Search

Mahubiri

Somo la 9: Warumi (Maoni juu ya Kitabu cha Warumi)

[SURA YA 8-5] Kutembea Katika Haki ya Mungu (Warumi 8:12-16)

(Warumi 8:12-16)
“Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu,” 
 

Mtume Paulo, kama mtu aliyepokea wokovu toka kwa Mungu alisema kuwa wale waliozaliwa tena upya hawapaswi kuishi kwa jinsi ya mwili bali kwa jinsi ya Roho. Hasahasa Paulo alisema kuwa ikiwa sisi ambao tunayo haki ya Mungu tutaishi kwa jinsi ya mwili basi tutakufa, na kwamba kama tutaishi kwa jinsi ya Roho basi tutaishi. Hivyo ni lazima tuamini katika ukweli huu. Je, inakuwaje basi kwa wale wanaoamini katika haki ya Mungu? Je, wanapaswa kuishi kwa mujibu wa haki ya Mungu au kwa tamaa ya mwili? Ni lazima watambue kile kilicho sahihi na kisha waiadabishe miili yao ili kujitoa kwa kazi za haki ya Mungu. 
 

Jukumu Lisilokwepeka
 
Mtume Paulo alidai kuwa tuna jukumu la kuishi kwa jinsi ya Roho, na si kwa asili ya dhambi zetu, kwa sababu sisi Wakristo tumeokolewa toka katika hasira ya Mungu na kuongozwa katika haki ya Mungu. Kabla hatujaifahamu haki ya Mungu na kuiamini kwa kweli tusingeweza kuishi kwa jinsi ya Roho. Lakini kwa kuwa sababu tunafahamu na kuamini katika haki ya Mungu tunaweza kuitoa mioyo yetu, mawazo, vipawa, miili, na muda katika kazi ya Mungu ya haki. Ni lazima tujitumie sisi wenyewe kama nyenzo katika kuihubiri haki ya Mungu na kuzifanya kazi zake za haki. 
 

Kuishi Kwa Jinsi ya Mwili 
 
Ikiwa umo ndani ya Kristo na unaishi kwa kufuata asili ya dhambi na wala si kwa jinsi ya Roho, Biblia inasema kuwa utaangamia kama watakavyo angamia wengine wasioamini. Hii ni kwa sababu hata kama ni Mkristo uliyezaliwa tena upya bado huishi kwa jinsi ya haki ya Mungu. Ikiwa utapenda kuwa Mkristo wa kweli basi hupaswi tena kuishi kwa jinsi ya mwili bali kwa haki ya Mungu, kwa kuwa umechaguliwa kuitumikia haki yake kwa kuwa unaiamini haki hiyo. Ikiwa unaishi kwa jinsi ya mwili badala ya kuishi kwa Roho, basi roho yako itakufa. Hata hivyo, ikiwa utaishi kwa mujibu wa haki ya Mungu basi utaishi kwa imani milele. 
 

Wana wa Mungu 
 
“Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” (Warumi 8:14).
Wale wanaoamini katika haki ya Mungu wanampokea Roho Mtakatifu kama karama na kisha Roho Mtakatifu anawaongoza. Hawa ni “wana wa Mungu.” “Wana wa Mungu” wana Roho Mtakatifu anayekaa ndani yao. Kwa hiyo, wale wasio na Roho Mtakatifu ndani yao basi hao si wa Mungu. Mahali pa kuanzia katika kumfuata Mungu panaanzia katika imani katika haki yake. Kufanyika mtoto wa Mungu kunaanza kwa kuamini katika Neno la injili ya maji na Roho. Kwa maneno mengine, kufanyika mtoto wa Mungu kunaanza kwa kuamini katika injili ya haki yake. Hii ina maanisha kuwa unafanyika kuwa mwana familia ya Mungu kwa kuamini katika haki yake na kwamba Mungu ametoa haki yake ili kukuokoa toka katika dhambi. 
Wakati Yesu alipoalikwa na Nikodemo aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa Kiyahudi, Yesu alimwambia hakuna anayeweza kufanyika mtoto wa Mungu pasipo kuzaliwa tena upya kwa maji na Roho. Nikodemo alishangazwa sana na neno hili akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee?” (Yohana 3:4). Yesu akamjibu, “Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yohana 3:5-8).
Yesu alisema kuwa yeye ambaye hajazaliwa kwa maji na Roho hawezi kufahamu maana ya kuzaliwa tena upya. Imani katika ubatizo wa Yesu alioupokea toka kwa Yohana Mbatizaji na damu yake aliyoimwaga Msalabani inawawezesha wote wanaoamini katika tendo lake la haki kupokea haki ya Mungu. Wale wanaoamini katika Neno la injili wanaweza kumpokea Roho Mtakatifu kama karama au zawadi. Mtu anaweza kuifikia haki ya Mungu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho. Yeyote anayeipokea haki ya Mungu anaweza kufanyika mtoto wa Mungu. Wale wanaofanyika watu wake ni kaka zetu na dada zetu. 
 

Roho Hutushuhudia Kuwa Sisi tu Watoto wa Mungu
 
“Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Warumi 8:15-16).
Kuna njia mbili tu ambazo kwa hizo tunaweza kuubeba ushuhuda kwa kuzingatia ukweli kuwa sisi tu watoto wa Mungu. Kwanza, haki ya Mungu ambayo imefunuliwa katika injili ya mji na Roho imetufanya sisi kuwa watoto wake; na pili, Roho Mtakatifu anakuja na kwetu. Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani ya injili ya maji na Roho. Mungu aliyapangilia mambo haya yote. Kuwa na imani katika injili ya maji na Roho ni ushuhuda kwetu wenyewe unaotueleza sisi kuwa tumefanyika kuwa watoto wa Mungu. Wale waliofanyika kuwa watoto wa Mungu kwa kufahamu na kuamini katika haki ya Mungu wanayo haki ya kuomba kwa Mungu wakisema “Abba” yaani Baba yetu. 
Hebu tujaribu kufikiri kimantiki. Inawezekanaje kwa mtu mwenye dhambi katika moyo wake kumuita Mungu Baba yake? Mungu Baba hajawahi kumtunza mwenye dhambi kama mtoto wake, na mwenye dhambi hajawahi kumtumikia Mungu kama Baba. Ni lazima ujiangalie ndani yako mwenyewe ili uone kama kwa namna yoyote unafanya makosa kama haya. Wale wanaoshuhudia kufanyika watoto wa Mungu kwa kupitia Roho Mtakatifu ni wale wanaoamini katika haki ya Mungu. Ni lazima tufikiri kwa kina kuhusu haki ya Mungu.