Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[22-2] Uwe na Furaha na Thabiti Katika Tumaini la Utukufu (Ufunuo 22:1-21)

(Ufunuo 22:1-21) 
 
Ufunuo 22:6-21 inatuonyesha juu ya tumaini la Mbinguni. Sura ya 22, ambayo ni aya ya mwisho katika Kitabu cha Ufunuo, inashughulikia juu ya uthibitisho na uaminifu unabii wa Maandiko na juu ya mwaliko wa Mungu katika Yerusalemu Mpya. Sura hii inatueleza kwamba Yerusalemu Mpya ni zawadi ya Mungu iliyotolewa kwa watakatifu ambao wamezaliwa tena upya kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. 
Mungu aliwafanya watakatifu waliozaliwa tena upya kumsifu Mungu katika nyumba ya Mungu. Katika hili ninamshukuru sana Bwana. Maneno hayawezi kuelezea jinsi tunavyoshukuru kwa kitendo cha Mungu kuturuhusu kuwa watakatifu, ambao kwa kuamini katika injili ya maji na Roho tumesamehewa dhambi zetu zote mbele ya Bwana. Ni nani ambaye hapa duniani ataweza kupokea baraka kubwa kuliko hii tuliyoipokea? Hakuna hata mmoja! 
Kifungu kikuu cha leo ni sura ya mwisho ya kitabu cha Ufunuo. Katika Kitabu cha Mwanzo, tunaona Mungu akitengeneza miundo mbinu yote kwa ajili ya mwanadamu, na katika Kitabu cha Ufunuo, tunaomuona Mungu akiitimiza mipango hii yote. Neno la Ufunuo linaweza kuelezewa kuwa ni mchakato wa kuharibu ulimwengu huu ili kuyakamilisha matendo yote kwa ajili ya mwanadamu kwa mujibu wa mpango wake. Kwa kupitia Neno la Ufunuo, tunaweza kuona Ufalme wa Mbinguni, tunaweza kuuona Ufalme wa Mbinguni mapema kama ulivyofunuliwa na Mungu. 
 

Muundo wa Mji wa Mungu na Bustani Yake
 
Sura ya 21 inazungumzia juu ya Mji wa Mungu. Aya ya 17-21 inatueleza hivi: “Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, maana yake, cha malaika. Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi. Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi; wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto. Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu.” 
Hili Neno la Ufunuo linaielezea Yerusalemu Mpya mji ambao Mungu ataupatia kwa watu wake waliozaliwa tena upya. Tunaambiwa kwamba, huu Mji wa Yerusalemu huko Mbinguni umejengwa kwa aina kumia na mbili za vito vya thamani, huku ukiwa na milango kumi na miwili ya lulu. 
Kisha sura ya 22 inazungumzia juu ya hali inayoonekana katika bustani ya Mji wa Yerusalemu. Aya ya kwanza inasema hivi, “Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo.” Katika Mji wa Mungu, mto wenye kungaa kama bilauri unatiririka na kupita katika bustani yake, ni kama vile Mungu alivyoumba mito minne ili itiririke katika Bustani ya Edeni. Mungu anatueleza kwamba hii ni bustani ambayo wenye haki wataifurahia hapo baadaye. 
Kifungu kikuu pia kinatueleza kwamba mti wa uzima upo katika bustani hii; na kwamba unazaa aina kumi na mbili za matunda, na kutoa matunda yake kila mwezi; na kwamba majani ya huo mti ni dawa ya kuwatibu mataifa. Inaonekana kwangu mimi kwamba hali ya Mbinguni ni mahali ambapo sio tu watu wanakula matunda tu, bali hata majani yake yanatumika, hii ni kwa sababu majani haya yana nguvu ya uponyaji. 
 

Baraka Zinazopokelewa na Wenyehaki!
 
Biblia inatueleza kwamba katika Mji wa Mungu, “Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao.” Biblia inatueleza kwamba sisi ambao tumesamehewa dhambi zetu zote tutatawala milele pamoja na Mungu ambaye ametuokoa. 
Wale ambao dhambi zao zimetoweshewa mbali kwa kuamini katika injili ya maji na Roho wakati walipokuwa wakiishi hapa duniani sio tu kwamba watapokea baraka ya kutoweshewa dhambi zao zote, bali watakuwa pia ni wana wa Mungu, watakuwa na malaika wengi wakiwatumikia watakapokuwa wameingia katika Ufalme wa Mungu, kisha watatawala na Bwana milele. Kifungu hiki kinatueleza kwamba wenye haki watapokea toka kwa Mungu baraka za milele kama vile kusimama kando ya mto wa uzima na kula matunda ya uzima, na kwamba kama sehemu ya baraka hii hakutakuwa na magonjwa tena. 
Pia kifungu hiki kinatueleza kwamba pia hawatahitaji mwanga wa dunia hii wala jua, kwa kuwa wataishi milele pamoja na Mungu katika Ufalme wa Mungu wenye utukufu, wataishi na Mungu ambaye yeye mwenyewe ni nuru. Kwa maneno mengine, watoto wa Mungu waliopokea ondoleo la dhambi zao kwa kupitia injili ya maji na Roho, wataishi kama Mungu. Hii ndio baraka ambayo wenye haki wanaipokea. 
Mtume Yohana, mmoja kati ya wanafunzi kumi na mbili wa Yesu ambaye aliandika Kitabu cha Ufunuo, pia ndiye aliyeandika Injili ya Yohana na Nyaraka tatu za Agano Jipya—yaani Waraka wa Kwanza wa Yohana, Waraka wa pili wa Yohana, na Waraka wa tatu wa Yohana. Yohana alipelekwa uhamishoni katika Kisiwa cha Patmo kwa sababu ya kukataa kumtambua Mtawala wa Rumi kuwa ni Mungu. Akiwa katika uhamisho huu, Mungu alimtuma malaika wake kwa Yohana na akamwonyesha yale ambayo yatakuja kutokea hapa duniani, huku akimfunulia na kumwonyesha juu ya maangamizi ya ulimwengu na mahali ambapo hatimaye watakatifu wataingia na kuishi ndani yake. 
Ikiwa tutakielezea Kitabu cha Mwanzo kama msingi wa uumbaji, basi tunaweza pia kukielezea Kitabu cha Ufunuo kama ni ukamilifu wa msingi wa uumbaji. Kwa miaka 4,000, Bwana wetu amewaeleza wanadamu kwamba atazifanya dhambi zao zote kutoweka kwa kupitia Yesu Kristo. Na katika kipindi cha Agano Jipya, basi wakati ulipowadia, Mungu alizimitiza ahadi zake zote, kwamba atamtuma Yesu Mwokozi hapa duniani, na kwamba atamfanya Yesu abatizwe na Yohana, na kwamba atazifanya dhambi zote za ulimwengu kutoweka kwa kupitia damu ya Yesu Msalabani. 
Wakati mwanadamu alipoangukia katika uongo wa Ibilisi na kisha kunaswa katika uharibifu wake kwa sababu ya dhambi, basi Bwana wetu aliahidi kwamba atamkomboa mwanadamu toka katika dhambi zake. Kisha akamtuma Yesu Kristo, akamfanya abatizwe na kuimwaga damu yake, na kwa sababu hiyo amemwokoa mwanadamu kikamilifu toka katika dhambi zake. 
Kwa kupitia Neno la Ufunuo, Mungu ameandika kwa kina juu ya aina ya utukufu unaowangojea wale waliopokea ondoleo la dhambi zao, na juu ya aina ya adhabu inayowangojea wenye dhambi. Kwa maneno mengine, Mungu anatueleza kwamba, kuna watu wengi sana ambao wataishia kuzimu pamoja na kuwa wanadai kumwamini Mungu kwa uaminifu (Mathayo 7:21-23).
Bwana wetu amewaokoa wenye dhambi toka katika dhambi zao, na ametueleza kutolitia muhuri Neno la baraka ambalo ameliandaa kwa ajili ya wenye haki. 
 

Ni Akina Nani Wenye Kudhulumu na Wachafu?
 
Aya ya 11 inasema, “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.” Ni akina nani hawa wenye “kudhulumu”? Wenye kudhulumu si wengine zaidi ya wale wasioamini katika upendo wa injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Kwa kuwa watu wanatenda dhambi wakati wote, basi wanapaswa kuamini katika injili ya maji na Roho ambayo Bwana amewapatia na hivyo kuishi maisha yanayomtukuza Mungu. Kwa kuwa ni Mungu tu ndiye anayepaswa kupokea utukufu toka kwa mwanadamu, na kwa kuwa ni yeye ndiye aliyetuvika katika neema yake ya wokovu, basi sisi sote tunapaswa kuishi maisha ambayo yanamtukuza Mungu. Wale wasiomtii Mungu ni wachafu, hii ni kwa sababu hawaliamini Neno lake wakati wote. 
Katika Mathayo 7:23, Bwana wetu aliwaambia watu wa dini wanaodai kumwamini Yeye kwa midomo tu akisema, “Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu!” Bwana wetu aliwaita watu hao kuwa ni “ninyi mtendao maovu.” Aliwakemea kwa sababu watu hawa wanamwamini Yesu kwa kupitia matendo yao tu, badala ya kuamini katika injili ya maji na Roho kwa mioyo yao yote. Kutenda maovu ni dhambi, pia kutoliamini Neno la Mungu kwa moyo pia ni dhambi. Hivyo basi, watu wanapotenda maovu mbele za Mungu, ina maanisha kwamba hawauamini upendo na wokovu wa maji na Roho ambao Mungu amewapatia. Kutenda maovu si kitu kingine zaidi ya kulibadilisha Neno la Mungu ili kukidhi matakwa ya mtu binafsi na kisha kuamini katika kile mbacho mtu anafikiri kuwa ni sahihi. 
Wale wanaomwamini Yesu kwa kweli ni lazima wakipokee kile ambacho Mungu ameshakianzisha kama kilivyo. Tunamwamini Yesu, lakini huku kumwamini Yesu hakuturuhusu kwa namna yoyote ile kubadili mpango wa Mungu na ukamilifu wake wa wokovu. Ujumbe wa kifungu hiki kikuu ni kwamba Mungu atatoa uzima wa milele kwa wale wote wanaamini katika wokovu wake kama unavyojitegemea, lakini atawapelekea kuzimu wale wote wanaoifanyia mabadiliko Sheria ya Mungu na kisha kuamini kwa namna zile zinazoridhisha nia zao binafsi. 
“Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu.” Hii inatueleza kwamba watu wa jinsi hiyo, hali wakiwa katika ugumu wao, hawauamini wokovu uliopangwa na Mungu. Wao ni wenye kudhulumu, na hii ndio sababu wakati wote wenye dhambi ni wadhulumaji. 
Kifungu hiki kinaendelea kusema, “na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu.” Hii inawangumzia wale ambao, pamoja na kuwa ni wenye dhambi, na mbali na ukweli kwamba Yesu amezifanya dhambi zao zote kutoweka kwa maji na kwa Roho, watu hao hawana dhamira yoyote ile ya kuzisafisha dhambi zao kwa imani. Kwa hiyo, Mungu atawaacha kivyao hawa watu wasio na imani kama walivyo, kisha atawahukumu. Mungu amewafanya wanadamu waweze kuzitambua dhambi katika mioyo yao kwa kuwapatia dhamiri. Lakini bado hawana dhamira ya kuzisafisha dhambi katika mioyo yao, wala kuifahamu injili ya maji na roho. Mungu anatueleza kwamba atawaacha watu hawa wawe kama walivyo. 
Mithali 30:12 inasema kuwa, “Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao.” Wakristo-wakidini wa siku hizi ni watu ambao hawataki kusafishwa dhambi zao. Hata hivyo, Yesu, ambaye yeye mwenyewe ni Mungu, alikuja hapa duniani kuwaokoa wenye dhambi, alizisafishilia mbali dhambi zao zote kwa kuzichukua dhambi za mwanadamu katika mwili wake kwa ubatizo wake mara moja, alihukumiwa mara moja kwa ajili ya dhambi hizo zote kwa kusulubiwa, na kwa sababu hiyo ametuokoa toka katika dhambi sisi tunaoamini. 
Kwa yeyote anayefahamu na kuamini katika Neno la injili ya maji na Roho ambayo kwa hiyo Yesu Kristo amewaokoa wenye dhambi, basi Bwana wetu amemruhusu mtu huyo kusamehewa dhambi zake zote bila kujalisha aina ya dhambi husika. Hata hivyo, kuna watu wengi ambao bado hawajapokea ondoleo la dhambi kwa kupitia imani. Hawa ndio wale ambao wameamua kutojaribu kuzisafishilia mbali dhambi zao. Mungu atawafanya wawe kama walivyo. 
Huku ni kuitimiza haki ya Mungu. Hii ni kuonyesha kuwa Mungu ni Mungu wa haki. Watu hawa watatupwa katika moto wa kibiri na kuungua milele. Ndipo watakapotambua jinsi Mungu wa haki alivyo. Pamoja na kuwa wanamkiri Yesu kuwa ni Mwokozi, basi ukweli ni kuwa hawazidanganyi dhamiri zao bali pia wanazichafua dhamiri za wengine. Kwa kuwa wameikataa injili ya maji na Roho, basi Mungu atawalipa sawasawa na walivyofanya. Siku itakapowadia, Mungu ataileta ghadhabu yake kwa wale wote wanaostahili. 
 

Mpe Kila Mtu Sawa na Matendo Yake
 
Kuna aina mbili za watu hapa duniani: wale waliokutana na Bwana, na wale ambao hawajakutana naye. Bwana wetu atamlipa kila mtu kulingana na matendo yake. 
Hakuna mtu anayeweza kuhesabiwa haki kwa kutegemea haki yake binafsi, lakini kuhesabiwa haki kunatoka kwa Yesu. Yesu alizichukua dhambi zetu zote za mwanadamu katika mwili wake kwa ubatizo wake mara moja na kwa wote, alizichukua dhambi za ulimwengu kwenda Msalabani, na hali akiwa Msalabani alikabiliana na hukumu ya dhambi ambayo mwanadamu alipaswa kukabiliana nayo. Mwanadamu anaweza kuwa mwenye haki kwa kuuamini ukweli huu. Wale wanaouamini ukweli huu ndio wale waliokutana na Bwana. 
Mungu anawataka wale wasio na dhambi, yaani wale wanaofahamu na kuamini katika ukweli huu, kuihubiri injili hapa duniani na kulitunza Neno lake takatifu kadri wanavyoendelea kuishi. Mungu anasema, “na mtakatifu na azidi kutakaswa.” Ni lazima tuishike amri hii katika mioyo yetu, tuilinde imani yetu takatifu, na kisha kuihubiri injili kamilifu. Kwa nini? Kwa sababu kuna watu wengi sana hapa ulimwenguni ambao hawaifahamu injili hii ya kweli, na kama matokeo imani yao inakuwa si sahihi. 
Wapo wengine hapa duniani ambao pasipo masharti yoyote wanaunga mkono fundisho la kiimani la utakaso unaozidi. Pamoja na kuwa Bwana amekwisha kuzifanya dhambi za mwanadamu kutoweka, watu wanaoamini katika fundisho hilo bado wanaendelea kuomba sala za toba kila siku, hata hivi sasa. Wanajaribu kuzisafishilia mbali dhambi zao kwa kutoa sala za toba kila siku, wanafanya hivyo ili kupata utakaso unaozidi ili kwamba hatimaye waweze kuwa wenye haki ambao hawatendi dhambi yoyote, na hivyo kuwa mfano wa Yesu. Lakini Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ni Mfalme, Nabii na Kuhani Mkuu. 
Watumishi wa kweli wa Mungu si tu wanafanya kazi ya kuhakikisha kwamba kila mtu anasamehewa dhambi zake, bali wanamwongoza kila mtu kuelekea katika ukweli kama watenda kazi wa Mungu. Watumishi wa Mungu, ni wale ambao, kwa kupitia Neno lililoandikwa wana ufahamu sahihi wa mambo ambayo yatakuja kutokea. 
Aya ya 12-13 inasema, “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.” Kwa hakika Bwana wetu ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Wakwanza na Wamwisho. Tunapaswa kuamini kila kitu ambacho Bwana ametuambia tena kwa hofu. 
Bwana wetu atawazawadia watakatifu kwa baraka ambazo ni kubwa sana kuliko matendo yao, hii ni kwa sababu Bwana ni mwenye utukufu na mwenye rehema. Bwana ni mwenye rehema na mwenye upole ambaye ametuokoa toka katika dhambi zetu zote, na kama vile Neno la Ufunuo linavyosema kuwa, Mungu ni wa mamlaka na haki ambaye ataitimiza kazi yake ya wokovu. Na ukamilifu huu wa wokovu, ambao utakuja hivi punde, unawaruhusu watakatifu kuingia kwa utukufu katika Mji wa Yerusalemu Mpya, ambao ni zawadi ya kutosha ya Bwana wetu kwa ajili ya kazi zao. 
 

Wamebarikiwa Wale Wanaozifanya Amri Zake
 
Tukiendelea na aya ya 14, kifungu kikuu kinatueleza kwamba, “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.” Kwa kuzingatia aya hii, kuna watu wengi sana wanaodai kwamba wokovu unakuja kwa matendo—kwa maneno mengine, ni kwa kufuata amri zake. 
Lakini ni kweli kwamba, “kuzifanya amri zake” maana yake ni kuamini na kulishika Neno la Mungu lililoandikwa kwa imani. Mtume Yohana aliandika, “Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri” (1 Yohana 3:23). Hivyo, tunapoamini katika injili ya kweli ya maji na Roho, na kisha kujitoa katika kuihubiri injili ili kuziokoa nafsi zote zilizopotea katika ulimwengu wote, basi hapo tunakuwa tukizifanya amri zake mbele ya uwepo wa Mungu. 
Ukweli ni kwamba dhambi zote tunazozitenda katika maisha yetu yote zimekwisha toweshewa mbali kwa kupitia ubatizo wa Yesu alioupokea toka kwa Yohana Mbatizaji. Baada ya ubatizo huu, inafuatia damu ya Bwana Msalabani, ufufuo wake, na kupaa kwake mbinguni, vitua ambavyo vimetufanya kuzaliwa tena upya na kuishi maisha mapya katika ukweli huu. 
Wakati wowote tunapoangukia katika dhambi baada ya kuwa tumezaliwa tena upya, basi hapo tunapaswa kulirudia Neno la kweli ambalo limetusafisha dhambi zetu zote; hali tukitambua kwamba mizizi yetu ipo hivyo na kwamba hatuwezi kukwepa kufanya dhambi; na kisha kurudi tena katika imani ya Mto Yordani ambapo Bwana wetu aliuchukua udhaifu wetu wote, mapungufu yote, na dhambi, kisha tukabatizwa pamoja na ubatizo wa Yesu na kisha tukazikwa pamoja na Kristo aliyekufa Msalabani. Tunapofanya hivyo, basi hatimaye tunaweza kuwekwa huru toka katika dhambi tulizozifanya baada ya kuzaliwa tena upya, na kisha kuoshwa dhambi zetu na kuwa safi. Pia tunapaswa kuishikilia haki ya Mungu kwa kuukiri wokovu wetu wa milele wa upatanisho na kwa kumshukuru Mungu kwa wokovu wake unaodumu na mkamilifu. 
Yesu amekwishazioshelea mbali dhambi zote za ulimwengu huu. Tatizo lipo katika dhamiri zetu. Ingawa Bwana wetu amekwisha zishughulikia dhambi zote za ulimwengu kwa ubatizo wake, na kwa kuwa sisi wanadamu hatufahamu kwamba Bwana amekwisha zisafishilia mbali dhambi zetu zote kwa ubatizo wake na kwa kusulubiwa kwake, basi ndio maana dhamiri zetu zinaendelea kupata shida kama vile ni watenda dhambi. Hivyo ndio maana wakati mwingine tunajaribiwa kufikiri kwamba bado tuna dhambi ndani yetu, wakati tunachopaswa kukifanya ni kuamini kwamba dhambi zetu zimekwisha oshelewa mbali kwa kupitia injili ya maji na Roho iliyotolewa na Yesu Kristo. 
Ikiwa mioyo yetu imeumizwa kwa dhambi zetu, basi tutayatibu vipi majeraha ya dhambi hizi? 
Ukweli ni kwamba majeraha haya yote, yanaweza kuponywa kwa kuamini katika injili ya maji na Roho—yaani kwa kuamini kwamba Bwana wetu alizichukua dhambi zote za ulimwengu katika mwili wake kwa kubatizwa na Yohana katika Mto Yordani, na kwamba alizifanya dhambi zote kutoweka kwa kuzichukua dhambi hizo kwenda Msalaba wa Kalvari na kuimwaga damu yake Msalabani. Kwa maneno mengine, dhambi za matendo yetu yote tunayoyafanya baada ya kupokea ondoleo la dhambi zinaweza pia kuoshwa tunapoikiri tena imani yetu katika injili kwamba Yesu Kristo amekwisha zisafishilia mbali dhambi zetu zote, zikiwemo dhambi hizo za matendo yetu. 
Dhambi za ulimwengu huu zilisafishiliwa mbali mara moja wakati Yesu Kristo alipoupokea ubatizo wake na kusulubiwa. Kwa hiyo, hakuna dhambi ya ulimwengu au dhambi binafsi ambayo inahitaji kuoshelewa mbali mara mbili au tatu, kana kwamba zinapaswa kusafishwa katika hali ya mwendelezo. Ikiwa mtu anafundisha kwamba ondoleo la dhambi linapatikana kidogo kidogo, basi injili ambayo mtu huyo anaihubiri ni injili ya uongo. 
Mungu amezifanya dhambi za ulimwengu kutoweka mara moja. Waebrania 9:27 inatueleza kwamba, “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu” Kama tunavyokufa mara moja kwa sababu ya dhambi, basi ni mapenzi ya Mungu kwamba tuweze kupokea ondoleo la dhambi mara moja. Kwa kuja hapa duniani, Yesu alizichukua dhambi zetu zote katika mwili wake mara moja, akafa mara moja, kisha akahukumiwa kwa niaba yaetu mara moja pia. Hakufanya mambo haya yote mara kadhaa. 
Tunapopokea ondoleo la dhambi kwa kumwamini Yesu Kristo kwa mioyo yetu yote, basi ni sahihi pia kuamini mara moja na kisha kupokea ondoleo la milele la dhambi zetu zote. Kwa kuwa dhambi tunazozifanya kuanzia hapo na kuendelea zinaidhuru mioyo yetu katika nyakati mbalimbali, basi tunachopaswa kukifanya ni kwenda mbele ya Neno hili la wokovu, kwamba Bwana wetu amezioshelea mbali dhambi zetu zote mara moja, na hivyo tutaweza kuiponya mioyo yetu iliyodhoofu kwa imani: “Bwana, nina mapungufu mengi sana. Nimefanya dhambi tena. Sikuweza kuishi maisha makamilifu kwa mujibu wa mapenzi yako. Lakini wakati ulipobatizwa na Yohana katika Mto Yordani na kisha kuimwaga damu yake Msalabani, je hukuzishughulikia dhambi zangu hizi zote? Haleluya! Ninakusifu Ewe Bwana!”
Kwa imani hiyo, tunaweza kulithibitisha na kulikiri ondoleo la dhambi zetu na kisha kumshukuru Bwana wakati wote. Sura hii ya mwisho ya Ufunuo inatueleza kwamba kwa kwenda mbele za Yesu Kristo, ambaye ni mti wa uzima, na kwa kuamini kwamba Bwana amekwishazioshelea mbali dhambi zote za ulimwengu, basi wale waliopokea ondoleo la dhambi wamepata haki ya kuingia katika Ufalme wa Mungu, na katika Mji Mtakatifu kwa kupitia imani yao. 
Yeyote anayetaka kuingia katika mji wa Mungu ni lazima aamini kwamba Yesu Kristo amezipatanisha dhambi za mwanadamu milele kwa kuupokea ubatizo wake mara moja na kwa kuimwaga damu yake. Pamoja na kwamba sisi sote tuna matendo yenye mapungufu, kwa kuamini katika ubatizo na damu ya Yesu Kristo Mwokozi wetu, basi imani yetu inaweza kuthibitishwa na Mungu kuwa ni kweli, na sisi sote tunaweza kwenda mbele ya mti wa uzima. 
Ni kwa kuamini tu katika ubatizo wa Kristo na damu yake ndipo tunapoweza kupata haki ya kunywa maji ya uzima yanayotiririka toka katika Yerusalemu Mpya na pia kuyala matunda ya mti wa uzima. Kwa kuwa sifa ya kuingia katika Mbingu na Nchi Mpya, ambayo haiwezi kutwaliwa na yeyote yule, inatoka katika injili ya maji na Roho, basi sisi tunapaswa kuilinda imani yetu na kisha kisha kuihubiri kwa watu wengine. Vivyo hivyo, sentensi inayosemae “(ku) zitenda amri zake” ina maanisha ni kwa sisi kuushinda ulimwengu kwa imani—yaani ni kuamini na kuishika injili ya maji na Roho, na kisha kujitoa katika kuihubiri injili ya kweli ulimwenguni mwote. 
Katika Mathayo 22, Yesu anatueleza juu ya “mfano wa sherehe ya harusi.” Hitimiso la mfano huu ni kwamba wale wasio na mavazi ya harusi watatupwa katika giza la nje (Mathayo 22:11-13). Tunawezaje kuyavaa mavazi yetu ya harusi ili kushiriki katika karamu ya harusi ya Mwana-kondoo, na mavazi hayo ya harusi ni yapi? Mavazi ya harusi ambayo yanatuwezesha kuingia katika karamu ya harusi ya Mwana-kondoo ni haki ya Mungu tunayopewa kupitia injili ya maji na Roho. Je, unaamini katika injili ya maji na Roho? Ikiwa ni hivyo, basi ni wazi kuwa umevikwa katika haki ya Mungu ili uweze kuingia Mbinguni ukiwa bibi harusi wa Mwana usiye na dhambi. 
Sisi tuliozaliwa tena upya, pia tunatenda dhambi kila siku. Hata hivyo, ni watakatifu tu waliosamehewa dhambi zao mbele ya Mungu ndio wanaostahilishwa kuzioshelea mbali dhambi zao za kila siku katika mavazi yao ya haki kwa imani. Kwa kuwa wale wanaotenda dhambi hawajasamehewa basi hawastahilishwi kuzioshelea mbali dhambi zao, hii ni kwa sababu hawataweza kujiosha kutokana na dhambi zao kwa kutegemea sala za toba za kila siku. Ule kweli kwamba tumeokolewa toka katika dhambi za ulimwengu kwa kumwamini Bwana kumewezekana kwa kufahamu na kuamini kwamba Bwana amezioshelea mbali dhambi zetu zote za ulimwengu kwa kuja hapa ulimwenguni, kwa kubatizwa, na kwa kuimwaga damu yake. 
Kwa maneno mengine, tunaweza kuthibitisha kwamba dhambi zetu za kila siku zimekwisha oshelewa mbali katika injili yake ya kweli. Wale waliopokea ondoleo la dhambi zao toka kwa Bwana kwa kupitia Neno la maji na damu wanaweza pia kuwa na uhakika wa wokovu wao toka katika dhambi ambazo wanazifanya kadri wanavyoendelea kuishi katika maisha yao. 
Kwa kuwa Bwana amezifanya dhambi zetu zote kutoweka mara moja, basi ndio maana tunaweza kuzioshelea mbali dhambi tunazozifanya kwa matendo yetu kwa kuuamini wokovu huu wa upatanisho wa milele. Kwa maneno mengine, kama isingelikuwa hivi, ikiwa Bwana wetu asingelikuwa amezioshelea mbali dhambi zetu zote mara moja, basi tungeliwezaje kuwa tusio na dhambi? 
Tutawezaje kuingia katika Mji Mtakatifu wa Mbinguni? Tutawezaje kwenda mbele za Yesu Kristo, ambaye ni mti wa uzima? Tunaweza kuingia katika Ufalme wa Mbinguni tukiwa watu safi na wasio na mawaa kwa kumwamini Bwana wetu ambaye amezifanya dhambi zetu kutoweka, na wakati tunapofanya dhambi katika maisha yetu, basi tunaweza kwenda mbele za Bwana na kuthibitisha kwamba Bwana amezifanya dhambi hizi pia kutoweka, na kwa kufanya hivyo tunaweza kuwekwa huru toka katika dhambi hizo. Hii ndio sababu ninawaeleza kwamba wale waliozaliwa tena upya wana fursa ya kusamehewa dhambi zao za kila siku kwa imani.
Mfalme Daudi, pamoja na kuwa alikuwa ni mtumishi wa Mungu bado alifanya dhambi kuu mbele za Mungu. Alifanya uzinzi na mke wa mtu aliyekuwa ameolewa, kisha akamuua mume wake aliyekuwa mtumishi wake mwaminifu. Hata hivyo, alimsifu Mungu kwa msamaha na rehema zake kama hivi: 
“Heri aliyesamehewa dhambi zake, 
Na kusitiriwa makosa yake. 
Heri BWANA asiyemhesabia upotovu, 
Ambaye rohoni mwake hamna hila (Zaburi 32:1-2).” 
Ni nani aliyebarikiwa zaidi katika ulimwengu huu mbele za Mungu? Walibarikiwa si wengine bali ni sisi tuliozaliwa tena upya; ambao tumeokolewa; na ambao kila inapotendwa dhambi katika maisha yetu, tunauangalia ukweli kwamba Bwana amezifanya dhambi zetu zote kutoweka, kisha tunaenda katika chemichemi ya uzima kila siku, kisha tunaiosha mioyo yetu iliyochafuka kila siku. Huku ni kufikiria kwa kina juu ya ukombozi wetu na kuuthibitisha neema kuu ya Bwana wetu ya wokovu. 
Ni wenye haki tu ndio waliopokea ondoleo la dhambi, na kuyafanya mapungufu yao kuwa ukamilifu. Matendo yao ni makamilifu, na pia hata mioyo yao ni mikamilifu. Baada ya kufanyika wenye haki pasipo mawaa, basi tunaweza kuingia katika Ufalme ambao Mungu ametuandalia, ambao ni Ufalme wa Mbinguni. Ikiwa tutakipokea kile ambacho Yesu Kristo, ambaye ni lango la wokovu na mti wa uzima amekifanya kwa ajili yetu, basi nguvu na mamlaka yake vitafunuliwa, na kwa sababu hiyo sisi sote tutapokea ondoleo la dhambi na kisha kuingia Mbinguni. 
 

Wale Wanaokwenda Mbele ya Mti wa Uzima
 
Sababu inayotufanya sisi tuliopokea ondoleo la dhambi kwenda mbele za Bwana wakati wote ni kuthibitisha kwamba Bwana wetu amezifanya dhambi zetu zote kutoweka, kuitafakari neema ya wokovu kwa mara nyingine, kuikumbuka neema hiyo, na kisha kumsifu Mungu kwa sababu ya neema hiyo, ili kwamba sisi sote tuweze kuingia katika Ufalme wa Mungu. Hii ndio sababu tunaihubiri injili. 
Kuna idadi kubwa ya Wakristo ambao wameshindwa kuonana na watumishi wa Mungu ili kuwaongoza na kuwafundisha Biblia kiusahihi, na kwa sababu hiyo wamebanwa katika kutolielewa Neno na hivyo kuwa na imani isiyo sahihi. Hata sasa, kuna watu ambao wametingwa sana kwa sababu ya matendo yao, huku wakitoa sala za toba kila asubuhi na usiku wote. Kwa nini wanafanya mambo hayo? Kwa sababu wanaamini kwamba kwa kufanya hivyo, basi dhambi zao zitasamehewa. Wanaamini hivyo kwa kuwa wamefundishwa mafundisho ya kidini yenye makosa. Lakini matendo hayo ni mateso yasiyo ya haki mbele za Mungu. Watu wa jinsi hiyo ni wa kuhurumiwa sana maana hawaifahamu haki ya Mungu wala upendo wake usio na masharti. 
Biblia si kitu ambacho kinaweza kuchukuliwa kwa wepesi, yaani kana kwamba inaweza kufafanuliwa kadri mtu anavyotaka. Lakini kwa kuwa watu wameifafanua, wameifundisha, na wameiamini kwa kuzingatia mawazo yao binafsi, basi ndio maana matokeo yamekuwa kama yalivyoelezwa hapo juu—yaani, wamebakia kutoifahamu haki na upendo wa Mungu. Kila kifungu katika Biblia kina maana kamili, na vifungu hivi vinaweza kufafanuliwa kiusahihi na manabii wa Mungu tu waliopokea ondoleo la dhambi. 
Kitendo cha kwenda mbele ya mti wa uzima ni kumwamini Bwana hapa duniani, na kukumbuka kila siku kwamba Bwana wetu amezifanya dhambi zetu kutoweka, na kisha kumsifu Bwana, na kuihubiri injili hii. Sisi tuliozaliwa tena upya, tunapaswa kukumbuka pia kwamba Bwana alizichukua dhambi zetu katika mwili wake, na tunapaswa kuuthibitisha ukweli huu kila siku, na kisha kumwabudu Yeye kwa furaha na shukrani. 
Hata hivyo, ni sahihi kusema kwamba Wakristo ulimwenguni kote wamekifafanua vibaya kifungu hiki na kisha kuamini kimakosa kwamba wanaweza kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kuzifanya dhambi zao kuoshelewa mbali kwa kutegemea sala za toba za kila siku. Lakini kifungu hiki hakimaanishi hivyo. 
Baada ya kupokea ondoleo la dhambi zetu, basi mioyo yetu inaweza kuwa na amani kwa kuthibitisha kwamba Bwana wetu amezifanya dhambi tunazozifanya kila siku kwa matendo yetu kutoweka. Kwa kulithibitisha ondoleo la dhambi zetu ZOTE, basi hapo tunakuwa hatujafungwa na dhambi. Hii ndio njia ya kwenda mbele ya mti wa uzima huko Mbinguni. 
Maandiko ni tofauti kabisa na mawazo ya mwanadamu. Kwa hiyo, ili kuufahamu ukweli, basi tunapaswa kwanza kujifunza na kuusikia ukweli toka kwa watumishi wa Mungu waliozaliwa tena upya. 
 

Wale Walio Nje ya Mji
 
Aya ya 15 inasema, “Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.” Neno hili linawahusu wale wote wa nyakati za mwisho ambao hawajazaliwa tena upya. Ni jambo la kushangaza kuona Mungu akiwaelezea watu hao kwa usahihi kiasi hicho. 
Tabia mojawapo ya mbwa ni kucheua na kutapika—yaani ni kucheua kile ambacho wamekila na kisha kukila tena, na kisha kutapika kile ambacho wamekila na kisha kukila tena. Bwana wetu anasema hapa kwamba hawa “mbwa” hawataweza kuingia katika Mji. 
Je, hili neno kuhusu mbwa linawahusu akina nani? Kuna watu ambao huwa wanaomba kwa sauti wakisema “Bwana, mimi ni mwenye dhambi; tafadhali naomba uzioshelee mbali dhambi zangu,” kisha wanamsifu Mungu wakiimba, “Mimi nimesamehewa, wewe umesamehewa, sisi tumesamehewa!” Lakini muda mfupi baadaye, watu hawa wanaanza tena kuomba, “Bwana, mimi ni mwenye dhambi; ukinisamehe walau mara moja zaidi, basi sintafanya dhambi tena.” Kisha wanaimba tena sifa wakisema, “Mimi nimesamehewa kwa damu ya Kalvari!” 
Watu hawa huenda mbele na nyumba kama hivi mara kadhaa kiasi kwamba mtu hawezi kufahamu ikiwa watu hao wamesamehewa au la. Hawa si wengine bali ndio hao “mbwa” ambao Biblia inawazungumzia. Mbwa hubwekwa kila siku. Mbwa hubweka asubuhi, hubweka mchana, na hubweka jioni. Watu hawa hawabweki kama wanavyobweka hao mbwa, bali wanapiga kelele huku wakisema kuwa wao ni wenye dhambi, pamoja na kuwa wamesamehewa dhambi zao. Wanafanyika kuwa wenye haki kwa dakika moja, kisha wanageuka na kuwa wenye dhambi dakika moja baadaye. 
Kwa namna hii, wanakuwa kama vile mbwa ambao hutapika kilicho ndani yao kisha kukila tena, na kisha kukitapika na kukila tena zaidi ya mara moja. Kwa kifupi, Biblia inawataja Wakristo ambao bado wana dhambi katika mioyo yao kuwa ni “mbwa.” Hawa mbwa hawawezi kuingia Mbinguni, bali wanaweza kuwa nje ya Mji. 
Ni akina nani ambao ni “wachawi?” Hawa ndio wale ambao hali wakitumia fursa za hisia za waenda makanisani, huwaibia fedha zao kwa maneno mazuri, na ndio wale wanaowadanganya watu kwa ishara na miujiza ya uongo huku wakidai kuwaponya magonjwa yao. Kwa kuwa wanalitumia jina la Mungu kwa utupu, basi ni hakika kwamba hawawezi kuingia katika Mji Mtakatifu. 
Pia, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na wale wanaoupenda na kuufanya uongo hawawezi kuingia katika huo Mji. Nyakati za mwisho zitakapowadia, mbwa na wachawi watawadanganya watu, na Mpinga Kristo atatokea. Mpinga Kristo anayewadanganya watu wengi kwa ishara na miujiza ya uongo, ataziiba roho zao, atasimama kinyume na Mungu, na atatafuta kujiinua juu kama vile Mungu ili aabudiwe, hivyo wafuasi wake wote hawataweza kuingia katika Mji huo. 
Kwa hiyo, ikiwa tutaangukia katika uongo wa wale wanaodai kuwa bado wana dhambi, au ikiwa tutaangukia katika uongo wa ishara na miujiza ambavyo vinaamsha hisia zetu, basi sisi sote tutaishia kuwa nje ya Mji pamoja na Mpinga Kristo na Shetani, huku tukiomboleza na kusaga meno, kama Neno linavyotuonya. 
Aya ya 16-17 inasema, “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi. Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.”
Je, umepokea ondoleo la dhambi bure? Bwana wetu ametupatia injili ya maji na Roho inayotuwezesha kuyanywa maji ya uzima kupitia Roho Mtakatifu na Kanisa la Mungu. Yeyote anayeona njaa kwa ajili ya haki ya Mungu, yeyote anayeona kiu ya Neno la kweli, na yeyote anayetaka kwa nguvu kupokea ondoleo la dhambi—basi Mungu ameahidi, kwa watu kama hao, kuwafunika kwa rehema yake na anautoa mwaliko huo kupitia Neno lake, ambalo ni maji ya uzima ya wokovu wake. Kupokea ondoleo la dhambi ni njia pekee ya kuutikia mwaliko huu katika Mbingu na Nchi Mpya mahali ambapo maji ya uzima yanatiririka. 
 

Amina, Na Uje Bwana Yesu! 
 
Aya ya 19 inasema, “Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.” Hatuwezi kuamini kwa namna yoyote ile tunayoitaka kwa kutegemea mawazo yetu binafsi mbele za Mungu. Kama imeandikwa katika Neno la Mungu, basi tunachoweza kusema ni “ndiyo,” kwa kuwa kama mtu yeyote atasema “hapana” kwa Neno, basi Bwana wetu atamtupilia mbali akisema, “Wewe si mtoto wangu.” Hii ndio sababu inatupasa kumwamini Bwana kwa mujibu wa Neno. Hatuwezi kuongeza wala kupunguka chochote katika Neno la Mungu, bali tunapaswa kuliamini hilo Neno kama lilivyoandikwa. 
Kuwashikilia watumishi wa Mungu na kuamini kile ambacho Roho Mtakatifu anaongea kupitia Kanisa la Mungu ndio vitu muhimu vya imani ya kweli. Hata hivyo, watu wengi, kwa kuwa wameiondoa injili ya maji na Roho toka katika imani yao, wamebakia kuwa na dhambi katika mioyo yao. Hata wakati Neno linapowaeleza mara kwa mara kwamba wasio na dhambi ndio wanaoweza kuingia katika ule Mji Mtakatifu wa Mungu, inashangaza kuona kwamba watu hao bado wameuacha ubatizo wa Yesu katika imani yao, na badala yake wanatilia mkazo matendo yao kama vile kusali sala za toba na kutoa sadaka za mali na vitu. 
Wale wanaomwamini Yesu kuwa ni Mwokozi wako wanapaswa kuikiri imani yao kwamba dhambi zote za mwanadamu zilipitishwa kwenda kwa Yesu kwa kupitia ubatizo ambao Yesu aliupokea toka kwa Yohana Mbatizaji katika Mto Yordani. Ikiwa utauondoa ubatizo wa Yesu basi ni dhahiri kuwa unaiondoa imani yako. Kwa maneno mengine, ikiwa hauiamini injili ya maji na Roho, basi kwako wewe damu ya Msalaba haina maana na hata ufufuo wa Kristo ni bure tu. Ni wale tu wanaoamini kwamba Mungu amezifanya dhambi zao zote kutoweka ndio wanaoona maana juu ya ufufuo wa Yesu, na ndio hao wanaoweza kushangilia kwa sauti ujio wa Bwana Yesu, yaani kama Mtume Yohana alivyofanya katika aya ya 20. 
Aya ya 20 inasema, “Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu!” Ni wenye haki tu ndio wanaoweza kusema hivi. Hivi punde Bwana wetu atarudi tena hapa duniani, na hii ni kwa mujibu wa maombi ya wenye haki. Ni wenye haki tu, ambao wamepokea ondoleo la dhambi kamilifu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho, ndio watakaofurahia na kusubiri kwa hamu ujio wa Bwana. Hii ni kwa sababu wale wanaojiandaa kumpokea Bwana ni wale tu ambao wamevikwa vazi la injili ya maji na Roho—yaani, wale wasio na dhambi. 
Bwana wetu anaingojea siku ambayo ataitikia wito wa watakatifu wanaongoja, yaani siku ambayo atakuja hapa duniani. Atatuzawadia Ufalme wa Milenia, na atatuvika sisi wenye haki, kwa baraka yake kuu ya kuingia katika Mbingu na Nchi Mpya mahali ambapo maji ya uzima yanatiririka. Huku kumsubiri Bwana wetu hakutakawia sana. Kwa hiyo, kile tunachoweza kukisema ni “Amina, na uje, Bwana Yesu!” Hivyo, kwa imani na shukrani tunakusubiria kurudi kwa Bwana. 
Hatimaye, aya ya 21 inasema, “Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote.” Mtume Yohana alimalizia Kitabu cha Ufunuo kwa sala yake ya mwisho ya baraka kwa kila mtu. Aliitoa sala hii ya baraka mwishoni, huku moyo wake ukitarajia kila mtu kumwamini Yesu, kuokolewa, na hatimaye kuingia katika mji wa Mungu. 
Wapendwa wenzangu watakatifu, kule kusema kwamba tumeokolewa na Mungu maana yake ni kwamba Mungu ametupenda, ametukomboa toka katika dhambi zetu zote, na ametufanya kuwa watu wake. Kwa kweli ni jambo la kushangaza na kushukuru kwamba Mungu ametufanya sisi kuwa wenye haki ili tuweze kuingia katika Ufalme wake. 
Hiki ndicho kiini ambacho Biblia inazungumza nasi. Mungu ameturuhusu wewe na mimi kuzaliwa tena upya kwa kuisikia injili hii ya kweli, na ametuokomboa toka katika dhambi zetu zote na hukumu ili kutufanya sisi tuishi milele katika Ufalme wake. Ninamsifu na kumshukuru Bwana kwa wokovu wake. 
Ni bahati nzuri kwamba tumepokea ondoleo la dhambi zetu. Sisi ni watu ambao tumebarikiwa sana na Mungu. Na sisi ni manabii wake. Kwa hiyo, ni lazima tuieneze injili ya ondoleo la dhambi kwa zile roho ambazo bado hazijaisikia injili hii, na pia ni lazima tuwahubirie Neno la Ufunuo, ambalo ni ukamilifu wa injili. 
Ninatumaini na kuomba ili kwamba kila mtu amwamini Yesu, ambaye ni Muumbaji, Mwokozi na Hakimu, na nyakati za mwisho zitakapowadia, aweze kuingia katika Mbingu na Nchi Mpya iliyotolewa na Bwana. Neema ya Bwana Yesu na iwe nanyi nyote.