Search

Mahubiri

Somo la 11: Maskani

[11-9] Imani Inayodhihirishwa Katika Madhabahu ya Sadaka ya Kuteketezwa (Kutoka 27:1-8)

Imani Inayodhihirishwa Katika Madhabahu ya Sadaka ya Kuteketezwa
(Kutoka 27:1-8)
“Nawe fanya madhabahu ya mshita; urefu wake utakuwa ni dhiraa tano; hiyo madhabahu itakuwa mraba; na kwenda juu kwake kutakuwa dhiraa tatu. Nawe fanya pembe nne katika pembe zake nne; hizo pembe zitakuwa za kitu kimoja na madhabahu; nawe utayafunika shaba. Na vyombo vyake vya kuyaondoa majivu yake utavifanya, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote utavifanya vya shaba. Nawe uifanyie hiyo madhabahu wavu wa shaba; kisha utie pete nne za shaba katika hizo pembe nne za ule wavu. Nawe tia huo wavu chini ya kizingo kiizungukacho madhabahu upande wa chini, ili huo wavu ufikilie katikati ya hiyo madhabahu. Nawe fanya miti kwa ajili ya madhabahu, miti ya mshita, na kuifunika shaba. Na hiyo miti itatiwa katika pete, na ile miti itakuwa katika pande mbili za madhabahu, wakati wa kuichukua. Uifanye ya mbao, yenye mvungu ndani yake; kama ulivyoonyeshwa mlimani, ndivyo watakavyoifanya.”
 
 
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa
Nitapenda kujadili juu ya imani inayodhihirishwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Wakati watu wa Israeli walipovunja mojawapo ya kanuni 613 za Sheria ya Mungu na maagizo yake ambayo walipaswa kuyatii katika maisha yao ya kila siku, na walipozitambua dhambi zao walimtolea Mungu sadaka isiyo na mawaa kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa uliowekwa na Mungu. Mahali walipozitolea sadaka hizi ni katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Kwa maneno mengine, watu wa Israeli, walipokea ondoleo lao la dhambi kwa kuiweka mikono yao katika kichwa cha mnyama wa sadaka asiye na mawaa, na kwa kukata koo la mnyama na kuikinga damu yake, na kuiweka damu hiyo katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kisha kuimimina ardhini damu iliyosalia, na hatimaye kumchoma mnyama huyo katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
 


Maana ya Kiroho ya Madhabahu ya Sadaka ya Kuteketezwa ni Ipi?

 
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, yenye vipimo vya mita 2.25 (futi 7.5) kwa urefu na upana na mita 1.35 (futi 4.5) kwa mwimo, ilitengenezwa kwa mti wa mshita na kisha ikafunikwa kwa shaba. Wakati waisraeli walipoiangalia madhabahu hii ya sadaka ya kuteketezwa, ndipo walitambua kuwa wao walikuwa wamefungwa katika kifungo cha hukumu na adhabu na kuwa wasingeweza kuikwepa hukumu yao. Na kama ambavyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa alivyouawa, ndipo walipotambua kuwa, hata wao walistahili kufa kwa sababu ya dhambi zao. Pia waliamini kuwa Masihi atakuja hapa duniani na atazitowesha dhambi zao kwa kuadhibiwa na kuuawa kama ilivyokuwa kwa mnyama wa sadaka ya kuteketezwa kwa sababu ya dhambi zao.
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ilikuwa ni kivuli cha Yesu Kristo Mwokozi wetu. Kama ambavyo wanyama wasio na mawaa walivyouawa kwa kuwekewa mikono na kisha kumwaga damu yao, Yesu Kristo alikuja kwetu kama Mwana wa Mungu na akabeba adhabu ya dhambi zetu zote. Kama ambavyo sadaka ya kuteketezwa ya Agano la Kale ilivyopokea dhambi zote kwa kuwekewa mikono na kumwaga damu, Yesu alizipokea dhambi zote za ulimwengu zilizopelekwa kwake kwa kubatizwa na Yohana, na akabeba adhabu ya dhambi hizi kwa kuimwaga damu yake Msalabani.
Kwa njia hii, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa inatuonyesha sisi kuwa Yesu Kristo alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo wake, alikufa Msalabani, akafufuka toka kwa wafu, na kwa hiyo ametuokoa sisi.
 

Ili Kusamehewa Dhambi Zao, Waisraeli Walipaswa Kutoa Sadaka Zao Za Kuteketezwa Katika Madhabahu ya Sadaka ya Kuteketezwa
 
Tunapoiangalia sura ya 4 ya Kitabu cha Mambo ya Walawi, tunaona kwamba, kila ilipotokea kuwa kuhani mtiwa mafuta, kusanyiko zima la Israeli, mtawala, au mtu yeyote wa kawaida alipotenda dhambi, walipokea ondoleo lao la dhambi kwa kuleta sadaka ya kuteketezwa kwa Mungu, wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake, wakamchinja, wakakinga damu yake, na wakaipeleka damu hiyo katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kisha wakaitoa kwa Mungu. 
Kusema kweli, kwa kuwa madhabahu hii ya sadaka ya kuteketezwa ndipo mahali ambapo waisraeli walitoa sadaka zao za dhambi kila siku, kwa kweli hakuna siku iliyopita bila mahali hapa kuwa na shughuli nyingi. Waisraeli waliotaka kujikomboa toka katika dhambi zao waliandaa mnyama asiye na mawaa na wakampelekea Mungu katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kama sadaka yao ya kuteketezwa. Wenye dhambi walizipeleka dhambi zao zote katika mnyama wa kuteketezwa kwa kuiweka mikono yao juu ya kichwa chake, na kama hukumu ya dhambi hizi, waliikinga damu yake kwa kuchinja koo la mnyama huyo. Kisha makuhani waliitia hii damu ya sadaka ya kuteketezwa katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na wakazichoma nyama na mafuta juu ya madhabahu. Hivi ndivyo watu wa Israeli walivyopokea ondoleo lao la dhambi.
Bila kujali kuwa ni nani aliyekuwa amefanya dhambi, kwamba ni kiongozi wa watu wa Israeli, Kuhani Mkuu, kuhani wa kawaida, jamii nzima, au mtu mwingine yeyote, hao wote walitakiwa kupokea ondoleo la dhambi zao kwa kumleta mnyama wa sadaka ya kuteketezwa, kama vile fahari la ng’ombe, mbuzi, au kondoo dume, na kisha kuvitoa kwa Mungu kama sadaka ya kuteketezwa.
Wenye dhambi au wawakilishi wao walipaswa kuweka mikono yao juu ya mwanasadaka wa kuteketezwa, kumchinja, na kisha kuiweka damu yake katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na kuimwaga damu iliyosalia ardhini, hatimaye kuyachoma mafuta ya mnyama wa sadaka ya kuteketezwa ili waweze kusamehewa dhambi zao. Kwa hiyo, wengi walipaswa kuleta wanyama wao wa kuteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, wakaweka mikono yao juu ya vichwa vya wanyama wa sadaka, wakakinga damu yao na kisha wakampatia kuhani.
Wakati sadaka ilipokuwa ikitolewa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, sadaka hizi za kuteketezwa zilipaswa kuwa zisizo na mawaa. Na wakati wenye dhambi walipotoa sadaka zao kwa Mungu, walitakiwa kuhakikisha kuwa wanaleta wanyama wasio na mawaa mbele za Mungu, na ni kwa kuiweka mikono yao juu ya vichwa vya wanyama hawa wa sadaka ya kuteketezwa wasio na mawaa ndipo dhambi zao zilipopitishwa kwa wanyama hao. Kwa hiyo, hakuna ambacho kilipaswa kuachwa wakati wa kutoa sadaka ya kuteketezwa.
Kwa kawaida, mtu aliyekuwa amefanya dhambi alipaswa kuweka mikono yake mwenyewe juu ya kichwa cha mnyama wa kuteketezwa, lakini ilipotokea kuwa jamii nzima ya Israeli imefanya dhambi, wazee wawakilishi wa hiyo jamii waliilaza mikono yao juu ya mnyama wa sadaka ya kuteketezwa (Mambo ya Walawi 4:15). Kwa kweli, mnyama wa sadaka ambaye kichwa chake kiliwekewa mikono aliuawa kwa kuchinjwa koo lake na kisha kuikinga damu yake. Na mwishowe, mnyama huyo aliteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
Moshi wa nyama iliyochomwa, mafuta, na kuni kwa kawaida vilipajaza mahali pale palipoizunguka madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na pembe zake na ardhi chini ya ile meza vyote vililoweshwa kwa damu za wanyama wa kuteketezwa. Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa palikuwa ni mahali pa ondoleo la dhambi ambapo sadaka za kuteketezwa zilizotolewa kwa Mungu ili kuzisafisha dhambi za watu wa Israeli.
Madhabahu hii ya sadaka ya kuteketezwa, ambapo moshi haukuisha, ilikuwa ni mraba wenye vipimo vya mita 2.25 (futi 7.5) kwa urefu na upana, pia ilikuwa na kipimo cha mita 1.35 (futi 4.5) kwa mwimo. Kichanja cha shaba kiliwekwa katikatika, na moshi ulifuka toka katika sadaka zilizochomwa juu ya kichanja hicho. Kwa hiyo, mahali ambapo sadaka ziliteketezwa na kutolewa kwa Mungu ilikuwa ni madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
 
 
Vyombo Vyote Vya Madhabahu ya Sadaka ya Kuteketezwa Vilitengenezwa Kwa Shaba
 
Vyombo vya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa vilivyotumika kuweka na kuondoa majivu vyote vilitengenezwa kwa shaba. Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa yenyewe ilitengenezwa kwa mti wa mshita na kisha ikafunikwa kwa shaba, na kwa hiyo madhabahu na vyombo vyake vyote vilitengenezwa kwa shaba.
Shaba hii ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ina maana kamili ya kiroho. Shaba inamaanisha hukumu ya dhambi mbele za Mungu. Kwa hiyo, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ni mahali panapotuonyesha vizuri kwamba wenye dhambi kwa hakika watahukumiwa kwa dhambi zao. Kwa hakika, Mungu atawaadhibu watu kwa dhambi zao pasipo kushindwa. Madhabahu hii ya sadaka ya kuteketezwa ni mahali ambapo wanyama wa sadaka ya kuteketezwa walihukumiwa kwa ajili ya wenye dhambi kwa kuteketezwa, madhabahu hii na vyombo vyake vyote vilitengenezwa kwa shaba; kwa hiyo, vitu hivi vinatueleza sisi kuwa kwa hakika kila dhambi inahusisha hukumu yake.
Madhabahu inatuonyesha sisi kuwa kwa sababu ya dhambi zao, watu wamefungwa kuadhibiwa na kisha kuuawa, lakini kwa kuwaleta wanyama wao wa kuteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kumpatia Mungu, wanaweza kuoshwa dhambi zao, kupokea ondoleo la dhambi, na kisha kuishi tena kwa upya. Hapa, sadaka zilizotekekezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa vyote vinatueleza kuwa ubatizo wa Yesu Kristo na kule kuimwaga damu yake kumezisamehe dhambi za waamini. Kwa hiyo, imani hii iliyotoa sadaka ya kuteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa inaendelezwa katika kipindi cha Agano Jipya kama imani katika ubatizo na damu ya Yesu Kristo.
Tunapomwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wetu, ni lazima tumpe Mungu imani yetu inayoamini katika ubatizo na damu ya Yesu kama ondoleo la dhambi zetu zote. Katika Agano la Kale, imani hii inahusianishwa na imani inayofungua na kuingia katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania lililokuwa limefumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa.
 


Sadaka Zote Ambazo Ziliteketezwa Katika Madhabahu ya Sadaka ya Kuteketezwa Zinamaanisha Yesu Kristo

MsalabaYesu Kristo alifanya nini alipokuja hapa duniani? Tulikuwa wenye dhambi; tulikuwa tumetenda dhambi kinyume na Mungu na tulikuwa tumevunja Sheria na maagizo yake. Lakini ili kuzitowesha dhambi zetu, Yesu Kristo alibatizwa na Yohana na akazichukua dhambi za ulimwengu katika mwili wake, na kwa hiyo akaimwaga damu yake Msalabani. Kamba ambavyo sadaka ya kuteketezwa ilizibeba dhambi za waisraeli kwa kuwekewa mikono juu yake, na kisha kuuawa na kuchomwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, vivyo hivyo Yesu Kristo alikuja hapa duniani kama sadaka ya kuteketezwa isiyo na mawaa, alibatizwa, ndipo akaweza kuimwaga damu yake ya kuteketezwa na akafa Msalabani badala yetu. Kwa kupigiliwa misumari katika mikono yote miwili na miguu yote na kwa kuimwaga damu yake, Bwana wetu alibeba hukumu ya adhabu kwa dhambi zetu zote ili sisi tusiadhibiwe kwa dhambi zetu. Kwa hiyo, ametuokoa toka katika dhambi zetu zote na adhabu.
Je, Yesu Kristo ambaye amefanyika kiini halisi cha madhabahu hii ya kuteketezwa, amefanya nini alipokuja hapa duniani? Yesu Kristo ametuokoa kwa kuzichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo wake, akasulubiwa na kufa Msalabani, na kisha akafufuka tena toka kwa wafu. Bwana wetu alikuja hapa duniani akautimiza wokovu wetu kamili, na kisha akapaa kwenda katika Ufalme wa Mbinguni.
 

Sisi Ambao Hatuwezi Kujisaidia Bali Tutakaotenda Dhambi Kila Siku
 
Pia kuna maana nyingine ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ambayo ni “kupaa.” Kusema kweli, wewe na mimi tunatenda dhambi kila siku. Kwa hiyo, inatulazima kutoa sadaka zetu za kuteketezwa kila wakati mbele za Mungu, na kwa sababu ya hali hii, moshi wa adhabu ya dhambi zetu kila siku unapaa kwenda kwa Mungu. Je, kuna siku yeyote ambayo hautendi dhambi bali unaishi kiukamilifu? Sadaka ya kuteketezwa ya watu wa Israeli ilitolewa kila siku hadi pale makuhani walipochoka kabisa kuzitoa sadaka hizi ambazo zilileteleza msamaha kwa dhambi za waisraeli wengi. Kwa sababu watu wa Israeli waliivunja Sheria na wakafanya dhambi kinyume na Mungu kila siku, vivyo hivyo walipaswa kutoa sadaka zao za kuteketezwa kila siku.
Musa, akiliwakilisha taifa la Israeli, alizitamka kanuni 613 za Sheria na amri za Mungu kwa waisraeli: “Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu. Nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.” (Kutoka 19:5-6).
Kisha watu wa Israeli wakaahidi, “Hayo yote aliyoyasema BWANA tutayatenda” (Kutoka 19:8). Hivyo watu wa Israeli walitaka kumtambua na kumwamini huyu Mungu aliyemtokea Musa na akaongea nao kwa kupitia Musa kama Mungu wao halisi, na walitaka Mungu huyu awalinde. Pia walipenda kufanyika si tu hazina maalum ya Mungu, bali pia ufalme wa makuhani na taifa takatifu la Mungu kwa kuyatunza yale ambayo Mungu aliwaambia. Kwa hiyo, walijitahidi kuzitunza amri zote za Mungu ambazo aliwapatia.
Je, Mungu alifahamu mapema kuwa waisraeli watatenda dhambi? Kwa kweli alifahamu. Hii ndiyo sababu Mungu alimuita Musa katika Mlima Sinai, akamwonyesha Hema Takatifu la Kukutania katika maono, akamwelezea juu ya muundo wake kwa kina, akamweleza kulijenga, na kisha akamfanya Musa kulijenga kama alivyomwamuru. Pia akaanzisha utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa ambao kwa huo sadaka zilipaswa kutolewa katika hili Hema Takatifu la Kukutania.
Wakati watu wa Israeli walipotakiwa kutoa sadaka ya dhambi kwa Mungu, walitakiwa kumleta fahari, au kondoo, au mbuzi, au kinda la njiwa, au njiwa, wasio na mawaa; walitakiwa kuhakikisha kuwa wanazipitisha dhambi zao katika sadaka zao za kuteketezwa kwa kuiweka mikono yao juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka (Mambo ya Walawi 1:1-4). Na kisha kuikinga damu yake kwa kuchinja koo la mnyama na kisha kuwapatia makuhani hiyo damu. Kisha makuhani wao waliichukua damu hii, wakaiweka katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, wakaimwaga damu iliyosalia ardhini, wakamkata mnyama wa sadaka katika vipande, wakaweka vipande hivi katika madhabahu, kisha wakavitoa vipande hivyo kwa Mungu kwa kuviteketeza kwa moto.
Hivi ndivyo ambavyo waisraeli waliweza kusamehewa dhambi zao. Wakati sadaka ilipokuwa ikiteketezwa, hawakuteketeza nyama yake tu, bali waliteketeza pia mafuta yote toka katika utumbo na maini. Kwa njia hii Mungu alizisamehe dhambi za waisraeli.
 


Njia Pekee ya Kupokea Ondoleo la Dhambi Zote

 
Tunapojiangalia sisi wenyewe, ndipo tunapoweza sisi sote kutambua kuwa hatuwezi kukwepa bali tutajikuta tunatenda dhambi wakati wote. Tunaishi maisha yetu kila wakati tukitenda dhambi. Tunafanya dhambi nyingi zisizohesabika kwa makusudi mbalimbali, pengine kwa sababu sisi ni dhaifu, tuna mawaa mengi, ni wachoyo sana, au tuna nguvu kupita kiasi. Hata miongoni mwa wale wanaomwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wao, hakuna hata mmoja asiyetenda dhambi.
Njia pekee kwetu sisi ambao tunafanya dhambi kama hivi hata pale tunapomwamini Mungu, ili tuweze kuoshwa dhambi zetu na kuokolewa ni kwa kuamini katika ubatizo wa Yesu Kristo. Yeye ni Mungu mwenyewe aliyekuja kwa njia ya maji na damu (1 Yohana 5:6); alikuja hapa duniani kama sadaka ya kuteketezwa kwa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Wakati huyu Yesu alipozichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kubatizwa na kulipa mshahara wa dhambi zetu kwa kuimwaga damu yake na kufa Msalabani, ni kwa nini basi tusipokee ondoleo la dhambi kwa kupitia imani? Kwa sababu ya wokovu wa Masihi wetu Yesu Kristo, mimi na wewe tuliweza kupokea ondoleo la dhambi zetu zote mara moja kwa kupitia imani.
Ingawa kwa kweli tunatenda dhambi kila wakati, kwa sababu ya wokovu wa ubatizo na damu ya Yesu Kristo uliotimizwa wakati Yesu alipokuja hapa duniani, sisi tuliweza kuwa huru toka katika dhambi zetu zote. Bwana wetu alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa ubatizo wake, akazibeba dhambi za ulimwengu Msalabani na akasulubiwa, na kwa hiyo ametukomboa sisi sote toka katika dhambi zetu kikamilifu. Kwa kubatizwa kwa ajili ya dhambi zetu, kwa kuibeba adhabu ya dhambi zetu zote kwa kusulubiwa kwake, na kwa kufufuka tena toka kwa wafu, kwa kweli ametuokoa sisi sote tunaouamini ukweli huu. Ingawa tusingeweza kukwepa bali kuadhibiwa kwa sababu ya dhambi zetu, kwa sababu ya upendo wa wokovu na rehema ambazo Yesu ametupatia kwa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu, wewe na mimi tumeokolewa kwa imani. Kwa maneno mengine, Mungu ametuokoa sisi toka katika dhambi zetu. Ni kwa kumwamini Yesu ndio maana tumekombolewa toka katika dhambi zetu zote. Hivi ndivyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa inavyotueleza.
Unaweza kufikiria kuwa ndani ya Hema Takatifu la Kukutania kila kitu kilikuwa kizuri, lakini kama ungeingia katika ua wake, ungekutana na madhari isiyotarajiwa na yenye kuhuzunisha. Madhabahu ya shaba ya sadaka ya kuteketezwa, iliyokuwa na muundo mraba, itakuwa ni ya kutisha kwa sababu ya kutoa moshi na moto wakati wote. Madhabahu ya shaba itakuwa ikiwasubiri wenye dhambi, ardhi yake itakuwa imeloanishwa kwa damu, na kila mtu atatambua kuwa mahali hapa ni mahali pa adhabu kwa dhambi. Kwa kuwa mahali hapa ni mahali ambapo sadaka ya kuteketezwa ilitolewa kila siku, bila shaka utashangazwa na harufu ya kuungua kwa nyama na kuni.
Chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, damu itakuwa ikimiminika kama vile mto. Kila wakati waisraeli walipofanya dhambi, walileta mnyama wao wa kuteketezwa katika Hema Takatifu la Kukutania, wakazipitisha dhambi zao juu ya mnyama huyo kwa kuiweka mikono yao juu ya kichwa chake, wakamchinja koo lake, wakaikinga damu yake, na kisha wakawapatia makuhani damu hiyo. Kisha kuhani akaiweka damu hii katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kisha akaimwaga damu iliyosalia ardhini.
Kisha waliikata hiyo sadaka katika vipande pamoja na figo zake na mafuta, wakaiweka nyama yake katika kichanja cha shaba na kisha wakaviteketeza. Wakati damu inapokingwa, mara ya kwanza huwa katika hali ya kimiminika ikitiririka kwa wekundu. Lakini baada ya kitambo, inagandamana na kuwa nzito kidogo. Ikiwa ungeliingia katika Hema Takatifu la Kukutania, ungeweza kuiona damu hii ya kutisha.
Kila ilipotokea kuwa watu wa Israeli wamezivunja amri za Mungu, kwa kupitia madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, walitambua kuwa walipaswa kufa kama ambavyo sadaka yao ya kuteketezwa ilivyokufa madhabahuni. Kwa nini? Kwa sababu Mungu alifanya agano nao kwa damu. “Ikiwa mtaifuata Sheria yangu, mtakuwa watu wangu na ufalme wa makuhani, lakini ikiwa mtashindwa kuifuata, mtakufa ninyi kama sadaka hizi za kuteketezwa zinavyouawa.” Hivi ndivyo Mungu alivyolianzisha agano lake kwa damu. Kwa hiyo, watu wa Israeli wakalipokea hilo agano kwa ukweli kuwa ikiwa watafanya dhambi na kuivunja Sheria, ni lazima waimwage damu yao.
Kusema kweli, sio waisraeli tu, bali wote wanaomwamini Mungu ni lazima pia watoe damu ya kuteketezwa kwa ajili ya dhambi zao. Inatuonyesha kuwa mtu yeyote anayefanya dhambi mbele za Mungu na kwa hiyo ana dhambi katika moyo wake, bila kujali jinsi dhambi hiyo ilivyo kubwa au ndogo, mtu huyo ni lazima apambane na adhabu ya dhambi kama matokeo ya dhambi hizo. Ingawa sheria ya hukumu inasema, mshahara wa dhambi ni mauti na kwamba inafanya kazi kwa kila mtu mbele za Mungu, kuna watu wachache ambao wanaiogopa hukumu ya Mungu na kwa hiyo wanajaribu kujiweka chini ya sheria ya Mungu ya wokovu iliyodhihirishwa katika utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa.
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa inatueleza sisi kuwa kulingana na sheria iliyowekwa kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, Yesu Kristo ametuokoa sisi toka katika dhambi zetu na adhabu kwa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa zilizodhihirishwa katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania. Kwetu sisi ambao tunafanya dhambi mara kwa mara na kwamba tunastahili kuadhibiwa kwa dhambi zetu, Kristo alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, akazichukua dhambi zote za mwanadamu katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana, akazibeba dhambi hizi za ulimwengu Msalabani, alisulubiwa na kuimwaga damu yake Msalabani, akabeba mateso na maumivu makubwa, akasulubiwa, na kwa hiyo ametuokoa mimi na wewe toka katika dhambi zetu zote.
Ni kwa sababu Kristo aliuteketeza mwili wake binafsi na kwa hiyo ametuokoa sisi ili kwamba mimi na wewe tuweze kukombolewa toka katika dhambi zetu zote kwa imani. Yesu Kristo alizichukua dhambi zote za wale ambao hawakuwa na jinsi zaidi ya kufa kwa sababu ya dhambi zao. Kwa maneno mengine, Yesu Kristo alizichukua dhambi zao zote katika mwili wake kwa ubatizo wake, alisulubiwa hadi kifo, akafufuka tena toka kwa wafu, na kwa hiyo amewaokoa toka katika dhambi zao zote na adhabu.
Tunapoiangalia madhabahu hii ya sadaka ya kuteketezwa ndipo tunapokuja kuwa na imani hii. Hali tukiona kuwa sadaka ya kuteketezwa ilitolewa wakati wote katika madhabahu, basi tunaweza kutambua na kuamini kuwa ingawa ni sisi ndio tuliotakiwa kufa kwa sababu ya dhambi zetu za kila siku, Mungu hakutugeuza sisi kuwa sadaka yake ya kuteketezwa, bali Bwana wetu yeye mwenyewe alikuja hapa duniani na akautimiza wokovu wetu. Kwa kubatizwa, kwa kuimwaga damu yake Msalabani, na kwa kufufuka tena toka kwa wafu, Yesu ametuokoa sisi.
Hii ndio sababu Mungu Baba alizipokea sadaka za kuteketezwa za waisraeli na akazisamehe dhambi zao badala ya kuwaadhibu kwa dhambi zao. Mungu alizisamehe dhambi za waisraeli kwa kuwafanya watu wa Israeli kuzipitisha dhambi zao katika wanyama wao wa kuteketezwa kwa kuiweka mikono yao katika vichwa vya wanyama hao, na kwa kuwafanya wawaue wanyama hao na kisha kuitoa damu yao, nyama, na mafuta kwa Mungu. Pia ameziosha dhambi zetu zote kwa kupitia sadaka hii ya kuteketezwa. Hii ni rehema ya Mungu na upendo wake.
 

Mungu Hajashughulika Nasi Kwa Sheria Tu
 
Ikiwa Mungu angetuhukumu mimi na wewe, na watu wote wa Israeli kwa mujibu wa Sheria yake, je, ni wanga pia ambao wangebakia hai katika ulimwengu huu? Ikiwa Mungu anatupima na kutuhukumu kwa Sheria yake tu, hakuna hata mmoja wetu ambaye anaweza kuishi hata kwa siku moja. Wengi wetu tusingedumu kwa masaa ishirini na nne, bali tungekufa baada ya dakika chache tu. Baadhi yetu tungeweza kudumu na kufa baada ya saa moja ilhali wengine wangeweza kudumu walau kwa masaa 10, lakini tofauti hiyo ni ndogo sana na kwa kweli sisi sote tungepaswa kufa. Watu wasingeweza kuishi hadi kufikia miaka wanayoishi hivi sasa, yaani miaka 60, 70, 80, na zaidi. Kwa wakati wote kila mmoja atahukumiwa adhabu.
Hebu fikiria kilichotokea asubuhi ya leo. Mwana wako bado anahangaika kuamka kitandani baada ya kuwa ameutumia usiku mzima akifanya sherehe. Mkeo anajaribu kumwamsha. Kunajitokeza mashindano yenye sauti kali huku mwana wako akimpigia kelele mama yake kwa kumwamsha, na huku mke wako akimpigia kelele mtoto wake kwa kitendo cha kumgombeza—na hivyo ndivyo mashindano ya asubuhi yalivyoanza. Mwishowe, mama na mtoto wanaishia kufanya dhambi mbele za Mungu, na hakuna hata mmoja kati yao ambaye angeweza kuishi hata kwa siku moja, kwa kuwa wote wangeadhibiwa kwa dhambi hii.
Lakini Mungu hajashughulika nasi kwa Sheria yake ya haki tu. “Hakututenda sawasawa na hatia zetu, wala hakutulipa kwa kadri ya maovu yetu” (Zaburi 103:10).
Akiachilia mbali kutuhukumu kwa Sheria yake ya haki, Mungu aliandaa sadaka ya kuteketezwa ambayo itazichukua nafasi yetu ili kuitimiza Sheria ya haki. Kwa kutufanya sisi tuweze kuzipitisha dhambi zetu katika sadaka hii ya kuteketezwa kwa kuiweka mikono yetu juu yake, na kwa kutufanya sisi kumpatia yeye Mungu damu ya sadaka hii badala ya uhai wetu, Mungu ameupokea uhai wa sadaka ya kuteketezwa badala ya uhai wetu, na amezisamehe dhambi zote za wanadamu, zikiwemo dhambi zetu na zile za waisraeli, ametuokoa toka katika dhambi hizo zote, na ametufanya tuishi tena kwa upya. Mungu amewafanya waamini kuwa watu wake kwa kuwaokoa toka katika dhambi zao. Hivi ndivyo Mungu alivyowafanya watu wa Israeli kuwa makuhani wa Ufalme wa Mungu.
Sadaka ya kuteketezwa hapa si nyingine bali ni Yesu Kristo. Yesu Kristo alifanyika kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa sababu ya dhambi zetu, na ili kutuokoa sisi ambao tulipaswa kukutana na adhabu ya dhambi, Yesu alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo wake, akaimwaga damu yake na kisha akafa Msalabani. Ili kutuokoa sisi toka katika dhambi zetu, Mwana pekee wa Mungu alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu na akafanyika kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa kupitia ubatizo wake, akifanya yote kwa mapenzi ya Baba. Yesu ametuokoa mimi na wewe kikamilifu kwa kuzichukua dhambi za wanadamu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake alioupokea toka kwa Yohana, kwa kuzibeba dhambi hizi Msalabani, kwa kusulubiwa, kwa kuimwaga damu yake, kwa kufa na kufufuka tena toka kwa wafu.
Tunapolisikia Neno la Wokovu likitueleza kuwa Yesu, alibatizwa, akasulubiwa, na akafufuka tena toka kwa wafu baada ya siku tatu, mioyo yetu inavuviwa vizuri sana. Kwa sababu yeye asiye na dhambi aliupokea ubatizo badala yetu, ubatizo ambao ulizipitisha dhambi zote katika mwili wake, na kama mshahara wa dhambi hizi, alibeba aina zote za mateso, manyanyaso, maumivu, kuugua, na hatimaye kifo, vitu ambavyo vilistahili kuwa vyetu. Wakati Kristo alipotuokoa toka katika dhambi zetu, hakuna kitu kinachoweza kuwa kibaya zaidi ya kutouamini ukweli huu.
 

Ni Lazima Tuamini Katika Wokovu Uliotimizwa Katika Nyuzi za Bluu, Zambarau, na Nyekundu
Ni Lazima Tuamini Katika Wokovu Uliotimizwa Katika Nyuzi za Bluu, Zambarau, na NyekunduWakati Yesu Kristo alipozibeba dhambi zetu na adhabu ya dhambi hizi kwa kupitia ubatizo wake kwa ajili yetu, na wakati alipotuokoa mimi na wewe toka katika dhambi zetu kwa kujitoa mwenyewe badala yetu, ni lazima sisi sote tuwe na aina ya imani inayosema, “Asante Bwana!” Ingawa watu wengi wanatiwa moyo kirahisi kwa kugusia habari za upendo, habari za maisha, au kwa habari nyingine yoyote inayogusa mioyo, inapofikia katika mioyo yao juu ya upendo wa Mungu usio na masharti, watu hao wanakuwa baridi kama barafu. Wakati neema ya Bwana wetu ni kubwa sana kiasi kwamba alibatizwa na kufa Msalabani kwa ajili yetu, bado kuna watu watukutu ambao hawawezi kuitambua neema hii na hawamshukuru Mungu kwa neema hiyo kabisa.
Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, alikuja hapa duniani na akafanyika sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yetu. Alizipokea dhambi zetu zote katika mwili wake binafsi kwa ubatizo wake na akajitoa yeye mwenyewe kwa kuusulubisha mwili wake Msalabani. Alipigwa makofi, alichapwa mijeredi angali uchi, aliteswa na kunyanyaswa, alipata yote hayo kwa ajili yetu. Hivi ndivyo alivyotuokoa. Ni kwa kuuamini ukweli huu kwamba tumefanyika kuwa wana wa Mungu. Hili ni jambo la kutia moyo kuliko mambo yote, ni neema kuu ya Mungu ambayo haiwezi kuelezewa kwa maneno. Wakati hivi ndivyo ambavyo Kristo ametuokoa sisi, inanihuzunisha sana kuona kuwa watu wengi bado hawaamini na kumshukuru Mungu hata baada ya kuusikia ukweli huu.
Ni kwa sababu Yesu alikuja hapa duniani, akaupokea ubatizo wake, na akajitoa mwenyewe ili kwamba mimi na wewe tuweze kuokolewa toka katika dhambi zetu. Kwa hiyo, Isaya 53:5 inasema, “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maouvu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Tunafanya dhambi muda wote katika maisha yetu. Ili kutuokoa sisi ambao tusingeweza kukwepa adhabu toka katika dhambi zetu, hukumu ya adhabu, uharibifu na laana, Bwana wetu aliacha kiti cha enzi cha Ufalme wa Mbinguni, na akaja hapa duniani. Alikiinamisha kichwa chake mbele ya Yohana Mbatizaji na akabatizwa, akazibeba dhambi hizi Msalabani na akateseka sana, akaimwaga damu yake ardhini, akafufuka tena toka kwa wafu, akafanyika sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yetu, na amefanyika Mungu wa kweli wa wokovu wetu.
Je, unafikiria kuhusu ukweli huu na unauweka ukweli huu katika kina cha moyo wako? Unapolisikia Neno, ni vizuri ikiwa utaliamini na kutiwa nguvu katika moyo wako kwamba kwa kweli Yesu Kristo alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, na kwamba alibatizwa, akasulubiwa hadi kifo, na akafufuka ili kuwaokoa watu wake toka katika dhambi. Ikiwa tunatambua kuwa sisi sote tulifungwa kuzimu, basi tunaweza kutambua kwa kina katika mioyo yetu jinsi ambavyo wokovu huu ni wa kuvutia na wenye shukrani. Ingawa tulipenda kuamini katika Mungu na kufanyika watu wake, hakukuwa na njia kwetu sisi ya kuweza kufanikisha jambo hili. Lakini kwangu mimi na kwako ambao tumepokea kwa hakika ondoleo la dhambi, Yesu amekutana nasi kwa Neno la kweli kwamba Kristo alikuja hapa duniani, alibatizwa, alikufa Msalabani, na kisha akafufuka tena toka kwa wafu baada ya siku tatu.
Isingelikuwa ni huku kujitoa kwa Yesu, je, tungewezaje sisi kupokea wokovu wetu? Tusingeweza kuupata! Kama isingelikuwa ubatizo wa Yesu na damu yake ya Msalaba, na kama isingekuwa wokovu katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa vilivyodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania, kwa kweli wokovu ungekuwa ni ndoto ya mchana kwetu sisi. Kama isingelikuwa kusulubiwa kwake, kamwe tusingeweza kuwekwa huru toka katika dhambi zetu na kukwepa adhabu yake, bali tungetupwa katika moto wa milele wa kuzimu na kisha kuteseka daima. Lakini Kristo ametuokoa kwa kujitoa mwenyewe kwa ajili ya yetu kama ilivyokuwa kwa sadaka ya kuteketezwa katika Agano la Kale.
 


Wokovu wa Nyuzi za Bluu, Zambarau, na Nyekundu Umetimizwa Katika Agano Jipya

 
Wasomaji wangu wapendwa, msisahau kamwe ukweli wa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa vilivyotumika katika Hema Takatifu la Kukutania. Kitani safi ya kusokotwa ni Neno la Agano la Kale na Agano Jipya, Neno ambalo Mungu aliliahidi tangu zamani kwamba yeye mwenyewe atakuja kwetu kama Mwokozi wetu, na kulingana na ahadi hii, Yesu Kristo alikuja hapa duniani. Nyuzi za bluu zinatueleza sisi kuwa Kristo, alipokuja hapa duniani, alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa ubatizo wake. Kwa maneno mengine, alibatizwa kwa mujibu wa ahadi kuwa atatuokoa sisi toka katika dhambi zetu na kutukomboa toka katika adhabu yetu. Yesu alibatizwa na Yohana ili aweze kuzichukua dhambi za kila mtu katika ulimwengu huu katika mwili wake, na kwa hakika alizibeba dhambi zote za ulimwengu. Ni lazima tusisahau jambo hili, kwa maana ikiwa tutasahau kuwa Yesu alikuja kuwa sadaka yetu ya kuteketezwa na kwamba alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake, basi hakutakuwa na wokovu.
Mara nyingi tunaishi katika ulimwengu huu hali tukijiwekea umuhimu kwetu sisi binafsi. Mioyo ya watu iko hivyo, ingawa haipendi na haiwezi kuvumilia inapomsikia mtu mmoja akijivuna, mioyo hiyo nayo inapenda pia kujivuna. Lakini ulikuwepo wakati ambapo nilianza kujivuna si kwa sababu ya mimi binafsi, bali kwa sababu ya mtu mwingine, na huu ulikuwa ni wakati nilipokuwa nikimshukuru sana Yesu kwa kuniokoa mimi kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Kwa maneno mengine, nilianza kujivunia Yesu. Kwa sasa ninaeleza na ninajivuna mara nyingi kadri niwezavyo kwamba Yesu alikuja hapa duniani; ili kuzitowesha dhambi zetu, alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake kwa kubatizwa ili kwamba Yesu aweze kusulubiwa kutokana na ule ubatizo wake; na kwamba hivyo ndivyo Bwana wetu alivyotuokoa. Kwa kweli sishindwi kujivunia ukweli huu, kuuhubiri, na kumpatia Mungu utukufu wote.
Lakini bado kuna watu wengi ambao pamoja na kukiri kumwamini Yesu, wanaendelea kulihubiri Neno hali wakiuacha ubatizo wake, au wanajivuna wao wenyewe kwa kuliazima jina la Yesu. Palikuwa na mtumishi mwongo ambaye alizoea kudai kuwa alitumia dola 300 kwa mwezi kwa ajili ya yeye kuishi. Alizoea kujivuna sana kana kwamba yalikuwa ni mafanikio makubwa, alikuwa akijivuna kuwa anaweza kuishi mwezi mzima kwa kutumia dola 300, na kwamba alikuwa hahitaji kuchukua fedha yoyote anaposafiri kwa sababu wafuasi wake walimlipia gharama zake zote. Lakini je, fedha ya waumini sio fedha? Je, fedha hii haina thamani yoyote kiasi kuwa ni fedha yake tu ndiyo anayoijali? Kiongozi huyu wa Kikristo alidai kuwa kila alipokuwa anahitaji kitu fulani basi alichotakiwa kufanya ni kuomba. “Mungu, lipia gharama zangu za kusafiri! Ninakuamini, Bwana!” Mtumishi huyu alishuhudia kuwa, kwa maombi haya, baadhi ya watakatifu waliinuka na kumpatia bunda la fedha taslimu. Unapowaangalia watu wa jinsi hiyo wanaozungumzia mambo haya kana kwamba ni vitu vya kujivunia, je unapata mawazo gani?
Mathayo 3:13-17 inaeleza, “Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.’” Kifungu hiki kinaelezea kilichotokea wakati Yesu alipobatizwa. Wakati Yesu alipobatizwa na Yohana Mbatizaji katika Mto Yordani akapanda toka majini, lango la Mbingu lilifunuka na sauti ya Mungu Baba ilisikika: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Yohana Mbatizaji alishangazwa.
Yohana Mbatizaji alishangazwa mara mbili katika Mto huu wa Yordani. Kwanza alishangazwa alipomuona Yesu anakuja kwake ili abatizwe naye, na pia alishangazwa tena baada ya kumbatiza Yesu wakati mlango wa mbinguni ulipofunguka na akaisikia sauti ya Mungu Baba ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”
Sababu ya Yesu kubatizwa na Yohana Mbatizaji ni ipi? Mathayo 3:15 inatupatia jawabu. Hebu tusome aya ya 15 na 16 tena: “Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake”
Mathayo 3:15 inatueleza sababu juu ya kwanini Yesu alibatizwa na Yohana Mbatizaji. Ingawa Yesu alikuwa ni Kuhani Mkuu wa Ufalme wa Mbinguni na Mwana pekee wa Mungu, hata hivyo, alikuja hapa duniani ili kutuokoa sisi watu wake toka katika dhambi zetu. Kwa maneno mengine, Yesu alikuja hapa duniani kama sadaka ya kuteketezwa inayolipia mshahara wa dhambi zetu kwa kuzichukua dhambi hizi katika mwili wake na kusulubiwa badala yetu. Hii ndiyo sababu Yesu alihitaji kubatizwa na Yohana.
Lakini kwa nini Yesu hakubatizwa na mtu mwingine zaidi ya Yohana Mbatizaji? Kwa sababu Yohana Mbatizaji alikuwa ni mwakilishi wa wanadamu, kwa kuwa alikuwa ni mkuu kuliko wote wanaozaliwa na wanawake. Mathayo 11:11 inasema, “Amini, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji.” Yohana Mbatizaji alikuwa ni mtumishi wa Mungu aliyetabiriwa katika Agano la Kale katika kitabu cha Malaki: “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na ya kuogofya” (Malaki 4:5). Yohana Mbatizaji alikuwa ni huyu Eliya ambaye Mungu aliahidi kumtuma.
Kwa nini Mungu alimwita Yohana Mbatizaji kuwa ni Eliya? Eliya alikuwa ni nabii aliyeigeuza mioyo ya waisraeli kumrudia Mungu. Katika kipindi hicho, watu wa Israeli walikuwa wakimwabudu Baali kama Mungu wao, lakini Eliya aliwaonyesha kikamilifu juu ya Mungu halisi, kwamba alikuwa ni Baali au Yehova Mungu. Alikuwa ni nabii ambaye, kwa imani na kwa kupitia sadaka ya kuteketezwa, aliwadhihirishia watu wa Israeli Mungu aliye hai, na hivyo akawaongoza tena watu ambao walikuwa wakiabudu sanamu kumwabudu Mungu wa kweli. Hii ndiyo sababu mwishoni mwa Agano la Kale, Mungu aliahidi, “Nitawapelekea Eliya.” Kwa sababu watu wote walioumbwa katika sura na mfano wa Mungu walikuwa wamepotoka katika kuabudu sanamu na kuabudu mashetani, Mungu alisema kuwa atamtuma mtumishi wake ambaye atawaongoza kumrudia Mungu. Kwa hiyo yeye ambaye atakuja ni Yohana Mbatizaji.
Mathayo 11:13-14 inasema, “Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana. Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja.” Huyu Eliya ambaye atakuja si mwingine bali ni Yohana Mbatizaji. Katika aya ya 11-12, imeandikwa, “Amini, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye. Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.”
Kwa hiyo kifungu kinaposema kwamba “hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji,” ina maanisha kuwa Mungu alimwinua Yohana Mbatizaji kama mwakilishi wa wanadamu wote. Mungu alimfanya Yohana Mbatizaji kuzaliwa katika dunia hii miezi sita kabla ya kuzaliwa kwa Yesu. Na Mungu alimwandaa yeye kama nabii wa mwisho na kuhani wa Agano la Kale. Kwa hiyo, kama Kuhani Mkuu wa duniani, Yohana Mbatizaji alimbatiza Yesu Kristo na kwa hiyo alizipitisha dhambi zote za wanadamu juu ya Yesu. Kwa maneno mengine, sababu iliyomfanya Yohana Mbatizaji akambatiza Yesu ilikuwa ni kuzipitisha dhambi zote za ulimwengu katika mwili wa Yesu. Sababu iliyomfanya Yesu Kristo akabatizwa na Yohana Mbatizaji ilikuwa ni kuzichukua dhambi zote za wanadamu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake.
Hii ndio maana Yesu alisema katika Mathayo 3:15, “Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote.” Kwa sababu haki yote ingeweza kutimizwa pale tu Yesu alipoupokea ubatizo wake toka kwa Yohana Mbatizaji ili kuzikubali dhambi zote za ulimwengu, Yesu alisema ndivyo itupasavyo.
 

Kwa Hiyo Bwana Wetu Amewaokoa Wenye Dhambi kwa Njia Hii
ubatizo wa YesuUbatizo huu ambao Yesu aliupokea toka kwa Yohana ni sawa na kitendo cha kuwekewa mikono cha Agano la Kale. Kwa maneno mengine, kitendo cha kuwekewa mikono kilifanywa mbele ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa katika kipindi cha Agano la Kale ili kuzipitisha dhambi za mtu fulani katika sadaka ya kuteketezwa. Kwa kuja hapa duniani na kwa kubatizwa, Yesu Kristo aliitimiza ahadi ya kuwekewa mikono—ahadi iliyofanywa kila wakati sadaka ya kila siku ilipotolewa wakati wenye dhambi walipozipitisha dhambi zao katika sadaka ya kuteketezwa kwa kuiweka mikono yao juu ya kichwa cha mwanasadaka; na kila wakati sadaka ya mwaka ilipotolewa katika siku ya 10 ya mwezi wa saba, siku ya upatanisho mkuu, siku ambayo Kuhani Mkuu alizipitisha dhambi za mwaka mzima za waisraeli katika sadaka ya kuteketezwa kwa kuiweka mikono yake katika kichwa chake.
Kama ilivyo kwa kitendo cha kuwekewa mikono katika Agano la Kale, Yesu alizipokea dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa kubatizwa, aliziosha dhambi hizi zote, na kwa sababu alikuwa amezichukua dhambi hizi za wanadamu katika mwili wake, alibeba adhabu ya dhambi hizi kwa niaba yetu na akasulubiwa. Hivyo ndivyo Yesu Kristo alivyoweza kuwa Mungu wa kweli kwa wokovu wetu.
Kwa hiyo, ni lazima tukiri kuwa kwa sababu ya dhambi zetu, tusingeweza kukwepo bali tungekikabili kifo na kuadhibiwa. Ni lazima tulifahamu hili na tulifikirie. Na ni lazima tutambue kuwa Yesu Kristo Mwokozi wetu ametuokoa kwa kuja hapa duniani na kwa kusulubiwa kwa ajili yetu— hii ni kusema kuwa, kwa kupitia kazi zake za wokovu kwa ubatizo wake na ufufuko, Yesu Kristo ameziosha dhambi zetu zote na ametuokoa kikamilifu toka katika dhambi zetu. Ni lazima pia tuamini kuwa Yesu ametupatia zawadi ya wokovu, kwamba ameutimiza wokovu wetu na ametupatia wokovu huu ulio kamili kama zawadi yake kwetu sisi. Yesu ameitimiza haki yote, ili kwamba ikiwa mtu ataamini, na ikiwa mtu atamkubali, basi kwa hakika ataokolewa.
Ili kutufanya sisi kuelewa jambo hili, lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania lilifumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Hii pia ndio sababu inayotufanya tuione kwanza madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ikiwa tutafungua na kuingia katika lango la ua wa Hema Takatifu la Kukutania. Sadaka zilizotolewa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa pia zilikuwa ni kivuli cha njia ya wokovu ambayo kwa hiyo Yesu Kristo ametuokoa. Sadaka zilizoteketezwa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa zilipaswa kupokea uovu wa wenye dhambi kwa kuwekewa mikono na kisha kumwaga damu hadi kifo kwa niaba ya wenye dhambi. Damu ya sadaka ya kuteketezwa iliwekwa katika pembe za madhabahu, na damu iliyosalia ilinyunyizwa ardhini. Kisha waliitoa nyama na mafuta ya wanyama katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Hii ilikuwa ni njia ambayo kwa hiyo sadaka ya kuteketezwa ilitolewa kwa Mungu. Vionjo hivi vyote vya sadaka ya kuteketezwa vinafanana sana na njia ambavyo Yesu Kristo amefanyika kuwa Mwokozi wetu. Kwa maneno mengine, kwa kupitia sadaka ya kuteketezwa, Mungu ametuonyesha sisi kuwa Yesu Kristo atakuja hapa duniani na kutuokoa kwa njia hii.
Mikono ya wenye dhambi ilitakiwa kuwekwa juu ya wanyama wa sadaka ya kuteketezwa waliotolewa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa bila kukosa. Hii ndiyo sababu Hema Takatifu la Kukutania linatueleza sisi juu ya injili ya maji na Roho. Kwa kuja hapa duniani, Yesu Kristo alibatizwa ili kuzichukua dhambi za wanadamu katika mwili wake. Ubatizo ni ufananisho wa wokovu ambao Kristo aliupokea ili kufanyika sadaka ya kuteketezwa kwa wenye dhambi wote wa ulimwengu mbele ya Mungu Baba.
Kwa kupitia hili Hema Takatifu la Kukutania, sasa tunaweza kuwa na imani sahihi. Kama ambavyo sadaka ya kuteketezwa ilizipokea dhambi za watu wa Israeli katika siku ya upatanisho kwa kuwekewa mikono na Kuhani Mkuu, na kama ambavyo sadaka hiyo iliteketezwa kwa niaba yao kwa kuwa dhambi zao zilikuwa zimepitishwa katika sadaka hiyo (Mambo ya Walawi 16), Yesu Kristo alikuja hapa duniani ili kuzichukua dhambi zetu katika mwili wake na kufanyika sadaka yetu ya kuteketezwa kwa ajili ya dhambi hizi, kwa kweli ametuokoa toka katika dhambi zetu zote na adhabu. Tunaweza kuuamini sasa upendo huu wa wokovu kikamilifu. Ni kwa kuuamini ukweli huu ndipo tunapoweza kushukuru na kulipa deni letu kwa Mungu kwa wokovu huu wa upendo ambao ametupatia.
Haijalishi ni kiasi gani mtu anaweza kuwa analifahamu Hema Takatifu la Kukutania, ikiwa mtu huyo haamini, basi ufahamu huo wote unakuwa hauna maana. Kwa hiyo, ni lazima tutambue na pia tuamini jinsi ambavyo ubatizo wa Yesu ni wa muhimu. Hema Takatifu la Kukutania lilikuwa na malango matatu, ambayo yote yalifumwa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Watu wanaweza kulielezea kila lango kiutofauti kwa sababu ya kutokufahamu kwao.
Katika mpangilio wake wa nyuzi, nyuzi za kwanza kufumwa zilikuwa ni nyuzi za bluu, kisha zikafuatia nyuzi za zambarau, nyekundu, na kitani safi ya kusokotwa. Ni kwa kulifanya lango katika namna hii tu ndipo tunapoweza kulielezea lango hilo kuwa ni lango halisi la Hema Takatifu la Kukutania, kwa kuwa hivi ndivyo Mungu alivyowaamuru waisraeli kulijenga hilo lango katika kipindi cha Agano la Kale.
Kulikuwa na sababu iliyolifanya lango litengenezwe kwa namna hii. Bila kujali jinsi ambavyo Yesu alizaliwa katika ulimwengu huu kama Mwokozi wa wanadamu katika mwili wa mwanadamu na kwa kupitia mwili wa Bikira Maria, ikiwa angekuwa hakubatizwa, kwa kweli asingeweza kufanyika Mwokozi wa kweli. Ikiwa angekuwa hakubatizwa, basi asingeliweza kusulubiwa na kisha kufa Msalabani. Kwa hiyo, nyuzi za bluu zilifumwa kwanza na hivyo umuhimu wake kiutekelezaji ulikuwa ni wa maana sana.
 

Ni Yupi Ambaye Ni Lazima Tumwamini?
 
Kwa hiyo, ni lazima tumwamini Yesu Kristo ambaye ametuokoa sisi toka katika dhambi zetu. Tunaweza kuzaliwa upya kweli pale tu tunapouamini wokovu ambao huyu Mwana wa Mungu, Yesu Kristo Mwokozi wetu ametupatia. Tunapomwamini Mwana wa Mungu kuwa ni Mungu wa wokovu wetu, na tunapouamini ukweli kuwa alikuja hapa duniani, akazichukua dhambi zetu katika mwili wake mara moja kwa kubatizwa kwa ajili yetu, na akabeba adhabu yetu Msalabani, basi ndipo tunapoweza sisi sote kuupokea wokovu wetu wa kweli.
Kwa sababu Yesu hakuweza kuzichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa njia nyingine yoyote isipokuwa kwa kupitia ubatizo wake, basi ni kwa kuzibeba dhambi zetu kwa njia hii sahihi ndipo angeliweza kuuendea Msalaba, kumwaga damu yake na kufa Msalabani. Haijalishi kuwa yeye ni Mwana wa Mungu, na kuwa alikuja hapa duniani kama Mwokozi wetu, kama asingelizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake, kwa hakika wokovu wetu usingeweza kupatikana katika ulimwengu huu.
Kwa hiyo, ni muhimu sana kwako kuthibitisha ushahidi wa kibiblia kwa kina ili uweze kuwa na uhakika kamili kuwa dhambi zako zimekwishatoweshwa tayari.
Hebu tufikirie kwa muda kwa wewe unadaiwa deni kubwa. Halafu mtu mmoja anakueleza, “Usihofu; nililipa deni lote kwa ajili yako. Hakuna haja ya kuhofu; nitalitatua tatizo hilo.” Kila unapokutana na mtu huyu anaendelea kukueleza, “Je, sikukuambia usihofu? Nilikueleza kuwa nitalishughulikia jambo hilo!” Hebu tufikirie kuwa mtu huyu anafikia hata kiasi cha kukasirika, hali akikuuliza kuwa kwa nini humwamini. Hata kama mtu huyu anakueleza kila siku, “Nililipa deni lako lote; wewe niamini mimi,” wakati kwa kweli hajalipa deni lako, je unaweza kweli kuwekwa huru toka katika deni hili kwa kumwamini tu? Kwa kweli si kweli!
Haijalishi anakueleza kwa kujiamini kiasi gani, “Ikiwa utaniamini mimi, deni lako lote litapotea,” ikiwa kweli hakulilipa deni hilo lote, basi deni lako linabakia kama lilivyo, na kwa kweli mtu huyu atakuwa anakudanganya tu. Basi unamuuliza tena na tena, “kwa hiyo ulilipa deni langu lote?” Kisha anakueleza kwa kurudia, “Kwa nini una mashaka sana? Wewe niamini mimi bila masharti! Nilikueleza kuwa nililipa deni lako lote. Unachotakiwa kufanya ni kuniamini mimi, lakini bado unaonekana kuhofia! Usiwe hivyo!” Kwa hiyo, hebu tufikirie tena, kuwa ulimwamini kwa moyo wako wote. Lakini haijalishi ni kwa kiwango gani ulimwamini, ikiwa hakulilipa kweli deni lako lote, basi maneno hayo yote ni uongo mtupu.
 

Hivi Ndivyo Imani ya Wakristo Wengi wa Leo Ilivyo.
 
Wakristo wa leo wanasema, “Yesu amekuokoa kwa kuimwaga damu yake ya thamani Msalabani. Aliibeba adhabu yote ya dhambi pale Msalabani. Hivi ndivyo alivyokuokoa wewe.” Wachungaji wengi wanahubiri hivi katika makusanyiko yao. Wakati mtu mmoja anaposimama katika kusanyiko na kuwaeleza, “Lakini mimi bado ni mwenye dhambi,” wanasema, “Hiyo ni kwa sababu una imani ndogo. Wewe amini tu! Hakuna dhambi zaidi ya kutokuamini kwako” “Mimi pia ninapenda kuamini, lakini sielewi kwa nini siwezi kuamini.” “Sielewi kwa nini bado mimi ni mwenye dhambi pamoja na kuwa ninaamini.” “Huna imani ya kutosha. Unahitaji kuamini zaidi. Panda mlimani na ujaribu kufunga. Amini hali ukiruka baadhi ya milo yako.” “Je, kwani siwezi kuamini bila ya kuiruka milo?” “Hapana, ni lazima ujaribu kuamini hali ukiwa umefunga.”
Wachungaji wengi wa sasa wanakueleza uamini, lakini hawatatui tatizo la dhambi zako, na wanakukemea kwa kutokuamini. Kwa upande wako, unajaribu kuamini lakini bado ni vigumu sana kuamini, au unaamini kwa kweli katika hali ya upofu lakini tatizo la dhambi zako linabakia palepale. Kuna shida gani hapa? Nini kinaweza kuelezea hali hii? Watu hawawezi kuwa na imani ya kweli na yenye nguvu kwa sababu hawatambui kuwa Yesu Kristo alizichukua dhambi zao zote katika mwili wake kwa ubatizo wake. Ni kwa sababu wanauamini uongo ambao kwa huo hawawezi kutatua tatizo la dhambi zao hata kama wanaamini kiasi gani.
Je, imani inakuja kwa kuamini pasipo masharti na pasipo ushahidi wowote wa kweli? Kwa kweli sivyo! Imani kamili inakuja yote mara moja pale unapofahamu jinsi ambavyo tatizo la dhambi lilivyotatuliwa na kisha uuamini ukweli huo. “Japokuwa nilikuonea mashaka, kwa kweli ni wazi kabisa kwamba umekwisha tatua tatizo la dhambi zangu. Haijalishi ni jinsi gani siwezi kuamini, bado siwezi kujisaidia zaidi ya kuuamini wokovu wako, kwa kuwa wokovu huu ni wa hakika sana. Asante sana kwa kulitatua tatizo langu.” Kwa maneno mengine, ingawa tunaweza kuwa na mashaka mara ya kwanza, lakini kwa sababu ushahidi wa wokovu wetu ni wa uhakika, basi hatuwezi tena kuendelea kuhofia tena. Kama alama ya wokovu wetu na ushuhuda wake, Yesu ametuonyesha risiti inayoitwa injili ya maji na Roho. “Nimeyalipa madeni yako kwa njia hii.” Ni pale tu tunapoiangalia risiti hii inayoonyesha kuwa madeni yetu yote yamelipwa basi ndipo imani ya kweli inapokuja kwetu.
Hatuwezi kuamini hata pale tunapokiri kumwamini Mungu, tukisema, Yesu Kristo, Mungu mwenyewe, ni Mwokozi wetu, na kudai kumwamini Mwokozi, wakati hatuna ushahidi wa jinsi alivyotuokoa na jinsi ambavyo dhambi zetu zilitoweshwa. Kwa maneno mengine, hatuwezi kuwa na uhakika zaidi hadi pale tutakapoina risiti inayoonyesha malipo kamili ya mshahara wa dhambi. Watu wanaoamini pasipo kuona risiti hii wanaweza kuonekana kana kwamba wana hisia za imani yenye nguvu mwanzoni, lakini kwa kweli imani yao ni imani yenye upofu. Imani ya jinsi hiyo ni imani ya kidini na ya kilokole tu.
 

Je, Unaifikiria Imani ya Kidini-Kilokole Kuwa ni Imani Nzuri?
 
Je, utapendaje ikiwa mchungaji mwenye imani ya kidini anadai imani hiyo hiyo ya kidini toka kwa wengine? “Amini! Pokea moto! Moto, moto, moto! Roho Mtakatifu ambaye ni kama moto anatujaza moto! Ninaamini kuwa Bwana atawabariki ninyi nyote! Ninaamini kuwa atawafanya ninyi nyote kuwa matajiri! Ninaamini kuwa atawabariki! Ninaamini kuwa atawaponya ninyi!” Wakati mchungaji wa aina hiyo anapotoa onyesho kama hilo, masikio ya wasikilizaji yanaanza kupiga kelele na mioyo yao inaanza kurukaruka. Hali maneno ya mchungaji huyo yakitoka katika vyombo vya sauti vya kisasa wakati mchungaji akipiga kelele, “Moto, moto, moto,” mioyo ya wasikilizaji inaanza kuruka kwa sababu ya sauti yake ya kushangaza. Ndipo wanaposhangazwa kihisia, kana kwamba imani yenye nguvu imekuja kwao, halafu wanaanza kupiga kelele hali wakisema, “Njoo, Bwana Yesu! Njoo, Roho Mtakatifu!”
Katika wakati kama huu, mchungaji anapambisha hisia za wasikilizaji zaidi na zaidi kwa kusema, “Hebu tuombe. Ninaamini kuwa Roho Mtakatifu sasa anashuka na anatujaza sisi sote.” Baada ya maneno hayo bendi inayopiga nyimbo za kuhamasisha inaanza kupigia nyimbo hizo, na kisha watu wanainyosha mikono yao juu, hali wakitahamaki kwa shauku, na hisia zao zinapasuka na kufikia ukomo. Hali wakiwa wamesimama katika foleni, huu ndio wakati ambapo mchungaji anasema, “Hebu tutoe sadaka zetu. Katika hali ya pekee, jioni hii Mungu anataka kupokea sadaka maalum toka kwako. Hebu tutoe sadaka maalumu kwa Mungu.”
Hali wakiwa wamechanganyikiwa na hisia zao, hapo ndipo watu wanapoishia wakiwa wamekausha mifuko yao. Mchungaji huyu wa uongo amekwisha tayarisha mimbari kubwa ambayo ni kubwa na inatosha kuzitunza fedha zote zilizokusanywa, na ameweka dazani ya vyandarua vya kipepeo (mabakuli ya sadaka) pale mbele. Wakati bendi inapoanza kupiga nyimbo na mioyo ya watu imeshindwa kabisa na mshangao wao, ndipo anapowatuma wakusanyaji wa vipepeo (wale wanaojitolea kupitisha maboksi ya kukusanyia sadaka) kati ya halaiki.
Kwa kudanganya kuwa sadaka nyingi ndizo baraka nyingi, na kwa kuziamsha hisia za watu, wachungaji waongo wa jinsi hiyo wanawahamasisha watu kumwaga machozi yao na kufungua pochi zao. Ni ili kuwafanya watu kutoa fedha zao pasipo wao kutambua kwa kuzishusha chini fikra za watu na mtazamo wao na kisha kuwashangaza kwa hisia zao. Jambo hili halitokani na Neno la Mungu, au na aina yoyote ya mahubiri, bali ni suala la kidini-kilokole na la kiupofu ambalo linakazia katika kupata fedha kwa udanganyifu. Kama hivi, wachungaji ambao imani yao ni ya kidini-kilokole wanaziamsha hisia za watu ili waweze kuyafikia malengo yao ya siri.
Ikiwa tunafahamu kuwa Bwana wetu alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kupitia ubatizo wake, na ikiwa tutamwamini huyu Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wetu, basi kwa jinsi hiyo hatuyumbishwi, bali tutabakia katika amani. Kitu ambacho kinatuvutia sisi kimyakimya ni kwamba Yesu alizibeba dhambi zetu kwa ubatizo wake na alisulubiwa hadi kifo. Tunapofikiria kuhusu jambo hili, kwamba Yesu, Mungu mwenyewe, alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa ubatizo wake na alikufa ili kulipa mshahara wa dhambi hizi, basi ndipo tunapokuwa na shukrani sana, na mioyo yetu inajazwa na furaha kuu. Hata hivyo, kuvutiwa huku kulikotulia katika mioyo yetu ni kwa maana zaidi kuliko kitu chochote katika ulimwengu huu; kuliko ukiri wa kimahaba wa mapenzi, na kuliko zawadi ya almasi ya thamani katika ulimwengu huu.
Kinyume chake, kuvutiwa kihisia kwa watu wa kidini-kilokole hakudumu kwa muda mrefu. Ingawa wanaweza kudumu katika mvuto huu kwa kitambo, wanapotenda dhambi kila siku na kujisikia vibaya kwa dhambi hizo, kwa kweli hawawezi kufanya lolote zaidi ya kuzificha nyuso zao kwa aibu. “Wakati Yesu alipobeba adhabu na kufa Msalabani kwa ajili yetu, kwa nini ninaendelea kufanya dhambi kila siku?” Kwa hiyo wanaona aibu na hawawezi tena kuvutiwa kadri muda unavyozidi kwenda; kinachofuatia ni kuwa hali wakiwa na aibu wanashindwa hata kwenda mbele za Mungu.
Hii ndiyo sababu Mungu ametuonyesha sisi madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Sadaka ya kuteketezwa ambayo ilitolewa katika madhabahu hii ya kuteketezwa kwa mujibu wa utaratibu wa sadaka ya kuteketezwa si nyingine bali ni Yesu Kristo Mwokozi wetu. Kwa hiyo, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa inadhihirisha kuwa Yesu alikuja hapa duniani na kwa hakika ametuokoa sisi sote mara moja kwa kupitia nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa. Mungu ametufanya sisi kuiona madhabahu hii ya sadaka ya kuteketezwa, na anataka sisi tuokolewe kwa kuiamini.
 

Je, Tunatakiwa Kufanya Nini Katika Wakati Huu?
 
Kuna mambo mengi ambayo sisi tuliozaliwa upya tunatakiwa kuyafanya katika wakati huu. Kwanza, tunatakiwa kuihubiri injili ya maji na Roho katika ulimwengu mzima. Ni lazima tuueneze ukweli kwa wale ambao wanabakia wajinga kuhusu ukweli huu wa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, na hivyo ni lazima tuwasaidie ili waokolewe toka katika adhabu ya moto wa kuzimu. Kwa nini? Kwa sababu kuna watu wengi ambao wanamfuata Yesu pasipo hata kuitambua na kuiamini injili ya maji na Roho iliyodhihirishwa katika Hema Takatifu la Kukutania.
Ili kuueneza ukweli huu kwao, bado kuna mambo mengi sana kwetu ya kuyafanya. Ni lazima tuchapishe vitabu vyetu vinavyopelekwa ulimwenguni kote; tangu kutafsiri, kuhakiki, na kuhariri, kuvifanya vitabu hivi kupata fedha ili kuweza kuvichapa na kisha kuvituma katika nchi mbalimbali ulimwenguni, kwa hakika kuna kazi nyingi ambazo zinahitaji kufanyika.
Kwa hiyo tunapowaangalia watenda kazi wenzetu na watumishi, tunaona jinsi ambavyo wametingwa kwa kazi nyingi. Kwa sababu watakatifu wote na watenda kazi ya Kanisa la Mungu wana kazi nyingi kwa njia hii, wakati mwingine wanapitia vipindi vigumu kimwili. Inasemekana kuwa wanariadha wa marathoni wanafikia katika kiwango fulani wanapokuwa katika kilomita 42.195 za mazoezi ambapo huwa wanachoka sana kiasi kuwa wanakuwa hawana hakika ikiwa wanakimbia au wanafanya kitu kingine tofauti. Kwa ufupi, kuchoka kupita kiasi kunawafanya wao kuwa watupu kiakili. Pengine tumefikia hali hii katika mbizo zetu za injili. Kuishi maisha yetu kwa ajili ya injili ni kama vile kukimbia umbali mrefu kuelekea lengo letu pasipo kusimama, kama wanavyofanya wanariadha wa marathoni. Kwa sababu mbio zetu kwa ajili ya injili ni lazima kuendelea hadi siku ile Bwana wetu atakapokuja, kwa hiyo sisi sote tunakutana na magumu.
Lakini kwa sababu Bwana wetu yumo ndani yetu, kwa sababu tuna injili ya maji na Roho, kwa sababu imani yetu inaamini kwamba Bwana wetu ametuokoa kwa nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, na kwa sababu tunauamini ukweli halisi, basi sisi sote tunaweza kupokea nguvu mpya. Ni kwa sababu Yesu ametupatia zawadi ya wokovu ndio maana mimi na wewe tumeipokea zawadi hiyo. Kwa hiyo magumu yetu ya mwili hayawezi kutusumbua. Kwa upande mwingine, kadri tunavyopata ugumu, ndivyo wenye haki wanavyozidi kupata nguvu. Kwa kweli ninamshukuru sana Bwana.
Kiroho, katika mioyo yetu, katika mawazo yetu, na katika mazingira yetu yanayotuzunguka, tunaweza kupata nguvu mpya ambayo Bwana wetu ametupatia, na kwamba yupo pamoja nasi. Kwa sababu tunaweza kuona kuwa anatusaidia na kutushikilia, na kwamba yupo pamoja nasi, basi tunampatia shukrani nyingi sana. Kwa hiyo Mtume Paulo alisema, “Ninayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Wafilipi 4:13). Kwa hiyo tunakiri kila siku kwamba hatuwezi kufanya kitu chochote ikiwa Mungu hajatuwezesha na kutupa nguvu. Si kwamba Yesu Kristo alibatizwa tu kwa ajili yetu, bali alisulubiwa kwa ajili yetu, akakikabili kifo chake, akafufuka tena toka kwa wafu, na kwa hiyo amefanyika kuwa Mwokozi wetu wa kweli. Kila tunapoiangalia madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ndipo tunapojikumbusha sisi wenyewe kuhusu ukweli huu.
Madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa ilitengenezwa kwa mti wa mshita, na kisha ilifunikwa ndani na nje kwa shaba nene. Mwimo wake ulikuwa ni mita 1.35, na kichanja chake, kilichosukwa kwa shaba, kiliwekwa karibu na kati kati pa hiyo madhabahu, karibu sentimeta 68 kwa mwimo. Nyama ya sadaka iliwekwa katika kichanja hiki na kisha ikachomwa.
Kila tunapoiangalia madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ni lazima tuweze kuona kwamba Yesu Kristo alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kubatizwa mwili wake, na kwamba alibeba adhabu zote za dhambi zetu kwa kuimwaga damu yake Msalabani. Kwa kweli mimi na wewe tusingeweza kukwepa bali kufa mbele za Mungu kwa sababu ya dhambi zetu na adhabu. Kwa sababu ya dhambi zetu wewe na mimi tusingeweza kukwepa bali tungekufa na kulaaniwa milele. Lakini kwa sababu ya Yesu Kristo, aliyekuja hapa duniani kama sadaka ya milele ya upatanisho, alibatizwa, akafa, yote hayo kwa ajili yetu, kama ilivyokuwa kwa sadaka ya kuteketezwa katika Agano la Kale, kwa hiyo sisi nasi tumeokolewa.
Mnyama wa kuteketezwa anaweza kuonekana mzuri na anayevutia kwa kumkumbatia anapokuwa hai, lakini inatisha kiasi gani anapokuwa akitoa damu kuelekea kufa, hali koo lake likiwa limekatwa wazi, baada ya kuwa mnyama huyo amezipokea dhambi kwa kuwekewa mikono? Ni baraka kubwa kwamba, sisi tuliostahili kufa katika hali ya kutisha kama hivi tumeikwepa adhabu yetu. Baraka hii imewezekana kwa sababu Bwana wetu ametupatia zawadi ya wokovu. Kama ilivyodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, Yesu Kristo alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, ametuokoa mimi na wewe kwa kupitia ubatizo wake na damu yake Msalabani, na kwa hiyo ametupatia zawadi ya kweli ya wokovu. Kwa hiyo, Mungu ametupatia mimi na wewe zawadi ya wokovu—je unaliamini hili katika moyo wako? Je, unaamini katika zawadi hii ya wokovu, ambayo ni upendo wa Yesu? Ni lazima sisi sote tuwe na imani hii.
Tunapoiangalia madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ni lazima tutambue kuwa Yesu Kristo ametuokoa kwa njia hii. Alisulubiwa kama hivi ili kutupatia zawadi ya wokovu. Wakati mikono ilipowekwa katika mnyama wa kuteketezwa, na mnyama huyu akatoa damu hadi kifo, Yesu ametupatia wokovu wetu kwa kuteseka kwa njia hii. Hivi ndivyo alivyotuokoa toka katika dhambi zetu. Ni lazima tulitambue hili, tuliamini katika mioyo yetu mbele za Mungu, na kisha tumpatie Mungu shukrani kwa mioyo yetu yote.
Kwa kupitia imani, Mungu anataka sisi tupokee zawadi ya upendo na wokovu ambayo ametupatia. Anataka tuamini katika mioyo yetu katika wokovu wa ubatizo na damu ya Msalaba ambayo aliitimiza kwa kuja kwake kwa kupitia maji na Roho. Ni matumaini yangu kuwa ninyi nyote mtaamini katika upendo wa Bwana wetu katika mioyo yenu na kuipokea zawadi yake ya wokovu. Je, mnaupokea ukweli huu katika moyo wako?
 

Ni Nani Aliyesulubiwa Kwa Njia Hii Kwa Ajili Yako?
 
Niliwahi kukiona kipeperushi cha ushuhuda kilichosema, “Nani atakufa kwa ajili yako? Ni nani uliyekutana naye siku hii ya leo ambaye amekufariji? Yesu Kristo alisulubiwa kwa ajili yako. Je, moyo wake haujafarijika kwa jambo hili?” Ni nani ambaye atabeba dhambi zako kwa kubatizwa na kufa Msalabani kwa niaba yako ili kuzitowesha dhambi zako? Ni nani atakayeimwaga damu yake yote na kisha kufa ili kukupatia upendo wake? Ni nani ambaye yuko tayari kukabiliana na kusulubiwa kwa ajili yako? Je, ni ndugu yako? Mtoto wako? Mzazi wako?
Hakuna hata mmoja! Ni Mungu peke yake aliyekuumba wewe. Ili kukuokoa toka katika dhambi zako, huyu Mungu alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, alibatizwa ili kuzichukua dhambi zako katika mwili wake, alisulubiwa na kuimwaga damu yake ili kubeba adhabu ya dhambi zako, amefanyika kuwa Mwokozi wako wa kweli, akafufuka tena toka kwa wafu, anaishi hata sasa, na amekupatia wokovu wake na upendo kama zawadi. Je, unapenda kweli kuupokea wokovu huu katika moyo wako? Je, unaamini kweli katika moyo wako?
Yeyote anayeamini atampokea Bwana, na yeyote anayempokea ataokolewa. Kumpokea yeye maana yake ni kuupokea wokovu na upendo ambao Kristo ametupatia sisi. Ni kwa kuamini katika mioyo yetu katika upendo huu, katika ondoleo hili la dhambi, katika kuzibeba dhambi, na adhabu ya dhambi, ndio maana sisi tunaokolewa. Hii ni imani ambayo inaipokea zawadi ya wokovu.
Kila kitu cha Hema Takatifu la Kukutania kinamdhihirisha Yesu Kristo. Mungu hahitaji sadaka yoyote ya kuteketezwa toka kwetu. Kitu pekee anachokiomba toka kwetu ni kwamba tuamini katika zawadi ya wokovu ambayo ametupatia katika mioyo yetu. “Ili kukupatia zawadi ya wokovu, nilikuja hapa duniani. Kama vile sadaka ya kuteketezwa ya Agano la Kale, nilizipokea dhambi zako zote zilizopitishwa kwangu kwa kuwekewa mikono, na kama ilivyo kwa sadaka hii ya kuteketezwa, nilibeba adhabu ya kutisha ya dhambi zako kwa ajili yako. Hivi ndivyo nilivyo kuokoa wewe.” Hivi ndivyo Mungu anavyotueleza sisi kupitia Hema Takatifu la Kukutania.
Haijalishi jinsi ambavyo Mungu ametuokoa sisi, jinsi ambavyo ametupenda sana, na jinsi ambavyo ametupatia sisi zawadi ya wokovu kamilifu kwa njia hii, ikiwa hatuamini, kila kitu ni bure. Chumvi iliyopo katika kabati lako ni lazima iwekwe katika supu ili iweze kutoa radha yake ya chumvi; vivyo hivyo, ikiwa wewe na mimi hatuamini katika mioyo yetu, basi hata ule wokovu wake mkamilifu unageuka kuwa ni kitu kisicho na maana kabisa. Ikiwa hatushukuru katika mioyo yetu kwa ajili ya injili ya maji na Roho na kuikubali katika mioyo yetu, basi sadaka ya Yesu ya kuteketezwa inakuwa haina maana.
Wokovu unaweza kuwa wako pale tu unapofahamu juu ya sadaka ya kuteketezwa na upendo wa Yesu, ambaye ni Mungu Mwokozi, aliokupatia, na kisha uukubali katika moyo wako na kumshukuru Mungu kwa ajili yake. Ikiwa hauzikubali zawadi za wokovu mkamilifu za Kristo katika moyo wako, na ikiwa unazifahamu tu kwa kichwa, basi haina maana kabisa kwako wewe kufahamu hivyo.
 

Unachotakiwa Kufanya Ni Kuunyakua Ukweli
 
Haijalishi kuwa ni kiasi gani cha supu yako inachemka katika jiko la stovu; ikiwa unafikiria wewe mwenyewe kuwa unakwenda kuweka chumvi halafu hufanyi hivyo, ukweli ni kuwa supu yako haiwezi kuwa na chumvi. Unaweza kuokolewa pale tu unapoamini na kupokea katika moyo wako kwamba Bwana wetu amekuokoa wewe toka katika dhambi zako kwa kubatizwa na kusulubiwa kwa ajili yetu, kama ilivyokuwa kwa sadaka ya kuteketezwa iliyotolewa katika madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Wakati Mungu anakupatia zawadi ya wokovu, wewe uipokee kwa shukrani. Wakati Bwana wetu anatueleza sisi kuwa ametuokoa kikamilifu, kitu sahihi tunachopaswa kukifanya ni kuamini hivyo.
Je, upendo wa Mungu ambao amekupatia ni wa nusunusu? Kwa kweli si hivyo! Upendo wa Bwana wetu ni mkamilifu. Kwa maneno mengine, Bwana wetu ametuokoa mimi na wewe kikamilifu na kiuhakika. Kwa sababu alizichukua dhambi zetu katika mwili wake kikamilifu kwa ubatizo wake na akafa Msalabani kwa uhakika, kwa kweli hatuwezi kuwa na wasiwasi wowote kuhusu upendo huu. Ametuokoa sisi kiukamilifu na ametupatia zawadi ya wokovu. Ni lazima sisi sote tuipokee zawadi hii ya wokovu ambayo Mungu ametupatia.
Hebu tufikirie kwa muda kuwa mimi ninashikilia kito cha thamani sana kilichotengenezwa kutokana na madini ya thamani sana. Ikiwa nitakupatia wewe kama zawadi, unachotakiwa kukifanya ni kuipokea zawadi hiyo kikamilifu. Je, si ndio hivyo? Je, si rahisi sana kuifanya zawadi hiyo kuwa yako? Ili kukifanya kito hiki kuwa chako, unachotakiwa kukifanya ni kukifikia na kukinyakua. Ni hivyo tu.
Ikiwa mtaifungua mioyo yenu na kuzipitisha dhambi zenu zote kwa Yesu kwa kupitia ubatizo wake, ninyi nyote mnaweza kupokea ondoleo la dhambi zenu kirahisi na kisha mkaijaza mioyo yenu mitupu kwa ukweli. Hii ndio sababu Bwana alisema kuwa atatupatia wokovu kama zawadi ya bure. Wokovu unaweza kuwa wako kwa kuufikia na kuunyakua.
Tumeupokea wokovu wetu kama zawadi pasipo kulipa hata senti moja kwa ajili ya huo wokovu. Na kwa sababu Mungu ndiye anayependezwa kutoa zawadi hii kwa yeyote anayetaka kuipokea, basi wamebarikiwa wale walioipokea kwa shukrani. Wale wanaoukubali upendo wa Mungu katika furaha wamefungwa katika upendo wake, na ni wao ambao wanampenda huyu anayetoa, kwa kuupokea upendo huo, wameupendeza moyo wa Mungu. Kuipokea zawadi hii ni kitu cha maana sana kukifanya. Ni pale tu unapoipokea zawadi ya wokovu mkamilifu ambayo Mungu amekupatia ndipo zawadi hii ya wokovu wa kweli inapoweza kuwa yako. Ikiwa hauupokei ukweli katika moyo wako, basi zawadi ya wokovu haiwezi kuwa yako hata kama utajaribu kwa nguvu kiasi gani.
Mimi pia nimeipokea zawadi ya wokovu. “Aah! Bwana alibatizwa kwa njia hii kwa ajili yangu. Hivyo kwa kubatizwa hivyo, aliivunja adhabu ya dhambi zangu zote. Alibatizwa kikamilifu kwa ajili yangu. Asante Bwana!” Hivi ndivyo nilivyokuja kuamini. Kwa hiyo, kwa sasa mimi sina dhambi. Nimepokea ondoleo la dhambi kamilifu. Ikiwa wewe pia utataka kupokea ondole hili la dhambi na kuokolewa, basi uipokee zawadi ya wokovu sasa hivi.
Nimekuwa nikifikiria kuhusu zawadi hii ya wokovu muda wote tangu wakati ule na kuendelea. Hata sasa, ninapofikiria juu ya wokovu huo tena, ninatambua kuwa hakuna chochote ninachoweza kukiona zaidi ya kumshukuru Bwana kwa ajili ya wokovu wangu. Kwa sababu upendo huu wa wokovu umo katika moyo wangu, kwa kweli siwezi kuusahau kamwe. Mara ya kwanza nilipopokea ondoleo la dhambi zangu kwa kuipokea na kuiamini injili ya maji na Roho, kwa kuuamini ukweli uliodhihirishwa katika nyuzi za bluu, zambarau, na nyekundu na kitani safi ya kusokotwa, kwa kweli nilimshukuru sana Mungu. Na hata sasa, baada ya miaka mingi kupita, bado ninamshukuru Mungu sana katika moyo wangu, na ninafanywa upya kila siku.
Kwa hakika Yesu alikuja hapa duniani kuniokoa mimi, alibatizwa ili kuzichukua dhambi zangu katika mwili wake, na akafa Msalabani ili kubeba adhabu ya dhambi zangu. Nilipotambua kuwa mambo haya yote yalifanywa kwa ajili yangu, kwa kweli niliyakubali mara moja na nikayafanya kuwa yangu. Ninatambua wakati wote kuwa hili lilikuwa ni jambo jema nililowahi kulifanya katika maisha yangu yote, tendo la busara na zuri kuliko yote. Kwa hiyo ninaamini kwamba Bwana ananipenda mimi kwa kweli na kunijali, na pia ninaamini na kukiri kuwa alifanya mambo haya yote kwa sababu alinipenda mimi. “Bwana ninatoa shukrani zangu zote kwako. Kama ulivyonipenda mimi, pia mimi ninakupenda wewe.” Kukiri hivyo ni furaha sana kwa waliozaliwa upya.
Upendo wa Bwana wetu haubadiliki kamwe. Kama ambavyo upendo wake kwetu usivyobadilika milele, basi pia upendo wetu kwake hauwezi kubadilika milele. Kwa baadhi ya nyakati tunapoteseka na kukutana na magumu, mioyo yetu inaweza kugeukia mbali na tunaweza tukatamani hata kuusahau na kuusaliti upendo huu. Lakini hata pale ambapo tumezidiwa na maumivu yetu na ufahamu wetu unatuangusha, na hata pale ambapo kila tutakachokifikiria ni maumivu yetu, Mungu bado anatushikilia sisi kwa uaminifu ili kwamba mioyo yetu isisahau kamwe upendo wake.
Mungu anatupenda milele. Kwamba Bwana wetu alikuja hapa duniani kama sehemu ya uumbaji kwa ajili yetu ni kwa sababu alitupenda hadi kifo chake. Sasa, ninakusihi uuamini upendo huu wa Mungu kwa ajili yako. Na kisha muupokee katika mioyo yenu. Je, unaamini sasa?
Ninamshukuru Bwana kwa kutuokoa sisi kikamilifu toka katika dhambi zetu kwa upendo wake.