Search

Mahubiri

Somo la 10: Ufunuo (Ufafanuzi juu ya Ufunuo)

[14-1] Sifa za Wafia-dini Waliofufuka na Kunyakuliwa (Ufunuo 14:1-20)

(Ufunuo 14:1-20)
“Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao. Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao; na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne elfu, walionunuliwa katika nchi. Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa. Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji. Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake. Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo. Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake. Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu. Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao. Kisha nikaona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa. Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa. Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana. Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu. Shinikizo lile likakanyagwa nje ya mji, damu ikatoka katika shinikizo mpaka kwenye hatamu za farasi, kama mwendo wa maili mia mbili.”
 

Mafafanuzi
 
Aya ya 1: Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao.
Hii ni kuhusiana na watakatifu waliozaliwa tena upya, ambao walifufuliwa na kunyakuliwa baada ya kuuawa kama wafia-dini na Mpinga Kristo, wapo wakimsifu Bwana Mbinguni. Watakatifu waliouawa na Mpinga Kristo kama wafia-dini na watakatifu waliokufa hapo kabla sasa watakuwa Mbinguni, huku wakimsifu Bwana kwa wimbo mpya. Katika aya ya 4 tunaona kwamba watu 144,000 waliimba wimbo huu mpya. Sasa unaweza kushangaa, kwamba watakatifu wanaweza kuwa ni hao watu 144,000 tu. Lakini namba 14 ina maanisha kwamba mambo yote yamebadilika (Mathayo 1:17).
Tunapaswa kutambua kwamba baada ya mauaji ya wafia-dini na kunyakuliwa kwa watakatifu, Bwana ataubadilisha ulimwengu huu wa sasa kuwa katika ulimwengu mpya. Badala ya ulimwengu huu, Bwana wetu ataujenga ulimwengu ambao ataishi ndani yake pamoja na watu wake. Haya ni mapenzi ya Muumba.
Wale wanaomsifu Bwana Mbinguni ni wale ambao wamefanyika kuwa watakatifu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Kristo wakati alipokuwa hapa duniani. Kwa hiyo, katika vipaji vya nyuso zao wameandikwa majina ya Mwana-Kondoo na Mungu Baba, kwa kuwa sasa wao ni mali ya Kristo.
 
Aya ya 2: Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao. 
Watakatifu wanaonekana Mbinguni ni wale ambao waliuawa kama wafia-dini ili kuulinda wokovu wao ulitolewa na Bwana na pia katika kuilinda imani yao kwamba Bwana ndiye Mungu wao, na ambao walifufuliwa baadaye. Kwa kuwa miili yao ilifufuliwa na walinyakuliwa kwa nguvu za Bwana, basi ndio maana wanamsifu Bwana wakiwa Mbinguni kwa ajili ya wokovu wake na baraka yake ya kuwapatia mamlaka. Sauti ya sifa zao ni nzuri kama sauti ya maji mengi yanayotiririka, na ni kuu kama vile ngurumo. Wote wameokolewa milele toka katika dhambi zao zote kwa kupitia ukombozi wa dhambi zao kwa kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana wakati alipokuwa hapa duniani. 
 
Aya ya 3: Na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne elfu, walionunuliwa katika nchi.
Watu 144,000 ina maanisha ni watakatifu walionyakuliwa. Katika Biblia, namba 14 ina maanisha ni mabadiliko mapya. Wale wanaoweza kumsifu Bwana kwa wimbo mpya Mbinguni ni wale ambao wamebadilishwa na kutengenezwa wakati walipokuwa hapa duniani kwa kupokea ondoleo la dhambi na kisha kuzaliwa tena upya kwa kupitia imani yao katika injili ya maji na Roho. Hii ndio sababu Bwana anasema hapa kwamba kulikuwa na watu 144,000. 
Nje ya hao, hakuna hata mmoja anayeweza kumsifu Bwana kwa baraka yake ya ukombozi kwa kupitia injili ya maji na Roho. Hivyo, Bwana wetu anasifiwa na wale ambao dhambi zao zimesamehewa kwa kuamini katika injili ya maji na Roho na ambao wamempokea Roho Mtakatifu kama karama yao. 
 
Aya ya 4: Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.
Watakatifu ndio wale ambao hawajaitia unajisi imani yao kwa nguvu yoyote ile ya kiulimwengu au dini ya kiulimwengu. Kuna watu wengi katika ulimwengu huu ambao wanabadili imani zao kiurahisi. Lakini kwa wale waliofanyika kuwa watakatifu kwa kuamini katika ubatizo wa Bwana na damu yake Msalabani, na kwa sababu hiyo kupokea ondoleo la dhambi zao, basi watu hao imani zao haziwezi kubadilishwa kamwe na kitu chochote katika ulimwengu huu. 
Watakatifu wanaopaa kwenda Mbinguni na kumsifu Bwana ndio wale ambao wameishikilia na kuitunza injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana na kisha wakazilinda imani zao pasipo kubadilika. Kwa hiyo, wale wanaoweza kumsifu Bwana katika Ufalme wa Mbinguni ni wale ambao wamenyakuliwa na Bwana kwa sababu ya imani yao katika injili ya maji na Roho. 
Katikati ya aya ya 4 imeandikwa hivi, “Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako.” Unapawa kutambua kwamba wale waliosafishwa dhambi zao zote mara moja kwa kupitia imani yao katika injili ya maji na Roho wanapaswa kumfuata Bwana popote anapowaongoza kwenda, wanapaswa kufanya hivi baada ya kuwa wamezaliwa tena upya. Kwa kuwa wamepokea ondoleo la dhambi zao, basi ndani ya mioyo yao unapatikana utayari wa kumfuata Bwana kwa furaha popote anapowaongoza kwenda. Hivyo katika nyakati za mwisho, watakuwa wakimsifu Bwana Mbinguni, watafanya hivyo baada ya kuwa wameuawa kama wafia-dini na Mpinga Kristo kwa sababu ya imani yao, na kisha wakafufuliwa na kunyakuliwa na Bwana. 
Pia imeandikwa hivi, “Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.” Kati ya watu wengi sana wanaoishi katika ulimwengu huu, ni wachache sana ambao wameokolewa toka katika dhambi zao zote kwa kuamini katika injili ya maji na Roho iliyotoelwa na Bwana. Hii ndio sababu katika Yeremia 3:14 Bwana wetu anasema kwamba, “Nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni” Wale waliokutana na injili ya maji na Roho na kupokea ondoleo la dhambi zao ni wachache kiasi hiki. 
Kwa kuwa watu hao ni mali ya Mwana-Kondoo, basi hao watakuwa wa kwanza kupokea malimbuko ya ufufuo, ambao wamenyakuliwa kwa nguvu ya Bwana, na ambao wanamsifu Kristo milele, yote hayo yatakuwa kama yalivyoahidiwa na Bwana. Na hapa duniani, hao ndio wale wanaomfuata Bwana mahali popote anapowaongoza kwenda. Mambo haya yote ni kwa neema na mamlaka ya Mungu. 
 
Aya ya 5: Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.
Wale waliozaliwa tena upya kwa kuamini katika injili ya maji na Roho wanaweza kuihubiri injili hii ya kweli kwa vinywa vyao. Ingawa kuna watu wengi siku hizi ambao wanaihubiri injili kwa njia zao binafsi, ukweli ni kwamba ni wachache sana kati yao ambao ndio wanaoihubiri injili ya kweli ya maji na Roho. 
Wale wanaoihubiri damu ya Yesu ya Msalabani tu hawaihubiri injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Kwa nini? Kwa kuwa hakuna injili nyingine zaidi ya injili ya maji na Roho ambayo ndio injili ya kweli ya Biblia. Kwa kuwa dhambi zote katika mioyo ya wenye haki zimechukuliwa mbali na Neno la injili ya kweli, basi watu hao wanaweza kuihubiri injili hii kwa vinywa vyao kwa ushawishi mkamilifu. 
 
Aya ya 6-7: Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.”
Watakatifu waliozaliwa tena upya wanapaswa kuendelea kuitangaza injili ya maji na Roho hapa duniani. Hivyo, kazi hii ya kuihubiri injili ya maji na Roho, ni lazima iendelee hapa duniani hadi siku ile watakatifu watakaponyakuliwa. 
Ni wale tu wanaoamini katika injili ya maji na Roho ndio watakaouawa na Mpinga Kristo na kuifia-dini ili kuilinda imani yao, na ni hao tu ndio watakaoinuliwa kwenda katika Ufalme wa Mbinguni. Kila mtu anapaswa kumwogopa Mungu, kuamini katika injili ya maji na Roho, na hivyo kupokea ondoleo la dhambi zake na Roho Mtakatifu kama karama yao. Ikiwa Wakristo wa leo hawawezi kuiamini injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana na katika shukrani, basi imani yao katika Yesu itakuwa ni utupu tu. 
Yeye aliyeuumba ulimwengu wote na vitu vyote vilivyomo si mwingine bali ni Yesu Kristo. Kwa hiyo, wanadamu ni lazima wamtambue Yesu Kristo kuwa ni Mungu wao aliyewaumba na kuwapa wokovu wao kwa msamaha wa dhambi zao, na hivyo wanapaswa kumwabudu Mungu vilivyo, hii ni kwa sababu vitu vyote viliumbwa kwa mikono yake na vikakamilishwa. Watu wote wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na kisha kupokea baraka ya kuwa na Roho Mtakatifu kwa kuamini katika injili ya maji na Roho katika mioyo yao. 
Ulimwengu huu ni lazima ujiandae kupokea hukumu ambayo Yesu Kristo ataitoa kwa wale wanaosimama kinyume na Mungu. Hivyo, ni lazima tuiandae imani yetu kwamba hivi punde tutanyakuliwa na Bwana, hii ni kwa sababu siku ya hukumu ya Bwana inakaribia. Njia ya kujiandaa kwa ajili ya unyakuo ni kwa kuamini katika Neno la injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana. Kwa nini? Ni kwa sababu watu wanaweza kupokea Roho Mtakatifu kwa kuamini katika injili ya Bwana ya maji na Roho, na siku ya mwisho itakapowadia, watavikwa utukufu wa kuinuliwa angani na Bwana katika unyakuo wao. 
Hivyo, wenye dhambi wote ni lazima wamwamini Yesu Kristo kuwa ni Mungu wa uumbaji na wokovu mara moja, na kisha wamwabudu Mungu ipasavyo. Wanapaswa kuikubali injili ya maji na Roho katika mioyo yao, na hivyo kupokea neema ya ukombozi wake na Roho Mtakatifu kama karama. Wale wanaomwabudu Mungu wanapokea katika mioyo yao injili ya maji na Roho iliyotolewa na Bwana na hawaikatai, kwa kuwa hivi ndivyo wanavyoweza kumwabudu Mungu. 
 
Aya ya 8: Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.”
Ulimwengu huu utatoweka kwa hukumu ya Yesu Kristo ya kutisha. Kwa kuwa dini za ulimwengu huu kimsingi zimejengwa katika mafundisho ya uongo, basi ndio maana ulimwengu huu utaangamizwa na Mungu. Dini hizi za kiulimwengu zimewafanya watu kuufuata ulimwengu kuliko kumfuata Mungu Mwenyewe, na zimewatumia watu kama vyombo vya kusimama kinyume na Mungu. Hivyo, ulimwengu huu utaangamizwa, kwa sababu watu wake wamemwacha Mungu na wamezitamani hizo dini za kiulimwengu. 
Kule kusema kwamba watu wamefuata dini za kiulimwengu maana yake ni kwamba wameifuata miungu ya uongo, ambayo ni mashetani. Hivyo, Mungu atauangamiza ulimwengu huu kwa ghadhabu yake. Kila kitu katika ulimwengu huu na dini zake zote za uongo vitaangushwa na Mungu, na vitakunywa mvinyo ya ghadhabu ya Mungu. Kwa hiyo, wale wanaosimama kinyume na Mungu, pamoja na mashetani ambayo yanaishi kama minyoo nyonyaji iliyojiunga na dini za ulimwenguni, itaangushwa yote chini kwa mapigo ya Mungu na kisha watatupwa kuzimu milele. 
 
Aya ya 9-10: Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, “Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo.”
Hapa Mungu anamwonya kila mtu, huku akisema kwamba ikiwa mtu yeyote atamwabudu Mnyama na sanamu yake, au ikiwa atapokea alama yake katika mkono au kipaji cha uso, basi mtu huyo atapokea adhabu ya milele kuzimu. Hali akifanya kazi kupitia watu wengi, Shetani atawashurutisha wanadamu wote kuiabudu sanamu ya Mpinga Kristo, lakini wale waliozaliwa tena upya watapambana na Mpinga Kristo na kisha kuuawa kama wafia-dini na hivyo kuilinda imani yao. Hivyo, watakatifu waliozaliwa tena upya ni lazima wailinde imani yao kwa kusimama kinyume na Mpinga Kristo na kisha kuuawa kama wafia-dini. 
Ikiwa mtu yeyote, hali akisalimu amri kwa Mpinga Kristo, ataisujudia sanamu ya Mpinga Kristo na kisha kupokea alama ya jina lake au namba yake, basi mtu huyo atajipatia ghadhabu ya Mungu ambayo itamtupa katika ziwa la moto na kibiriti milele. Wakati wa Dhiki utakapowadia, watakatifu ni lazima wamwombe Mungu, wailinde imani yao katika Bwana, na kisha waliweke tumaini lao katika Ufalme wa Mungu. Ni lazima wasimame kinyume na Mpinga Kristo na kisha kuilinda imani yao kwa kumwamini Yesu Kristo, na kisha kujiunga katika mauaji ya kuifia-dini, ufufuo, na unyakuo, na hivyo kupokea baraka ya milele ya kuishi pamoja na Bwana katika Ufalme wake. 
 
Aya ya 11: Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake. 
Wale wanaomwabudu Shetani kuwa ni Mungu watapewa mapigo ya Mungu na mateso ya milele bila kupumzika huko kuzimu. Yeyote atakayesalimu amri kwa Mpinga Kristo katika nyakati za mwisho na kisha kuiabudu sanamu yake kama ni Mungu atateswa katika ziwa la moto na kibiriti lililojazwa ghadhabu ya Mungu. Sisi sote ni lazima tuamini kwamba yeyote anayemfuata Mnyama na sanamu yake, na yeyote anayeipokea alama ya Mnyama hataona raha usiku na mchana. 
 
Aya ya 12: Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.
Kama vile watakatifu wanavyoamini juu ya utajiri wote, utukufu, na baraka ambazo Bwana amewaahidi, basi ni lazima wavumilie kwa ustahimilivu. Pia ni lazima wavumilie wakati wa kipindi cha Dhiki. Ahadi ambayo Bwana ameifanya kwa watakatifu wa nyakati za mwisho ni kwamba atawapatia baraka ya kuishi pamoja naye baada ya kuifia-dini, na kufufuliwa kwa nguvu za Bwana, na kisha kuinuliwa Mbinguni. 
Hivyo, watakatifu wanavumilia kwa sababu wanaamini katika baraka hii ambayo itawaruhusu kuingia katika karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo pamoja na Bwana, na kwamba watatawala pamoja na Bwana kwa miaka elfu moja, na kisha wataishi milele pamoja na Bwana katika Ufalme wa Mbinguni. Wakati nyakati za mwisho zitakapowadia, watakatifu watahitaji kuuawa na kuifia-dini ili kuilinda imani yao. Hivyo ni lazima wavumilie kupita katika dhiki yote ya wakati huo kwa ustahimilivu. 
Watakatifu wanaoishi katika wakati wa sasa wanapaswa kupokea mauaji ya kufia-dini hali wakiamini katika ahadi za Bwana, hasa wakati ule ambapo Mpinga Kristo atawataka waikane imani yao kwa vitisho, misukumo, na kwa ulaghai. Kwa nini? Kwa sababu mara baada ya hapo, baraka zote za Bwana wetu zitatimizwa kama alivyotuahidi. Watakatifu wote wanaweza kupokea zawadi zao ikiwa tu watailinda imani yao katika Neno la Mungu na katika Bwana. Hivyo, itunze imani yako katika Neno la Bwana. Mungu atawakaribisha watakatifu ambao wameilinda imani yao katika Neno lake na katika Yesu Kristo kuingia katika ulimwengu wake mpya. 
Kuna sababu nyingi kwamba ni kwa nini watakatifu wanaoitumikia injili ya Bwana wanapaswa kuyavumilia magumu yote ya nyakati za Dhiki kwa ustahimilivu. Kwa kuwa mema zaidi yapo baadaye, basi kuna kila sababu ya kuvumilia mateso ya sasa kwa ustahimilivu. 
Warumi 5:3-4 inatueleza kwamba, “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini.”
Watakatifu watakaovumilia wakati wa Dhiki Kuu kwa kuamini katika Bwana wataishi maisha ya baraka, watapokea ufufuo wao na kunyakuliwa toka kwa Bwana na kisha kutawala katika Ufalme wa Mungu. Kwa hiyo, sisi sote ni lazima tuvumilie na kupita katika Dhiki kwa imani yetu. Watakatifu wanaweza kuvumilia kupita katika Dhiki Kuu ya nyakati za mwisho kwa kuilinda imani yao katika Bwana. Watakatifu wanaviamini vitu vyote ambavyo Bwana atavitimiza kwa ajili yao katika ulimwengu huu na huko Mbinguni. 
 
Aya ya 13: Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.”
Aya hii inatueleza kwamba, “Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa.” Kwa nini? Kwa sababu wakati nyakati za Dhiki zitakapowadia—yaani wakati Mpinga Kristo atakapoutawala ulimwengu—hivyo wenye dhambi wote wanaoishi katika ulimwengu huu wataangamizwa. Hivyo, watakatifu ni lazima watazamie ujio wa Ufalme wa Kristo, wailinde imani yao, na wapokee kuuawa na kuifia-dini kwa imani. Wale waliouawa na kuifia-dini ili kumpatia Bwana utukufu wamebarikiwa, na kwa sababu hiyo, ni lazima wapokee kuuawa na kuifia-dini ili kuilinda imani yao. 
Kisha Bwana atawashughulia watakatifu wa jinsi hiyo, huku akiruhusu ufufuo wao na kunyakuwali ili kuwaiunua kwenda katika Ufalme wake. Kazi zote za watakatifu hapa duniani hatimaye zitakoma, na badala yake wataishi huku wakifurahia zawadi iliyotolewa na Bwana. Wakati huu, watakatifu wote watakuwa na furaha ya kutawala pamoja na Bwana na maisha ya milele, na utajiri na utukufu wa Ufalme wa Mungu vitakuwa ni mali yao milele. 
Hii ndio sababu wale waliouawa kuifia-dini katika nyakati za mwisho ili kuilinda imani yao wamebarikiwa sana, kwa kuwa wataishi pamoja na Bwana katika utajiri wote na utukufu wa Ufalme wa Milenia na Ufalme wa Mbinguni milele. Kwa wale ambao hawatasalimu amri kwa Mnyama na kisha kuilinda imani yao katika Bwana, basi Mungu atawapatia baraka ya kutawala pamoja na Bwana milele. 
 
Aya ya 14: Kisha nikaona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali. 
Aya hii inatueleza kwamba Bwana atarudi kuwanyakua watakatifu. Kwa kuwa Bwana ni Kiongozi wa watakatifu, basi atawafufua watakatifu ambao watakuwa wameuawa kuifia-dini ili kuilinda imani yao na kisha kuwainua kwenda katika Ufalme wa Mungu kwa unyakuo. Basi ni hakika kwamba unyakuo utakuja kwa watakatifu wakati wa Dhiki Kuu. 
 
Aya ya 15: Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa.”
Hili neno lina maanisha ni ukamilifu wa unyakuo wa watakatifu utakaofanywa na Bwana. Kwa maneno mengine, unyakuo utatokea baada ya mauaji makubwa ya watakatifu kama wafia-dini. Bwana ataruhusu unyakuo wa watakatifu ambao wakati huo watakuwa wamelala mauti, pamoja na wale ambao watakuwa wameuawa ili kuifia-dini. Ukamilifu wa imani ya watakatifu unapatikana katika wokovu wao, ufufuo, unyakuo, na uzima wa milele. Muda wa unyakuo wa watakatifu ni baada ya kuuawa na kuifia-dini kutokana na mateso ya Mpinga Kristo, na vifo vya kuifia-dini vitaandaman na ufufuo wao. 
 
Aya ya 16: Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa. 
Aya hii pia, ina maanisha ni unyakuo wa watakatifu. Kunyakuwali maana yake ni kuinuliwa kwa watakatifu kwenda angani. Je, hii ina maanisha kwamba watakatifu watainuliwa angani, na kisha kushuka chini pamoja na Bwana? Lakini ukweli nikwamba! Baada ya watakatifu kunyakuliwa, Bwana wetu ataiangamiza dunia, bahari, na vitu vyote vilivyo ndani yake kwa kuyamimina mapigo ya mabakuli saba, na baada ya kuuangamiza ulimwengu, basi Bwana atashuka hapa duniani pamoja na watakatifu walionyakuliwa. 
Kisha, Bwana na watakatifu wake watatawala hapa duniani kwa miaka elfu moja, na baada ya kuisha kwa karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo, watapaa tena kwenda katika Ufalme wa Mbinguni wa milele. Wakati watakatifu watakapoungana na Bwana katika karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo, basi Bwana atakuwa ameushaufanya ulimwengu na vitu vyote ndani yake kuwa vipya. 
Baada ya kunyakuliwa, watakatifu watakaa angani pamoja na Bwana kwa kitambo, na mara baada ya kuisha kwa mapigo ya mabakuli saba, watatelemka katika dunia itakayokuwa imefanywa upya ili kutawala pamoja na Bwana kwa miaka elfu moja. Kisha wataingia katika Ufalme wa Mungu pamoja na Bwana, na kuishi pamoja na Bwana milele. 
 
Aya ya 17: Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali. 
Malaika anayeonekana hapa ni malaika wa hukumu. Malaika huyu atayaleta mapigo makuu kwa watu wa ulimwengu waliosimama kinyume na Mungu, kisha atawatupa katika moto wa milele. Kazi yake ni kuwatupa na kuwafunga wenye dhambi wote wa ulimwengu ambao hawajazaliwa tena upya pamoja na Mpinga Kristo katika shimo la kuzimu lisilo na mwisho. 
 
Aya ya 18: Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana.” 
Neno hili linatueleza kwamba wakati umefika sasa kwa wenye dhambi kuhukumiwa na Mungu kwa ajili ya dhambi zao za kusimama kinyumena Mungu. Kwa mujibu wa nyakati za Mungu, sasa ni masaa ya kutekeleza mipango yake. Ili aweze kuwapatia wenye dhambi hukumu yake, basi Mungu atawakusanya wenye dhambi wote ambao walisimama kinyume na Mungu na kisha kuwaadhibu ipasavyo. 
 
Aya ya 19: Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu.
Neno hili linatuonyesha kwamba baada ya kunyakuliwa kwa watakatifu, Mpinga Kristo na wenye dhambi watateseka sana chini ya mapigo ya mabakuli saba. Mungu ataileta ghadhabu yake pia hapa duniani kwa wenye dhambi kwa kuyamimina mapigo yake ya kutisha juu yao, na kisha itafuatiwa na adhabu ya kuzimu. Hivyo, mapigo ambayo Mungu atayamimina, kwa Mpinga Kristo na wafuasi wake ni ghadhabu yake ya haki. Haya ni majaliwa ya Mungu kwa wenye dhambi ambao wanasimama kinyume naye. 
 
Aya ya 20: Shinikizo lile likakanyagwa nje ya mji, damu ikatoka katika shinikizo mpaka kwenye hatamu za farasi, kama mwendo wa maili mia mbili.
Hii aya inatueleza kwamba jinsi adhabu ya ghadhabu ya Mungu ilivyo kali na jinsi mateso yake yatakavyokuwa kwa wale watakaokuwa wamebakia hapa duniani, kwa wanadamu na kwa viumbe hai, mateso ambayo yataletwa kwa mapigo ya mabakuli saba yatakayomiminwa juu yao. Pia aya hii inatueleza kwamba mapigo haya yatatawanyika katika ulimwengu mzima. Wakati watakatifu watakapouawa na kuifia-dini, kufufuliwa, na kunyakuliwa, basi kuanzia wakati huo na kuendelea, ghadhabu ya mapigo ya mabakuli saba itashushwa na hivyo kumaliza kila kitu. 
Hakuna hata mmoja atakayeweza kuyakwepa mapigo haya ya kutisha zaidi ya watakatifu Mbinguni na malaika ambao walisimama upande wa Mungu. Kwa upande mwingine, wale wanaosimama kinyume na Mungu, basi ni vema wafahamu kwamba adhabu ya kuzimu inawangojea. Lakini wakati huo wale waliozaliwa tena upya watajikuta katika karamu ya chakula cha harusi ya Mwana-Kondoo angani, huku wakimshukuru na kumsifu Bwana kwa ajili ya wokovu wake. Kuanzia hapo, watakatifu wataishi pamoja na Bwana milele katika baraka yake ya milele.