Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[12-2] Pokea Kuuawa kwa Kuifia-Dini Kwa Imani Thabiti (Ufunuo 12:1-17)

(Ufunuo 12:1-17)
 
Sura ya 12 inatuonyesha jinsi ambavyo Kanisa la Mungu litakabiliana na dhiki ya nyakati za mwisho. Aya ya 1 inasema, “Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake,na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili.” Hii sentensi ya “Mwanamke aliyevikwa jua” ina maanisha ni Kanisa la Mungu hapa duniani, na sentensi inayosema “na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake” ina maanisha kwamba Kanisa la Mungu bado lipo chini ya utawala wa ulimwengu. Hii inatuonyesha kwamba Kanisa la Mungu hapa ulimwenguni, na watakatifu ambao ni sehemu ya Kanisa hilo, watamtukuza Mungu kwa kuuawa na kwa kuifia-dini.
Msemo au sentensi inayosema, “na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili,” unaonyesha kwamba katika nyakati za mwisho Kanisa litapambana na Shetani na kisha litauawa na kuifia-dini kwa imani. Kama Neno la Mungu linavyotueleza, ni hakika kwamba Kanisa la Mungu litashinda. Pamoja na kuwa mapenzi ya Shetani ni kuiangamiza imani yetu, kututisha kwa namna zote, kutufanya tuteseke, kutudhuru, na hatimaye kudai hata uhai wetu, ukweli ni kwamba tutailinda imani yetu na kisha kuuawa kwa haki na kuifia-dini. Huu ni ushindi wa kiimani.
Katika kipindi cha Kanisa la Kwanza, watakatifu wengi waliotutangulia waliuawa pia na kuifia-dini. Mauaji haya ya kuifia-dini hayaji kwa sababu ya nguvu zetu, bali yanakuja kwa uwezo wa Roho Mtakatifu anayekaa ndani ya mioyo yetu.
Kutokana na sentensi inayosema, “mwanamke aliyevikwa jua,” basi hili neno “mwanamke” lina maanisha ni Kanisa la Mungu, na kule kusema kwamba “limevikwa jua” maana yake ni kwamba Kanisa litesubiriwa vya kutosha. Hata kati ya dhiki ya kutisha na wakati wa mapigo ya nyakati za mwisho, watakatifu watailinda imani kikamilifu na hawatamtii Shetani. Kwa nini? Kwa sababu Roho Mtakatifu aliyeko katika mioyo yao atawafanya wasimam na kumpinga Shetani, na huyo Roho Mtakatifu atawapatia imani isiyosalimu amri kwa vitisho na mateso ya aina yoyote ile ikiwemo utayari wa kuyatoa maisha yao.
Pia, kwa kuwa wale walioliweka tumaini lao katika Ufalme wa Mbinguni wanaamini katika Neno la Mungu linalowaeleza kwamba mapigo ya matarumbeta saba yatafikia ukomo na kisha kufuatwa na mapigo ya mabakuli saba ambayo yataufuta ulimwengu, basi ndio maana hawasalimu amri mbele ya Shetani.
Wale wanaofahamu na kuamini kwamba ulimwengu bora zaidi unawangojea hawawezi kamwe kumsujudia na kusalimu amri mbele ya Shetani. Mapigo ya mabakuli saba yatakayomiminwa kwa Mpinga Kristo na wafuasi wake yatawapiga bila kuchoka na bila huruma. Kwa watakatifu wanaoyafahamu vizuri mapigo hayo, ni hakika kuwa asilimia 100 ya watakatifu hao hawataitupilia mbali imani yao ati kwa sababu ya vitisho, hii ni kwa sababu Roho Mtakatifu atafanya kazi ndani ya mioyo yao. Roho Mtakatifu anayekaa ndani yetu atatupatia nguvu ya kusimama kinyume na Shetani, na kumshinda, na kisha kuuawa kwa kuifia-dini.
Wakati pigo la tarumbeta la nne litakapopita na kisha kuwasili kwa pigo la tarumbeta la tano na la sita, basi hapo ndipo “kufia-dini” kutakapotufikia. Wale watakaoilinda imani yao na kisha kuuawa na kuifia-dini ni wale tu waliozaliwa tena upya kwa maji na Roho. Wakati mapigo ya matarumbeta saba yatakaposhuka, Mpinga Kristo atakuwa na mamlaka kwa muda juu ya ulimwengu akiwa ameruhusiwa na Mungu.
Hali akifahamu kuwa mamlaka haya yatadumu kwa muda mfupi tu, watumishi wa Shetani, ambaye ni Mpinga Kristo watawatesa wale wote wanaomtumikia Yesu Kristo kama Bwana wao, ili kwamba aweze kuwachukua watu wengi kadri atakavyoweza kwenda nao kuzimu. Lakini wale waliozipitisha dhambi zao zote kwenda kwa Yesu kwa kupitia ubatizo wa Yesu hawata salimu amri kwa mateso ya Mpinga Kristo, bali watailinda injili iliyotolewa na Yesu Kristo na kisha kuuawa na kuifia-dini kwa ujasiri.
Hivyo, kuifia-dini ni ushahidi wa kiimani. Wale walio na ushahidi huu wataupata Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya zilizoandaliwa na Bwana. Hii ni kwa wale wote wanaoamini katika injili ya maji na Roho na waliotawanyika sehemu mbalimbali duniani. Biblia inatueleza kwamba watakatifu karibu wote waliozaliwa tena upya watauawa na kuifia-dini katika nyakati za mwisho.
Lakini wale ambao, kwa nia ya kukwepa vifo vya kuifia-dini, watasimama upande wa Mpinga Kristo, na kisha kumtumikia na kumwabudu kama Mungu watauawa na mapigo ya mabakuli saba na pia katika mikono ya Mpinga Kristo mwenyewe. Vifo vyao havitakuwa ni vile vya kuifia-dini bali vitakuwa ni vifo vya bure tu. Wakati Shetani na Mpinga Kristo watakapokuwa wametupwa kuzimu, basi watu waliowafuata watakwenda pamoja nao kuzimu.
Kumkana Yesu Kristo kwa nia ya kukwepa mauaji ya kuifia-dini na kupunguza magumu ya dhiki kuu hata kama ni kwa uchache tu litakuwa ni jambo la kijinga sana. Wakati mapigo ya matarumbeta saba yatakapokuwa yameisha huku wale walioilinda imani yao wakiwa wameuawa na kuifia-dini, basi hapo ndipo mapigo ya mabakuli saba yatakapoipiga dunia hii, hali yakiwaacha watu wachache tu. Kilichowazi ni kwamba wale waliopokea ondoleo la dhambi ni hakika kuwa watauawa na kuifia-dini, hivyo ili na sisi tusiweze kumkana Bwana wetu katika kipindi hiki cha kuifia-dini, tunapaswa kuiandaa imani yetu sasa kwa kuamini hali tukiwa na ufahamu sahihi wa nyakati za mwisho na uelewa sahihi wa Neno. 
Tumepokea ondoleo la dhambi zetu, hivyo wakati tutakapokuwa tukiuawa na kuifia-dini, tutakutana na furaha isiyoelezeka, kwa kuwa Mungu atatutia nguvu. Hivyo, hebu tuiweke imani yetu kwa wazi kabisa katika mioyo yetu kwamba wewe na mimi tumepangiwa kuuawa na kuifia-dini kwa ajili ya Bwana. Wakati kipindi hiki cha mauaji ya kuifia-dini kitakapopita, ni hakika kuwa Mungu atatupatia ufufuo na unyakuo, na ataturuhusu kutukuzwa katika Ufalme wa Milenia, na atatupatia Mbingu na Nchi Mpya na kutufanya tutawale ndani yake, na kuturuhusu tuishi milele katika utajiri—hasa ikiwa tutakuwa tukiyaamini haya yote kwa ujasiri, pia ni hakika kuwa mateso yetu yote yatageuzwa na kuwa furaha.
Mtume Paulo alisema, “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu” (Warumi 8:18). Paulo aliteseka sana wakati alipokuwa akiitumikia injili, mara kadhaa alipigwa karibu na kufa. Lakini kwa kuamini kwamba mateso haya yalikuwa ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, maumivu ya Paulo yaligeuzwa na kuwa furaha ya ajabu. Kwa mujibu wa rekodi za kihistoria na elimu ya mapokeo ya jadi, takribani mitume wote akiwemo Paulo, waliuawa na kuifia-dini. Inasemekana kwamba Petro alisulubiwa katika Kilima cha Vatikani kichwa chini miguu juu. Viongozi wa Kanisa la Kwanza akiwemo Polikap, pamoja na watakatifu wengine wengi waliimba nyimbo za kumsifu Mungu hata pale walipokuwa wakichomwa moto hadi kifo. Mambo kama hayo yasingeliwezekana ikiwa Mungu asingeliwatia nguvu watakatifu wake.
Pamoja na kwamba kulikuwa na watakatifu waaminifu kama hao katika nyakati hizo, ukweli ni kuwa kulikuwa na baadhi yao ambao waliikana imani yao. Origeni, ni mtheolojia anayeheshimiwa sana na watheolojia wa leo, na alikuwa ni mtu aliyeisikia injili moja kwa moja toka kwa mitume. Lakini wakati wa yeye kuuawa na kuifia-dini ulipowasili, alitoroka, yeye alisalimika ingawa watakatifu wenzake waliuawa na kuifia-dini. Jambo hili lisingeliwezekana ila kwa ukweli kwamba alikana kila kitu ambacho Yesu alikuwa amekifanya kwa ajili yake. Hivyo, Origeni alikuwa ni mwakilishi wa wale wote waliokuwa wameukana uungu wa Yesu. Lakini pamoja na yeye kumkana Yesu, watheolojia wa leo wanamwinua juu na kumuona ni miongoni mwa watheolojia wenye heshima.
Kwa nini Origeni alikwepa kuuawa na kuifia-dini wakati watakatifu wengine walipokea kuuawa kwao kwa mikono miwili? Si kwa sababu nguvu ya maamuzi ya Origeni ilikuwa dhaifu wakati ya wale watakatifu wengine ilikuwa imara. Watakatifu waliouawa na kuifia-dini huku wakimsifu Mungu walifanya hivyo kwa sababu waliamini kile ambacho Paulo alikuwa amekiongea—yaani “kwamba mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu” Kwa maneno mengine, waliweza kuyavumilia mateso yao ya sasa kwa kuwa waliamini katika Neno la Mungu la ahadi kwamba atawafufua na kuwanyakua, na kisha kuwapatia Ufalme wake wa Milenia.
Ni lazima tutambue waziwazi kwamba mauaji ya kufia-dini yatatufikia. Wale wanaoishi maisha ya imani hali wakiwa na ufahamu sahihi wa ukweli huu ni tofauti na wengine waliosalia. Wale wanaoamini kwamba picha ya watakatifu waliouawa na kuifia-dini katika Kanisa la Kwanza ni picha yao pia, basi hao wanaweza kuishi maisha ya kiimani yenye nguvu, na yenye heshima na ujasiri, hii ni kwa sababu Neno lote la Biblia litakuwa ni hadithi yao. Wataishi wakati wote wakiwa na imani inayoweza kuwawezesha kupokea mauaji ya kuifia-dini—yaani, maisha ya kuamini wakati wote kwamba, baada ya kuuawa na kuifia-dini, Mungu atawapatia ufufuo na unyakuo, na Mbingu na Nchi Mpya ambavyo alivipanga na kuwaandalia tangu zamani.
Wale wanaoamini hili wanaweza kuishi maisha ya ujasiri ya kiimani, kwa kuwa wanafahamu kwamba imani yao inawaandaa kukabiliana na mwisho wao, yaani wakati watakapoweza kufa hali wakimtukuza Mungu. Na kwa kuwa hili si jambo la fundisho la kiimani, bali jambo la imani halisi, basi wale wasioliamini Neno hili na Injili kikamilifu watakuwa wa kwanza kutuuza kwa Mpinga Kristo. Hii ni sababu, ikiwa wewe na mimi tutatambua kwamba wakati fulani tutauawa na kuifia-dini, basi ni hakika kuwa kaka na akina dada katika Kanisa la Mungu, walio na imani sawa na ya kwetu watakuwa pamoja nasi milele, na jambo hili ni la muhimu sana. Kwetu sisi, watumishi wa Mungu, watu wake, na Kanisa lake—wote ni wa thamani sana kwetu sisi.
Watakatifu wa kipindi cha Kanisa la Kwanza walikuwa na imani iliyokuwa kamilifu na ya haki zaidi ya imani yetu tunaoishi katika kipindi hiki cha nyakati za mwisho. Waliamini juu ya kuifia-dini, na juu ya ufufuo na unyakuo utakaokuja, na juu ya Ufalme wa Milenia na Mbingu na Nchi Mpya. Hii ndio sababu waliishi maisha yao ya kiimani kana kwamba wanaishi katika kipindi cha Dhiki Kuu, na kana kwamba kuja kwa Bwana kulikuwa kumekaribia. Hivyo, sisi tunaoishi katika kipindi kinachokaribia ujio wa kipindi cha Dhiki tunaposoma habari zao, basi habari zao zinaonekana kwetu kuwa ni za kweli na halisi, hii ni kwa sababu wao pia waliamini katika Neno lote la Mungu kuhusu Dhiki, kufia-dini, kufufuliwa, na kunyakuliwa.
Kwa kuwa tunaishi maisha yetu hali nyakati za mwisho zikiwa zimekaribia katika macho yetu, basi ni lazima tuiandae imani yetu ya kuifia-dini kwa uthabiti kabisa katika mioyo yetu. Shetani atamsumbua yeyote anayeamini katika maji na damu ya Kristo, hali akijaribu kuishusha imani ya anayeamini. Ili kutosalimu amri kwa usumbufu huu wa Shetani, ni hakika kuwa tunapaswa kuishikilia injili ya maji na Roho katika mioyo yetu, kisha kuichunguza hali tukiwa na tumaini katika Mbingu na Nchi Mpya, na kisha kuhakikisha kwamba imani yetu hii hailegei hadi wakati wa kuuawa kwetu na kuifia-dini.
Sababu iliyowafanya watakatifu wa kipindi cha Kanisa la Kwanza kuilinda imani yao kikamlifu ni kwa sababu walifahamu na kuamini katika Neno lote la Maandiko juu ya Dhiki, na juu ya kuuawa kwao na kuifia-dini, na juu ya ufufuo na unyakuo. Wewe na mimi pia tutauawa na kuifia-dini. Mimi nitakufa, vivyo hivyo na ninyi pia—sisi sote tutakufa ili kuilinda imani yetu. Pengine, mimi nitakuwa wa kwanza kuburuzwa na kuuawa. Jambo kama hili litaonekana kuwa ni la kutisha, lakini hatimaye, hakuna cha kuogopa, kwa maana hitimisho la kuogopa kuuawa na kuifia-dini litakuwa ni kuikana imani yetu, kitu ambacho hatuwezi kukifanya kabisa.
Mwisho wa yote, Mungu anapaswa kutukuzwa kwa kupitia vifo vyetu vya kuifia-dini, na Mungu amepanga hivi kama majaliwa yetu. Hivyo, hii ni hali ambayo tunapaswa kuipitia angalau mara moja. Kwa kuwa hatuwezi kuikwepa hali hiyo, basi hebu tuikimbilie hali tukiwa na nguvu kamili na kuisha kuirukia kwa ujasiri. Sisi tunayo mamlaka ya Mfalme ambayo hakuna mwingine yeyote aliyenayo, pia tunalo tumaini la baraka za milele. Hivyo, tunaweza kumwomba Mungu wakati wote ili atuimarishe, na kisha tukampatia utukufu zaidi. Sisi tutapokea furaha kubwa zaidi kwa kuamini pasipo hofu juu ya kuifia-dini. Huu ni utukufu mkuu wa Mungu, na baraka kubwa kwetu sisi.
Mungu aliandika Kitabu cha Ufunuo ili kutueleza kuhusu mauaji ya watakatifu ya kuifia-dini, ufufuo na unyakuo, Ufalme wa Milenia, na Mbingu na Nchi Mpya. Hivyo, ikiwa una ufahamu sahihi wa Ufunuo, basi unaweza kuishi vizuri kwa imani yako katika ulimwengu huu unaokwisha. Barabara kuelekea katika Mbingu na Nchi Mpya iliyoandikwa katika Kitabu cha Ufunuo haiwezi kutumiwa pasipo injili ya maji na Roho. Na imani hii haiwezi kuthibitika pasipo kupitia kifo cha kuifia-dini. Hivyo, ninatumaini na kuomba kwamba utaiweka imani yako katika moyo kikamilifu, hali ukiamini kwamba hautaikana injili na kwamba utauawa na kuifia-dini wakati utakapowadia, na kwamba utasonga mbele kwa imani yako. Sasa, naamini kwamba maisha yako ya kiimani yatabadilika kuanzia wakati huu.
Hatutakufa pasipo sababu ya maana, hali tukiwa tumeshikwa katika mitego ya Shetani. Tutakufa ili kuilinda imani yetu kufuatia kazi ya Roho Mtakatifu katika mioyo yetu. Na huku ndio kuifia-dini. Ni hakika kwamba siku ya kuifia-dini itawadia. Lakini hatuiogopi, kwa kuwa tunafahamu kwamba hata kama miili yetu itauawa na Shetani, Mungu atatufanya tuishi tena katika miili yetu mipya na yenye utukufu. Pia tunafahamu kwamba mauaji ya kuifia-dini yatafuatiwa na ufufuo na unyakuo, na kwamba kitakachokuwa kinatungojea kuanzia hapo na kuendelea ni baraka ya kutawala katika Ufalme wa Milenia na ufalme wetu Mbinguni.
Hapo zamani, Mtawala wa Rumi aliyeitwa Nero aliuchoma mji wa Rom ili aweze kuujenga upya. Wakati wenyeji wa Roma walipokasirika kwa sababu ya jambo hili, yeye Nero alizipeleka lawama zote kwa Wakristo na akawaua kwa mauaji ya kimbari. Vivyo hivyo, wakati majanga ya asili yatakapoupiga ulimwengu wakati wa Dhiki Kuu, Mpinga Kristo atatulaumu watakatifu kwa mapigo yote, atatushutumu na kutuua.
Hivyo, kuanzia sasa na kuendelea ni lazima tumwombe Mungu, ili atupatie imani ya kuifia-dini, yaani imani ambayo twaweza kufa kwa hiyo. Ikiwa hatuiachi imani yetu na kisha tukauawa na kuifia-dini, basi ni hakika kuwa utukufu wa Mungu utaonekana. Lakini ikiwa tutaiacha imani yetu, na kusalimu amri kwa Mpinga Kristo, na kumkubali kuwa yeye ni Mungu, ni hakika kuwa tutatupwa katika moto wa milele. Kwa maneno mengine ikiwa tutamwomba Mungu kwa imani ambayo kwa hiyo tutamshinda Mpinga Kristo, basi Bwana wetu atatupatia nguvu na ujasiri, lakini ikiwa hatuiandai mioyo yetu kikamilifu na kuikana imani yetu, basi atakachotupatia Mungu ni kuzimu.
Hebu nikusimulie hadithi fupi toka katika Vita ya Korea. Vikosi vya majeshi ya Korea Kaskazini vilifika katika kanisa fulani kusini mwa Korea, mahali ambapo dikoni mmoja aliyeitwa Chudal Bae alikuwa akilisimamia kanisa hilo. Baada ya kuona kwamba kiwanja cha kanisa ni kichafu, wale askari wavamizi walimwambia yule dikoni akisafishe. Lakini huyu dikoni alikataa, kwa madai kwamba alipaswa kuishika na kuitunza siku ya Bwana takatifu. Wale askari wakashindwa kuvumilia na wakamtishia kumuua mbele ya waumini wote ikiwa atakataa kuusafisha uwanja wa kanisa. Lakini yule dikoni aliendelea kukataa, huku akisema kwamba anapaswa kuilinda imani yake, na hatimaye aliuawa. Baadaye kidogo, baadhi ya Wakristo walikutaja kufa kwake kuwa ni kuifia-dini, lakini ni kweli kwamba kifo cha huyu dikoni si kuifia-dini. Kwa nini? Kwa sababu kuifia-dini ni kufa kwa ajili ya kazi ya haki—yaani, kuufunua utukufu wa Mungu. Kufa kwa sababu ya ugumu wa mtu binafsi kwa kisizingizio cha Mungu ni tofauti kabisa na kuifia-dini kwa haki.
Je, tunaweza kuutupilia mbali upendo wa wokovu ambao Mungu ametupatia? Yesu Kristo alizichukua katika mwili wake dhambi zetu zote kwa ubatizo wake na alisulubiwa hadi kifo kwa sababu ya makosa na dhambi zetu. Ikiwa hatutauheshimu kikamilifu upendo huu wa Bwana wetu aliounyesha hadi kifo, basi ni hakika kwamba tunaweza kuitupilia mbali injili ambayo inatupatia Mbingu na Nchi Mpya kwa sababu ya kuupendelea mwili ambao utapotea wakati wa vifo vyetu. Tulizaliwa katika ulimwengu huu kwa majaliwa ya kuokolewa, kuihubiri injili ya wokovu kwa kila mtu katika dunia hii, na kisha kufa hali tukiihubiri injili hii. Usisahau kwamba majaliwa ya watakatifu waliopokea ondoleo la dhambi, yaani majaliwa yetu binafsi, ni kuishi kwa imani na kisha kuuawa na kuifia-dini ili kuyashinda majaribu ya kiimani ya Shetani kwa ajili ya utukufu ambao Mungu atatupatia.
Sisi tuna mapungufu mengi sana na tuna mawaa mengi sana kiasi kwamba hatuwezi kumpatia Mungu utukufu kwa kitu chochote. Kwa watu kama sisi, Mungu ametupatia fursa ya kumpatia Bwana utukufu mkuu, na fursa hii si nyingine bali ni kuifia-dini. Usikwepe kuifia-dini. Hebu tumwamini Mungu ambaye atatulegezea wakati wa Dhiki ikiwa tutamwomba, hali tukiwa tumelishikilia tumaini letu la urithi wa Mbingu na Nchi Mpya, hebu tuyashinde mateso yetu ya mpito ambayo yataisha haraka. Hebu tuishi hali tukiamini kwamba Bwana hataruhusu mateso makubwa mno kwa wale wambao wamekuwa wakiishi kwa uaminifu kwa ajili yake, na kwamba hataruhusu kitu chochote ambacho kinaweza kuwafanya kuikana imani yao, na kwamba Mungu atawalinda na kuwapatia neema nyingi zaidi.
Hali tukitambua kwamba tutauawa na kuifia-dini, ni hakika kwamba tunahitaji uzoefu wa kukutana na magumu, kuvumilia mateso, na kutenda kazi ya Bwana. Kwa kupitia mambo hayo, tunaweza kuikuza imani yetu kwa kupitia uzoefu wa kutembea pamoja na Bwana, na nyakati za mwisho zitakapowadia, tutaweza kukabiliana na vifo vya kuifia-dini kwa nguvu tuliyopewa na Bwana. Ikiwa hatutakuwa na uzoefu wowote wa mateso kwa ajili ya Bwana, yaani kujitoa kwa Bwana, uzoefu wa kufanya kazi na kujitoa muhanga kwa ajili ya Bwana, basi ni hakika kuwa hofu itatutawala hasa wakati mauaji ya kuifia-dini yatakapowasili kwa ujio wa Dhiki Kuu. Ni wale tu waliopitia mateso yao na kuyashinda maumivu hapo kabla ndio wanaoweza kuyashinda mateso kwa mara nyingine tena.
Ninamwomba Mungu ili kwamba maisha yako ya kiimani yawe ni yale ya mateso kwa ajili ya Bwana na yawe ya kushinda mateso hayo, ili kwamba wakati mauaji ya kuifia-dini yatakapowasili, wewe nawe uwe miongoni mwa waaminifu wanaoweza kuikumbusha mioyo yao na kukiri kwa vinywa vyao kwamba mambo haya yote ni utukufu wao ulioruhusiwa kupitia baraka na neema ya Mungu.
Ikiwa utataka kwa nia kuuchukua Ufalme wa Mbinguni kwa imani yako, basi ni dhahiri kwamba Mbingu na Nchi Mpya zitakuwa ni mali yako. Mungu anatamani kuona watu wote wakiokolewa na kuupata ufahamu wa kweli (1 Timotheo 2:4).