Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[20-1] Joka Atafungwa Katika Shimo la Kuzimu Lisilo na Mwisho (Ufufuo 20:1-15)

(Ufufuo 20:1-15)
“Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache. Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake; naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari. Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala. Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele. Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.
Bwana Mungu wetu atawapatia watakatifu thawabu ya Ufalme wa Kristo kwa miaka elfu moja, atafanya hivyo kuwafidia kwa kazi waliyoifanya kwa ajili ya injili. Ili kufanya hivyo, Mungu ni lazima kwanza amwamuru malaika wake kumkamata Joka na kumfunga katika shimo la kuzimu lisilo na mwisho kwa miaka elfu moja. Kwanza, Mungu ataifanya kazi hii, kwa sababu Joka ni lazima akamatwe na kisha kufungwa katika Lindi-kuu ili kuwawezesha watakatifu kuishi katiak Ufalme wa Milenia wa Kristo. Hivyo, Mungu anampatia malaika wake ufunguo wa shimo la kuzimu lisilo na mwisho na mnyororo mkubwa, na anamwamuru kuianza kazi ya kumshika na kumfunga Joja katika Lindi-kuu.
 
Aya ya 2: Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; 
Yeye aliyemjaribu na kuwafanya Adamu na Hawa kuanguka ni huyu huyu joka. Biblia inamta huyu joja kuwa ni Ibilisi na Shetani. Mungu atamshika huyu Joka na kumfunga katika shimo la kuzimu lisilo na mwisho kwa miaka elfu moja, ili kwamba watakatifu waweze kuishi pamoja na Kristo katika Ufalme wa Milenia kwa amani. 
 
Aya ya 3: akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache. 
Ili kuujenga Ufalme wa Kristo katika dunia hii na kuwafanya watakatifu watawale na Bwana kwa miaka elfu moja, Mungu atamfunga Joka katika Lindi-kuu kwa miaka elfu moja na kumzuia ili asiwadanganye watakatifu. 
Kifungu hiki kinasema kwamba, “na baada ya hayo yapaswa afunguliwe muda mchache.” Baada ya kukamilika kwa miaka elfu moja, Mungu atamfungua yule Joka kwa muda mchache, ili kwamba atakapoanza kuwatesa watakatifu tena, basi Mungu atampeleka kuzimu milele, na hataonekana kamwe. 
 
Aya ya 4: Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. 
Katiak Ufalme wa Kristo, Wakristo waliozaliwa tena upya watapokea mamlaka ya kuhukumu. Wakatifu, baada ya kufanywa kuwa makuhani wa Kristo, watatawala Ufalme wa Milenia pamoja na Bwana. Wale ambao hawakuipokea alama ya Mnyama wala kuiabudu sanamu yak, ndio watakaokuwa wakazi wa ufalme huu, ambao waliuawa na kuifia-dini kwa ajili ya kumshuhudia Yesu na kuilinda imani yao. 
Hao ndio wale waliouawa na kuifia-dini wakati wa dhiki iliyokuwa imeletwa na Mpinga Kristo, naye Mungu atawafufua ili waishi tena na atawafanya watawale Ufalme wa Kristo kwa miaka elfu moja itakayokuja. Kwa kweli, wale walioshiriki katika ufufuo wa kwanza pia watapewa baraka iyo hiyo. 
Kuna ufufuo mara mbili uliotolewa na Bwana: ufufuo wa kwanza na ufufuo wa pili. Watakatifu watakaoishi katika Ufalme wa Milenia ndio wale ambao watashiriki katika ufufuo wa kwanza. Wale wote watakaoshiriki katika ufufuo huu wa kwanza pia watashiriki katika utukufu wa kuishi katika Ufalme wa Milenia, ambao ni Ufalme wa Kristo. Ufufuo wa kwanza utatokea wakati Yesu Kristo atakaporudi ili kuwanyakua watakatifu wote (1 Wathesalonike 4:15-17). Lakini ufufuo wa pili utatokea wakati wa mwisho wa Ufalme wa Milenia kwa kuwa ufufuo huu umeandaliwa kwa ajili ya wenye dhambi ili kuwahukumu kifo cha milele. 
Mamlaka kwa watakatifu ya kutawala miaka elfu moja imetolewa na Bwana Mwenyezi. Hao wamepewa Ufalme wa Kristo kwa sababu waliiamini injili ya Bwana ya maji na Roho na waliyatoa maisha yao ili kuilinda imani hiyo. 
 
Aya ya 5: Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. 
Wale ambao watakuwa hawakupokea ondoleo la dhambi zao toka kwa Bwana, na ambao watakwenda kwake baada ya kuishi hapa duniani kama wenye dhambi hawataweza kushiriki katika ufufuo wa kwanza ambao Bwana awatapatia watakatifu. Kwa hiyo, hata wakati ambapo watakatifu wataishi miaka elfu moja katika Ufalme wa Kristo katika hali ya kusherehekea, wale wengine hawatapokea ufufuo wa kwanza, bali watashiriki katika ufufuo wa pili. Hii ni kwa sababu watakatifu ambao watapokea baraka ya ufufuo wa kwanza watakuwa wamepokea pia mamlaka ya kuishi katika Ufalme wa Kristo, katika hali ya utajiri na utukufu, kwa miaka elfu moja. 
Hata hivyo, Mungu ataruhusu “ufufuo wa pili” kwa wenye dhambi. Kwa nini? Kwa sababu wakati wa ufufuo wa pili, Mungu atawafufua toka katika kifo ili kwamba aweze kuwahukumu kwa ajili ya dhambi zao. Hilo ndilo jaliwa lao, kwamba wafufuliwe toka kwa wafu ili waweze kuhukumiwa kwa ajili ya dhambi zao. Na hii ndio sababu ufufuo wa wenye dhambi unatofautiana sana kwa mfuatano na kwa matokeo. 
Mbali na wale ambao watashiriki katika ufufuo wa kwanza kwa sababu ya imani yao katika injili ya maji na Roho, Bwana hataruhusu mwingine yeyote kuishi tena hadi ile miaka elfu moja itakapokwisha. Hivyo, ufufuo wa wenye haki unakuja miaka elfu moja kabla ya ufufuo wa wenye dhambi. Ufufuo wa wenye haki ni kwa ajili ya kuwafanya wapokee uzima na baraka za milele, lakini ufufuo wa wenye dhambi ni kwa ajili ya wao kupokea adhabu ya milele kwa ajili ya dhambi zao. 
 
Aya ya 6: Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. 
Biblia inatueleza kwamba mauti ya pili haina nguvu juu yao watakaoshiriki katika ufufuo wa kwanza. Kwa hiyo, Biblia inatueleza kwamba washiriki hawa wa ufufuo wa kwanza wamebarikiwa, kwa kuwa watatawala katika Ufalme wa Milenia. 
 
Aya ya 7-8: Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake; naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.
Baada ya kufunguliwa toka katika shimo la kuzimu alipokuwa amefungwa kwa miaka elfu moja, yule Joka atajaribu kusimama kinyume na watakatifu kwa mara nyingine tena, hivyo Mungu atamtupa katika ziwa la moto na kibiriti ili kwamba asiweze kutoka tena. Kutokana na hukumu hii, yule Joka ataweza kuonekana kuzimu tu, na si kwingineko. 
Sasa tunaweza kujiuliza, “Je, hii ina maanisha kwamba wale ambao hawajazaliwa tena upya wataendelea kuwepo katika Ufalme huu wa Milenia?” Jibu ni “Ndio.” Ufunuo 20:8 inaeleza kwamba kuna watu wengi wa dunia katika Ufalme wa Kristo. Hatufahamu kwa hakika ikiwa watakuwa ni watu wapya walioumbwa na Mungu, au waliokuwa wakiishi hapa duniani kabla. Lakini tunachofahamu ni kwamba Mungu anawafahamu watu hao, na kwamba ili watakatifu waweze kutawala, basi inawabadi watu hao wawepo wengi sana kama mchanga wa bahari. 
Ukweli ni kwamba wakati watakatifu wanapoishi katika Ufalme wa Kristo, bado wataweza kuwaona watu wa hapa duniani. Watu wa dunia hii watakuwepo ili kuwatumikia watakatifu, na idadi yao itakuwa ni kubwa kama mchanga wa bahari. Pamoja na kuwa wataungana na Joka ili kusimama kinyume dhidi ya watakatifu kwa mara nyingine, watu hao wataangamizwa na moto utakaoletwa na Mungu, watapokea hukumu ya milele toka katika kiti kikuu cha enzi cha Mungu, kisha watatupwa katika moto wa milele. Baada ya tukio hili, Ufalme wa Milenia utafikia mwisho wake, na kuanzia hapo watakatifu wataenda katika Mbingu na Nchi Mpya ambako wataishi milele. 
 
Aya ya 9: Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala. 
Joka ni Shetani ambaye amesimama wakati wote dhidi ya Mungu na watakatifu wake. Pamoja na kuwa awatawadanganya watu wa dunia wanaoishi katika Ufalme wa Kristo na kisha kuwatisha watakatifu, na kwa kuwa Mungu ni mkuu, basi ataleta moto toka angani na kisha moto huo utawala wote, na kisha atamtupa yule Joka katika moto wa milele ambapo hataweza tena kusimama kinyume na Mungu na watakatifu wake. 
 
Aya ya 10: Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele. 
Kwa kumtupa yule Joka katika ziwa la moto na kibiriti, Mungu atahakikisha anateseka mchana na usiku. Hii ni hukumu ya Mungu ya haki, ni mateso ambayo Joka na wafuasi wake wanastahili. 
 
Aya ya 11: Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.
Baada ya kuwa amewapa thawabu watakatifu wake kwa miaka elfu moja, Mungu ataumba Mbingu na Nchi Mpya na kisha ataishi nao milele. Ili kuthibitisha hili, Mungu atazikamilisha kazi hizi zote na kuzihitimisha. Tendo la mwisho la Mungu ni pale ambapo ataketi katika kiti cheupe cha enzi akiwa kama Hakimu na kisha kuitoa hukumu yake ya mwisho kwa wenye dhambi wote, ambao matendo yao yameandikwa katika Kitabu cha Matendo, hukumu hii haitawahusu wale ambao majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima. 
Hukumu ya Mungu kwa kwenye dhambi itaishia hivyo, na kuanzia hapo milki ya Nchi na Mbingu Mpya itafunguliwa. Bwana wetu ataifanya mbingu na nchi ya kwanza kutoweka, kisha atauumba ulimwengu wa pili wa Mbingu na Nchi Mpya, kisha atawaruhusu watakatifu kuishi ndani ya huu Ufalme wa kimbingu. Mungu ataitoa Nchi na Mbingu Mpya kwa kundi moja la watu na kisha atatoa adhabu ya kuzimu kwa kundi jingine kutokana na yale ambayo yameandikwa katika Kitabu cha Uzima na Kitabu cha Hukumu. 
 
Aya ya 12: Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.
Hukumu ya Kristo kwa wakati huu ndio itakayohitimisha hukumu ya mwisho—yaani, ataitoa hukumu yake ya mwisho kwa kwenye dhambi kwa kuwapatia adhabu ya kuzimu. Watahukumiwa kwa mujibu wa matendo yao, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Hukumu. Hivyo, wenye dhambi watakufa mara mbili. Mauti yao ya pili itakuwa ni ile ya mateso ndani ya kuzimu, ambapo Biblia inaielezea hali hiyo kama ni mauti ya milele. Wenye dhambi hawawezi kuikwepa adhabu ya kuzimu. Hivyo, ni lazima watafute kujifunza Neno la injili ya maji na Roho hivi sasa, yaani wakati huu wakiwa wanaishi hapa duniani, kisha waiamini, na hatimaye wapokee baraka ya majina yao kuandikwa katika Kitabu cha Uzima. 
 
Aya ya 13: Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 
“Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake,” hii ni kwa sababu wenye dhambi wote ni lazima wapokee adhabu ya mwisho kwa ajili ya dhambi zao. Maeneo yanayotajwa katika kifungu hiki—Mauti na Kuzimu, ni mahali ambapo watumishi wa Shetani watakuwa wamefungwa, yaani wale ambao walidanganywa na Shetani na kisha kutawaliwa naye walipokuwa hai, na kisha wakasimama kinyume na Mungu. Aya hii inatueleza kwamba Mungu alikuwa ameisitisha hukumu yake kwa ajili ya dhambi zao kwa kitambo tu, sasa wakati umefika kwa ajili ya hukumu yao ya mwisho. 
Kwa hiyo, mahali popote ambapo watu wanaweza kuishi, wanapaswa kutambua kwamba ni muhimu sana kuzingatia upande waliopo, yaani kwamba ni upande wa Mungu au la. Wale ambao watakuwa walifanya kazi kama watumishi wa Shetani wakati walipokuwa hapa duniani watafufuliwa toka kwa wafu kwa ufufuo wa adhabu ili kupokea adhabu yao ya mwisho, lakini wale ambao waliitumikia injili ya maji na Roho watahusishwa katika ufufuo wa uzima wa milele na baraka. 
Hivyo, watu wanapokuwa hapa duniani wanapaswa kutambua kwamba injili ya maji na Roho, ambayo kwa hiyo Bwana amezitoweshea mbali dhambi za wanadamu, ni ya muhimu sana. Wale ambao watakuwa walifanya kazi kama watumishi wa Shetani walipokuwa hapa duniani watafufuliwa kwa ufufuo wa adhabu, lakini wale ambao watakuwa wamezitumika kazi za haki za Bwana watafufuliwa kwa ufufuo wa uzima wa milele na baraka. Wenye dhambi wote watahukumiwa kwa makosa yao na kisha watapokea adhabu yao ya mwisho huko kuzimu. Na hii ndio sababu kwamba ni muhimu sana, hasa tunapokuwa hapa duniani, kuiamini injili ya maji na Roho, injili ambayo kwa hiyo Bwana ameziondolea mbali dhambi zetu zote. 
 
Aya ya 14: Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.
Hii inatueleza juu ya hukumu ya dhambi za wanadamu mbele ya Mungu, yaani dhambi ambazo wanadamu walizifanya kwa kusimama upande wa Shetani. Adhabu iliyowekwa kwa wale waovu ambao waliwaongoza watu kwenda kwa Shetani ni kutupwa katika ziwa la moto. Hii ni mauti ya pili ambayo Mungu ataileta kwa wenye dhambi, na ni adhabu ya ziwa la moto. Kifo ambacho Biblia inakizungumzia hapa si kifo cha kutoweka, bali ni adhabu ya mateso ya milele katika moto wa kutisha wa kuzimu. 
Wokovu uliozungumzwa katika Maandiko si wa muda mfupi, bali ni wa kudumu na wa milele. Wale wanaoamini katika injili ya maji na Roho wanapokuwa hapa duniani wataingia katika Ufalme wa Mbinguni wa milele na kuishi humo kwa furaha milele. Tofauti kati ya thawabu ambayo waamini wa injili ya maji na Roho wataipata na hukumu kwa wale wasioamini ina tofauti kubwa kama vile mbingu na nchi zilivyo mbali. 
 
Aya ya 15: Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.
Neno “yeyote” katika aya hii linaifanya aya hii kutueleza kwamba, kuandikwa ama kutoandikwa kwa majina ya watu katika Kitabu cha Uzima kunategemea ikiwa watu hao wanaamini au hawaamini katika Neno la injili ya maji na Roho, injili ambayo kwa hiyo dhambi zao zote zimesamehewa, na kuwa nyeupe kama theluji, na bila kujalisha kwamba wanaenda kanisani au la, na bila kujalisha ikiwa makanisa yao ni yale ya Orthodoksi au la. Hivyo, wale ambao majina yao hayajaandikwa katika Kitabu cha Uzima cha Bwana watatupwa wote katika ziwa la moto pasipo shaka. 
Watu wa kidini katika ulimwengu huu wana tabia ya kuweka mkazo zaidi katika desturi zao za kidini kuliko ukombozi toka katika dhambi. Lakini wanaposimama mbele za Mungu, ukweli ni kuwa kama injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu haionekani katika mioyo yao, basi ni hakika kwamba majina yao hayataandikwa katika Kitabu cha Uzima, na kwa sababu hiyo wataishia kutupwa katika ziwa la moto hata kama walikuwa ni Wakristo wazuri. 
Hivyo basi, wakati ukingali unaishi hapa duniani, unapaswa kuisikiliza kwa masikio yako injili ya Bwana ya maji na Roho ambayo imezifanya dhambi zako zote kutoweka, na unapaswa kuiamini injli hiyo kwa moyo wako wote. Hapo ndipo utakapopokea utukufu kwa jina lako kuandikwa katika Kitabu cha Uzima.