Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[6-2] Nyakati za Mihuri Saba (Ufunuo 6:1-17)

(Ufunuo 6:1-17)
 
Wazo kuu la kila sura ya Ufunuo linaweza kufupishwa na kuhitimishwa kama ifuatavyo:
Sura ya 1 – Utangulizi wa Neno la Ufunuo
Sura ya 2-3 – Barua kwa makanisa saba ya Asia
Sura ya 4 – Yesu aketiye katika kiti cha enzi cha Mungu
Sura ya 5 – Yesu Aliyetawazwa kama Mwakilishi wa Mungu Baba
Sura ya 6 – Nyakati saba zilizopangwa na Mungu
Sura ya 7 – Wale watakaookolewa wakati wa Dhiki Kuu
Sura ya 8 – Matarumbeta yanayotoa mlio wa mapigo saba
Sura ya 9 – Mapigo ya shimo lisilo na mwisho
Sura ya 10 – Kunyakuliwa kutatokea lini?
Sura ya 11 – Je, ile miti miwili ya mizeituni na wale manabii wawili ni akina nani?
Sura ya 12 – Kanisa la Mungu ambalo litakabiliana na Dhiki Kuu
Sura ya 13 – Kutokea kwa Mpinga Kristo na kuuawa kwa watakatifu kwa kuifia-dini
Sura ya 14 – Ufufuo na kunyakuliwa kwa watakatifu na jinsi watakavyomsifu Mungu mawinguni
Sura ya 15-16 – Kuanza kwa Mapigo ya mabakuli saba
Sura ya 17 – Hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi
Sura ya 18 – Kuanguka kwa Babeli
Sura ya 19 – Ufalme utakaotawaliwa na Mwenyezi
Sura ya 20 – Ufalme wa Milenia
Sura ya 21 – Mji mtakatifu toka mbinguni
Sura ya 22 – Mbingu na Nchi Mpya, ambapo maji ya uzima yanatiririka
Tangu sura ya kwanza, kila sura ya Neno la Ufunuo ina wazo kuu, na kila unapoyaangalia hayo mawazo Kuu utaona wazi kuwa yanaungana na kukubaliana vizuri hadi sura ya mwisho. Kama ilivyo kwa Warumi, ambapo tunaona kuwa sura ya 1 ni utangulizi, sura ya 2 ni Neno la Mungu kwa Wayahudi, na sura ya 3 ni Neno la Mungu kwa Wamataifa, basi vivyo hivyo Kitabu cha Ufunuo kina wazo kuu ambao ni mwendelezo unaopatikana katika kila sura.
Sababu inayonifanya nikielezee kitabu cha Ufunuo kwa msingi wa Neno zima ni kwa sababu kuna watu wengi sana ambao wamekijadili kitabu cha Ufunuo kwa kutumia nadharia mbalimbali, na ikiwa unasoma kitabu cha Ufunuo kwa kupitia mtazamo wa nadharia hizo, basi ni hakika kuwa hutaweza kujizuia katika kufanya makosa makubwa.
Kwa kuwa Biblia iliandikwa kwa kupitia watu wa Mungu waliokuwa wamevuviwa na Roho Mtakatifu, basi ni hakika kuwa haina kitu kinachohitaji masahihisho. Ukilinganisha na waandishi wa kidunia, utaona kuwa vitabu vya kidunia vina makosa mengi sana ambayo yanahitaji kusahihishwa; makosa haya hutokea hata kama mwandishi atakuwa na ufahamu na upeo mkubwa wa hali ya juu. Lakini Neno la Mungu halijabadilika kabisa pamoja na kuwa limekuwa likirithishwa tangu kizazi hadi kizazi kwa maelfu ya miaka. Pamoja na miaka hiyo yote, Neno la Mungu limebakia kuwa lisilo na makosa kwa kuwa liliandikwa kwa kupitia watumishi wa Mungu ambao walivuviwa na Roho Mtakatifu.
Kwa kuwa kile ambacho Mungu anataka kutueleza kimefichwa katika Biblia, basi ndio sababu wengi wetu tumebakia kutoyafahamu Maandiko vizuri. Lakini tangu wakati wa uumbaji, Biblia haijabadilika hata mara moja. Lakini kwa kuwa watu wengi walikuwa na uelewa duni wa Neno la Mungu na mpango wake, basi walianza kuyatafsiri Maandiko kwa kufuata mawazo yao binafsi.
Kwa kuwa Mungu haifunui siri yake kwa kila mtu, basi wale wasiomwabudu Yeye na wasioamini kwa mujibu wa Neno, yaani wale wanaojaribu kuzitimiza tamaa zao kwa kulichukulia jina la Mungu bure hawawezi kulielewa Neno la Ufunuo hata kama wakijaribu kufanya hivyo. Watu wa jinsi hiyo wanafanya makosa mengi kwa sababu wanashindwa kulifahamu Neno la Mungu kiasi kuwa wengine wanaishia kuamini juu ya nadharia zisizo na maana juu ya nyakati za mwisho, huku baadhi yao wakifikia hatua ya kutangaza siku ya kuja kwa Yesu mara ya pili na huku wengine wakiitafsiri Biblia kwa matakwa yao binafsi na kufanya makosa mengi.
Miongoni mwa wanatheolojia ambao wanaweza kuwawakilisha wenzao waliopotoka katika kulifahamu Neno ni Abraham Kuyper na Louis Berkhof ambao walitetea kuwa hakuna kipindi cha ufalme wa milenia; mwanatheolojia mwingine ni C. I Scofield ambaye ndiye aliyeiunda nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Lakini ukweli ni kuwa nadharia hizi zote zinazotetewa na hawa wanazuoni zote zina makosa na zimejengwa katika fikra zao binafsi.
Kwanza kabisa, fundisho la kiimani la amilenia linalotetewa na wahafidhina wengi linadai kuwa hakuna Ufalme wa Milenia utakaokuwepo, na kwamba Ufalme huu wa Milenia unatimizwa katika mioyo ya watakatifu wanaoishi katika dunia hii kwa sasa. Nadharia ya amilenia inakana uwepo halisi wa Ufalme wa Milenia hapo baadaye. Nadharia hii inautafsiri Ufalme wa Milenia kama ni lugha ya picha huku wakikichukulia kipindi hiki ambacho watakatifu wanaishi hadi siku atakayorudi Yesu Kristo kuwa ndiyo kipindi cha Ufalme wa Milenia. Lakini ufafanuzi unaotolewa na nadharia ya amilenia, kwamba Ufalme wa Milenia unatokea katika mioyo ya watakatifu pasipo uwepo wa Dhiki Kuu ni ufafanuzi wenye makosa.
Pia kuna nadharia nyingine ambayo imeenea sana ulimwenguni kuliko hata nadharia ya amilenia na nadharia hiyo ni ile ya kunyakuliwa kabla ya dhiki ambayo imeelezewa na mwanazuoni Scofield. Lakini nadharia hii imeishia kuubadili mpango wa Mungu. Mungu alizipanga nyakati saba hata kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu huu, na kadri siku zinavyokwenda amekuwa akitimiza kila kitu kwa mujibu wa mpango wake. Lakini watu wasioujua mpango wa Mungu uliofunuliwa katika Ufunuo sura ya 6 wametengeneza nadharia hii potofu ya kunyakuliwa kabla ya dhiki. Wao wanadai kuwa wale waliozaliwa tena upya miongoni mwa Wamataifa watanyakuliwa kabla ya kuanza kwa Dhiki Kuu, na kwamba baadhi ya watu wa Israeli wataokolewa wakati wa kipindi cha miaka saba ya Mateso.
Nadharia hii inabakia kama fundisho la kiimani ambalo limewatupa watu wengi katika mkanganyiko mkuu. Kama kunyakuliwa kwa watakatifu kungelitokea kabla ya Dhiki Kuu kama inavyodaiwa na nadharia ya kunyakuliwa kabla ya dhiki, basi kusingelikuwa na mateso kwa watakatifu na kusingelikuwepo kuuawa kwa kuifia-dini kunakoelezwa katika Ufunuo sura ya 13. Hivyo, waamini wanaomwamini Yesu ni lazima waachane na fundisho hili la kunyakuliwa kabla ya dhiki na kisha waziandae imani zao kwa kuamini ule ukweli kuwa kunyakuliwa kwao kutakuja katikati ya Dhiki Kuu.
Neno la Ufunuo linatufunulia jinsi Mungu atakavyouongoza ulimwengu kwa mujibu wa nyakati zake saba. Hivyo ni lazima tuone kwa kupitia lenzi ya mpango wa nyakati saba zilizopangwa na Mungu na kama zilivyozungumziwa katika Ufunuo sura ya 6. Watu wanachanganyikiwa na imani zao zinayumba kwa kuwa hawaufahamu ukweli wa nyakati hizi saba za Maandiko. Hivyo, ni lazima tuamini kile kilichoandikwa katika Ufunuo sura ya 6. Ili kufanya hivyo, ni lazima tuamini katika Neno la siri la nyakati saba zinazoshuhudiwa na Biblia nzima na si kufanya hivyo kwa kutumia vifungu vichache ambavyo haviungani na kukubaliana na Maandiko yote.
Kama ambavyo injili ya maji na Roho ilivyofichwa kwa watu, basi ndivyo nyakati saba za Mungu zilivyofichwa pia. Pamoja na kuwa wanazuoni wa kibiblia wamejaribu kulifahamu Neno la Ufunuo na kupendekeza nadharia nyingi kwa kukazia mawazo yao binafsi, ukweli ni kuwa Neno la Ufunuo limebakia kuwa ni gumu sana kulifahamu. Hii inatokana na ukweli kuwa injili ya maji na Roho imefichwa hadi sasa. Lakini nadharia ambazo wanazuoni wamekuja nazo juu ya kurudi kwa Kristo, kunyakuliwa kwa watakatifu, au juu ya Ufalme wa Milenia hazijawaletea faida wale wanaomwamini Yesu.
Ili tuweze kulifahamu Neno la Ufunuo, basi ni muhimu sana kwetu kuifahamu sura ya 6. Sura hii ni ufunguo muhimu katika kulifahamu na kulitatua Neno lote la Ufunuo. Lakini kabla hatujajaribu kulifahamu Neno lote la Ufunuo kuna kitu kimoja ambacho ni lazima tujikumbushe: kwamba haiwezekani kukifahamu kitabu cha Ufunuo pasipo kutambua na kuamini katika injili ya maji na Roho. Ni lazima utambue kwamba ukweli wa Mungu unaweza kutambuliwa pale tu unapofahamu na kuamini katika injili ya maji na Roho.
Kama ilivyoandikwa katika Ufunuo sura ya 8, inasema kuwa “alipoifungua muhuri ya saba,” ndipo Mapigo ya matarumbeta saba yatakaposhuka ulimwenguni. Hii inaelezea matukio ambayo yatatokea katika wakati wa nne kama yalivyoandikwa katika Ufunuo sura ya 6, yaani wakati wa farasi wa kijivujivu. Hivyo, pasipo kuzifahamu nyakati saba zilizopangwa na Mungu, basi huwezi kuyafahamu Mapigo ya matarumbeta saba. Ili kulifahamu Neno la Ufunuo kwa ukamilifu wake wote tunapaswa kwanza kutambua na kuamini katika injili ya maji na Roho ambayo Mungu ametupatia. 
Neno la Mungu katika Ufunuo sura ya 6 linatoa mpangilio wa jinsi Mungu alivyopanga wakati alipomuumba mwanadamu. Mungu ameugawa mwanzo na mwisho wa mwanadamu katika nyakati saba tofauti.
Nyakati hizo ni: kwanza, wakati wa farasi mweupe; pili, wakati wa farasi mwekundu; tatu, wakati wa farasi mweusi; nne, wakati wa farasi wa kijivujivu; tano, wakati wa kuuawa kwa kuifia-dini na kunyakuliwa kwa watakatifu; sita, wakati wa maangamizi ya ulimwengu; na saba, wakati wa Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya. Tunaamini na kutii kwamba Mungu ameugawa mpango wake kwa mwanadamu katika nyakati hizi saba. Kwa sasa, ulimwengu upo katika kipindi cha farasi mweusi baada ya kuwa umeshazipita nyakati za farasi mweupe na farasi mwekundu.
Maandiko yanatueleza kuwa wakati huu ambapo sasa tunaishi ni wakati wa njaa. Lakini wakati wa farasi wa kijivujivu unakaribia pia. Baada ya kuwasili kwa wakati wa farasi wa kijivujivu basi utafuatiwa na wakati wa kuuawa kwa watakatifu na kuifia-dini na kuingia katika kipindi cha miaka saba ya Dhiki Kuu. Kipindi hiki cha mateso na mauaji ya kuifia-dini ni kipindi cha farasi wa kijivujivu.
“Na alipoifungua ile muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! Nikaona, na tazama farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.” Hiki kifungu cha maandiko kinachosema, “Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue...hayawani wa nchi” kina maanisha kuwa Mpinga Kristo atainuka katika wakati au kipindi cha farasi wa kijivujivu na atawaua watakatifu ambao wataifia-dini.
Matukio ambayo yatajitokeza katika wakati wa farasi wa kijivujivu yameandikwa katika Ufunuo 8:1-7. Maelezo hayo yameandikwa hivi: “Hata alipoifungua muhuri ya saba, kukawa kimya mbinguni kama muda wa nusu saa. Nami nikawaona wale malaika saba wasimamao mbele za Mungu, nao wakapewa baragumu saba. Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi. Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika. Na huyo malaika akakitwaa kile chetezo, akakijaza moto wa madhabahu, akautupa juu ya nchi, kukawa radi na sauti na umeme na tetemeko la nchi. Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari ili wazipige. Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea.”
Maelezo hayo hapo juu kuhusu Mapigo ya matarumbeta saba katika Ufunuo sura ya 8 yanaeleza ukweli wa wakati wa farasi wa kijivujivu uliozungumziwa katika Ufunuo sura ya 6. Neno hili linaeleza kwa kina juu ya kutokea kwa Mpinga Kristo na mapigo ya matarumbeta saba na mabakuli saba ambayo yatajitokeza wakati wa farasi wa kijivujivu.
Kwa upande mwingine, sura ya 4 na 5 inatueleza kuwa Yesu Kristo atatawala juu ya ulimwengu na yale yote yatakayokuja akiwa kama Mungu, na kwamba mpango mzima wa Baba utatimizwa na Yesu Kristo kama Mungu. Hivyo, kwa kupitia Ufunuo sura ya 4 na 5 tunatambua jinsi Yesu alivyo Mungu Mwenyezi na jinsi alivyo na nguvu.
Ufunuo sura ya 8 inatueleza kuwa: “Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari ili wazipige. Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea.” Utakapowadia wakati wa farasi wa kijivujivu, theluthi ya misitu ya dunia itaungua na kuteketea, na yatafuata mapigo mengine zaidi.
Pigo la tarumbeta la kwanza litasababisha kuteketea kwa theluthi ya misitu na nyasi. Tatizo hili litakapoukumba ulimwengu, basi misitu iliyosalia itaharibiwa kwa mchanganyiko wa ukungu na moshi utakaotokana na kuungua kwa theluthi ya ulimwengu, na ule moshi wake utalifanya jua lisiweze kupenyeza mionzi yake duniani. Mazao yataanguka, na ulimwengu mzima utaangukia katika njaa kali.
Katika wakati huu wa njaa, mshahara wa siku utaweza kununua kibaba cha ngano na vibaba vitatu vya shayiri. Kwa sasa ulimwengu unakabiliana na ujio wa hii njaa ya ajabu ya kipekee. Njaa hii ya ulimwengu itakuja kimwili na kiroho pia. Kwa sasa kuna njaa ya kiroho ambayo ipo katika ulimwengu wa sasa.
Siku hizi makanisa yamejazwa na Wakristo wa mazoea, hali wakiwa hawawezi kuushuhudia mkate wa kiroho na uzima wa injili ya maji na Roho ulimwenguni. Watu duniani kote, kuanzia Ulaya hadi Asia hadi katika bara la Marekani wanaishi katika kipindi cha maangamizi yao. Kwa kweli katika Ukristo wa leo kuna watu wachache sana wanaotoa mkate wa kiroho kwa nafsi zenye njaa.
Tunauelezea wakati wa farasi wa kijivujivu kama wakati wa kujitokeza kwa Mpinga Kristo. Katika wakati au kipindi hiki, majanga ya asili yatasababisha mkate na maji kuwa bidhaa haba, ambapo kila mtu ataweza walau kujikimu tu katika njaa nzito itakayokuwepo. Pamoja na kuwa ulimwengu utaendelea katika maendeleo yake ya kisayansi, ukweli ni kuwa kiwango cha maisha kitashuka na kuangukia katika umaskini mzito ambao haujawahi kutokea hapo kabla. Je, watu watakaokuwa wakiishi katika ulimwengu wa jinsi hiyo watakuwa na hamu ya kuendelea kuishi?
Katika kipindi hicho cha Dhiki, basi sisi sote ni lazima tuyakubali na kupokea kule kuuawa kwetu kwa ajili ya kuifia-dini na kisha kumtukuza Mungu kwa kuamini katika Neno la injili ya maji na Roho. Hivyo, watakatifu wanaoamini katika injili ya maji na Roho watampatia Mungu utukufu wote kwa kule kuuawa kwao kwa kuifia-dini. Kwa upande wake, Mungu atawainua kwenda mbinguni wale wote ambao waliuawa wakati wakiitetea imani yao na atawaalika katika karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo.
Mtume Paulo alisema kuwa alifanywa kuwa mtumishi wa Mungu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Mitume waliihubiri injili ya maji na Roho ili kwamba watu wengi waweze kuingia katika Ufalme wa Milenia.
Wakati wa kipindi cha Dhiki Kuu kutakuwa na watu miongoni mwa Waisraeli ambapo pia watauawa kwa kuifia-dini na kisha kunyakuliwa kwa kumwamini Yesu. Hivyo watakatifu watakuwa ni sehemu katika kipindi cha Dhiki Kuu katika kipindi au wakati wa farasi wa kijivujivu. Wakati Dhiki Kuu itakapokuja, basi kila mtu hapa ulimwenguni atakuwa akimtarajia mtu fulani ambaye ataleta utaratibu na amani kwa ulimwengu uliokumbwa na matatizo. Watamtafuta na kumtamani yeye atakayeweza kutatua matatizo yaliyoletwa na majanga ya kiasili, na ambaye atatatua matatizo mengine ya kisiasa, kiuchumi, na kidini. Hapo ndipo yule Mpinga Kristo atakapoinuka.
Hivi karibuni kuna mwandishi wa Kijapani ambaye ameandika mfululizo wa vitabu vinavyoitwa Hadithi ya Warumi, ambavyo havina kitu chochote zaidi ya kuwasifia watawala wa Kirumi. Madai makuu ya mwandishi ni kwamba muda si mrefu ulimwengu utahitaji kiongozi ambaye ataweza kuwa na nguvu kamilifu. Kuna watu wengi sana ambao walikubaliana na mwandishi huyo. Katika kipindi cha Dhiki Kuu, watu watahitaji kuwepo kwa mtawala mwenye nguvu atakayeweza kuutawala ulimwengu wote kwa mkono wa chuma—na si watawala wengi ambao kila mmoja ana utawala wake, bali mtawala mmoja tu mwenye nguvu ya kuutawala ulimwengu wote.
Kwa sasa, ulimwengu umegawanyika katika mataifa mengi na kila taifa lina kiongozi wake. Lakini katika nyakati za mwisho, watu watahitaji kiongozi wa kiroho wa dunia ambaye atatatua kikamilifu matatizo yao yote. Kwa sasa ulimwengu unamsubiri kiongozi huyu, yaani Mpinga Kristo ambaye atautawala ulimwengu mzima.
Biblia inatueleza kuwa wakati wa farasi wa kijivujivu utakapowadia, basi Mpinga Kristo atatokea akiwa na nguvu kubwa na atamtiisha kila mtu chini ya utawala wake. Pia Biblia inatueleza kuwa wakati wa farasi wa kijivujivu utakapowadia, basi moto utaishukia dunia na kuteketeza theluthi ya misitu ya dunia. Na wakati huu utakapowadia, basi Mpinga Kristo atatawala juu ya ulimwengu na kwamba hakuna atakayeweza kununua wala kuuza pasipokuwa na alama ya huyo Mpinga Kristo. Katika kipindi hiki watakatifu watauawa na kuifia-dini kwa kukataa kupokea alama ya huyo Mpinga-Kristo na kuabudu sanamu, na kisha watakatifu hao watafufuliwa na kunyakuliwa. Kipindi au wakati wa farasi wa kijivujivu utakapoisha, basi wakati wa Ufalme wa Milenia utaanza.
Bwana alituambia kuwa maangamizi ya ulimwengu huu na Dhiki Kuu vitakuja kama mwizi. Hivyo, ni lazima tuiandae imani itakayoweza kushinda majaribu yote ya Dhiki Kuu na maangamizi. Maandalizi haya yanawezekana kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Lakini kwa wale wasiojiandaa, basi mapigo yote na maangamizi yatawaangukia wale wote wasioamini katika injili ya maji na Roho.
Hivyo, ni lazima tuelewe vizuri na kuamini kwamba wakati wa sasa ni wakati wa farasi mweusi. Na kwamba ni lazima tuamini katika injili ya maji na Roho na kujiandaa kwa yatakayokuja kabla ile siku ya mwisho haijawadia.
Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho watanyakuliwa kwa kule kuuawa kwao kwa kuifia-dini. Wale walio matajiri hawataendelea kuishi kwa starehe wala wale walio maskini hawataendelea kuishi katika umaskini wao. Hivyo, hatupaswi kujivuna wala kuwa na huzuni kwa mambo ambayo yanatokea hivi sasa kwa maana tunaamini kuwa wakati wa farasi wa kijivujivu umekaribia na kwamba watakatifu wote wataweza kuuawa na kuifia-dini.
Kwa nyakati mbalimbali tumewaona baadhi ya watu ambao wanasababisha mkanganyiko mkubwa kwa kuchanganua juu ya muda ambapo Kristo atarudi na kufikia hatua ya kutangaza siku yao maalum na saa ambapo Bwana atakuja mara ya pili, na kwa sababu hiyo wamekuwa wakiwapoteza watu wengi kwa maelezo yao. Lakini kwa mujibu wa Biblia, kurudi kwa Kristo hakutatokea hadi itakapopigwa tarumbeta ya saba. Hivyo, hatupaswi kufanya makosa ya kulifanyia mahesabu Neno la Biblia na kisha kutangaza tarehe yetu binafsi juu ya kurudi kwa Bwana.
Pia tunapaswa kujihadhari na wale ambao wanadai kuwa wameiona tarehe ya kurudi kwa Kristo katika ndoto au maono. Kwa kweli ndoto zao si lolote bali ni ndoto za kawaida. Lakini kwa kuwa Bwana anatueleza kuhusu wakati wa kunyakuliwa kwa kupitia Neno lake, basi sisi tunapaswa kuliamini Neno lake.
Wakati wa farasi wa kijivujivu utakapowadia, ambao ni wakati wa nne katika Ufunuo sura ya 6, basi wafia-dini watainuka pamoja na mapigo ya matarumbeta saba, na kisha ufufuo na kunyakuliwa kwa watakatifu kutafuata.
Ni muhimu tukafahamu kuwa hivi sasa tunaishi katika wakati wa nne kati ya zile nyakati saba zilizopangwa na Mungu. Ni lazima tutambue kuwa wakati wa sasa ni wakati wa farasi mweusi. Tutakapofahamu hivyo, basi tunaweza kuipanda mbegu ya injili ya maji na Roho, na kwa kuipanda mbegu hiyo tutaweza kuvuna wakati wa farasi wa kijivujivu utakapowadia.
Katika ulimwengu wa asili ulioumbwa na Mungu kuna mimea ambayo inaweza kuchipua, ikatoa maua, na kisha kuzaa matunda katika muda wa wiki moja tu. Kama ilivyo mimea iliyoko jangwani, basi wakati wa farasi wa kijivujivu utakapowadia basi wale waliookolewa kwa kuamini katika injili ya maji na Roho ambayo tunaihubiri watauawa na kuifia-dini, na kisha wataungana nasi katika ufufuo na kunyakuliwa ambavyo Bwana ameviruhusu kwa ajili yetu. Katika kipindi cha Mateso kutakuwa na watu wengi wanaoamini katika injili ya maji na Roho kuliko hivi sasa. Kwa maneno mengine, kutakuwa na watu wengi ambao watauawa na kuifia-dini kwa ajili ya imani yao katika injili ya maji na Roho.
Neno la Ufunuo haliweki ukomo wa wokovu kwa watu wa Israeli. Ikiwa mtu anaamini kuwa Ufunuo umewekwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya Waisraeli peke yao, basi mtu huyo ni vema afahamu kuwa anafanya kosa kubwa sana. Kwa nini? Kwa sababu wakati wa Ufunuo utakapowadia, kuna idadi kubwa sana ya Wamataifa ambao wataokolewa kwa kuamini katika injili ya maji na Roho na kuuawa kwa kuifia-dini katika kuilinda imani yao. Kwa hiyo, haijalishi kwamba una ufahamu mkubwa katika Neno la Ufunuo au la, ukweli ni kuwa imani katika injili ya maji na Roho italeta tofauti kubwa katika imani yako.
Hivyo, ni lazima utambue kuwa ni makosa kwa Wakristo wa leo kuamini juu ya fundisho la kiimani la kunyakuliwa kabla ya dhiki. Biblia inatueleza kuwa mauaji ya wafia-dini kwa watakatifu yatatokea katikati ya muda mfupi wa miaka saba ya Dhiki Kuu, na kwamba kunyakuliwa kwao kutatokea baada ya haya. Ni lazima tulitatue na kulisoma Neno la Ufunuo kama lilivyoandikwa sura kwa sura na aya kwa aya ndani ya injili ya maji na Roho. Kwa kufanya hivyo tunaweza kusahihisha ufahamu wetu juu ya Neno la Ufunuo.
Ufunuo sura ya 7 inatueleza kuwa watu wengi wasiohesabika miongoni mwa Wamataifa pia watapokea wokovu kwa imani yao na kisha watauawa na kuifia-dini kwa ajili ya imani yao. Ni lazima tuiamini Biblia kama ilivyoandikwa—na wala si kuamini nadharia za kunyakuliwa kabla ya dhiki wala kunyakuliwa baada ya dhiki wala katika amilenia (yaani kwamba hakuna Ufalme wa Milenia) na badala yake tunapaswa kuamini katika nyakati saba zilizopangwa na Mungu.
Sura ya 1 ya Neno la Ufunuo ni Utangulizi, sura ya 2 na ya 3 inazungumzia juu ya mauaji ya watakatifu kwa kuifia-dini, na sura ya 4 inatueleza kuwa Yesu Kristo ni Mungu na kwamba anaketi katika kiti cha enzi cha Mungu. Sura ya 5 inatuonyesha jinsi Yesu atakavyoutimiza mpango wote wa Mungu Baba, na sura ya 6 inaeleza juu ya mambo yote ya msingi kuhusiana na nyakati saba zilizopangwa na Mungu. Mipango hii yote imeelezwa katika Neno la Ufunuo.
Kama Neno la Ufunuo linavyotueleza, “Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa,” na kuendelea, watakatifu wanaishi katika tumaini la ufufuo na Ufalme wa Milenia.
Ufunuo 8:10-11 inaelezea juu ya pigo jingine: “Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya theluthi ya mito, na juu ya chemchemi za maji. Na jina lake ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalitiwa uchungu.” Hapa inaelezwa kuwa nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa iliangukia katika mito na chemchemi. Hii nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ina maanisha ni kimwondo. Kwa maneno mengine, kadri mbingu zinavyotikisika basi nyota zitagongana na vipande vinavyomeguka toka katika nyota hizo zinazogongana zitaangukia duniani.
Ufunuo 8:12-13 inaendelea kueleza juu ya pigo jingine: “Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na theluthi ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, wala usiku vivyo hivyo. Kisha nikaona, nikasikia tai mmoja akiruka katikati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya nchi! Kwa sababu ya sauti zisaliazo za baragumu za malaika watatu, walio tayari kupiga” Hii inatueleza kuwa theluthi ya ulimwengu utatiwa giza kama vile mchana unavyogeuka kuwa usiku.
Hivyo, wakati mapigo ya yale matarumbeta saba yatakapoanza, basi ni hakika kuwa wewe na mimi tutakuwa tukiishi katikati ya hayo mapigo. Lakini watakatifu watakaokuwa hai watauawa mara moja na kuifia-dini, na watamshinda Shetani kwa imani yao.
Ikiwa unazifahamu vizuri nyakati saba katika Ufunuo sura ya 6, basi utakuwa na ufahamu mzuri wa yale unayopaswa kuyafanya na pia utaifahamu aina ya imani ambayo unapaswa kuwa nayo katika wakati wa sasa. Kwa kuwa wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho watauawa na kuifia dini katika kipindi cha Ufunuo na kwamba wanapaswa kukutana na kipindi hiki hali wakiwa na tumaini kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Watakatifu wanapokuwa wakiishi hapa ulimwenguni ni lazima wajiandae kwa ajili ya kuuawa na kuifia-dini katika nyakati za mwisho kwa ajili ya imani yao, na pia ni lazima wajitaabishe sana katika kuueneza Ufalme wa Mungu kwa kuieneza imani hii.
Je, unafahamu na kuamini katika nyakati saba zilizopangwa na Mungu? Je, unaweza kutanabaisha kuwa sasa tunaishi katika wakati wa farasi mweusi? Ikiwa huiamini na wala huifahamu injili ya maji na Roho sasa, basi ni hakika kuwa hutaweza kuyakwepa mateso ambayo yataushukia ulimwengu huu. Hivyo, ni lazima ujiandae hivi sasa. Ili uweze kuwa na imani inayoweza kuyashinda mateso, basi kwanza kabisa unapaswa kupatanishwa dhambi zako zote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho na kisha ujiandae kuingia na kuishi katika Ufalme wa Milenia kwa kumpokea Roho Mtakatifu kama zawadi yako.
Hebu jiandae. Ikiwa unataka kuahirisha na halafu uje kuiamini injili ya maji na Roho wakati mapigo ya matarumbeta saba yatakapowadia, basi ni hakika kuwa utapata mateso mengi. Ni matumaini yangu kuwa mtaamini katika injili ya maji na Roho wakati huu ili muweze kuzaliwa tena upya na kuyaandaa maisha yenu ya baadaye kama watu wa Mungu.
Nyakati saba zilizopangwa na Mungu:
1.    Farasi mweupe: kipindi cha kuanza na kuendelea kwa injili ya maji na Roho.
2.    Farasi mwekundu: Kuharibika kwa amani na kuanza kwa wakati wa Shetani.
3.    Farasi mweusi: Wakati wa kipindi cha njaa ya kimwili na kiroho. Yaani wakati wa sasa.
4.    Farasi wa kijivujivu: Wakati wa mauaji ya watakatifu kwa kuifia-dini pamoja na kuinuka kwa Mpinga Kristo.
5.    Wakati wa ufufuo na kunyakuliwa kwa watakatifu, na wakati wa karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo.
6.    Wakati wa maangamizi ya ulimwengu wa kwanza.
7.    Wakati wa Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya vitakavyotawaliwa na Bwana na watakatifu wake.
Hizi ni nyakati saba zilizopangwa na Mungu. Wale wanaozifahamu nyakati hizi vizuri na wanaoamini katika injili ya maji na Roho ndio wale walioiandaa imani yao ili kuweza kuishi katika nyakati za mwisho. Ninatumaini na ninaomba ili kwamba wewe nawe uweze kuzitanabaisha nyakati hizi za imani ya kweli zilizopangwa na Mungu.