makosa mawili makubwa.
Kosa la kwanza, walikuwa hawajaiamini injili ya maji na Roho, kwa lugha nyepesi waliendelea kumsubiri Bwana hali wakiwa na dhambi katika mioyo yao. Wao walishikilia na kuitegemea damu ya Yesu tu Msalabani, lakini ukweli ni kuwa hakuna kiwango cha kutubu ambacho kingeliweza kuwaondolea kikamilifu dhambi zao wanazozifanya kila siku. Hata hivyo, usiku na mchana waliendelea kusubiri kuja kwa Kristo mara ya pili. Walikusanyika pamoja katika makanisa yao kwa ajili ya kutubu dhambi zao, kuomba na kusifu usiku kucha, hali wakisubiri kunyakuliwa kwao. Hakukuwa na ubaya wa wao kusubiri kunyakuliwa kwao. Lakini walifanya kosa la kungojea kunyakuliwa pasipokuwa na imani sahihi—yaani, kutoiamini injili ya maji na Roho, imani pekee inayoturuhusu kusimama mbele za Mungu kama watoto wake.
Kosa la pili ni kwamba baadhi yao walidiriki kutangaza kuja kwa Yesu mara ya pili huku wakitoa tarehe maalum pasipo kuufahamu mpango wa Mungu. Hali hii sio tu kwamba iliwafanya waamini kusubiri bure, bali ilileta uharibifu mkubwa sana kwenye jamii na ikaufanya Ukristo ueleweke vibaya na kuharibu heshima yake kwa wasioamini.
Kwa sababu ya makosa haya mawili, basi kule kunyakuliwa ambako kulitegemewa sana na watu kuliposhindwa kutokea, basi hali hiyo iliwafanya watu wengi kufikiri kuwa suala la kunyakuliwa halipo kitu ambacho kiliwapelekea kuwa mbali na ukweli. Kwa sasa, ambapo ni wakati muafaka kuzungumzia juu ya kuja kwa Kristo mara ya pili na kwamba kurudi kwake kunakaribia, ukweli ni kuwa watu wengi sana hawazungumzii kabisa kuhusu hilo tena—wote hao wanashukuru kushindwa kwa wale wachache waliokuwa hawajui. Kifungu cha maandiko ambacho tunakizungumzia hivi sasa ndicho kile ambacho Mungu alikiandika kwa malaika wa Kanisa la Pergamo kwa kupitia Yohana. Mungu alimsifia mtumishi wa Kanisa na watakatifu kwa kuilinda imani yao hadi mwisho kwa kuuawa kwao kwa kuifia-dini. Lakini sifa alizozitoa Mungu kwa Kanisa la Pergamo ziliambatana na maonyo kadhaa, kwa kuwa Kanisa la Pergamo lilikuwa na baadhi ya waumini wanaoufuata ulimwengu. Hii ndiyo sababu Mungu aliliambia Kanisa kutubu ama sivyo atakuja kuliadhibu Kanisa hilo.
Tunahitaji kuzingatia kile ambacho Mungu amekisema kwa ujumla kupitia Yohana kwa makanisa yote saba ya Asia: “Yeye aliye na sikio na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.” Hii ina maanisha kuwa Mungu anahakikisha kuwa anauzungumza ukweli wake kwa watakatifu na kwa nafsi kwa kupitia makanisa yake na watumishi wake. Jambo la kukumbuka, Mungu aliliambia Kanisa la Pergamo: “Yeye aliye na sikio na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.”
Hebu nisisitizie juu ya msemo huu, “Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa,” Hii ina maanisha kuwa wale wanaomsubiri Bwana wanapaswa kuwashinda maadui wa Mungu. Ina maanisha kuwa ni lazima wapambane dhidi ya wale wanaoufuata ulimwengu, na kwamba ni lazima wajitenge na wale wapenda ulimwengu. Wale wanaomfuata Balaamu ndio wale wanaomfuata nabii wa uongo. Mungu anatueleza kuwa watu wa jinsi hii wanautafuta utajiri wa ulimwengu katika tamaa yao ya dhambi ni wafuasi wa fundisho la kiimani la Balaamu.
Si kila kanisa ni kanisa la Mungu. Viongozi wengi wa makanisa ya leo wanakubali kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, lakini hawaamini kuwa Yesu ni Mungu. Wapo wengi ambao hawaamini kuwa Yesu Kristo aliumba ulimwengu huu.
Kwa nyongeza, watu wengi wanakuja kanisani ili waweze kubarikiwa kwa mali. Viongozi wengi wa kanisa wanawaeleza waumini wao kuwa watabarikiwa ikiwa watatoa fedha zaidi kwa kanisa. Hali wakiwa wanadanganywa na mafundisho ya jinsi hiyo, waamini wengi wanafikiri kuwa kiasi wanachotoa ndicho kinachoonyesha imani yao. Wengi kati ya waamini hao wamethibitishwa kuwa ni waamini wazuri kwa sababu ya kutoa matoleo yao na kuhudhuria kanisani mara kwa mara. Zaidi ya yote, baadhi yao wanapewa nafasi za uongozi kanisani kama vile ushemasi au uzee wa kanisa kwa sababu tu ya kuhudhuria kanisani kila siku na kutoa cheki zenye pesa nyingi kama sadaka. Mambo haya yote ndiyo njia ya Balaamu, na ni mambo ambayo tunapaswa kuachana nayo.
Ni lazima tupambane dhidi ya imani za jinsi hiyo. Ikiwa unapenda kweli kulishwa mana iliyofichwa, basi ni lazima kwanza utambue ikiwa kanisa lako linafuata Neno la Mungu. Kama kanisa utakalokuwemo halifuati Neno la Mungu, basi ni lazima upambane na kulishinda. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo unapoweza kulishwa ukweli wa maji na Roho.
Ni kwa kujilisha toka katika Neno la maji na Roho, ambayo ni mana iliyofichwa, ndipo unapoweza kuzaliwa tena upya, na ni kwa kuzaliwa tena upya tu ndipo unapoweza kuendelea kulishwa Neno la Mungu lililotolewa na Mungu. Ni kwa namna hii ndipo wale waliozaliwa tena upya wanapoweza kujadiliana juu ya Neno la Mungu, kujilisha, kulisikia, na kushiriki Neno hilo na wengine.
Ikiwa kweli unapenda kunyakuliwa na Mungu, na ikiwa kweli unapenda kuzaliwa tena upya, basi itakuwa ni jambo la kijinga kuendelea kuhudhuria kanisa ambalo ni kanisa kwa jina tu. Kitendo cha kuhudhuria kanisa ambalo si la Mungu, basi ni hakika kuwa hautaweza kujilisha Neno la kweli la uzima hata kama utakuwa ukienda kanisani kwa muda mrefu—kwa lugha nyingine, kwenda kanisani kwa miaka mia moja, miaka elfu moja, au zaidi hakuwezi kukuweka katika njia sahihi ya wokovu.
Watu wa jinsi hiyo sio tu kwamba hawawezi kuzaliwa tena upya kwa imani, bali ukweli ni kuwa wataishia kufanya makosa ya kijinga ya kusubiri kunyakuliwa wakati hawajatimiza masharti ya kunyakuliwa huko—yaani pasipo hata kuzaliwa tena upya. Ukiwa na aina hii ya imani ya uongo; basi hata kama unasubiri kuja kwa Kristo kwa juhudi sana, na hata kama unampenda Bwana kwa moyo wako wote, na hata kama upo tayari kufa kwa ajili ya Yesu, basi mambo hayo yote yatakuwa hayana maana. Watu wa jinsi hiyo hawataweza kukutana na Bwana. Upendo wao kwa Mungu utaishia kama upendo usio na matokeo mazuri.
 Hii ndiyo sababu Mungu aliyaeleza makanisa saba ya Asia: “Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa.,” Mungu hatuelezi kuwa tunaweza kuwa na Neno lake pasipo kuhangaika. Ikiwa hatupambani na kuwashinda waongo, basi hatutaweza kuila mana yake, ambayo ni Neno la uzima. Hata kama umekuwa ukihudhuria katika kanisa lako, ikiwa hauifahamu kweli, basi hii ina maanisha kuwa yale yote uliyoyafahamu hadi sasa ni uongo. Ni lazima uukwepe uongo huu kwa kupambana na kuwashinda hasa unapoutafuta ukweli. Utaweza kuila mana ya uzima pale tu utakapokuwa umekutana na ukweli unaopatikana katika kanisa linalolishuhudia Neno la Mungu na kuihubiri injili ya maji na Roho.
Sisi hatuna kitu chochote kinachotuzuia kulipokea Neno la kweli la maji na Roho katika mioyo yetu. Mioyo ya wale wanaohubiri na kulisikia Neno hili la maji na Roho inaungana, na Roho Mtakatifu anakaa katika mioyo yao sawasawa. 
Mungu ameahidi kuwa atawapatia mana yake iliyofichwa wale wote watakaoshinda; kwa hiyo, ni lazima tumshinde Shetani katika mapambano yetu dhidi yake, na pia ni lazima tupambane na kuwashinda waongo. Ikiwa unapenda uzima wa milele, basi ni lazima uzaliwe tena upya; na ikiwa unapenda kunyakuliwa na Mungu, basi unapaswa kuwa na imani sahihi. Ni lazima upambane na kuwashinda waongo wa ulimwengu huu, pamoja na waongo wanaopatikana katika ulimwengu wa Kikristo.
Imani yako haipaswi kuwa ile isiyo na maamuzi, yaani imani inayoyumba toka upande mmoja hadi mwingine na inayozolewa na mkondo wa aina yoyote utakaojitokeza katika wakati husika. Ikiwa kanisa lako ni kanisa ambalo halihubiri Neno la Mungu kama lilivyo, basi unapaswa kuacha kuhudhuria kanisa kama hilo. Mungu atakutana na wale wote ambao mioyo yao inayatafuta mapenzi ya Mungu kwa kupitia Neno lake la mana ambalo ni Neno la kweli la maji na Roho.
Mimi nilikuwa mwanafunzi mzuri sana nilipokuwa nikisoma seminari. Sikuwahi kukosa darasani, na nilifaulu vizuri sana. Nilisoma kwa juhudi na kwa uaminifu. Lakini bado kulikuwa na mambo mengi ambayo nilikuwa siyafahamu. Hii ni kwa sababu kabla ya kukutana na Yesu na kumwamini mimi na familia yetu yote tulikuwa ni wabudha, na kwa sababu hiyo ufahamu wangu juu ya Yesu ulikuwa mdogo kwa wakati ule. Pia hata uelewa wangu wa Neno ulikuwa mdogo sana na ndio maana niliyasoma Maandiko kwa udadisi sana. Hali nikiwa na kiu ya ufahamu wa Neno la Mungu, niliazimia kujifunza toka kwa maprofesa wengi katika seminari, kwa kuwauliza maswali mengi huku nikidhani ya kuwa majibu yao yataikata ile kiu yangu ya kuifahamu Biblia.
Lakini hakuna kati ya hao maprofesa aliyeweza kunipatia jibu la wazi. Nilipokuwa nikileta maswali yangu kwa maprofesa ili wanisaidie kwa ufahamu wao wa Maandiko, wao walikuwa wakisifia uelewa wangu binafsi wa Biblia badala ya kuyajibu maswali yangu. Katika seminari mbalimbali, maprofesa hawalihubiri Neno bali wanafundisha “nadharia” zao binafsi juu ya Biblia. Lakini nadharia zao hizo kuanzia Theolojia ya Agano la Kale hadi Theolojia ya Agano Jipya, Theolojia Maalum hadi Historia ya Ukristo, toka katika mafundisho ya Kalvin hadi katika mafundisho ya Arminian, toka katika Kristolojia hadi kwenye elimu ya Roho, na toka katika utangulizi hadi katika mafafanuzi ya kina, yote hayo ni matokeo ya mawazo ya mwanadamu. Maprofesa hao wanafundisha nadharia mbalimbali zilizotayarishwa na wanazuoni, hakuna tofauti na ule uzoefu uliopata ukiwa chuoni ambapo umesoma nadharia mbalimbai kuhusiana masomo mbalimbali ya kidunia.
Nilikuwa ni mtu asiyeifahamu Biblia. Haijalishi jinsi nilivyokuwa nimefundishwa vizuri katika vyuo, na haikujalisha jinsi watu kadhaa walivyousifia uelewa wangu mpana wa Biblia, na wala haijalishi jinsi nilivyoweza kutoa mahubiri yangu yenye msingi katika ufahamu huo—ukweli ni kuwa kadri nilivyoendelea kujifunza Biblia na theolojia, ndivyo nilivyozidi kuwa na mashaka katika njia niliyokuwa nikiiendea. Ndipo nilipofikia hatua ya kutambua kuwa nilikuwa sifahamu lolote lile, na kwamba nilipaswa kuanza mwanzo kabisa. Hivyo, nikaanza kuinua maswali ambayo hapo mwanzoni yalionekana kuwa ni mageni na ya ajabu katika darasa. Moja ya swali hilo lilikuwa ni hili: “Kwa nini Yesu alibatizwa?” Sikuwahi kupata jibu sahihi na la wazi kwa swali hili. Hakuna aliyeweza kunipatia jibu sahihi, ambalo ni kuwa Yesu alibatizwa katika Mto Yordani na Yohana Mbatizaji ili kuzichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake.
Pia nilikuwa na swali kuhusiana na miujiza ya Yesu ambayo aliifanya, kama ule ambapo Yesu aliwalisha zaidi ya wanaume elfu tano kwa mikate mitano tu na samaki wawili. Hivyo nikauliza, “Wakati Yesu alipoibariki ile mikate mitano na samaki wawili, je iliongezeka ghafla na kuwa lundo la mikate na samaki mara moja, au iliendelea kuongezeka kadri walivyokuwa wakiwagawia watu?” Mara nyingi nilizomewa na kusemwa kwa kuuliza maswali kama hayo.
Hivyo nilifikia hatua ya kutambua kwamba “hivi ndivyo theolojia ilivyo. Tunajifunza yale ambayo mtu wa Kifaransa Kalvin aliyoyaandika katika nadharia ya kiwanazuoni na katika nadharia ya kiwanazuoni na mafafanuzi yake. Hatufahamu lolote kuhusu Biblia.” Hivyo nikaanza kusoma na kufanya utafiti binafsi kwa kukusanya machapisho mbalimbali toka katika madhehebu tofauti na kuyalinganisha na Biblia. Hata hivyo sikuweza kupata chochote.
Machapisho hayo yote yalikuwa yakifia hitimisho lile lile kwamba wakati watu wanapomwamini Yesu, basi dhambi zao zinaanza kupotea taratibu huku wakitakaswa kwa sara zao za toba, na kwamba hatimaye wanafikia hatua ya kutokuwa na dhambi wanapofikia kifo chao na hapo ndipo wanapoingia Mbinguni. Tofauti za kimadhehebu hazikujalisha—maana hitimisho lao lote lililenga kuwa Wakristo ni lazima watoe sala za toba na utakatifu unaoongezeka mambo ambayo hayahusiani kabisa na Neno. Madai haya yote yamepotoka na yanatofautiana na yale ambayo Neno la Mungu linasema. Hivyo, nikapiga magoti mbele za Mungu na nikamwomba anipe ukweli wake.
Hapa ndipo Mungu aliponifundisha juu ya injili ya kweli ya maji na Roho. Kwa kweli ukweli huu ulinishangaza. Na nilipotambua kuwa ukweli wa maji na Roho unapatikana katika vitabu vyote 66 vya Biblia, basi macho yangu yenye upofu yalifunguka na nikaanza kuliona Neno la Biblia kwa wazi. Niliweza kuona jinsi Agano la Kale na Agano Jipya yanavyokubaliana, na hapo ndipo Roho Mtakatifu alipokuja kukaa ndani ya moyo wangu. Baada ya kuona na kulitambua hili Neno la kweli, basi zile dhambi nyingi ambazo zilikuwa zimeupiga moyo wangu na kunielemea zilitoweka kabisa katika tendo la Mungu la upendo na neema.
Kama vile mawimbi yanavyotokea wakati jiwe dogo linapotupwa katika ziwa, basi vivyo ndivyo furaha ya kweli na nuru ilivyouingia moyo wangu. Maana kwa hii nuru niliweza kutambua ukweli wa Neno jinsi ulivyo. Katika wakati huu, Roho Mtakatifu aliingia ndani ya moyo wangu, na kwa sababu ya uwepo wa Roho Mtakatifu niliweza kuliona Neno la Biblia vizuri na kwa wazi. Tangu wakati huo, nimekuwa nikiihubiri injili ya maji na Roho.
Hadi leo hii, injili ya maji na Roho imeuimarisha moyo wangu, imenifariji na kunitia nguvu, na imeufanya moyo wangu kuwa msafi wakati wote. Hivi ndivyo nilivyoweza kujilisha Neno la Mungu. Nilipodumu katika Neno, hali nikiwa na uelewa wangu mzuri, basi baraka ya kweli ilikuja na kuujaza moyo wangu, na kwa sababu hiyo nilianza kuogelea katika bahari hii ya neema. Ni kama vile moyo wangu ulivyojazwa baraka wakati mlipoliamini Neno la Mungu la wokovu kwa waliozaliwa tena upya, vivyo hivyo Neno la Mungu litawafikisha katika neema yake.
Nilipoifungua Biblia na kudumu katika Neno, mashaka yangu yote na mawazo yasiyotulia yalitoweka, na badala yake moyo wangu ulijazwa furaha na amani. Kila nilipoulizwa kuhusu Biblia niliwezeshwa wakati wote kujibu yale ambayo Mungu alimaanisha kuhusu Neno lake. Ni kwa kufahamu na kuamini katika injili ya maji na Roho ndipo mtu anapoweza kujilisha Neno la Mungu, na ni kwa kujilisha katika Neno la Mungu ndipo mtu anapoweza kuzaliwa tena upya. Kwa kuwa wenye haki hawana dhambi ndani ya mioyo yao, basi haijalishi kuwa Bwana atarudi lini, maana wao wapo tayari kwa ajili ya kunyakuliwa wakati Bwana atakapowainua kwenda mawinguni.
 

Imani Inayoweza Kutuongoza Kwenda Katika Kunyakuliwa 
 
Kunyakuliwa ndilo jambo tunalolingojea baada ya kupokea ukombozi wetu kwa kufahamu na kuamini katika injili ya maji na Roho. Na tunaposubiri, tunapaswa kusubiri tukiwa na uelewa mzuri wa nyakati zilizopangwa na Mungu. Nyakati zilizopangwa na Mungu ni zile nyakati saba, na katika nyakati hizi wakati wa farasi wa kijivujivu ni wakati wa kuuawa kwa kuifia-dini. Wakati wa farasi wa kijivujivu ni wakati wa nne katika zile nyakati saba zilizopangwa na Mungu. Kwa upande mwingine, wakati huu ambapo tunaishi ni wakati wa farasi mweusi.
Tunapoupanda mlima mrefu, mara nyingi tunaitegemea sana ramani ili iweze kutuongoza. Lakini ili kuweza kukifikia kituo kwa usalama na usahihi kwa kutumia ramani hii, basi kitu cha kwanza tunapaswa kupafahamu mahali tulipo. Haijalishi jinsi unavyoweza kuwa mashuhuri katika kusoma ramani na pia haijalishi jinsi ramani yenyewe inavyoweza kuwa sahihi—ukweli ni kuwa ikiwa hupafahamu mahali ulipo, basi hiyo ramani uliyonayo itakuwa haina maana. Ni pale tu utakapo pafahamu mahali ulipo ndipo unapoweza kukifikia kituo unachokwenda.
Vivyo hivyo, ni kwa kuzaliwa kwa kupitia injili ya maji na Roho ndipo unapoweza kutambua wakati utakapoweza kunyakuliwa. Wakati sahihi wa kibiblia kuhusu kunyakuliwa ni mara baada ya kupita nusu ya kwanza katika ile miaka saba ya Dhiki Kuu —yaani baada ya miaka mitatu na nusu ya Dhiki. Hivi ndivyo Mungu alivyopanga katika Yesu Kristo wakati alipouumba ulimwengu huu.
Mpango wa Mungu wa wokovu katika Yesu Kristo, ambao kwa huo alimtuma Mwanawe pekee kuja hapa duniani, akamfanya abatizwe na kuuawa Msalabani, akamfufua toka kwa wafu, si mpango pekee, bali Mungu amezipanga pia nyakati saba kwa ajili ya ulimwengu huu, tangu uumbaji hadi mwisho. Hata sisi wanadamu tunachora ramani kabla ya kujenga nyumba zetu na pia tunapanga mipango ya baadaye katika biashara zetu—kama haitoshi, katika asasi zetu tunadiriki kupanga yale ambayo tutayafanya kwa siku moja. Je, ingeliwezekana kwa Mungu kuumba ulimwengu huu, kumuumba mwanadamu, yaani wewe na mimi katika Yesu Kristo pasipo mpango wowote? Kwa kweli hapana! Mungu alituumba akiwa na mpango wake!
Mpango huu wa Mungu unafunuliwa kwa wazi katika Neno la Ufunuo. Tunapolifungua na kudumu katika Neno hili, tunaweza kuuona mpango wa Mungu jinsi ulivyo. Neno hili ni ukweli. Ingawa Neno la Mungu ni lake kwa maelfu ya miaka, ukweli unabaki kuwa Neno hili ni ukweli usiobadilika na wala usioweza kupunguzwa na kuongezewa kitu. Wale wasiofahamu hivi na ambao hawajazaliwa tena upya kwa maji na Roho watabakia katika hali ya kutoufahamu ukweli uliofunuliwa kwetu kwa Neno la Mungu. Lakini wale wanaodumu katika Neno wataweza kuupata na kuutambua ukweli wote uliofunuliwa katika Biblia.
Katika kifungu cha maandiko ambapo Mungu ana ahidi kuwapatia mana yake wale wote watakaoshinda kina maanisha kuwa Mungu atawapatia nuru ya kulielewa Neno lake wale wote watakaoweza kupambanua kati ya uongo na kweli na kisha kuwashinda waongo kwa kulifahamu Neno lake la kweli. Wale walioweza kuukwepa uongo na walioweza kuupata ukweli ni lazima waushinde uongo huu kwa kuuhubiri ukweli huu. Mungu ametuahidi kuwa wale wanaoamini katika injili hii atawapatia baraka ya kuila mana yake: “Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.”
Mana iliyofichika hapa ina maanisha kuwa ni Neno la Mungu. Kwa upande mwingine, jiwe jeupe maana yake ni kuwa majina yetu yataandikwa katika Kitabu cha Uzima. Wakati watu wanapoamini katika injili ya maji na Roho ambayo Mungu amewapatia, basi ni hakika kuwa mioyo yao inabadilika. Hali mioyo yao ikiwa imejazwa na Neno la Roho Mtakatifu, wanafikia hatua ya kutambua kuwa dhambi zao zote katika mioyo yao zimetoweka kwa kuliamini Neno. Baada ya kuwa wamesafishwa dhambi kwa maji na Roho, basi majina yao yanaandikwa katika jiwe jeupe.
Mungu anatueleza kuwa hakuna anayelifahamu hili jina jipya isipokuwa yeye anayelipokea. Wale waliosamehewa dhambi zao zote ni lazima watambue kuwa mioyo yao haina dhambi kabisa iliyoachwa ndani yao, na kwamba majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima. Kwa maneno mengine, wanafahamu kuwa injili ya maji na Roho imezichukulia mbali dhambi zao zote za mioyo yao. Hivyo, ni wale tu waliozaliwa tena upya kwa kulifahamu Neno la kweli la maji na Roho na kuupokea ukombozi wao ndio wanaoweza kumfahamu Bwana na ile kweli yake. Wale ambao hawajazaliwa tena upya hawatambui kuwa wanapaswa kuzaliwa tena upya. Lakini wale waliozaliwa tena upya wanaweza kuwatambua watu wa jinsi hiyo kwa urahisi, kwamba bado hawajaila mana ya Mungu, na kwamba majina yao hayajaandikwa katika jiwe jeupe.
Je, ni kweli kuwa unapenda kunyakuliwa? Ikiwa unapenda kunyakuliwa, basi ni lazima ustahilishwe kuila mana. Kustahilishwa kuila mana, maana yake ni lazima uzaliwe tena upya kwa maji na Roho. Ili uweze kuila mana, basi ni lazima upambane na kuwashinda waongo kwa imani yako. Walimu wa uongo hawaleti ukombozi kwa wenye dhambi, bali wanazinyonya nafsi zao na mali zao. Ni lazima tupambane na kuyashinda makanisa ya uongo kama hayo, mitume wa uongo kama hao, na watumishi wa uongo wa Ukristo wa leo.
Kwa msingi wa Biblia, ni lazima tufahamu kwa usahihi kabisa jinsi Yesu alivyozichulia mbali dhambi zetu zote, pia ni lazima tufahamu kuwa ni kwa nini alibatizwa, kwa nini alizichukua dhambi za ulimwengu katika mwili wake, kwa nini alikufa Msalabani, na kwamba ni kwa nini alifufuka tena toka kwa wafu. Ni lazima tufahamu kwa usahihi kabisa kuwa ni kwa nini Yesu alikuja hapa duniani katika mwili na akayafanya haya yote, na pia ni lazima tufahamu kuwa huyu Yesu ni nani hasa. Lakini makanisa ya uongo, badala ya kuzifundisha kweli hizi, wao wanamwita kila anayehudhuria katika ibada zao kuwa ni “mtakatifu” kwa mamlaka yao binafsi. Wao huwauliza hivi tu, “Je, mnamwamini Yesu?” Ikiwa jibu litakuwa “Ndiyo, tunaamini,” basi haya makanisa ya uongo yatawaita watu hao kuwa ni watakatifu, watawabatiza ndani ya mwaka mmoja, na kisha wataendelea kuwaomba aina tofauti za matoleo toka kwao, kuanzia na sadaka ya shukrani hadi sadaka maalum wawapo ndani ya yale makanisa yao yenye majengo makubwa na ya kifahari. Makanisa kama haya, ambayo yametawaliwa na fedha na tamaa yao ya kujenga majengo ya kanisa makubwa yanayong’ara na ya kifahari ni makanisa ya uongo.
Tunapoila mana, basi ni lazima tupambane dhidi ya makanisa ya uongo na wale wanaoeneza mafundisho ya uongo. Ikiwa tutashindwa katika vita hii, basi hii haita maanisha kuwa sisi si watakatifu wa Mungu tena, bali itamaanisha pia kuwa hatutanyakuliwa na Mungu. Kutokuwa watakatifu wa Mungu ni sawa na kutokuwa watoto wa Mungu; hata kama Yesu angelikuwa anarudi kwa mara ya 100, ukweli ni kuwa hatutanyakuliwa.
Mathayo 25 inatueleza juu ya mfano wa wanawali kumi, watano kati yao walikuwa na busara na watano walikuwa ni wajinga. Mfano huo unatueleza jinsi wale wanawali watano wajinga ambao walizibeba taa zao pasipo mafuta kisha wakaenda kununua wakati Bwana harusi alipowasili. Tunapaswa kuwa wanawali wenye busara waliozitayarisha taa zao na mafuta mapema. Kwa kuwa na imani inayoandaa mafuta, basi ni hakika kuwa tutastahilishwa kuila mana mbele ya Yesu, tutawashinda waongo, na kisha tutazaliwa tena upya kwa Neno la maji na Roho.
Tunapoyasikia mahubiri, ni lazima tujiulize ikiwa mchungaji huyo analihubiri Neno la Mungu au la. Pia tunahitaji kujiuliza ikiwa kanisa linazitumia fedha zake kama Mungu anavyotaka iwe—yaani kutumia fedha za kanisa katika kazi ya Mungu na si kwa kazi zake binafsi. Kwa maneno mengine, ni lazima tulitafute kanisa la kweli la Mungu. Pia tunapaswa kuchoshwa na makanisa ambayo yanatoa ibada za kawaida badala ya kulihubiri Neno la Mungu na mafundisho yake.
Haijalishi jinsi wanavyoongea vizuri kuhusu toba, ukweli ni kuwa matendo yao yatakueleza kuwa wao ni akina nani na kwamba wapo kwa ajili gani—yaani ikiwa wapo kwa ajili ya kujenga majengo makubwa ya kanisa; ikiwa wapo kwa ajili ya kuwaangalia maskini au kwa ajili ya kuwahudumia matajiri tu; na kwamba ikiwa wapo kwa ajili ya kuzisaidia roho za watu ili ziokoke. Mungu amekupatia macho na masikio ilikwamba uweze kuona na kuamua wewe mwenyewe. Na utakapofikia hitimisho kuwa kanisa lako si kanisa sahihi, basi usisite kujitoa ndani ya kanisa hilo, kwa maana kitendo cha kuendelea kuhudhuria kanisa kama hilo ni sawa na kujaribu kuingia kuzimu. Na kwa sababu hiyo unaweza ukayapoteza maisha yako.
Je, unafahamu jinsi injili ya maji na Roho ilivyo njema? Unapoufahamu na kuukubali ukweli huu ambao ni injili ya maji na Roho ndani ya moyo wako, basi ni hakika kuwa unafanyika kuwa mtu mpya mkamilifu. Wale waliokuwa mali ya dunia hapo kabla sasa ni mali ya Mbinguni, na wale waliokuwa wameteswa na mapepo sasa wamewekwa huru.
Mapepo yanaweza kuingia na kuzitesa nafsi za wale walio na dhambi katika mioyo yao na ambao kwa sababu hiyo wamefungwa katika dhambi zao. Lakini Bwana alikuja hapa duniani na akazichukulia mbali dhambi zetu zote kwa injili ya maji na Roho. Kwa kuwa amekwishazichukulia mbali dhambi zetu zote, basi mapepo hayawezi kabisa kutusumbua au kuziiba roho zetu. Hii ndiyo sababu unapoifahamu na kuiamini injili hii, basi mapepo yanafukuzwa na maisha yako yanabadilika.
Kwa maneno mengine, wale waliokuwa watumishi wa ulimwengu wanawekwa huru toka katika utumishi huo. Mungu amefanya tendo la kushangaza la kuwageuza wenye dhambi kuwa wenye haki, hali akiwafanya wale waliokuwa wa duniani kuwa wa Mbinguni, na wakati Bwana atakaporudi atawainua na kuwapeleka katika Ufalme wake.
Maisha yetu ya kidunia sio mwisho wetu. Baada ya kutufanya kwa mfano wa sura yake, Mungu hakutuweka katika dunia hii ili tuweze kuishi kwa muda mfupi. Kwa kweli maisha katika mwili ni mafupi sana. Mara tunapotoka shuleni tunakuwa katika miaka ya 20. Tunatumia ile miaka ya 30 katika kujaribu kuweka misingi ya maisha yetu, na inapofikia wakati ambapo msingi huu upo tayari, tunajikuta tukiwa tumefikia miaka ya 40 au 50. Tunapofikia wakati ambapo tunafikiri tunaweza sasa kupunguza spidi na kuyafurahia maisha yetu, basi tunajikuta kuwa muda wetu wote wa maisha umekwisha tupita na kwamba tunakabiliana na mwisho wake. Kama maua yanavyochanua asubuhi na kisha kunyauka mchana, basi ndivyo inavyokuwa kwetu, yaani wakati tunapofikiri kuwa sasa tumeyafikia maisha yetu ndipo tunapotambua kuwa muda umeisha na kwamba sasa tunakaribia mwisho wa maisha yetu.
Hivi ndivyo maisha yetu mafupi yalivyo. Lakini kitu kibaya zaidi ni kuwa kuna watu wengi sana ambao hawautambui ufupi huu wa maisha. Hata hivyo mwisho wa maisha katika miili yetu sio mwisho wetu, kwa maana huo ndio mwanzo wa maisha ya nafsi zetu kiroho. Kwa nini? Kwa sababu Mungu ametuandalia si tu Ufalme wa Milenia bali ametuandalia pia Mbingu na Nchi Mpya ambako tutaishi milele, Mungu amefanya hivi ili kutufidia ile miaka michache ya maisha yetu hapa duniani. Hii ni baraka ya Mungu ya maisha ya milele ambayo amewapatia wale tu waliozaliwa tena upya kwa kuamini katika Neno la maji na Roho.
Ni mpaka utakapokuwa umeila ile mana iliyofichwa na jina lako litakapokuwa limeandikwa katika jiwe jeupe ndipo unapoweza kunyakuliwa. Mungu anatueleza kuwa wale walioila mana yake wataweza kumshinda Shetani katika kipindi cha Dhiki Kuu, na kwamba majina ya wale watakaoshinda tu ndiyo yatakayoandikwa katika jiwe jeupe. Kwa hiyo, wale wasioshinda wasiote ndoto ya kunyakuliwa wala wasiote ndoto ya kuzaliwa tena upya.
Ili uweze kupata kitu cha thamani ni lazima utoe gharama ya kujitoa. Mfano mzuri ni dhahabu; ili kupata dhahabu inachukua muda mrefu, na juhudi nyingi, na pia inahusisha hatari mbalimbali. Watu wengi sana wamekufa katika migodi ya dhahabu hata kabla hawajaweza kupata kipande kidogo cha dhahabu. Kitendo cha kuchimba dhahabu kinahusisha pia kuteseka kwa namna nyingi. Kitendo cha kulijaza lori zima udongo kinatoa dhahabu kidogo sana. Zaidi ya yote, kazi hii haiwezi kufanyika katika kila mto, ni lazima kwanza upate mto ambao una ardhi yenye dhahabu. Kwa maneno mengine, inagharimu jitihada ngumu katika kutafuta dhahabu na wakati mwingine inaweza kukugharimu hata maisha yako. Sasa, ni kwa nini watu wanajaribu kutafuta dhahabu? Wanafanya hivyo kwa sababu wanafikiri kuwa dhahabu ni ya thamani kiasi hicho kiasi cha kuhatarisha maisha yao binafsi.
Lakini kitu ambacho ni cha thamani sana kuliko fedha na dhahabu ni ule ukweli kuwa tunaweza kufanyika watoto wa Mungu. Mungu anaweza kukupatia furaha inayopita katika mwili wako, lakini kufanyika watoto wa Mungu kunakupatia furaha ya milele isiyo na mwisho. Ili uweze kunyakuliwa, kufurahia utajiri, kufurahia mafanikio, na kupata heshima ya Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya, na kuishi maisha kama hayo milele, basi unatakiwa kuamini katika injili ya maji na Roho na kisha uilinde imani yako na kupata ushindi.
Kuna uongo mwingi sana katika ulimwengu huu ambao unajaribu kupata nafasi wakati wote ili uweze kuinyakua mioyo yetu kwa kujaribu kutufanya tuipoteze imani yetu. Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho na wana ukweli katika mioyo yao wanafahamu jinsi imani hii ilivyo ya thamani. Kwa kuwa wanafahamu uthamani wa imani hii, basi wanapambana dhidi ya mafundisho ya uongo yanayojaribu kuiiba imani hiyo toka kwao. Ikiwa tutatambua jinsi watu wengi wanavyojaribu kuipata imani hii lakini wanashindwa, na ikiwa tutatambua kuwa ni imani hii tu ndiyo itakayoweza kutuvisha ili tuweze kukaribishwa katika karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo na kutupatia baraka yake ya uzima wa milele, basi ni lazima tuifanye imani hii kuwa yetu na tusimruhusu awaye yote kuinyakua toka kwetu. Hii ndiyo aina ya imani inayopambana na kushinda.
Kwa kweli nilishawishika kuwa ni muhimu kuutangaza ufahamu sahihi na uelewa wa Neno la Ufunuo—ili kuhakikisha kuwa unaweza kuilinda injili yenye thamani ya maji na Roho—hii ni kwa sababu nilifahamu kuwa walimu wengi wa uongo watajaribu kutumia Neno la Ufunuo kuwadanganya na kuwachanganya waliozaliwa tena upya na watu wa kawaida. Hii ndiyo sababu ninalihubiri Neno la Ufunuo katika mahubiri yangu na katika vitabu ili kuhakikisha kuwa unaweza kuishi maisha ya imani hali ukiwa na ufahamu sahihi kuhusiana na nyakati za mwisho.
Kitabu cha Ufunuo kinatupatia jambo la muhimu sana. Lakini Neno la Ufunuo haliwafunulii chochote wale ambao hawawezi kuila mana ya Mungu iliyofichwa na ambao hawana Roho Mtakatifu katika mioyo yao. Katika Neno la ufunuo kumeandikwa ishara zote za nyakati za mwisho na kuhusu kunyakuliwa ambalo ni tumaini la kila Mkristo, na pia kumeandikwa juu ya Mbingu na Nchi Mpya, ambao ni mpango wa Mungu wa ajabu na usio wa kawaida. Lakini kwa sababu ya hekima ya Mungu ambapo Mungu hamfunulii kila mtu siri zake, basi ukweli unabakia kuwa kitabu cha Ufunuo ni andiko gumu ambalo hakuna mtu anayeweza kulifahamu. Wale wanaoweza kulifahamu Neno la Ufunuo ni wale tu ambao wamelishwa mana ya Mungu na ambao majina yao yameandikwa katika jiwe jeupe kwa kuzaliwa tena upya kwa maji na kwa Roho na kwa kuushinda uongo.
Hii ndiyo sababu, wale ambao hawajazaliwa tena upya wanazungumzia juu ya kunyakuliwa kabla ya dhiki au kunyakuliwa baada ya dhiki kwa sababu ya kutokufahamu kwao, na hii ndio sababu tuna watu wanaodai kuwa Ufalme wa Milenia ni lugha ya picha tu. Neno la Mungu ni kweli, na linaeleza wazi kuwa kunyakuliwa hakutatokea pasipo Dhiki Kuu. Linatueleza kuwa kunyakuliwa kutatokea mara baada ya nusu ya miaka saba ya Dhiki Kuu—yaani baada ya kuuawa kwa watakatifu kwa kuifia-dini ambako kutaambatana na ufufuo wao.
Ninasikitika kuwaeleza kuwa kunyakuliwa hakutatokea wakati watu wakiendelea katika maisha yao ya kawaida—ambapo marubani watatoweka, na akina mama watatoweka wakiwa kwenye meza ya chakula. Bali, kunyakuliwa kutatokea wakati matatizo makuu yatakapouangukia ulimwengu, wakati matetemeko ya nchi yatakapokuwa yakienea ulimwenguni, wakati nyota zitakapoanguka toka angani, na wakati ardhi itakapopasuka. Kwa maneno mengine, kunyakuliwa hakutatokea katika siku ya amani kama wengi wanavyodhani.
Hadi sasa nyota bado hazijaanguka, theluthi ya dunia haijateketea kwa moto, na bado bahari haijageuka kuwa damu. Nina maanisha nini ninaposema haya? Nina maanisha kuwa wakati wa kunyakuliwa bado haujafika. Mungu anatueleza kuwa atatupatia ishara ambazo sisi sote tutaweza kutambua kabla ya kunyakuliwa hakujatokea. Alama hizi ni matatizo ambayo yataukumba ulimwengu huu—theluthi ya bahari na mito kugeuka na kuwa damu, theluthi ya misitu kuteketea kwa moto, nyota kuanguka, maji yasiyoweza kunyweka, n.k.
Wakati ulimwengu utakapokuwa umegubikwa na matatizo haya makuu, ndipo Mpinga Kristo atakapoinuka ili kuleta nidhamu. Kwanza atatokea kama kiongozi mashuhuri wa dunia, na baadaye atageuka na kuwa dikteta katili ambaye atautawala ulimwengu kwa nguvu zake. Biblia inatueleza kuwa ni katika wakati huu ambapo utawala wa kikatili wa Mpinga Kristo utakapokuwa umeanzishwa hapa duniani, ndipo Bwana atakaporudi duniani kuwachukua watakatifu wake. Kunyakuliwa hakutatokea wakati majanga ya kiasili bado hayajatokea na wakati Mpinga Kristo hajainuka.
Kwa maneno mengine, ni makosa kwa watu kuacha kazi zao, kuacha kwenda shule, na kufikia hatua ya kutofanya lolote kwa kudhani kuwa kunyakuliwa kwao kumekaribia wakati ishara hizi zote ambazo Mungu ametuahidia bado hazijaonekana. Kwa kweli hupaswi kudanganywa kwa namna hii, maana kwa kufanya hivyo utakuwa umeangukia katika mitego ya Shetani ya uongo.
Ni lazima tupambane na kukishinda kila kitu ambacho mafundisho ya uongo yamekiweka ili kututega. Imani pekee ambayo inaweza kuyashinda mafundisho ya uongo ni imani katika injili ya maji na Roho. Ni wale tu wanaoamini katika ubatizo wa Yesu ambao umezichukulia mbali dhambi zao zote ndio waliohuru toka katika minyororo ya dhambi hizi. Kwa kuwa Yesu alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa ubatizo wake, na kwa kuwa ametununua kwa damu yake ambayo imezisafishilia mbali dhambi zetu, basi sisi tuliupokea wokovu wake mkamilifu kwa kuamini katika mambo haya yote ambayo Bwana ameyafanya kwa imani tu. Wale wanaoliamini Neno hili sasa wamefanyika kuwa watoto wa Mungu, na kwa sababu hiyo watashinda katika mipango yote ambayo Mungu ameipanga kwa ajili yao.
Kwa upande mwingine, kitu pekee kinachowangojea waongo wanaodai kumwamini Yesu ingawa wana dhambi katika mioyo yao, na ambao wanatafuta kuzitimiza tamaa zao binafsi wanapomtumikia Bwana, ni adhabu ambayo watakabiliana nayo wakiwa pamoja na Shetani. Hii ndiyo sababu injili yetu ya maji na Roho ni ya thamani sana. Ni wale tu wanaoifahamu injili hiyo na ambao wanaweza kutofautisha kati ya injili ya kweli na injili ya uongo ndio wanaoweza kuila mana ya Mungu iliyofichwa, ndio wanaoweza kuushinda uongo wote hapo mwishoni, na ndio watakaoweza kuingia katika Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya. Hebu lisome Neno na ujionee mwenyewe ukweli halisi unaoweza kukuokoa, unaoweza kukupa tumaini, na unaoweza kukubariki kwa uzima wa milele. Utambue ukweli huo na kisha uuamini. Hii ni imani ya ushindi.
Ushindi katika vita vyetu vya kiroho ni wa muhimu sana kwetu kwa sababu ikiwa tutashindwa katika vita hii, basi hii haimaanishi kuwa ni kushindwa kwa kawaida, bali ina maanisha kuwa ni kushindwa kwa kufungwa kuzimu. Katika mapambano mengine tunaweza kupona baada ya kupata hasara au kupoteza, lakini katika vita hii ya kiimani hakuna nafasi ya kupona. Hivyo ni lazima uwe tayari kutofautisha kati ya ukweli na mawazo yako binafsi, tamaa ya mwili wako, na uongo wa walimu wa uongo, na pia ni lazima uiandae imani yako kwa ajili ya nyakati za mwisho kwa kuupata ufahamu sahihi kwa nyakati zake kwa msaada wa mwanga wa Neno.
Mungu ameyaandaa mapigo ya matarumbeta saba na mabakuli saba, na ameiruhusu Dhiki Kuu kuja juu yetu. Wakati ulimwengu utakapokuwa umekumbwa na majanga mengi ya kiasili—yaani moto mkubwa unaoteketeza, nyota zinazoanguka, bahari, mito, na chemchemi kubadilika na kuwa damu—basi hapo ndipo Mpinga Kristo atakapoinuka, na hapo unapaswa kutambua kuwa huo utakuwa ndio mwanzo wa kipindi cha miaka saba ya Dhiki Kuu. Kuuawa kwa kuifia-dini, ufufuo, na kunyakuliwa kwa watakatifu kutatokea wakati wa pigo la mwisho la tarumbeta, yaani wakati tarumbeta ya mwisho itakapopiga, lakini itakuwa ni kabla ya yale mapigo saba ya mabakuli hayajamiminwa.
Wakati muhuri wa nne wa Mungu utakapoondolewa, Mpinga Kristo atawataka watakatifu kuikana imani yao. Wakati huo, wale wote ambao majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima—yaani watakatifu waliozaliwa tena upya na walioila mana na ambao majina yao yameandikwa katika jiwe jeupe—watauawa na kuifia-dini kwa ujasiri. Hii ndiyo imani ya mwisho na iliyo kuu na inayompatia Mungu utukufu. Hii ndiyo imani yenye ujasiri kwa wale wote wanaoamini na kuishi kwa mujibu wa injili ya maji na Roho. Kwa ufupi, hii ni imani ambayo kwa hiyo tunaweza kuwa washindi katika vita ya kiroho.
Tunapaswa kuwashinda maadui zetu kwa gharama zote. Baada ya kuzaliwa tena upya, ni lazima tuendelee kupambana na kuwashinda waongo. Ili kufanya hivyo, ni lazima tuishi maisha yanayojilisha katika mana ya Mungu na kulipenda Neno la Bwana wetu hadi mwisho. Mungu ameahidi kuwapatia utukufu wake na baraka kwa wale watakaoshinda. Mambo yafuatayo watapewa wale ambao wameipokea mana ya Mungu iliyofichwa kwa kuwashinda waongo kwa imani katika Neno la Mungu, mambo hayo ni imani inayomstahilisha mtu kupaishwa mawinguni na Mungu, tumaini la kweli kwa waamini, na uhakika wa Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya.
Wale wanaofahamu thamani ya ukweli huu, wanauza kila kitu ili waweze kuupata ukweli huo na pia wanavumilia na kujitoa ili waweze kuutunza ukweli huo. Kwa kuwa kujitoa huku kutatujia si kama maumivu bali kama furaha, na kwa kuwa hii ni hazina ya kweli yenye thamani sana ambayo mwishoni itatupatia kila kitu, basi ni sahihi kwetu kuacha kila kitu tulichonacho ili kuilinda hazina hii.
Ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa na tumaini juu ya Ufalme wa Milenia na juu ya Mbingu na Nchi Mpya, na kwamba utawashinda maadui wote kwa tumaini hili, na hatimaye kuinuka kama mshindi wa furaha kuu mwishoni.