Search

Mahubiri

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 8-9] Vitu Vyote Vinafanya Kazi Pamoja Kwa Ajili ya Mema (Warumi 8:28-30)

(Warumi 8:28-30)
“Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliwaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”
 

Leo, hebu tukiangalie kifungu hicho hapo juu kinachotoka katika Warumi sura ya 8. Kifungu kinasema kuwa Mungu alituchagua tangu asili, alituita, na akatutukuza sisi tulio katika Yesu Kristo Mwana wa Mungu. Tutazungumzia juu ya hili na jinsi watu wanavyolielewa Fundisho la Utakazo Unaozidi. 
Warumi 8:28 inasema, “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake” Ni lazima tufikirie ile sehemu isemayo “wale wampendao Mungu” kuwa inawahusu akina nani. 
Je, ni kweli kuwa vitu vyote vinafanya kazi kwa ajili ya mema? Mungu amesema hivyo. Hapo mwanzo kabla Mungu hajawaumba wanadamu, Mungu alikuwa amepanga kutufanya sisi kuwa watu wake kwa mujibu wa kusudi lake na amefanya hivyo kwa ajili ya mema katika Yesu Kristo Mwanawe pekee. 
Ni lazima tukumbuke kuwa katika Bustani ya Eden kulikuwa na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Kwa nini Mungu aliupanda mti huu? Pengine ingekuwa bora kama Mungu asingeliupanda mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Watu wengi wana udadisi mwingi kuhusiana na suala hili. 
Lakini kulikuwa na madhumuni na kusudi la Mungu pana katika mpango mzima. Mungu aliwaumba watu ili kuwafanya wawe katika sura na mfano wake. Kwa kweli, mwanadamu hakuwa na tofauti na uumbaji mwingine hadi pale tulipoipokea haki ya Mungu. 
 

Kwa Nini Mungu Aliupanda Mti wa Ujuzi wa Mema na Mabaya? 
 
Hii ndiyo sababu inayotufanya tufahamu kuwa ni kwa nini Mungu aliwaamuru Adamu na Hawa kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Kulikuwa na sababu gani? Ilikuwa ni kumuweka mwanadamu chini ya Sheria ya Mungu na kutufanya sisi kuwa watoto wake kwa kutukomboa kwa kupitia Yesu Kristo. Haki yote ya Mungu imefichwa katika Neno, “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema” Kwa kuwa Mungu alisema, “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake” (Warumi 8:28), ni lazima tutafute jibu la swali hili katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu Kristo. 
Ili kufanya hivyo, ni lazima kwanza tuikiri injili ya Mungu. Hapo ndipo tutakapotambua kuwa kila kitu anachokipanga Mungu na kukifanya ni chema. Lakini ili kuulewa ukweli huu ni lazima tuzaliwe tena upya kwa imani katika injili ya maji na Roho. Ni lazima tulitafute jibu katika injili ambayo Mungu ametupatia. 
Sababu iliyomfanya Mungu akatuumba, akapanda mti wa ujuzi wa mema na mabaya katika Bustani ya Eden, akamruhusu Adamu na Hawa kula matunda ya mti huo, na kisha akatufanya sisi kuifahamu Sheria; yote haya yalikuwa na lengo la kutufanya sisi kuwa watoto wake. Bwana wetu aliyetukomboa sisi sote, aliyaruhusu haya yote kutokea ili kwamba atupatie msamaha wa dhambi, uzima wa milele, utukufu na Mbingu. Mungu alimuumba mwanadamu toka katika mavumbi, mwanadamu aliumbwa na kuzaliwa ili awe dhaifu. Mara nyingi Biblia inatufananisha sisi na vyombo vya udongo vya mfinyanzi. Mungu, ambaye ndiye mfinyazi alimuumba mwanadamu toka katika udongo wa mfinyanzi. Mungu alimuumba mwanadamu toka katika mvumbi na akampulizia upendo wa maji na Roho. Mungu ametupatia ukweli wa maji na Roho ili kutufanya sisi kuwa watoto wake. 
Vyungu au vyombo vya udongo vilivyotengenezwa kwa udongo wa mfinyazi huvunjika kirahisi. Kwa namna hii, Mungu aliuumba kwanza mwili wa mwanadamu na roho yake ili viwe dhaifu ili amfanye mwanadamu huyo kuwa mtoto wake. Kusudi lake lilitimizwa na Yesu ambaye alizioshelea mbali dhambi za mwanadamu na kisha akawafunika kwa utakatifu wa Mungu ili kuwapatia wanadamu uzima wa milele kwa kuwafanya kuzaliwa tena upya kwa injili ya maji na Roho. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Mungu akatuumba sisi kuwa wadhaifu na tusio na ukamilifu tangu mwanzo. 
 

Kwa Nini Mungu Alimuumba Mwanadamu Akiwa Mdhaifu Tangu Mwanzo?
 
Kwa nini Mungu aliupanda mti wa ujuzi wa mema na mabaya katika Edeni na kisha akawaamuru Adamu na Hawa kutokula matunda ya mti huo? Sababu ya Mungu kufanya hivi ni lazima ifahamike na kuaminika katika injili ya maji na Roho. Baada ya Adamu na Hawa kuanguka katika dhambi, kwa nini Mungu alisema kuwa uzao wa mwanamke utamponda kichwa Shetani na kwamba Shetani atamgonga kisigino? Mambo haya yote yalikuwa na lengo la kuwafanya watu kuwa watoto wake mwenyewe. Huo ulikuwa ni mpango wa Mungu juu yetu katika Yesu Kristo Mwanawe pekee. 
Sasa, hao “walioitwa” kwa ajili ya kusudi la Mungu ni akina nani? Ni wale ambao wanazikiri dhambi zao na maovu yao na wanaozitafuta rehema za Mungu na upendo wake. Ni lazima tutambue kuwa madai ya kitheolojia yatokanayo na Fundisho la Kuchaguliwa Asili na Fundisho la Utakatifu Unaozidi ni madai ya uongo. Fundisho la Kuchaguliwa Asili ni lenye makosa kwa sababu Mungu wetu si yule anayeweza kuwachagua tu watu bila sababu hali akiwaacha wengine bila sababu. 
Bali, wale ambao Mungu anawachagua na kuwaita ni wale wanaozinung’unikia dhambi zao na kukiri kuwa hawana la kufanya zaidi ya kwenda kuzimu—hao ndio wale ambao Mungu anawaonea huruma na anawaita kwa injili ya maji na Roho. 
Miongoni mwa watu wengi wasio na hesabu wanaozaliwa katika ulimwengu huu na kurudi kwa Mungu hakuna hata mmoja ambaye Mungu anaweza kumkataa au kumwacha pasipo sababu yoyote. Ikiwa Mungu asingelikuchagua wewe kwa sababu yoyote basi bila shaka ungeasi mbele za Mungu. Ingekuwa haina maana kusema kuwa Mungu amekufanya wewe au mtu fulani kuwa mtoto wa shetani pasipo sababu yoyote. Kwa kweli Mungu hajafanya hivi. 
Ikiwa hujachaguliwa na Mungu, basi itakuwa ni kwa sababu huamini katika injili ya maji na Roho. Ikiwa huamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Mungu, basi Mungu atakukataa wewe kwa kuwa Bwana wetu alisema, “Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi” (Mathayo 9:13). Kwa bahati mbaya kile ambacho watheolojia wamekifanya ni kumgeuza Mungu kuwa mbaguzi. 
 

Ni Wapi Walioitwa Kwa Mujibu wa Kusudi la Mungu? 
 
Wale walioitwa na Mungu ni wenye dhambi ambao wamefungwa kwenda kuzimu. Wanakuja mbele za Mungu na kukiri kuwa wanastahili kwenda kuzimu kwa kuwa wao ni wadhaifu na kwamba hawana la kufanya zaidi ya kutozitii amri za Mungu hadi watakapokufa. Mungu aliwaita wenye dhambi na akawatakasa kwa injili ya maji na Roho. Mungu aliwaita wale ambao hawana la kufanya zaidi ya kwenda kuzimu na akawakomboa toka katika dhambi zao kwa injili ya maji na Roho. 
Mungu hakuja kuwaita wale walio wema na wanaoitii Sheria. Mungu anawaita wale ambao wanajaribu hasa kuishi kwa kufuata mapenzi yake lakini wanashindwa na hivyo kukiri kuwa udhaifu wao unawasukuma wao kutenda dhambi ingawa wana imani na wanamtegemea Mungu. Kusudi la Mungu ni kuwaita wadhafu, wenye mapungufu, na wanyonge ili kuwafanya hao kuwa wenye haki na kuwafanya kuwa watoto wake. Huu ndio wito wa Mungu kwa mujibu wa kusudi lake. Mambo yote yanafanya kazi pamoja kwa ajili ya wale walioitwa kwa mujibu wa kusudi lake. 
Ni lazima tuamini katika wito wa Mungu. Hatupaswi kusema kuwa tunamwamini Yesu pasipo sababu yoyote. Imani ya jinsi hiyo si imani sahihi. Imani sahihi ni kuwamini Bwana kwa mujibu wa kusudi la Mungu na si kwa kusudi lako binafsi. Hii ina maanisha kuwa ni kuamini kuwa Mungu anaufahamu udhaifu wetu vizuri na kwamba alizichukulia mbali dhambi zetu zote mara moja na kwa wote, na kwamba kwa sababu hiyo ametufanya sisi kuwa tusio na dhambi. Kwa kuiweka imani yetu katika kusudi la Mungu, ambalo ni ubatizo na damu ya Yesu Kristo, basi sisi tunaweza kufanyika watoto wake. Mapenzi ya Mungu ni kutufanya sisi kuwa watoto wake wakati tunapolikiri na kulikubali kusudi lake—watu wa jinsi hii ndio wale ambao Mungu anawapenda kwa hakika na ndio anaowaita. 
 

Ni Akina Nani Hao Waliochaguliwa na Mungu? 
 
Mungu hawezi na hapendi kuwaweka watu katika mistari miwili na kisha akamchagua kila mtu katika mkono wake wa kuume na kusema, “Njoo na umwamini Yesu kisha uende Mbinguni,” halafu akageukia mkono wake wa kushoto na kusema, “we nenda kuzimu tu.” 
Wakalvin wanadai kuwa Mungu aliwachagua baadhi ya watu pasipo sababu yoyote na kisha akaamua kuwaacha wengine tangu mwanzo. Lakini Mungu hayupo hivyo. Mungu alivifanya vitu vyote kufanya kazi pamoja kwa ajili ya mema ya wale walioitwa kwa kusudi lake. Itakuwa haina maana kufikiria kuwa tulichaguliwa bila kusudi lolote. 
Je, ina maana kuwa Mungu si Mungu wa haki? Kwa kweli hapana. Kila mtu yupo sawa mbele za Mungu na mbele za Sheria. Pia kila mtu yupo sawa mbele za hukumu. Sisi tumepokea neema ya wokovu toka kwa Mungu ambayo imetuokoa toka katika dhambi zetu kwa kupitia Yesu Kristo. Nafasi ya kuamini katika ukweli huu pia ipo sawa kwa watu wote. Mungu anawaruhusu wale waliolipokea kusudi la Mungu na wanaoufahamu udhaifu wao kuitambua na kuiamini injili ya maji na Roho. 
Je, kuchaguliwa tangu asili na kuchaguliwa ni mambo ya kimungu? Mambo hayo yapo kwa ajili yetu sisi tulioitwa kwa kusudi la Mungu katika injili ya maji na Roho ambayo Mungu ametupatia. Sisi tulizaliwa katika ulimwengu huu na tukapewa nafasi ya kuisikiliza injili kwa sababu Mungu amezichukulia mbali dhambi zetu kwa kupitia Yesu na kwamba alipanga kutufanya sisi kuwa watoto wake. Mungu aliyapanga mambo haya yote tangu hapo zamani katika Yesu Kristo. Huu ulikuwa ni mpango wa Mungu. Tunapokuja mbele za uwepo wa Mungu, basi ni lazima tuzingatie na kujiuliza kwanza ikiwa sisi tu kama Yakobo au Esau. 
Maandiko yanatueleza kuwa Mungu alimpenda Yakobo na kwamba alimchukia Esau. Pia yanaeleza juu ya Kaini na Habili, na kwamba Mungu alimpenda Habili na alimchukia Kaini. Je, ni kweli kuwa Mungu aliwachukia Esau na Kaini na akawapenda Yakobo na Habili pasipo sababu yoyote ile? Hapana. Ni kwa sababu Esau na Kaini walizitumainia nguvu zao tu na hawakuwahi kuomba rehema za Mungu, ilihali Yakobo na Habili waliyatambua madhaifu yao, waliomba rehema za Mungu na waliliamini Neno lake. 
Maandiko yanaelezea juu ya mpango wa kuchaguliwa tangu asili na kuchaguliwa kwa kuwatumia watu kama hawa kama mfano. Je, sisi tupo upande gani? Je, tunaweza kuonana na Mungu ikiwa tunazitumainia nguvu zetu wenyewe kama Esau alivyofanya? Hapana, hatuwezi! Njia pekee inayoweza kutufanya kuonana na Mungu ni kukutana naye kwa kupitia injili ya maji na Roho ambayo imejazwa na rehema za Mungu. Je, sisi tunasimama mbele za Mungu hali tukiwa upande gani kati ya pande hizo mbili? Sisi ndio wale ambao tunapenda kubarikiwa katika uwepo wa Mungu, lakini mara nyingi tunashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udhaifu wetu. Ingawa tunapenda kuishi kwa kufuata kusudi la Mungu, lakini ukweli ni kuwa sisi bado ni wadhaifu na wenye mapungufu mbele za Mungu na hivyo tunachoweza kukifanya ni kuomba rehema za Mungu. 
Ikiwa tunapenda kubarikiwa na Mungu basi inatupasa tuwe kama Yakobo, na kuwa na ile imani ambayo Habili alikuwa nayo. Ni lazima tuukiri ule ukweli kuwa sisi tu wenye dhambi mbele za Mungu na wenye mapungufu. 
Zaburi ya 145:14 inasema, “BWANA huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.” Kwa kweli, kila mtu anainama chini mbele ya uwepo wa Mungu. Hatuna ujasiri. Tunafanya mapatano na manung’uniko kwa faida ndogo. Sisi ni wanyonge. Kwa baadhi ya nyakati tunaweza kuonekana kuwa tuna ujasiri lakini ujasiri huo huwa kwa sekunde chache. Ikiwa tutayaangalia maisha yetu kwa karibu sana, basi tunaweza kuona kwa urahisi jinsi tulivyo wanyonge. Wakati mwingine tunajiweka chini ya viumbe vyenye nguvu na visivyo vya kweli ambavyo vinatusukuma sisi kuukataa ukweli. Lakini Mungu amewaita wanyonge ili awapende na awapatie wokovu katika Yesu Kristo na amewafanya wanyonge hao kuwa watoto wake. 
Tunapaswa kutambua jinsi tulivyo wanyonge na wenye dhambi ili tuweze kupendwa na Mungu. Ni lazima tujiulize ikiwa kweli tunaweza kuitii Sheria katika ukamilifu wake wote. Pia ni lazima tufike katika ukweli wa kutambua kuwa hatuwezi kuishika na kuifuata Sheria na kwamba kama ni hivyo basi hatuwezi kuishi maisha makamilifu. 
Ikiwa ningelikuwa ni mkamilifu, basi nisingehitaji Mwokozi. Ikiwa tungelikuwa ni wakamilifu, tungeuhitaji msaada wa Mungu wa nini? Tunahitaji msaada na baraka zake kwa kuwa sisi ni wadhaifu sana. Tunahitaji rehema zake. Huruma za Mungu kwetu zilikuwa na nguvu sana hata akamtuma Mwanawe pekee kuja hapa ulimwengu na kisha akamfanya kuzichukua dhambi zetu zote katika mwili wake na kuzioshelea mbali. Kisha Mungu alipitisha hukumu yake juu ya dhambi katika Yesu badala yetu ili kwamba tuweze kukombolewa toka katika dhambi. Hivi ndivi inavyotupasa kuamini. 
Ni kwa imani hii ndio tunaweza kufanyika watoto wa Mungu wapendwao. Katika kuufikia wokovu wetu tumefunikwa katika neema yake kwa sababu ya rehema zake na si kwa sababu ya juhudi zetu. 
Pamoja na kuwa Wakristo wengi wanafundisha na kulifuata Fundisho la Kuchaguliwa Tangu Asili na Kuchaguliwa, ukweli ni kuwa wakristo hao bado wana mashaka kuhusiana na fundisho hili. Hii ni kwa sababu mara nyingi wanashangaa na kufikiria ikiwa walichaguliwa na Mungu au la. 
Mafundisho haya mawili ndiyo yanayounda asilimia 90% ya theolojia ya Wakalvin. Swali linabakia kuwa ni kweli kuwa na wao wamechaguliwa au la? Na swali hili linawafanya wao kuwa na mashaka. Lakini suala si kuchaguliwa au kutochaguliwa. Bali jambo la msingi kwako ni kuamini katika injili ya maji na Roho ili uweze kuokolewa kwa kuipokea haki ya Mungu. Wale ambao wameipokea haki hii ya Mungu kwa imani ndio waliochaguliwa. 
Kuliwahi kuwepo na daktari wa theolojia ambaye alichukuliwa kuwa ni miongoni mwa wakongwe na wazamili wa theolojia kama ilivyo. Yeye alikuwa ameweka mawazo na mkazo mkubwa katika mafundisho ya Ukalvin kama vile Fundisho la Kuchaguliwa Tangu Asili na Fundisho la Kuchaguliwa Kimungu. 
Siku moja alikuwa akitoa mafundisho kuhusu mada hizi halafu mwanafunzi mmoja akamuuliza, “Sawa, je, umechaguliwa na Mungu? Unawezaje kuwafahamu wale ambao Mungu amewachagua?” 
Yule mwanatheolojia akajibu, “Ni nani awezaye kulifahamu hilo? Tutakuja kulifahamu hilo siku tutakaposimama mbele za Mungu.” 
Basi hapo yule mwanafunzi akauliza tena, “Sasa utafanyaje utakapokwenda mbele za Mungu halafu Mungu akakuambia kuwa hujachaguliwa?” 
Yule Profesa akajibu, “Nitafanya nini tena kwa jambo ambalo Mungu amekwishaliamua? Ndio maana nimesema kuwa utafahamu siku utakaposimama mbele za Mungu.” 
Wanafunzi wakafikiri, “huyu ni mtu mnyenyekevu sana. Hata mtu mkuu kama yeye anasema wazi kuwa haelewi ikiwa amechaguliwa au la. Basi ni wazi kuwa hakuna anayeweza kufahamu ikiwa amechaguliwa au la.”
Lakini ule ukweli ambao kwa huo haki ya Mungu ilikuwa imefichwa sasa umedhihirika. Kulikuwa na mambo machache ambayo Mungu alikuwa amemficha mwanadamu, lakini Mungu amejifunua mwenyewe kwa wakati. Inawezekanaje kwa wainjilisti kuhubiri injili ikiwa hawana hakika ikiwa wameokoka au wamechaguliwa? Wale walioitwa na Mungu ni wale wanaoamini katika haki ya Mungu. 
Warumi 8:29 inasema, “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.” Mungu Baba alichagua tangu asili kutufananisha sisi katika sura na mfano wa Mwanawe pekee Yesu Kristo ili kwamba awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Hapa Yesu anatajwa kuwa ni “mzaliwa wa kwanza.” Ikiwa tunamwamini Yesu na ikiwa tunaamini katika injili ya maji na Roho ambayo Mungu ametupatia, basi sisi tumeokolewa toka katika dhambi zetu zote na tumefanyika kuwa watoto wa Mungu. Sasa, mahusiano yetu na Yesu yanakuwaje? Atakuwa ni kaka yetu mkubwa. Yeye ni mtoto wa kwanza wa Mungu na sisi ni wadogo zake wa kiume na wa kike. 
Hapo zamani, nilipokuwa nikiishi katika nyumba ya maombi, mwinjilisti mmoja mzee alinitembelea. Yeye alianza kumwamini Yesu alipokuwa huko China kisha akahamia Korea. Siku moja nilimsikia akiomba hivi: “Kaka Yesu na Mungu Baba, asante sana kwa kuniokoa. Kaka Yesu, tafadhali naomba nisaidie.” Yesu ni kaka yetu!
Tunaweza kujiuliza ikiwa Mungu anafahamu kila kitu kuhusu sisi. Jibu ni ndiyo, Mungu anafahamu kila kitu kuhusu sisi. Mungu Baba anafahmu kila kitu kuhusu sisi. Mungu alipanga kutuokoa sisi toka katika dhambi zetu kwa kupitia Mwanawe pekee hata kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu huu. Huu ulikuwa ni mpango wa Mungu. Mwanawe Yesu alikuja hapa ulimwenguni, alibatizwa na akasulubiwa ili kutuokoa sisi toka katika dhambi zetu. Mungu alikuwa amekwisha panga jambo hilo. 
Tunaweza kusema kuwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, Mungu aliitisha “mkutano wa utatu.” Mungu Utatu—Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu—alipanga kuwakomboa wale wanaoamini katika haki yake. Mpango wake ulikuwa ni kuwaumba watu na kisha kuwafanya kuwa watoto wake ili aishi pamoja nao katika Ufalme mkamilifu. 
Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu wote walikubaliana na mpango huo. Sasa katika mpango wa kufikiri jinsi atakavyowaumba wanadamu na kuwafanya kuwa watoto wake, basi Mungu alipanga kumtuma Mwana wake Yesu kuja ulimwenguni na kumfanya abatizwe na kuuawa Msalabani ili kwamba wanadamu waweze kufananishwa na mfano wa Mwana wake. 
Je, kusudi la Mungu katika kutuumba ni lipi? Ilikuwa ni kutufanya sisi kuwa watoto wake. Je, Yesu ni mzaliwa wa kwanza wa Mungu? Ndiyo, yeye ni mzaliwa wa kwanza wa Mungu, na kwa kuwa sisi tumefanyika kuwa watoto wa Mungu basi sisi ni wadogo zake pia. 
Alipokuwa akiishi hapa duniani kwa miaka 33, Yesu aliyapitia madhaifu na mapungufu yote ya mwanadamu. Hii ndiyo sababu tunapoomba tunasema, “Yesu, mimi ni dhaifu sana. Hivi ndivyo nilivyo. Tafadhali naomba unisaidie na unilinde. Lainisha mioyo ya watu ili walipokee Neno lako, waangalie, wape neema, na uwasaidie.” Bwana anasikia na kuyajibu maombi yetu. Kumwomba Yesu na kumwomba Mungu ni kitu kimoja. 
Je, kusudi la Mungu katika kutuumba ni lipi? Ilikuwa ni kutufanya sisi kuwa watoto wake. Mungu anafahamu kila kitu kuhusu sisi. Mungu alitufanya sisi tuzaliwe katika ulimwengu huu na akatuokoa toka katika dhambi zetu zote kwa kupitia ubatizo wa Yesu na damu yake Msalabani, hii ni kwa kuwa alikuwa ametuchagua tangu asili hata kabla ya kuundwa kwa misingi ya ulimwengu ili aturithi sisi kuwa watoto wake wa kiume na wa kike. Si kwamba Mungu anajua maisha yetu na kifo chetu tu, bali anafahamu kila kitu kinachotuhusu. Mungu anafahamu siku tuliyozaliwa, siku tuliyooa, siku tuliyozaa watoto wetu, na yale yaliyotokea katika maisha yetu. Mungu, anayefahamu kila kitu kuhusu maisha yetu alitupatia injili ya maji na Roho ili kwamba tuweze kuamini katika Yesu Kristo na kufanyika watoto wa Mungu. 
Mungu alikwishatufahamu sisi na alikwishatuchagua tangu asili. Warumi 8:30 inasema, “Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.” Ninashindwa kukazia vya kutosha jinsi ilivyo muhimu kwetu sisi kukifahamu na kukielewa kifungu hiki. 
Watu wengi wanakitumia kifungu hicho hapo juu kuunga mkono Fundisho la Utakaso Unaozidi. Hali wakijengea msingi katika kifungu hiki—kwamba Mungu alituchagua tangu asili, akatuita, akatuhesabia haki, na akatutukuza—basi watu hao wanadai kuwa pamoja na kuwa tuna dhambi katika mioyo yetu, Mungu anatuhesabu sisi kuwa hatuna dhambi na kwamba baada ya kupita katika kipindi fulani cha utakaso basi sisi tutatukuzwa, kana kwamba kuna hatua ambazo zinatufanya kuwa watakatifu. 
Je, Mungu aliwachagua wenye dhambi wote ili kuwaita katika Yesu Kristo? Mungu alituita sisi sote lakini kuna baadhi ya watu ambao hawaupokei wito wake. Watu hao ni kama Esau na Kaini. Hao ndio wale wanaopelekwa kuzimu. 
 

Katika Rehema za Mungu
 
Mungu Baba alipanga kutuita sisi katika Mwanawe pekee Yesu Kristo na akatuchagua tangu asili ili aturithi kama wanawe mwenyewe kwa kuzioshelea mbali dhambi zetu kwa maji na Roho. Watu ambao bado hawamwendei Mungu hata pale anapowaita wapo nje ya wokovu wa Mungu. Watu wa jinsi hiyo wameondolewa toka katika neema yake na wamefungwa kuzimu. Lakini pia kuna watu ambao wameuheshimu wito wa Mungu. Wanasema, “Bwana, pamoja na kuwa mimi ni dhaifu kiasi hiki, je, utanikubali mtu kama mimi?” 
Mungu anasema, “Kwa kweli nitakukubali.” 
“Kweli? Je, utanikubali wakati mimi ni dhaifu kiasi hicho?” 
“Kwa kweli nitakukubali wewe.” 
“Mungu, sina kitu chochote cha maana cha kukupatia wewe na siwezi hata kukuahidi kuwa nitakuwa mwema tangu sasa na kuendelea.” 
“Bado nitakukubali.” 
“Sina hakika kama nitakuwa bora na kwa kweli sina hata ule uwezo wa kufanya hivyo.” 
“Hata hivyo bado nitakukubali.” 
“Labda ni kwa sababu hunifahamu. Nina hakika utanikatia tamaa.” 
Je, mara nyingi hatujisikii kana kwamba tumedhalilishwa, kana kwamba tunataka kujificha mahali fulani hasa pale tunapojifahamu jinsi tulivyo halafu mtu mmoja anatuambia kuwa anatuamini? Kwa nini huwa tunataka kujificha? Huwa tunataka kujificha kwa sababu hatuwezi kuwa bora na hatuwezi hata kudumisha yale ambayo tumeyafanya hadi sasa. 
Hii ndio sababu tunaendelea kuuliza, “je, utanikubali pamoja na kuwa mimi ni dhaifu sana? Je, ni kweli kuwa utanikubali? Je, ninaruhusiwa hata kukuamini? Je, mtu kama mimi anaweza kupokea msamaha wa dhambi? Je, mtu kama mmi anaweza kuwa mwenye haki hata pale ambapo siwezi kuwa mwema katika maisha ya baadaye?” Lakini Mungu wetu ana uwezo wa kuugeuza mzaituni mwitu kuwa mzaituni halisi. 
Kwa asili sisi ni miti ya mizeituni ambayo kwa asili yake ni ya mwituni, lakini tulifanyika kuwa mizeituni halisi kwa injili ya Yesu ambayo ametupatia. Mungu alituita sisi ambao hatukuweza kufanya lolote zaidi ya kuendelea kutenda dhambi. Je, Mungu alituita wakati tulipokuwa na udhaifu kidogo? Mungu alituita hata wakati ule tulipokuwa na uwezo. Pamoja na mapungufu na madhaifu yetu mengi, Mungu alituita katika Yesu Kristo. Mungu alituita sisi ambao si wakamilifu. Sasa alifanya kitu gani baada ya kutuita? Mungu alizichukulia mbali dhambi zetu zote na akatupatia haki yake ili kwamba tuwe na uzima wa milele. 
Je, Mungu aliyafanyaje mambo haya yote? Katika sura ya 3 ya Mathayo tunaambiwa kuwa Yesu alikuja ulimwenguni na akabatizwa ili kuitimiza haki yote ambayo Mungu ameiweka kwa ajili ya wanadamu wote. Yesu alibatizwa na Yohana, akazichukua katika mwili wake dhambi zote za wanadamu, alikufa Msalabani hali akiwa amezibeba dhambi hizo zote, kisha siku ya tatu akafufuka tena toka kwa wafu ili kuwaokoa wanadamu toka katika dhambi za ulimwengu. Mungu alitupatia maisha mapya, na kwa kufanya hivyo, alituhesabia haki na akazioshelea mbali dhambi zetu zote. Yesu alituita, akazioshelea mbali dhambi zetu kwa maji na damu, akatupatia haki ya Mungu, akatufanya tusio na dhambi, na kisha akatutukuza sisi ambao alituhesabia haki akitufanya kuwa watoto wa Mungu. 
Yesu alitutukuza sisi ili kuingia Mbinguni na kuishi milele kama watoto wa Mungu. Je, unalifahamu hili? Lakini mafundisho ya kidini yanafundisha kuwa, pamoja na kuwa u mwenye dhambi, ikiwa utamwamini Yesu basi unaweza kutakaswa taratibu kwa wakati na kwamba hadi kufikia wakati utakapokufa unaweza kwenda kusimama mbele za Mungu ukiwa mtu mkamilifu. Maelezo haya ni kinyume na ukweli. Hii si imani ya kweli. Aina hiyo ya imani ni kwa ajili ya Fundisho la Kutakaswa na si fundisho la ukweli. 
Bwana ametuokoa sisi toka katika dhambi zetu na Mungu ametuchagua tangu asili, ametuita, amezioshelea mbali dhambi zetu kwa maji na damu mara moja na kwa wote, ametufanya kuwa watoto wake, ambao tumetakaswa, na ametubariki ili kwamba tuweze kuingia katika Ufalme wa Mungu katika utukufu. Huu ndio ukweli, na hivi ndivyo alivyozungumzia kuhusu ukweli kwa kuziweka baraka zote katika Yesu Kristo. Kifungu hiki hakizungumzii kuhusu hatua saba za Fundisho la Utakaso Unaozidi. Kifungu hiki hakisemi kuwa tutafanyika kuwa watakatifu polepole baada ya kuwa tumezipitia hatua saba ili hatimaye kutakaswa kikamilifu. 
Warumi 8:30 haisemi kuwa Mungu atatuita baada ya kumwamini Yesu au kwamba tutatakaswa kadri tunavyozidi kuwa wazee. Pia aya hiyo haisemi kuwa tunapanda ngazi ya utakaso polepole hatua kwa hatua hadi tutakapoufikia utakaso mkamilifu. Wakati tulipomfahamu Yesu Kristo, na Yesu Kristo alipotuita, alitusamehe dhambi zetu mara moja na kwa wote kwa maji na damu. Ni mpaka pale tutakapomwendea Mungu hali tukiwa na injili ya kweli ndipo tutakapokumbatiwa katika mikono ya Mungu. 
Baadhi ya watu wanasema, “Hapo kabla nilikuwa sizifahamu hata dhambi zangu, lakini baada ya kuyasikia mahubiri, sasa ninaanza kutambua. Kuna dhambi moja au mbili ambazo ninazikumbuka hapo zamani na pengine ninaweza kuendelea kutenda dhambi hapo baadaye, kwa hiyo sidhani kama ninaweza kuendelea kumwamini Mungu.” Lakini hiyo si sahihi. Badala yake tunapaswa kufikiria kama ifuatavyo, “Aah! Hiyo ni sawa. Nilikuwa sizifahamu dhambi zangu hata pale nilipokuwa nikizitenda. Neno la Mungu lote ni sahihi. Ni lazima niamini katika Neno lake, lakini siwezi kuishi kwa kulifuata Neno hilo kikamilifu. Kwa kweli mimi ni mwenye dhambi mkubwa ambaye nimepangiwa kwenda kuzimu. Hii ndiyo sababu Yesu alikuja.”
Tunafanywa wasio na dhambi kwa kuamini katika Yesu na kwa kupokea msamaha wa dhambi. Tunatakaswa na kufanyika watoto wa Mungu. Kwa kuwa tumefanyika kuwa watoto wa Mungu, basi tunaweza kuingia Mbinguni na kutukuzwa. Hii ndiyo haki ya Mungu na kweli. 
Mungu alituchagua tangu asili, alituita, alituhesabia haki, na alitutukuza. Unaweza kufikiri kuwa Fundisho la Utakaso Unaozidi ni sahihi hali ukisema, “Hatimaye nitabadilika na kuwa mtu nisiye na dhambi.” Lakini unahesabiwa haki na kutakaswa mara tu unapoiamini injili ya maji na Roho. Moyo wako haubadiliki kwa hatua. Moyo wako unafanyika kuwa hauna dhambi mara moja, na ni imani yako ndiyo inayoweza kukua kwa hatua kadri unavyoliamini Neno la Mungu na kanisa lake. 
Imani yetu inakua kwa hatua na taratibu kadri tunavyozidi kulishwa Neno la Mungu hadi kufikia hatua ambayo na sisi tunaweza kuwafundisha wengine. Lakini msisitizo kuwa tutafanyika watoto wa Mungu baada ya kufanyika wakamilifu zaidi na tusio na dhambi hautokani na Biblia. Tunafanyika kuwa wasio na dhambi na tunatakaswa mara moja na daima. 
Je, Mungu alituita kwa mujibu wa kutuchagua tangu asili katika Kristo Yesu? Ndiyo, alifanya hivyo. Mungu alituita katika Yesu Kristo na akatufanya kuwa wenye haki na tusio na dhambi. Mungu alituhesabia haki na akatufanya tusio na dhambi kwa kupitia Yesu Kristo, akatuchukua kama watoto wake na akatutukuza ili kuingia katika Ufalme wajke. 
Tulifanyika kuwa wenye haki mara moja kwa kuamini katika wokovu wa Yesu Kristo ambaye aliitimiza haki yote ya Mungu. Sisi tumebarikiwa kwa sababu tuliutii wito wa Mungu na tuliamini kuwa pamoja na madhaifu yetu Yesu alizioshelea mbali dhambi zetu zote ili kutufanya sisi kuwa watoto wa Mungu wenye haki na wasio na dhambi, yaani watu wa Ufalme wa Mungu. 
Hii ndiyo sababu kuwa Fundisho la Utakaso si sahihi. Halina maana. Biblia inatueleza wazi kuwa, “Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.” Imani inakua taratibu, lakini msamaha wa dhambi, kufanyika watoto wa Mungu, na kuingia Mbinguni—haya yote yanatokea mara moja na kwa wote. Je, unaamini katika hili? 
Sisi tuliweza kufanyika watoto wa Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Mungu ameyaokoa maisha yetu yaliyokuwa hayana maana toka katika dhambi zetu zote kwa kupitia neema ya maji na Roho. Je, tulifanya kitu chochote kwa Mungu kwa namna yoyote ile kwa ajili ya wokovu wetu? Je, tulichangia katika kufanyika wenye haki? Hakuna kitu tulichokipanga, na hakuna mtu anayeamua kumwamini Yesu kabla hajazaliwa. Je, kuna yeyote anayeamua kumwamini Yesu wakati angali katika tumbo la mama yake? 
Ilitokea tukausikia ukweli toka kwa wale walioihubiri injili ya maji na Roho, na tukatambua kuwa ni ukweli, na kisha tukafikiria, “Kweli sina uchaguzi zaidi ya kuuamini ukweli huu; mwenye dhambi kama mimi ni lazima niuamini ukweli huu.” Tangu wakati huo na kuendelea tulianza kuiamini injili ya maji na Roho, tukapokea msamaha wa dhambi na tukafanyika watoto wa Mungu. 
Wenye haki tu ndio watoto wa Mungu. Mungu anawatukuza milele kwa utajiri wa milele na heshima ya Ufalme wa Mbinguni. Na hiyo ndiyo maana ya kutukuzwa ilivyo. Mungu amezitoa baraka hizi kwa waamini wanaoikubali na kuipokea injili ya maji na Roho. 
Bwana Asifiwe!