Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[19-1] Ufalme Utakaomilikiwa Na Mwenyezi (Ufunuo 19:1-21)

(Ufunuo 19:1-21) 
“Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu. kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake. Wakasema mara ya pili, Haleluya. Na moshi wake hupaa juu hata milele na milele. Na wale wazee ishirini na wanne, na wale wenye uhai wanne, wakasujudu na kumwabudu Mungu, aketiye katika kile kiti cha enzi, wakisema, Amina, Haleluya. Sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Msifuni Mungu wetu, enyi watumwa wake wote, ninyi mnaomcha, wadogo kwa wakuu. Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki. Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari. Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing`arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu. Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu. Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii. Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita. Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe. Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu. Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi. Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA. 
Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, Njoni mkutane kwa karamu ya Mungu iliyo kuu; mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa. Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake. Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti; na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, “Haleluya; wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu.”
Kifungu hiki kinawaelezea watakatifu wakimsifu Bwana Mungu wakati siku yao ya harusi na Mwana-kondoo ikikaribia. Bwana, Mungu wetu amewapatia watakatifu wokovu wao na utukufu, ili kwamba waweze kumsifu Bwana kwa nia njema. Watakatifu walionyakuliwa angani wataendelea kumsifu Bwana Mungu, kwa kuwa neema zake ni kuu kwa kuwakomboa toka katika dhambi zao zote na adhabu ya dhambi hizo isiyokwepeka. 
Neno “Alleluya” au “Halleluya” ni neno unganishi linalounganisha maneno mawili ya Kiebrania ya “halal,” lenye kumaanisha kusifu, na “Yah,” lenye kumaanisha “Yehova.” Hasahasa, Zaburi ya 113-118 katika Agano la Kale zinatajwa kuwa ni “Halle za Misri” yaani “Sifa za Misri” na Zaburi 146-150 zinatajwa kuwa ni “Zaburi za Hallel au Zaburi za Sifa.” 
“Zaburi hizi za Sifa” ni nyimbo ambazo zinaendana na furaha na huzuni ya watu wa Kiyahudi, hali zikiwapatia nguvu nyakati za huzuni na dhiki, na wakati mwingine ziliimbwa kama nyimbo za furaha hasa katika nyakati za wokovu na ushindi. Pia sifa hizi za “Halleluya” zilikuwa zikiimbwa na kutolewa kwa Mungu tu. Hii ni kwa sababu hukumu ya Bwana ya mapigo makuu kwa ulimwengu huu ni ya kweli na ya haki, na kwa sababu wokovu, nguvu, na mamlaka ni vya Mungu tu. 
 
Aya ya 2: “Kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.”
Kule kusema kwamba Mungu atawalipia kisasi watakatifu kwa kuyamimina mapigo ya mabakuli saba juu ya wanadini wote wa dunia hii na wasioamini, ni hukumu ya Mungu ya kweli na ya haki. Kwa kuwa wanadini wa ulimwengu huu waliwaua wasio na dhambi na watumishi wenye haki wa Mungu, basi sasa ni zamu yao kuhukumikiwa na Mungu kwenda katika mauti ya milele. 
Kuna kitu chochote kibaya ambacho watakatifu wamekifanya hapa duniani ambacho kinawastahilisha kuuawa na hawa wanadini wa ulimwenguni? Kwa kweli hapana! Lakini wanadaini wote wa hapa ulimwenguni wameungana ili kuwaua wana wa Bwana Mungu. Kwa hiyo, kitendo cha Mungu cha kuyamimina mapigo haya ya mabakuli saba juu ya hawa wauaji ni ya haki, na inadhihirisha haki ya Mungu. 
 
Aya ya 3: “Wakasema mara ya pili, Haleluya. Na moshi wake hupaa juu hata milele na milele!”
Watakatifu wanamsifu Bwana Mungu angani kwa sababu siku ya harusi yao pamoja na Yesu, ambaye amefanyika kuwa Mwana-kondoo, imekaribia. 
“Na moshi wake hupaa juu hata milele na milele.” Hii ina maanisha ni moshi unaotoka katika ulimwengu huu ulioangamizwa na kuunguzwa na mapigo makuu ya mabakuli saba yaliyomiminwa na Mungu. Hii inatuonyesha kwamba ulimwengu huu hautaweza kupona toka katika magofu yake, kwa kuwa maangamizi yake yatakuwa ni ya kutisha na ya milele. 
 
Aya ya 4: “Na wale wazee ishirini na wanne, na wale wenye uhai wanne, wakasujudu na kumwabudu Mungu, aketiye katika kile kiti cha enzi, wakisema, Amina, Haleluya.” 
Ule ukweli kwamba siku ya harusi ya watakatifu na Bwana Yesu imekaribia ni tukio lenye utukufu kiasi kwamba wale wazee 24 na wale wenyeuhai wanne huko Mbinguni wanamwabudu na kumsifu Bwana Mungu aketiye katika kicha chake cha enzi. Hii ndio sababu watumishi wa Mungu wanamsifu Bwana Mungu wakiwa angani. 
 
Aya ya 5: “Sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Msifuni Mungu wetu, enyi watumwa wake wote, ninyi mnaomcha, wadogo kwa wakuu.”
Kwa kuwa siku ya harusi ya Mwana-kondoo pamoja na watakatifu ni siku ya furaha sana kwa watumishi na watakatifu wake wote ambao wameokolewa kwa kumwamini Bwana Mungu, basi ndio maana sauti toka katika kiti cha enzi inawaamuru kumsifu Bwana. Sasa, wakati umefika kwa watumishi wa Mungu na watakatifu wake wote kufurahi na kumsifu Bwana. 
 
Aya ya 6: “Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki.”
Aya hii inatueleza kwamba kwa kuwa wakati wa utawala wa Bwana Mungu umekaribia, basi sasa ni wakati wa watakatifu wake na watumishi kupokea amani, furaha, na baraka ya milele zinazotiririka kama mto. Na hii ndio sababu wanamsifu Bwana Mungu. Watakatifu wanamsifu Mungu wetu wakiwa angani ilhali mapigo makuu yakiendelea hapa duniani kwa kuwa wakati umefika wa wao kutawaliwa na Bwana Mungu—yaani, sasa ni wakati wa Mungu kuwatukuza watakatifu wake. Sauti ya watakatifu wakisifu wakati huu ni kama sauti ya ngurumo ya maji mengi. Hivyo, chakula cha harusi ya Ufalme wa Mbinguni kinaanza kwa sifa nzuri za watakatifu. 
 
Aya ya 7: “Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.”
Sasa, wakati ambapo mapigo ya mabakuli saba yaliyoletwa na Mungu yakiisha, aya hii inatueleza kwamba wakati umefika kwa watakatifu wote kushukuru na kushangilia. Watakatifu wanashukuru na kufurahia kwa sababu siku imewadia ya wao kufunga harusi na Bwana na kisha kuishi katika Ufalme wake. Ili aweze kuishi pamoja na watakatifu, Bwana Mungu wetu ameandaa Mbingu na Nchi Mpya, mji mtakatifu na bustani zake, na utukufu wote na utajiri, na kwamba hivi sasa Bwana anawangojea hao watakatifu. Kuanzia sasa na kuendelea, watakatifu watatawala pamoja na Bwana milele. 
 
Aya ya 8: Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu. 
Bwana amewapatia watakatifu mavazi mapya, ambayo yametengenezwa kwa kitani safi. Yeyote anayeishi huku akimtumikia Bwana Mungu anakuwa amevikwa mavazi haya. Kwa maneno mengine, Mungu anawavika watakatifu kwa mavazi ya Mbinguni. Mavazi haya ya kimbingu ya kitani safi hayawezi kulowanishwa na jasho. Hii inatueleza kwamba sisi tumefanyika kuwa mabibi harusi wa Mwana-kondoo si kwa sababu ya jitihada zetu binafsi, bali imewezekana hivyo kwa imani yetu katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana Mungu. 
Ikilinganishwa na vazi jekundu na la zambarau linalovaliwa na Mpinga Kristo, hii kitani safi ni ya thamani sana na imekuwa ikitumika kutengeneza mavazi ya makuhani na wafalme. Hali ikitoa uhuru wa kuwa mbali na jasho, kitani safi inatuonyesha kwamba wale walivikwa na neema ya Mungu na haki yake sasa wamefanyika kuwa watu wake. 
Sentensi hii inayosema, “kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.” Ina maanisha kwamba wale waliofanyika na kuwa watakatifu kwa neema ya wokovu iliyotolewa na Bwana Mungu walimpatia Mungu utukufu kwa kuuawa na kuifia-dini, yaani kwa kuuawa na Mpinga Kristo na wafuasi wake katika kuilinda imani yao. Kwa maneno mengine, “Matendo ya haki,” hayamaanishi ni haki ya Torati, bali ni vifo vya watakatifu wakiifia-dini ili kuilinda imani yao ya thamani. Vivyo hivyo, mabibi harusi wote wa Yesu Kristo wa nyakati za mwisho ni wafia-dini, ambao ili kuilinda imani yao katika Bwana, walisimama kinyume na kupambana na Mpinga Kristo na wafuasi wake wakati walipokuwa hapa duniani. 
Ili kujiandaa kwa imani ya kuweza kuifia-dini, watakatifu wote ni lazima waimarishwe kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu katika ile miaka ya Dhiki Kuu, kwa kuwa baada ya kuisha kwa hii miaka mitatu na nusu, ni hakika kwamba watauawa na kuifia-dini. 
 
Aya ya 9: Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.”
Wakati mapigo ya Mungu yatakapoisha hapa ulimwenguni, Bwana Mungu atawaalika watakatifu wote katika karamu ya harusi ya Mwana-kondoo (Ufalme utajengwa na kutawaliwa na Bwana), na atawaruhusu kuishi katika Ufalme wa Kristo. Wale walioalikwa katika karamu ya harusi ya Mwana-kondoo ni wale waliobarikiwa. Mungu wetu ametueleza kwamba hatashindwa kulitimiza hili Neno la ahadi. Itafika siku ambapo watakatifu watafunga harusi na Bwana. Bwana wetu atakuja hapa duniani ili kuwachukua wanaharusi wake, yaani wale waliosafishwa dhambi zao zote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Naye Bwana ataishi pamoja na wanaharusi wake milele na milele katika Ufalme wake. 
Muungano wa watakatifu pamoja na Bwana utakamilika wakati watakatifu watakaponyakuliwa na Kristo, ambapo watapokea utukufu usioisha na thawabu ya Ufalme wa Milenia. Halleluya! Ninamsifu na kumshukuru Bwana Mungu ambaye ametufanya sisi kuwa watu wake. 
 
Aya ya 10: Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.”
Watakatifu ni lazima wampatie utukufu wote Bwana Mungu pekee. Mungu wetu Utatu ndiye anayestahili kupokea sifa zote na kuabudiwa na watakatifu wote. 
Sentensi inayosema, “Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii,” ina maanisha kwamba ushuhuda na unabii wa Yesu unakuja kwa kupitia Roho Mtakatifu. 
 
Aya ya 11: Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.
Wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, Bwana Mungu wetu, hali akiwa amepanda farasi mweupe, atapigana na Shetani kwa haki yake na kumfunga na kumtupa katika shimo la kuzimu lisilo na mwisho na katika ziwa la moto. 
Hapa, jina la Yesu Kristo ni “Aminifu” na la “Kweli.” Neno “Aminifu,” lina maanisha kwamba Kristo anastahili na anaaminika, linaelezea uaminifu wa Yesu na usahihi wake, wakati neno “Kweli,” lina maanisha kwamba Yesu yupo mbali na uongo, na linatueleza kwamba Kristo atamshinda Mpinga Kristo kwa hukumu ya haki ya Mungu. 
 
Aya ya 12: Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe. 
Kule kusema kwamba macho ya Bwana yalikuwa “kama mwali wa moto” kunatueleza kwamba Yeye ana nguvu ya kuwahukumu wote. Kwa upande mwingine, sentensi inayosema “na juu ya kichwa chake vilemba vingi,” ina maanisha kwamba Bwana wetu anashinda wakati wote katika mapambano yake dhidi ya Shetani, kwa kuwa Yeye ni Mungu Mwenyezi na mwenye nguvu. 
 
Aya ya 13: Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
Bwana wetu atawalipia kisasi watakatifu dhidi ya adui zao kwa kuwahukumu maadui wake kwa ghadhabu kuu, yaani maadui ambao walisimama kinyume naye. Huyu Mungu si mwingine bali ni Yesu Kristo Mwenyewe. Kama alivyo ahidi kwa Neno lake, ni hakika kwamba Bwana wetu alikuja hapa duniani katika mwili wa mwanadamu, akabatizwa na Yohana ili kuzibeba dhambi zote za ulimwengu, akazibeba hizo dhambi hadi Msalabani, na akazifanya dhambi za wanadamu wote kutoweka. 
Sentensi hii “vazi lililochovywa katika damu” haizungumzii damu ya Kristo. Inazungumzia juu ya damu ya maadui ikiwa imerukia katika vazi la Bwana hasa wakati akiileta hukumu yake ya kutisha ya ghadhabu kwa maadui hao na wakati ambapo akiwakanyaga kwa miguu yake yenye nguvu. 
Hii sentensi “Neno la Mungu” ina onyesha juu ya tabia ya Yesu. Kwa kuwa Bwana wetu anafanya vitu vyote kwa kupitia Neno lake lenye nguvu, basi ndio maana anatajwa kuwa ni “Neno la Mungu.” 
 
Aya ya 14-16: Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi. Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA.
Jeshi la Bwana Mungu litazifanya kazi za Mungu wakati wote, hali likiwa limevikwa katika neema yake yenye utukufu. 
Mungu atauhukumu ulimwengu huu kwa Neno linalotoka katika kinywa chake. Bwana wetu ametuahidi wakati wote kwa Neno la kinywa chake, na analitimiza hili Neno wakati wote kwa nguvu zake. Yeye atakaye uhukumu ulimwengu na kumuangamiza Shetani ni Yesu Kristo, Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana. 
 
Aya ya 17: Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, “Njoni mkutane kwa karamu ya Mungu iliyo kuu;”
Hatimaye ulimwengu huu pamoja na Shetani na wafuasi wake vitaangamizwa na Yesu Kristo. Biblia inaelezea kuangamizwa huku kwa ulimwengu kuwa ni karamu kuu ya Mungu. 
 
Aya ya 18: “mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa.”
Hili Neno linatueleza kwamba kwa kuwa ulimwengu mzima na kila mtu akaaye ndani yake atakuwa ameuawa mara baada ya mapigo makuu ya Bwana Mungu yatakapokuwa yameisha, basi ndege warukao angani watayajaza matumbo yao kwa kula mizogo ya watu hao. Hao ndege watafanya hivyo kwa kuwa Mungu atakuwa ameyamimina mapigo makuu ya mabakuli saba katika ulimwengu huu. Bwana wetu alituambia kwamba, “Kwa kuwa popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai (Mathayo 24:28).” Katika ulimwengu wa nyakati za mwisho, kutakuwa na maangamizi, vifo, na adhabu ya kuzimu kwa wenye dhambi. Lakini kwa watakatifu, kutakuwa na baraka ya kutawala katika Ufalme wa Kristo. 
 
Aya ya 19: Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake. 
Mpinga Kristo, ambaye ni mtumishi wa Shetani, na wafuasi wake watasimama dhidi ya watumishi wa Mungu na watakatifu wake na watajaribu kuwashinda hadi mwisho wako utakapofikia. Lakini kwa kuwa Bwana wetu ni Mfalme wa wafalme, atamkamata Mpinga Kristo na yule nabii wa uongo, atawatupa katika ziwa la moto, na kisha atawaua watumishi wao kwa upanga wa Neno lake. 
 
Aya ya 20: Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. 
Hili neno “Mnyama” lina maanisha ni Mpinga Kristo. Na hili neno “nabii wa uongo” ni mtumishi wa Mpinga Kristo, ambaye kwa kufanya ishara na miujiza, atawageuza watu waiache imani katika Neno la kweli. Bwana Mungu wetu atamuangamiza Shetani, Mnyama (Mpinga Kristo), nabii wa uongo, na wafuasi wa Shetani ambao waliiabudu sanamu ya Mpinga Kristo na wakasimama kinyume na Mungu, kinyume na watakatifu, na kinyume na injili ya maji na Roho. 
Hili “ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti” lina maanisha ni jehanamu. Jehanamu ni tofauti kidogo na shimo kuzimu lisilo na mwisho. Wakati shimo la kuzimu lisilo na mwisho ni mahali ambapo Shetani atafungwa kwa muda, “ziwa la moto” ni mahali ambapo watapata adhabu yao ya milele. Kimsingi, moto na kiberiti vimekuwa vikitumika katika Biblia mara kwa mara kama zana za Mungu za adhabu na hukumu. 
Baada ya ulimwengu huu kuangamizwa, Bwana wetu atarudi hapa duniani pamoja na watakatifu wake, atamwangamiza kwanza Shetani na watumishi wake, kisha ataungua Ufalme wa Kristo. Kisha watakatifu wataishi na kutawala pamoja na Bwana ktika Ufalme wa Kristo kwa miaka elfu moja itakayofuata. 
 
Aya ya 21: Na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.
Ulimwengu huu uliumbwa na Neno toka katika kinywa cha Bwana Mungu wetu; vivyo hivyo, maadui wa Mungu wataangamizwa wote kwa Neno la hukumu toka katika kinywa cha Bwana. Kisha Ufalme wa Kristo utaanzishwa hapa duniani. Hivyo, watakatifu wanapaswa kuliweka tumaini lao katika Ufalme wa Kristo na kisha kmpatia Mungu utukufu kwa kupigana dhidi ya Shetani, Mpinga Kristo na wafuasi wake, na kwa kuvipokea na kuvikubali vifo vya kuifia-dini kwa imani.