Search

Mahubiri

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 8-4] Kuwa na Mawazo ya Kimwili ni Kifo, Bali Kuwa na Mawazo ya Kiroho ni Uzima na Amani (Warumi 8:4-11)

(Warumi 8:4-11) 
“ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho. Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamuufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.”
 

Umisionari katika nchi za nje unakuwa mzuri zaidi unapokuwa ukifanywa kwa kupitia uandishi, ambayo ndiyo kazi tunayoifanya hivi sasa. Tunabarikiwa tunapolisoma Neno la Mungu na imani yetu inakua kwa sababu tunaamini katika Neno lake. 
Watu wamekuwa wakiteseka kwa karne tano zilizopita hali wakidanganywa na mafundisho potofu ya kiimani kama vile Fundisho la Utakatifu Unaozidi, Fundisho la Kuhesabiwa Haki kwa Imani, na mafundisho mengine ambayo yanasisitiza kuwa ukombozi unawezekana kwa kupitia sala za toba. 
Warumi 8:3 inatueleza sisi kuwa Mungu alifanya kile ambacho Sheria isingaliweza kukifanya kwa kuwa ilikuwa ni dhaifu kwa kupitia mwili. Mungu alimtuma Mwana wake pekee katika mfano wa mwili wenye dhambi, akaihukumu dhambi katika mwili wake, na akamhukumu ili kutukomboa sisi toka katika dhambi zetu zote. 
Sasa, tunageukia Warumi 8:4-11 kwa ajili ya ukweli wa Mungu. Warumi 8:3-4 inasema, “...Mungu ...aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioendnenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” Kwa kweli swali linabaki kuwa aya hizi zina maanisha nini? 
 

Kwanza, Kuishi kwa Kutofuata Mambo ya Mwili Kuna Maanisha Nini? the flesh?
 
Hii ina maanisha kuwa kutotafuta faida ya mwili. Ni kutenganisha kati ya matakwa ya Roho na tamaa za mwili, na kukaa mbali na wale ambao hawalitii Neno la Mungu. Aya ya 5 inasema, “Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili.” Haya mambo ya mwili yana maanisha kitu gani? Hii ina maanisha kuwa kuna wale ambao pamoja na kuwa wanahudhuria kanisani wapo pale kutafuta matamanio yao binafsi. 
Kwa lugha rahisi, Wakristo hawapaswi kwenda kanisani kwa lengo la kupata au kutafuta faida ya kibiashara ulimwenguni. Huku ndiko kuishi kwa kuufuata mwili. Watu hawa wanakwenda katika makanisa yaliyo na waumini wengi ili kuzitambulisha na kuzitangaza biashara zao kwa matumaini kuwa wanaweza kupata wateja wa mara kwa mara na wa kudumu. Wanahudhuria kanisani na wanamwamini Yesu kwa ajili ya miili yao wenyewe. 
Kuna wengine pia. Wale ambao wanafundisha umadhehebu kati ya jumuiya ya Wakristo; wale ambao wanawafundisha wafuasi wao kuzitafuta baraka za mali tu na wao pia ndio wanaoishi kwa kuufuata mwili na ambao wamezielekeza akili zao katika vitu vya kimwili. 
Tunaweza kuliona kwa urahisi kabisa suala la umadhehebu katika jumuiya ya Kikristo. Je, hawa wanamadhehebu ni watu gani? Hawa ni watu ambao wanajidanganya wao wenyewe hali wakiwa na imani iliyopotoshwa hali wakijivunia madhehebu yao. Wanasema kuwa dhehebu lao lilianzishwa na fulani na kwamba wamekuwa na wanatheologia kama vile fulani na fulani, na kwamba dhehebu lao ni kubwa na linalofahamika duniani kote na kwamba wana desturi na mapokeo yenye nguvu sana na kadhalika. Majivuno haya yote ndiyo yanayoufanya uharibifu wa watu hawa na hivyo wanaijenga imani yao binafsi. Kuna watu wengi wenye imani kama hiyo katika ulimwengu huu. 
Wanamadhehebu wanamwamini Yesu kwa faida za miili yao binafsi. Wale wanaoishi kwa kuufuata mwili bado wanaendelea kujivunia makanisa yao na baraka ambazo wamezipata katika upande wa mali kwa kuhudhuria katika makanisa yao makubwa. Baadhi ya makanisa yana lengo moja la kijamii kama vile “mpende mkeo.” Pia lengo kama hili ni sehemu ya wale wanaoishi kwa kuufuata mwili. Je, makanisa yanapaswa kuweka lengo lao katika mkazo wa mtu kumpenda mke wake? Kwa kweli hayapaswi kufanya hivyo. Je, kwa hiyo ninasema kuwa tusiwapende wake zetu? Kwa kweli sio hivyo! Lakini malengo ya jinsi hiyo hata kama yatakuwa ni mazuri hayapaswi kuwa ndio msingi wa dhumuni la Kanisa. 
Wale wanaoishi kwa kuufuata mwili wanazielekeza akili zao katika mambo ya mwili. Watumishi wengi siku hizi wamegeuka na kuwa watu wa jinsi hiyo hasa pale wanapokuwa wakivutiwa na kuongezeka kwa idadi ya waumini katika makanisa yao, ongezeko la matoleo na majengo—mambo haya kwa sasa yamefanyika kuwa ndio malengo yao makuu. Kujenga kanisa kubwa zaidi, refu, na la kutosha imekuwa ndio lengo lao kuu. Hata kama wanasema kwa nje kuwa lengo lao ni kukusanya wafuasi wengi ili kuwapeleka watu wengi Mbinguni lakini ukweli unabaki kuwa lengo lao kuu ni kupata fedha nyingi zitokanazo na sadaka ili kuweza kujenga majengo makubwa ya kanisa. 
Ili waweze kuyafanya makanisa yao kuyafuata mambo ya mwili basi wanawageuza wafuasi wao kuwa wakereketwa wa dini. Baadhi ya wachungaji wameyajenga mafanikio yao katika uwezo wa kuwageuza waumini wao kuwa wakereketwa wa dini, wenye nusu-upunguani, wenye kujidanganya, na waliopotoshwa. 
 

Wale Wanaoishi Kwa Kufuata Roho wa Mungu
 
Hata hivyo, miongoni mwa Wakristo wapo wale ambao kwa kweli wanaishi kwa kufuata mambo ya Roho wa Mungu. Wakristo hawa wanaoishi kwa kufuata mambo ya Roho wanaishi kwa kulifuata Neno la Mungu, wanakiamini kile kilichoandikwa katika Maandiko hali wakiyakana mawazo yao binafsi, wanafanya kile ambacho Mungu anapenda, na wanaihubiri injili ya maji na Roho. 
Biblia inasema kuwa wale wanaoishi kwa kuifuata Roho wanazielekeza akili zao katika mambo ya Roho. Ikiwa tumesamehewa dhambi zetu zote kwa kuamini katika haki ya Mungu, basi hatupaswi kuishi pasipo kufikiria bali tuishi hali tukitafakari juu ya kazi ya Roho. Wale wanaoishi kwa Roho wanafikiria kiroho na wanajitoa kufanya mambo ya Roho kwa imani. Heri yao wanaoyafuata mambo ya Roho. Hao ndio watu ambao wanamfurahisha Mungu, wanaowaokoa wengine toka katika dhambi za ulimwengu, na ndio hao hao wanaoishi kwa imani. Sisi tumesamehewa dhambi zetu na kwa hiyo ni lazima tuzielekeze akili zetu katika mambo ya Roho na tuishi kwa kufuata mambo ya Roho. 
Katika maisha yetu lengo liwe ni kuitimiza kazi ya Roho, ambayo ni kuihubiri injili ya maji na Roho. Ni lazima tuzielekeze akili zetu katika mambo ya Roho. Je, ni umezielekeza akili zako katika mambo ya Roho kwa kiasi gani? Sisi tunapambana na vita ya kiroho na ni lazima tuyafanyie mazoezi mambo ya kiroho kwa kuamini katika haki ya Mungu na kwa kuihubiri haki hiyo. Hata kama tutakuwa dhaifu na wenye mapungufu ni lazima wakati wote tufikirie yale yanayo mfurahisha Bwana na kisha kuweka changamoto katika kazi ya Roho kwa kuzielekeza akili zetu katika kazi ya Mungu. Inapotokea kuwa kazi fulani imefanyika basi ni lazima tuongeze juhudi ili kufanya kazi zaidi ambazo zinampendeza Mungu. 
Sasa tunaihubiri injili ya maji na Roho katika ulimwengu mzima kwa kupitia uandishi wa vitabu. Takribani watu 200 hadi 300 wanavipokea vitabu vyetu vya Kikristo vya bure na vitabu-pepe kila siku kwa kuitembelea tovuti yetu. Sisi tunaitumikia injili pamoja nawe katika Kanisa la Mungu kwa kuing’ang’ania imani katika kuhubiri injili ya maji na Roho kwa kila mtu ulimwenguni. Ikiwa tungelikuwa hatujazielekeza akili zetu katika mambo ya Roho, basi kwa hakika tungekuwa hatujapewa matunda haya ya Roho. Sisi ni lazima tuiendeleze kazi yake moja baada ya nyingine hali akili zetu zikiwa zimeelekezwa katika mambo ya Roho. Basi kwa kufanya hivyo, kwa hakika tutampendeza bwana harusi wetu wa kiroho, Yesu Kristo, kama vile mke mwema anayepatikana katika Mithali sura ya 31. 
Aya ya 8 inasema, “Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.” Hii inazungumzia wale ambao hawajapokea msamaha wa dhambi. “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu” (Warumi 8:7-8). Kwa hiyo, wenye dhambi ambao hawana Roho ndani yao hawawezi kuifanya kazi ya Mungu wala hawawezi kumpendeza Mungu. 
Wenye dhambi hawaitii sheria ya Mungu. Wala hawaitii haki ya Mungu. Hivyo hawawezi kumpendeza Mungu. Hii ni kwa sababu watu wa jinsi hii hawawezi kuyafahamu mapenzi ya Mungu jinsi yalivyo kwa kuwa Roho Mtakatifu hakai ndani yao. Kinachomfurahisha Bwana ni kuzisamehe dhambi zote za wanadamu kwa injili ya maji na Roho. Mungu hafurahishwi na sifa na maombi ya wenye dhambi. 
Mungu hafurahishwi wakati wenye dhambi wanapomsifu. Haijalishi ni kwa kiasi gani wenye dhambi watainua mikono yao ili kusifu na kumwaga machozi yao katika ibada, bado wenye dhambi hao hawawezi kumpendeza Mungu. Wakristo wenye dhambi wanajaribu kumpendeza Mungu kwa kuleweshwa na mihemko ya hisia. Ukweli ni kuwa hawawezi kumpendeza Bwana. Wale walio na dhambi hawawezi kumpendeza Mungu kwa kuwa ni wenye dhambi. Haijalishi ni kwa kiasi gani wanajaribu kufanya, ukweli ni kuwa wenye dhambi hawawezi kumpendeza Bwana. Suala la msingi hapa si halihusiani na kiwango cha nia waliyonayo katika kumpendeza Bwana; bali ni ule ukweli kuwa haiwezekani kwa wao kumpendeza Bwana. 
Je, Mungu atapendezwa ikiwa watu watajenga makanisa makubwa? Kwa kweli hatapendezwa. Ikiwa ni muhimu kuhamia katika jengo kubwa la kanisa, basi kanisa kubwa ni lazima lijengwe kwa jitihada zote. Lakini kujenga kanisa kubwa ati kwa sababu ya jengo tu hilo haliwezi kumpendeza Mungu kabisa. 
Kwa mfano hivi karibuni kanisa moja katika mji wangu lilitumia takribani dola za kimarekani millioni 3 ili kujenga jengo jipya la kanisa wakati kanisa la kwanza lipo likiwa imara na likiwa limesimama katika hali nzuri. Jengo hilo jipya la kanisa lilipojengwa kulikuwa na waumini kati ya 200-300, je kulikuwa na haja yoyote ya kujenga jengo jipya la kanisa? Kanisa la Mungu halijengwi kwa matofali. Mungu anatueleza sisi kuwa tu hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani ya mioyo ya wenye haki. 
Ni sahihi kujenga kanisa kubwa ikiwa kuna uhitaji wa kufanya hivyo, lakini kujenga makanisa makubwa tu peke yake kunampatia Mungu utukufu? Jibu ni hapana. Je, kuwakusanya watu wengi kuingia kanisani kunampatia Mungu utukufu? Hapana, huwezi kumfurahisha Mungu kwa kufanya hivyo. Wale walio katika mwili hawawezi kumpendeza Bwana. 
Wakati fulani hata watu wenye haki wanafukuzia faida za mwili tu. Watu hawa hawawezi kumpendeza Bwana. Kuna baadhi ya watu miongoni mwa wenye haki ambao bado wamefungwa na mawazo ya mwili kama ilivyo kwa wenye dhambi. Watu wa jinsi hii hawawezi kumpendeza Mungu. Kwa kweli, watu hawa hawezi kuishi maisha ya imani yenye afya katika kanisa, bali huendelea kulalamika, na hatimaye huliacha kanisa la Mungu. 
Kwa hiyo, sisi ambao ni wenye haki tunapaswa kuishi maisha ambayo ni ya haki na yanayompendeza Mungu, na wala si maisha yanayotafuta faida ya mwili tu. Ni lazima tufikirie juu ya kazi za Mungu na haki yake, ni lazima tuzitumikie kazi za haki yake, na kisha tutumie miili yetu, akili, na vyote tulivyonavyo kama vyombo vya haki ya Mungu. Ni lazima tuishi maisha ambayo yanampendeza Mungu. 
 

Wale Walio Katika Roho wa Kristo 
 
Hebu tusome aya ya 9 pamoja. “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamuufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”
Kwa mujibu wa Paulo, kifungu hiki kina maanisha kuwa ikiwa tunaamini katika injili ya maji na Roho—kwa maneno mengine, ikiwa tunaamini katika haki ya Mungu—na ikiwa tumekombolewa toka katika dhambi zetu, basi sisi hatumo tena katika mwili bali katika Roho. Ikiwa mtu awaye yote ana Roho wa Mungu basi mtu huyu yumo katika Kristo, na ikiwa mtu hana Roho wa Kristo basi huyo si wake. 
Hivyo basi, sisi hatumo katika mwili bali tumo katika Roho. Sisi ambao tumo katika Roho na ambao tumekombolewa toka katika dhambi kwa kupitia injili ya maji na Roho hatupaswi kusahau kuwa sisi ni maaskari wa haki ambao tuna uwezo wa kumpendeza Mungu kama wenye haki katika Kristo. Sisi hatupaswi kufa moyo kwa sababu ya udhaifu wa miili yetu bali tumpendeze Mungu kwa imani kwamba ingawa tu wadhaifu, sisi ni mali yake na kwamba tumo ndani yake na kwamba sisi tu watenda kazi wake. 
Ni lazima tutambue kuwa baada ya kuzaliwa tena upya hairuhusiwi kutafuta faida za mwili tu. Ni lazima tuishi hali tukifahamu kuwa wenye haki wamepangiwa ili kuishi kwa ajili ya haki ya Mungu tu. Aya ya 10 inatuonyesha jinsi Wakristo tunavyopaswa kuishi: “Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki.”
Kusema kweli, miili yetu ilisulubiwa na kufa pamoja na Yesu Kristo kwa sababu ya dhambi zetu. Tumeokolewa toka katika dhambi zetu zote kwa kupitia tendo la haki la Mungu. Kwa sababu ya haki hii, basi roho za wenye haki zina uzima wa milele! Ni lazima tutambue kuwa wale waliohesabiwa haki kwa imani hawaruhusiwi tena kuishi kwa ajili ya miili yao tu. Wale ambao hawaishi kwa ajili ya haki ya Mungu hata baada ya kuzaliwa tena upya, basi watu hao wapo mbali na baraka za Mungu. 
Sisi tulipangiwa ili kuishi kwa ajili ya haki ya Mungu. Pengine baadhi yenu baada ya kuwa mmezaliwa tena upya kwa maji na Roho mmekuwa na mawazo ya kukata tamaa hali wakiwaza, “Biblia inasema kuwa wale walio katika mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Bila shaka mimi nitakuwa mmoja wao.” Lakini hii si kweli. Mungu ametuzaa tena upya ili kuishi kama askari wa haki yake. 
Baadhi ya watu wanafikiria hivyo labda kwa sababu wameielewa vibaya Biblia. Hata kama baadhi ya wenye haki wanafikiri kuwa hawawezi kuishi kwa kumfuata Mungu kwa sababu ya miili yao inaishi kwa kuufuata mwili na kwamba miili hiyo ni dhaifu, ukweli ni kuwa wale walio na Roho Mtakatifu wanafurahia kwa kuzifanya kazi za Mungu. Kule kuzifanya kazi za Mungu kunawafanya wao kuwa na furaha. Kwa upande mwingine, maisha pasipo kuzifanya kazi za Mungu ni maisha pasipo motisha wala dhumuni na ni maisha yaliyo laaniwa. 
Baada ya kuwa tumeipokea injili ya maji na Roho na kisha kukaa katika haki ya Mungu, basi Roho Mtakatifu atakaa ndani yetu. Roho Mtakatifu anakuja na kukaa juu ya mtu yeyote ambaye ameupokea ukombozi. Je, nini kinachotokea ndani ya wale ambao Roho Mtakatifu anakaa ndani yao? Hao wamepangiwa kuitumikia haki ya Mungu na kuifanya kazi ya Mungu ya haki. 
Kwa ufupi, wale waliopokea msamaha wa dhambi na wamehesabiwa haki basi wanapaswa kuishi kwa imani. Wenye haki wanaweza kuitunza imani yao pale tu wanapoishi kwa imani na wanapozifanya kazi za Mungu. Ikiwa unafikiri kuwa utaishi katika ulimwengu huu kwa mwili wako pamoja na kuwa umehesabiwa haki, basi utambue wazi kuwa hii ni kwa sababu hujatambua kuwa umepokea ondoleo la dhambi. 
Mahali pa wenye haki walipopangiwa pamebadilika. Kabla hawajazaliwa tena upya, walikuwa wakiishi kwa ajili ya ulimwengu na kwa ajili yao binafsi, na walikuwa na furaha wakati huo walipokuwa wakiishi kwa kufuata tamaa zao za kimwili. Hata hivyo, baada ya kuzaliwa tena upya, basi ni vigumu kuendelea kuishi kama vile tena. Sisi tumepokea ondoleo la dhambi. Je, tutakuwa na furaha hata kama tutapata pato la sita zaidi? Tunapojitoa sisi wenyewe katika kuzikomboa nafsi nyingine toka katika ulimwengu huu, tunawezaje basi kuridhishwa na mambo yahusianayo na mali? 
Kwa maneno mengine, ninakuomba ufikiri kwa kina kuhusu mambo ya mwili na yale ya Roho. Hupaswi kuyatenda mambo hayo ndipo uweze kuyafahamu; unachopaswa kukifanya ni kufikiria kwa kina kuhusiana na jambo hili. 
Nimekwisha hubiri mara nyingi katika kitabu cha Warumi kuanzia sura ya 1 hadi ya 6 katika kitabu changu cha mahubiri kilichopita cha Warumi, na pia nimehubiri katika sura ya 7 hadi ya 16 ya kitabu cha Warumi katika kitabu hiki. Vitabu hivi viwili vya mahubiri, kitabu cha 4 na cha 5 katika mfuatano wa vitabu vyangu vya Kikristo vitatolewa kwa Wakristo katika ulimwengu mzima ili waweze kujisomea. Nina hakika kuwa watu wengi wataweza kuifahamu haki ya Mungu kwa kupitia mfuatano au mfululizo wa vitabu hivi. Kwa kupitia mfululizo wa vitabu vitatu vya mahubiri nilivyovitoa, nimezungumzia juu ya mafundisho ya msingi kuhusiana na wokovu wa Mungu. Toleo la kwanza lilizungumzia juu ya injili, toleo la pili lilizungumzia juu ya masuala ya kitheolojia, na toleo la tatu lilizungumzia juu ya Roho Mtakatifu na juu ya njia sahihi ya jinsi ya kumpokea Roho Mtakatifu. Na toleo hili na nne na tano katika Warumi yanazungumzia kwa kina jinsi ambavyo mafundisho mengi ya kitheolojia yalivyo na makosa, pia vinajibu maswali kama kwa nini dhambi haitoweki hata pale ambapo Wakristo wanamwamini Yesu? Na pia vinaeleza jinsi ambavyo injili ya maji na Roho inavyofunuliwa kuwa ndiyo haki ya Mungu. 
Ninaamini kuwa injili itaenea kwa upana zaidi ulimwenguni kwa kupitia kitabu hiki. Kumekuwa na maendeleo mazuri katika kuihubiri injili hasa pale tulipochapisha kitabu cha tatu kuliko wakati tulipokuwa tumechapisha vitabu viwili vya kwanza. Sasa, baada ya toleo la tatu, watu wengi sana wamekuwa wakiviulizia vitabu vya toleo la kwanza na toleo la pili katika mfuatano au mfululizo wa vitabu vyangu vya Kikristo. 
Baada ya kuwa vitabu hivi viwili vimechapishwa, ndipo tutakapoweza kutambua jinsi injili ya maji na Roho ilivyo na nguvu kuu. Ninaomba kuwa baraka nyingi za Mungu ziwaendee wale wote ambao watafikia kuifahamu haki ya Mungu. Hii ni kwa sababu wataweza kukifahamu vizuri kitabu cha Warumi na huko ndiko kufahamu kwa imani kunakohusisha injili ambayo ina haki ya Mungu. 
Sisi sote tunafanya kazi kwa ajili ya injili. Je, wewe huifanyi kazi ya Mungu? Wewe unaiunga mkono huduma ya kuihubiri injili ili kuwaokoa wenye dhambi toka katika dhambi zao. Tunapokuwa waaminifu kwa upande wetu na tunapoitumikia injili, basi ni hakika kuwa nafsi nyingi ulimwenguni kote zitakombolewa toka katika dhambi zao. Tunawezaje basi kuiacha kazi hii ya thamani ati kwa sababu ya kazi ya kidunia? 
Ninapenda kuweka wazi mbele yako kuwa, sisi wenye haki, tumepangiwa kutoishi kwa ajili ya miili yetu tu. Sasa, sisi tumepangiwa kuikamilisha haki ya Mungu, kuziokoa nafsi, na kuishi kwa ajili ya haki ya Mungu. Ni lazima ulitambue jambo hili na kisha uutumie muda wako uliosalia kuishi kwa ajili ya Mungu, kwa ajili ya injili ya kweli, na kwa ajili ya wokovu wa nafsi zilizopotea katika dhambi. 
Hivi ndivyo kitabu cha Warumi kinavyosema kuhusiana na sehemu hii. Hebu tuangalie aya ya 10 na ya 11. “Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihusisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.”
Kifungu hicho hapo juu kina maanisha kuwa miili yetu sisi imekufa kwa sababu ya dhambi zetu. Lakini roho zetu zi hai kwa sababu ya haki ya Mungu na imani. Ikiwa mtu yeyote anaamini katika haki ya Mungu, basi mtu huyo atapata maisha mapya. Sisi tumeyapata maisha mapya kwa kuamini katika haki ya Mungu. 
Aya ya 11 inasema, “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu inakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihusisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.” Hii ina maanisha kuwa Yesu atatufua sisi mwisho wa dunia. Maisha ambayo tutakuwa tumeyaishi kwa muda mrefu uliopita kwa ajili ya mwili na dhambi sasa yamepita, na mahala petu pamebadilika ili kuyaishi maisha yetu yaliyosalia kwa ajili ya Mungu na haki yake. 
Unaweza kuudhiwa na maisha ya wenye haki, hali ukisema, “hakuna shaka kuwa wenye haki watakusanyika na kusema yale wanayoyasema.” Hata hivyo, hata kule kuusikia mwayo wa mwamini aliyezaliwa tena upya au kumsikiliza akisifu kwa sauti kutayafanya mawazo yako kuwa mapya hasa pale utakapokuwa ukidumu kuwepo kanisani. Hii ni kwa sababu Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani ya kanisa la Mungu na katika mioyo ya waamini. Mawazo yako yatafanywa upya na utapata nguvu mpya katika moyo wako, utalishwa mkate wa kiroho wa uzima, na kisha utayapata majukumu yako ya kiroho ili kuweza kwenda nje ya kanisa na kuzifanya kazi za kiroho. 
Unaweza kuburudishwa unapokuwa umekusanyika katika kusanyiko la waamini. Ule ukweli kuwa wewe umetenganishwa na ulimwengu ni uthibitisho tosha kuwa hatma yako imebadilika. Hii ndiyo sababu wale wanaoishi kwa kuufuata mwili wamezielekeza akili zao katika mambo ya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kuifuata Roho, wamezielekeza akili zao katika mambo ya Roho. Sisi ambao tumehesabiwa haki hatuishi kamwe kwa kuufuata mwili. Wenye haki hawapendi kamwe kuwa watumwa wa dhambi. Kwa kweli tunapenda kuishi kwa kuifuata Roho na kisha kuzielekeza akili zetu katika mambo ya Roho. Wenye haki wanafanya mambo ya Roho ambayo ni kazi ya kuzipata nafsi kwa ajili ya Kristo. 
Ni lazima tufanye kazi kwa juhudi kwa ajili ya kazi ya Mungu, ni lazima tuyakane mawazo na akili zetu binafsi, na kisha tuzielekeze akili zetu katika kazi ya Mungu. Ni lazima tuishi maisha yetu yaliyosalia kwa jinsi hii. Mustakabali wako umebadilika na unakufanya uishi kwa ajili ya haki ya Mungu tu, hii ni kwa sababu umeupokea ukombozi kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Ninaamini kuwa unaufahamu ukweli huu. 
Samahani sana, lakini ukweli ni kuwa huwezi tena kurudi katika ulimwengu na kwenda kuwa mtumwa wa dhambi kwa mara nyingine. Ikiwa utaurudia ulimwengu, hiyo itakuwa ni sawa na kuyarudia mauti. Kuwa na mawazo ya kimwili ni kifo. Ikiwa utaendelea kuzifuata tamaa za mwili, basi ujue kuwa roho yako itakufa, akili zako zitakufa, na mwili wako utakufa. Mara baada ya kutoka Misri Waisraeli hawakurudi tena Misri; wala hawakuwa na furaha kuonana na Mmisri baada ya kuwa wameivuka Bahari Nyekundu. Vivyo hivyo, sisi ambao tumehesabiwa haki hatuwezi kamwe kurudi tena Misri, wala hatuwezi kuwa na furaha ya kukutana na Mmisri wa kiroho. 
Ikiwa mwenye haki, mtu aliyezaliwa upya anauendea ulimwengu na anaishi pamoja na wenye dhambi wa ulimwenguni, basi mtu huyo atapata changamoto ya kutaka kurudi tena katika kanisa la Mungu. Mtu wa jinsi hiyo atalikosa kanisa la Mungu. Hivyo, hebu tuishi hali akili zetu zikiwa zimeelekezwa katika mambo ya Roho. 
Je, hayo mambo ya Kiroho ya Mungu yana maanisha nini? Je, mambo hayo si mambo ya Mungu? Je, si mambo yanayohusiana na kuitumikia injili ya Mungu? Je, sisi si wadhaifu na wenye mapungufu? Wewe ni dhaifu na mimi pia ni dhaifu. Lakini, hukupokea msamaha wa dhambi hata pale ulipokuwa ukingali ni mdhaifu na mwenye mapungufu? Kwa kweli ulipokea msamaha! Je, Roho Mtakatifu anakaa ndani yako? Bila shaka jibu ni ndiyo!
Je, sisi tunaweza kuyaelekeza mawazo na akili zetu katika mambo ya Roho au hatuwezi? Kwa kweli tunaweza—sisi sote tunaweza kuyaelekeza mawazo na akili zetu katika mambo ya Roho. Je, unafahamu kuwa Mungu ameubadilisha mustakabali wako ili kwamba uweze kuyafanya mambo ya Roho? Je, unaamini hivi? 
Mawazo na akili zetu sasa zimebadilishwa. Ikiwa haufahamu kuwa mawazo na akili zako zimebadilishwa hata pale inapoonekana hivyo, basi utambue kuwa kuna tatizo ndani yako. Ni lazima uzielekeze akili zako kwa nguvu zote katika haki ya Mungu. Ukifanya hivyo, basi kanisa la Mungu litakuwa ndio nyumbani kwako, waamini wenzako watakuwa ndio ndugu zako na wazazi wako na familia yako katika Roho. Kila mmoja katika kanisa lako atakuwa sehemu ya familia yako. Ikiwa ulikuwa hujafikiria hivyo hapo kabla basi sasa ni wakati wako wa kuyatafakari kwa kina mafundisho haya. 
Usifikirie kuwa familia yako ambayo mna uhusiano wa damu na nyama ndiyo familia yako pekee. Mahali walipo wale waliozaliwa tena upya ndio nyumbani kwako na kila aliyezaliwa tena upya ni mmoja wa wanafamilia wako. Ninyi nyote ni sehemu ya familia ya Mungu. Na hii ndio sababu inatupasa kuishi kwa kuifuata Roho. Ni lazima tuishi kwa ajili ya Mungu, kwa kuwa na akili za kiroho ni kuipata amani.