Search

Mahubiri

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 15] Hebu Tuihubiri Injili Katika Ulimwengu Wote

“Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe. Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe” (Warumi 15:1-2).
Wale wanaoamini katika haki ya Mungu hawapaswi kuitafuta hai yao wenyewe kwa kuwa Yesu Kristo hakuitafuta haki yake mwenyewe. Wenye haki wanaishi kwa ajili ya Ufalme wa Mungu na wanaihubiri injili kwa ajili ya mema ya wengine. Paulo alisema kuwa wenye nguvu wanapaswa kubeba mapungufu ya wadhaifu badala ya kujipendeza wao wenyewe. 
Waamini wa haki ya Mungu ni lazima waihubiri injili ili kwamba waweze kuzisafisha dhambi za wengine kwa ubatizo na damu ya Yesu Kristo. Hii ndiyo sababu inayomfanya Mungu awachukie wale walio wazembe na wasio huburi injili ili kuwaokoa wenye dhambi. Hivyo hatupaswi kutafuta haki yetu wenyewe bali tunapaswa kuihubiri injili kwa wengine. Ni lazima tuifikishe injili ya maji na Roho ili kwamba wenye dhambi waweze kuokolewa kwa kupitia imani. Pia ni lazima tujengane sisi kwa sisi. 
 

Usijenge Nyumba ya Imani Katika Msingi wa Mtu Mwingine
 
Aya ya ishirini inasema, “Kadhalika nikijitahidi kuihubiri injili nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.”
Kulikuwa na kitu ambacho si cha kawaida katika injili ambayo Paulo aliihubiri. Ni kwamba alijitahidi kuihubiri injili ya maji na Roho tu. Waamini wa haki ya Mungu ni lazima wajitahidi kuihubiri injili ya maji na Roho kama Paulo alivyofanya. Ili kufanya jambo hili litokee, ni lazima tuwapendeze wengine badala ya kujipendeza sisi wenyewe. Watu wanaotafuta kuwapendeza wengine wanafanya hivyo kwa sababu wamesulubiwa pamoja na Kristo na wamefufuka pamoja naye. Wale wanaomwamini Kristo hawajafa bali wanaishi. 
“Ndiyo sababu nalizuiwa mara nyingi nisije kwenu. Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena tangu miaka mingi nina shauku kuja kwenu; wakati wowote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu]. Kwa maana nataraji kuwaona ninyi katika kusafiri kwangu, na kusafirishwa nanyi, moyo wangu ushibe kwenu kidogo. Ila sasa ninakwenda Yeresalemu niwahudumu watakatifu; maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya watakatifu huko Yerusalemu walio maskini. Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumu kwa mambo yao ya mwili. Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia muhuri tunda hilo nitapitia kwenu, kwenda Spania. Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo” (Warumi 15:22-29).
 

Paulo Alikuwa ni Mhubiri Anayesafiri na Mwangalizi wa Kanisa la Mungu
 
Wakati Paulo alipokuwa katika safari yake kwenda katika Kanisa la Yerusalem ili kuwatumikia Wakristo wa Kanisa hilo alitoa mchango kwa Kanisa hilo uliotoka Makedonia na Akaya. Paulo aliongeza kwa kusema kuwa ikiwa Wamataifa wamefanywa kuwa washiriki wa mambo yao ya kiroho, basi jukumu lao pia ni kuwahudumia wao kwa mambo ya kimwili. Watakatifu pale Yerusalem walikuwa katikati ya mateso kwa wakati huo, na kwa sababu hiyo hawakuweza kujiweka huru kutokana na upungufu wa mahitaji ya kimwili. Kanisa la Yerusalem, ambalo lilikuwa likipata mateso makubwa kwa sababu ya kumwamini Yesu Kristo lilitiwa moyo sana na ndugu na akina dada Wamataifa. 
Kwa sasa kama ilivyokuwa hapo zamani, imekuwa ni kama desturi kwa makanisa ya Mungu kushirikishana utajiri wao na walio katika uhitaji badala ya kuufurahia wao wenyewe. Waamini waliojazwa Roho hawawezi kuishi kwa manufaa yo binafsi tu. Kwa nini? Kwa sababu Roho Mtakatifu anakaa ndani yao! Wao ni wale waliozaliwa tena upya na wanaoongozwa na Roho Mtakatifu anayekaa ndani yao. 
Ni jambo la kufurahisha kuona kuwa makanisa ya Wamataifa yalilisaidia Kanisa la Yerusalem. Hii ilikuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu alilisaidia Kanisa la Yerusalem kwa injili ya maji na Roho kwa kila mtu na akalipatia msaada wa vifaa au mahitaji ya kimwili pia. Kwa wakati huo pale Israeli, watu wengi walipigwa, walifungwa jela, na hata wengine waliuawa kwa ajili ya imani yao katika Kristo kama Mwokozi wao. 
Katika vipindi vya maelezo vya Televisheni, tunaweza kuona mabaki ya wafia dini wa Katakombi pamoja na maficho yao katika mapango ya milima. Haya ndiyo ambayo Kanisa la Yerusalem liliyapitia kwa wakati huo. Sisi pia ni lazima tutoe mkono wa msaada kwa makanisa ya Mungu pale yanapokutana na magumu. 
Tunaweza kuushusha umuhimu wa kusaidiana ambapo Makanisa ya Kwanza yalisaidiana, lakini huu ulikuwa ni wakati ambapo waamini walipaswa kuishi mafichoni ili kujiweka huru na mateso. Ni Roho Mtakatifu tu ndiye aliyefanya hata kule kusaidiana kuwezekana katika mazingira kama hayo. Kwa kuwa Kanisa la Yerusalemu lilikuwa chini ya mateso, basi ilikuwa ni kawaida kwa makanisa mengine kulisaidia kanisa hilo. Kwa kuwa kazi hii ilikuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu basi kazi hiyo ilikuwa inastahili na njema. 
Wewe, mwamini wa haki ya Mungu unapaswa kushiriki katika kazi kama hizo pia. Makanisa shiriki ya Huduma ya Utume wa Maisha Mapya yanachangisha fedha na kuziwekeza katika kuieneza injili katika ulimwengu mzima. Makanisa hayo yote yana aina fulani ya ugumu wa masuala ya kifedha lakini bado yana ile nia ya kuieneza injili ili kuziokoa nafsi nyingine. 
Ili aweze kuihubiri injili ya maji na Roho, Paulo alifanya kazi kama mshona mahema. Wakati kulipokuwa na mtu ambaye angaliweza kulihudumia kanisa, basi Paulo alimkabidhi mtu huyo kanisa hilo kisha Paulo alikwenda katika eneo jingine ili kuihubiri injili—hali akiwa anapata mapato yake kwa kutengeneza mahema. 
Ni kama ambavyo wewe huishi kwa ajili yako pekee, vivyo hivyo watumishi wetu hawaishi kwa ajili yao binafsi. Wale walio na Roho Mtakatifu akaaye ndani yao wanajitoa kwa ajili ya kazi za Mungu—yaani kwa ajili ya kuwaokoa wenye dhambi toka katika dhambi zao zote. Watumishi pamoja na walei katika utume wetu wanashiriki katika kuihudumia injili kwa kupitia “huduma ya kushona mahema,” kwa kuwa wanafanya kazi zao binafsi ili kujikimu wao wenyewe na kwa wakati huo huo wanatoa mchango wao katika kuieneza injili kwa kutoa fedha na kwa kujitolea kufanya kazi. 
Vivyo hivyo, tunaweza kuona kufanana sana kati ya huduma ya Paulo na ile ya kanisa la Mungu siku hizi. Sisi sote tuna aina ile ile ya ufahamu na tunaishi maisha ambayo yanampendeza Roho Mtakatifu. Ni nini kinachokuwepo katika akili zetu kunapokuwa na baridi kali sana? Kwa hakika tunawafikiria watumishi wenzetu wa Mungu na Wakristo wenzetu kuwa pengine wanateseka kutokana na baridi hii kali. Sisi, Wakristo tuliozaliwa tena upya tunajaliana na kulindana. Wenye haki wote katika Biblia walihitajiana na waliitumikia haki ya Mungu kwa pamoja. Maisha ya imani ndiyo maisha halisi ya wenye haki. 
Tumekuwa tukiishi kwa mtazamo huo wa fikra. Mara ya kwanza tulipoanza kuihubiri injili ya maji na Roho tulipaswa kuanza upya kwa kuwa hatukuwa na kitu chochote. Tulikuwa na mbinyo mkubwa wa kifedha kiasi kuwa mara nyingi tulikuwa tunapata shida sana kupata wala dola chache ili kulipia pango na bili kwa ajili ya jengo la kanisa. Lakini tulijitoa sana sisi wenyewe katika huduma ya maandiko katika nchi nzima. 
Tulipokuwa tunakutana na matatizo ya kifedha basi ni Mungu ndiye aliyetatua matatizo hayo kwa ajili yetu kwa kuwa alituruhusu kuyaona matunda ya huduma yetu. Kwa kuwa Roho Mtakatifu anaishi katika mioyo yetu basi ile shauku ya kuieneza injili inachemka ndani ya mioyo yetu bila kujalisha magumu yanayokuwepo mbele yetu. Tunapenda kuushiriki upendo wa Mungu pamoja na nafsi zote zilizopotea kwa kuihubiri injili ya maji na Roho kama ambavyo makanisa ya Mungu na wenye haki walioandikwa katika Biblia walivyofanya. 
Tunaweza kuona kuwa Wakristo waliozaliwa tena upya wa Kanisa la Mwanzo walikuwa wakiangaliana kama tunavyofanya sisi pia. Kufanya hivi hakuwezekani pasipo mwongozo wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu amekuwa akiieneza haki ya Mungu katika ulimwengu wote kwa kupitia kule kujitoa kwa waliozaliwa tena upya na ataendelea kufanya hivyo. 
 

Hata Kama Siku za Mwisho Zinatukaribia!
 
Watu wanasema kuwa sasa tunaishi katika siku za mwisho ambapo magumu yote yaliyotabiriwa katika Biblia yatatimizwa. 
Majanga na shida yatajikita yote katika siku hizo za mwisho. Kama waamini tunapaswa kusimama kwa ujasiri zaidi katika imani yetu katika haki ya Mungu na kuihubiri injili ya maji na Roho kwa juhudi zaidi. Wale wanaoamini katika haki ya Mungu ni lazima wawe na moyo wakujaliana na kupendana wao kwa wao hasa katika zama hizi za mwisho. Mioyo yetu binafsi inaweza kufanywa migumu kama inavyofanywa mioyo ya watu wa kidunia inavyofanywa migumu, lakini hatimaye tunaweza kuushinda ulimwengu huu kwa sababu tunaye Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu. Tunahitajia kuyaangalia na kuyatunza makanisa ya Mungu na nafsi zake bila kujalisha mazingira yalivyo. Ni lazima tuwajali wale ambao wanahitaji msaada wetu, tuwapende, tuwafikirie kaka zetu na dada zetu na kisha tuieneze injili hadi mwisho. 
Ni lazima tujitoe sisi wenyewe kwa ajili ya wokovu wa watu wengine zaidi ya kuitafuta haki yetu wenyewe. Bado kuna nafsi nyingi sana katika ulimwengu mzima ambazo bado hazijaisikia injili ya maji na Roho. Kuna watu wengi katika nchi nyingi ambao hawajaisikia bado injili ya maji na Roho na wala hawajapata fursa ya kuifahamu haki ya Mungu. Ni lazima tuyaweke mawazo na fikra zetu kama askari ambao tunapigana ili kuzipata nafsi na mataifa yaliyopotea kwa injili ya maji na Roho. Utume huu hautokani na shuruti, kana kwamba tunasukumwa na nguvu fulani, bali nguvu hii inatoka katika mioyo ya wale ambao Roho Mtakatifu anakaa ndani yao. 
Agizo Kuu ya Utume la kuihubiri injili ya maji na Roho hadi miisho ya dunia lipo hai katika mioyo yetu hata sasa. Ninachotaka kukueleza wewe ni kuwa kadri magumu yanavyozidi kuenea katika ulimwengu huu ndivyo Mungu anavyozidi kumwaga Roho wake Mtakatifu juu yetu. Tunaieneza injili kwa kupitia vitabu vyetu vilivyochapishwa na vitabu-pepe vikitolewa bure kwa wale walio na kiu ya kuupata ukweli huu. Tutaendelea na huduma yetu katika mtandao wa intaneti duniani kote. 
Ingawa sisi si matajiri kuliko Wamarekani na watu wa Ulaya, bado tunaweza kuwapatia injili iliyo na haki ya Mungu. Sisi tuna mawazo na fikra zilezile ambazo Petro alikuwa nazo, “Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende” (Matendo 3:6). 
Tunaweza kuwapatia injili bure ambayo imeitimiza haki ya Mungu ambayo walikuwa hawaifahamu. Ingawa sisi si bora kuliko mtu mwingine yeyote kwa vipimo vya kidunia, ukweli unabaki kuwa sisi ni watumishi wa Mungu ambao tunaweza kuitoa injili iliyo na haki ya Mungu. Wale ambao wanaweza kuielewa na kuiamini injili hii kwa kupitia huduma zetu watabarikiwa sana. 
Hiki ni kipindi cha intaneti na kwa kupitia kipindi hiki Mungu ametupatia njia ya kuweza kuufikia ulimwengu mzima. Tumeona jinsi watu walivyokuwa na furaha wakati tulipowapatia injili ambayo imeitimiza haki ya Mungu. Kadri ulimwengu unavyozidi kuwa mgumu ndivyo sisi tunavyozidi kuwa na shukrani na nguvu zaidi wakati tunapoihubiri injili ya haki ya Mungu kwa waliopotea. Je, ulimwengu utaishia tu namna hii? Au Mungu atatupatia nafasi zaidi za kuieneza injili yake? Hivi ndivyo inavyotupasa kufikiri na kuomba. Kila kitu kitatimizwa kikamilifu kwa Roho Mtakatifu. 
Kabla sijazaliwa tena mara ya pili, nilizoea kuwa mbinafsi hapo zamani, na nilikuwa nikiujali mwili wangu tu. Sisi mimi tu bali wengi wetu tulikuwa kama hivyo. Wale wanaoishi kwa ajili ya starehe za mwili tu wanaweza kudai kuwa wana upendo, lakini ukweli ni kuwa hawawezi kuwapenda wengine. Hii ndiyo tofauti kati ya wale walio na Roho Mtakatifu na wale wasio na Roho Mtakatifu. Wenye dhambi wanaweza kuishi kwa ajili yao wenyewe, lakini wale walio na Roho Mtakatifu wana nguvu ya kuishi kwa ajili ya watu wengine na kwa kweli wanaishi kwa ajili ya watu wengine pia. Mungu Utatu anawapatia waamini wake nguvu ya kuishi kwa ajili ya nafsi nyingine. Kwa kuwa Mungu anaishi katika mioyo yao na anawaongoza, basi watu hao wanaweza kuzifanya kazi zake za haki. 
Haijalishi kuwa kuna makanisa mangapi ulimwenguni, karibu mengi ya makanisa hayo yamekuwa ni kama taasisi za kiraia tu. Wanatumia fedha nyingi katika kujenga majengo makubwa ya ibada na wana bajeti kubwa zilizo katika mamilioni ya dola na wanatoa kidogo sana katika masuala ya ya kazi za kimsaada. Wamepata wazimu kwa kupata mali nyingi katika dunia hii hali wakiuacha utume wao halisi wa kuziokoa nafsi toka katika dhambi kwa kuuweka kama ni kitu cha ziada na ambacho si cha msingi. Makanisa ya jinsi hiyo hayawezi kuwa sehemu ya kanisa la Mungu, kwa kuwa kanisa la Mungu halifuatilii mambo yake binafsi kwa kuyaacha yale ya Mungu. 
Kanisa la kweli la Mungu linatumia raslimali zake katika kuziokoa nafsi zilizopote kwa uwazi na heshima. Kama Biblia inavyosema, “Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” (Mathayo 5:7), Mungu ametupatia moyo wa kuzijali nafsi katika ulimwengu huu na kisha kuziongoza kwenda katika ukombozi, na Mungu ameyafanya mambo haya yote yawezekane. Injili ya maji na Roho sasa imewekwa pamoja katika uandishi ambao umetafsiriwa katika zaidi ya lugha kuu 40 na zaidi ya matoleo 60, huku kila mojawapo ikishuhudia juu ya haki ya Mungu kwa wale ambao wanakabiliwa na kifo cha kiroho. 
Mungu atafurahishwa sana ikiwa tutaomba kwa juhudi na kuieneza injili ya maji na Roho kwa wenye dhambi wengi ili waweze kuokolewa kabla ulimwengu huu haujavamiwa na Mapigo Makuu na kufikia mwisho wake? Hebu tusikatishwe tamaa bali tuwe waaminifu hadi ule mwisho. 
Hapo zamani, maskini waliweza kuishi kwa sababu ya kusaidiana wao kwa wao. Lakini sasa tumeshaingia katika kipindi ambacho kina ushindani usio na mwisho ambapo ni wenye nguvu tu ndio wanaoweza kuendelea kuishi. Kila tunapokiangalia kizazi hiki, basi tunapata uhakika kuwa tunapaswa kuieneza injili ya maji na Roho kwa wale ambao bado hawajaisikia. Sisi sote tuna ule moyo wa kuihubiri injili ambayo italeta amani kwa wale ambao wamechoka na kudhoofika kutokana na mapambano yao yasiyo na mwisho katika ulimwengu huu mkali. Hebu tuzitoe baraka za kiroho za injili ya maji na Roho kwa watu hao. Tunaweza kuishi kwa ajili ya Kristo kwa imani zetu katika haki ya Mungu kwa kuwa Mungu amekwisha zichulia mbali dhambi zetu zote. 
Injili ambayo ina haki ya Mungu itaenea mara kumi, mara mia, mara elfu moja, mara milioni moja kwa ulaini katika wakati huu. Tutakuwa na kazi nyingi za kufanya na kwa sababu hiyo hebu na tuwe waaminifu. Wale walio na vipawa mbalimbali wanapaswa kuvitoa vipawa vyao kwa Bwana na kisha kuieneza injili kwa kila nafsi. Sisi sote ni lazima tufanye kazi katika kuieneza injili kwa mujibu wa vipawa alivyotupatia Mungu. Sisi hatuna nguvu zetu binafsi, lakini ninaamini kuwa ikiwa tutamwomba Mungu kwa jinsi ya Roho Mtakatifu ambaye yumo ndani yetu, basi Mungu atatupatia matakwa yetu. 
Kristo ametupatia sisi upendo wake wa kweli unaowapenda wenye dhambi. Tumeokolewa toka katika dhambi za ulimwengu huu kwa imani yetu katika haki ya Mungu. Hii ndiyo sababu inatupasa kufanya kazi zaidi katika kuieneza injili hata pale inapokuwa ni vigumu sana kuishi katika ulimwengu huu. Sisi tuna jukumu la kuifikisha injili kwa wale ambao bado hawajaisiki. 
Mungu alisema, “Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali” (Warumi 11:4). Bado kuna watu wengi sana katika ulimwengu huu ambao wanahitaji kupokea injili ya maji na Roho. Kuna nafsi nyingi sana, kwamba ni wachungaji, watheolojia, au walei. 
Tunaweza kuendelea kutenda kazi kwa ajili ya injili kwa sababu ya upendo wa Kristo. Bado tuna kazi nyingi za kufanya kiasi kuwa wakati mwingine tunajisikia kuwa tumezidiwa na kazi hizo. Lakini kadri tunavyopata magumu basi inatunapasa kuwa waaminifu zaidi na kuihubiri injili kwa juhudi zaidi. Huu ndio moyo wa Kristo. Ninaomba kuwa wewe mwenye haki usijifikirie wewe mwenyewe. Ikiwa utajifikia wewe mwenyewe, basi kutakuwa hakuna haja ya maombi au imani kwa kuwa utakuwa unajaribu kuishi kwa ajili yako binafsi na si kwa nafsi zilizopotea. Lakini ikiwa utapata mshahara wako kwa ajili ya kujikimu wewe mwenyewe na kuzisaidia nafsi zingine pia, ni kitu gani ambacho kitatokea? Nina hakika kuwa utaomba msaada kwa Mungu kwa kuwa wewe ni mtu dhaifu. 
Hivi ndivyo imani yetu na maombi yetu yanavyokua. Na hii ndio sababu Mungu anasema, 
“Kuna atawanyae, lakini huongezewa zaidi; 
Kuna azuiaye isivyo haki, 
Lakini huelekea uhitaji” (Mithali 11:24).
Kuwashirikisha wengine injili ya maji na Roho ndio maisha hasa ya Wakristo wenye haki. Maisha ya kiroho ni yale ambayo yanahusisha kuihubiri injili ya kweli inayowaongoza watu kwenda kwa Kristo. Hebu tuwaangalie jirani zetu na nafsi zao na kisha tuihubiri injili katika ulimwengu wote. Baraka za haki ya Mungu na ziwe juu yako daima. 
Halleluya! Na tumsifu Bwana wetu! Ninamshukuru Mungu kwa kuturuhusu kuzitenda kazi zake njema na za haki, na kwa kutukomboa toka katika nguvu za giza na kutuongoza kwenda katika Ufalme wa Mwana.