Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[15-1] Watakatifu Wanaoyasifia Matendo ya Bwana ya Kushangaza Angani (Ufunuo 15:1-8)

(Ufunuo 15:1-8)
“Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia. Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema: 
‘Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, 
Ee Bwana Mungu Mwenyezi! 
Ni za haki, na za kweli, njia zako!
Ee Mfalme wa mataifa.
Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? 
Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu. 
Kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele yako, 
Kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.’ 
Na baada ya hayo nikaona, na hekalu la hema ya ushuhuda mbinguni lilifunguliwa; na wale malaika saba wenye mapigo saba, wakatoka katika hekalu, wamevikwa mavazi ya kitani safi, ya kung’aa, wamefungwa vifuani mwao mishipi ya dhahabu. Na mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba vitasa saba vya dhahabu, vimejaa ghadhabu ya Mungu, aliye hai hata milele na milele. Hekalu likajazwa moshi uliotoka kwenye utukufu wa Mungu na uweza wake. Wala hapakuwa na mtu aliyeweza kuingia ndani ya hekalu, hata yatimizwe mapigo saba ya wale malaika saba." 
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia. 
Sura ya 15 inatueleza juu ya mwisho wa ulimwengu utakaoletwa na mapigo ya mabakuli saba yatakayomiminwa na malaika saba. Je, hii “ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu,” ambayo Mtume Yohana aliiona ni nini? Ni mwonekano wa kushangaza wa watakatifu wakiwa wamesimama katika bahari ya kioo huku wakizisifia kazi za Bwana. 
 
Aya ya 2: Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu. 
Hii sentensi inayosema “kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto” inatueleza kuwa maombolezo ya kuteseka katika dunia hii yatafikia ukomo wake wakati Mungu atakapoyamimina mapigo ya mabakuli saba katika dunia, na kwa upande mwingine, watakatifu watakuwa wakimsifu Bwana angani. Mapigo ya Mungu ya mabakuli saba katika dunia hii yataletwa ili watakatifu walipize kisasi kwa adui zao. 
Wakati huu, watakatifu, baada ya kuwa wameshiriki katika ufufuo wao na kunyakuliwa na Mungu, watakuwa wamesimama katika bahari hii ya kioo iliyochangamana na moto huku wakizisifu kazi za Mungu. Watakatifu waliofufuliwa na kunyakuliwa kwa kupitia nguvu za Mungu, baada ya kuuawa na kuifia-dini hapa duniani watamsifu Bwana milele kwa ajili ya wokovu na nguvu zake. Watakatifu wanaosifu ni wale ambao watakuwa wameufikia ushindi wa kiimani kwa kumshinda Mpinga Kristo kwa imani inayomkataa yeye, na sanamu yake, na alama ya jina lake au namba ya jina lake. 
 
Aya ya 3: “Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema: ‘Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi! Ni za haki, na za kweli, njia zako! Ee Mfalme wa mataifa.”
Watakatifu wakiwa wamesimama katika bahari ya kioo wanauimba wimbo wa Musa na wimbo wa Mwana-kondoo. Na mashairi yake ni: “Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi! Ni za haki, na za kweli, njia zako!” Mashairi ya wimbo huu, kama yalivyoandikwa, yanamsifu Mungu kutokana na ukweli kuwa, Mungu, kwa kupitia nguvu zake kuu hakuna asichoweza kukifanya. Pia imeandikwa hapa kwamba “Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako [Mungu].” 
Neno “ya ajabu” lina maanisha ni “kitu ambacho ni kikuu ambacho maneno hayawezi kuelezea vizuri.” Kwa maneno mengine, ni jambo la kushangaza na la ajabu kwamba Bwana Mungu wetu amewaokoa watakatifu wote wa Agano la Kale na wale wa Agano Jipya toka katika dhambi zetu kwa kupitia injili ya maji na Roho, na kisha kuwafanya wasio na dhambi, na anawaruhusu watakatifu hawa, ambao wameokolewa kwa kupitia imani yao, kumsifu Bwana wakiwa angani kwa kuwafufua toka katika kifo cha mwili na kuwainua angani. Watakatifu hawa wanamsifu Bwana Mungu kwa kuwa Mwokozi wao, Bwana wao, na Mungu Mwenyezi. 
Je, unaamini kwa kweli kuwa Bwana Mungu ameumba ulimwengu na vitu vyote vilivyomo ndani yake, ukiwemo wewe na mimi, na kwamba Yeye ni Bwana? Wale tu wanaoamini katika ukweli huu ndio wanaoweza kuwa waamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Wale walio na imani hii ndio wale walio na imani ya kweli kabisa. Wakristo wanapaswa kufahamu na kuamini kwamba Yesu ni Muumba aliyeumba ulimwengu wote na kila kitu kilichomo ndani yake. Na wanapaswa kumsifu na kumwabudu Bwana Mungu kwa kuyafahamu na kuyaamini matendo yake. “Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi!” Kusifu huku kwa imani kunaionyesha imani ya kweli ya watakatifu waliozaliwa tena upya wanaouimba wimbo wa Mungu na wimbo wa Mwana-kondoo. 
Je, unaamini kwamba Bwana Yesu ni Mungu Mwenyezi? Wale wanaoamini kwamba Yesu ni Mungu Mwenyewe aliyeumba ulimwengu mzima pia wanaamini kwamba Bwana alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, na kwamba akiwa na umri wa miaka 30 alibatizwa na Yohana ili kuzichukua dhambi za mwanadamu katika mwiliw ake mara moja, na kwamba aliimwaga damu yake Msalabani na kisha akafufuka tena toka kwa wafu. Kwa kupitia imani yao wanapokea ondoleo la dhambi na kufanywa watakatifu. Wale wanaoufahamu ukweli huu, na walio na imani ya kweli, basi ni hakika kuwa watu hao wanaweza kutajwa kuwa ni watu wa imani kubwa. 
Kifungu hiki kinaeleza kuwa watakatifu walionyakuliwa walimsifu Mungu wakiwa angani, wakisema, “Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako” Kwa maneno mengine, walikuwa wakimsifu Bwana Mungu kwa kuumba ulimwengu na wanadamu, kwa kuwaokoa wenye dhambi katika dunia hii kwa kuzioshelea mbali dhambi zao zote mara moja kwa kupitia ubatizo wa Bwana alioupokea toka kwa Yohana, na kwa kuwapatia haki ya kufanyika wana wa Mungu—alifanya hayo yote kwa kupitia injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Ule ukweli kwamba watakatifu wanaweza kushiriki katika kuifia-dini, katika ufufuo na unyakuo, na katika uzima wa milele—basi haya yote ni baraka zilizotolewa na Mungu. 
Watakatifu wote ni lazima wampatie Mungu sifa zao ambazo zinaufunua utukufu wa Mungu kwa matendo yote ya haki ambayo Bwana ameyafanya kwa wenye dhambi—yaani, kwa kuzifanya dhambi zote kupotea, na pia kwa matendo mengine yote ambayo Bwana ameyafanya alipokuwa hapa duniani. Watakatifu wanaimba wimbo wa Musa na wimbo wa Mwana-kondoo wakiwa angani. Wanamsifu Bwana huku wakiimba jinsi ukuu wake na maajabu yake yalivyo, yaani kile ambacho Bwana Mungu Mwenyezi amekifanya kwa adui zake. 
Kwa hakika, kile ambacho Bwana amekifanya kwa watakatifu na kwa wale wote wanaosimama kinyume na Mungu si jambo la kushangaza kwetu tu, bali pia ni jambo la ajabu. Dhumuni la Mungu kwa kuumba ulimwengu huu ulilenga kuwafanya wanadamu kuwa watu wake. Hivyo, matendo yake yote aliyoyafanya kwa mwanadamu yanaonekana kwetu kuwa ni matendo ya kushangaza na ya ajabu. Tunamtolea Mungu utukufu kwa kuyaamini yale yote ambayo ameyafanya kwa ajili yetu, na tunamsifu kwa kuyaamini matendo yake yote. 
Kule kusema kwamba Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano wake ni jambo la ajabu pia. Kule kusema kwamba Mungu alitoa Sheria kwa kila mtu, na kwamba alitenda kwa kupitia Bikira Maria ili kumtuma Yesu Kristo kuja hapa duniani pia ni mambo ya ajabu mbele ya macho yetu. Lakini, kwa wakati huo huo, tunaamini kwamba matendo haya yote yalifanywa kama njia ya kuwaokoa wenye dhambi toka katika dhambi zao. Pia ni jambo la ajabu kwamba Bwana wetu amezipitisha dhambi zote za ulimwengu kwenda katika mwili wa Yesu Kristo, mara moja, kwa kumfanya aupokee ubatizo toka kwa Yohana, ili kwamba aweze kuifanya kila dhambi ya mwanadamu kutoweka kikamilifu na kwa usahihi. 
Kwa wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho, kwamba Bwana Mungu amewapatia ondoleo la dhambi la milele pamoja na Roho Mtakatifu ni jambo la kushangaza na la ajabu. Pia kule kusema kwamba Bwana amewafanya watakatifu waliookolewa kuihubiri injili ya maji na Roho katika ulimwengu mzima ni jambo jingine la kushangaza, yaani kitu ambacho ni cha ajabu kwetu sisi. Ule ukweli kwamba Mungu ataruhusu vifo vya kuifia-dini kwa wataktifu, na kuwaruhusu kufufuliwa na kunyakuliwa, na kuwafanya waishi katika utukufu milele huko Mbinguni—basi ni hakika kuwa matendo haya yote ni baraka za kushangaza. 
Baada ya kupanga mambo haya yote, Mungu atayatimiza kwa yote kama alivyopanga mara wakati utakapowadia—matendo haya ya Bwana yanayowafanya watakatifu kumsifu na kumtukuza Mungu yanabadilishwa na kuwa baraka kuu katika mioyo yetu. Pia tunamshukuru Bwana na tunabarikiwa kutokana na ukweli kwamba atalipiza kisasi kwa wapinzani wake kwa nguvu zake kuu kwa kupitia mapigo ya mabakuli saba. 
Kwa kuwa matendo yote ya Bwana Mungu yanaonekana mbele ya macho ya watakatifu kama kitu kilicho mbali na upeo wao, basi ndio maana wanamsifu Bwana. Hivyo wanamsifu Bwana kwa nguvu zake kuu, na kwa matendo na nguvu zake za ajabu. Bwana Mungu wetu anastahili kupokea sifa zote si tu toka kwa kila mwanadamu, bali toka kwa kila uumbaji katika ulimwengu huu. Helleluya!
Wale waliofahamu, waliopata uzoefu, na walioshuhudia kwa macho yao yale ambayo Bwana Mungu ameyafanya kwao hawawezi kufanya lolote zaidi ya kumsifu kwa nguvu zake kuu, kwa hekima yake kamilifu, kwa haki yake, kwa hukumu yake ya haki isiyobadilika, na na kwa upendo wake wa milele na usiobadilika. Bwana amewaruhusu watakatifu kumsifu milele kwa matendo yake ya ajabu. 
Kwa hiyo, watakatifu wanamsifu Bwana Mungu milele kwa matendo yote ambayo ameyafanya kwa ajili yao, na wanafanya hivyo kwa sababu ya wema na ukuu wa Mungu. Bwana Mungu wetu anastahili kupokea sifa toka katika vitu vyote hapa ulimwenguni, kwa kuwa matendo yake yote yamewezekana kutokana na nguvu zake kuu. Helleluya! Ninamsifu Bwana kwa nguvu zake na kwa upendo wake wa milele, usiobadilika na uliobarikiwa!
 
Aya ya 4: “Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu. Kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele yako, Kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.” 
Watakatifu wakiwa angani wanaimba sifa wakisifu matendo ya Bwana kwa vinywa vyao. “Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako?” Hizi ni sifa zilizojazwa na tumaini la kiimani, huku zikitangaza kwa ujasiri kwamba hakuna anayeweza kusimama kinyume na utukufu wa Bwana Mungu, na kwamba hakuna anayeweza kudiriki kumzuia Mungu kupokea sifa. Ni nani anayeweza kusimama mbele ya jina la Bwana pasipo kutetemeka kwa hofu? Hakuna hata mmoja wala hakuna kitu kinachoweza katika dunia hii, na katika ulimwengu mzima, kusimama na kumshinda Bwana Mungu wetu, kwa kuwa Yesu ni Mfalme wa wafalme, na Mungu Mwenyezi. 
Watu wote katika ulimwengu huu pamoja na watakatifu hawawezi kufanya lolote zaidi ya kutetemeka kwa hofu mbele ya jina la Yesu Kristo, mbele ya nguvu Bwana Mungu mwenyezi, na mbele ya ukweli wa Mungu. Kwa kuwa nguvu za Bwana Mungu ni kubwa sana, na kwa kuwa Yeye ni wa kweli na mkamilifu, basi viumbe vyote vinampatia shukrani, vinampatia utukufu na kulisifu jina lake. Kila mtu ni lazima awe na moyo unaomwogopa Mungu. Kila kitu katika ulimwengu huu ni lazima kilisifu jina la Bwana wetu. Kwa nini? Kwa sababu Bwana wetu ni mtakatifu, na amewakomboa wanadamu wote toka katika hali ya kutokuwa na haki. 
Kutokana na mapigo ya mabakuli saba ambayo Bwana atayamimina kwa Mpinga Kristo, basi wafuasi wake na wanadini wanaoishi katika ulimwengu huu wataidhihirisha haki ya Mungu, na kwa sababu hiyo hatuna la kufanya zaidi ya kumsifu Bwana. Kwa kuwa haki ya Bwana inafunuliwa kupitia mapigo makuu ya mabakuli saba, basi ni hakika kuwa Bwana Mungu wetu anastahili kupokea utukufu, sifa, na kuabudiwa na viumbe vyote hai, malaika, na watakatifu angani. 
Ni nani anayeweza kudiriki kutoliogopa jina la Bwana Yesu Kristo? Bwana wetu si kiumbe, bali ni Bwana Mungu Mwenyezi. Kwa kuyamimina mapigo ya kutisha ya mabakuli saba kwa wale wote wanaosimama kinyume na Mungu, basi ni hakika kuwa Bwana Mungu anafanya kila kiumbe kisikwepe kumsifu kutokana na nguvu na uweza wake. 
“Kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele yako, Kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.” Hivyo, ni lazima tutambue kwamba hakuna hata mmoja anayeweza kusimama na kulitukana jina la Bwana kisha akaishi kwa furaha. 
Aina ya sifa ambazo jina lake listahili kupokea ni kupiga magoti mbele ya jina la Bwana, kuliamini, kumshukuru na kumsifu Mungu kwa uweza wake, ukuu na nguvu zake, kwa rehema zake, na kwa wokovu na upendo wake mkuu. Hivyo, uumbaji wote ni lazima uamini kile ambacho Bwana amekifanya alipokuwa hapa duniani, na kisha umsifu na kumwabudu Yeye. Bwana wetu anastahili kupokea sifa toka kwa watu wote na mataifa yote. Amin. Halleluya!
 
Aya ya 5: Na baada ya hayo nikaona, na hekalu la hema ya ushuhuda mbinguni lilifunguliwa.
Aya hii inatueleza kwamba baada ya kuisha kwa mapigo ya mabakuli saba ambayo Bwana Mungu atayamimina hapa duniani, Mungu atawapatia watakatifu nyumba yake ya Mbinguni. Mambo haya yote yatatimizwa na Bwana Mungu. Sasa hili hekalu la hema ya ushuhuda ni kitu gani? Ni nyumba ya Mungu ambayo ni kama hema takatifu la kukutania la hapa duniani. Msemo huu, “hekalu la hema ya ushuhuda mbinguni lilifunguliwa” una maanisha kuwa kipindi cha Ufalme wa Bwana Mungu kitafunguliwa kuanzia hapo. 
Mapigo ya mwisho na Ufalme wa Bwana Mungu utaletwa hapa duniani kwa kuufungua mlango wa hekalu la hema ya ushuhuda. Hakuna imani itakayoruhusiwa kuingia mbele za Mungu ikiwa haiifahamu injili ya maji na Roho. Hivyo, tunapaswa kuifahamu na kuiamini injili hii na kisha kutambua na kuamini kwamba wakati wa sisi kwenda kuishi katika Ufalme wa Kristo unakaribia.
 
Aya ya 6: na wale malaika saba wenye mapigo saba, wakatoka katika hekalu, wamevikwa mavazi ya kitani safi, ya kung’aa, wamefungwa vifuani mwao mishipi ya dhahabu. 
Neno hili linatuonyesha kuwa wakati Mungu atakapoyamimina mapigo ya mabakuli saba katika ulimwengu huu, Mungu atafanya kazi kupitia malaika wanaoamini juu ya umuhimu wa haki na usawa wa haya mapigo saba. Kwa maneno mengine, neno linatueleza kuwa watumishi wa Mungu wanaweza kustahilishwa kumtumikia Bwana na kuwa watumishi wake pale tu wanapokuwa wakiamini katika haki yake na kuyaweka matumaini yao yote katika wema wa Mungu. 
Watumishi wa Mungu wanaweza kuzifanya kazi za Mungu pale wanapokuwa wakiamini kwamba matendo ya Bwana ni sahihi wakati wote. Hivyo, watakatifu wanaweza kutumiwa kama watumishi wa Mungu wenye thamani pale tu wanapokuwa wamejivika haki ya Mungu, na kujivisha tumaini la wokovu kama kofia ya chuma, na kuilinda imani yao, na kisha kuishi maisha ambayo yanamtukuza Bwana. 
 
Aya ya 7: Na mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba vitasa saba vya dhahabu, vimejaa ghadhabu ya Mungu, aliye hai hata milele na milele. 
Hii inatueleza kwamba wakati Mungu anapofanya kazi kupitia watumishi wake, basi anawafanya watende kazi katika namna yenye utaratibu, na kwamba kazi hizo pia zinatimizwa kwa utaratibu mzuri. Msemo, “mmoja wa wale wenye uhai wanne,” unatuonyesha kuwa Bwana anao watumishi wa thamani sana waliowekwa kwa ajili ya madhumuni yake, na kwamba Mungu anafanya kazi kupitia watumishi hao. Viumbe wenye uhai wanne wanaoonekana hapa ni watumishi wanne wa Bwana ambao ni wa thamani zaidi ambao wakati wote wapo karibu naye, na watumishi hao ndio wa kwanza katika kuyatimiza madhumuni ya Mungu. Tunapaswa kuyatambua mamlaka ya Mungu na uweza wake mkuu, pia ni lazima tuamini kwamba Mungu anafanya kazi kupitia watumishi wake. 
 
Aya ya 8: Hekalu likajazwa moshi uliotoka kwenye utukufu wa Mungu na uweza wake. Wala hapakuwa na mtu aliyeweza kuingia ndani ya hekalu, hata yatimizwe mapigo saba ya wale malaika saba.
Ni hakika kuwa hakuna hata mmoja anayeweza kuingia katika Ufalme wa Mungu kabla Bwana Mungu hajaitimiza hukumu yake hapa duniani. Hii inatueleza jinsi utakatifu wa Mungu ulivyo mkamilifu. Pia inatueleza kuwa yeye si Mungu anayeufurahia uovu (Zaburi 5:4). Hivyo, ni lazima tukumbuke kuwa ikiwa mtu yeyote anataka kuingia katika Ufalme wa Mungu, basi imempasa mtu huyo kuamini katika injili ya maji na Roho ambayo Bwana ameitoa kwa wanadamu. Bwana Mungu wetu anawaruhusu wale tu wanaoamini katika injili ya maji na Roho kuingia katika Ufalme wake. 
Mungu ametoa baraka kwa watakatifu waliopokea ondoleo la dhambi kuishi milele katika Ufalme wake, hii ni baada ya kuwa amewaangamiza maadui zake kwa kuwamiminia mapigo ya mabakuli saba. Kazi na matendo yote ya Mungu yanakwenda na kufanyika kupita uwezo wa fikra za mwanadamu, na kwa sababu hiyo Mungu anaufunua ukuu wake na mamlaka yake. Mungu anadhihirisha ukuu na nguvu zake kwa kuwahukumu maadui zake. Kama Mungu asingelikuwa na nguvu ya kuwaadhibu maadui zake kwa sababu ya dhambi zao na kwa kule kusimama kinyume naye, basi ni hakika kuwa asingeliweza kupokea sifa toka kwa wote. 
Lakini, akiwa ni Mungu anazo nguvu zaidi za kuwaadhibu wale wanaosimama kinyume naye, ni hakika kuwa Bwana Mungu ataleta hukumu yake kwa maadui zake, na atawaadhibu kwa adhabu ya milele ya kuzimu. 
Bwana Mungu wetu anastahili zaidi kupokea sifa milele toka kwa kila mtu katika kila taifa. Hivyo, Mungu ataitimiza hukumu yake dhidi ya maadui zake kwa dhambi zao zote kisha ataufungua Ufalme wake. Amin. Tunamshukuru Bwana Mungu wetu kwa nguvu zake kuu, na kwa utukufu na utakatifu wake. Halleluya!