Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[7-1] Ni Nani Atakayeokolewa Wakati wa Dhiki Kuu? (Ufunuo 7:1-17)

(Ufunuo 7:1-17)
“Baada ya hayo nikaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za nchi, wakizizuia pepo nne za nchi, upepo usivume juu ya nchi, wala juu ya bahari, wala juu ya mti wowote. Nikaona malaika mwingine, akipanda kutoka mawio ya jua, mwenye muhuri ya Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao. Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu: 
Wa kabila la Yuda kumi na mbili elfu waliotiwa muhuri. 
Wa kabila la Reubeni kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Gadi kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Asheri kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Naftali kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Manase kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Simeoni kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Lawi kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Isakari kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Zabuloni kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Yusufu kumi na mbili elfu. 
Wa kabila la Benyamaini kumi na mbili elfu waliotiwa muhuri. Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo. Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti ch enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu, wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Nao wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.”
 

Mafafanuzi 
 
Aya ya 1: “Baada ya hayo nikaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za nchi, wakizizuia pepo nne za nchi, upepo usivume juu ya nchi, wala juu ya bahari, wala juu ya mti wowote.”
Hii inatuonyesha kuwa kuvuma au kutovuma kwa upepo wa mapigo kunategemea kikamilifu juu ya ruhusa ya Mungu. Mungu amekwisha amua kwamba atawaokoa watu 144,000 toka katika makabila ya Israeli na kuwafanya kuwa watu wake kabla ya kuiruhusu Dhiki Kuu hapa duniani.
 
Aya ya 2-3: “Nikaona malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, mwenye muhuri ya Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao.”
Katika vifungu hivi tunaona kuwa Mungu anawaamuru malaika wanne waliokuwa wamepewa kuidhuru nchi na bahari kwamba wasiidhuru nchi hadi Waisraeli 144,000 watakapokuwa wametiwa muhuri. Kwa maneno mengine, Mungu aliwaambia wale malaika kuwa wasidhuru hadi watu 12,000 watakapokuwa wamechaguliwa toka kila kabila la Israeli na hadi watakapokuwa wametiwa muhuri wa Mungu wa uzima katika vipaji vya nyuso zao. Hii ilikuwa ni amri maalum ya Mungu inayoonyesha jinsi Mungu anavyowajali watu wa Israeli.
 
Aya ya 4: “Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu”
Wale wote ambao watapigwa muhuri na Mungu watapokea ulinzi maalum toka kwa Mungu na baraka yake ya wokovu hata wakati wa Dhiki Kuu ya nyakati za mwisho.
 
Aya ya 5-9: “Wa kabila la Yuda kumi na mbili elfu waliotiwa muhuri. Wa kabila la Reubeni kumi na mbili elfu. Wa kabila la Gadi kumi na mbili elfu. Wa kabila la Asheri kumi na mbili elfu. Wa kabila la Naftali kumi na mbili elfu. Wa kabila la Manase kumi na mbili elfu. Wa kabila la Simeoni kumi na mbili elfu. Wa kabila la Lawi kumi na mbili elfu. Wa kabila la Isakari kumi na mbili elfu. Wa kabila la Zabuloni kumi na mbili elfu. Wa kabila la Yusufu kumi na mbili elfu. Wa kabila la Benyamaini kumi na mbili elfu waliotiwa muhuri. Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.”
Kifungu hiki kinatueleza idadi ya waliotiwa muhuri miongoni mwa watu wa Israeli—yaani watu 12,000 toka katika kila kabila la Israeli watatiwa muhuri wakiwa kama wapokeaji wa neema maalum ya Mungu. Mungu atawapatia wokovu watu 12,000 toka katika kila kabila la Israeli na atawafanya kuwa watu wake; neema hii maalum itatatolewa kwa usawa kwa kila kabila.
Kama Mungu alivyolipenda kila kabila la Israeli kwa usawa, basi vivyo hivyo aliwapatia baraka sawa ya kufanyika kuwa watu wake. Mungu aliwafunika Waisraeli kwa neema hii ili kuyatimiza Maneno yake aliyomwahidia Ibrahimu na uzao wake. Kama inavyoweza kuonekana, Mungu anatimiza kila kitu alichokiahidi na alichokipanga kwa mwanadamu.
Hii inatueleza kuwa idadi kuwa wa wamataifa pia wataokolewa katika kipindi cha Dhiki Kuu na watafanyika kuwa watu wa Mungu. Kwa maneno mengine, kutakuwa na idadi kubwa ya watu isiyoweza kuhesabiwa miongoni mwa wamataifa ambao watakombolewa pia toka katika dhambi zao kwa kuamini katika injili ya maji na Roho na kisha kuuawa kwa kuifia-dini kwa imani yao katika nyakati za mwisho. Hivyo ni lazima tukumbuke kuwa Mungu anatenda ili kuwafanya wamataifa kuwa watu wake hata katika ile siku yenyewe ya mwisho.
 
Aya ya 10-11: “wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo. Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti ch enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu,”
Mungu anaitoa neema yake ya wokovu hata katika nyakati za mwisho kwa Waisraeli na kwetu pia, sisi tulio wamataifa. Hivyo, Bwana wetu anastahili kusujudiwa, na kupokea sifa, na utukufu. Kwa watakatifu, hakuna kitu chochote kile bali Mungu ndiye msingi wa maombi na ibada yao.
 
Aya ya 12: “wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina.” 
Watumishi wote wa Mungu wanamsifu Bwana ambaye ni Mungu. Kwa kweli ni sahihi kabisa kwamba Mungu apokee sifa hizi zote na heshima. 
 
Aya ya 13-14: “Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Nao wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.”
Mungu atayakusanya mavuno yake ya mwisho baada ya kuwa ameuinua upepo wa Dhiki Kuu ili kuwafanya watakatifu kushinda kuuawa kwao kwa kuifia-dini na kwa sababu hiyo kuilinda imani yao ya kweli. 
Wakati wa ile miaka mitatu na nusu ya kwanza katika kipindi cha Dhiki Kuu utakapopita, watakatifu watateswa sana na Mpinga Kristo na watauawa na kuifia-dini kwa ajili ya kuilinda imani yao. Mateso haya ya kuuawa kwa kuifia dini yana kiwango tofauti na mateso mengine yoyote yale ambayo yametangulia katika Historia ya Kanisa; kwa kweli yatagharimu imani kamilifu ya watakatifu wanaomwamini Mungu hapa duniani. Kwa kweli kuuawa kwa kuifia-dini ni heshima kubwa kwa watakatifu. Watakatifu wanaweza kuionyesha imani yao ya kweli kwa Mungu kwa kupitia kuuawa na kuifia-dini. Katika nyakati za mwisho za Dhiki Kuu, watakatifu wote watailinda imani yao kwa kupitia kuuawa kwa kuifia-dini, watashiriki katika ufufuo na kunyakuliwa, na kisha watasimama mbele ya kiti cha enzi cha Mungu.
 
Aya ya 15-16: “Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote.”
Wale walio na imani ya kweli mbele za Mungu watauawa na kuifia-dini katika nyakati za mwisho za Dhiki Kuu ili kuilinda imani yao katika wokovu wa injili ya maji na Roho. Hivyo, Mungu atawapatia watakatifu wenye imani hiyo ulinzi na baraka maalum, na kisha atawakumbatia katika mikono yake.
Baada ya kuwa wamepigana na Mpinga Kristo na kisha kuuawa na kuifia-dini na kisha kufufuka, basi watakatifu hawatakufa tena kamwe wala hawatateseka kamwe katika Ufalme wa Mungu. Wataishi milele katika baraka iliyotolewa kwa watoto wa Mungu. Wale watakaoishi hali wakiwa wamekumbatiwa na mikono ya Mungu hawatapungukiwa chochote, na wala hawatateseka au kusumbuliwa kamwe na maovu. Kitakachokuwa kikiwangojea ni thawabu maalum ya Mungu, upendo, na utukufu ambavyo watapewa milele.
 
Aya ya 17: “Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.”
Mungu atakuwa ni Mchungaji wa milele wa watakatifu na atawapatia baraka zake za milele. Mungu atawaongoza watakatifu kwenda katika chemchemi ya maji ya uzima na kuwaruhusu kuumega mkate pamoja na Bwana mbele ya kiti cha enzi ili kuwapa thawabu kwa ajili ya mateso yote na kuuawa kwa kuifia-dini walikokupitia kwa ajili ya Bwana walipokuwa hapa duniani. Kwa kuwa watakatifu walipokuwa hapa duniani, waliamini katika injili ya maji na Roho, wakaishi maisha ya huduma kwa ajili ya utukufu wa Mungu, na wakauawa kwa ajili ya jina lake, basi Mungu atawaruhusu wale waliolinda imani yao kuishi milele katikati ya utukufu wake ndani ya Mbingu na Nchi Mpya, na katika Ufalme wa Mungu. Halleluya! Bwana wetu Asifiwe!