Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[21-1] Mji Mtakatifu Unaoshuka Toka Mbinguni (Ufunuo 21:1-27)

(Ufunuo 21:1-27)
“Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli. Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure. Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili. Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo. Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo. Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake. Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa. Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, maana yake, cha malaika. Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi. Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi; wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto. Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu. Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo. Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake. Na milango yake haitafungwa kamwe mchana; kwa maana humo hamna usiku. Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yake. Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. 
Hili Neno lina maanisha kwamba Bwana Mungu wetu ataitoa Mbingu na Nchi Mpya kama zawadi kwa watakatifu walioshiriki katika ufufuo wa kwanza. Kuanzia wakati huo, watakatifu hawataishi katika mbingu na nchi ya kwanza, bali wataishi katika mbingu na nchi ya pili. Baraka hii ni zawadi ya Mungu ambayo ataitoa kwa watakatifu wake. Mungu ataitoa baraka ya jinsi hiyo kwa watakatifu tu ambao wameshiriki katika ufufuo wa kwanza. 
Kwa maneno mengine, wale ambao wataifurahia baraka hii ni watakatifu ambao wamepokea ondoleo la dhambi kwa kuamini katika injili takatifu ya maji na Roho iliyotolewa na Kristo. Bwana wetu ni Bwana harusi wa watakatifu. Kuanzia sasa na kuendelea, kinachowangojea mabibi harusi ni kuvikwa ulinzi, baraka, na mamlaka ya Bwana harusi Mwana-Kondoo, na kisha kuishi kwa utukufu katika Ufalme wake wenye utukufu. 
 
Aya ya 2: Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. 
Mungu ameandaa mji mtakatifu kwa ajili ya watakatifu. Mji huu ni mji wa Yerusalem Mpya, Kasri Takatifu ya Mungu. Kasri hii imeandaliwa kwa ajili ya watakatifu wa Mungu. Na hii imepangwa katika Yesu Kristo kwa ajili ya watakatifu, hata kabla ya Bwana Mungu wetu kuumba ulimwengu. Hivyo, watakatifu hawawezi kufanya lolote zaidi ya kumshukuru Bwana Mungu kwa zawadi yake ya neema na kisha kumpatia Mungu utukufu kwa imani yao. 
 
Aya ya 3: “Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.” 
Kuanzia muda huu, watakatifu wataishi pamoja na Bwana katika Hekalu la Mungu milele. Hii yote ni kwa neema ya Bwana Mungu, ni zawadi ambayo watakatifu wataipokea kwa ajili ya imani yao katika Neno la wokovu la maji na Roho. Hivyo, wale wote waliovikwa katika baraka ya kuingia katika Hekalu la Bwana na kisha kuishi pamoja naye watampatia Bwana Mungu shukrani na utukufu milele. 
 
Aya ya 4: “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”
Sasa, kwa kuwa Mungu anaishi pamoja na watakatifu, basi hakutakuwa na machozi tena na huzuni, wala hakutakuwa na maombolezo juu ya wapendwa wao waliopotea, wala hakutakuwa na kilio wala huzuni. 
Huzuni zote za mbingi na nchi ya kwanza zitatoweka toka katika maisha ya watakatifu, na kitakachowangojea watakatifu ni kuishi maisha yaliyobarikiwa na kutukuzwa pamoja na Bwana Mungu wao katika Mbingu na Nchi Mpya. Bwana Mungu wetu, baada ya kunyika kuwa Mungu wa watakatifu, basi atafanya vitu vyote kuwa vipya, ili kwamba kusiwe na machozi ya huzuni tena, kusiwe na kulia, wala kifo, wala kuomboleza, wala magonjwa, wala kitu chochote ambacho kiliwatesa katika ile dunia ya kwanza. 
 
Aya ya 5: “Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.”
Sasa, Bwana atafanya vitu vyote kuwa vipya, ataiumba mbingu na nchi mpya. Ataufanya uumbaji wake wa mbingu na nchi ya kwanza kutoweka, Yeye ataifanya mbingu na nchi mpya ya pili. Inachotueleza aya hii sio kwamba Mungu ataukarabati ulimwengu wa zamani, bali ataumba ulimwengu mpya. Hivyo, Mungu ataifanya Mbingu na Nchi Mpya na kisha kuishi humo pamoja na watakatifu. Watakatifu walioshiriki katika ufufuo wa kwanza watashiriki pia katika baraka hii. Hiki ni kitu ambacho mwanadamu hawezi hata kukiotea ndoto kwa mawazo yake ya kibinadamu, lakini hiki ndicho ambacho Mungu amekiandaa kwa watakatifu wake. Hivyo, watakatifu na vitu vyote wanampatia Mungu utukufu, shukrani, heshima, na sifa kwa kazi hii kuu. 
 
Aya ya 6: Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.”
Bwana Mungu wetu amepanga na kuyatimiza mambo haya yote, tangu mwanzo hadi mwisho. Mambo yote ambayo Bwana ameyafanya, aliyafanya kwa ajili yake na kwa ajili ya watakatifu. Hivi sasa watakatifu wanaitwa “Wa-kristo” na wamefanywa kuwa watu wa Mungu. Wale waliofanyika kuwa watakatifu wa Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho sasa wanatambua kwamba ingawa wanampatia Mungu shukrani na sifa milele, ukweli ni kwamba hawana namna ya kuweza kumshukuru vya kutosha kutokana na upendo na matendo ya Bwana Mungu. 
“Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.” Bwana wetu ametoa chemichemi ya maji ya uzima kwa watakatifu katika Mbingu na Nchi Mpya. Hii ni zawadi kubwa kulizo zote ambazo Mungu amewapatia watakatifu. Sasa, watakatifu wataishi milele katika Mbingu na Nchi Mpya na kisha kunywa katika chemichemi ya maji ya uzima, ambapo hawataona tena kiu mille. Kwa maneno mengine, sasa watakatifu wamefanyika kuwa watoto wa Mungu ambao watakuwa na uzima wa milele, kama vile Bwana Mungu alivyo, kisha wataishi katika utukufu wake. Ninamshukuru na kumpa Bwana Mungu utukufu kwa mara nyingine kwa kutupatia baraka hii kuu. Halleluya!
 
Aya ya 7: “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.”
“Yeye ashindaye” hii sentensi ina maanisha ni wale walioilinda imani yao iliyotolewa na Bwana. Imani hii inawaruhusu watakatifu wote kuushinda ulimwengu na maadui wa Mungu. Imani yetu katika Bwana Mungu na katika pendo la kweli kwa injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana ndiyo inayotupatia ushindi dhidi ya dhambi zote za ulimwengu, na dhidi ya hukumu ya Mungu, na dhidi ya maadui zetu, na dhidi ya udhaifu wetu, na dhidi ya mateso ya Mpinga Kristo. 
Ninatoa shukrani na kumpatia Bwana Mungu utukufu kwa kutupatia ushindi juu ya hayo yote. Watakatifu wanaomwamini Bwana Mungu wanamshinda Mpinga Kristo kikamilifu kwa imani yao. Bwana Mungu wetu amempatia kila mtakatifu imani hii ambayo kwa hiyo anaweza kushinda dhidi ya mapambano na adui zake. 
Sasa Mungu amewaruhusu watakatifu, ambao wameushinda ulimwengu na Mpinga Kristo kwa imani yao, kuirithi Mbingu na Nchi Mpya. Bwana Mungu wetu amewapatia imani ya ushindi watakatifu wake ili kwamba waweze kuurithi Ufalme wa Mungu. Kwa kuwa Mungu ametupatia imani inayomshinda Mpinga Kristo, basi sasa Mungu ameshakuwa Mungu wetu, na sisi tumeshakuwa watoto wake. Ninamshukuru na kumsifu Bwana Mungu wetu kwa kutupatia imani hii ya ushindi dhidi ya maadui zetu wote. 
 
Aya ya 8: “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.” 
Katika uwepo wake, Bwana Mungu wetu ni Mungu wa kweli na Mungu wa upendo. Sasa, kimsingi, ni akina nani ambao ni waoga mbele ya macho ya Mungu? Hawa ni wale ambao wamezaliwa katika dhambi ya asili na ambao hawajazisafisha dhambi zao zote kwa Neno la injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Hii ni kwa sababu wao wanamwabudu mwovu kuliko kumwabudu Mungu, na ni hakika kwamba wamefanyika kuwa watumishi wa Shetani. Ni kwa sababu wanamwabudu mwovu mbele ya Bwana Mungu, na kwa sababu wanapenda na kuifuata giza kuliko nuru, na kwa sababu hiyo wanaishia kuwa waoga mbele za Bwana Mungu. 
Katika hali yake Mungu ni nuru. Hivyo, huu ni ukweli kwamba watu hawa ambao wao wenyewe ni giza wataendelea kumwogopa Mungu. Kama ambavyo roho ambazo ni mali ya Shetani zinapande giza, basi ndio maana roho hizo zinakuwa na woga mbele za Mungu ambaye Yeye mwenyewe ni nuru. Hii ndio sababu wanapaswa kuyachukua maovu yao na udhaifu wao kwenda kwa Mungu na kisha kupokea ondoleo la dhambi zao toka kwa Mungu. 
Wale “wasioamini,” ambao kimsingi mioyo yao haiamini juu ya upendo wa Bwana Mungu wetu na katika injili yake ya maji na Roho, ni maadui wa Mungu na watenda dhambi wakuu mbele za Mungu. Hivyo nafsi zao zipo kwenye machukizo, na wanasimama kinyume na Mungu, wanapenda na kutenda kila dhambi, wanazifuata ishara za uongo, wanaabudu kila aina ya sanamu, na wanazungumza kila aina ya uongo. Hivyo, kwa kuzingatia hukumu ya haki ya Mungu, watu hao watatupwa katika ziwa liwakalo moto na kibiriti. Hii ni adhabu yao ya kifo cha pili. 
Mungu hajaruhusu Mbingu na Nchi Mpya kwa watu hawa ambao waoga mbele yake, yaani watu wasioiamini injili ya maji na Roho, na ambao baada ya kugeuzwa na kuwa watumishi wa Shetani, wamekuwa machukizo. Badala yake, Bwana wetu amewaruhusu kuingia katika adhabu yake ya milele, hali akiwatupa wote (wakimo wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote) katika ziwa la moto na kibiriti. Hivyo, kuzimu, ambayo Mungu atawapatia itakuwa ndio mauti yao ya pili. 
 
Aya ya 9: “Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo.”
Mmoja wa malaika aliyekuwa ameleta moja ya mapigo ya mabakuli saba alimwambia Yohana, “Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo.” Hapa, sentensi “mke wa Mwana-Kondoo” ina maanisha ni wale waliofanyika kuwa mabibi harusi wa Yesu Kristo kwa kuamini kwa mioyo yao katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Mungu. 
 
Aya ya 10-11: Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri.
“Mji mkubwa, mji mtakatifu Yerusalemu” hii ina maanisha ni Mji Mtakatifu ambapo watakatifu wataishi pamoja na Bwana harusi. Mji huu ambao Yohana aliuona kwa kweli ulikuwa ni mzuri sana na wenye kupendeza sana. Kwa kipimo ulikuwa ni mji wenye fahari, ukiwa umepambwa kwa vito vingi vya thamani ndani na nje, ulikuwa safi na ung’aao. Malaika alimwonyesha Yohana mahali ambapo mabibi harusi wa Yesu Kristo wataishi pamoja na Bwana harusi wao. Huu Mji Mtakatifu wa Yerusalemu ushakao toka mbinguni ni zawadi ya Mungu ambayo atampatia mke wa Mwana-Kondoo. 
Mji wa Yerusalemu unang’aa sana, na mwanga wake ni kama kito cha thamani sana, ni kama kito cha Yakuti, na nuru yake ni angavu kama bilauri. Hivyo, kwa wale wote wanaoishi ndani ya mjiti huo, basi utukufu wa Mungu utakuwa pamoja nao milele na milele. Ufalme wa Mungu ni ule wa nuru, kwa hiyo ni wale tu waliosafishwa giza lao lote, udhaifu nadhambi ndio wanaoweza kuingia katika Mji huu. Kwa hiyo, sisi sote ni lazima tuamini kwamba ili sisi tuweze kuingia katika huu Mji Mtakatifu, tunapaswa kujifunza, kuifahamu, na kuiamini kweli ya Neno la injili ya maji na Roho ambayo Bwana wetu ametupatia. 
 
Aya ya 12: Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. 
Milango ya Mjji huu inalindwa na malaika kumi na mbili, na juu ya milango hiyo kuliandikwa majina ya makabila kumi na mbili ya wana wa Israeli. Mji huu ulikuwa na “ukuta mkubwa na mrefu,” na hii inatueleza kwamba kuingia katika mji hii ni vigumu sana. Kwa maneno mengine, kuokolewa toka katika dhambi zao hakuwezekani kwa kuzitegemea jitihada za kibinadamu au kwa kutegemea fedha na mali za hapa ulimwenguni zitokanazo na uumbaji wa Mungu. 
Ili tuweze kuokolewa toka katika dhambi zetu zote na kisha kuingia katika Mji Mtakatifu wa Mungu, tunapaswa kuwa na imani ile ile waliyokuwa nayo wanafunzi wa Yesu, yaani imani inayoamini katika ukweli wa injili ya maji na Roho. Kwa hiyo, hakuna yeyote asiyekuwa na imani hii katika injili ya maji na Roho anayeweza kuingia katika Mji Mtakatifu. Hii ndio sababu malaika kumi na mbili wamewekwa na Bwana ili kuilinda milango ya mji huu. 
Sentesi inayosema, “na majina yameandikwa,” kwa upande mwingine inatueleza kwamba wamiliki wa Mji huu wamekwisha amuliwa. Na wamiliki wake si wengine zaidi ya Mungu Mwenyewe na watu wake, kwa kuwa Mji huu ni mali ya watu wa Mungu ambao sasa wamefanyika kuwa wana wa Mungu. 
 
Aya ya 13: Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu.
Kwa kuwa milango mitatu iliwekwa upande wa mashariki wa Mji, na kaskazini, kusini, na magharibi kulikuwa na milango mitatu katika kila upande. Hii inatuonyesha kwamba wale tu waliopokea ondoleo la dhambi kwa kuamini katika injili ya maji na Roho kwa mioyo yao yote ndio wanaoweza kuingia katika Mji huu. 
 
Aya ya 14: Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo. 
Miamba mikubwa hutumika kama misingi ya kujengea au kuimarisha jengo. Neno ‘mwamba’ linatumika katika Biblia kumaanisha imani katika Bwana Mungu wetu. Aya hii inatueleza kwamba ili kuweza kuingia aktika Mji Mtakatifu wa Bwana Mungu, basi tunapaswa kuwa na imani ambayo Bwana amewapatia wanadamu, yaani imani inayoamini katika ukombozi wake mkamilifu toka katika dhambi zetu zote. Imani ya watakatifu ni ya thamani sana kuliko hata vito vya thamani ya huu Mji Mtakatifu. Aya hii inatueleza kwamba ukuta wa Mji huu umejengwa juu ya misingi kumi na mbili, na juu ya misingi hiyo yameandikwa majina ya mitume kumi na mbili wa Mwana-Kondoo. Hii inatueleza kwamba Mji wa Mungu unaruhusiwa kwa wale tu ambao wana imani kama ile waliyokuwa nayo mitume kumi na mbili wa Yesu Kristo. 
 
Aya ya 15: Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake. 
Neno hili lina maanisha kwamba ili kuweza kuingia katika Mji uliojengwa na Mungu, basi inampasa mtu kuwa na aina ya imani ambayo imekubaliwa na Mungu, yaani aina ya imani ambayo itampatia mtu huyo ondoleo la dhambi zake. Hapa andiko linasema kwamba malaika aliyezungumza na Yohana alikuwa na mwanzi wa dhahabu ili kuupima ule Mji. Hii ina maanisha kwamba tunapaswa kuamini kwamba Bwana wetu ametupatia baraka hizi zote ndani ya injili ya maji na Roho. Kwa kuwa “imani ni kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo (Waebrania 11:1),” basi ni hakika kwamba Mungu ametupatia Mji Mtakatifu na Mbingu na Nchi Mpya, vitu ambavyo ni vikubwa zaidi kuliko yale tunayoyatarajia. 
 
Aya ya 16: Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa.
Mji ule ulikuwa umejengwa kama mraba, ambapo urefu wake, upanda, na kimo chake ni sawa. Hii inatueleza kwamba sisi sote tunapaswa kuwa na imani ya kuzaliwa tena upya kama watu wa Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Kusema kweli, Bwana wetu hatamruhusu mtu yeyote yule ambaye hana imani katika injili ya maji na Roho kuingia katika Ufalme wa Mungu. 
Kuna watu wengi sana walio na ufahamu mbovu kwamba wataingia katika Mji Mtakatifu ati kwa kuwa wao ni Wakristo, hata kama wana dhambi. Lakini Bwana wetu ametoa wokovu toka katika dhambi na Roho Mtakatifu na amewafanya kuwa watu wake wale wanaoamini katika ukweli kwamba Bwana amewasamehe dhambi zao zote kwa kupitia ubatizo wake hapa duniani na damu yake Msalabani. Hii ni imani ambayo Bwana wetu anataka tuwe nayo. 
 
Aya ya 17: Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, maana yake, cha malaika. 
Maana ya kibiblia ya namba nne ni mateso. Imani ambayo Bwana anaihitaji toka kwetu si kitu ambacho kila mtu anaweza kuwa nacho, lakini imani hii inaweza kuwapo kwa wale wanaolipokea Neno la Mungu, hata kama hawawezi kulielewa vizuri Neno hilo kwa fikra zao binafsi. Kama Mkristo, ukweli ni kwamba haiwezekani kuingia katika Mji Mtakatifu wa Mungu kwa kuuamini Msalaba wa Yesu peke yake, na kuamini kwamba Bwana Mungu ni Mwokozi. Unafahamu ni kitu gani Bwana alimaanisha wakati aliposema katika Yohana 3:5, kwamba, “Amin, amin, nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu”? Je, unafahamu maana ya Bwana wetu kuja hapa duniani, kubatizwa na Yohana, kuzibeba dhambi za ulimwengu kwenda nazo Msalabani, na kuimwaga damu yake juu yake? Ikiwa utalijibu swali hili, basi utaweza kufahamu kuwa nazungumzia kitu gani hapa. 
 
Aya ya 18: Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi. 
Aya hii inatueleza kwamba imani inayoturuhusu kuingia katika Mji Mtakatifu wa Mungu ni safi na haina kitu chochote cha kiulimwengu. 
 
Aya ya 19-20: Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi; wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto.
Misingi ya ukuta wa Mji ilikuwa imepambwa kwa aina nyingi za vito vya thamani. Hili Neno linatueleza kwamba tunaweza kujengwa kwa mitazamo mbalimbali toka katika Neno la Bwana wetu. Na hivi vito vya thamani vinatuonyesha aina ya baraka ambayo Bwana wetu atawapatia watakatifu wake. 
 
Aya ya 21: Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu. 
Katika Biblia Lulu ina maanisha ni ‘Ukweli’ (Mathayo 13:46). Mtafutaji halisi wa Ukweli ataziacha mali zake zote ili aweze kuumiliki Ukweli ambao unampatia uzima wa milele. Aya hii inatueleza kwamba watakatifu ambao wataingia katika Mji Mtakatifu wanapaswa kuwa na uvumilivu mwingi wanapokuwa hapa duniani, hali wakiwa wamesimama imara na katikati ya imani yao katika ukweli. Kwa maneno mengine, wale wanaoamini katika Neno la kweli lililozungumzwa na Bwana Mungu, wanapaswa kuwa na uvumilivu mkuu ili kuilinda imani yao. 
 
Aya ya 22-23: Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.
Kifungu hiki kina maanisha kwamba watakatifu wote watapokelewa katika mikono ya Yesu Kristo, Mfalme wa wafalme. Na kwamba Mji Mtakatifu wa Yerusalemu hauhitaji nuru ya jua wala mwezi, kwa kuwa Yesu Kristo, ambaye ni nuru ya ulimwengu, atauangazia mjia huo. 
 
Aya ya 24: “Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake.”
Kifungu hiki kinatueleza kwamba watu walioishi katika Ufalme wa Milenia sasa wataingia katika Mbingu na Nchi Mpya. Hii sentensi inayosema “Wafalme wa nchi” ina maanisha ni watakatifu waliokuwa wakiishi katika Ufalme wa Milenia. Kuhusu hawa wafalme wa nchi, aya hii inaendelea kusema kwamba, “huleta utukufu waona heshima ndani yake.” Hii inatueleza kwamba watakatifu ambao wamekuwa wakiishi katika miili yao yenye utukufu sasa watatoka katika Ufalme wa Milenia na kwenda katika Ufalme wa Mungu mpya, yaani Mbingu na Nchi Mpya. 
Kwa hiyo, ni wale tu ambao walizaliwa tena upya kwa kuamini katika injili ya maji na Roho walipokuwa hapa duniani na hivyo kuweza kunyakuliwa na kuishi katika katika Ufalme wa Kristo wa miaka elfu moja ndio watakaoweza kuingia katika Mji Mtakatifu wa Yerusalemu. 
 
Aya ya 25: Na milango yake haitafungwa kamwe mchana; kwa maana humo hamna usiku. 
Kwa kuwa Mbingu na Nchi Mpya, mahali ambapo Mji Mtakatifu upo, imeshajawa na mwanga mtakatifu, basi hakutakuwa na usiku ndani yake, wala hakutakuwa na waovu ndani yake. 
 
Aya ya 26: Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yake.
Hii inatueleza kwamba kwa kupitia nguvu za Bwana Mungu za ajabu, wale waliokuwa wakiishi katika Ufalme wa Kristo kwa miaka elfu moja sasa wanastahili kuhamia katika Ufalme wa Mbingu na Nchi Mpya, Ufalme ambao ndani yake upo Mji Mtakatifu. 
 
Aya ya 27: Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.
Wale wote wasioufahamu ukweli wa injili ya maji na Roho miongoni mwa Wakristo na wasio Wakristo katika ulimwengu huu ni wanyonge, wafanya machukizo, na waongo. Hivyo hawataingia katika Mji Mtakatifu. 
Hapa Neno la Mungu linaturuhusu kuthibitisha jinsi injili ya maji na Roho ambayo Bwana ametupatia hapa duniani ilivyo na nguvu. Pamoja na kuwa injili ya maji na Roho imeshahubiriwa kwa watu wengi katika dunia hii, ukweli ni kwamba kulikuwa na wakati ambapo injili hii ilidharauliwa na kudhihakiwa hata na wale wanaojiita Wakristo. Lakini injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana ndiyo ufunguo pekee kwenda Mbinguni. 
Kuna watu wengi ambao bado hawafahamu juu ya ukweli huu, lakini upaswa kufahamu kwamba yeyote anayetambua na kuamini kwamba Bwana amempatia funguo za Mbinguni na ondoleo la dhambi kwa kupitia injili ya maji na Roho ambayo Bwana ameitoa, basi ni hakika kwamba jina lake litaandikwa katika Kitabu cha Uzima. 
Ikiwa unaukubali na kuuamini ukweli wa injili ya maji na Roho, basi ni hakika kwamba utavikwa baraka ya kuingia katika Mji Mtakatifu.